Rafed English

Ukweli Uliopotea - Sehemu ya Nne

Ukweli Uliopotea - Sehemu ya Nne by : Sheikh Mu’tasim Sayyid Ahmad

 

Kitabu kilichoko mikononi mwako ni tarjuma ya kitabu cha Kiarabu kiitwacho al-Haqiqatu ‘dh-Dha’i’ah kilichoandikwa na Sheikh Mu’tasim Sayyid Ahmad. Sisi tumekiita, Ukweli Uliopotea. Kwa vile kitabu hiki ni kikubwa, sisi tumekigawa katika juzuu tano ili kiwe chepesi kusomwa na wasomaji wetu wa Kiswahili. Hiki ulichonacho mkononi mwako ni juzuu ya nne.

Kitabu hiki ni utafiti uliofanywa na mwanachuoni huyo wa Kiislamu kuhusu madhehebu za Kiislamu. Utafiti wake huu ulihusisha pia mahojiano na mijadala baina yake na na masheikh wa Kiwahabi na maustadh wake katika chuo alikosoma.

Kama kawaida katika utafiti wake, ametumia sana vitabu vya historia ya Kiislamu na vya hadithi vilivyoondikwa na wanavyuoni wa Sunni na Shia, kisha akahitimisha kwa Qur’ani Tukufu na Sunna. Baadhi ya vitabu hivyo ameviorodhesha ndani ya kitabu hiki ili msomaji aweze kuvirejelea. Lakini bahati mbaya sana mengi ya matoleo mapya ya vitabu hivyo yamefanyiwa mabadiliko na baadhi ya sehemu kuondolewa, hususan zile zinazounga mkono madai ya Shia. Ufuatao hapa chini ni mfano mdogo tu wa yanay- ofanywa katika vitabu hivyo:

Katika ukurasa wa 301 wa juzuu ya 3 ya Tafsir al-Kashshaaf iliyokusany- wa chini ya maelekezo ya Sheikh Mustafa al-Halabi (toleo la pili, 1319 A.H. liliochapishwa na Main Government Printing House ya Amiriah Bulaq ya Misri), beti zinazojitokeza ambazo kwazo Jarallah Zamakhshari, mfasiri wa al-Kashshaaf, alitangaza wazi imani yake katika uhalali wa Ushia. Lakini katika toleo la mwaka wa 1373 A.H. kutoka Printing House Istiqamah bi ‘l-Qahara, shairi lililotajwa halionekani tena.

Marehemu Allamah Sayyid Saeed Akhtar Rizvi katika kitabu chake kiitwa- cho, Uimamu, ukurasa wa 37, anaandika kushangazwa kwake kutokana na maneno yaliyoondolewa katika kitabu cha at-Tarikhat-Tabari, chapa ya Leiden (ya mwaka 1879 Miladia).

Chapa hii ya Leiden imeyanakili maneno ya Mtukufu Mtume (s.a.w.) aliyoyatumia wakati wa karamu mashuhuri ya ndugu wa karibu aliyoitayarisha ambapo katika khutba yake alisema: “Enyi watu wangu! Huyu Ali ni ndugu yangu, Wasii wangu na Khalifa wangu miongoni mwenu; msikilizeni na mtiini.” Lakini katika chapa ya Misri ya mwaka 1963, (chapa inayodaiwa kuwa imechekiwa na ile ya Leiden) maneno haya muhimu: “Wasii wangu na Khalifa wangu” yamebadilishwa na kuandikwa “kadha wa kadha” na kusomeka hivi: “Huyu Ali ni ndugu yangu na kadha wa kadha.” Huu ni msiba mkubwa.

Huu ni mchezo umefanywa na unaendelea kufanywa mpaka leo. Na lengo ni kuficha ukweli. Lakini hata hivyo, ‘ukweli siku zote unaelea’; matoleo ya zamani yapo mengi na yamehifadhiwa kwenye maktaba zetu.

Ni muhimu kufikia kila aina ya maoni katika kujaribu kuamua ukweli. Uislamu kimsingi uko dhidi ya kufuata kibubusa. Utafiti huu umefanywa ili kuwaelemisha Waislamu kwa ujumla juu ya madhehebu za Kiislamu ili kujenga maoni yao kuhusu mtazamo mzuri wa mtu mwenyewe, na ni muhimu mtu kuelewa hoja za wale ambao hakubaliani nao. Inawezekana kusemwa kwamba wale ambao hawaelewi kabisa mtazamo wa maoni tofauti, hawaelewi kwa ukamilifu (mtazamo) wa kwao wenyewe.

Tumekiona kitabu hiki ni chenye manufaa sana, hususan wakati huu wa maendeleo makubwa ya elimu katika nyanja zote, ambapo uwongo, ngano za kale na upotoshaji wa historia ni mambo ambayo hayana nafasi tena katika akili za watu.

Kutokana na ukweli huo, taasisi yetu ya Al-Itrah Foundation imeamua kukichapisha kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili kwa madhumuni yake yaleyale ya kuwahudumia Waislamu, hususan wazungumzaji wa Kiswahili.

Tunamshukuru ndugu yetu, Sheikh Harun Pingili kwa kukubali jukumu hili la kukitarjumi kitabu hiki. Vilevile tunawashukuru wale wote walioshiriki kwa njia moja au nyingine hadi kufanikisha kuchapishwa kwake.

Mchapishaji:

Al-Itrah Foundation
S. L. P. 19701
Dar-es-Salaam, Tanzania.
Kwa aliyezaliwa kwenye ngome ya umaasumu na uchamungu, na mashukio ya wahyi na uongofu, na mrithishwa wa fadhila tukufu na ukarimu.

Imwendee mwanamke mwema, na mpambanaji mtoa nasaha, aliye huru mkataaji, na ni muujiza Muhammadiyah, na ni hazina Haydaria, na ni amana Fatmiyah.

Imwendee aliyekuwa mtii wa Mwenyezi Mungu, katika hali ya siri na ya wazi, na aliyetoa changamoto kwa msimamo wake dhidi ya wanafiki na wafitini.

Imwendee aliyewatia hofu masultani wakorofi kwa msimamo wake thabiti, na alizishangaza akili kwa umadhubuti wa moyo wake, na alifanana na baba yake Ali kwa ushujaa wake, na alishabihiana na mama yake Zahra’a kwa utukufu wake na balagha yake.

Imwendee aliyenasibika na ukoo wa kinabii na uimamu, aliyetunukiwa shani ya cheo, utukufu na karama.

Imwendee shujaa wa Karbalaa bibi wa kibani Hashim.

Sayyidatiy wa Maulatiy Zaynab (a.s.).
Madhehebu Manne Chini Ya Darubini
Kwa kweli athari za Saqifa na kuugeuza ukhalifa kutoka kwa Ahlul-Bayt zimekuwa kinyume katika kila nyanja zikiathiri kinyume katika historia na elimu ya Hadithi, na elimu nyingine zisizokuwa hizo. Na athari zake za wazi zimejitokeza katika fiqhi ya kiislamu, kwa mujibu huo madarasa za kifiqhi zimekithiri na kujitenga mbali na zingine.

Historia imenakili kuwa kila jamaa yapendelea fikra za chuo chake cha kifiqhi na yaliyotokea kati yao, kama vile ilivyoweka wazi sauti zilizopanda na mzozo hadi kufikia daraja ya kukufurishana, pia imetuwekea wazi mchango wa utawala unaohukumu jinsi ulivyokuwa ukiichezea dini ya waislamu, kwa hiyo mwanachuoni anayeafikiana nayo kulingana na utashi wake yeye huwa ndio imamu wa waislamu na dola huwalazimisha watu kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja kumfuata na kumtii.

Rejea za kifiqhi zimetia nanga baada ya hali nyingi tofauti zilizojiri juu ya wanne miongoni mwa mamia ya mujtahidina na hao ni: Malik, Abu Hanifa, Shafii na Ahmad bin Hanbali. Halafu ijtihadi ilipigwa marufuku baada ya hawa na watu wote walipopewa amri ya kuwafuata hawa wanne. N

a hilo larejea katika historia ya mwaka 645 A.H. pale mamlaka iliyokuwa inatawala ilipoona kuwa masilahi yake yapo katika kuiwekea wigo ijtihadi kwa hawa masheikh wanne.

Na kundi miongoni mwa wanavyuoni lilipendelea fikra hii na walitangaza kuliunga mkono kwao. Na kundi lingine lilizingatia kitendo hiki kuwa ni kuukandamiza uhuru na kupokonya uwezo wa mtu. Ibnu Al-Qayim ametunga mlango mrefu katika kitabu Iilamul-Muwaqiina, humo amefuatilia dalili za wasemao wajibu wa kuufunga mlango wa ijtihadi na kuusimamisha, kwa dalili zenye nguvu.

Japokuwa rai isemayo ni wajibu kusimama kwenye ijtihadi za maimamu wanne zipo kinyume na dini na akili iliyo salama, ila ni kwamba ilikuwa ndio yenye ushindi kwa sababu ya kuungwa mkono rai hii na dola ambayo inadhamini maslahi yake.

Ustadh Abdul-Mutaali Swaiidiy anasema: “Kwa hakika mimi naweza kuhukumu baada ya hivi kuwa kuzuia ijtihadi kulifanyika kwa njia za kidhalimu, na kwa nyenzo za kulazimisha na kuvutwa kwa kupewa mali, na hapana shaka nyenzo hizi lau zingepatikana kwenye madhehebu yasiyokuwa haya manne - ambazo tunazifuata hii leo – jamhuri ingebaki inazifuata pia na zingekuwa zakubalika hivi sasa kwa wanaozikataa.

Basi sisi tuko huru hatulazimiki kujifunga na madhehebu hizi nne ambazo tumelazimishwa nazo kwa njia hizo mbaya, na tuko huru kurejea kufanya ijtihadi katika hukumu za dini yetu, kwa kuwa kuizuia kwake hakukufanyika ila kwa njia ya mabavu, na uislamu hauridhii ila lipatikanalo kwa njia ya ridhaa na ushauri kati ya waislamu. Kama alivyosema (s.w.t.): ‘’Na mwenendo wao ni kushauriana wao kwa wao” (Surat Shura: 38)”1

Huu ni ukweli mchungu aufikiao mtafiti mwenye insafu katika historia ya madhehebu manne, kwa haki gani wamewajibishiwa waislamu kufanya ibada kupitia mmoja wao, na kwa dalili gani wanavyuoni wamezuiliwa ijtihadi, na kwa nini wamechaguliwa hawa wanne na si wengine?! Hali wakiwepo wanavyuoni wenye elimu zaidi na bora kuliko wao. Kwa mfano:
Sufian Thauriy:
Alizaliwa mwaka 65 A. H. Alikuwa na madhehebu mahsusi lakini hakuyafanyia kazi kwa muda mrefu kwa uchache wa wafuasi, na kutokuungwa mkono na utawala. Naye ni mmoja wa wanafunzi wa Imam Sadiq (a.s.) na mhitimu wa madrasa yake, na azingatiwa kuwa miongoni mwa wanavyuoni ambao hufanyiwa safari mtu kwenda kwake kutafuta elimu, na kutoka kwake wameelezea (wasimulizi wa hadithi) ishirini elfu. Mansur alitaka amuue hakufanikiwa na alikimbia akijificha mbali naye mpaka alipokufa mwaka 161 A.H. Madhehebu yake yalibaki yakitendewa kazi mpaka karne ya nne.
Sufian Bin Uyayna:
Mwanachuoni na mwanafiqhi thabiti aliichukuwa elimu kutoka kwa Sadiq (a.s.), Zuhriy na Ibnu Diynar na wengine. Shafii amesema kumhusu: “Sijapata kumuona mwenye kutosheleza kuliko yeye katika kutoa fatwa.’’ Na ana madhehebu yalikuwa yakitendewa kazi yametoweka katika karne ya nne.
Al-Awzaiy:
Al’Awzaiy alikuwa miongoni mwa wanazuoni, madhehebu yake yalienea Sham - Syiria – na watu wa Sham walifanya ibada kwa mujibu wa madhehebu yake kwa muda, na Al-Awzaiy alikuwa akiheshimiwa na kuwa mtu wa karibu na dola. Alikuwa miongoni mwa wanaoiunga mkono na kwa minajili hiyo dola ilimfanya nembo ya kidini.

Na walipoingia watawala wa Bani Abbas walimsogeza karibu kwa sababu ya nafasi yake kwa watu wa Sham. Hivyo Mansur alikuwa anamtukuza na kumtumia alipomtambua kuwa amepotoka mbali na ali Muhammad swalawatullahi alayhim.

Lakini pamoja na hayo madhehebu ya Al-Awzaiy yalitoweka alipoainishwa Muhammad bin Uthman, mfuasi wa Shafii kuwa Kadhi wa Damascus, hapo basi hukumu ikawa kwa mujibu wa madhehebu ya Shafii na aliyalazimisha katika Sham, kiasi kwamba watu wa Sham waligeuka na kuwa mashafi mwaka 302 A.H.

Na wengine miongoni mwa makumi ya mamujtahidi mfano wa Ibnu Jarir Tabariy, Daudi Ibnu Ali Dhwahiriy, Al-Liyth Ibnu Said, A’amash, Shaabiy na wengine.

Kwa nini zilibaki madhehebu haya manne na yakaenea na si mengine?! Je maimamu wake walikuwa watu wenye elimu zaidi kuliko wengine katika zama zao?! Au ridhaa za watu zilijikusanya na kuwafanya wao ndio maimamu wao?

Haya yote hayakuwa kwa madhehebu haya manne. Yakutosha historia ambayo yathibitisha kuwepo kwa wanavyuoni ambao walikuwa na elimu zaidi kuliko wao. Kwani akili peke yake inahukumu kutokuwepo kwa sharti hili, kwa sababu kuuwekea mpaka ujuzi ni jambo gumu. Kama ambavyo kuenea kwa madhehebu haya na maimamu wake kuwa mashuhuri haikuwa katika hali na mazingira yenye uhuru na usafi wa kielimu, bali yadhihiri kwa mwenye kufuatilia hali yake kihistoria kuwa haya madhehebu yalilazimishwa juu ya waislamu katika wakati ambao waislamu hawakuwa makini katika jambo lao.

Ama watu kuafikiana na kuwaridhia ni jambo halikuwa na athari katika historia ya kiislam, bali lilikuwa kinyume kabisa. Kila watu waliipendelea madhehebu yao na walikebehi zile itikadi za wenzao, mpaka ulifikia kuwa mzozo wa kumwaga damu, maelfu ya waislamu wamekwenda muhanga, kwa minajili hiyo walikuwa maadui wanaohasmiana na waliwatendea baadhi yao utendewaji wa waliotoka nje ya dini, kiasi kwamba Muhammad bin Musa al-Hanafii ambaye alikuwa Qadhi wa Damascus, aliyefariki dunia mwaka 506 A. H. akasema: ‘’Lau ningekuwa na kauli ningechukua Jizya2 kutoka kwa mashafii.’’

Na Abu Hamidi Tusiy aliyefariki mwaka 567 A.H. anasema: “Lau ningekuwa na amri ningewawekea mahambali kodi.”

Hivyo matukio kati ya mahanafii na mahanbali na kati ya mahanbali na mashafii yalikithiri. Wakawa makhatibu wa kihanafii wanawalaani mahanbali na mashafii juu ya mimbari. Na mahambali wanaunguza msikiti wa mashafii huko Muruwu. Moto wa fitna na upendeleo kati ya mahanbali na mashafii ulilipuka huko Nisabur hivyo soko na madrasa zilichomwa moto, walikithiri waliouwawa upande wa mashafii. Halafu mashafii wanavuka kiwango katika kulipa kisasi kwao na hilo lilitokea mwaka 554 A.H. Na mfano kama huo ulitokea kati ya mashafii na mahanbali, mpaka dola ililazimika kumaliza mzozo kwa nguvu, na hilo lilitokea mwaka 716 A.H.3

Mahanbali walikuwa wanaacha kazi zao kwa amani na wanafanya fujo Baghdad, na walikuwa wanajihami kwa vipofu dhidi ya mashafii ambao waliokuwa wanakimbilia msikitini, ikiwa mtu wa madhehebu ya Shafii atawapitia, hatimaye watampiga.4

Na madhehebu mengine yanajikusanya dhidi ya Hanbali kughadhibika dhidi ya vitendo vya Ibnu Taymiyyah. Palinadiwa huko Damascus na mahali pengine kuwa: Mwenye kuwa katika dini ya Ibnu Taymiyyah mali yake na damu yake ni halali. Kwa maana ya kuwa wao hutendewa watendewavyo makafiri wapiganaji. Na kwa kulikabili hilo twamkuta Sheikh Ibnu Hatim ambaye ni Hanbali anasema: “Asiyekuwa Hanbali si mwislamu.”5 Hivyo yeye anawakufurisha waislamu wote isipokuwa

Hanbali, na kinyume chake ni Sheikh Abu Bakr al-Maghribiy, yeye ni mhutubu katika vyuo vikuu vya Baghdad, yeye anawakufurisha Hanbali wote.6

Na mengine miongoni mwa matukio ambayo yanaliza nyoyo. Baadhi ya upendeleo binafsi umefikia kuwaua wanavyuoni na wanafiqhi kwa hila, kwa kutumia sumu. Na mwanachuoni huyu Abu Mansur aliyefariki mwaka 567 A.H. mahanbali wamemuuwa kwa sumu kwa msukumo wa chuki dhidi yake. Ibnu Al-Jawzi amesema: “Kwa kweli Hanbali walimtuma mwanamke kwa hila alikuja kwake na sahani ya haluwa, na akasema: ‘Ewe bwana wangu hii ni katika ufumaji wangu.’ Alikula yeye, mkewe, mtoto wake na mtoto wake mdogo, na hatimaye wakawa maiti, alikuwa miongoni mwa wanavyuoni wa kishafiiy waliojitokeza.”7 Na wengi walio mfano wao miongoni mwa wanavyuoni waliouliwa na upanga wa chuki binafsi.

Ni kama hivi kila kundi lilikuwa linafanya upendeleo kwa ajili ya maimamu wao kiasi kwamba wao waliweka Hadithi za ubora wao na walizinasibisha kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) kwa uwongo na uzushi, kwa hiyo zikawatoa nje ya mipaka ikubaliwayo kiakili iwezayo kupimika. Na mfano wa Hadithi walizomnasibishia Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.): “Kwa hakika Adam alijionea fahari kwa mimi, na mimi najionea fahari kwa mtu miongoni mwa umma wangu jina lake ni Nuuman.” Kwa sura nyingine imekuja: ‘’Manabii wanajionea fahari kwa mimi, na mimi najionea fahari kwa Abu Hanifa, mwenye kumpenda amenipenda mimi na mwenye kumchukia amenichukia mimi.’’8

Kwa hakika walikumbwa na uvukaji mpaka kumhusu Abu Hanifa mpaka wakasema katika fadhila zake: Mwenyezi Mungu amemfanya awe mahsusi kwa sheria na kwa karama, na katika jumla ya karama zake ni kuwa al-Hidhru alikuwa akija kwake kila siku wakati wa asubuhi na alikuwa akijifundisha kwake hukumu za sheria muda wa miaka mitano, na alipokufa al-Hidhru alimuomba Mola wake akasema: “Ewe Rabi, ikiwa mimi nina daraja kwako mpe idhini Abu Hanifa anifundishe kutokea kaburini kama kawaida yake ili niwafundishe watu sheria za Muhammad kwa ukamilifu, ili nipate tarika.” Mola wake akamkubalia ombi hilo. Hidhru darasa lake lilitimia kwa Abu Hanifa hali akiwa kaburini mwake. Mpaka mwisho wa hadithi hii ambayo husomwa kwenye majlisi za kihanafi misikitini mwao huko uhindini.”9

Na watu wa madhehebu ya Malik wamejigamba mambo mengi kumhusu imamu wao, miongoni mwayo ni kuwa: Imeandikwa pajani kwake kwa kalamu ya Kudura: ‘’Malik ni hoja wa Mwenyezi Mungu katika ardhi yake.’’ Na kuwa yeye anahudhuria kwa maiti miongoni mwa swahiba zake kaburini mwao na kuwaondoa malaika wawili mbali na maiti, wala hawaachi wamuhesabu amali zake.10

Na imeelezwa kuwa kitabu chake al-Muwatau kilitupwa majini wala hakikulowa.

Wanahambali wamesema kumhusu imamu wao: ‘’Ahmad bin Hambali ni imamu wetu na asiyeridhia ni mtu wa bidaa. Hivyo basi kulingana na kanuni hii waislamu wote wasioukubali uimamu wa Ahmad ni watu wa bida.’’

Na wanasema kuwa hajafanya jambo la uislamu yeyote baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) kama alivyofanya Ahmad bin Hanbali, wala Abu Bakr Swiddiq hakufanya mfano wake. Na kuwa Allah alikuwa akilizuru kaburi lake. Kama alivyoeleza Ibnu al-Jawziy katika Manaqib Ahmad Uk. 454, amesema:

“Amenihadithia Abu Bakr bin Makarim Ibn Abi Ya’aliy al-Harbiy – alikuwa Sheikh mwema – Amesema: ‘Ilikuja mvua nyingi mno katika baadhi ya miaka kabla mwezi wa Ramadhani haujaingia kwa siku chache, usiku mmoja nililala katika mwezi wa Ramadhan niliona usingizini kana kwamba nimekuja kwenye kaburi la imamu Ahmad bin Hanbali namzuru kama kawaida yangu. Nikaona kaburi lake limeambatana na ardhi kadiri ya safu – yaani safu ya mchanga au tofali - au safu mbili, nikasema: Hakika haya yamelifika kaburi la Imam Ahmad kwa sababu ya wingi wa mvua. Ghafla nikamsikia akisema toka kaburini:

“‘Hapana hiyo ni haiba ya al-Haqi Azza Wajalla, alinizuru nikamuuliza siri ya ziara yake kwangu kila mwaka, Azza Wajalla akasema: Ewe Ahmad ni kwa sababu wewe umeyanusuru maneno yangu kwa hiyo yanaenezwa na yanasomwa katika mihrabu.’ Niliuendea mwana ndani wake na kuibusu halafu nilisema: Ewe Bwana wangu nini siri ya kuwa halibusiwi kaburi la yeyote ila kaburi lako? Aliniambia: Ewe mwanangu hii sio karama kwangu lakini hii ni karama ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) kwa sababu mimi nina vijinywele kutoka kwenye nywele zake swalallahu Alayhi Wasalam, mwenye kunipenda mimi ananizuru katika mwezi wa Ramadhani. Alisema hivyo mara mbili.”

Na mengine miongoni mwa sifa njema ambazo zajulisha upendeleo wao na uvukaji wao mipaka uliyo mbaya mno, na umejitokeza upendeleo huu waziwazi kabisa katika mashairi yao.

Mshairi wa kihanafii akasema: Madhehebu ya Nuuman madhehebu bora, mwezi ung’arao na ni sayari bora.

Na mshairi wa kishafii anasema: Mfano wa Shafii kati ya wanavyuoni ni mfano wa Badru katika nyota za mbingu.

Mwambie alinganishwaye na Nuuman kwa ujinga. Je giza hulinganishwa na nuru!

Na mshairi wa Malik asema: Wakisema vitabu vya elimu ni hai, je kitabu al’Muwatau ni utunzi wa Malik!

Hali ni kama hiyo kila mmoja avutia moto kwenye mkate wake, na anamshabikia imamu wake, na kujionea fahari madhehebu yake na anajiepusha mbali na madhehebu nyingine mpaka ilisemwa: ‘’Kwa kweli mwenye kuingia uhanafii huvuliwa, na mwenye kuingia ushafii huadhibiwa.’’11 Na Bw. Sabakiy ameeleza katika kitabu Tabaqatus-Shafiiyyah kwa kauli yake: “Hivyo huyu Abu Said aliyefariki mwaka 562 A.H. alikuwa madhehebu yake ni Hanafiya na aligeuka na kuwa Shafiiya, ndipo alipata taabu na kutihaniwa kwa ajili hiyo.

Na huyu Samaniy alipohama madhehebu ya Hanafi alipata mtihani na taabu, na zilifanyika vita, na moto wa fitna ulikolezwa kati ya makundi mawili, ilikuwa unajazwa kati ya Khurasani na Iraqi, na kwa ajili hiyo watu wa Muruu waliyumba myumbo wa kufadhaisha, mlango wa matatizo ulifunguliwa.

Na watu wa rai walijiambatanisha na watu wa hadithi, na walikweda mlangoni kwa Sultani…”12 Mpaka mwisho wa aliyosimulia.

Matukio kama haya ni mengi hayahesabiki. Na tuliyotaja yanatosha kama mfano wa harakati wa tofauti na upendeleo kati ya madhehebu manne, mpaka ikawa kuficha madhehebu ni lazima.

Abu Bakr Muhammad bin Abdil-Baaqi aliyefariki mwaka 535 A.H., alikuwa Hambalia, anaelezea hali ya kuficha kwa kauli yake: “Hifadhi ulimi wako usihalalishe vitatu: Jino, mali uwezavyo na madhehebu.”

Zamakhshariy amebainisha tofauti na ukali wa kulumbana kati ya madhehebu kwa kauli yake:

“Wakiuliza madhehebu yangu siyadhihirishi.
Nitayaficha ufichaji wa kusalimika kwangu.

“Ukisema ni Hanafiya, watasema kuwa:

mimi nahalalisha Talaa, nacho ni kinywaji haramu.

“Ukisema ni Shafiiya, watasema kuwa:

mimi nahalalisha ndoa ya binti hali binti ni haramu.

“Ukisema ni Malikiya, watasema kuwa:

mimi nawahalalishia kula mbwa nao ni wao.

“Ukisema ni Ahlilhadithi na kundi lake,
watasema beberu hajui wala hafahamu.”13
Kisimamo Pamoja Na Maimamu Wa Madhehebu Manne
Kwa hakika kufanya utafiti kuhusu historia ya mimamu wa madhehebu manne kuna ugumu. Kwa kuwa kuzipata habari zao ni ima iwe kwa kuzinakili kutoka kwa wenye kuwapendelea walio na uvukaji mipaka kuwahusu wao, au iwe kupitia maadui zao wanaowasingizia, na kati ya safu mbili hizi zinazopingana ni vigumu kutoka na mtizamo wa pekee ulio safi.

Ahmad Amin anasema: “Kama ambavyo upendeleo wa kimadhehebu umewafanya baadhi ya wafuasi wa kila madhehebu wazushe habari ili kuinua hadhi ya imamu wao, kutokana na mlango huu ni Hadithi walizoeleza kuwa Nabii (s.a.w.w) alibashiri kumhusu kila imamu, mfano wa ilivyoelezwa kuwa Nabii (s.a.w.) alisema kuhusu watu wa Iraqi:

‘Mwenyezi Mungu ameweka hazina ya elimu yake katika wao.’ Na mfano:

‘Katika umma atakuja kuwepo mtu ataitwa Nuuman bin Thabiti, kuniya yake itakuwa ni Abu Hanifa, mkononi mwake Mwenyezi Mungu atahuisha Sunna yangu katika Uislamu.’ Mpaka mwisho imefikia kudhania kuwa Taurati imembashiri Abu Hanifa. Ni kama hivyo wamefanya baadhi ya mashafii kumhusu Shafii na mamaliki kumhusu Malik, na halikuwatosha hilo. Kwa minajili hiyo imekuwa vigumu kwa mtafiti kuelewa historia sahihi ya kila imamu. Ilikuwa kila kikija kizazi kinazidisha fadhila za imamu wake.”14

Ni Abu Hanifa peke yake amepata bahati ya fadhila hizi kwa kuwekewa kundi la vitabu. Tunataja miongoni mwavyo kwa mfano tu: Uqudul- Marjani Fii Manaqibi Abi Hanifan-Nuuman cha Abu Ja’far at-Tahawiy, Manaqibu Abihanifa cha al-Khawarzamiy, al-Bustanu Fii Manaqib Ibni Nuumani cha Sheikh Muhiyudin Abdul-Qaadir bin Abil-Wafaa.

Na Shaqaiqun-Nuumani Fii Manaqib Ibni Nuumani cha Zamakhshariy. Na vingine. Na hii ikijulisha lolote itakuwa yajulisha daraja ya uvukaji mipaka na upendeleo kwa ajili ya Abu Hanifa, mzozo na kupaza sauti kuzihusu madhehebu na maimamu wa madhehebu hizo, vinginevyo kuna haja gani ya kuandika vitabu hivi vyote, ambavyo hawakuipata hadhi kama hii Khulafau Rashidun (Abubakr, Umar na Uthman)?!

Na kati ya safu mbili hizi zinazopingana ambazo ni uvukaji mipaka na kusingizia, tutajaribu kufichua mtazamo wa pekee wa historia ya madhehebu na kiwingu kilicho tanda juu ya wazo hili.
Imamu Abu Hanifa

Makuzi Ya Abu Hanifa:
Yeye ni Nuuman bin Thabit, alizaliwa mwaka 80 A.H, zama za ukhalifa wa Abdul Malik bin Marwani. Na amefariki huko Baghdad mwaka 150 A.H. Ameinukia katika mji wa Kufa, wakati wa al-Hujjaj. Na Kufa ulikuwa ni mojawapo ya miji mikubwa ya Iraqi ambayo duru za elimu zilikomaa. Shauku zenye kupingana, na rai katika mapambano ya kisiasa, elimu, na misingi ya itikadi vilionesha mduwazo wakati ule. Katika hali hii Abu Hanifa alijitokeza na ubingwa wa theolojia (scholastical) na mjadala, alifanya majadiliano humo mjini. Halafu alihamia kwenye duru za fiq’hi mpaka zikawa mahsusi kwake. Na alisoma kwa Hamad bin Abi Sulayman aliyefariki dunia mwaka 120 A.H.

Na alikuwa miongoni mwa wanafunzi wake wenye kujitokeza mno, na Abu Hanifa alikuwa wa pekee baada ya kufa Hamad, hivyo basi sauti yake ilisikika na jina lake likawa mashuhuri, pia alikuwa amesoma kwa masheikh wa zama zake, na alihudhuria kwa Atai bin Rabbahi huko Makka, na kwa Naafiu huria wa Ibnu Umar huko Madina, na kwa wengine. Na alikuwa anabaki sana na Hammad bin Sulayman, na alichukuwa riwaya kutoka kwa Ahlul-Bayt, kwa mfano kutoka kwa Imam Muhammad al-Baqir na mwanawe As-Swadiq (a.s.).
Fiqhi Ya Abu Hanifa:
Abu Hanifa hakujulikana kuwa na Fiqhi makhsusi isipokuwa kwa njia ya wanafunzi wake. Hivyo yeye mwenyewe hakuandika fiqhi wala hapakusajiliwa kitu kutoka katika rai zake. Na Abu Hanifa alikuwa na wanafunzi wengi, lakini walioyachukua madhehebu yake na kuyaeneza ni wanne, nao ni: Abu Yusuf, Zufar, Muhammad bin al-Hasan al-Shiibaniy na al-Hasan bin Ziyad al-Luuluiy.

Abu Yusuf ambaye ni Yaaqubu Bin Ibrahim ametoa mchango mkubwa kuieneza madhehebu ya Hanafii. Alipata bahati ya kukubaliwa na makhalifa wa kibani Abbas, naye alishikilia uraisi wa ukadhi katika zama za al-Mahdiy na al-Hadiy na Rashid, na alipata kwa Rashid hadhi makini.

Hivyo Abu Yusuf alifurahia cheo hiki akakitumia kueneza madhehebu ya Hanafii katika nchi nyingi mikononi mwa makadhi aliokuwa akiwaainisha katika swahiba zake, ikawa kupita kwa sauti ya madhehebu ya Hanafii kwategemea nguvu yake.

Ibnu Abdil-Bari amesema kuhusu hilo: “Abu Yusuf alikuwa Kadhi wa makadhi, alikuwa Kadhi wa makhalifa watatu, alitawalia ukadhi baadhi ya siku za al-Mahdiy kisha akawa Kadhi wa al-Haadiy halafu wa ar-Rashid. Na ar-Rashid alikuwa anamheshimu na kumtukuza, na alikuwa kwake mwenye hadhi makini. Kwa ajili hiyo yeye alikuwa na mkono mrefu katika kueneza utajo wa Abu Hanifa na kuinua daraja yake kwa sababu ya nguvu ya usulutani na usulutani wenye nguvu.”15

Mwanafunzi wa Abu Hanifa, Muhammad bin al-Hasan al-Shiiban ameshiriki kuitangaza madhehebu ya Abu Hanifa kwa tunzi zake ambazo ziligeuka kuwa ndio rejea ya kwanza ya fiqhi ya Abu Hanifa, japo kuwa yeye ni mwanafunzi pia wa Thauriy, al-Awzaiy na Malik. Na aliingiza Hadithi katika fiqhi ya wafuasi wa rai.

Ama Zufar Ibnu Hudhaili naye ni miongoni mwa swahiba wa mwanzo wa Abu Hanifa. Aliyaeneza madhehebu ya Abu Hanifa kwa ulimi wake, na alitawalia ukadhi katika zama za Abu Hanifa huko Basra. Alikuwa mfanya ulinganishi sana, kiasi kwamba Ahmad bin al-Maadil al-Maliky alimdhihaki kwa kauli yake: “Ukiwa muongo uliyonihadithia ni juu yako dhambi za Abu Hanifa au Zuffar, wafanyao ulinganishi makusudi, wasiopenda kushikamana na habari.”

Abu Hanifa na swahiba zake walikuwa wanaaibishwa sana kwa kufanya ulinganishi. Na imeelezwa katika kitabu Iqdul-Farid, Uk. 408 kuwa: “Musawiru akasema kumuhusu Abu Hanifa: ‘Tulikuwa na wasaa kabla ya hii leo katika dini, mpaka tulipopatwa na balaa la watu wa ulinganishi. Wametoka sokoni mapato yao yaliposimama, wakatumia rai baada ya juhudi na umasikini.”’

Abu Hanifa alikutana naye akamwambia: ‘’Umetudhihaki ewe Musawiru, sisi tutakuridhisha.’’ Akampa Dirham - (pesa za huko).

Listaajabishalo ni kuwa wanavyuoni walioasisi madhehebu ya Hanafii na kuyaandika, hawakuwa wenye kumfuata Abu Hanifa katika rai zake, bali walikuwa ni wanavyuoni wanaojitegemea, pengine wanaafikiana na ustadhi wao na kuwa tofauti naye mahali pengine. Kwa ajili hiyo tunavikuta vitabu vya kihanafi vina kauli nne katika mas’ala moja. Abu Hanifa ana kauli yake, Abu Yusuf ana kauli yake, Muhammad ana kauli yake, na Zuffar ana kauli yake.

Allama al-Khudhwiriy anasema: ‘’Baadhi ya mahanafii wamejaribu wazifanye kauli zao zilizotofautiana kuwa ni kauli za Imam alizoziacha. Lakini huu ni mghafala mkubwa wa historia ya maimamu hawa, bali wa yaliyosemwa katika vitabu vyao. Kwani Abu Yusuf anasema rai ya Abu Hanifa katika kitabu al-Kharaju halafu anataja rai yake akieleza bayana kuwa yuko kinyume naye, na anabainisha sababu ya tofauti.

Na kama hivyo anafanya katika kitabu Abu Hanifa na Ibn Abi Layla. Kwani yeye mahala pengine huisema rai ya Ibnu Abi Layla baada ya kutaja rai mbili. Na Muhammad, Mungu amrehemu anaeleza katika kitabu chake kauli za imamu, kauli za Abu Yusuf na kauli zake, na anaeleza wazi tofauti iliyopo kati ya kauli hizo. Kwa kuwa lau (Abu Hanifa) angekuwa kama walivyosema, basi rai walizoziepuka zisingekuwa ndio madhehebu!

“Na, ni miongoni mwa yaliyothibiti kuwa Abu Yusuf na Muhmmad waliziacha rai alizokuwa nazo Imam, walipoona Hadithi walizonazo watu wa Hijazi. Lililo hakikiwa kihistoria ni kuwa maimamu wa kihanafi ambao tumewataja baada ya Abu Hanifa, rahimahu llahu, hawamfuati yeye.”16

Muhtasari ni kuwa: Madhehebu ya Hanafii yalipanuka na kuenea kwa juhudi za watu wake. Na walisaidiwa na nguvu za dola alizokuwa nazo Abu Yusuf. Hivyo madhehebu ya Hanafii ni taasisi ya kundi la wanafaqihi, ambao kila mmoja akijitegemea mwenyewe wala haikutokana na imamu mmoja ambaye ni Abu Hanifa. Na hili jaribio la mahanafii, la kuyarejesha yote kwake ni jambo lisilo sawa.
Kashfa Kwa Abu Hanifa:
Kulikuwa na wasiomshabikia ambao ni upande mwingine miongoni mwa wanachuoni waadilifu wa zama zake ambao walimsingizia Uzandiki, na kutokuwa makini, na walisema kuwa ni mtu aliyeharibikiwa kiitikadi na ana utovu wa nidhamu wa kidini, na yuko kinyume na Kitabu na Sunna, walimrarua katika dini yake, na kumvua imani.17

Walikusanyika Sufiyan At-Thauri, Shariiku, Hasan bin Swalihu na Ibnu Abi Layla, walituma kwa Abu Hanifa na wakasema: “Wasema nini kuhusu mtu aliyemuua baba yake na kumuingilia mama yake na akanywea pombe kichwa cha baba yake?”

Akasema: “Ni muumini.” Ibn Abi Layla akasema: “Sitokukubalia ushahidi abadan.” Na Sufianu At-Thauri alimwambia: “Sitosema na wewe abadan.”18

Na Ibrahimu bin Bishar alihadithia kutoka kwa Sufian bin Uyayna kuwa amesema: “Sijapata kumuona yeyote mwenye kuthubutu mno juu ya Mwenyezi Mungu kuliko Abu Hanifa.” Na pia kutoka kwake:

“Abu Hanifa alikuwa anaipigia mfano Hadithi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu na kuiepusha kwa elimu yake.”19

Na imeelezwa kutoka kwa Abu Yusuf, aliulizwa: “Je Abu Hanifa alikuwa Marjaiy?” Alijibu: “Ndio.” Aliulzwa: “Alikuwa Jahamiy?” Alisema: “Ndio.” Aliulizwa: “Ukonaye vipi?” Akasema: “Abu Hanifa alikuwa mwalimu tu, hivyo basi endapo kauli yake itakuwa nzuri tutaikubali na endapo itakuwa mbaya tutamuachia.”20

Hii ndio rai ya waliokuwa karibu mno na yeye, mwanafunzi wake na muenezaji wa madhehebu yake, je itakuwaje rai ya watu wengine!

Na kutoka kwa al-Walid bin Muslim amesema: “Malik bin Anasi aliniambia: ‘Je Abu Hanifa hutajwa nchini kwenu?’ Nilimwambia: Ndio. Alisema: ‘Haipaswi nchi yenu kuwa makazi ya kuishi.”’21

Al-Awzaiy akasema: “Kwa hakika sisi hatumkemei Abu Hanifa kuwa na rai, kila mmoja wetu anayo rai, lakini sisi tunamkemea kwa sababu yeye humjia Hadithi kutoka kwa Nabii (s.a.w.w) anaigeuza vingine.”22

Amesema Ibn Abdil-Bari: “Na miongoni mwa waliomkashifu na kumuumbua ni, Muhammad bin Isma’il al-Bukhariy. Amesema katika kitabu chake Ad-Dhuafaau Wal-Matrukuuna: “Ni Abu Hanifa an- Nuuman bin Thabit al-Kufiy. Naim bin Hamad amesema: Alituhadithia Yahya bin Said na Muadhi bin Muadhi kuwa, tulimsikia Sufiani At- Thauriy anasema: Abu Hanifa alitakiwa afanye toba ya kuachana na ukafiri mara mbili. Na Naimu al-Fuzariy amesema: Nilikuwa kwa Sufiani Bin Uyayna, likaja tangazo la kifo cha Abu Hanifa, alisema….Alikuwa anaubomoa Uislamu tanzi moja baada ya lingine, hajazaliwa katika uislamu mtoto wa shari kuliko yeye. Haya ndio aliyoyasema al- Bukhariy.”23

Ibn al-Jaarud amesema katika kitabu chake ad-Dhuafau Wal-Matrukuuna: “Ni al-Nuuman bin Thabit, hadithi zake zote ni mawazo. Na imepokewa kutoka kwa Wakii bin al-Jarahi kuwa yeye amesema: ‘Nimemkuta Abu Hanifa amekhalifu Hadithi mia mbili kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu.’ Na aliambiwa Ibnu Mubaraka: ‘Watu walikuwa wanasema kuwa wewe unakwenda na kauli ya Abu Hanifa.’ Akasema: ‘Sio kila wasemalo watu ni kweli. Tulikuwa tukimwendea muda hali tukiwa hatumjui, lakini tulipomjua.....”24

Ni wazi kuwa kauli hizi zimetambulika kuwa ni za malengo, hivyo hazikuwa tusi au kebehi au kutoka nje ya mpaka wa kiakili bali hizo ni shaka za kielimu dhidi ya Abu Hanifa. Na hapa tumefumbia macho kero za maadui zake na kukithirisha kwa wafuasi wake, na tumetosheka na rai za wanavyuoni katika hilo, nayo yatosha kuutia dosari utu wake, vipi ilimfalia awe imamu, hali ikiwa katika umma kuna anayestahiki zaidi yake yeye, kifiqhi, kielimu na kiuadilifu?! Lakini ni siasa, waijuaje siasa!
Abu Hanifa Na Imam Ja’far As-Sadiq (A.S):
Alikuwa mfanya mjadala sana, mshindani hodari hivyo Mansur alitaka kumtumia kumpiga kumbo Imam as-Sadiq (a.s.) ambaye alikuwa anatajika kila mahali na umaarufu wake ukiwa umenyanyuka, na ilikuwa inamuia vigumu Mansur kuona Kufa, Makka, Madina na Qum duru za kielimu zinazoshabihiana na matawi ya madrasa ya Imam Ja’far bin Muhammad as-Sadiq (a.s.), kwa ajili hiyo Mansur alilazimika kumleta Imam (a.s.) kutoka Madina mpaka Kufa na alimtaka Abu Hanifa aandae mas’ala zilizo muhimu amuulize Imam (a.s.) katika kikao cha jumla ili amdhiki Imam Sadiq (a.s.) na kumpunguzia daraja yake.

Alisema: “Sijapata kumwona faqihi zaidi ya Ja’far bin Muhammad as- Sadiq. Mansur alipomleta alinitumia na akasema: ‘Ewe kwa kweli watu wamefitiniwa na Ja’far bin Muhammad basi hebu muandaliye mas’ala magumu.’ Nilimuandalia mas’ala arobaini.

“Halafu Abu Ja’far alinitumia mjumbe hali akiwa huko Hayra, nilimjia nikaingia kwake, na Ja’far bin Muhammad akiwa ameketi kuliani kwake, nilipomtia machoni, haiba ya Ja’far bin Muhammad as-Sadiq iliniingia kiasi ambacho haikuniingia haiba ya Abu Ja’far al-Mansur. Nilimtolea salamu, alinifanyia ishara nilikaa, halafu alimgeukia na akasema: ‘Ewe Abu Abdillahi huyu ni Abu Hanifa.’ Akasema: ‘Naam, ametujia.’ Kana kwamba amechukia ambayo husemwa na kaumu yake kumhusu kuwa yeye amuonapo mtu humjua.

“Halafu Mansur aligeukia kwangu na akasema: ‘Ewe muulize Abu Abdillahi maswali yako.’ Nikawa namuuliza naye ananijibu, anasema:

‘Ninyi mnasema hivi na watu wa Madina wanasema hivi na sisi tunasema hivi, huenda tukafuata na huenda wakawafuata na huenda tukawakhalifu wote.’ Mpaka nikaleta maswali arobaini. Kisha Abu Hanifa akasema: ‘Si tumeeleza kuwa mwenye elimu zaidi ni mjuzi zaidi wa tofauti za watu.”25

Imam as-Sadiq (a.s.) alikuwa anamkataza asikisie na alikuwa mkali kumkataza. Na alikuwa anasema: “Zimenifikia kuwa wewe unakisia dini kwa rai yako, usifanye hivyo kwa kuwa wa kwanza kukisia ni Ibilisi.”26

Na alimwambia: “Ewe wasemaje kwa aliye katika hali ya ihramu aliyevunja rubaiyyah27 ya mnyama swala?!” Akasema: “Ewe mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu sijui hilo.” Akasema: “Wewe unachanganyikiwa hujui kuwa swala hana rubaiyyah bali ni meno tu ya kawaida abadan.”28 Abu Naim alituhadithia kuwa: “Abdullahi bin Ubayy Shibrima na Ibnu Abilayla waliingia kwa Ja’far bin Muhammad as-Sadiq, alimuuliza Ibnu Abilayla: ‘Ni nani huyu aliye pamoja nawe?’ Alisema: ‘Huyu ni mtu ana uoni na sauti katika dini.’ Akasema: ‘Huenda anakisia jambo la dini kwa rai yake.’ Akasema: ‘Ndio.’ Ja’far alimuuliza Abu Hanifa: ‘Jina lako ni nani?’ Akasema: ‘Nuuman.’ Akasema: ‘Sioni kama unafanya vizuri kitu chochote.’ Halafu akawa anamuuliza maswali ikawa jibu la Abu Hanifa ni kutokuwa na majibu yake. Ndipo Imam alipoyajibu.

“Halafu akasema: ‘Ewe Nuuman baba yangu alinihadithia kutoka kwa babu yangu kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) alisema: Wa kwanza kukisia jambo la dini kwa rai yake ni Ibilisi. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alimwambia: Sujudu kwa ajili ya Adam. Akasema: Mimi ni bora kuliko yeye, umeniumba mimi kutokana na moto na umemuumba yeye kutokana na udongo. Hivyo mwenye kukisia dini kwa rai yake Mwenyezi Mungu atamuunganisha na Ibilisi Siku ya Kiyama, kwa kuwa yeye ni miongoni mwa wafuasi wake katika kukisia.”’

Fakhru Raziy anasema: “La ajabu ni kuwa tegemeo lake lilikuwa kukisia na hali mahasimu wake wanamlaumu kwa sababu ya kukithiri kukisia. Wala haijanakiliwa kutoka kwake wala kwa mmoja miongoni mwa swahiba zake kuwa alitunga lau karatasi kuthibitisha ukisiaji. Wala hakuwahi kutaja katika mojawapo ya maandishi yake shubha yoyote, achia mbali hoja, wala hakujibu dalili za mahasimu wake katika kukanusha ukisiaji, bali wa kwanza aliyesema katika mas’ala hii na kuitolea dalili ni Shafii.”29

Kwa ajili hiyo tunamkuta Imamu as-Sadiq (a.s.) anauelekeza umma njia zilizo sahihi katika kuopoa hukumu za kisheria hasa baada ya kutapakaa ukisiaji na kuufanyia kazi kama chimbuko miongoni mwa chimbuko za uwekaji sheria.

Hivyo basi walihitimu kutoka madrasa yake maelfu ya wanavyuoni na mujtahidu. Miongoni mwao alikuwa ni Abu Hanifa ambaye alibakia naye muda wote wa miaka miwili aliyoishi Madina. Na kuhusu hilo husema: “Lau si miaka miwili angeangamia Nuuman.”

Na alikuwa hamsemeshi mwenye kikao ila kwa kauli: “Nimefanywa fidia yako ewe mwana wa binti ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.).”30

Na Abdul Halim al-Jundiy anatoa maoni yake kuhusu Abu Hanifa kusoma kwa Imam as-Swadiq (a.s.): “Ikiwa utukufu wa Malik ni kuwa kwake miongoni mwa masheikh wakubwa wa Shafii au utukufu wa Shafii ni kuwa kwake mkubwa mno miongoni mwa maustadhi wa Ibnu Hanbali, au ni utukufu kwa wawili hao kusoma kwa masheikhe wao hawa. Basi kwa kweli uwanafunzi kwa Imam Swadiq umeivalisha utukufu fiqhi ya madhehebu manne ya Ahlus Sunna. Ama Imam as-Sadiq utukufu wake haukubali ziada au nuksani. Kwa kuwa Imam ni mubalighi kwa watu wote wa elimu ya babu yake alayhi swalatu wassalamu. Na Uimamu ni daraja yake, na maimamu wa kisunni kujifunza kwake ni utukufu kwao kwa kumkurubia mwenye daraja.”31

Ni kweli kabisa kuwa kuketi na Imam as-Swadiq (a.s.) ni utukufu wa kujifaharisha nao. Yeye ni mwanachuo wa Ahlul-Bayt, chimbuko la hekima. Ubora wake maadui wameutambua. Mansur amesema: “Huu mwiba – yaani Ja’far Sadiq - uliokwama shingoni kwangu ni mjuzi mno katika watu wa zama zake. Na yeye ni miongoni mwa wanaoiwania akhera sio dunia.”

Na suala hapa sio kuutambua ubora alionao, au kupata heshima ya kuketi pammoja naye basi, bali litakiwalo ni kumfuata na kutii amri yake kwa kuwa kumtii yeye ni faradhi kutoka kwa Mwenyezi Mungu juu ya kila mwislamu, kama ilivyothibiti kwa Hadithi ya Vizito Viwili: “Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu,” na yasikitisha kuwa Abu Hanifa hakuwa miongoni mwa wanaosalimu amri yake, bali alijitenga pekeyake anatoa fatwa kwa rai yake na kukisia katika dini, kwa ajili hiyo akienda kinyume na Hadithi za Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) ambazo hakuzikubali ila Hadithi kumi na saba…! Ninahitimisha maongezi haya kwa mjadala uliojiri kati ya Imam as-Sadiq (a.s.) na Abu Hanifa, pindi alipokuja kwake:

As-Sadiq (a.s.): Wewe ni nani?
Abu Hanifa: Abu Hanifa.

As-Sadiq (a.s.): Ni mufti wa watu wa Iraqi?
Abu Hanifa: Ndio.
As-Sadiq (a.s.): Kwa kitu gani unawatolea fatwa?
Abu Hanifa: Kwa kitabu cha Mwenyezi Mungu.

As-Sadiq (a.s.): Hivi wewe ni mjuzi wa Kitabu cha Mwenyezi Mungu? Waijua nasikhu na mansukhu zake? Aya Muhkamu na mutashabihu zake? Abu Hanifa: Ndio.

As-Sadiq (a.s.): Nipe habari kuhusu kauli ya Mwenyezi Mungu “Na tukapima humo safari, nendeni usiku na mchana kwa amani.” (Surat Sabaa: 18) ni mahali gani hapo?

Abu Hanifa: Hapo ni kati ya Makka na Madina.

Imam aligeuka kulia kushoto: “Namuapa Mwenyezi Mungu, je mnakwenda kati ya Makka na Madina na hampo katika amani ya damu zenu kwa kuuwawa? Na kuibiwa mali zenu?” Kwa sauti moja waliohudhuria wakasema: “Ewe Mungu wangu, ndio.”

Mara hii Imam (a.s.) aligeuka kumuelekea Abu Hanifa: “Ole wako ewe Abu Hanifa! Kwa kweli Mwenyezi Mungu hasemi ila ukweli.”

Alinyamaza dakika kadhaa, halafu alibadilisha kauli yake ya mwanzo, akasema: “Sina elimu ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu.” Hapo alileta epusho jipya: “Mimi ni mtu wa ukisiaji tu.”

Imam (a.s.) akasema: Angalia katika ukisiaji wako, ikiwa ni mkisiaji. Ni ipi mbaya zaidi kwa Mwenyezi Mungu: Kuuwa au kuzini?

Abu Hanifa: Ni kuuwa.
As-Sadiq: Vipi ameridhia katika kuuwa mashahidi wawili wala hakuridhika katika kuzini ila wanne? Lafanyiwa ukisiaji hili kwako?
Abu Hanifa: Hapana.
As-Sadiq: Vyema. Je swala ndiyo bora au Swaumu?
Abu Hanifa: Swala ndio bora.

As-Sadiq: Hivyo basi kulingana na kauli yako itakuwa wajibu juu ya mwenye hedhi alipe Swala zilizomfutu katika siku zake za hedhi. Si Swaumu. Na hali Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewajibisha juu yake alipe Swaumu sio Swala.

As-Sadiq: Je mkojo ndio mchafu zaidi au manii?
Abu Hanifa: Mkojo mchafu zaidi.
As-Sadiq: Hivyo kulingana na ukisiaji wako itakuwa wajibu kuoga, kwa sababu ya mkojo, na si manii, na hali Mwenyezi Mungu Mtukufu amewajibisha kuoga kwa kutokwa na manii wala si mkojo. Je hili lafanyiwa ukisiaji kwako?

Alinyamaza, na akasema: “Mimi ni mtu wa rai tu.” Haraka sana Imam alimuuliza: “Nini rai yako kuhusu mtu ambaye alikuwa na mtumwa, alioa na akamuolea mtumwa wake mke usiku mmoja. Na wakawaingilia wake zao usiku mmoja, wakawaweka wake zao katika chumba kimoja kisha wakasafiri, na wale wanawake wakazaa watoto wawili wa kiume. Halafu kile chumba kikawabomokea wale wanawake wawili, wao wakafariki lakini watoto wakabaki hai. Ni yupi kulingana na rai yako atakuwa mmiliki na yupi atakuwa mmilikiwa? Na yupi kati ya wawili hao mrithi na yupi mrithiwa?”

Kwa mara ya tatu, alibadili msimamo wa kauli yake kuwa ni mtu wa rai, na alitangaza baada ya muda wa ukimya, kufikiri, kuduwaa, na aibu: “Mimi ni mtu wa hadi za kisheria.” Imam (a.s.) akasema: “Waonaje kuhusu kipofu amepofoa jicho la mtu aliyekuwa mzima, na aliyekatika mikono amekikata kipande cha mkono wa mtu. Vipi itatekelezwa hadi ya kisheria juu ya wawili hawa?”

Alijaribu kujibu maswali ya Imam ili apate kuhalalisha uandikaji nne wake juu ya kiti cha enzi cha fatwa huko Iraq, lakini alishindwa kisha kwa masikitiko akasema: “Sina elimu…sina elimu...... Lau sio watu kusema kwamba ameingia kwa mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu na wala hakumuuliza kitu, mimi nisingekuuliza kitu.

As-Sadiq: Hivyo basi fanya ukisiaji ikiwa ni mkisiaji.

Abu Hanifa: La, sitoongea kwa rai na ukisiaji katika dini ya Mwenyezi Mungu baada ya kikao hiki.

Lakini Imam (a.s.) alitabasamu akisema: “Hapana… hapana, kwa kusema kweli kupenda ukubwa hakutokuacha wewe kama hakujawaacha waliokuwa kabla yako.”
Imam Malik Bin Anas
Yeye ni Abu Abdillahi, Malik bin Anas. Alizaliwa Madina mwaka 93 A.H. kulingana na baadhi ya kauli, na alifariki mwaka 179 A.H. kulingana na kauli mojawapo. Wakati wa Malik uling’ara kwa elimu, na Madina siku hizo ilijaa wanafunzi kutoka nchi tofauti za kiislam, na madrasa ya Madina ilijulikana kwa kushikamana na Hadithi na kuipiga vita madrasa ya rai ya huko Kufa iliyokuwa chini ya uongozi wa Abu Hanifa, ni miongoni mwa yaliyozua mfarakano kati ya madrasa mbili hizo na mabishano yaliyotoka nje ya mpaka wa kielimu.

Na changamoto ya madrasa hii ilikuwa ni madrasa ya Imam as-Sadiq (a.s.) ambayo ilikuwa imejaa wanachuoni na mikusanyiko ya misafara kutoka pande mbalimbali za dunia ya kiislamu, ambao walikuwa wanagawana fursa ya kukutana na maimamu wa Ahlul-Bayt (a.s.), na Imam as-Sadiq (a.s.) alikuwa na nafuu kidogo ya ukandamizaji wa watawala, ukimlinganisha na maimamu wengine wa Ahlul-Bayt. Na Malik alijiunga na madrasa yake muda mrefu na alichukua Hadithi kutoka kwake. Na anazingatiwa kuwa ni miongoni mwa masheikh wakubwa wa Malik.

Halafu Malik alisoma kwa idadi kadhaa ya masheikh. Mfano wa Amiru bin Abdillah bin Zubair bin al-Awwam, na Zayd bin Aslam na Said al-Maqbariy na Abu Hazim, na Swafwan bin Salim na wengine. Na Malik alikuwa makhsusi kwa kujiambatanisha na kuchukua kutoka kwa Wahbi bin Hurmuz, na Nafiu huria wa Ibnu Umar, na Ibnu Shihabi az-Zuhriy, na Rabiatu ar-Raayi, na Abu Zanad.

Malik aliendelea mpaka alichukua ukuu wa madrasa ya Hadithi, lakini haraka sana siasa ilijiingiza, ili iinusuru madrasa ya rai, na wakasirishwe watu wa Hadithi, na kwa ajili hiyo Malik bin Anas alikuwa lengo la ukandamizaji wa dola mpaka walifikia kumzuia kuelezea Hadithi, na alipigwa mjeledi kwa sababu ya fatwa aliyoitoa isiyokubaliana na utashi wa dola, na hilo lilikuwa zama za uliwali wa Ja’far bin Sulayman, mwaka wa 146A.H. Kwa kweli yeye alimvua Malik na kumnyoosha na kumcharaza kwa mijeledi mpaka mabega yake yaling’oka.

Ibrahim bin Hammad akasema: “Nilikuwa namwangalia Malik aliposimamishwa kutoka kikazi chake, mkono wake wa kulia au wa kushoto ulibebeshwa juu ya mwingine.”

Na ni miongoni mwa ajabu na lenye kusisimua sana ni kuwa baada ya zama kidogo, Malik alikuwa anawekwa mbele katika dola, mwenye kutiliwa maanani, na alifikia daraja ambayo kwayo watawala walikuwa wanamwogopa. Swali ambalo lenyewe linakuja, ni kitu gani kimepatikana kwa Malik mpaka dola imridhiye na imnyanyue mpaka daraja hii? Hivi ni kuwa dola ilikuwa yamchukia kwa rai maalumu ambayo sasa Malik ameachana nayo? Au alibakia thabiti katika rai yake na dola ikaichukua na kuacha msimamo wake kwa ajili ya Malik? Au kuna kitu kingine?

Swali hili linaloduaza, na ulizo linalojitokeza mbele ya anayeidurusu historia ya imamu Malik, ataona kubadilika kwa uhusiano kati yake na dola, kutoka hali ya kukandamizwa na ghadhabu mpaka kufikia Malik na Mansur wanapendana na kusifiana. Hivyo basi Mansur anamwambia Malik: “Wallahi wewe ni kati ya watu wachache na umjuzi mno, ukipenda nitaiandika kauli yako kama misahafu inavyoandikwa, na nitaituma pande mbali mbali za nchi na nitawalazimsha nayo.”

Kutokea hapo madhehebu ya Imam Malik ilianza kuenea alipokuwa aridhiwa na Sulutani. Vinginevyo kwa kweli mas’ala sio elimu na kutokuwa na elimu bali ni ya ufalme na usulutani, kujigamba, na kujitangaza. Na watu kuchukuliwa wakiwa wanaridhia au kwa kahari kuifuata madhehebu. Na hili ndilo ambalo limemfanya Rabiatu ar-Raayi -Ustadhi wa Malik na mwenye elimu nyingi kuliko yeye - aseme: “Hamjui kuwa uzito wa dola ni bora kuliko mzigo wa elimu.”32

Na Malik alipopata ridhaa hii kutoka kwa Sulutani akawa anasema: “Nimemkuta Mansur mjuzi mno wa Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake na athari za waliotangulia.”

Subhanallah! Ni elimu gani aliyonayo Mansur kiasi awe ni mjuzi mno katika watu wa Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake (s.a.w.w)?! Si chochote bali ni kujikurubisha na kujisogeza kwa mfalme na Sultani.

Ama dalili ya kuwa Malik alikuwa amejitenga mbali na Sultani, hiyo historia haijatuhadithia kuwa alithubutu kusimama mbele ya Mansur, akimpinga jambo au kuipinga njia yake, kama alivyofanya Abdullahi bin Marzuq alipokutana na Abu Ja’far katika tawafu, hali watu wamejitenga kumpisha. Abdullahi akasema kumhusu: “Ni nani amekufanya uwe na haki zaidi ya nyumba hii kuliko watu, unawazuia kati ya nyumba na wao, na unawaweka kando nayo?!” Abu Ja’far alimwangalia usoni kwake na alimtambua, na akasema: “Ewe Abdullah bin Marzuq, nani amekufanya uthubutu kufanya hili, na nani amekutanguliza mbele ya hili”?

Abdullah akasema: “Utanifanya nini? Je mkononi mwako muna madhara au manufaa? Wallahi siogopi madhara yako wala sitarajii manufaa kwako, mpaka Mwenyezi Mungu awe amekuidhinisha kwangu.”

Mansur akasema: “Kwa hakika wewe umeihalalishia nafsi yako na umeiangamiza.” Abdullahi akasema: “Allahuma ikiwa mkononi mwa Abu Ja’far kuna la kunidhuru, usiache chochote katika madhara ila kiteremshe juu yangu, na ikiwa mkononi mwake kuna manufaa yangu, yakate manufaa yote kutoka kwake, wewe ewe Mola wangu mkononi mwako mna kila kitu na wewe ni mmiliki wa kila kitu.” Hapo Abu Ja’far alitoa amri kumhusu, alimchukua mpaka Baghdad alimuweka jela huko halafu alimfungua.33

Kwa minajili hiyo twamwona Malik yuko mbali na Imam Ja’far as-Sadiq (a.s.) kwa kuwa yeye haafikiani na rai zake za kujiepusha mbali na Sultani na kuwa mbali naye.

Mimi kwa mtazamo wangu ni kuwa sababu ya msingi ya utawala kumghadhibikia Malik hapo mwanzo ni kuwa uliona upendo kwa Imam as-Sadiq (a.s.), na tuhuma iliyokuwa yazunguka wakati ule ni kuwa Waarabu wanataka kufanya mageuzi kwa ajili ya Ahlul-Bayt, ndio maana tunaona utawala uliwasogeza karibu vipenzi vyao na ulimnusuru Abu Hanifa huko Kufa. Na jambo hili lilipotoweka, utawala haukupata njia ila kuing’arisha shakhsia ya Malik na kumweka kama mfano wa kidini kwa dola, ili ithibiti kwa watu jina la dola ya kiislamu, na hasa ukizingatia kuwa Abasiyina waliwaasi Amawiyina kwa hoja ya kuwa wao wako mbali na dini.

Kwa ajili hii tunakuta amri ya mfalme ilinena waziwazi uaminifu wa Malik usiozoeleka kwa mwanachuoni yoyote hapo kabla: “Ikikuingia shaka kutoka kwa liwali wa Madina au liwali wa Makka au kutoka kwa yeyote miongoni mwa maliwali wa Hijazi, aidha kuhusu dhati yako au ya mtu mwingine, au uovu au shari kwa raia yoyote, niandikie nitawashushia wanayoyastahiki.”

Kutokana na hali hiyo daraja ya Malik ilitukuka, wakawa maliwali wanamwogopa sawa sawa na kama wamwogopavyo Mansur. Kama alivyohadithia Shafii alipofika Madina akiwa na barua ya liwali wa Madina kutoka kwa liwali wa Makka, na alikuwa ataka aifikishe kwa Malik.

Liwali akasema: “Ewe kijana kwa hakika kutembea kwa mguu kutoka ndani ya mji wa Madina mpaka ndani ya Makka bila viatu, ni rahisi mno kwangu kuliko kwenda kwenye mlango wa Malik, sioni udhalili ila nisimamapo mbele ya mlango wa nyumba yake.”34

Na alipokuja al-Mahdi baada ya Mansur nafasi ya Malik ilizidi kutukuka na alizidi kuusogelea utawala, al-Mahdi alikuwa anamtukuza na kumheshimu na kumpa zawadi kubwa kubwa na kumpa mengi na kuwadhihirishia watu hali yake na daraja yake ya juu.

Na alipokuja ar-Rashid hakubadilisha akamhifadhia Malik nafasi na alimtukuza upeo wa kumtukuza, hivyo haiba ya Malik iliingia nyoyoni. Ndivyo siasa ilivyo, wamuinua umpendae kumwinua, na unaisahaulisha kumbukumbu ya umtakiaye hivyo. Baada ya hivyo ni pingamizi gani itazuia kuenea kwa madhehebu ya Malik baada ya kuwa aridhiwa na dola?!

Wako ni Mwenyezi Mungu ewe bwana wangu Ja’far bin Muhammad as- Sadiq (a.s.), wanatambua kuwa haki ni yako na ipo kwako, wala uimamu hauwi jaizi kwa asiyekuwa wewe.

Je Malik hakusema: “Jicho langu halijapata kuona wala sikio kusikia, wala kuingia katika moyo wa mwanadamu aliye bora kuliko Ja’far as-Sadiq, kiubora kielimu, kiibada na kiuchaji Mungu.”35

Pamoja na kudhihiri fadhila zake, hakupata (a.s.) na Shia wake ila kukandamizwa, kutishwa, mauaji na kufurushwa, na linalotoa ushahidi wa hayo ni historia ya Shia, tokea kutawafu Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) na muda wote wa historia yao.

Lakini mimi najiuliza kama anavyojiuliza mwandishi wa kitabu al-Imam Sadiq Mualimul-Insani aliposema: “Kwa hakika mimi sijiulizi kwa nini waislamu wameendelea kuchanika na kuwa Sunni na Shia? Hapana. Isipokuwa najiuliza na kuduwazwa: Vipi Shia wameweza kubaki imara mpaka hii leo! Japokuwa kulikuwa na hali ya mambo yenye kukandamiza, na hali ngumu walioipita katika kivuli cha vitisho vya kifikra na vya kimwili?!. na japokuwa kulikuwa na majaribio mengi ya kufutilia mbali ishara za ukweli na kuurarua uislam?!”36

Kama sivyo, je! Sio miongoni mwa dhuluma kuitanguliza kila madhehebu mbele ya madhehebu ya Ja’far bin Muhammad as-Sadiq?! Bali yasikitisha mno kuwa si mashuhuri mpaka hii leo hata kati ya wasomi miongoni mwa tabaka za jamii.

Nakumbuka siku moja, mwalimu wetu huko chuo kikuu alikuwa anatusomesha fiqhi ya Malik, hivyo kundi la wanafunzi lilimpinga wakisema: Kwa nini hautusomeshi fiqhi ya madhehebu manne?! Alisema: “Mimi ni Mmaliki, na Wasudani wote ni Mamaliki, na ambaye si Mmaliki miongoni mwenu mimi nipo tayari kumsomesha madhehebu yake kwa sura mahsusi.”

Nilimwambia: Mimi sio Mmaliki je utanisomesha madhehebu yangu? Alisema: “Ndio, madhehebu yako ni madhhebu gani? Je wewe ni Shafii?” Nilimwambia: Hapana. Akasema: “Je wewe ni Hanafi?” Nikamwambia: Hapana. Akauliza: “Je wewe ni Hanbali?” Nilimwambia: La. Hapo mshangao na kuchanganyikiwa kulijitokeza usoni kwake, na akasema: “Hivyo basi wamfuata nani?!” Nikasema: Ja’far bin Muhammad as-Sadiq (a.s.). Akasema: “Ja’far ni nani?!”

Nilisema: Ni Ustadhi wa Malik na yeye ni miongoni mwa dhuria wa Ahlul-Bayt, madhehebu yake yalikuwa mashuhuri kwa jina la madhehebu ya Ja’fariyah. “Alisema sijapata kusikia madhehebu hii hapo kabla.” Nilisema: Sisi ni Shia. Alisema: “Najikinga kwa Mwenyezi Mungu dhidi ya Shia.” Na alitoka….!

Hivyo basi mwenye kuwa na hadhi, kujitangaza na mamlaka atafika kilele cha juu zaidi. Kwani Malik mwenyewe hakuwa na tamaa ya daraja hii kwa kuwa yeye alikuwa anajua kuna wengi wanaofaa zaidi kwa ajili ya nafasi hii kuliko yeye, lakini utawala wamtaka yeye awe marejeo ya watu wote katika fatwa. Mansur alimwamuru aweke kitabu awalazimishe watu kwacho kwa kahari, Malik alikataa, ndipo Mansur akasema: “Weka – yaani kitabu – hakuna yeyote hii leo mjuzi zaidi kuliko wewe.”37 Akaweka kitabu al-Muwatau, na mpiga mbiu wa Sultani alinadi siku za Hijja kuwa: “Yeyote asitoe fatwa isipokuwa Malik.”
Kuenea Kwa Madhehebu Ya Malik:
Madhehebu ya Malik ilienea kwa njia ya makadhi na wafalme, hivyo basi katika nchi ya Hispania mfalme wake aliwalazimisha watu kuyafuata madhehebu ya Malik, hiyo ni pindi yalipomfika maneno ya kumsifu kutoka kwa Malik alipoulizwa kuhusu sera ya mfalme katika Uhispania, alitaja sifa zilizompendeza kumhusu, akasema: “Tunamuomba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alipambe eneo letu takatifu kwa mfalme wenu.” Kauli yake ilipofika kwa mfalme aliwabebesha watu madhehebu yake, na aliyatupilia mbali madhehebu ya Al-Awzaiy, na watu walimfuata kutii mamlaka yake, kwani watu wako pamoja na dini za wafalme wao.

Na pia madhehebu ya Malik yalienea Afrika kwa njia ya Kadhi Sahnoun. Miqriziy anasema: “Na al-Maaziy bin Baadiys aliposhika uliwali aliwalazimisha watu wa Afrika kushikamana na madhehebu ya Malik na kuacha yasiyokuwa yake. Kwa hiyo watu wa Uhispania na wa Afrika wote walifanya rejea kwenye madhehebu yake, wakitaka kilicho kwa Sultani na pupa ya kuitaka dunia, kwa sababu ukadhi na utoaji fatwa katika miji yote hiyo hauwezi kuwa ila kwa anayejiita madhehebu ya Malik.

Hivyo basi watu wa kawaida wakadharurika kupata hukumu zao na fatwa zao. Hivyo ikatapakaa madhehebu hii huko, na ikapata hadhi ya kukubaliwa, si kwa sababu ya kustahiki kwake na unyofu wake kiroho. Bali yalienda tu kulingana na nidhamu ya mabavu ambayo watu walilazimika kuitii bila ya uangalifu.”38

Hivyo hivyo ilienea huko Moroko alipotawala Ali bin Yusuf bin Tashifayni, katika dola ya Bani Tashifayni, aliwatukuza wanachuoni na kuwasogeza karibu. Na ilikuwa hamsogezi karibu ila mwanachuoni wa madhehebu ya Malik, hivyo watu walishindana kuyapata madhehebu ya Malik, vitabu vya madhehebu ya Malik vilipata soko na watu walivitendea kazi na kuviacha visivyokuwa vya madhehebu ya Malik, mpaka hima ya watu kukielekea kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Nabii wake ilipungua.

Ni kama hivyo, siasa iliichezea dini ya waislamu ikawa siasa ndiyo yenye kauli katika itikadi zao na kuziendesha ibada zao. Hivyo basi watu walirithi madhehebu zilizolazimishwa na waliyapokea bila ya mjadala au kuhoji. Na ilikuwa yapendeza kila kizazi kiwe huru kulijua hilo na kisifanye ufuasi, yaani kisiige na kutii utii wa kipofu kumtii mwenye uoni.

Ibnu Hazmi amenena: “Madhehebu mbili zimeenea mwanzoni mwa suala lao kwa utawala na mamlaka: Madhehebu ya Abu Hanifa, kwa kuwa Abu Yusufu alipotawalia ukadhi alikuwa hamtawalishi Kadhi isipokuwa kutoka swahiba zake wenye kujiunga na yeye na madhehebu yake.

“Pili: Madhehebu ya Malik tuliyonayo Uhispania, kwa kuwa Yahya bin Yahya alikuwa na sauti kwa Sultani mwenye kukubaliwa katika ukadhi. Alikuwa hamtawalishi Kadhi katika miji ya Uhispania ila kwa ushauri wake na uchaguzi wake, wala haendi ila na maswahiba wake, na watu ni wenye haraka kuielekea dunia, wakaelekea wanakotarajia kufikia malengo yao.”39
Kebehi Kwa Maliki

Kashfa Juu Ya Malik:
Hapa zimekithiri kauli za wenye kumpendelea, na nimeacha fadhila walizonazo, ambazo Mwenyezi Mungu hajateremsha ufalme wowote juu yake, kwa kuwa zenyewe sio kipimo halisi cha kujua shakhsia ya Malik, na miongoni mwa mifano hiyo yakujia: Kwa hakika al-Qaysiy alimuona Nabii (s.a.w.w) akitembea njiani na Abu Bakr nyuma yake, na Umar nyuma ya Abu Bakr na Malik bin Anas nyuma ya Umar na Sahnoun40 nyuma ya Malik.41

Na mamia mfano wake, nayo ni mambo yasiyo na maana na ni fadhila za kutengenezwa hazifai kujadiliwa.

Na hapa nimetosheka na maneno ya wanachuoni na ya baadhi waliokuwa katika zama moja na Malik, nazo ni rai huru si zaidi ya vile achukuliwavyo mtu kielimu.

Shafii amesema: “Liithu ni mtaalamu zaidi kuliko Malik, ila tu swahiba zake hawakutendea kazi taaluma yake. Na Said bin Ayyub amesema: Lau Liithu na Malik wangekutana Malik angekuwa bubu mbele ya Liithu na Liithu angemuuza Malik kwa amtakaye.”42

Ali bin Madiiniy alimuliza Yahya bin Said: “Ni rai ya yupi mmojawapo yakupendeza mno, ya Malik au rai ya Sufyan?” Akasema: “Rai ya Sufyani haina shaka katika hili.” Na akasema: “Sufyan ni zaidi ya Malik katika kila kitu.”

Na Yahya bin Muiin akasema: “Nimemsikia Yahya bin Said akisema: Sufyan anipendeza mno kuliko Malik katika kila kitu.”43

Na Sufyani Thauriy akasema: “Hana uwezo wa kuhifadhi - yaani Malik.” Na amesema Ibnu Abdul-Bari: “Ibnu Dhuaibi alinena kumhusu Malik bin Anas maneno makavu yenye kukwaruza, nimeona vibaya kuyataja.”44

Na alinena kumhusu Malik, Ibrahim bin Sa’ad na alikuwa akimwombea dua mbaya, na pia alinena kumhusu Malik Abdur Rahman bin Zayd bin Aslam, Ibnu Abu Yahya, Muhammad bin Is’haqa al-Waqidiy, na Ibnu Abu Zinad, na walikebehi vitu katika madhehebu yake. Na Salmatu bin Sulayman alimwambia Ibnu Mubarak: “Umeweka kitu katika rai ya Abu Hanifa na kwa nini haujaweka katika rai ya Malik?” Alisema: “Sikumuona yu mwanachuoni.”45

Na amesema Ibnu Abdil-Bar kumuhusu Malik: “Kwa kweli wao wamevitia dosari vitu katika madhehebu yake. Na kutoka kwa Abdillahi bin Idrisa amesema: ‘Alikuja kwetu Muhammad bin Is’haq tulimwambia kitu kuhusu Malik, na akasema: Leteni elimu yake. Na Yahya bin Swalih akasema: Ibnu Akthum aliniambia: Umemuona Malik na umesikia kutoka kwake na umekuwa pamoja na Muhammad bin al-Hasan ni yupi alikuwa na elimu zaidi? Nilisema: Muhammad bin al-Hasan anavyojichukua binafsi ni mwanachuoni zaidi kuliko Malik.”46

Na Abu Muhammad bin Abu Hatmi alikuwa akisema: “Kutoka kwa Abu Zar’a kutoka kwa Yahya bin Bakir kuwa yeye alisema: ‘Liithu ni mwanachuo zaidi kuliko Malik ila tu hadhi ilikuwa ni ya Malik.”47

Na Amesema Ahmad bin Hanbal: “Ibnu Abu Dhuaybi anashabihiana na Said bin Al-Musayab, na alikuwa bora kuliko Malik, ila Malik watu wanamtakasa zaidi kuliko yeye.”48

Kutokana na maneno yote haya tunaweza kusema kuwa: Malik hana ubora zaidi ya mwingine miongoni mwa wanachuoni, na wala hana kinachompambanua na kumfanya awe anastahiki kuwa marejeo ya kifiqhi, lakini siasa haiangalii mahali stahiki, yenyewe ina kipimo chake mahsusi inakitumia kwa misingi ya vipimo vyake vya kisiasa na maslahi yake. Hivyo basi mwanafiqhi ambaye hapingani na siasa yake ndiye faqihi ambaye wajibu juu ya waislamu kumfanya kigezo na kufuata mfano wake.
Imamu Shafii
Yeye ni Abu Abdillahi Muhammad bin Idrisa bin Al-Abbas bin Uthman bin Shafii. Alizaliwa mwaka 150 A.H. Na kuna kauli isemayo kuwa ni siku ambayo alikufa. Na kuna tofauti kuhusu mahali alipozaliwa kati ya Ghaza, Asqalani na Yemen, na kauli isiyo ya kawaida iliyotupiliwa mbali ni Makka. Na alikufa Misri mwaka 204 A.H.

Alihama akiwa na mama yake naye akiwa mdogo kwenda Makka. Na humo alijiunga na chuo cha Qur’ani na alihifadhi Qur’ani tukufu, na alijifundisha kuandika na baada yake alitoka kwenda Badiyah na aliambatana na Hudhaylu akiwa na miaka ishirini kulingana na alivyohadithia Ibnu Kathiir katika al-Bidaya Wan-Nihayah, na miaka kumi na saba kama alivyohadithia yeye mwenyewe katika Muujamul-Buldaan. Hivyo aliupata ufasaha wa Hudhaylu, na katika muda huu wote Shafii hakuwa na mwelekeo wa kielimu na kifiqhi kwa kuwa hakuelekewa ila katika kumi la tatu la umri wake. Na ikiwa kubakia kwake Badiyah ni miaka ishirini basi utafutaji wake wa fiqhi ni katika kumi la nne, yaani baada ya kuivuka kwake miaka thelathini.

Shafii amejifunza kwa masheikh wa Makka, Madina, Yemen na Baghdad, na wa kwanza ambaye kutoka kwake Shafii amepata elimu ni Muslim bin Khalid al-Makhzumiy aliyekuwa maarufu kwa jina la az-Zanjiy, na alikuwa sio miongoni mwa wanaotegemewa katika Hadithi. Wamemzingatia kuwa ni dhaifu na wamemkebehi mahafidhu wengi kama Abu Daudi na Abu Hatim na Nasaiy.49

Halafu alisoma kwa Said bin Salum al-Qudahi, na alituhumiwa kuwa ni miongoni mwa Murjiah. Na alichukua kutoka kwa Sufyani bin Uyaina, mwanafunzi wa Imam as-Sadiq (a.s.), naye ni moja miongoni mwa madhehebu zilizotoweka. Kama ambapo amechukua elimu kutoka kwa Malik bin Anas huko Madina. Na kutoka kwa wengine, Ibnu Hajar amewataja themanini miongoni mwao, na humo kuna aina ya kutia chumvi. Na Raziy kwa chuki binafsi amekanusha madai ya kuwa Shafii amechukua elimu kutoka kwa Muhammad bin al-Hasan Shiibaniy, aliyekuwa Kadhi na mwanafunzi wa Abu Hanifa, lakini utashi wake binafsi hauna nafasi, kwani Shafii mwenyewe amekiri kuchukuwa elimu kutoka kwake.

Ama wanafunzi wa Shafii miongoni mwao kuna ambaye ni Mwiraki na miongoni mwao kuna ambaye ni Mmisri. Na hapo baadaye walitengeneza sababu ya misingi ya kusambaa kwa madhehebu yake. Katika Wairaki ni Khalidu al-Yamaniy al-Kalbiy Abu Thauri al-Baghdady ambaye anahesabika kuwa ni mwenye madhehebu ya pekee, alikuwa na watu wanaomfuata mpaka karne ya pili. Na amefariki mwaka 240 A.H.

Wengine ni al-Hasan bin Muhammad bin Swabah az-Zaafaraniy, al-Hasan bin Ali al-Karabisiy, Ahmad bin Abdul-Azizi al-Baghdady, na Abu Abdur Rahman Ahmad bin Muhammad al-Ash’ariy. Huyu alikuwa anashabihiana na Shafii na anasifika naye, kwa sababu yeye ni nusra ya madhehebu na aliwahami swahiba zake kwa sababu ya nafasi aliyokuwa nayo kwa Sultani na daraja yake kuwa juu katika dola, kwa hiyo yeye alikuwa na jaha kubwa mno.

Na miongoni mwa wanafunzi wake ni Ahmad bin Hanbal, japo mahanbali wajigambe kuwa Shafii alikuwa anasema Hadithi kutoka kwa Ahmad na kuwa alisoma kwake kama ilivyokuja katika Tabaqatul-Hanabila.

Ama wanafunzi wake Misri, walikuwa na

Share this article

Comments 0

Your comment

Comment description

Latest Post

Most Reviews

MOST READ