Rafed English

Visa Vya Wachamungu

Visa Vya Wachamungu by : Ustadh Shahid Murtadha Mutahhari

 

Kitabu kilichoko mikononi mwako ni tarjuma ya kitabu cha Kiingereza kiitwacho, Anecdotes of Pious Men kilichoandikwa na Shahid Ayatullah Murtadha Mutahhari. Sisi tumekiita, Visa vya Wachamungu.

Kitabu hiki ni mkusanyiko wa visa vya kweli vya wachamungu mbalimbali wa Kiislamu. Visa hivi vimefika kwetu kama viigizo na mafundisho kwa waumini ili nao angalao wapate kufikia kiwango cha uchamungu wa kweli. Ndani ya kitabu hiki mna visa ambavyo huweza kuhuisha nyoyo za waumini, na iwapo vitazingatiwa sawa- sawa, vitamfanya muumini kufanya ibada zake kwa usahihi na kuji- amini.

Tumekiona kitabu hiki ni chenye manufaa sana, hususan wakati huu wa maendeleo makubwa ya elimu katika nyanja zote. Kutokana na ukweli huo, Taasisi yetu ya Al-Itrah Foundation imeamua kukichapisha kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili kwa madhumuni yake yaleyale ya kuwahudumia Waislamu, hususan wazungumzaji wa Kiswahili.

Tuwamshukuru ndugu zetu, Hussein Hassan na Rajab Osman kwa kukubali jukumu hili la kukitarjumi kitabu hiki. Vilevile tunawashukuru wale wote walioshiriki kwa njia moja au nyingine hadi kufanikisha kuchapishwa kwake.

Ni matumaini yetu kwamba kitabu hiki kitakuwa ni changamoto kubwa kwa wasomaji wetu.
Mchapishaji:
Al-Itrah Foundation
Akiwa amechoka na huku amebeba kiriba cha maji mgongoni, mwanada- da huyo alikuwa akielekea nyumbani kwake akiwa mlegevu, na wanawe wachanga wakiwa wanamsubiri mama mzazi awasili.

Alipokuwa njiani mwanadada huyo alikutana na mgeni aliyemsaidia kube- ba kile kiriba cha maji. Punde si punde waliwasili nyumbani kwa dada huyo. Baada ya mlango kufunguliwa watoto walimuona mama na mgeni ambaye aliteremsha kiriba cha maji na akasema:

“Naam, yaonekana kwamba hamna mtu yeyote wakuwatekea maji! Imekuwaje hadi mkawa na upweke kiasi hiki?”

Mwanadada huyo alijibu kwa huzuni: “Mume wangu alikuwa mwanajeshi; Ali (a.s) alimtuma kwenye mstari wa kwanza vitani, na ndipo alipouwawa. Na hivi sasa nimebaki mpweke na watoto hawa.”

Mgeni huyo alikata kauli na hakuendelea kuzungumza zaidi. Aliinamisha kichwa chake na akaondoka. Lakini wazo la mjane na mayatima waliokuwa hawajiwezi halikumtoka.

Na ikawa ndio sababu ya kutolala usiku huo. Kulipokucha, mgeni huyo alichukua kapu lake, na ndani yake akaweka kipande cha nyama, unga, na tende. Kisha moja kwa moja alielekea hadi nyumbani kwa mjane yule na kubisha mlango.

“Ni nani wewe?”

‘’Ni mimi yule bwana aliyekubebea maji jana. Na hivi sasa nimewaletea watoto vyakula.”

“Mwenyezi Mungu (swt) akujaalie kila la kheri na ahukumu baina yetu sisi na Ali.”

Kisha mwanadada huyo alifungua mlango na kumpokea bwana huyo. Alipoingia, alitamka na kusema:

“Natamani kutenda mema. Ima uniruhusu nikande unga na nipike mikate, au uniruhusu niwaangalie watoto.”

“Nashukuru, lakini nadhani nina ujuzi wa kupika zaidi yako. Wewe waangalie watoto hadi nitakapomaliza upishi.”

Bila kupoteza muda mwanadada huyo alielekea kukanda unga na bwana huyo alianza kumega nyama aliyoileta na kuwalisha watoto. Wakati alipokuwa akiweka tonge la chakula mdomoni mwa kila mmoja wao alikuwa akisema:

“Mwanangu msamehe Ali kama hakuweza kutekeleza wajibu wake juu yako!”

Unga ulipokuwa tayari kupikwa; mwanadada yule aliita: “Ewe bwana mungwana washa jiko tafadhali.” Bwana huyo alifanya hivyo. Moto ulipowaka alisogeza uso wake karibu ya moto na kusema, “Onja joto la moto.” Hii ndiyo adhabu ya wale walioshindwa kutekeleza wajibu wao kwa mayatima na wajane.”

Kwa bahati, mwanamke mmoja aliyekuwa jirani aliingia na baada ya kum- tambua mgeni huyo alitiririkwa na machozi. “Ah! Kwani haumtambui huyu bwana anayekusaidia? Yeye ndiye Amirul-Muuminiin ( Kiongozi wa waumini) Ali bin Abi-Talib (a.s).”

Mjane huyo alisogea mbele huku akilia kwa kuona haya “Laana na aibu iwe juu yangu. Naomba msamaha wako.”

Hapana, mimi ndiye naomba msamaha kwa kutotimiza wajibu wangu juu yenu.”
“Ingelipendeza kiasi gani lau ungeliowa na ukaanzisha familia, na iwe ndio mwisho wa maisha ya ukiwa na upweke? Na hivyo ungeliweza kutimiza mahitaji yako ya kimaumbile na vile vile yeye angelikusaidia kufikia mahi- taji na malengo yako ya kidunia na ya kiroho.”

“Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu mimi sina mali wala sura ya kupen- deza, wala sijatoka kwenye ukoo wenye heshima au nasaba. Ni nani atakayekubali kuolewa nami? Na ni mwanamke yupi apendae kuwa mke wa mtu masikini, mfupi, mweusi na mwenye sura mbaya kama mimi?”

“Ewe Juwaibir! Mwenyezi Mungu alibadilisha thamani ya watu kupitia Uislamu. Watu wengi walikuwa wamepewa vyeo kwenye jamii zili- zokuwepo kabla ya Uislamu, na dini ya kiislamu ikawashusha. Wengi walikuwa wamedharauliwa na kuonekana si chochote, na dini ya kiislamu ikawapa heshima na hadhi kubwa na kuwainua. Uislamu umeondoa ubaguzi na ufakhari wa kiukoo uliokuwako usiyo wa kiislamu.

Hivi sasa watu wote ni sawa bila kuzingatia rangi zao na sehemu walizotoka. Hakuna yule mwenye ubora juu ya wengine ila tu kwa kumuamini na kum- cha Mwenyezi Mungu (s.w.t). Miongoni mwa waislamu, mtu ambaye maadili na vitendo vyake ni bora zaidi kushida vyako ndiye mmbora wako. Hivi sasa fanya kama ninavyokwambia.”

Maneno haya yalizungumzwa siku moja baina ya Mtume (s.a.w.w) na Juwaibir, wakati Mtume (s.a.w.w) alikuja kuwaona watu wa “Suffa.”

Juwaibir alikuwa mwenyeji wa “Yamamah” sehemu ambayo alijulia habari za Bwana Mtume (s.a.w.w) na kuwasili kwa dini ya Kiislamu. Yeye alikuwa ni masikini, mweusi na mfupi, lakini wakati huo huo alikuwa ni mwerevu wakutafuta ukweli na mtu mwenye uamuzi. Alikuja Madina ili kutazama Uislamu kwa karibu na kwa muda mfupi alisilimu na kufuata Uislamu.

Kwa vile hakuwa na hela, nyumba wala marafiki, kwa kipindi fulani alikuwa akipata malazi msikitini pamoja na Waislamu wengine masikini kwa idhini ya Mtume (s.a.w.w). Na pindi Mtume (s.a.w.w) alipo- julishwa kuwa msikiti sio sehemu ya malazi na kuishi, ilibidi wahamishwe na kupelekwa kwingine. Mtume (s.a.w.w) alichagua sehemu nje ya msiki- ti na kuwajengea kivuli. Sehemu hiyo ilijulikana kama “Suffa” na watu waliyoishi hapo walitambulika kama “As-hab-u-Suffa” - wote walikuwa ni masikini kutoka sehemu za mbali na Madina.

Siku moja Bwana Mtume (s.a.w.w) alikuja kuwatembelea. Alipomtambua Juwaibir miongoni mwao aliamua kumtoa kwenye maisha haya ya upweke. Wazo la kumiliki nyumba na kuwa na mke katika hali aliyokuwa nayo Juwaibir ilikuwa ni mbali na ndoto zake. Na hiyo ilikuwa ndio sababu ya Juwaibir kumjibu Mtume (s.a.w.w) na kwamba ingeliwezekanaje mtu yeyote kumkubali kwa ndoa aliposhauriwa na Mtume (s.a.w.w) aowe. Lakini ili Mtume (s.a.w.w) kumtoa ile shaka, alimueleza mabadiliko ambayo Uislamu ulileta kwenye jamii na kubadilisha mtizamo wa watu.

Baada ya kumtoa Juwaibir kwenye mawazo duni, Mtume (s.a.w.w) alimuelekeza yeye Juwaibir nyumbani kwa Ziad ibni Lubaid ili amuombe kumposa bintiye.

Ziad alikuwa ni mmoja kati ya matajiri wakubwa wa Madina na alikuwa amehishimiwa sana na watu wa kabila lake. Wakati Juwaibir alipoingia nyumbani kwake alizingirwa na jamaa zake na baadhi ya watu wa kabila lake. Juwaibir aliketi na kubaki kimya kwa muda mfupi na kisha akainua kichwa chake na kusema, “Nimewaletea ujumbe kutoka kwa Mtume (s.a.w.w). Mngependa kuusikiza kwa siri au niuweke wazi?

Ziad alijibu, “Ujumbe kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) ni heshima kwangu na bora useme hadharani. Basi Juwaibir alinena, “Mtume (s.a.w.w) amenitu- ma nimpose binti wenu”

“Yeye ndiye aliyependekeza wazo hilo kwa ajili yako?” aliulizwa.

“Mimi sizungumzi kwa matakwa yangu. Kila mtu anajua kuwa mimi sio muongo”

“Hii ni ajabu! Sisi huwa hatutoi mabinti zetu kwa watu wenye hadhi tofau- ti nasi wala kabila tofauti nasi. Wewe rudi, mimi nitakwenda kuzungumza na Mtume (s.a.w.w) mwenyewe.”

Juwaibir aliondoka mahala pale huku akinung’unika, “Wallahi, chochote ambacho Qur’ani inafunza na chochote ambacho ndio makusudio ya utume wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) ni tofauti kabisa na anachokisema Ziad.”

Wale waliokuwa karibu walisikia manung’uniko ya Juwaibir.

Zalfa, yule binti mzuri sana wa Ziad, aliyekuwa malikia wa urembo wa Madina, aliyasikia maneno hayo ya Juwaibir. Alimuendea babake na kumuuliza, “Baba, ni nini huyo bwana aliyetoka alichokuwa akisema? Na alikuwa akimaanisha nini?”

“Alikuwa amekuja kukuposa huku akidai kuwa ametumwa na Mtume (s.a.w.w) kuhusu hilo”

“Je, haiwezekani kwamba kweli ametumwa, na hivyo kukataa kwako kukaonyesha kutotii maagizo ya Mtume (s.a.w.w)?”

“Wewe unaonelea vipi kuhusu hilo?’

“Naonelea ni vyema ungemrejesha kabla hajafika kwa Mtume (s.a.w.w), na kisha uende mwenyewe ili upate ukweli.”

Alimrejesha Jawaibir ndani ya nyumba kwa heshima ya hali ya juu kisha yeye mwenyewe akaharakisha kwenda kwa Mtume (s.a.w.w). Alipomuona Mtume (s.a.w.w) alisema;

“Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, Jawaibir amekuja nyumbani kwangu na akaja na ujumbe kama huu kutoka kwako. Mimi ningependa kukujul- isha kuwa desturi yetu ni kuwatoa mabinti wetu kwa watu hadhi sawa na yetu, tena wa kabila letu, na ambao wote ni wasaidizi na masahaba wako.”

“Ewe Ziad, Juwaibir ni bwana muaminifu. Hiyo hadhi na heshima ambazo wewe unazungumzia zimekwishafutwa. Kila muumini wa kiume yuko sawa {katika madhumuni ya ndoa} kwa kila muumini wa kike.”

Ziad alirejea nyumbani kwake na kumuelezea jambo hilo bintiye. Kisha binti akasema, « Tafadhali usiyakatae mapendekezo aliyotoa Mtume (s.a.w.w.). Haya maneno yananihusu mimi. Ninamkubali Juwaibir kwa hali yake yoyote ile atakayokuwa nayo. Kama Mtume (s.a.w.w) ameridhika nayo pia nami nimeridhia.”

Nikaha hiyo ilitimizwa kulingana na sheria ya kiislamu. Ziad alilipa mahari kutokana na mali yake mwenyewe na akawapa zawadi nyinginezo nzuri. Kisha walimuuliza bwana harusi, “Je unayo nyumba ya kumpeleka biharusi?” Alisema, “Hapana, sikuwa na wazo la kuwa nitapata mke na kuishi maisha ya ndoa naye. Bali ni Mtume (s.a.w.w) ambaye alinijia ghafla na kuzungumza nami na kisha kunituma nyumbani kwa Ziad”

Ziad alimuandalia nyumba iliokuwa na vyombo kamili vya matumizi ya nyumbani, na akamhamisha biharusi huyo kwa shangwe na nderemo akiwa amepambwa kwa madoido na manukato.

Usiku ukafika, Juwaibir hakuweza kujua nyumba iliyokusudiwa yeye ilikokuwa. Aliongozwa hadi huko na akaingizwa kwenye chumba cha biharusi. Alipoona nyumba na vifaa vyake na kumuangalia biharusi alivy- opendeza, alikumbuka alivyokuwa hapo awali. Kisha alijiambia,

“Nilikuwa masikini kiasi gani wakati ninaingia kwenye mji huu. Sikuwa na chochote - siyo pesa wala uzuri, wala nasaba yoyote wala familia. Hivi sasa Mungu amefanya utajiri wote huu kuwa mikonini mwangu kupitia Uislamu. Kwa kweli ni Uislamu ndio umeniletea mabadiliko haya katika muonekano wa jamii ya watu kinyume na matarajio. Namshukuru Mwenyezi Mungu kiasi gani kwa kunipa neema ya vyote nilivyo navyo!”

Kwa upeo wa hisia za kiroho alikwenda pembeni mwa chumba, akatumia usiku wake kwa kusoma Qur’ani na kuswali. Kulipopambazuka ndipo aka- jitambua, kisha aliamua kufunga ili kumshukuru Mwenyezi Mungu. Wakati wanawake walipokuja kumtembelea Zalfa asubuhi walimkuta bado hajaguswa. Walimficha Ziad jambo hilo. Siku mbili na usiku wake zilipita hali ikiwa vilevile. Alikuwa akifunga mchana na usiku akiswali. Wanawake wa upande wa familia ya mke wakawa na wasiwasi. Walidhani pengine Juwaibir alikuwa hana nguvu za kiume na hakuwa na haja ya kuwa na mke. Hatimaye walilifikisha suala hili kwa Ziad. Yeye alimjulisha Mtume (s.a.w.w) na Mtume (s.a.w.w) alimuita Juwaibir na kumuuliza, “Je, huna haja ya kuwa na mke?”

“Kwa bahati mbaya au nzuri, nina haja kubwa ya kuwa naye.” “Basi kwa nini hujamkaribia bibi harusi wako?”

“Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, nilipoingia ndani ya nyumba ile nili- jikuta kati ya neema zile. Hali ya kushukuru na kuabudu ilinijia. Nilidhani ni bora kumshukuru Allah na kuswali kabla ya kuchukua hatua yoyote. Usiku wa leo nitamkaribia mke wangu, insha’allah.”

Juwaibir na Zalfa waliishi maisha mazuri ya furaha. Wakati mwito wa vita vya Jihad (Vita tukufu) ulipofika, alishiriki kwa roho moja kama Mwislamu shupavu, na akafa shahidi chini ya bendera ya Uislamu.

Baada ya shahada yake, Zalfa alikuwa ndiye mwanamke aliyetafutwa sana kwa ajili ya kuwa mke, na watu wengi walikuwa na moyo wa kulipa mahari ya juu kabisa kwa ajili yake.
Majirani wawili; mmoja Mwislamu na mwengine mkristo, walikuwa na uhusiano mzuri kama marafiki. Katika hali ile yakujali maslahi ya kila mmojawao walikuwa wakijuliana hali, na walikuwa wakibadilishana mawazo kila mara. Jirani Mwislamu akiwa mcha-Mungu na mwenye kushika dini, alikuwa akiisifia sana dini yake na matokeo yake ilikuwa ni kusilimu kwa huyo jirani Mkristo.

Usiku ulipita na ilikuwa yakaribia alfajiri. Mkristo huyo, aliyekuwa amesilimu mara tu, alisikia mtu akibisha mlango wake. Kwa mshangao na bila ya subira aliuliza kwa sauti: “Ni nani wewe?

Sauti kubwa ilisikika kutoka nyuma ya mlango, “Mimi ni fulani bin fulani,” akijitambulisha. Alikuwa ni yule jirani Mwislamu ambaye alikuwa na heshima ya kumsilimisha kuwa Mwislamu.

“Wataka nini nyakati hizi za usiku?”

“Harakisha, vaa nguo zako na ushike udhu, ili twende msikitini pamoja”. Bwana huyo Mwislamu mpya, alishika udhu kwa mara ya kwanza katika maisha yake na kuandamana na rafikiye Mwislamu hadi msikitini. Marafiki hao walifika kabla ya wakati kuwadia. Ilikuwa wakati mzuri wa sunna ya swala ya usiku ambayo ni baada ya usiku wa manane. Waliswali hadi alfajiri - wakati wa swala ya asubuhi (subhi) ukaingia.

Marafiki hao waliswali swala ya subhi, kisha wakamsabihi Mwenyezi Mungu (s.w.t) na nyuradi hadi kukapambazuka. Wakati yule bwana aliyesilimu aliamka kutaka kuelekea mlangoni, rafiki yake Mwislamu alimuuliza:

“Unakwenda wapi?”

“Naelekea nyumbani, maadamu nishamaliza swala ya subhi, hakuna jambo lingine tena la kufanya sasa.”

“Subiri kiasi na umkumbuke Mwenyezi Mungu kwa kuzitaja sifa zake (nyiradi) mpaka pale jua litakapochomoza.” “Sawa sawa.”

Bwana huyo alikaa na kusoma kama alivyoagizwa hadi jua lilipochomoza. Wakati alipoinuka ili aondoke, rafiki yake alimpa Qur’ani mikononi na akamwambia, “Soma hadi jua lichomoze zaidi kidogo. Na nakushauri ufunge saumu leo hii. Kwani hujui kufunga kuna ubora na malipo (thawabu) kiasi gani?” Basi Mwislamu huyo mgeni alifuata maamrisho jinsi alivyokuwa ameelekezwa, aliendelea kusoma Qur’ani hadi kukaribia wakati wa adhuhuri. Jirani Mwislamu alimwambia: “Sasa hivi wakati wa adhuhuri umekaribia, ni bora tukiswali swala ya adhuhuri hapa msikitini.”

Hivyo swala ya dhuhri ikaswaliwa. Kisha akasema tena: “Baada ya muda mfupi, swala ya Alasiri itaswaliwa. Na hiyo pia inabidi tuiswali kwa wakati wake uliotengwa.” Swala hiyo pia iliswaliwa. Kisha akasema, “Sasa hivi Magharibi imewadia” na akamuweka aliyesilimu hadi wakati wa swala ya Magharibi. Wakati alipoamka kufunguwa saumu yake, jirani alimwambia, “Kuna swala moja imebaki na inaitwa “Ishaa.” Kwa hivyo walisubiri kipindi cha swala kiingie. Baada ya hapo yule bwana aliyekuwa amesilimu siku za karibuni aliamka na kuenda zake.

Siku ya pili yake masaa yale ya usiku alisikia tena kubishwa hodi mlango- ni. Akauliza: “Nani mwenzangu?”

“Mimi ni fulani bin fulani….. jirani yako. Harakisha, vaa nguo zako na ushike udhuu ili tuende pamoja msikitini”

“Jana usiku baada tu ya kurudi kutoka msikitini, nilijiuzulu na kuwachana na dini yako. Tafadhali nenda zako na ukamtafute mtu mwingine asiyekuwa na la kufanya katika dunia hii, ili kwamba aweze kutumia muda wake wote msikitini. Mimi ni masikini na nina mke na watoto wa kulisha. Afadhali niendelee na shughuli zangu ili nipate riziki yangu.”

Imam Ja’far Sadiq (a.s.) akisimulia kisa hiki kwa marafiki pamoja na wafuasi wake. Alisema, “Hivi ndivyo yule bwana mcha Mungu baada yakumsilimisha jirani yake, yeye mwenyewe alimfukuza kwenye Uislamu. Yabidi kila mtu azingatie jambo hili kichwani na asiwasumbue watu bila dharura. Inawabidi mjue nguvu zao na kiwango chao na kutenda ipasavyo, ili waweze kujenga uhusiano na dini na wasiwe ni wenye kuikimbia. Kwani hamjui kwamba sera za Bani Ummaya zilitegemea ukatili, dhulma na vitisho wakati ambapo njia na taratibu zetu misingi yake ni huruma, undugu na ushawishi mzuri?”
Kovu kubwa kwenye mabega ya Nasiba, bintiye Kaab linaashiria kuwepo kwa kidonda kikubwa cha muda uliopita. Wakati wowote wanawake, haswa vijana ambao hawakuiona enzi ya Mtume (s.a.w.w) au walikuwa wadogo wakati huo, walipoliona shimo hilo katika bega lake, waliuliza kwa udadisi mkubwa kuhusu tukio hilo la kutisha ambalo lilisababisha jer- aha hilo kwenye bega lake. Walipenda kusikia kuhusu vituko vyake vya kutisha katika vita vya Uhudi kutoka kwenye mdomo wake mwenyewe.

Nasiba hakudhani angeweza kupigana bega kwa bega pamoja na mumewe na wanawe wawili wa kiume kwa kumlinda Mtume (s.a.w.w) kwenye vita vya Uhudi. Alikuwa amebeba tu kiriba cha maji mgongoni mwake ili awanyweshe majeruhi na pia alikuwa amebeba bandeji za kienyeji kwa ajili ya kuwafunga majeraha yao. Hakuwa amejifikiria kuwa angefaa kwa kazi yoyote nyingine siku hiyo.

Ingawa Waislamu walikuwa wachache na walikuwa na vifaa vichache, waliweza kuwashinda vibaya maadui zao na kuwafanya wakimbie kwenye uwanja wa vita kwa visigino vyao. Lakini baada ya muda mfupi, kwa sababu ya kutojali na kupuuza kwa walinzi wa “Vilima vya Ainain” maadui walifanya shambulizi la kushitukiza kutoka nyuma yao na kugeuza ushindi wa Waislam kuwa kushindwa. Waislamu waliokuwa wamemzun- guka Mtume (s.a.w.w) walikimbia na kumuacha Mtukufu Mtume (s.a.w.w) karibu peke yake kwenye medani ya vita.

Nasiba alipoiona hali hiyo ya hatari mbaya aliweka kiriba cha maji chini, na akachukua upanga mkononi mwake. Alipigana kwa upanga na pia aka- tumia vizuri upinde na mishale; na akachukua ngao iliyoachwa na mpi- ganaji anayekimbia. Mara aligundua kuwa kuna mtu ambaye alikuwa akimtafuta Mtume (s.a.w.w), na akiuliza kwa sauti, “Yuko wapi Muhammad mwenyewe?” Alimwendea ghafla na kumpiga mara kadhaa. Lakini yule mtu alikuwa amevaa deraya mbili na hivyo mapigo yake hayakuweza kuwa na athari kubwa mwilini mwake. Kisha akampiga yule mwanamke dhoruba kubwa kwenye bega lake lisilo na deraya na kum- jeruhi kiasi ambacho lilihitaji matibabu ya mwaka mzima.

Alipoona damu ikimwagika kutoka kwenye bega la Nasiba, Mtume (s.a.w.w) alimwita mmoja wa watoto wake wa kiume ili amfunge jeraha lake. Alimfunga bandeji kwenye bega lake na akaendelea tena kushughuli- ka na vita.

Wakati huo huo mmoja wa watoto wake akajeruhiwa. Mama yule alitoa bandeji na akamfunga yule kijana kwenye jeraha lake. Mtume (s.a.w.w) akiangalia kitendo hicho na akatabasamu kwa ushujaa na ushupavu wa bibi huyu. Baada ya mama huyo kumhudumia yule kijana alimshauri aendelee na vita. Alipokuwa akiendelea kuzugumza maneno hayo Mtume (s.a.w.w) alimwonyesha yule mtu ambaye alimuumiza na kumjeruhi mwanawe.

Alimshambulia yule mtu kama simba jike na kumpiga upanga wake kwenye mguu mpaka akaanguka chini. Mtume akasema, “Vema, sasa umelipiza kisasi. Sifa njema ni zake Mwenyezi Mungu ambaye amekuwezesha kupata ushindi dhidi yake na kupoza jicho lako.”

Waislamu wengi walikufa mashahidi na wengine kujeruhiwa. Nasiba mwenyewe alikuwa amejeruhiwa sana na hakuwa na matumaini yoyote ya kuishi. Baada ya vita vya Uhud, Mtume (s.a.w.w) aliwaamrisha wale Waislamu waliojeruhiwa kuwafuata maadui mpaka Hamra-ul Asad ili kuhakikisha juu ya nia na hali zao.

Nasiba pia alitaka kuandamana nao lakini yale majeraha makubwa aliyokuwa nayo hayakumruhusu kwenda. Walipokuwa wanarudi kutoka Hamra-ul-Asad, kabla ya Mtume (s.a.w.w) kufika nyumbani kwake, alim- tuma mtu kwenda kumjulia hali Nasiba na alifurahi sana kujua kuwa bado alikuwa hai.
Imam Ali (a.s) katika zama za ukhalifa wake, yeye mwenyewe alikuwa akisikiza malalamishi na manung’uniko ya watu moja kwa moja. Katika siku za joto jingi watu hawakuweza kutoka kwenye nyumba zao baada ya adhuhuri. Imam Ali (a.s) alikuwa akiketi nje kwenye kivuli cha ukuta kila siku ili kama mtu yeyote alikuwa na malalamiko aweze kuonana naye ana kwa ana. Wakati mwingine alikuwa akitembea vichochoroni na barabarani akiangalia hali za watu zilivyo.

Siku moja alirudi kwenye makao yake akiwa amechoka huku jasho likim- toka, na alimkuta mwanamke mmoja akimsubiri. Mwanamke yule alipo- muona alisogea karibu na akasema:

“Nina matatizo. Mume wangu amenionea. Amenifukuza kwenye nyumba na amenitishia kunipiga. Nakuomba uje uhukumu haki baina yetu.”

“Ewe mja wa Mungu, kuna joto jingi hivi sasa, subiri hadi nyakati za jioni joto lipungue ndipo nije kusawazisha manung’uniko yako.”

“Ikiwa nitachelewa nje kwa muda mrefu nahofia atakasirika zaidi.” Aliinamisha kichwa chake kwa muda na kisha akakiinua akijiambia,

“Hapana, ninaapa kwa Mweyenzi Mungu haifai kuchelewesha hukumu ya mwenye kudhulumiwa. Na haki yake lazima ichukuliwe kutoka kwa mwenye kudhulumu. Na uoga wa wowote ule lazima utolewe kwenye moyo wa mdhulumiwa, ili aweze kusimama imara mbele ya muonevu na kudai haki yake.”

“Nieleze nyumba yenu iko wapi?” “Ni mahali fulani.”

“Twende pamoja.”

Aliandamana naye hadi nyumbani kwake. Walipofika alisimama mlangoni na kuita kwa sauti kubwa, ‘Ewe Bwana mwenye nyumba! Amani iwe juu yako’

Bwana mwenye umri wa wastani alijitokeza na ndie alikuwa mume wake. Hakuweza kumtambua Imam Ali (a.s). Alimuona ni mtu mzima mwenye umri wa karibu miaka sitini ambaye aliandamana na mkewe na akachukulia kuwa amemleta kama mtetezi na msuluhishaji lakini alinyamaza kimya.

“Mwanamke huyu, ambaye ni mkeo ana malalamiko dhidi yako. Anadai kuwa wewe umemuonea na kumfukuza nyumbani. Pamoja na hayo umetishia kumpiga. Nimekuja kukueleza kuwa umuogope Mwenyezi Mungu na uwe mpole na mkarimu kwa mke wako.” Imam Ali (a.s) alisema.

“Inakuhusu nini kama sikumtendea vema mke wangu? Ndio, nimetishia kumpiga, lakini kwa sababu amekuleta wewe ili kumuombea, basi nitamtupa kwenye moto na kumchoma akiwa hai.”

Imam Ali (a.s) hakufurahishwa na ukaidi wa yule kijana. Alichomoa upanga wake huku akisema; “Nakushauri tu kutenda mema na kukukanya kutokana na matendo mabaya (maovu), lakini wewe unanijibu kwa namna hii ya wazi kuwa utamchoma mwanamke huyu kwenye moto. Unadhani hakuna mamlaka katika duniani hii?”

Sauti kubwa ya Ali iliwavuta wapita njia na punde si punde umati mkubwa wa watu ukakusanyika hapo. Kila aliyekuja aliinama kwa heshima na kumuamkua yule mzee kwa kusema “Amani iwe juu yako Ewe Kiongozi wa waumini.”

Wakati yule kijana mfedhuli alipomgundua aliyekuwa akiongea naye, alitetemeka na kuomba, “Ewe kiongozi wa waumini, nisamehe. Ninakiri makosa yangu na nakuahidi kwamba kutoka leo nitamtii mke wangu. ”

Ali alimgeukia yule mke na akamwambia aingie nyumbani kwake, kisha alimkanya kutotenda yatakayomkasirisha mume wake tena.
Kabla kuja kwa Uislamu, waarabu walikuwa na viongozi huru wa kikabila. Watu walikuwa wamezoea utawala wa machifu wao na walikuwa wakiwatii; na kila wakati wakiwalipa ushuru na kodi. Hatim, aliyekuwa mkarimu na mashuhuri kutoka kabila la Tai alikuwa mmoja wa machifu wa kiarabu. Mwanawe ‘Adi alimrithi baba yake baada ya kufariki kwake na kabila lake lilikubali uongozi wake. Alikuwa akiwatoza ushuru kwa kiwango cha robo ya mapato yao kila mwaka.

Uongozi wake ulitukia sawia na zama za Mtume (s.a.w.w). Kabila la Tai lilikuwa likiabudu masanamu, lakini Adi mwenyewe alikuwa mkristo na aliwaficha watu wake dini yake. Watu hao baada ya kuyafahamu mafunzo bora ya kiislamu, walipata faraja ya kuondolewa katika mzigo wa viongozi wao ambao mpaka wakati huo walikuwa wamelazimisha utawala wao juu ya watu.

Kutokana na jambo hili, Adi kama viongozi wengine alikuwa akiutazama Uislamu kama tishio kubwa kwake na alikuwa akificha uadui kwa Mtume (s.a.w.w) lakini uamuzi ulikuwa umeshapita. Watu walikuwa wakiingia katika Uislamu makundi makundi na dini ya Mwenyezi Mungu ilikuwa ikienda mbele siku baada ya siku. Alijua kwamba siku inakuja ambapo Waislamu watakuja kumtafuta yeye pia, na huo ndio utakuwa mwisho wa uongozi wake. Kwa hivyo alimwamrisha mfanyakazi wake maalum, ambaye ni mtumwa, kila siku kuwaweka tayari ngamia wenye nguvu na mbio karibu na kambi yake na kuwa macho.

Siku moja yule mtumwa wake alimjia na kusema “Fanya kila maandalizi unayotaka kufanya kwa sababu waislamu wako karibu sana.” Adi alipandisha familia yake kwenye ngamia na kuchukua vitu vilivyo kuwa na thamani na mzigo ambao angeweza kubeba na kutoroka kwenda Damascus, ambako watu walikuwa wa dini yake. Lakini katika kuchanganyikiwa huko alisahau kumchukua dada yake Saffana pamoja naye na akaachwa huko nyuma.

Waislamu waliwashinda kabila hilo kwenye vita; na baadhi yao wakachukuliwa mateka. Waislamu walimchukua Saffana na mateka wengine na kuwapeleka Madina na kumuelezea Mtume (s.a.w.w) kuhusu kutoroka kwa Adi.

Wafungwa walipewa makao katika kambi yenye ukuta mfupi karibu na msikiti. Siku moja Mtume (s.a.w.w) alipokuwa akienda msikitini alipitia karibu na sehemu ile ya wafungwa. Saffana aliyekuwa mwenye akili na mzungumzaji aliinuka kutoka mahali pake na kusema;

“Baba yangu amefariki na mlezi wangu amejificha, kuwa mkarimu kwangu na Mungu atakuwa mwema kwako!!’’

Mtume (s.a.w.w): “Ni nani mlezi wako?” Saffana: “Adi mwana wa Hatim.”

Mtume: “Yule ambaye amemtoroka Mwenyezi

Mungu na Mtume wake?”

Alipotamka maneno hayo, Mtume (s.a.w.w) aliondoka zake. Siku iliyofuata, Saffana alirudia maneno yale yale, na akajibiwa sawa kama alivyojibiwa siku iliyopita. Maombi yake hayakuwa na mafanikio. Siku ya tatu alipokuwa amepoteza matumaini aliamua kukaa kimya. Lakini kijana mmoja ambaye alikuwa akitembea nyuma ya Mtume (s.a.w.w) alimuashiria kuwa arudie matakwa yake. Akarudia maneno yale yale. Mtume (s.a.w.w) akasema;

“Sawa kabisa, namsubiri mtu muaminifu kutoka kwenye kabila lako. Punde tu mtu kama huyo atakapopatikana basi nitakutuma wewe pamoja na mtu huyo kwenye kabila lenu. Nijulishe ukipata habari za mtu kama huyo atakapokuja hapa Madina.”

Mwanamke huyo aliwauliza watu, ni nani yule kijana ambaye alikuwa nyuma ya Mtume (s.a.w.w) aliyemhimiza kurudia madai yake. Wakasema, alikuwa Ali.

Baada ya muda mfupi Saffana akamjulisha Mtume (s.a.w.w) kuwa kuna watu wa kabila lake wamekuja Madina. Mtume (s.a.w.w) akampa mavazi mapya na pesa za matumizi njiani na ngamia wa kusafiria. Alifuatana nao moja kwa moja hadi kwa nduguye ambaye alikuwa Syria.

Wakati alipomuona nduguye, alimkemea huku akisema; “Uliwachukua mke na watoto wako na kunisahau mimi kumbukumbu ya baba yako!” Adi alimuomba msamaha. Na kwa vile alikuwa ni mwanamke mwenye hekima, Adi alimuomba ushauri kuhusu mpango wake. Alimuuliza: “Ungenishauri nifanye nini kwa kuwa umemuona Muhammad kwa karibu? Nijiunge naye ama nijitenge?”

“Naamini bora ungejiunga naye. Kama yeye ni Nabii wa Mwenyezi Mungu itakuwa ni nyongeza kwenye heshima na uungwana wako. Na kama yeye sio Mtume, anataka tu kuwa kiongozi wa kidunia, tena kwenye sehemu (Madina), ambapo sio mbali na Yemen, hakuna mtu yeyote atakayethubutu kukuvunjia heshima, kwa sababu ya heshima uliyokuwa nayo kwa watu wa Yemen. Vyovyote itakavyokuwa utahakikishiwa heshi- ma yako.”

Adi alivutiwa na wazo hilo. Akaamua kwenda Madina na kuchunguza mwenendo wa Mtume (s.a.w.w) kwa undani. Kama atakuwa Mtume atamfuata sawa na Waislamu wengine. Lakini ikiwa yeye ni mtu mwenye tamaa za kidunia ya uongozi na mali, basi atashirikiana naye hadi kiasi cha kunufaika wote sawa.

Aliingia msikiti wa Madina na kumsalimia Mtume (s.a.w.w). Mtume (s.a.w.w) akampokea kwa heshima inayostahili na kumkaribisha kwake nyumbani.

Walipokuwa wanaelekea nyumbani mama mmoja aliyesawijika alishika nguo ya Mtume (s.a.w.w) na akaanza mazungumzo naye. Muda mrefu ulipita na Mtume (s.a.w.w) alijibu maswali yake kwa upole na subira.

Adi alijiambia moyoni, “Hii ni ishara moja toka kwenye tabia yake kuonyesha kuwa huyu mtu ni Mtume. Watu wenye matamanio ya kidunia hawana tabia na moyo wa kumjibu mama masikini kwa subira kiasi hiki na upole.”

Walipoingia ndani ya nyumba, Adi alikuta kuwa maisha yake yalikuwa ya chini sana na yasiyo na majivuno. Palikuwa na tandiko la kulalia ambalo pia Mtume alikuwa akilitumia kwa kukalia, lakini sasa analitandika ili Adi akalie. Adi alisisitiza kuwa Mtume (s.a.w.w) alikalie lakini Mtume (s.a.w.w) alikataa. Kisha Adi alikalia lile tandiko na Mtume (s.a.w.w) aliketi chini kwenye sakafu. Adi akajiwazia “Hii ni ishara ya pili ya tabia ya huyu mtu. Hii ni tabia ya Mitume siyo ya wafalme.

Mtume (s.a.w.w) alimgeukia na kumuuliza, “Lakini Ukristo haukuwa dini yako wewe?” Adi alijibu, “ndio, kwa nini?” Mtume (s.a.w.w) akasema “Basi ni kwa nini na kwa misingi gani, ulikuwa ukichukuwa robo ya mapato ya watu wako? Hiyo haikatazwi na dini yako ?”

Adi ambaye alikuwa ameficha dini yake hata kwa watu wake wa karibu, alishangaa kusikia maneno haya kutoka kwa Mtume (s.a.w.w). Akanena moyoni, “Hii ni ishara ya tatu kuwa mtu huyu ni Mtume.

Kisha Mtume (s.a.w.w) alisema “Unaona umasikini na udhaifu wa sasa wa Waislamu. Unaona Waislamu leo wanaishi maisha ya dhiki. Wamezungukwa na makundi ya maadui na hawana usalama wa maisha yao na mali zao. Hawana uwezo mikononi mwao. Wallahi wakati utafika karibuni ambapo utajiri huo mkubwa utawafikia na hakutakuwa na masikini miongoni mwao. Wallahi, maadui wao watashindwa na kutakuwa na amani kiasi cha mwanamke kusafiri kutotaka Iraq hadi Hijaz peke yake bila ya mtu kumsumbua. Wallahi, wakati unakaribia yale makasiri meupe ya Babiloni yatakuwa katika mikono ya Waislamu.’’

Adi aliingia katika Uislamu kwa Imani kamili na uaminifu na alibakia kuwa mwaminifu mpaka mwisho wa maisha yake. Aliendelea kuishi kwa miaka kadhaa baada ya Mtume (s.a.w.w). Alikuwa kila mara akikumbuka mazungumzo yake na Mtume (s.a.w.w) wakati walipokutana kwa mara ya kwanza na vile alivyotabiri wakati ule juu ya hali ya baadaye ya Waislamu. Alikuwa ana mazoea ya kusema “Wallahi katika wakati wa uhai wangu nimewaona Waislamu wakishinda na kuteka makasiri meupe ya Babiloni, na kuna amani na utulivu kiasi cha kumwezesha mwanamke kusafiri kutoka Iraq hadi Hijaz bila mtu kumsumbua. Wallahi naamini siku itafika ambapo hakutakuwa na masikini miongoni mwa Waislamu.
Ibni Sayyaba mkazi wa Kufa alikuwa kijana ambaye baba yake alikuwa amefariki. Msiba wa kifo cha baba yake ukiambatana na umasikini na ukosefu wa kazi ulikuwa unavunja moyo wa mtu mwenye hisia. Siku moja alipokuwa katika nyumba yake alisikia mlango ukibishwa. Alikuwa ni rafiki ya baba yake. Baada ya kumpa pole, alimuuliza,

“Je babako alikuwachia kitu chochote?” “Hapana,” alijibu.

“Basi chukua hizi Dirhamu elfu moja; jaribu kuzifanya kuwa mtaji na faida yake utumie kwa mahitaji yako.

Alipomaliza maneno hayo aliondoka. Kwa furaha aliokuwa nayo Ibni Sayyaba alikwenda kwa mama yake kumuonyesha pesa zile na kumueleza kisa hicho. Siku hiyo hiyo alitumia pesa hizo kununua bidhaa na kufungua duka na kuweka moyo wake hapo. Alifanya maendeleo ya haraka. Muda mfupi baadaye alifahamu kuwa siyo tu aliweza kujimudu kimaisha kutokana na faida bali pia mtaji ulikuwa umeongezeka marudufu. Alifikiria kwenda kuhiji na alimuendea mama yake kwa ushauri. Mama yake alimwambia “Tafadhali, kwanza ungerudisha zile pesa za watu”

Alikwenda kumuona yule rafiki ya baba yake na kumkabidhi zile Dirham elfu moja huku akisema “Tafadhali pokea pesa zako.” Bwana yule alidhani kuwa Ibni Sayyaba anamrejeshea pesa zile zile kwa sababu hazikutosha kufanyia biashara yeyote, kwa hivyo alimwambia: “Kama kiwango hicho cha pesa hakitoshi katika biashara naweza kukiongeza.”

“Mungu wangu mwema, zilitosha. Pesa hizo zimetuletea mafanikio makubwa na kwa kuwa sasa naweza kujimudu vizuri kifedha, nimekuja kurejesha (kulipa) pesa zako, na kukushukuru, haswa wakati ambapo nimeamua kwenda kuhiji.”

Alirudi nyumbani na kufungasha mzigo wake tayari kwa safari ya Makka. Baada ya kutimiza Hija tukufu alielekea Madina na akaenda kumuona

Imam Sadiq (a.s) pamoja na mahujaji wenzake. Kulikuwa na umati mkubwa wa watu katika nyumba ya Imam (a.s). Kwa vile alikuwa mdogo aliamua kuketi mbali mwisho wa umati huo wa watu. Hapo aliwaona watu wakiingia na kutoka; pia alisikia maswali yao yakijibiwa na Imam (a.s). Wakati nyumba ilipokaribia kuwa tupu Imam (a.s) alimuashiria kidole na akasema “Naweza kukusadia vipi?”

“Mimi naitwa Abdul Rahman mwana wa Sayyaba kutoka Kufa (kabila la Bijilli).’’

“Baba yako anaendeleaje?” “Alifariki.”

“Ah! Ah! Mwenyezi Mungu amrehemu, je alikuwachia chochote?” “La, hakuniachia”

“Basi umewezaje kwenda Kuhiji?”

“Baada ya kifo cha baba yangu tulikuwa na shida. Kwa upande mmoja kifo chake na upande mwingine umaskini na ukosefu wa kazi. Yote hayo yalit- ulemea vibaya. Siku moja rafiki ya baba yangu alinipa Dirham elfu moja na kunishauri nifanyie biashara. Nilifuata ushauri wake na kutokana na faida ya hizo pesa ndiyo nimeweza kuja kuhiji.”

Kabla hajamaliza kisa chake Imam (a.s) alisema, “Niambie ulifanya nini kuhusu pesa ya rafiki ya baba yako?” “Nilimrejeshea pesa zake zote kwa mujibu wa ushauri wa mama yangu kabla sijakuja kuhiji.” “Vizuri sana je ungependa nikupe ushauri?”

“Niwe fidia yako; ndio tafadhali”

“Kuwa mkweli na muadilifu. Mtu muaminifu na muadilifu ni mshirika katika utajiri wa wengine.”
Aqiil aliwasili kama mgeni katika Nyumba ya Serikali zama za ukhalifa wa nduguye, Ali (a.s). Ali (a.s.) alimuamrisha mwanae mkubwa, Hasan ampe ami yake vazi. Hasan alimpa joho na kilemba. Usiku ulipofika, hali ya anga ilikuwa ya joto. Walikuwa wameketi juu ya paa la nyumba wak- izungumza kwa furaha. Ulikuwa wakati wa chakula cha jioni. Aqiil alijiona kuwa ni mgeni wa mtawala mkuu kabisa wa ulimwengu wa Waislamu, hivyo alitarajia chakula cha kupendeza cha kitajiri. Lakini kwa mshangao wake kilikuwa ni chakula cha kawaida sana. Akauliza; “Hiki ndicho chakula chote?”

Ali (a.s) alimuuliza, “Je hii sio riziki ya Mwenyezi Mungu? Ndani ya moyo wangu namshukuru Mwenyezi Mungu muumba kwa kunipa riziki hii.”

Aqiil alisema “Basi afadhali nikueleze mahitaji yangu haraka ili niondoke. Ninadaiwa, hivyo basi tafadhali amrisha kulipwa kwa madeni yangu hara- ka iwezekanavyo; pia msaidie nduguyo masikini kadiri ya uwezo wako. Ili nirudi kwangu nikiwa nimeondokewa na mzigo”

“Una deni la kiwango gani? “Dirham elfu mia moja”

“Oh! Dirham elfu mia moja! Kiwango kikubwa sana! Samahani ndugu yangu sina kiwango hicho cha pesa za kukupa; lakini subiri hadi wakati wa kulipa mishahara. Nitatoa katika fungu langu na kukupa, ndio ushirikiano na undugu. Kama familia yangu na watoto hawangekuwa na haja ya matu- mizi yao ningekupa fungu langu lote.”

“Unasema nini?!! Yaani nisubiri hadi utakapolipwa mshahara wako? Hazina ya umma iko mikononi mwako na unaniomba nisubiri hadi utakapopata mshahara ndipo unipe kutokana na fungu lako! Unaweza kutoa kiasi upendacho kutoka kwenye hazina ya umma! Basi mbona unani- taka nisubiri hadi siku hiyo? Hata hivyo, fungu lako ni kiasi gani? Hata kama utanipa fungu lako lote utaniondolea kiwango gani cha shida yangu?”

“Nashangaa kusikia mapendekezo yako. Inatuhusu vipi kati yangu na wewe kama kuna pesa kwenye hazina ya Waislamu au la? Sisi ni kama Waislamu wengine. Kwa kweli, wewe ni ndugu yangu na lazima nikusai- die iwezekanavyo, lakini kutokana na pesa zangu binafsi, siyo katika haz- ina ya umma.”

Mabishano yaliendelea na Aqiil akamuomba na kumsisitizia Ali kwa kila njia. Alisisitiza kuwa Ali ampe kutoka kwenye hazina ya waislamu. Sehemu waliokuwa wameketi waliliona soko la mji wa Kufa na wangeweza kuyaona masanduku ya pesa ya wafanyabiashara. Ali (a.s) alisema; “Kama bado unasisitiza na hauko tayari kunisikiliza, basi nina wazo jingine kwa ajili yako. Ukilifuata utalipa madeni yako yote na utabaki na pesa nyingi!”

“Ni wazo lipi hilo?”

“Pale chini kuna masanduku ya pesa. Pindi tu soko litakapofungwa na kukawa hakuna mtu hapo, nenda na uyavunje hayo masanduku na uchukue chochote utakacho.”

“Ni makasha ya akina nani”

“Ni mali ya watu masikini wa soko hili. Wanahifadhi pesa zao humo.” “Ajabu! Unaniambia niibe pesa za watu masikini ambao wamezipata kwa kazi zao ngumu na wamekwenda nyumbani wakaziwacha hapo kwa kumuamini Mwenyezi Mungu?”

“Basi kwa nini unanisisitizia nikufungulie hazina ya serikali? Ni mali ya watu gani? Hii pia ni ya watu hao hao ambao wamelala kwenye nyumba zao bila ya wasiwasi na kwa starehe. Sawa, basi nina wazo lingine, lifuate kama utapenda.”

“Ni wazo gani hilo?”

“Kama uko tayari basi chukua upanga wako na mimi nitachukua wangu. Mji wa zamani wa Hirah hauko mbali na hapa. Kuna wafanyabiashara wakubwa na matajiri, twende huko tumvamie na tumshambulie mmoja wao wakati wa usiku na tumnyang’anye mali nyingi’’

“Ndugu yangu, sikuja hapa kwa wizi na unyang’anyi kwamba ndiyo unishauri mambo hayo. Nakuomba tu uwaamrishe waweka hazina wanipe pesa ambazo ziko chini ya mamlaka yako ili niweze kulipa madeni yangu.”

“Kama tukiiba mali ya mtu mmoja siyo bora zaidi ya kuiba mali ya mamil- ioni ya Waislamu? Ni vipi kwamba kuchukua mali ya mtu mmoja binafsi kwa upanga ni wizi na kunyakua mali ya umma sio wizi?” Unavyochukulia ni kuwa wizi unamaanisha tu kumvamia mtu binafsi na kumnyang’anya mali yake kwa nguvu. Wizi wa aina mbaya zaidi ni ule ambao unanishau- ri na kunisisitizia mimi kuufanya hivi sasa.”
Habari zilizosikika mara kwa mara kutoka Makka kwa kabila la Bani Ghiffar zilimvutia Abu Dhar, bwana ambaye alikuwa mtu mdadisi. Alikuwa anataka kujua kwa kina maendeleo yale yaliyokuwa Makka, laki- ni habari potofu ambazo alikuwa akipata mara kwa mara kutoka kwa watu binafsi zilikuwa hazimkinaishi.

Jambo la wazi tu alilojua ni kuwa kuna sauti ngeni imezuka kule Makka na wenyeji wake wanafanya juhudi ili kuinyamazisha. Lakini ni sauti gani hiyo mpya, na kwa nini watu wa Makka walikuwa wakiipinga? Haya ndiyo maswali yaliobaki bila ya kujibiwa. Alimueleza nduguye aliyekuwa akien- da Makka, kuwa, “Watu wananiambia kuwa huko Makka ametokea mtu na ameleta habari mpya, na yeye anadai kuwa amefunuliwa habari hizo kuto- ka kwa Mungu. Kwa vile unaelekea Makka, nichunguzie mambo hayo na uniletee habari kamili.”

Siku zikapita huku akimsubiri kaka yake kwa hamu. Aliporudi Abu Dhar alimwambia, ‘‘Nipe habari ya mambo yalivyo huko?”

“Kulingana na udadisi wangu yeye ni mtu ambaye anawaita watu kwenye maadili mema pia ameleta maneno ambayo sio mashairi.”

“Nilikuwa nataka ufanye uchunguzi makini zaidi na wa kina. Hizi habari ulizoleta hazitoshi kwa lengo langu. Afadhali niende mwenyewe kujua ukweli.” Alibeba mkoba wake kisha moja kwa moja alielekea Makka. Alikuwa amedhamiria sana kukutana na yule bwana ambaye ameleta maneno mapya na angepeda kusikia maneno hayo kutoka kwenye kinywa chake mwenyewe. Lakini hakumjua mtu huyo wala hakuona umuhimu wa kuuliza kwa wengine kumhusu.

Hali ya Makka ilikuwa mbaya kwa dhuluma na kuogofya. Bila kudhi- hirisha nia yake kwa mtu yeyote alikuwa akichunguza kila mahali huku akisikiliza mazungumzo ya watu karibu naye akitumaini kupata dalili. Msikiti wa Makka ndio ulikuwa kituo cha habari ya matukio yote. Ndipo alipokwenda na mzigo wake mgongoni. Usiku ulifika lakini hakupata habari yoyote. Aliamua kujinyoosha kidogo. Baadaye kijana fulani alipita karibu na alimuangalia Abu Dhar kwa macho ya kupeleleza na kwenda zake. Kumuangalia kwake kulikuwa na maana kubwa kwake. Aliona huen- da huyo bwana mdogo ndiye angelifaa kumueleza siri yake. Alimfuata lakini alirudi bila kuthubutu kusema naye.

Siku ya pili pia aliketi Msikitini mchana kutwa kwa makini akitafuta kidokezo chochote kile lakini hakufanikiwa.

Usiku ulifika na akajinyoosha mahala pale pale. Kijana yule alikuja tena kwa heshima na akasema: “Wakati haujafika wa wewe kwenda nyumbani kwako na kulala huko?” Baada ya kusema hivyo alimchukua nyumbani kwake. Abu Dhar hakumfunulia siri yake usiku huo, wala bwana mdogo hakumuuliza. Asubuhi Abu Dhar alimuaga na akaenda msikitini kuendelea na uchunguzi wake. Siku hiyo pia ilipita na usiku ukafika na hakuweza kupata chochote kutokana na mazungumzo ya watu. Kijana yule alimjia tena na akaenda naye hadi kwake, lakini wakati huu alizungumza.

“Waweza kuniambia ni kwa nini umekuja katika mji huu?” “Nitakueleza tu kama utaahidi kunisaidia.”

“Nakuahidi nitajaribu kadiri ya uwezo wangu kukusaidia ”

“Ukweli ni kwamba tumekuwa tukisikia kutoka miongoni mwa makabila yetu kwamba kuna bwana amezuka huku Makka na ameleta mazungumzo fulani akidai yametoka kwa Mungu. Nimekuja ili nimuone na nimchunguze. Kwanza nieleze unaamini nini kuhusu yeye? La pili, unaweza kunielekeza kwake?”

Nakuhakikishia kuwa yuko kwenye haki na anayoyasema yanatoka kwa Mwenyezi Mungu. Nitakupeleka kwake asubuhi. Lakini kama ujuavyo hawa watu wakijua, maisha yako na yangu yatakuwa hatarini. Kesho asubuhi nitatembea mbele yako na utanifuata nyuma kwa mbali kidogo, kama nitaona hatari yoyote nitasimama na kuinama chini kama mtu ambaye anamwaga kitu kutoka kwenye chungu, kisha utoroke. Na kama hakuna hatari basi utanifuata popote niendapo.”

Asubuhi iliyofuata kijana huyo ambaye alikuwa si mwingine bali ni Ali alitoka kwenye nyumba yake, na Abu Dhar akamfuata. Bahati nzuri njiani kulikuwa hakuna matatizo yoyote na walifika kwa Mtume (s.a.w.w) kwa salama.

Alifanya uchunguzi makini kuhusiana na tabia ya Mtume (s.a.w.w) na pia kusikiliza aya za Qur’ani. Haukupita muda mrefu akasilimu kwa moyo wake wote. Alichukuwa ahadi kwa Mtume (s.a.w.w) kuwa hatasikiliza lawama yoyote katika njia za Allah maishani mwake na atazungumza kweli ingawa itakuwa chungu kwa upande mwingine.

Mtume (s.a.w.w) alimwambia “Sasa urudi kwa makabila yako na ukawalinganie katika Uislamu hadi utakapopata amri nyingine kutoka kwangu.” Akasema, “Sawa kabisa; lakini kabla sijaondoka katika mji huu nitakwenda mbele ya watu hawa na kutangaza wito wa Uislamu mbele yao wapende wasipende, lolote liwalo.”

Alikwenda moja kwa moja hadi katikati mwa jiji (Msikitini) na akasema kwa sauti mbele ya umati wa Makureshi. “Nashuhudia kuwa hapana mola ila Allah na Muhammad ni mja na Mtume Wake. ”

Waliposikia mwito huo kutoka kwa mtu wasiyemjua, watu wa Makka walimkimbilia upesi na kama Abbas bin Abdul Muttalib asingekuja kumuokoa wangemkatakata vipande vipande. Abbas alisema: “Huyu bwana ni wa kabila la Ghifar, na misafara ya biashara ya maquraishi kati ya Makka na Syria hupitia kwenye ardhi yao. Hamfikirii kwamba mkimuua mmoja wa watu wao hamtakubaliwa kamwe kupita kwenye nchi yao kwa amani?

Abu Dhar aliokolewa kutoka mikononi mwao. Hata hivyo hakuridhika. Alisema, “Kwa mara nyingine nitarudia mwito huu wacha hawa watu wasikie kile ambacho hawataki kukisikia kabisa. Kama wakikisikia mara kwa mara watakizoea.”

Kesho yake alirudia maneno yale yale tena. Wale watu wakamshambulia na Abbas ambaye alikuwepo hapo akamuokoa kutokana na ukatili wao.

Baada ya hapo kulingana na amri ya Mtume (s.a.w.w), alirudi nyumbani na akaanza kulingania Uislamu miongoni mwa kabila lake. Wakati Mtume (s.a.w.w) aliguria Madina, Abu Dhar naye alikwenda na kubaki huko Madina hadi mwisho wa maisha yake. Alikuwa mkweli na mwenye msi- mamo na kutokana na sifa za uadilifu wake alifukuzwa na kuhamishwa wakati wa khalifa Uthman, mwanzoni kwenda Syria na baadaye mahali palipoitwa Rabdha karibu na Madina. Huko alifariki kifo cha upweke. Mtume (s.a.w.w) alikuwa amesema kuhusu yeye:

“Mwenyezi Mungu amrehemu Abu Dhar! ataishi peke yake atakufa peke yake, na Siku ya Kiyama atafufuliwa peke yake.
Muawiyah alikuwa akitawala Syria kama gavana wake kwa muda uliokaribia miaka kumi na sita; na alikuwa akipanga kwa siri kunyakuwa ukhalifa akitumia vizuri kila fursa iliyowezekana. Kisingizio chake kizuri cha yeye kuasi dhidi ya Mamlaka Kuu na kutangaza ukhalifa wake mwenyewe kilikuwa ni kuuawa kwa Khalifa Uthman. Muawiyah haku- fanya lolote kuhusiana na maombi ya Uthman alipotaka msaada alipokuwa hai bado. Bila shaka alikuwa akisubiri auwawe ili aweze kutumia nafasi hiyo kama kisingizio cha mpango wake. Uthman akauwawa na Muawiya aliamua kutumia fursa ya hali hiyo kwa lengo lake mwenyewe.

Kwa upande mwengine, watu baada ya kuuliwa Uthman, walijikusanya nyuma ya Ali (a.s) (ambaye kwa sababu fulani alisita kuchukua jukumu la ukhalifa) na wakatangaza kiapo chao cha utii kwake. Ali (a.s) alipotizama na kuona jukumu hilo sasa limegeuziwa kwake rasmi, alikubali na ukhali- fa huo ukatangazwa rasmi mjini Madina, ambao ulikuwa mji mkuu na kituo cha ulimwengu wa kiislamu enzi hizo. Maimbo yote yaliyokuwa chini ya utawala wa kiislamu yalikubali kumtii – isipokuwa Syria uliokuwa chini ya uongozi wa Muawiyya. Alikataa kutoa kiapo cha utii kwa Ali (a.s). Na kumtuhumu Ali (a.s) kuwa aliwapa hifadhi wauwaji wa Uthman. Muawiyya aliandikisha idadi kubwa ya wapiganaji wa Syria na akajiandaa kutangaza uhuru wa jimbo lake.

Baada ya kumaliza maswala ya vita vya Jamal (ngamia), Ali (a.s) alielekeza nadhari yake kwa Muawiyah. Alimuandikia barua kadhaa, bila mafanikio. Pande zote mbili zilisogeza askari kwa kukaribiana. Abul Aawar Salmi ndiye aliongoza kikosi kilichosonga mbele upande wa Muawiyah na Malik Ashtar upande wa jeshi la Ali (a.s). Walikutana ufuk- weni mwa mto Furat.

Maelekezo yake Ali (a.s) kwa mkuu wa jeshi lake yalikuwa kwamba wao wasiwe wa kwanza kushambulia. Lakini Abul Aawar alifanya shambulizi kali kwa nia ya kuwatia hofu jeshi la Ali (a.s). Hapo Malik akawarudisha nyuma kabisa wapiganaji wa jeshi la Syria. Salmi alianza kufikiria mkakati mpya. Alikwenda hadi Ghat, mteremko kwenye ukingo wa Furati, sehemu pekee iliyokuwa bora ya kupatia maji. Aliwasambaza warusha mikuki na mishale wake kwenye eneo hilo na kuwazuia Malik na wanajeshi wake kukaribia sehemu hiyo. Baada ya muda mfupi Muawiyah aliwasili na jeshi kubwa. Muawiyah alifurahishwa sana na hatua ya mkuu wa jeshi lake na akaamua kuongeza idadi ya wanajeshi wanaolinda eneo la njia ya kufikia mto huo.

Wanajeshi wa Ali (a.s) waliwekwa kwenye dhiki kutokana na upungufu wa maji. Muawiyah kwa furaha tele alisema: “Huu ndio ushindi wetu wa kwanza.” Ila mtu mmoja tu, Amr bin Al-Aas, waziri muerevu wa Muawiyah hakufikiria kuwa hiyo ilikuwa sera nzuri. Kwa ule upande mwengine, Ali (a.s) mwenyewe alikuwa amewasili na kupashwa habari kuhusiana na hali iliyojiri. Alimtuma Saasa’a na barua kwa Muawiyah, ikimjulisha:

“Sisi tumefika hapa, lakini vyovyote iwezekanavyo hatutaki vita vya kuuwana baina ya Waislamu. Kwa kweli tunatarajia kusuluhisha tofauti zetu kwa mazungumzo na maelewano. Lakini tumeshuhudia kuwa wewe na wafuasi wako mumeanza kutumia silaha za uharibifu kabla ya kujaribu lolote. Isitoshe umewanyima maji watu wangu. Waelekeze watu wako kuacha wafanyalo, ili tuweze kuanza mazungumzo. Bila shaka kama ham- taki lolote ila vita sisi hatuogopi.”

Muawiyah aliposhauriana na washauri wake, fikra ya jumla iliyokuwepo ni kutumia hiyo fursa adimu ya kipekee na kupuuza hiyo barua. Amr bin Al- Aas peke yake ndiye aliyepinga fikra hiyo. Alisema, “Mnakosea, ukweli ni kwamba Ali (a.s) na watu wake hawataki kuanza wao vita, na ndio maana wamenyamaza kimya kwa sasa na kujaribu kuwahimiza mubadili mipangilio yenu kwa kupitia barua hii. Msidhani kuwa watarudi nyuma kama mtapuuza barua yao na muendelee kuwanyima maji. Kwa sababu hapo sasa watachukua silaha na hawatatosheka hadi watakapowatoa kwa fedheha kwenye mto Furati.”

Lakini wengi wa washauri wa Muawiyah walionelea kuwa kuwanyima maadui maji kutawadhoofisha na kuwalaz- imisha kurudi nyuma. Muawiyah mwenyewe alikubaliana sana na wazo hilo. Mjadala huo ulifika kikomo. Sa’asa aliomba majibu; Muawiyah, aki- tumia mbinu ya ucheleweshaji alimwambia kuwa atatuma majibu baadaye. Kisha aliwaagiza wanajeshi wake wanalinda maji yale wawe makini zaidi na wazuie kuja na kuondoka kwa wanajeshi wa Ali (a.s).

Maendeleo haya yalimsikitisha Ali (a.s), kwa sababu yaliondoa matumaini yote ya kumaliza hali hii kwa amani kwa njia ya mazungumzo, na ilionye- sha kuwa upande wa pili hauna nia nzuri. Iliyobaki hivi sasa, ni kutumia mabavu. Ali (a.s) aliwahutubia wanajeshi wake hotuba fupi nzito, iliyokuwa na madhumuni yafuatayo:

“Watu hawa wameanza dhulma na kufungua mlango wa mgogoro na kuwakaribisha kwa uhasama. Wana njaa ya vita na wanadai vita na umwa- gaji damu kutoka kwenu. Wamewanyima maji. Hivi sasa inawabidi mch- ague moja kati ya hizi njia mbili, hakuna ya tatu. Ima mkubali kudhalil- ishwa na kuonewa na mbaki na kiu kama mlivyo, ama mtoe kiu cha mapanga zenu kwa damu zao chafu ili hatimae muondoe kiu chenu na maji yale matamu. Kifo ni kuishi maisha ya kushindwa na udhalilifu, na uhai ni kuwa mshindi hata kama ni kwa gharama ya kifo. Kwa hakika, Muawiyah amekusanya idadi kubwa ya wajinga na waliopotoka; na anatumia vizuri fursa ya ujinga wao, hivyo kwamba wameweka shingo zao kwa shabihio la mishale ya kifo.”

Khutba hii iliwatingisha wanajeshi wa Ali (a.s) na kufanya damu yao ichemke. Walifanya shambulio kali kiasi cha kuwalazimu wanajeshi wa Muawiyah kurudi nyuma na wao wakuchukua umiliki wa sehemu ile.

Amr bin Al-Aas (ambaye utabiri wake hivi sasa unaonekana wa kweli) alimwambia Muawiyah: “Wakati huu kama Ali (a.s) na wanajeshi wake watakulipa na ile sarafu yako mwenyewe (vitendo vyako) utafanyaje? Je! Waweza kuitwaa tena sehemu ile kwa mara ya pili kutoka kwao?” Muawiyah alimuuliza, “Kwa mtazamo wako, Ali atashughulika vipi nasi sasa?”

“Naamini, Ali hatofanya kama vile ulivyofanya wewe. Yeye hatotunyima maji. Yeye hakuja hapa kwa matendo kama haya.”

Wanajeshi wa Ali (a.s) baada ya kuwatoa wanajeshi wa Muawiyah kutoka sehemu ile (Ghat), walimuomba Ali (a.s) ruhusa ya kupalinda na kuzuia maadui kuteka maji. Ali (a.s) aliwaambia, “Msiwanyime maji. Hii ni mbinu ya wajinga. Siruhusu mikono yangu kufanya vitendo kama hivyo. Nitakwenda kujadiliana nao kwa misingi ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu (s.w.t). Lau watakubaliana na mapendekezo yangu, ni vema na kheri; na lau watakataa, nitapigana nao, lakini kiungwana na si kwa kuwanyima maji. Sitoweza kamwe kufanya jambo kama hilo na sitawadhulumu kwa kuwawekea upungufu wa maji.

Baada ya muda usio mrefu baadaye wanajeshi wa Muawiyah walikuwa wakija sehemu hiyo na wakiteka maji bega kwa bega na wanajeshi wa Ali (a.s), na hakuna yeyote aliyewazuia.
Bwana mmoja mrefu mwenye misuli alikuwa akipita kwenye soko la mji wa Kufa, hatua zake zikuwa imara na za uhakika. Alikuwa na umbo zuri na uso uliobabuka na jua; mapambano kwenye uwanja wa vita yameacha alama kwenye mwili wake na pembeni ya moja ya jicho lake palikuwa na mpasuko. Mchuuzi mmoja, kwa kuwafurahisha marafiki zake, alimwagia ukufi wa taka mwilini mwake. Yule bwana aliendelea kutembea vile vile bila ya kubadili mwendo wala kumuangalia yule muuza duka. Alipokuwa amekwenda, mmoja wa marafiki wa yule mchuuzi alimuuliza:

“Je huyu bwana uliemfanyia ufedhuli hivi punde unamjua ni nani?” aka- jibu, “La simtambui, alikuwa ni mpita njia tu kama wengine wanaopita hapa kila siku. Lakini hebu niambie, ni nani mtu yule?”

“Ajabu! Hamkumjua? Alikuwa ni Malik Ashtar, amiri jeshi mkuu maarufu wa Ali.”

“Ni ajabu kweli! Ashtar huyu huyu ambaye ujasiri wake hugeuza moyo wa simba kuwa maji na ambaye kutajwa kwa jina lake hufanya maadui zake watetemeke kwa hofu?”

“Ndio, yule alikuwa ni Malik Ashtar mwenyewe!”

“Ole wangu! nimefanya nini? Sasa atatoa amri ya kuniadhibu vikali. Ni lazima nimkimbilie sasa hivi nikamtake radhi na kumuomba msamaha kwa adabu yangu mbaya”

Alimkimbilia Malik. Akamuona akigeuka kuelekea msikitini, alimfuata hadi msikitini na kumkuta tayari ameanza kuswali. Alingojea hadi alipo- maliza kuswali. Kwa unyenyekevu kabisa alijitambulisha na akamuambia; “Mimi ndiye yule bwana ambaye ametenda kitendo cha ujinga na kutokuwa na adabu mbele yako”

Malik akamwambia; “Wallahi sikuja msikitini bali ni kwa ajili yako; kwa sababu nilijua kuwa wewe ni mtu jahili na mpotofu na unawapa watu taabu bila ya sababu. Nilikuonea huruma na nimekuja kukuombea na kumuom- ba Mwenyezi Mungu akuongoze kwenye njia sahihi. Hapana, kamwe sikuwa na madhumuni kama hayo yaliyokufanya ukawa muoga.
Baada ya kifo cha Ali (a.s) na Muawiyah kuchukua mamlaka na ukhalifa, alijaribu kulazimisha uhusiano baina yake na wafuasi halisi wa Ali (a.s). Alifanya jitihada kubwa kuwataka wafuasi hao wakiri kuwa uhusiano na Ali (a.s) haukuwa na manufaa wala maslahi yeyote kwao. Bila ya shaka wafuasi hao walipoteza mali na vitu vyao vingi kwa sababu ya uhusiano huo. Muawiyah alikuwa na hamu sana ya kusikia majuto na malalamishi ya hao wafuasi kuhusiana na usuhuba wao na Ali (a.s), lakini matumaini yake hayo hayakufua dafu.

Wafuasi hao baada ya kifo cha Ali (a.s) walitambua ubora na utukufu wake zaidi. Vile walivyojitolea muhanga kwa hali na mali zama za uhai wake, baada ya kifo chake walifanya zaidi ya hivyo, kwa kumpenda kwa msi- mamo wake na kwa kudumisha kazi yake. Wafuasi hao walikabiliana na misukosuko na kupambana na mitihani kishujaa. Na matokeo yake ni kwamba juhudi za Muawiyah zilitoa natija tofauti na ile iliyokuwa iki- tarajiwa.

Adi mwanae Hatim, aliyekuwa mkuu wa kabila la Tai ambaye aliheshimi- ka sana baina ya watu wakabila hilo, alikuwa ni mtu mwaminifu na mwenye elimu miongoni mwa maswahaba na wafuasi wa Ali (a.s). Adi, alikuwa na vijana wakiume wengi. Yeye, wanawe na watu wa kabila lake walikuwa daima tayari kujitoa muhanga kwa ajili ya Ali (a.s). Watoto wake watatu wa kiume kwa majina ya Tarfa, Turaif, na Tarif waliuwawa katika vita vya Siffin chini ya bendera ya Ali (a.s). Muda ukapita; Ali akauawa kishahidi; Muawiya akapora ukhalifa; na Adi siku moja alikutana ana kwa ana na Muawiya.

Ili kufufua zile nyakati zake za huzuni na kumfanya akiri ni madhara kiasi gani aliyapata katika uhusiano wake na Ali (a.s). Alimuuliza: “Ni lipi lililowapata vijana wako watatu, Tarfa, Turaif na Tarif ?”

Adi alijibu: “Waliuwawa wote kwenye vita vya Siffin chini ya bendera ya Ali (a.s).”

Muawiyah aliendelea, “Ali hakukutendea haki.” Adi alimuuliza Muawiyah: “Kwa nini?”

“Kwa sababu aliwaelekeza vijana wako vitani na wake akawahifadhi.” Adi alisema: “ Mimi ndio sikumtendea Ali (a.s) haki.”

“Kwa nini wasema hivyo?”

“Kwa sababu yeye aliuwawa na mimi ningali hai. Nilipaswa kujitoa muhanga kwa ajili yake wakati wa uhai wake.”

Muawiyah alikata tamaa kwa kuona kuwa hapati kile anachotaka. Na tena kwa upande mwengine alikuwa na hamu sana ya kusikia kuhusu mienen- do na maisha ya Ali (a.s) kutoka kwa wale walioishi naye kwa muda mrefu. Basi hapo ndipo ilimbidi amuombe Adi (a.s) amuelezee juu ya tabia ya Ali (a.s) kama alivyoshuhudia. Adi aliomba aachwe asizungumze; lakini Muawiyah alisisitiza aongee na hapo Adi akasema:

“Naapa, Wallahi Ali (a.s) alikuwa ndiye mtu muona mbali zaidi ya wengine na mwenye nguvu. Alikuwa akiongea kwa haki, na aliamua kesi kwa uwazi kabisa. Alikuwa ni bahari ya elimu na hekima. Alikuwa ni mwenye kuchukia fakhari majivuno za kidunia, na mwenye kupenda faragha na utulivu wa usiku. Alililia sana kwa ajili ya Allah (s.w.t) na alikuwa ni mwenye kumfikiria Allah sana.

Katika faragha alijichunguza nafsi yake mwenyewe na kujisikitikia kwa yale yaliyopita. Alipendelea nguo fupi na kuishi maisha rahisi. Miongoni mwetu alikuwa kama mmoja wetu. Lau kama tungelitaka chochote kutoka kwake alikuwa ni mwenye kututimizia maombi yetu. Wakati wowote tulipokuwa tukimtembelea alipendelea tuketi karibu naye bila ya kuwacha nafasi baina yetu. Mbali na unyenyekevu wote huo, kuwepo kwake kulikuwa kunatia nidhamu ya woga kiasi kwamba hatukuthubutu kutamka neno kabla yake.

Alikuwa mtukufu kiasi kwamba hatukuweza kumuangalia. Akitabasamu meno yake yalikuwa yanaonekana kama uzi wa lulu. “Aliwaheshimu watu waliokuwa waaminifu na wacha-Mungu na alikuwa mkarimu kwa masikini na wasio- jiweza. Mtu mwenye nguvu hakuwa anaogopa kutotendewa haki naye wala masikini hawakukatia tamaa uadilifu wake. Wallahi na naapa, usiku mmoja nilimuona katika sehemu yake ya ibada wakati giza la usiku lilikuwa limekizingira kila kitu; machozi yakimtiririka usoni na kwenye ndevu; alikuwa hatulii kama aliyeumwa na nyoka na alikuwa akilia kama mtu aliyefiwa.”

“Naona kama hata hivi sasa nasikia sauti yake kama alivyokuwa aki- uhutubia ulimwengu: “ Ewe dunia, wewe ndiye mwenye kunifuata na kuta- ka kunihadaa mimi? (Nenda) kamdanganye mtu mwingine. Muda wako bado haujawadia. Mimi nimekupa talaka tatu ambapo hakuna rejea. Raha yako haina thamani na umuhimu wako hauna maana. Kwa bahati mbaya! Masurufu ni machache mno, na safari nayo ni ndefu na pia hakuna swahi- ba.”

Muawiyah aliposikia maneno aliyokuwa akitamka Adi, alianza kulia, na baada ya kufuta machozi, alisema:

“Namuomba Mwenyezi Mungu ambariki Abul Hassan (Ali). Alikuwa kama ulivyomtaja. Sasa niarifu, wajihisi vipi bila yeye?”

“Najihisi kama mama ambaye mpendwa wake amechinjiwa mapajani mwake”

“Hutaweza kamwe kumsahau?”

“Hivi dunia itaniruhusu mimi kumsahau?”
Mzee mmoja mfuasi wa dini ya kikristo, alifanya kazi maisha yake yote; lakini hakuweza kujiwekea akiba ya siku za uzeeni. Na nyakati zake za mwisho alikuja kuwa kipofu pia. Uzee, umaskini na upofu viliungana mkono, hivyo basi alikuwa hana njia nyingine ispokuwa kuomba. Alikuwa akisimama pembezoni mwa njia kwa ajili ya kuomba. Watu walikuwa wakimwonea huruma na kumpa sadaka ambayo alitumia kwa chakula chake kila siku na hivyo basi aliendelea na maisha yake ya huzuni.

Siku moja Ali, Kiongozi wa Waumini alipitia kwenye njia hiyo na kum- wona muombaji huyo katika hali hiyo, na kutokana na kujali maslahi ya wengine Ali aliuliza kuhusu huyo mzee. Alikuwa anataka kujua sababu ambazo zilimfanya awe katika hali hiyo. Alikuwa hana mtoto wa kum- saidia? Ama hakuna njia nyingine ya yeye kuishi maisha ya kuheshimika katika uzee wake?”

Watu ambao walimjua mzee huyo walisogea mbele na kumjulisha Ali (a.s.) kuwa alikuwa mkristo na alifanya kazi kwa bidii kwa muda mrefu alipokuwa na macho yake, na ni kijana mwenye nguvu zake. Lakini sasa alivyopoteza ujana wake na pia akawa kipofu hakuweza kufanya kazi yey- ote; pia hana chochote alichojiwekea akiba hivyo basi kumlazimu aombe. Ali akasema: “Ajabu! Alipokuwa na nguvu mlidondoa kazi za nguvu zake, lakini sasa mumemtelekeza peke yake?”

Kisa chake hiki kinaonesha kuwa alifanya kazi alipokuwa na nguvu. Kwa hivyo ni wajibu wa Serikali na Umma kumsaidia hadi atakapofariki. Nendeni mumpe malipo ya maisha uzeeni kutoka Hazina ya Taifa.
Mahujaji walikuwa wamekusanyika Mina. Imam Sadiq (a.s.) na maswaha- ba wake walikuwa wameketi sehemu fulani wakila zabibu zilizokuwa zimeandaliwa mbele yao.

Muombaji alitokea na kuomba sadaka. Imam alichukua zabibu na kumpa lakini alikataa kuchukua na akaomba pesa, Imam alimwambia kuwa amsamehe kwa kuwa hakuwa na pesa za kumpa. Muombaji yule akaenda zake akiwa amekasirika.

Baada ya kwenda hatua chache alijiwa na wazo na akarudi na kuomba zile zabibu. Imam sasa akakataa kumpa zile zabibu pia.

Muda mfupi baadaye muombaji mwengine alitokea na Imam alichukua zabibu ili ampatie. Alizichukua huku akisema, “Namshukuru Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe vyote na ambaye amenipa riziki yangu.” Kwa kusikia matamshi hayo Imam alimwambia asubiri na akamuongezea zabibu zingine. Maskini yule alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa mara ya pili.

Imam alimwabia tena asubiri huku akigeuka kwa mmoja wa marafiki zake na kumuuliza, “Una kiwango gani cha pesa?” Bwana yule alitafuta mfukoni mwake na akapata takriban dirham ishirini ambazo alimpa yule muombaji kwa amri ya Imam.

Masikini yule alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa mara ya tatu huku akisema “Shukrani zote zimuendee Mwenyezi Mungu, Ewe Mungu wewe ndio mpaji na hauna mshirika.” Kusikia maneno hayo Imam alivua joho lake na akampa muombaji huyo. Hapo mwombaji alibadilisha shukrani zake na kuzungumza mambo ya ziada ya kumshukuru Imam mwenyewe. Kisha Imam hakumpa kitu kingine na muombaji akaondoka zake.

Marafiki na maswahaba zake ambao walikuwa mahali pale walisema: “Tulidhani kuwa kama masikini huyo angeendelea kumshukuru Mwenyezi Mungu kama hapo awali, Imam angeendelea kumpa vitu zaidi na zaidi. Lakini alipobadilisha matamshi yake na kumshukuru Imam mwenyewe Imam hakuendelea na usaidizi wake.
Waislamu walikuwa wamehamia Abyssinia kwa sababu ya mateso na adhabu za makuraishi, lakini kila mara walikuwa wakisubiri habari kutoka kwao walikozaliwa kwa hamu. Wale ambao w

Share this article

Comments 0

Your comment

Comment description

Latest Post

Most Reviews

MOST READ