Rafed English

Umakini Katika Swala

by : Jameel Kermall

Umakini Katika Swala

 

Kitabu kilichoko mikononi mwako, ni tarjuma ya kitabu cha Kiingereza, kwa jina la Concentration In Prayer (Umakini katika Swala) kilichoandikwa na Jameel Kermalli, Daktari mwanasaikolojia.

Kitabu hiki kinafundisha namna ya mtu kuwa makini katika Swala yake. Kilichomsukuma mwandishi huyu kuandika kijitabu hiki, ni ukweli kwamba sisi kama binadamu hatuko huru kutokana na mawazo ya aina aina ambayo humjia mtu hata wakati akiwa katika Swala, wakati mwingine mawazo huwa makali sana kiasi cha kumbatilishia mtu Swala yake. Ni tatizo kubwa sana ambalo wengi wetu tunalo. Kwa hakika hali hii hutokea kwa kuchezewa na shetani aliyelaaniwa.

Kwa hiyo mwandishi katika kijitabu hiki ameonyesha njia mbali mbali za kuepukana na hali hii, hususan wakati wa Swala; ametumia mifano na mazoezi ya kufanya ili mtu aweze kuwa makini katika Swala yake.

Tumekiona kijitabu hiki ni chenye manufaa sana, na kitawafaa sana Waislamu wa rika na wa jinsia zote. Kama ilivyo ada yetu tumeona tukitoe kijitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili kwa nia ile ile ya kuwahudumia Waislamu wazungumzaji wa Kiswahili.

Tunamshukuru Ndugu yetu al-Akh Ramadhani Kanju Shemahimbo kwa kukubali jukumu hili la kukifanyia tarjuma kitabu hiki. Vile vile tunawashukuru wale wote walioshiriki kwa njia moja au nyingine hadi kufanikisha kuchapishwa kwa kitabu hiki.

Ni matumaini yetu kwamba kitabu hiki kitakuwa ni chenye manufaa kwa wasomaji wetu na insha-Allah kuwafanya kuwa makini katika Swala zao, na hivyo kuwa zenye kutakabaliwa.

Mchapishaji:

Al-Itrah Foundation
S. L. P. 19701
Dar-es-Salaam

Kwa jina Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Ukarimu, Mwingi wa Rehema

Sifa njema ni Zake Allah (s.w.t.) Mola wa ulimwengu!

Umakini katika Swala kiliandikwa kwa miaka michache na utafiti muhimu ulifanyika katika kukamilisha mradi huu. Lengo kubwa la kitabu hiki ni kuelimisha Waislamu juu ya umuhimu wa zile Swala tano za kila Siku na kuelezea jinsi ya kubuni, kujenga na kudumisha umakinifu ndani ya Swala. Hiki ni kipengele muhimu sana cha swala kwani Allah (s.w.t.) anataka tu utulivu wetu usiopungua wakati wa Swala.

Kitabu hiki juu ya Swala kinahitaji usomaji hai na ushiriki hai. Wasomaji wenye hamu watakuta utajiri wa habari, utafiti na mazoezi mtu anayoweza kutumia kwa kufaa zaidi kupata manufaa ya Swala hiyo. Inategemewa kwamba msomaji, hususan vijana na viongozi wa kesho, watakitegemea kitabu hiki na kutekeleza mapendekezo yake katika msingi wa kila siku. Ni wazi kabisa kwamba sio kitabu cha kusomwa mara moja! Majedwali na michoro imetolewa ili kumsaidia msomaji katika kuelewa asili ya kitabu hiki.

Hata kama kitabu hiki kikinukuu vyanzo vingi, wakati mwingine kinashindwa kutoa dondoo maalum na rejea kwa sababu ukusanyaji wa Hadithi katika kitabu hiki ulianza miaka michache iliyopita. Inatosha tu kusema kwamba Hadithi zilizonukuliwa ni sahihi na zinaunda vyanzo vya kutegemewa. Kwa msaada na usaidizi wa wanachuoni wasomi, mfano wa baba yangu – Yusuf Kermali, Maalim Muhsin Alidina, Maalim Muhammad Raza Dungersi, na marafiki wachache wa karibu, mradi huu ulikamilika hivi karibuni.

Kwa mara nyingine tena, ningependa kuwashukuru wazazi wangu ambao walinipatia mapenzi yao yasiyo na mpaka, na msaada katika utengenezaji wa kitabu hiki. Na mwishowe, mke wangu na watoto wangu wazuri wawili ambao Mwenyezi Mungu amenijaalia nao, kwa uvumilivu wao na imani katika uandikaji wote na utengenezaji wa kitabu hiki.

Kisomo cha Surat-ul-Fatiha kinaombwa kwa ajili ya kuirehemu roho ya mama yangu na roho za waumini wote ambao wametangulia katika njia ya Akhera.

Jameel Kermali.

Kitabu hiki kinajadili umuhimu wa zile Swala tano za kila Siku na nafasi yake mbele ya Allah (s.w.t.). Kitabu hiki pia kinajadili mikakati unayoweza kutumia kujenga na kudumisha kiwango cha hali ya juu cha uangalifu na umakinifu wakati unapowasiliana na Allah (s.w.t.), Ambaye anawataka waja Wake kuwa watulivu katika swala zao, zaidi kuliko ibada nyingine yoyote.Yeye, Muumba na Msanifu wa Ulimwengu, anamwambia yule mtu, ambaye anaiswali Swala yake kwa uangalifu mdogo, utulivu wa akili na umakinifu mdogo:

“Ewe Muongo! Unataka kunidanganya Mimi? Naapa kwa Ufahari na Utukufu Wangu kwamba Nitakunyima furaha ya maombi yako na starehe ya mawasiliano yako binafsi na Mimi.”(Hadith al-Qudsi)

Jameel Kermali amefanya utafiti wa uangalifu wa hali ya juu na amegawana nasi matokeo ya kazi yake katika hali ya uwazi na yenye kutia hamu ya kusoma.

Muhsin Alidina

Maelezo Muhimu

Hili zoezi la Siku – 30 ni zoezi kamili la kujenga uangalifu na umakini katika Swala. Kwa wale wanaotaka usaidizi, mnaweza kuwasiliana na mtunzi mwenyewe moja kwa moja kwa kutumia anuani hii: jameelyk@aol.com [12] Yeyote anayemaliza hili Zoezi la Siku 30 pamoja na fomu zote kujazwa, mtunzi atashukuru kama matokeo na faida zake yatatumwa kwake na yanaweza kuchanganuliwa. Faida za zoezi hili zitachapishwa, Insha Allah, katika jarida la kiislamu.

Wasifu Wa Mtunzi

Jameel Kermali ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Southampton, Uingereza, mwenye shahada ya kwanza (Hons) katika Saikolojia, ametaalimikia zaidi katika Saikolojia ya Afya. Yeye pia ni Mtaalamu wa Magonjwa ya Saikolojia aliyethibitishwa na Bodi na ni Daktari Mthibitishwa na Board of Certified Biofeedback Practitioner, akitaalimu hasa katika EEG Biofeedback. Shahada yake ya Udaktari ni ya madawa ya matibabu ya asili (Naturopathic Medicine) na nyanja yake maalum ni pamoja na tiba inayotoa dalili za ugonjwa kwa mtu asiye na ugonjwa huo (Homeopathic), Lishe na Dawa za Mitishamba. Jameel pia ni Mshauri wa Lishe aliyethibitishwa na Bodi ya Washauri wa Lishe.

Alikuwa mhitimu wa juu kabisa katika darasa lake katika al-Hussain Madrassa iliyoko Dar es salaam na yeye ni mwalimu katika masomo ya Kiislamu.

Anayo shughuli yake binafsi huko Long Island, New York Jameel pia ni sehemu ya timu ambayo imeanzisha Bodi ya Hajj ya Michezo (Hajj Board Game), ya kwanza ya aina yake, tayari kutolewa hivi karibuni. Hajj Board Game, inayofanana na umiliki pekee, inatoa maelezo kwa ufupi ya Hijja kwenye Nyumba ya Allah swt, yakikusanya elimu, burudani na mwujiza. Mchezo huo unawafaa watu wazima na vijana, wale wanaokwenda Hijja, wale ambao walikwisha kwenda Hijja na wale ambao bado hawajajaaliwa kwenda safari hii tukufu. Unakuja kamilifu pamoja na dadu 2 zenye doa moja, madoa mawili na isiyo na doa, kipima wakati; vifaa vinne vya kuchezea, kadi 90 za A, 90 za B, 90 za C, 90 za D, 90 za fursa ya uchaguzi, na 90 za kuokota na kadi za tahadhari.

Jameel pia ni mtunzi wa kitabu kilichotafitiwa sana, The Truth of Islam – A Contemporary Approach Towards Understanding Islamic Beliefs and Practices, ambacho kiko kwenye matayarisho. Kitabu hiki ni kazi ya kisayansi inayohusiana na Dhana ya Nguvu katika Ulimwengu, Habari zake, na jinsi imani na vitendo vya Kiislamu zinavyokubaliana moja kwa moja na ugunduzi wa kisayansi na wa kisasa unaojulikana.

Imam al-Sadiq (a.s.) anasimulia kwamba imeandikwa katika Taurati kwamba:

“Ewe mtoto wa mwanadamu! Kama ukijiweka huru mwenyewe, yaani, kama utajitenga na shughuli nyingine yoyote na kujifanya uwepo kwa ajili ya ibada Yangu, nitaujaza moyo wako utajiri na sitakutelekeza katika kile unachokitafuta na unachokitamani.

Na itakuwa ni juu Yangu Mimi kufunga mlango wa umasikini juu yako na nitaujaza moyo wako na heshima juu Yangu.

Na kama hutajiweka huru kwa ajili ya ibada Yangu, nitaujaza moyo wako na mishughuliko ya dunia. Sitaufunga mlango wa umasikini juu yako na nitakutelekeza kwenye yale unayoyatafuta.” (Al-Kulayni (r.a.), Usul al-Kafi, 2, “Kitab al-Iman wal-Kufr’ Bab al- Ibadah” Hadithi ya 1)

Umuhimu Wa Swala

Swala ni njia inayofaa sana ya uhamaji wa kiroho kuelekea kwa Allah (s.w.t.) na kupata nafasi ya juu sana katika ukaribu Naye. Pale Imam as-Sadiq (a.s.) alipoulizwa kama ni kitendo gani bora zaidi kinachowasogeza wanadamu karibu na Allah (s.w.t.) na ambacho pia Yeye anakipenda? Imam alijibu:

“Baada ya kuelimika kuhusu kuwepo kwa Mwenyezi Mungu, sikijui kitu kingine bora zaidi kuliko Swala. Kitendo chenye taadhima sana na cha kupendeza mbele za Allah (s.w.t.) ni Swala.

Swala ndio usia wa mwisho waliofia nao Mitume wote (a.s.)

Ni uzuri ulioje kwamba mwanadamu anaoga au kutawadha, kisha akajitenga kwenye sehemu ya faragha ambapo haonwi na mtu yeyote, na akawa na fursa ya kupiga magoti na kusujudu. Wakati mja anapoinama chini kusujudu na akairefusha sijida hiyo, basi Shetani husema: ‘Oh! Huzuni juu yangu mimi! Mja huyu amemtii Allah (s.w.t.), ambapo mimi nilihalifu, na amefanya sijida ile ambayo mimi niliikataa.’

Katika kitabu Falah al-Sail uk. 23, mlango wa 2, juu ya maelezo ya Swala, kutoka kwa Sayyid Ali ibn Tawus (r.a.), Imam as-Sadiq (a.s.) amesema:

“Swala haitakamilika isipokuwa kwa yule ambaye ana usafi kamilifu na ukamilifu uliopevuka, na yuko mbali na vishawishi na upotovu. Anamjua Allah (s.w.t.) na kwa hiyo anasimama mbele Yake, anamnyenyekea na anafululiza.Yeye kwa hiyo, anasimama kati ya kukata tamaa na matumaini, kati ya uvumilivu na wasiwasi, kana kwamba ahadi alizoahidiwa zimetimizwa, na vitisho juu yake vimetambulika, vikishusha umaarufu wake na kudhihirisha nia yake.

Anatoa muhanga nafsi yake kwa ajili ya Allah (s.w.t.), na anatembea juu ya ile njia kuelekea Kwake kama lengo lake kwa hiari kabisa. Anavunja uhusiano wa maslahi kwa ajili ya Yule Mmoja ambaye Kwake amejifunga na kumjia, na ambaye kutoka Kwake anaomba msaada. Kama akiyapata yote haya, swala hiyo itakuwa ya namna iliyoagizwa na iliyojulishwa, na ni ile Swala hasa ambayo inakataza maovu na uchafu.’

Katika Mustadrak al-Wasa’il, Kitabu cha Swala, Muhammad ibn Ya’qub (r.a.) anamnukuu Imam as-Sajjad (a.s.) kwamba amesema:

“Kuhusu haki za Swala, unapaswa kujua kwamba ni kumtembelea Allah (s.w.t.) na kwamba ndani yake unasimama mbele Yake. Kama umelitambua hilo, utakuwa unastahili kuwa, kupitia hiyo, katika nafasi ya mja ambaye ni dhaifu, mhitaji, unayesumbuka, unayeogopa, mwenye matumaini, mwenye huzuni, na unayeomba. Anayetukuza pia ile hali ya Yule ambaye amesimama mbele Yake kwa utulivu kabisa, kwa dhati kabisa, usalimishaji wa viungo, unyenyekevu, akijiombea Kwake vizuri sana, akimuomba Amfungulie shingo yake ambayo imezingirwa na makosa yake na kumezwa na madhambi yake. Na hakuna uwezo ila kwa Allah (s.w.t.).”

Uhalisi Wa Swala

Kuswali Swala yako kwa wakati wake ni kitendo kilichopendekezwa sana, na sio mwingine zaidi ya Allah (s.w.t) mwenyewe anayetukumbusha juu ya wajibu huu. Na pale yeye (mwenye kufanya ibada) anapojua kwamba ni wakati wa swala na asiswali, yeye kwa hakika ni mpuuzaji juu Yangu. (Hadith al-Qudsi)

Katika kitabu Wasa’il ul-shiah, Juz. 3, uk. 90, as-Sadiq (a.s.) anasema;

“Wale watakaotekeleza swala za wajibu mwanzoni mwa nyakati zake na wakazingatia shuruti zake, Malaika watawanyanyua mbinguni wakiwa weupe na wasafi. Swala hiyo itasema (kumwambia mwenye kuiswali): “Mwenyezi Mungu akuhifadhi wewe kama ulivyonihifadhi mimi na kunikabidhi kwa malaika mkarimu.

Lakini wale watakaoziswali (Swala zao) baada ya nyakati zake bila ya sababu yoyote, na wakawa hawakuzingatia taratibu zake, Malaika watawanyanyua mbinginu wakiwa weusi. Swala hiyo itawakemea wenye kuswali; ‘Umenipoteza mimi, Mwenyzi Mungu akupoteze na wewe na akupuuze kama ulivyonipuuza mimi’

Swala ina baadhi ya sifa za ndani zinazomfanya mwenye kufanya ibada kuwa mbora zaid kuliko malaika na zinafanya maisha kuwa yenye faida. Ni pale tu ukweli halisi wa Swala unapokuwa umeeleweka ndipo mtu anapumbazwa na ule utekelezaji wa kila siku. Katika kuielezea hali halisi ya Swala, al-Ridha (a.s.) anasema:

‘Sababu ya Swala ni kwamba ni utambuzi wa mamlaka ya Allah (s.w.t) na kukataa aina zote za washirika na wingi wa miungu juu Yake. Swala ni kusimama mbele ya Mwenyezu Mungu, kwa unyenyekevu, upole na kukiri dhambi, na kuomba msamaha juu ya dhambi zilizopita. Swala ni kuuweka uso juu ya udongo mara tano kwa siku kama ishara ya kuutambua na kuukiri Ukuu Wake.

Swala ni kwa ajili ya kumdhukuru Yeye na kujiepusha na kiburi na upuuzaji. Swala inaleta unyenyekevu, utii na udhalili mbele za Allah (s.w.t), na ukinaifu juu ya tamaa ya maendeleo ya mali na kiroho (katika dunia hii na ya Akhera pia).

Zaidi ya hayo, Swala humwezesha mtu kujishughulisha wakati wote katika kumkumbuka Allah (s.w.t) mchana na usiku pia, ili mtu asimsahau Mola wake, Mmiliki na Muumba wake kwani kumsahau huko kutasababisha maasi. Mtu, wakati anaposimama kwenye Swala, anajiweka mbele za Mola Wake na katika hali ya kumkumbuka Yeye, na hali hii hasa humkataza na kumzuia yeye kufanya madhambi na aina nyingi za udhalimu.”

Ili uweze kuwa sehemu ya udhihirisho wa mamlaka ya Allah (s.w.t) katika ulimwengu huu, ni lazima uonyeshe unyenyekevu kamili, kwa kufungwa, na utumwa kwa Mola wa ulimwengu wote. Ni lazima uyadhihirishe yote haya katika tabia yako kwa ujumla, kwa kumkumbuka Allah (s.w.t) wakati wote na kuzitafuta Radhi Zake na hasa kwa kutekeleza vitendo vya taratibu za ibada kama vile kutoa Zaka, kufunga na kadhalika.

Wanavyuoni wanaonyesha kwamba kama mtu hatatimiza masharti ya kanuni hii ya swala, anampuuza Allah (s.w.t) na kuwa muasi na tena shetani. Kwa mtu kuweza kufikia kiwango cha juu uwanja wa maisha, ni lazima ajishushe mwenyewe mbele ya Allah (s.w.t). Jinsi anavyojidhalilisha zaidi kwa Allah (s.w.t), ndivyo anavyofika juu zaidi katika uwanja wa maisha.

Umekuwa ni utaratibu wa Allah (s.w.t) kuficha neema muhimu kwa binadamu, na Swala haikutoka katika utaratibu huo. S.V. Mir Ahmad Ali (r.a) katika sherehe yake ya Quran anasimulia faida saba ambazo zimefichwa na Allah (s.w.t) Aliye Mtukufu Zaidi:

“Kwa mujibu wa baadhi ya maelezo, ule Usiku wa Cheo (Qadr) umefichwa katika mwaka mzima kwa jumla. Hii ni kwa sababu mtu aweze kuzitafuta baraka za Allah (s.w.t) kila usiku kwa kiasi atakachoweza. Vivyo hivyo, mmoja kati ya usiku wa siku kadhaa katika miezi ya Sha’aban na Ramadhani unasemekana kuwa ndio usiku wa Qadr, (Lailat-ul-Qadr), Usiku wa Cheo.

Jina kubwa kabisa la Allah (s.w.t), ambalo kwalo mtu anaweza kupata kila anachokitaka, limefichwa katika baadhi ya majina, ili kwamba mtu aweze kuyakumbuka na kuyatamka yale majina matukufu yote ya Mwenyezi Mungu.

Ile Swala ya al-Wusta, au ya katikati miongoni mwa Swala za wajibu za kila siku imefichwa katika zile Swala tano za kila siku ili kwamba mtu aswali kila Swala kwa shauku ya kupata hayo malipo yake maalum. Katika saa moja maalum ya siku ya Ijumaa, kila wiki inasemekana kwamba swala inasikika bila taabu. Hata hivyo, saa hiyo haikuelezwa bayana ili kwamba mtu aweze kujishughulisha na Swala kwa kutwa nzima kiasi atakavyoweza.

Radhi ya Mwenyezi Mungu imefichwa katika Swala ili mtu aweze kumuabudu Mwenyezi Mungu wakati wote.

Ghadhabu ya Mwenyezi Mungu imetajwa katika kufanya dhambi kwa jumla ili kwamba mtu aepukane na aina zote za dhambi.

Aliye mbora zaidi mbele ya Allah (s.w.t) ni yule mchamungu zaidi, ili mtu ajipatie uchamungu mwenyewe na atafute urafiki na wale wabora zaidi kwa Allah (s.w.t); awapende wachamungu na waadilifu, achukizwe na kufuru, na ajiepushe mbali na maasi.”

Mtume (s.a.w.w) katika masaa yake ya mwisho katika uhai wake aliwashauri zaidi wafuasi wake kuitilia maanani sana Swala, na kuswali kulingana na kile kilichoamriwa juu yao.

Thamani Ya Swala

Allah (s.w.t) hujidhihirisha kwa marafiki Zake wa kweli kwa namna ya upole, na kivutio cha upendo huwa ndio kiongozi chao. Kama Hadithi inavyosema kwamba Mtume wa Allah (s.a.w.w.) alikuwa amezoea kungojea wakati wa swala, hamu yake ilikuwa ikiongezeka daima, mpaka mwishowe humwambia Bilal (muadhini wa Mtume); “Tupe faraja, Ewe Bilal” (al-Mahajjat al-bayda fi Tahdhib al-Ahyi, juz.1 uk. 377).

Katika kumshauri Abu Dharr (r.a) Mtume (s.a.w.w) alisema:

“Ewe Abu Dharr!, Sifa Tukufu ni Zake Allah (s.w.t), ameifanya furaha ya jicho langu katika Swala (za kila siku), na amenifanya niipende Swala kama chakula kilivyofanywa kutamanisha kwa mwenye njaa, na maji kwa mwenye kiu. Na hakika, pale yule mwenye njaa, wakati anapokula anashiba, na yule mwenye kiu, wakati anapokunywa, hukata kiu yake, mimi sikinai kwenye swala.

“Ewe Abu Dharr! Yeyote yule mwenye kuswali kwa hiari rakaa kumi na mbili, mbali na zile za wajibu, anakuwa amejipatia haki ya Nyumba ndani ya Pepo.

“Ewe Abu Dharr! Kwa hakika, pindi ukiwa katika Swala, unabisha hodi kwenye mlango wa Mfalme Mkuu, na yeyote anayebisha hodi kwa muda mrefu kwenye mlango wa Mfalme mlango huo utafunguliwa kwa ajili yake.

Ewe Abu Dhar! Hapana muumini anayesimama katika Swala bali humshukia wema juu ya kile kilichokuwa baina yake na Arshi. Na Malaika anateuliwa kwa ajili yake ambaye anaita ‘Ewe mtoto wa Adamu (a.s.), kama ungalijua ni nini kilichopo kwa ajili yako ndani ya Swala na ni nani unayeongea naye, usingeiacha.

“Ewe Abu Dhar! Kuwa kama yule ambaye yuko kwenye sehemu ya upweke (ingawa peke yake), anaadhihi na kukimu Swala, na akaswali Swala yake. Hivyo Mola wako huwaambia Malaika, ‘mtazameni mja wangu! Yeye anaswali na hakuna anayemuona isipokuwa Mimi tu!’ kisha wanashuka malaika 70,000 na kuswali nyuma yake na kumuombea msamaha mpaka kesho yake.

Na mtu anayesimama katikati ya usiku na kuswali peke yake, akasujudu, na akaanguka usingizini akiwa kwenye sijda, Allah (s.w.t) husema; ‘Muangalieni mja wa Wangu! Moyo wake uko pamoja Nami na kiwiliwili chake kipo kwenye kusujudu; na kuwa kama mtu ambaye yuko katika vita na wenzake wote wanakimbia bali yeye anabakia imara katika mapigano mpaka anauawa.

“Ewe Abu Dhar! Hakuna mtu anayeweka paji la uso (kwenye sijida) mahali popote ardhini bali mahali hapo panatoa ushahidi wa hilo juu yake siku ya Kiyama. Hakuna sehemu ambayo kikundi cha watu wanaitembelea bali mpaka ianze ama kuwasalimia au kuwalaani.

Ewe Abu Dhar! Je unajua sababu ya kushuka kwa Aya hii; Kuwa mwenye subira na wahimize wengine kuwa na subira, simamisha Swala, na muogope Allah ili upate kufaulu!” Nikasema; “La siijui – baba na mama yangu wawe kafara juu yako.” Mtume (s.a.w.w) akasema; “Kwa ajili ya kusubiri Swala inayofuata baada ya kila Swala.”

Swala Na Siku Ya Kiyama

Siku ya Kiyama, kabla mtu hata hajaruhusiwa kuwasilisha matendo yake mema ambayo ameyatenda katika dunia hii, Swali la kwanza kuulizwa litakuwa linahusiana na Swala na ni baada ya hapo tu ndipo ataruhusiwa kuendelea. Mtume (s.a.w.w.) ameliweka wazi hili kwa kusema:

“Matendo mema yote yanategemea juu ya swala. Swala ndio msingi wa Uislamu. Kama Swala itakubaliwa basi matendo mema yatakubaliwa. Kama Swala haitakubaliwa, basi na matendo mema hayatakubaliwa.”

Tangazo hili linakuja kueleweka vizuri pale tunapoyachunguza maelezo ya Sheikh al-Qummi (r.a.) katika Manazil al-Akhirat yake, kwamba vitakuwepo takriban vituo 60 juu ya Siraat (daraja) katika Siku ya Kiyama. Kila mmoja wetu atapaswa kujibu maswali kwa namna ya kuridhisha katika kila kituo kimojawapo kati ya hivi. Ni pale tu baada ya mtu kumalizana na kituo kimoja, ndipo atakapoendelea kwenye kituo kinachofuata. Kila kituo kimepewa jina, na kituo cha kwanza, kwa mujibu wa Sheikh al-Qummi (r.a.), ni Swala.

Kwa hiyo, kituo cha kwanza katika Siraat kinahusiana na Kuulizwa juu ya Swala na jinsi ulivyotimiza wajibu huu. Kama, kwa hali yoyote ile, hukutimiza yanayohitajika katika kituo kile, basi isipokuwa labda upate shufaa ya Mtume na Maimam Ma’asum (a.s.) au kwa vitendo vyako mwenyewe, utaanguka chini kwenye matumbo ya Jahannam bila kuwasilisha mabaki ya matendo yako mema katika dunia hii.

Bila shaka, kitu cha kwanza Allah (s.w.t.) atakachouliza Siku ya Kiyama ni Swala, na hili linatufikia sisi kutoka kwa Mitume wote na Maimam (a.s.).

Baraka Za Swala

Muhammad ibn Ya’qub, akimnukuu Imam as-Sadiq (a.s.) anasema:

“Wakati unapoadhini na kukimu swala, safu mbili za Malaika zitasimama kuswali nyuma yako; lakini kama umekimu Swala tu, ni safu moja tu ya Malaika itasimama kuswali nyuma yako. (Furu’al-Kafi, Juz. 3, uk. 303)

Zipo Hadithi nyingine nyingi zenye maana hiyo hiyo, baadhi yake ambazo zinasema kwamba urefu wa kila safu ni kama ule umbali kati ya Mashariki na Magharibi.

Imam al-Baqir (a.s.) amesimulia kutoka kwa Mtume (s.a.w.w.) kwamba alisema: “Wakati mja aliyeamini anaposimama kwa ajili ya Swala, Allah (s.w.t.) humuangalia mpaka atakapomaliza. Rehema za Allah (s.w.t.) huweka kivuli juu ya kichwa chake, Malaika humzunguka yeye pande zote mpaka juu kwenye upeo wa mbingu, na Allah (s.w.t.) huteua Malaika kusimama kichwani kwake, akisema: ‘Ewe mwenye kuabudu! Kama unamjua ni nani anayekuangalia, na ni kwa nani unayemfanyia maombi yako, hutaangalia kwingineko kokote, wala hutaondoka kwenye nafasi yako hiyo.” (Mustadrak al-Wasa’il, Mlango wa 2, Hadithi ya 22)

Yeye (s.a.w.w.) ameendelea tena kusema: ‘Yeyote mwenye kuswali rakaa mbili za Swala bila ya kuvuta nadhari yoyote kwenye jambo la kidunia, Mwenyezi Mungu atamsamehe dhambi zake’ (Mustadrak al-Wasa’il, Mlango wa 2, Hadithi ya 13)

Umuhimu wa kutosha sana umeambatanishwa kwenye swala, na hakuna maneno yanayoweza kuelezea kiasi cha malipo ambacho Allah (s.w.t.) analipa kwa mtu huyu, ambaye anatekeleza wajibu tu. Maimam (a.s.) wamesema:

Swala ndio kitu kinachopendwa na Malaika,
Swala ni mwenendo wa Mitume wote (a.s.),
Swala ni mwanga wa ufahamu,
Swala ndio inayoifanya Imani kuwa imara,
Swala ndio inayofanya matendo yakubalike,
Swala inaongeza riziki.
Swala inakukinga na maradhi,
Swala Shetani anaichukia,
Swala ni silaha ya kukabiliana na maadui zako,
Swala ndio itakayokusaidia kwa Malaika wa mauti (a.s.),
Swala ndio mwanga wa kaburini mwako,
Swala ni jibu kwa Munkar na Nakiir (a.s.), na
Swala ndio itakayokusaidia kaburini mwako mpaka Siku ya Kiyama

Kupuuza Swala

Baadhi ya wake za Mtume (s.a.w.w.) wamesema kwamba:

‘Mtume wa Allah (s.w.t.) alikuwa akizungumza nasi na sisi tulikuwa tunazungumza naye. Lakini wakati wa Swala ulipoawadia alionekana kana kwamba alikuwa hatujui sisi nasi kama hatumjui, kwani nadhari yake ilikuwa imeelekezwa moja kwa moja, kwa Allah (s.w.t.).’ (Mustadrak al-Wasa’il, Mlango wa 2, Hadithi ya 17)

Ibn Tawus (r.a.) anasema katika kitabu Falah as-Sail, kwamba wakati Imam Husein alipokuwa akichukua wudhuu, uso wake ulibadilika rangi na viungo vyake vilitetemeka. Alipoulizwa juu ya sababu yake, Imam alisema: “Wakati mtu anapokwenda kusimama mbele ya Mmiliki wa Arshi, rangi yake inapaswa kupauka na viungo vyake kutetemeka.”

Msimulizi huyo huyo pia anaeleza kwamba al-Hasan, mtoto wa Ali (a.s.) alikuwa naye akipatwa na hali hiyo kabla na baada ya Swala. (Biharul-Anwar, Juz.77, uk. 346.)

Kwa bahati mbaya, wengi wetu tunaichukulia Swala kama aina nyingine ya ingizo kwenye kitabu chetu cha usajili. Baadhi yetu sio tunapuuzia tu ule utekelezaji wa swala kwa wakati wake, bali wengine wala hawafanyi wajibu huu, ambao ni jukumu lenye kubeba uzito mkubwa. Kwa wale wanaopuuzia Swala, Mtume (s.a.w.w.) anasema:

“Yule ambaye anapuuza Swala sio miongoni mwangu. Hapana! Wallahi mtu kama huyo hatofika kwenye bwawa la Kauthar.”

Kwa mujibu wa Mtume (s.a.w.w.), mtu anayepoteza Swala yake atafufuliwa pamoja na Qarun na Haman, ili iwe ni haki ya Allah (s.w.t.) kumwingiza Motoni pamoja na wanafiki.

Imam as-Sadiq (a.s.) alimwambia Zurarah (r.a.): “Usiwe mzembe kuhusu Swala zako. Hakika, Mtume (s.a.w.w.) alisema akiwa kwenye kitanda chake cha mauti: ‘Mtu anayepuuza Swala zake hayuko miongoni mwangu, au mtu anayekunywa vinywaji vinavyolewesha. Na, Wallah! Hatakutana nami kwenye Bwawa la Kauthar.’”(Furu’al-Kafi, iii, uk. 269)

Al-Kulayni (r.a.) anatoa maelezo zaidi pamoja na wasimulizi wake wanaoaminika, kutoka kwa Abu Bashir, kwamba Imam Musa al- Kadhim (a.s.) amesema:

“Wakati wa kifo chake baba yangu aliniambia, ‘Mwanangu, yule anayepuuza swala zake hatapokea uombezi (shufaa) wetu.’” (Furu’al-Kafi, iii, 270.)

Imam Khumeini (r.a.) anao ushauri ufuatao kwa wale wanaochukulia utekelezaji wa Swala Tano za kila siku kwa upuuzaji na kutojishughulisha:

‘Mtu mchamungu anapaswa kuwa mwangalifu wa nyakati zake za ibada katika mazingira yote. Kwa kweli, anapaswa kuzingatia nyakati za Swala, ambacho ndicho muhimu zaidi kati ya vitendo vya ibada, na aitekeleze katika kipindi chake kinaostahili kabisa cha wakati wake, akijiepusha na kushughulika na kazi nyingine yoyote muda wa nyakati hizo.

Kwa njia kama ile anayotengea muda fulani wa kujitengenezea maisha na kwa ajili ya kujifunza na kujadiliana, anapaswa kufanya vivyo hivyo kuhusu matendo haya ya ibada. Katika muda huu, ni lazima awe huru kutokana na shughuli nyinginezo, ili aweze kupata mtulizano katika moyo wake. Hii inaunda sehemu muhimu na kiini cha ibada.

Lakini endapo yeye, kama mwandishi huyu, anaswali Swala zake kwa kulazimishwa na anaona utekelezaji wa ibada ya Mwenyezu Mungu kama jambo lisilohitajika, kwa kweli ataichelewesha kwa muda wowote unaowezekana kuichelewesha. Na pale anapoiswali, anaiswali Swala hiyo kwa namna ya juujuu, akiichukulia kama kikwazo katika njia ya yale anayodhania kuwa majukumu yenye muhimu.

Hata hivyo, ibada kama hiyo siyo haina ufahari wa kiroho tu, inastahili ghadhabu ya kimungu, na mtu kama huyo ni mtu anayepuuza Swala na anaitelekeza kama kitu kisicho na umuhimu.

‘Ninaomba hifadhi kwa Mwenyezi Mungu kutokana na kupuuza Swala na kutoipa umuhimu wake unaostahiki (at-Tawhid, Quarterly Islamic Journal. 27th Hadith – Prayer and Concentration)

Asili Ya Swala Za Wajibu

Al-Majlisi anaandika simu lizi ndefu ndani ya kitabu chake, Hayaat al-Quluub (sehemu ya Pili), kuhusu moja ya matukio ambalo lilitokea wakati wa Mi’raj:

“Huko Bayt al-Ma’muur, Mtukufu Mtume aliiona Al- Ka’aba moja kwa moja chini yake, kiasi kwamba angedondosha kitu kutoka mkononi mwake, kingeangukia kwenye paa lake. Mtukufu Mtume (s.a.w.w) anasema: “Nilisikia sauti ikisema, ‘Hapa ndio mahali patakatifu, na wewe ndiye Mtume uliyekusudiwa, kutoa heshima kwenye msikiti huu. Kila kilichopo kwenye ardhi kina mfano wake ndani ya Pepo.’

Kisha Mola Wangu akaniamuru nifungue mkono wangu, na nichote kwenye maji yanayotiririka kutoka kwenye nguzo ya upande wa kulia wa Arshi,ambavyo nilifanya; na kwa sababu hii ikawa inastahili kuchukua maji ya wudhuu kwa mkono wa kulia.

Kisha sauti ikaamuru, ‘Osha uso wako kwa maji haya ili uweze kuwa msafi wa kuiona Nuru ya Utukufu Wangu na Fahari. Kisha osha mikono yako, kwani utalichukua Neno Langu. Kisha vuta mikono yako yenye unyevunyevu juu ya kichwa chako na miguu yako, ambayo inaashiria kwamba

Nitavuta Mkono wa Baraka juu ya kichwa chako, na kushusha Rehema Zangu juu yako. Kuvuta mkono juu ya mguu kutakunyanyua wewe kupitia kwenye maeneo mengi ambako hakuna mguu uliowahi kukanyaga, na ambao utakanyaga kamwe baada yako.’

“Yeye Aliye Mtukufu tena akaniamuru, ‘Geukia kwenye hilo Jiwe Jeusi ambalo liko mbele yako na unitukuze Mimi kulingana na idadi ya mapazia hayo kwa kusema ALLAH-U-AKBAR!’ Kwa ajili hiyo, marudio saba ya kalimah hii yamepitishwa kwa ajili ya Swala, kwa sababu yalikuwepo mapazia saba.”

Yeye (s.a.w.w.) alizipita mbingu saba na mapazia saba ya utukufu na heshima, na akafika karibu na sehemu ya kuzungumza faragha na Mweyezi Mungu Mtukufu.

Swala ni Upandaji Mbinguni wa Mu’min. Hivyo pale mumini wa kweli anapopanda, na akazisoma Takbiir hizo saba, yale mapazia ya giza, ambayo kwa sababu ya makosa ya kuipenda dunia yanakuja kati yake na Mwenyezi Mungu, yanaondolewa, naye anamkaribia Bwana wa Mabwana.

Mwenyezi Mungu tena akamuamuru Mtume (s.a.w.w.), ‘Sasa umefika katika sehemu hii ya kuzungumza na Mimi, tamka Jina Langu.’ Kwa hivyo Mtume (s.a.w.w.), kama ipasavyo akasema, ‘Kwa Jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu’, na kwa hiyo kifungu hiki cha maneno kikawa kimefanywa kama ndio mwanzo wa kila sura.

Kwa kuamriwa atoe sifa, yeye alisema, ‘Kila sifa njema ni Yake Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe’, na akaendelea kwa namna hiyo mpaka akaisoma Surat-al-Fat’ha yote.

Kisha sauti ikamuamuru asome Suratul-Ikhlaas ikisema, ‘Sura hiyo ni maelezo juu ya Kusifiwa Kwangu na Hususia Zangu. Kuna kufanana gani kunakoweza kuwepo kati Yangu na viumbe Vyangu?’

Nilipokwisha kuisoma Sura hii, ‘Sema! Yeye Mwenyezi Mungu ni Mmoja; Mwenyezi Mungu ndiye anayekusudiwa haja; hakuzaa wala hakuzaliwa; wala hana anayefanana naye hata mmoja,’ sauti hiyo ikasema, ‘Inama (rukuu) mbele ya utukufu Wangu, na weka mikono yako juu ya magoti yako na utazame kuelekea kwenye Arshi Yangu.’

“Katika kufanya hivi, Mwanga kutoka kwenye Utukufu wa Mwenyezi Mungu ulinizidi nguvu, nami nikazimia, na kwa nguvu ya msukumo wa kimungu, mimi nikasema, ‘Sifa zote na shukrani ni za Mwenyezi Mungu Mtukufu.’ Kwa utakaso kabisa, nilimtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu, na nikaingiza na Sifa Zake.

Baada ya kurudia hili, mara nikarejewa na fahamu, na kule kutetemeka kwa nafsi yangu kukapungua, pale ambapo, kwa msukumo wa kimungu, nilipokuwa nimekwishatamka mara saba uingizaji wa sifa. Ndipo akaagizwa kwamba msemo huu wa sifa, katika utekelezaji wa Swala, lazima usomwe katika hali ya kurukuu.

Allah (s.w.t.) kisha akaniamuru mimi ninyanyue kichwa changu na nisimame wima, nikazisikia sauti za Malaika zikitamka sifa na kuweka umoja na shukurani kwa Mwenyezi Mungu. Mimi nikasema, ‘Mwenyezi Mungu anamsikia kila anayemtukuza.’

Nilitazama juu na nikaona mwanga mkubwa kabisa kuliko ule ambao ulinifanya nizimie hapo kabla, na hofu yangu ikawa kubwa kuliko katika ule mfano wa mwanzo.

Kutokana na woga uliochanganyika na heshima, nilianguka na kusujudu mbele ya Mwenye Enzi, Mola wa Utukufu, na nikaweka uso wangu juu ya udongo wa udhaifu, na kwa sababu ya utukuzaji huo, nilishuhudia, kwa kurudia mara saba, kwa msukumo wa kimungu, ‘Kutakasika na kila Sifa ni kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.’

Katika kila marudio ya sifa hii ya pekee, hofu yangu ilipungua, mpaka nikaondokana na ile hali ya woga mwingi, na nikafikia kwenye ufahamu kamili wa Allah (s.w.t.).

Kisha nikainua kichwa changu kutoka kwenye sijda, na nikakaa mpaka nikazindukana kutoka kwenye ule mshangao ambamo nilikuwa nimeangukia. Kwa msukumo wa kimungu, nikaangalia juu tena, na nikaona mwanga wenye nguvu zaidi kuliko ule nilioshuhudia kabla, na nikaanguka tena bila hiari kwenye sijda mbele ya Mola, na nikarudia mara saba, ‘Kutakasika na kila sifa ni kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.’ Baada ya hapo, nikawa na uwezo zaidi wa kuweza kutazama ile mianga mitukufu.

Nilinyanyua tena kichwa changu, na nikaketi kwa muda kidogo, na nikaangalia upandu walikokuwa Malaika.”

Kwa sababu hii, al-Majlisi (r.a.) anasema, sijda mbili katika (rakaa moja) Swala zikaanzishwa, na kukaa kwa muda kidogo baada yake kukalazimu kustahili kabisa.

Mtume (s.a.w.w.) anaendelea:

“Kisha nikanyanyuka na kusimama katika namna ya mtumwa mbele ya Mola Wangu, ambapo aliniamuru kusoma tena Suratul- Fat’ha, na baada ya hapo Surat al-Qadr. Niliinama tena na mikono yangu juu ya magoti yangu, na kisha nikasujudu kwa kuweka kichwa changu juu ya ardhi. Nilipokuwa nataka kunyanyuka, Mwenyezi Mungu akaniamrisha, ‘Taja fadhila Zangu kwako na utamke Jina Langu.’

“Kwa msukumo wa kimungu mimi nikasema, ‘Kwa Jina la Allah, na Kwake Yeye, Hakuna mungu ila Allah, na majina yote mazuri ni yake Allah.’

“Nilipokuwa nimerudia shahada zote mbili, Yeye aliniamrisha, ‘Tamka rehema juu yako mwenyewe na juu ya Kizazi chako.’ Mimi nikaomba du’a, ‘Ewe Allah! Teremsha rehema juu yangu na juu ya Familia yangu,’ ambayo ilijibiwa kwa baraka nyingi kutoka kwa Mola Mtukufu.

Katika kutazama huku na huko, niliona Malaika na nafsi za Mitume wamejipanga katika safu nyuma yangu, Mwenyezi Mungu akaniamrisha niwasalimie na mimi nikasema, ‘As-Salaam alaykum wa Rahmatul-llahi wa Barakaatuh.’ yaani, Amani, rehema na baraka za Mwenyezi Mungu ziwe juu yenu. Allah (s.w.t.) akazungumza na mimi akisema, ‘Mimi Ndiyo Amani, Rehema na Baraka zako, na za Maimamu baada yako.”

Kuuhudhurisha Moyo Katika Swala

Imam Ja’far as-Sadiq (a.s.) amesema:

“Mpendwa wangu ni yule mumin kutoka miongoni mwenu anayemwitikia Mwenyezi Mungu kwa moyo wake wakati wa Swala na haushughulishi moyo wake na jambo lolote la kawaida. Kwani, wakati wowote mwenye kuabudu anapomgeukia Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa moyo wake, wakati wa Swala, Mwenyezi Mungu humsikiliza na huigeuzia kwake mioyo ya waumini ambao wana muangalia kwa upendo, kufuatia mapenzi ya Allah (s.w.t.) juu yake.”(al-Hurr al-‘Amili, Wasa’ilush- Shi’ah, vi, 686)

Amir-ul-mu’minin, Imam Ali (a.s.) anasema: “Kama yule mwenye kuabudu angelijua ni kwa kiwango gani Rehema za Mwenyezi Mungu zilizomzunguka wakati wa Swala, asingenyanyua kichwa chake kutoka kwenye hali ya kusujudu.”

Kwa mujibu wa baadhi ya Hadithi, Swala imeitwa – safari ya kimbinguni ya mu’min ambayo inamkinga na utovu wa maadili. Ayatullah Ibrahim Amini anasema katika kitabu chake, Self Building – ujenzi wa nafsi – kwamba, ‘ni mkondo halisi wa mambo ya kiroho unaopendeza, ambao, yeyote anayeuingia mara tano kwa siku atatakasa nafsi yake kutokana na aina zote za uchafu na najisi.’

Vivyo hivyo, Swala iliyoswaliwa bila ya kuhwudhurisha moyo, ingawa inatimiza utekelezwaji wa wajibu wa lazima wa kidini, hata hivyo, haimsaidii mwenye kuabudu katika kumnyanyua kuelekea kwenye upeo wa juu kabisa wa kiroho.

Katika Hadithi nyingine, yeye, Ali (a.s.), amesema:

“Swala, nusu yake inaweza ikakubaliwa, au moja ya tatu yake, au robo, au moja ya tano, au hata moja ya kumi. Swala nyingine inaweza ikakunjwa kama nguo chakavu, na ikarushwa usoni mwa mwenyewe. Hakuna sehemu ya Swala ambayo ni yako, isipokuwa ile ambayo unayoiswali kwa moyo unaozingatia.” (Bihar al-Anwar, Juz. 81, uk. 260, Mlango wa 16, Hadithi ya 59)

Hadithi kama hiyo inasimuliwa na al-Kulayni (r.a.) ndani ya al- Kafi, 3, uk. 363. Al-Baqir na as-Sadiq (a.s.) wameendelea kusema: “Hakuna chochote cha Swala ambacho ni chako isipokuwa kile ulichokifanya kwa moyo mzingativu.

Hivyo, kama mtu ameiswali yote kwa makosa, au amepuuza nidhamu zake, itakunjwa na kurushwa usoni mwa mwenyewe.”(Wasa’ilush–Shi’ah, Juz. 4, uk.687, Mlango wa 3, Hadithi ya 1)

Imam as-Sadiq (a.s.) anatuonya sisi kwamba:

“Wakati mja anaposimama ili kuswali, Allah (s.w.t.) humsikiliza yeye kwa makini, na hauhamishi uzingativu Wake mpaka mja huyo atakapokengeuka kutoka kwenye kumkumbuka Yeye kwa mara ya tatu. Wakati hili linapotokea, Allah (s.w.t.) Naye pia hugeuzia mbali mazingatio Yake kutoka kwa mwenye kuabudu.”

Kwa hiyo, kuhudhuria kwa moyo ni jambo la lazima katika kila tendo la ndani ya swala, na hiyo ndio njia pekee ya kuweza kupata faida zilizofichwa katika wajibu huu mkubwa. Imesimuliwa katika Bihar al-Anwar kwamba katika mifano hiyo ya hapo juu, kama mwenye kuabudu anarudisha mazingatio yake, na akajitahidi asipoteze umakinifu wake, basi madhambi yake yaliyopita yanafutwa na atapewa rehema ambazo kwamba malipo yake hayawezi kuhesabika. Allah (s.w.t.) Anasema:

“Fanya mazingatio juu Yangu, kwa sababu Mimi na Malaika tunakuangalia kwa makini (katika Swala yako).”

Kwa mujibu wa al-Khumeini (r.a.), ‘ukweli wa du’a na dhikri ni ule uombaji du’a wa moyo, ambao bila huo, maombi ya ulimi tu hayatafanikiwa na yatakuwa hayana maana yoyote. Hii imerejelewa katika idadi ya Hadithi.’

Katika kitabu chake, Self Building, al-Amini anasimulia:

‘Kwa vile ambavyo kuhudhuria kwa moyo ni muhimu na kwenye manufaa, kwa kiwango hicho hicho, upatikanaji wake ni mgumu sana. Mara tu mtu anapoanza swala yake, shetani ananong’oneza katika moyo wake na kumvuta kutoka upande mmoja hadi mwingine, na kuendelea kumshughulisha kwenye aina zote za mawazo na kumbukumbu.

Moyo unajishughulisha wenyewe na kuhesabu, kupanga, kuchunguza upya matatizo yaliyopita na yajayo, kutatua matatizo ya kitaaluma, yanayojikusanya mara kwa mara wakati wa Swala, na mambo, ambayo alikuwa ameyasahau kabisa. Na anapozinduka mwenyewe, anagundua kwamba Swala yake imekwisha.’

Mikakati Ya Kumakinika Katika Swala: Utangulizi

Mawazo ni kama msuli. Mwanzoni, pale unapojaribu kuweka mawazo yako juu ya jambo fulani, inaweza kuonekana kana kwamba unatumia nguvu nyingi zaidi na inachokesha. Dhana hiyo ni thabiti, kwani unapaswa kutumia nguvu ili kudumisha mawazo. Hata hivyo, jinsi unavyonyoosha zaidi mawazo yako hayo, ndio yanavyozidi kuwa na nguvu zaidi, na mepesi kuyashika.

Kuanzia ule muda unapozaliwa, ubongo wako hufanya kazi kila sekunde, dakika, saa, na siku ya maisha yako. Unafanya kazi mchana na usiku, na zaidi sana unapokuwa macho, pungufu kidogo unapokuwa umelala, lakini ni wenye kuendelea kufanya kazi.

Ni dhahiri, kwa hiyo, kwamba mfululizo wa mawazo utaendelea wakati unaposwali Swala yako isipokuwa kama utafanya mabadiliko kwenye namna unavyoshughulika kwenye Swala yako.

Kuandaa Mandhari Ya Swala Na Kuchoma Ubani

Mahali unaposwalia panapaswa pawe maalum. Kila kitu ambacho kinaweza kukuondoa mawazo yako kutoka kwenye Swala kinapashwa kushughulikiwa. Chumba hicho kiwe sio kile unachotumia wakati wote, na kiwe kisafi na nadhifu, joto la kuridhisha, na kiwe na giza.

Kwa kuwa na joto la kuridhisha, huna haja ya kuwa na wasiwasi wa kuendekeza mawazo ambayo yanaweza kukuchanganya wakati chumba kikiwa na joto au baridi. Ngozi ya mwanadamu imejaa vipokea joto ambavyo wakati wote vitakukumbusha juu ya mchafuko wowote kwenye mwili wako.

Kama chumba unachotumia kwa kuswalia kina giza kidogo, ile hisia ya giza inatuingizia hofu na woga, inaongeza umakinifu wa mtu kwa kuzuia zaidi uwezo wa kuona. Kadiri ya uchache wa vitu unavyoweza kuona wakati wa Swala, ndio inavyokuwa bora zaidi. Kuta lazima ziondokane na mapicha na vitu vinginevyo ambavyo vinaweza kuvuta mawazo yako au kuamsha kumbukumbu au fikra.

Unashauriwa vilevile kuchagua sehemu iliyojitenga isiyo ya kelele au vurugu. Hupaswi kuwa na ukaribu sana na simu, kwani mlio wake utasababisha fikira akilini mwako kuhusu umuhimu wa ujumbe wa simu hiyo.

Pia unapaswa ukae mbali na aina yoyote ya harufu nzuri kutoka jikoni ili kukuwezesha kulenga zaidi kwenye jukumu lililoko mbele yako, badala ya kutokwa na mate na kufikiria kuhusu chakula wakati wa Swala. Mwishowe, ni lazima uthamini na kuheshimu mawasiliano yako na Allah (s.w.t.) kwa kurudisha milango (sio kuifunga kabisa) ya chumba unachoswali ndani yake, ili usiweze kusikia watu wengine wa familia wakizungumza na watoto wakipigiana makelele.

Unapaswa kuchoma ubani ili kukinukisha manukato chumba chako cha Swala. Ni kitendo kilichopendekezwa sana na kinachukua uzito muhimu katika utafiti na sayansi. Kuna ushahidi wa maana kabisa katika matumizi ya kuchoma ubani, kwa vile hii ni njia moja kubwa ya kutuliza wasiwasi na mihemko ya mtu, na kutokana na kupumua kuzito na kutafakari, hali ya ndani kabisa ya utakaso mkubwa hupatikana. Wataalamu wa matibabu ya hewa nzuri ni mabingwa katika nyanja hii na mafuta wanayotumia kupaka kwenye ngozi au kuyachoma ili kutoa harufu yanaweza kwa uwazi kabisa kupunguza mfadhaiko katika ubongo, kulegeza mkazo wa misuli, kupunguza msongamano wa mawazo, na hivyo kuongeza mazingatio katika Swala.

Kwa mujibu wa watafiti, zile nguvu za kimanukato za mafuta fushi1 (essential oils), halisi na ya asili, ni kichocheo cha mabadiliko katika akili na mwili wa mwanadamu. Harufu nzuri ya mafuta fushi husisimua sehemu ya ubongo ambayo inaathiri hisia.

Umbo la molekuli ya mafuta fushi ni kama ufunguo unaofungua kitu kama kufuli katika vipokezi vya neva za harufu ndani ya mianzi ya pua zetu. Harufu ya manukato inapelekwa moja kwa moja na haraka sana kwenye limbic system – mfumo ulioko kwenye akili, ambamo kumbukumbu zinahifadhiwa, na furaha na mihemko hufahamika. Inapokuwa umezimuliwa, mfumo huo, limbic system, hutoa kemikali ambazo huathiri mfumo wa neva.

Serotonin (kisafirisha ujumbe viungoni) huzuia wasiwasi, endorphins kupunguza maumivu, na kadhalika.

Kuvuta hewa ya mafuta fushi kunaweza pia kumsaidia mtu kupata mlingano maridhawa wa kihisia.

Hali ya mlingano wa kihisia badala yake inaweza kuwa na matokeo ya maarifa ya tiba juu ya matatizo ya kimwili, hususan yale ambayo yanatokana na shinikizo la kazi.

Kwa hiyo, kuongeza kiwango chako cha umakinifu, kwa njia ya kujiliwaza kwa mafuta fushi, kwa kutumia uvutaji harufu yake moja kwa moja au kujifukiza kumependekezwa sana. Uvutaji hewa wa moja kwa moja una faida sana pale msaada wa haraka unapohitajika.

Kwa mfano, kutuliza mawazo yanayochokesha, wasiwasi au uzito kabla ya Swala, dondosha matone 2-5 ya dawa ya chamomile kwenye kitambaa cha mkono (leso), kishike chini ya pua yako kisha vuta hewa yake kwa nguvu.

Kwa sababu ya asili yao ya kugeuka hewa au mvuke, mafuta fushi yatasambaa kwenye hewa bila shida. Taa ya matibabu ya njia ya harufu, chombo cha ufinyanzi kilichowekwa kibeseni kidogo kuzuia mchanganyiko wa maji na mafuta fushi ni njia nzuri ya kufukiza manukato. Kibeseni hicho kinapashwa moto kutoka chini yake kwa mshumaa au taa ya umeme. Kufukiza mafuta yanayoliwaza kama Chamomile, marashi ya waridi au msandali kunaweza kupunguza kabisa uzito katika ubongo, hivyo kukuwezesha wewe kuwa makini katika Swala yako.

Wudhu Kama Njia Ya Kuongeza Mazingatio Yako

Wudhu ni mojawapo ya njia zinazofaa za kuandaa mandhari ya Swala yako ya kila siku. Ni njia yenye nguvu za kupangilia sawa sawa mawazo yako kabla ya Swala na kukusaidia katika kutekeleza Swala yako kwa kujiamini na usiyumbishwe na shetani aliyelaaniwa.

Kuchukua wudhu taratibu na kutafakari juu ya maneno ya kwenye du’a iliyopendekezwa katika kila uoshaji kutakusaidia kwa kiasi kikubwa sana kufikiri juu ya maisha yako, kifo na Muumba ambaye utasimama mbele Yake muda mchache ujao. Kwa njia hii, unachukua wudhu kama mkakati wa kupanga upya mawazo na kujiandaa kwa swala. Pasiwepo na mwanya wa kuzungumza na kujadili mambo ya kidunia baina ya uchukuaji wudhu na Swala yako.

Kama kutakuwa na mwanya, itakupasa usome du’a. Namna hii kiungo cha umakinifu kati ya wudhuu na swala kitapatikana. Kweli, jinsi unavyotumia muda mwingi katika kutaamali na fikra ya kuwa na wazo moja tu kabla ya Swala, ndio unavyokuwa na uwezekano zaidi wa kuswali bila ya kujichanganya.
________________________
1. Mafuta yanayotumika katika dawa kwa kufukiza au kuvuta hewa yake, yatokanayo na miti ya asili

Dua hii ni wakati unapoanza kutawadha, unaanza kwa Jina la Mwenyezi Mungu (s.w.t.), na kumshukuru Yeye kwa kuyafanya maji kuwa tohara.

Ni katika kuosha mikono, unamuomba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akuweke miongoni mwa wale wanaoomba msamaha Wake na wale ambao wametoharika.

Wakati unaposukutua kuosha mdomo wako, unamuomba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akufundishe njia sahihi ya kujibu maswali Siku ya Kiyama utakapokuwa kwenye Hadhara Yake Tukufu.

Wakati unaposafisha pua, unamuomba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) asikunyime harufu ya Peponi na akuweke miongoni mwa wale wanaoyanusa manukato yake.

Wakati wa kuosha uso, unamuomba Allah (s.w.t.) aung’arishe uso wako katika siku ambayo Yeye atazifedhehesha na kuzifanya nyeusi nyuso za idadi kubwa ya watu.

Wakati wa kuosha mkono wa kulia, unamsihi Allah (s.w.t.) kuweka daftari ya matendo yako kwenye mkono wako wa kulia na hati ya uthibitisho wa kudumu ndani ya Pepo kwenye mkono wako wa kushoto, na kwamba Akufanyie mahesabu yako kwa wepesi wa huruma.

Wakati wa kuosha mkono wa kushoto, unamuomba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) asiweke daftari ya matendo yako kwenye mkono wako wa kushoto, wala kutoka mgongoni kwako, na asikitundike kwenye shingo yako. Pia unatafuta kusalimika kutokana na Moto mkali wa kudumu wa Jahannam.

Wakati wa kupaka kichwa, unamuomba Allah (s.w.t.) akufunike na Rehema, Baraka Zake na Msamaha Wake.

Mwishowe, wakati wa kupaka miguu, unamuomba Allah (s.w.t.) akuimarishe katika Sirat Yake katika Siku ile ambapo miguu itateleza, na kuzifanya nguvu zako kama za wale ambao watamridhisha Yeye.

Imesimuliwa katika Hadithi sahihi kwamba Maimam Ma’sum (a.s.) walikuwa wakitetemeka na wakati mwingine hata rangi za nyuso zao zilibadilika, wakionyesha hofu na woga juu ya Allah (s.w.t.) wakati walipokuwa wakitekeleza hatua za wudhu. Mtu anapaswa kujenga na vilevile kudumisha hofu wakati anapotawadha.

Ni kwa faida yako kama wakati wote utakuwa unatafakari kuwepo kwa Allah (s.w.t.) na Nguvu Zake, Dalili na Maamuzi Yake kuhusiana na dunia hii na ile ijayo. Kutambua kuweko Kwake ni njia mojawapo ya kuleta hushui kwenye moyo wako na Kujinyenyekeza mwenyewe katika Swala yako iliyoswaliwa kwa uangalifu na kwa makini. Ni Yeye tu ambaye anakuangalia kwa upole kabisa wakati wa Swala yako, na unapaswa kuliweka hili akilini kila wakati unaposwali.

Abu Ja’far, mtoto wa Babawayh al-Qummi (r.a.) anasema:

“.......Allah (s.w.t.), Aliyetukuka, ni Mmoja na wa Pekee Kabisa. Hakuna mwingine kama Yeye. Ni Mkubwa; Yeye kamwe hakuwa, na kamwe hatakuwa, ila Mwenye kusikia na Mwenye kuona. Mjuzi wa yote; Mwenye Hekima; Aliye Hai; Wa Milele; Mwenye nguvu; Mtukufu; Mwenye Kujua; Mwenye Uwezo; Mwenye Kujitosheleza.

Yeye ni wa Pekee, Kimbilio la Milele; Hakuzaa kwamba anaweza kurithiwa, wala Hakuzaliwa kwamba Anaweza kushirikishwa na wengine. Hakuna mwingine kama Yeye.

Hana anayelingana naye wala mpinzani, mwenza wala wa kuandamana naye. Hakuna kinachoweza kufananishwa Naye. Yeye hana adui wala mshirika. Macho ya mwanadamu hayawezi kumuona, ambapo Yeye anatambua uwezo wa macho. Fikra za wanadamu haziwezi kumzingira, ambapo Yeye anazielewa. Usingizi haumpitii, wala halali. Yeye ni Mwingi wa Rehema na Mjuzi, Muumba wa vitu vyote. Hakuna mungu ila Yeye. Uwezo wa kuumba na Mamlaka ni Vyake peke Yake. Baraka ni za Allah (s.w.t.), Mola wa Ulimwengu.”

Kwa hiyo, uchamungu, ustahimilivu na kumtambua Mwenyezi Mungu na Uweza Wake ni viambato vyenye athari sana katika kujenga na kudumisha uangalifu wako katika Swala. Kwa njia hii, unaweza kujinyenyekeza mwenyewe katika Swala

Mfano mzuri ni kutoka kwa Mtume (s.a.w.w.) aliyekuwa akiiendea swala kwa dhati kabisa na alitoa uangalifu wake wote na umakinifu. Alimtambua na kumuelewa Muumba wake kiasi cha kutosha kuhofia Kuwepo Kwake na kuhudhuria kwa umakinifu kamili wakati anaposimama mbele Yake. Imam al-Khumein (r.a.) anasimulia Hadithi kwamba, Kwa miaka kumi Mtume wa Allah (s.w.t.) alisimama kwa vidole vyake (katika Swala) mpaka miguu yake mitukufu ikavimba na uso wake ukapauka. Na angeweza kusimama wima usiku wote, hadi ukafika muda ambapo Mwenyezi Mungu akamliwaza (kwa Aya ifuatayo):

مَا أَنْزَلْنَا عَلَيْكَ الْقُرْآنَ لِتَشْقَىٰ {2}

 

Hatukukuteremshia Qur’an ili upate mashaka (20: 2)

As-Saduq (r.a.) anasimulia ushauri ufuatao kutoka kwa Imam as- Sadiq (a.s.) ambao aliutoa kwa mmoja wa wafuasi wake waaminifu:

‘Ewe mja wa Allah! Wakati unaposwali, swali kama mtu anayeaga na anayehofia kwamba hatarudi tena kamwe (yaani, swali kwa namna kama unaswali swala ya mwisho ya maisha yako). Kisha elekeza macho yako kwenye sehemu yako ya kusujudia. Kama unapojua kuwa kuna mtu kulia au kushotoni kwako, huwa unakuwa muangalifu sana katika kutekeleza Swala yako; basi ufahamu kwamba unasimama mbele ya Anayekuona na wewe humuoni.’ (Al-Hurr al-Amili, katika Wasa’il as-Shi’ah, juz. iv, uk.685)

Moja ya sababu za kwa nini Adhana na Iqama zimesisitizwa sana kabla ya Swala ni kusimamisha kiungo imara kati ya mwenye kuabudu na Muumba wake, kabla hajajasiri kwenye safari hii takatifu Swala na kuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na Mwenyezi Mungu. Kwa njia hii, unaanza kujikumbusha na kujihakikishia wewe mwenyewe juu ya kuwepo kwa Allah (s.w.t.) kabla hujaianza Swala:

إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لَآيَاتٍ لِأُولِي الْأَلْبَابِ {190}

 

الَّذِينَ يَذْكُرُونَ اللَّهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِهِمْ وَيَتَفَكَّرُونَ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَٰذَا بَاطِلًا سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النَّارِ {191}

 

Hakika katika kuumba mbingu na ardhi, na kutofautiana kwa usiku na mchana, ni dalili kwa watu wenye akili. Ambao humkumbuka Mwenyezi Mungu wakiwa wamesimama wima, na wakiwa wamekaa, na wakilala, na wanatafakari juu ya kuumbwa kwa mbingu na ardhi, (wakisema) Mola wetu! Hukuviumba hivi bure tu, utukufu ni Wako, basi tuepushe na adhabu ya Moto. (3:190-191)

Hakika katika kuumba mbingu na ardhi, na kutofautiana kwa usiku na mchana, ni dalili kwa watu wenye akili. Ambao humkumbuka Mwenyezi Mungu wakiwa wamesimama wima, na wakiwa wamekaa, na wakilala, na wanatafakari juu ya kuumbwa kwa mbingu na ardhi, (wakisema) Mola wetu! Hukuviumba hivi bure tu, utukufu ni Wako, basi tuepushe na adhabu ya Moto. (3:190-191)

Mwanachuoni mkubwa, al-Mutahhari (r.a.) ananukuu Hadithi, ambayo imerejewa ndani ya kitabu kiitwacho The Light Within Me:

“Madhumuni ya Dhikr – kumkumbuka Allah (s.w.t.) ni kwamba moyo wakati wote uwe unalitambua al-Haqq, Jina la Mwenyezi Mungu (s.w.t.), yaani, Mkweli Zaidi, kwani kulitumia kwake kunaondosha ile hali ya kutokuwa makini.” Dhikr zina umuhimu kama ule wa maji yalivyo kwa chembe hai ndani ya mwili wako.

Chukulia kwa mfano, ile hewa unayovuta mchana na usiku, ambayo kwayo uhai wako na vilevile ule wa viumbe hai vingine unategemea, hakuna kinachoweza kubakia hai bila hiyo hewa. Ni zawadi nzuri ya ajabu iliyoje. Kama viumbe vyote vingepanga kitu kama hicho, haviwezi kulifanya hilo.

Na hilo linaingia hata kwenye zawadi nyingine ambazo tumezawadiwa bila wasiwasi wowote, kutoka kwa Mwenyezi Mungu (kama vile kuona, kusikia, kuonja na kadhalika), kila mojawapo ikiwa na faida zisizo na ukomo.

Anakutimizia mahitaji yako katika dunia hii na ya akhera, bila kuhitajia kuabudu kwako. Kuzishika amri Zake au kuzivunja hakuleti tofauti yoyote Kwake. Ni kwa ajili ya faida yako mwenyewe kwamba Yeye ameamrisha mema na kukataza maovu.

Imam al-Khumeini (r.a.) anaelezea kwamba ‘unapoyakumbuka yote haya, je, huoni kwamba kumheshimu na kumtii Mfadhili kama huyu ni muhimu juu yako? Yeye ndiye Muumba na Mfalme wa ulimwengu huu mkubwa, ambao kutokuwa na kikomo kwake hakuwezi kupimwa au kufikiwa na akili ya mwanadamu.

Sisi wanadamu, viumbe tunaotambaa juu ya moja ya sayari ndogo, kwa huzuni sana tunashindwa kufahamu eneo la udogo wa dunia yetu wenyewe, ambayo jua lake haliwezi kulinganishwa na majua ya makundi ya nyota yasiyo na idadi.

Mfumo wetu wa jua na sayari zake si chochote ukilinganishwa na mifumo midogo mingine ya jua, ambayo bado inayatatiza macho makini ya wavumbuzi wakubwa na wachunguzi wa dunia.’

Tumeshauriwa na wanavyuoni wa kiislamu kujaribu kumkumbuka Allah (s.w.t.) wakati wote unaowezekana. Hii ni pamoja na kukariri baadhi ya nyiradi za ibada na kujifunga, au inaweza kuwa namna ya tafakari, kuthamini dunia hii na ile ya akhera.

At-Tabatabai (r.a.) katika kitabu chake, al-Mizan, Juzuu ya Pili, anaelezea namna ya kuishi ambayo ni furaha zaidi na maisha ambayo ni yenye kudumu zaidi. Katika simulizi hii, ad-Daylami anasimulia katika al-Irshad yake kwamba Allah (s.w.t.) katika hatua moja wakati wa Mi’raj, alimwambia Mtume (s.a.w.w.):

“Na kwa njia ya furaha ya namna ya kuishi, ni ile ambayo ndani yake mtu hachoki kunikumbuka Mimi, hasahau neema Zangu, na hapuuzi haki Zangu (juu yake). Anazitafuta radhi Zangu mchana na usiku.

Uhai wa milele unatambulika pale mtu anapotumikia manufaa yake ya kiroho mpaka dunia ikapoteza umuhimu kwake yeye, na ikaonekana ni ndogo machoni mwake. Akhera inakuwa ndio kubwa kwake.

“Anatoa kipaumbele kwenye radhi Zangu kuliko kwenye matamanio yake; anazitafuta radhi Zangu; anaifikiria haki ya neema Yangu kuwa ni kubwa; anakumbuka akilini mwake yale Niliyomfanyia yeye (yaani, kwa manufaa yake); ananikumbuka Mimi mchana na usiku kila anaposhawishika kutenda ovu lolote lile au dhambi; anauweka moyo wake safi kutokana na yale ninayoyachukia Mimi; anamlaani shetani na minong’ono yake, na hamruhusu shetani kuanzisha ushikiliajia,au njia ya kuingilia kwenye moyo wake.

“Anapofanya namna hii, basi Mimi huweka mapenzi Yangu kwenye moyo wake, mpaka Ninaufanya moyo wake na vilevile mapumziko na kushughulika kwake, na mawazo na kauli zake, kuwa sehemu ya fadhila Zangu ambazo Nimezishusha juu ya wale miongoni mwa viumbe Wangu wanaonipenda; na Ninalifungua jicho na sikio la moyo wake, ili awe anasikia kwa moyo wake na anaangalia kwa moyo wake kwenye Utukufu na Ukuu Wangu; na Ninaifanya dunia kuwa nyembamba juu yake na kumfanya aichukie pamoja na starehe zake zote; na Ninamtahadharisha juu ya dunia na vyote ilivyonavyo, kama mchungaji anavyowazuia kondoo wake kwenye ardhi ya malisho yenye hatari.

“Hili linapotokea, anawakimbia watu na anahama kutoka kwenye nyumba ya kumalizia na kwenda kwenye makazi ya milele, na kutoka kwenye nyumba ya shetani kwenda kwenye Makao ya Allah (s.w.t.), Mkarimu. Ewe Ahmad! Mimi ninampamba na heshima na utukufu. Hivyo, hii ndio njia nzuri ya kuishi na ya maisha ya milele, na ndio hali ya wale ambao wameridhika (Nami).

“Kwa hiyo, yeyote atakayetenda kwa ajili ya radhi Zangu, Mimi humpa sifa tatu: Ninamfundisha shukrani, ambayo haikuchafuliwa na ujinga, ukumbusho, ambao haukuchanganyika na usahaulifu, na upendo ambao unachukua kipaumbele juu ya mapenzi ya viumbe. Kisha pale anaponipenda Mimi, Nami ninampenda na kulifungua jicho la moyo wake kwenye Utukufu Wangu. Sivifichi viumbe (Vyangu) maalum kwake yeye. Ninazungumza naye sirini katika giza la usiku na mwanga wa mchana, mpaka anakoma kuongea na kukaa na viumbe.

“Ninamfanya ayasikie maongezi Yangu na maneno ya Malaika Wangu. Ninaifanya siri Yangu ijulikane kwake, ambayo Nimeifanya ifichikane kwa viumbe (Wangu) wote. Ninamvalisha kwa kadiri, mpaka viumbe wote wawe na staha juu yake.

Anatembea katika ardhi (na madhambi yake yote yakiwa) yamesamehewa. Ninaufanya moyo wake kuwa wenye kusikia na kuona, na simfichi kitu chochote cha Peponi au Motoni. Ninayafanya yajulikani kwake, hofu na mateso yanayowangojea watu hiyo Siku ya Kiyama, na kuhusu mambo ambayo Nitawauliza matajiri na masikini, vilevile wasomi na wajinga.

“Nitamfanya alale (kwa amani) ndani ya kaburi lake, na Nitawatuma Munkar na Nakir (a.s.) kwenda kumuuliza maswali. Hatapatwa na huzuni ya kifo au tishio la utangulizi (la dunia ijayo). Kisha nitaisimamisha mizani yake ya vipimo kwa ajili yake, na nitakikunjua kitabu chake (cha matendo). Halafu nitakiweka kitabu chake kwenye mkono wake wa kulia na atakisoma kikiwa kimekunjuliwa. Tena Sitaweka mkalimani yoyote kati Yangu na yeye.

“Hivyo hizi ndio sifa za wapenzi. Ewe Ahmad! Fanya shughuli yako kuwa shughuli moja, fanya ulimi wako kuwa ulimi mmoja, na ufanye mwili wako (yaani, nafsi yako) kuwa hai ambayo kamwe haiwi yenye kutokunikumbuka (Mimi). Yeyote ambaye hanikumbuki Mimi, Sitajali ni kwenye bonde gani anakopotelea.”

Hali ya uchangamfu wa akili ni moja ya viambato vingi muhimu vya Swala. Kama umechoka na uko hoi taabani, ni bora kupumzika na ufanye mazoezi ya kuvuta hewa kwa nguvu na ya kulegeza mwili kabla ya kufanya uamuzi ya kusimama mbele ya Mola wako. Na hasa, inapendekezwa kuswali kwa kuchelewa kidogo lakini kwa mazingatio na umakini.

Kwa kweli, uchelewaji katika kusimamisha Swala kutoka kwenye wakati wake uliopangwa unapaswa uwe kwa kiasi cha muda mtu anaoweza kupumzika na kujirudishia nguvu, na kupata nishati ya kusimama mbele ya Mwenyezi Mungu. Kama Imam Ali (a.s.) alivyotushauri: ‘Usiswali katika hali ya kusinzia. Wakati unaposwali, usijifikirie wewe mwenyewe kwa sababu umesimama mbele ya Allah (s.w.t.).

Kwa hakika ni sehemu ile tu ya Swala itakayokubaliwa ambayo mtu ameweka uangalifu kamili kwa Allah (s.w.t.).’

As-Saduq (r.a.) anasimulia kutoka kwa Imam Ali (a.s.) kwamba alisema: ‘Mmoja wenu asisimame kwa ajili ya Swala katika hali ya uzembe na kusinzia, wala hupaswi kuruhusu mawazo (yasiyo na mpangilio) kupita kwenye akili yako (katika hali ya Swala). Kwani, katika hali hiyo, unasimama mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwa hakika malipo ambayo mwenye kuabudu anayoyapata kutoka kwenye swala yanalingana na kiwango chake anachokifanya kwa moyo uliotulia.’ (Al-Hurr al-Amili, katika Wasa’il al-Shi’ah, vi, 687)

Katika Fiqh al-Ridha imeelezwa kwamba: “Wakati unapotaka kuswali, usisimame kivivu, kwa kusinzia, haraka haraka, au kwa kutokujali. Iendee kwa utulivu, kwa taadhima na taratibu.

Lazima uonyeshe kujisalimisha, kwa kusihi sana na kwa unyenyekevu kabisa kwa Allah (s.w.t.). Unapaswa kuonyesha woga na dalili za hofu na matumaini, kwa tahadhari na wasiwasi. Kwa maana hiyo, unapaswa kusimama mbele Yake, kama mtumwa mtoro na mwenye makosa anavyosimama mbele ya bwana mmiliki wake; kwa tahadhari, na visigino vilivyokutanishwa, pingiti lililosimama wima, asiyemangamanga kulia au kushoto, ukifikiria kama unamuona Yeye. Kama wewe humuoni, Yeye kwa hakika anakuona... (Musradrak al-Wasa’il, Mlango wa 1, Hadithi ya 7)

Kisimamo cha Imam Ali (a.s.) kilimruhusu yeye kutulia na kuwa ameridhika. Kisimamo chako katika Swala vilevile ikuruhusu kubaki kuwa mchangamfu na mwenye fahamu. Kuna uhusiano wa namna mbili kati ya kujibwaga na mfadhaiko.

Usimamaji mzuri una maana kwamba kuna uwiano mzuri wa misuli na mifupa. Uwiano huu unasaidia kuzuia viungo katika uti wa mgongo kutokana na uzito mkubwa. Unalinda vilevile dhidi ya kujeruhiwa na uwezekano wa ulemavu. Usimamaji mzuri unasaidia kuzuia uchovu na maumivu ambayo husababisha mfadhaiko.

Vile umakini wako kwenye Swala unavyoongezeka, umetaboli (ujengaji na uvunjaji wa kemikali) kwenye mwili wako kwa jumla utashuka taratibu, mpaka mapigo yako ya moyo na upumuaji vinakuwa vigumu kutambulika.

Katika hatua hii, pale unapokuwa umeelekea moja kwa moja kwenye swala yako, ndipo unapopata mafanikio makubwa zaidi kutoka kwenye ibada ambayo ina malipo yasiyo na kikomo. Utaelekea kama uko kwenye hatua ambapo uchovu wa akili na mfadhaiko vinatoweka kirahisi.

Baada ya kumaliza Swala yako, mara nyingi utajihisi umeliwazika, umepata nguvu mpya, mchangamfu, na mwenye fikira nzuri. Hisia zako zitakuwa kali. Utajikuta mara nyingi ukiwa na hisia za utambuzi zilizoongezeka. Utajisikia kwa kawaida umwenye kujiamini na salama katika hali nzuri ya akili. Furaha itakuwa ni yako. Hii ndio hali ya akili unayopaswa kupigania kuipata baada ya kumaliza Swala yako.

Ni wazi kabisa kwamba kama hujitahidi kujifunza na kuelewa maana ya Aya na dhikr unazozitamka ndani ya Swala yako, unakuwa una nafasi ndogo sana ya kuendeleza na kudumisha ule umakini unaouhitaji kuulenga kwenye Swala. Kulenga kwenye maana za yale unayosoma kwa kawaida kutaishughulisha akili yako iwe itahusika kwenye Swala.

Katika kitabu Thawab al-A’mal, as-Saduq anasimulia kwa sanad ya wapokezi kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.):

‘Mtu anayeswali rakaa mbili za Swala kwa kukielewa anachokisema ndani yake, hazimalizi rakaa hizo bila ya Mwenyezi Mungu kumsamehe yeye kila dhambi iliyoko baina yake yeye na Mwenyezi Mungu.’ (Wasa’il al-Shi’ah, vi, 686)

Kuelewa kila neno unalolisoma ndani ya Swala kunasaidia katika kujenga akili tulivu na katika kukuwezesha kudhibiti mawazo na hisia zako zinazofuatia ambazo zinaweza kukuondoa kwenye Swala yako. Unahitaji pia kuyazingatia maneno hayo na maana zake katika lugha yako unayopendelea, yasome na kuyaelewa kiasi kwamba akili yako haitangitangi na inabakia imelengwa kwenye kazi iliyoko mbele yake.

Hata hivyo, mtu asifikiri na kutafakari juu ya maana yake kwani huu sio muda wake wa kutafakari, bali aishughulishe akili yake na maana ya vifungu vinavyosomwa.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) anasimuliwa kwamba alimwambia Abu Dharr:

“Rakaa mbili nyepesi za swala zilizotekelezwa kwa mazingatio ni bora zaidi kuliko usiku mzima uliotumika katika ibada” (Bihar al-Anwar, Juz.74, uk.82 na Wasa’il al-Shi’ah, vi, 686)

Mwenyezi Mungu ni Mkubwa
 

Tarjuma Ya Surat-Al-Hamd

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehma, Mwenye kurehemu

Kila sifa njema ni ya Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe

Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu

Mwenye kumiliki Siku ya malipo

Wewe tu, ndiye tunayekuabudu, na kwako tu tunataka msaada

Tuongoze katika njia iliyonyooka

Njia ya wale uliowaneemesha, siyo ya wale walioghadhibikiwa, wala ya wale waliopotea.

Tarjuma Ya Surat-Ul-Ikhlaas

Kwa Jina la Mweyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu

Sema; Yeye Mwenyezi Mungu ni Mmoja

Mwenyezi Mungu ndiye anayekukusudiwa kwa haja

Hakuzaa wala Hakuzaliwa

Wala hana anayefanana naye hata mmoja.

Tarjuma Ya Dhikr Wakati Wa Rukuu Na Sajidah

Ametakasika Mola wangu aliye Mtukufu na ninamtukuza

Ametakasika Mola wangu aliye Mkuu na ninamtukuza

Kabla Ya Kwenda Sijdah

Amezisikia na kuzikubali Mwenyezi Mungu, sifa za mwenye kumsifu

Istighfari Baina Ya Sajdah Mbili

Ninaomba maghfira kwa Mwenyezi Mungu, aliye Mola wangu na ninarejea Kwake

Wakati Unapokuwa Unanyanyuka

Ninasimama na kukaa kwa msaada na nguvu za Mwenyezi Mungu

Tarjuma Ya Tasbihi Nne

Utukufu ni wa Mwenyezi Mungu, na kila sifa njema ni Zake, na hakuna apasaye kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni Mkubwa kuliko kila kitu.

Tarjuma Ya Tashahudi Na Salaam

Nashuhudia kwamba hapana apasaye kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu, Ambaye ni Mmoja na hana mshirika.

Na ninashuhudia kwamba Muhammad ni mja na Mtume Wake

Ewe Mwenyezi Mungu mshushie rehema na amani, Muhammad na kizazi chake.

Amani iwe juu yako ewe Mtume, na rehema za Mwenyezi Mungu na baraka Zake .

Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yetu, wale tunaoswali, na juu ya waja wote wema wa Mwenyezi Mungu

Amani, rehema na baraka zake Mwenyezi Mungu ziwe juu yenu, enyi waumini!

Lugha ya Kiarabu inafikiriwa kuwa tamu zaidi katika lugha zote. Kwa hiyo, kuswali Swala kwa matamshi sahihi (Makhaarij) na kufuata kanuni za lugha ya Kiarabu (Tajwiid) na kujifunza kanuni za kusoma Qur’an Tukufu, kutazifanya juhudi zako katika kudumisha uzingatiaji kuwa rahisi mno.

Kuisikiliza sauti yako mwenyewe (na sauti za watu wengine), na jinsi zinavyoweza kusikika vibaya na butu wakati mwingine ni njia nyingine mbadala. Unapaswa kujaribu kubadili sauti yako hadi kufikia ile inayofaa.

Kuchanganya hizo kanuni za usomaji na marudio ya kusoma kwako ndio kunakotakikana na kunahitaji kufanyiwa mazoezi. Sifa hizi kwa Mtume (s.a.w.w.) ndizo zilizokuwa zikiwafanya watu kukaa na kumsikiliza Mtume (s.a.w.w.) akisoma Qur’an Tukufu.

Kama utakuwa nazo sifa hizi katika sauti yako, basi kamwe hutajihisi kuchoka na kuishiwa nguvu ya kusoma Sura ndefu za Qur’an tukufu au kusoma nyiradi ndefu na za kurudiarudia wakati wa Swala, kwa sababu utakuwa umezama kabisa katika sehemu za kisomo chenyewe. Hii ni njia yenye nguvu sana ya kurefusha kuinama (rukuu) kwako na kusujudu, na ni njia ya kurefusha Swala yako bila ya adha yoyote.

Share this article

Comments 0

Your comment

Comment description

Latest Post

Most Reviews

MOST READ