Rafed English

Shahidi Kwa Ajili Ya Ubinadamu

Shahidi Kwa Ajili Ya Ubinadamu by : Allamah Ali Naqvi Kitabu kilichoko mikononi mwako ni tarjumi ya kitabu cha Kiingereza kwa jina la: The Martyr For Mankind. Sisi tumekiita: Shahidi Kwa Ajili Ya Ubinadamu. Kitabu hiki kinazungumzia masaibu yaliyotukia Karbala.Masaibu ya Karbala ni maarufu sana. Kila mwaka unapofika mwezi wa Muharram, Waislamu duniani kote hufanya majlisi (mikusanyiko) kwa ajili ya kuomboleza masaibu yaliyompata Imam Husain (as) - mtoto wa Imam Ali (as) na Fatima (as) ambaye ni mjukuu halisi wa Mtukufu Mtume (saww).

Kwa hakika masaibu haya yanazidi kuwa maarufu kadiri miaka inavyozidi kwenda. Waislamu wanazidi kuathiriwa mno na masaibu haya, na kuwa na hamu ya kutaka kujua zaidi masaibu haya yaliyompata mjukuu huyu wa Mtukufu Mtume (saww) yametokana na nini na yamesababishwa na nini hasa.

Kama ilivyo vitabu vyingi vinavyohusu masuala ya dini vimeandikwa kwa lugha za kigeni, vivyo hivyo maelezo ya masaibu haya mengi yamo kwenye lugha za kigeni, na hivyo Waislamu wengi wazungumzaji wa Kiswahili wamekuwa hawazipati habari hizi moja kwa moja kupitia kwenye vitabu, ila kwa kuhudhuria majlisi.

Tumekiona kitabu hiki ni chenye manufaa sana, hususan wakati huu wa maendeleo makubwa ya elimu katika nyanja zote. Kutokana na ukweli huu, Taasisi yetu ya Al-Itrah Foundation imeamua kukichapisha kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili, kwa madhumuni yake yaleyale ya kuwahudumia Waislamu, hususan wazungumzaji wa Kiswahili.

Tunamshukuru ndugu yetu, Mganga B. Mnuve kwa kukubali jukumu hili la kukitarjumi kitabu hiki. Vilevile tunawashukuru wale wote walioshiriki kwa njia moja au nyingine hadi kufanikisha kuchapishwa kwake.

Mchapishaji:
Al-Itrah Foundation
S. L. P. 19701
Dar-es-Salaam. Tanzania
Dibaji
Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema Mwingi wa Ukarimu.

“Sifa zote njema zinamstahiki Allah Mola wa ulimwengu na rehema na baraka zimshukie mbora wa Wajumbe wake na juu ya kizazi chake kitoharifu.”

Nchini Saudi Arabia, sana sana sehemu kubwa ya nchi ni jangwa, Muhammad Bin Abdallah, akijitangaza kuwa ni Mtume karne sita baada ya Kristo alifundisha na kuhubiri dini kubwa ya kuleta mapinduzi ya Uislamu ambayo bila ya kubadili msimamo ilithibitisha umoja kamili wa Allah na ilikana ibada za masanamu, kiumbe binafsi na nguvu. Mafundisho haya yalitishia nguvu na uwezo kwa wale waliokuwa katika madaraka huko Arabuni wakati huo, na kwa mujibu huo wakawa maadui wa Mtume wa kuuana hasa.

Bani Umayyah waliuongoza upinzani dhidi ya Uislam ambao ulifanya ubora na ukamilifu katika utendaji kazi wa mtu, kama mwanaadamu kuwa kigezo cha sifa na heshima. Bani Umayyah hawakuweza kulingana na viwango hivi na Abu Sufyan bin Harb bin Umayyah kwa uchungu sana aliupinga Uislam. Baada ya kupatwa na shida nyingi kwa miaka mingi akiwa katika mji wake wa Makka Mtume alihamia Madina kuokoa maisha yake. Tukio hili lilikuwa ndiyo mwanzo wa zama za “HIJRA.”

Maadui wa Mtume mara kwa mara walijaribu kubomoa athari za Muhammad mjini Madina. Mashambulio yao yalipelekea kufika katika kupiganwa vita vingi, ambavyo katika hivyo vilivyokuwa vikubwa sana vilikuwa vile vya Badr, Uhud na vita vya Mtaro (Khandaq). Ushindi wa Uislam uliuvunjavunja kabisa uwezo na nguvu za Bani Umayyahh ambao waliukubali Uislamu ili kuokoa nafsi zao na wakati huohuo kutumia mitego ya imani mpya kuuharibu kutokea ndani yake.

Hawakuwa na muda mrefu wa kungojea, kwani kifo cha Mtume kiliyatupa mambo ya Waislam katika vurugu na wale ambao walibahatika kupata kuchaguliwa au kuteuliwa kama warithi wake waliona inafaa kukubaliana katika uimarishaji wa mamlaka ya Bani Umayyah nchini Syria ambao juu ya huo wakawa watawala. Waliukandamiza usawa wa Kiislam, wakazipinga amri za Qur’ani na kwa kiasi kikubwa wakayapotosha mafundisho ya Mtume.

Watetezi wa Uislamu hawakuweza kuvumilia mateso ya Bani Umayyah. Wakati Ali, binamu na mkwe wake Mtume, na uungwaji mkono wake usioshindika, alipotawalishwa kama Khalifa, aliingia kwenye vita vya kumwaga damu vya Siffin dhidi ya Muawiya, mtawala wa Syria (Sham) kitukuu cha Umayyah. Kazi ya Ali ilikuwa bado kabisa kukamilishwa wakati alipopigwa dharuba mbaya sana ya upanga wakati wa swala yake ya asubuhi.

Mwanawe mkubwa, Hasan, alimrithi na alilazimishwa kwa kubanwa kufanya mkataba wa amani na Mu’awiyah. Huyu Mu’awiyah alivunja ahadi zote ambazo aliyafanya na akafanya Hasan kutiliwa sumu kwa siri (na mkewe) katika chakula. Hasan (alipokufa) alirithiwa na mdogo wake Husein.

Miaka kadhaa baadaye Mu’awiyah alifariki dunia (mwaka 60 A.H.) na mtoto wake mpotovu, Yazid, akawa mtawala wa Syria. Urithi wake uliandaliwa na baba yake lakini alikuwa anatambua changamoto dhidi ya utawala wake kutoka kwa Husein. Kwa hiyo, aliamuru al-Walid bin Utba bin Abi Sufyan, gavana wa Madina, kuchukua kiapo cha utii cha Husein kwake yeye (Yazid). Hili lilikuwa ombi lisilowezekana (kukubaliwa) na Husein akatoka Medina kwenda Makkah pamoja na wategemezi wake wote kwa ajili ya kutafuta usalama (wa maisha yao). Makkah ni mahali patakatifu pa Mwenyezi Mungu na kwa hiyo pakawa ni lazima pawe ni mahali penye usalama. Hapa napo pia aligundua mipango inayotayarishwa ya kumuua. Katika siku ambazo Waislam kutoka ulmwenguni kote walikuwa wanajiandaa kwenda Makka kwa ajili ya utekelezaji wa ibada za Hijja, Husein aliondoka kwenda Kufa ambako alikuwa ameitwa alikuwa tayari alikwishampeleka binamu yake aitwaye Muslim bin Aqil kuona na kukadiria hali halisi ilivyokuwa kule.

Pamoja na kuwepo mambo machache tofauti, watu wa Kufa walishindwa kuziheshimu ahadi za msaada zilizopelekwa kwa Husein baada ya Ubaydullah bin Ziyad kuchukua ugavana. Muslim alisalitiwa na akauawa kikatili sana. Husein hakuweza kurudi Makkah, wala kusonga mbele kwenda Kufa kutoka mahali ambapo jeshi lenye silaha lilisonga mbele ili kumkamata na kumfanya mateka. Alilazimishwa kusimama Karbala.

Hapo majeshi makubwa yalikusanyika na kuungana ili kumshurtisha Husein ale kiapo cha utii kwa Yazid au akabiliane na maangamizi na kifo.

Kutoka mwezi saba ya Muharram, Husein na masahaba zake, pamoja na watoto wadogo walizuiwa kupata maji. Husein alijadiliana kuhusu amani na kamanda (mkuu) wa majeshi ya Yazid, Umar bin Sa’d, ambaye alishaw- ishika kutokana na dhamira zake za kuheshimika kwamba aandike kwa gavana wa Kufa, akipendekeza sululisho la amani kuhusu mzozo huu. Ubaydullah, hata hivyo, aliuchukulia msimamo wa kibusara wa Husein kama ni dalili ya udhaifu, na akasisitiza tu juu ya kiapo kisichostahili kwa ajili ya Yazid. Hili likakataliwa.

Vikosi vingi vya Ubaydullah vilianzisha mashambulizi juu ya Husein katika usiku wa mwezi tisa Muharram. Kwa shingo upande kabisa walimpa mjukuu wa Mtume mapumziko ya usiku tu ili utumike katika swala. Labda Husein naye pia alikuwa anataka kutoa fursa nyingine kwa rafiki na adui pia ili kufikiria upya suala lote zima na kutenda alivyoona ndiyo bora mno. Aliwaacha huru masahaba zake pia kwenye kiapo cha utii kwake, na akawashauri wachukue nafasi hiyo ya ufuniko (ulinzi) wa usiku ili kwenda popote pale walipotaka. Masahaba zake waaminifu na watiifu, kwa sauti moja walikataa kumtelekeza (kumwacha peke yake).

Asubuhi iliyofuatia vita hivi vya kifisadi na kiukatili visiyo na ulingano wa majeshi vilipiganwa mpaka karibu na nusu ya mchana wa tarehe kumi Muharram, marafiki wa Husein na wafuasi wake walijitoa mhanga kwa ajili ya utukufu wa haki na uadilifu na kwa ajili ya Allah. Kisha jamaa zake wakawasili katika uwanja wa vita. Miongoni mwao mtoto wake mkubwa Ali Akbar alikuwa wa kwanza kuyaonja mauti. Shujaa wa mwisho kuuweka chini uhai wake alikuwa Abbas bin Ali, ndugu shujaa wa Husein.

Kifo chake kilivunja kabisa ile nguvu ambayo alibakiwa nayo Husein ambaye kishapo alimchukua mtoto wake mchanga, Abdallah, aliyekuwa na umri wa takriban miezi sita, na akamyanyua katika mikono yake akimuombea maji. Hata hivyo, kutoka kule kwenye kundi la askari wengi wa Yazid, jawabu lilikuwa ni mshale tu ambao uliichana shingo ya mtoto mchanga huyo asiye na hatia.

Sasa ikabakia kwa Husein kutoa huo mhanga mkuwa. Ingekuwa ni rahisi zaidi kwake kufanya hivyo kwanza kabisa kabla ya kuachana na wafuasi waaminifu, marafiki wa tangu zamani, wapwa, watoto na kaka zake. Lakini aliahirisha kujitoa kwake mhanga mpaka mwisho ili kwamba mtihani wake uweze kuwa mrefu mno kuliko yote, wenye tofauti kubwa sana na wenye maumivu makali sana kuliko yote. Akiwa peke yake na aliyevunjika moyo, huku amezunguukwa pande zote na maadui wasio idadi, Husein aliuawa baada ya ushujaa mkubwa mbele ya maadui zake duni na waoga. Kichwa chake kisha kikanyanyuliwa juu juu kwenye ncha ya mkuki, na mwili wake na ile ya masahaba zake ikakanyagwa kanyagwa na farasi.

Kambi yake ilichomwa moto na vitu vyao kuporwa na wanawake wa nyumba takatifu kabisa ya Bara Arabu waliachwa bila hifadhi ya kufunika vichwa vyao na wakatembezwa kutoka mji mpaka mwingine kama wafungwa.

Mwanamume pekee aliyebaki wa familia ya Husein, ambaye ni mwanae aliyekuwa mgonjwa, Ali, alifungwa minyororo na, pamoja na ndugu zake wanawake, wakatembezwa kwa miguu kutoka Karbala mpaka Kufa na hadi Damascus (Syria).

Haya ni maelezo kwa muhtasari tu yaliyo ya wazi kabisa kuhusu msiba wa Karbala. Ulitokea nchini Iraq miongoni mwa Waislam. Umuhimu wa ujumbe wa Karbala umevuka mipaka finyu ya eneo la tukio na mpangilio wa jamii yote kwa sababu ya uhusiano wake wenye athari nyingi na kubwa kwa wanadamu wote. Mvuto huu wenye kuenea pote wa matukio ya Karbala hautokani tu na tabia ya kibinadamu ya kuwaonea huruma wenye kuonewana Husein alipatwa na misukosuko ya kunyang’anywa, kufiwa, kufanyiwa ukatili na ufidhuli kwa namna ambayo hakuna yeyote aliyewahi kupatwa nayo – bali pia kwa vile alipatwa na ukatili wote huu katika kutetea njia ya sawa, uhuru wa dhamira, haki na uadilifu na kuufichua upotofu na udhalimu wa watesaji wake.

Kwa kutoa mihanga kama hiyo isiyokadirika na kulinganishika kwa njia ya utulivu, azma, subira na kwa rikodi isiyo na doa ya matendo matukufu, Husein alitumikia lengo linalochangiwa kwa kufanana katika dini zote, la uendelezaji wa tabia ya mwanadamu kufikia ubora wa kimaadili.

Ni ubinadamu kushikilia furaha na kukwepa huzuni. Kwa hivyo kila mahali matukio ya furaha yanasherehekewa. Ni kifo cha kishahidi tu cha Husein ambacho ndicho kinakumbukwa kwa maombelezo katika nchi za mbali. Kwa vile picha hii bainifu sana imeadhimisha maombolezo ya msiba wa Karbala kwa zaidi ya miaka 1300, inawezekana kuwa kwamba kutoka kwenye huzuni na machozi hutiririka faida kwa waombolezaji.

Hakuna tukio katika historia limekusanyia lenyewe rundo kubwa la maaandishi kama la msiba wa Karbala, lakini hakuna hata kitabu kimoja pekee ambacho mtu anaweza kwa urahisi kurejea ili kuyafahamu matukio ya msiba huu katika mtazamo wao wa kihistoria, matokeo yake na maelezo muhimu kwa kinaganaga. Inatumainiwa kwamba kitabu hiki cha sasa kitasaidia kukidhi haja hii.

S.A.N.N.
Ibrahim anachukua nafasi ya pande zote, akiwa anatukuzwa na Mayahudi, Wakristo na Waislam sawasawa. Qur’ani inaonyesha kabisa kwamba Mtume wa Uislamu alidai kuifuata dini (imani) ya Ibrahim ambaye aliwaita wafuasi wake Waislam1. Ahadith nyingi zenye kuhusu maisha yake ni sehemu ya urithi wa Kiislam na kwa kiwango kikubwa sana zimeathiri mwendo wa Kiislam na maadili.

Ibrahim alikuwa na watoto wawili wa kiume, Is’haak na Isma’il ambao walikuwa kimpangilio ni mababu wa Waisrael na wa Mtume wa Uislamu.

Ibrahim na Isma’il waliinua Ka’aba iliyoko Makka ambayo dini iliifanya mahali pa kukutania watu wote wa ulimwengu mzima. Na miaka ilivyokuwa inapita hii iliota nafasi ya maana sana kwa kizazi cha Ibrahim.

Uislamu unatilia umuhimu mkubwa maelezo ya kimungu yasemayo kwamba Ibrahim alikuwa ameamriwa na Mungu kumtoa kafara mwanawe Isma’il, na akawa tayari kwa kutekeleza mtihani huo mkubwa kwa utulivu mkubwa. Isma’il, pia aliridhia utekelezwaji wa maatakwa ya ki-Mungu, lakini kitendo hasa cha kuchinja kiligeuzwa katika wakati wa mwisho kabisa, uingiliaji kati wa mbinguni ukambadilisha Isma’il kwa mnyama ambaye alitolewa karara badala yake. Hata hivyo ilitangazwa kwamba kafara hilo ambalo limeakhirishwa lingekuwa lije kufanywa kwa chinjo kubwa katika njia ya Mwenyezi Mungu.2 Uislamu unaadhimisha tukio hili kila mwaka kama Idd al-Adh’ha au Id al-Qurbani, sherehe ya kuchinja (kutoa kafara).

Vizazi vya watoto wawili wa Ismail, Nabit na Qaydhan vilifanya makazi katika Hijaz na vikazaana na kuongezeka kwa idadi kubwa sana. Mmoja wa watoto wa mwanzoni wa Nabit, aliyeitwa Adnaan alikua na kupata umaarufu mkubwa. Vizazi ishirini na moja na karibuni miaka 600 inasimama kati yake na Mtume wa Uislamu ambaye nasaba yake kwa Adnaan haipingiki, na imetolewa katika kiambatisho “A”. Hata hivyo, bado kuna wasiwasi kwamba ni yupi katika watangulizi wake alijipatia jina la Quraish. Wakati mmojawapo wa mababu (wahenga) wa Mtume, Qussay, vizazi vitano tu vilipita kutoka yeye, alipopanda madarakani, akaunganisha wato- to wa Nadhr na wakaling’oa kabila la Khuzaa likiwa ndiyo walezi wa Ka’aba, wakaichukua Makka mikononi mwao, wakajenga makazi hapo, wakajenga ukumbi wa halmashauri, wakapanga kanuni za sheria za mwenendo wa kijamii na wakaandaa utaratibu wa kuwapatia chakula na maji mahujaji waendao Hijja3

Abd Manaf, mwana wa Qusay, alijipatia jina (umaarufu) mwenyewe katika wakati wa uhai wa baba yake.4 Mwanae Amri, aliyefahamika zaidi kama Hashim aliwazidi ndugu zake na akapendelewa peke yake kupanga mpango wa kuwapatia maji na chakula mahujaji waendao Hijja.

Alianzisha safari (misafara) za kibiashara kwenda Sham (Syria) na Yemen, na katika wakati wa uhaba aliwahudumia watu wa Makka kwa kuwapatia vipande vya mikate iliyokatwakatwa na kuchovya kwenye supu, akajipatia jina la Hashim, ‘Hashm’ likiwa na maana ya “kuvunja vunja’, meng’enya n.k. kwa lugha ya kiarabu.5

Hashim alirithiwa na ndugu yake aliyeitwa Muttalib ambaye alifuatwa na mtoto wa Hashim, Shayba, ajulikanaye kama Abd al-Muttalib, ambaye aliwapita kwa utukufu na madaraka wale wote waliomtangulia kabla yake6 na akapewa cheo cha Sayyidul-Batha’ (kiongozi wa Makka)7. Wawili kati ya watoto wake wa kiume walikuwa Abdallah na Abu Talib.

Abdul-Muttalib alikuwa ameapa kumtoa mhanga mwanawe Abdallah, lakini aliweza kuepuka kufanya hivyo kwa kutoa mhanga mbadala wa ngamia mia moja.8

Abdallah alimtangulia baba yake kufa, na Abu Talib akarithi shughuli na utukufu wote wa baba yake. Jukumu lake kubwa kabisa, hata hivyo, lilikuwa la uangalizi wa malezi ya mtoto yatima wa Abdullah, Muhammad.

Mapema katika maisha yake mtume huyu wa baadaye alijipatia jina la Amin (mwaminifu) kutokana na uaminifu wake na kutegemewa kwake. Waarabu walikabidhi vitu vyao vya thamani kwake kwa ajili ya hifadhi salama na walikuwa wakikubali maamuzi yake katika masuala muhimu.

Uvunjikaji wa sheria wa jumla na uonevu ulifuatia kifo cha Abdal-Muttalib na dhuluma dhidi ya wanyonge na wageni walikaa bila ya kuadhibiwa. Wakati Muhammad bin Abdullah alikuwa amekaribia miaka ishirini aliungana na ndugu zake na baadhi ya makabila mengine ya Ki-Quraishi kuanzisha mapatano (mkataba) muhimu sana (hilf-alfudul), ambao kwawo wale wote waliohusika walikula kiapo ambacho kiliwalazimisha kuunga mkono njia ya wenye kuonewa, kupata haki za waliodhulumiwa waliotenzwa nguvu na hasara zao kufidiwa.

Kiapo hiki kilikwenda kinyume na msimamo wa desturi wa Ki-Arabu ambao ulihusisha kutetea fungamano (muungano) la kikabila tu, ambalo wakati mwingine lilikuza migogoro midogo midogo na kufikia kuwepo visasi vya kurithi vya kikabila. Kizazi cha Hashim kiliongoza katika kujaribu kuondosha hali hii ya mwenendo wa kitaifa na kuifanya haki, uadilifu na mwenendo mwema viheshimike mahali pote.

Ali alizaliwa na Abu Talib ndani ya Ka’aba mjini Makka, upendeleo ambao hakuupewa mtu mwingine yeyote yule. Muhammad wakati huo alikuwa na umri wa takriban miaka 30 (thelathini). Wakati Ali alipokuwa bado ni mchanga, njaa iliipiga Makka, na ikamwacha Abu Talib katika mazingira magumu sana, hivyo Muhammad alimchukua Ali kwenda kuishi pamoja naye ili kumwondolea ami yake sehemu ya mzigo wake.

Karne ya saba ya zama za Ukristo ilikuwa kipindi kisichokuwa na ufumo cha ujahilia wakati Uislamu ulipotokea huko Uarabuni. Kwa miaka kadhaa ujumbe wa dini (imani) mpya ulihubiriwa kwa siri sana. Kisha Mtume akaamriwa na Mungu aufikishe kwa ndugu zake wa karibu.9

Mtume kwa hiyo aliwaita watoto wote wa kizazi cha Abdul Muttalib, na akijitangaza mwenyewe kama Mtume wa Mwenyezi Mungu, alilingania upweke wa Mungu (Tawhid), na akawauliza wageni waliokusanyika hapo kama ni nani miongoni mwao angemuunga mkono katika kueneza ujumbe wa Uislamu kwa kuelewa wazi kwamba huyo angekuwa ni ndugu, wasii na mrithi wa Mtume. Suala hili aliliuliza kwa kulirudia rudia, lakini kila wakati alikuwa ni Ali tu, ingawa alikuwa bado ni mdogo sana, ndiye aliyejibu, akimuahidi usaidizi kamili. Mtume alimtangaza Ali kama ni ndugu, wasii na mrithi wake.

Kwa ueneaji wa Uislamu, uabudu masanamu ulifikia kukataliwa waziwazi, na kwa sababu hiyo Maquraishi wakawa maadui wa Mtume wasio na huruma na wakaazimia kumdhuru. Madhali Abu Talib alikuwa hai haiba yake yenye nguvu ilimzuia Mtume wa Uislamu kupatwa na huzuni.

Baada ya vifo vya Abu Talib na mke wa Mtume, Khadija, mateso ambayo alikuwa akabiliana nayo yaliongezeka ukali na marudio ya mara kwa mara, na Mtume akaamua kuondoka kwenda Madina. Walipozipata habari hizi, maquraishi waliizunguka nyumba yake usiku mmoja ili wamuue, lakini Mtume aliwatoka akimwacha Ali amelala katika kitanda chake.10

Kutoka kwa Mtume kwenda Madina, kuitwako Hijra, hakukuzuia uchokozi dhidi ya Waislam, na vita kama vile vya Badr, Uhud na Khandaq (mtaro) ilibidi vipiganwe, na ulikuwa wakati wote ni upanga wa Ali ndio ulileta ushindi wa kung’ara kwa Uislamu.

Mtume alimwozesha binti yake Fatima kwa Ali kwa mujibu wa amri ya ki-Mungu, na aliyakataa maombi ya wengine wengi kwa ajili ya posa ya kipande hiki cha nyama na damu yake mwenyewe,11 kiongozi wa wanawake wa peponi, ambaye kwamba Mtume alitumia kusimama wakati wowote Fatima alipokuwa akimtembelea. Kutokana na wazazi wa heshima kama hao, Ali na Fatima, walizaliwa watoto wawili wa kiume, Hasan na Husein.

Vipi Husein angeweza kusahau desturi za hali ya juu na sifa zisizo na kifani ambazo familia yake walikuwanazo siku zote tangu zama za kale? Aliwakilisha kawaida ambayo ilikuwa na rekodi isiyovunjika ya utoaji mhanga. Ni lazima awe amesikia jinsi gani babu yake mkubwa (mhenga) Ibrahim alivyoandaa kumtoa kafara mwanawe kwa kutii amri ya mbinguni, jinsi gani babu yake Abdul-Muttalib, alivyomtoa kafara mwanawe Abdullah, jinsi gani mhenga wake Hashim alivyoitumia mali kwa ajili ya kutoa huduma kwa wanadamu, na jinsi gani familia yake ilivyochukua wajibu mkubwa katika kuifanya hilf al-fudul kuwasaidia waliokuwa wanateswa na kusimamia haki kwa ajili ya wanaokandamizwa. Kwa hakika Husein alishikilia kwamba kiapo hicho kiliendelea kuwa halali kutumika.

Husein alijua kwamba babu yake mzaa mama yake, Mtume Muhammad (s.a.w.w.), alipatwa na taabu nyingi na mateso yasio na mwisho katika kuu- tangaza na kuueneza Uislamu, kwamba babu yake mzaa baba yake, Abu Talib, alimlinda Mtume na Uislamu kwa nguvu zake zote na uwezo wa haiba yake, kwamba wakati wowote hatari ilipotishia Uislamu, wa kwan- za kukabiliana nayo na kuipiga vita hiyo, bila ya kujali matokeo yote yatakayomtokea, alikuwa ni baba yake, Ali bin Abi Talib.

Ni kawaida tu kwamba simulizi za matendo haya bora na mwenendo wa wahenga wake ni lazima viwe vimewasha moto wa fikira na mawazo ya kijana Husein na kuzaa ndani mwake tamaa ya kutenda matendo makubwa kama hayo ya ucha-Mungu, ya utii kwa utashi wa Mungu, kutumikia haki na kuiletea heshima familia yake tukufu.
________________________
1. Qur'an 2:128

2. Qur’an; 37:107

3. Ibn Is’haaq, al-Sira, uk. 52-56

4. Ibn Is’haaq, uk. 55

5. Ibn Is’haaq, uk. 58

6. Ibn Is’haaq, uk. 61

7. Ibn Is’haaq, uk. 25

8. Ibn Is’haaq, uk. 66 - 68

9. Qur’ani; 26:214

10. Ibn Is’haaq, uk. 223

11. Sahih Bukhari, Juz. 2, uk. 74, 185, 189 na Sahih Muslim, Juz. 2, uk. 290
Habari zinaeleza kwamba wakati Hashim na Abd Shams, baba wa Umayyah walipozaliwa kama mapacha, kidole cha mmoja wao kilikutwa kimenasa kwenye paji la uso la mwingine. Kilikatwa ili kuwatenganisha vichanga hao, na damu ambayo ilitiririka kutoka kwenye jeraha ilichukuliwa kuonyesha ishara ya ndege mbaya ya kumwaga damu kati ya vizazi vyao.1

Umayyah alianza kusababisha nia mbaya kati yake na ami yake, Hashim. Kichocheo kikubwa cha wivu wake kilipatikana katika kipindi cha njaa ambayo iliipiga Makka, Hashim alipata kukubalika sana kwa umma kwa kule kuwagawia wakazi wa mji chakula kingi ambacho kilikuwa katika namna ya vipande vya mikate iliyovunjwa vunjwa na kuchovyekwa katika supu.

Umayyah akatafuta kwenda sambamba na ukarimu huu kwa kujitia kufanya vitendo vya ukarimu ambao hauna maana na mara baada ya muda mfupi wa kutosha uligunduliwa nia yake isiyo nzuri. Katika hali ya mfadhaiko, Ummayah alileta changamoto kwa Hashim la kushindania madai yake ya ubora mbele ya msuluhishi huru anayekubalika. Moja ya masharti lilikuwa kwamba upande utakaoshindwa utahamishwa kutoka Makka kwa kipindi cha miaka 10. Msuluhishi huyo aliamua dhidi ya Umayyah ambaye alihamia Sham (Syria) kwa miaka 10. Hivyo ukatokea uadui kati ya Bani Hashim na Bani Ummayah na uliendelea kuwepo kati yao kwa vizazi vingi.2

Kuzaliwa kwa Mtume miongoni mwa Bani Hashim lilikuwa pigo lililovunjavunja heshima ya Bani Umayyah. Kwa hiyo, wao waliutazama utume wa Muhammed kama ushindi wa Bani Hashim na walimfanyia upinzani mkali mno.
________________________
1. Tabari, Kitabu al-Ta'rikh, Juz.1 uk. 1089 2. Tabari, Kitabu al-Ta'rikh, Juz. 1 uk. 1090
Kipindi cha kabla ya Uislamu cha historia ya Uarabuni kinaitwa “kipindi cha zama za ujahilia” au “zama za giza”. Isije ikamaanisha kwamba Waarabu walikuwa hawazitambui sanaa na njia za maisha ya kijamii. Karne nyingi kabla ya kudhihiri Uislamu, Arabuni ya Kusini iliendeleza ustaarabu uliostawi na ilijishughulisha na biashara zenye kustawi.

Tungo zao za kishairi zikiwa na baadhi ya vielelezo bora kabisa vya fasihi ya Kiarabu, zinaonyesha kwamba Waarabu walikuwa wana viwango vya hali ya juu kabisa vya ujasiri, ukarimu, ukaribishaji, uaminifu, upendo wa kindugu na upendo wa ndoa. Wakati ambapo walikuwa wanashughulika zaidi na ibada ya sanamu, hawakuwa kwamba hawatambui kabisa kuwepo kwa Mungu Mmoja.

Walikusanyika kila mwaka mjini Makka kwa ajili ya kutekeleza Hijja, lakini walikuwa hawajui kabisa umuhimu halisi wa mikusanyiko hii. Dini nyingine zilizofuatwa katika nchi hiyo zilikuwa Uyahudi wa kuabudu moto na Ukristo. Waarabu walifanya misafara ya biashara kwenda Hijaz, Iraq na Syria. Hata hivyo hali ya jumla ya matatizo na ufukara ndani ya jangwa iliwafanya wawe mabahili, na wakajiingiza katika vita vya kulipiza kisasi, mara nyingi vikienea na kuendelea kwa miaka mingi. Dhana zilizoeleweka vibaya (visivyo) za kujistahi mara nyingi ziliwasababishia kuwauwa watoto wa kike walio wachanga.

Wazo la usawa wa binaadamu lilipuuzwa kabisa katika jamii ambamo ndani yake mlikuwa na ushindani binafsi, wivu wa kivikundi na chuki ya kikabila.

Ilikuwa ni katika mazingira haya kwamba Muhammad bin Abdallah aliyechaguliwa na Mwenyezi Mungu alitokea kueneza ujumbe wa Uislamu. Alikabiliana na kazi ya sulubu. Ingekuwa ni rahisi zaidi kwake kuwarudisha washenzi, watu wasiostaarabika, wanaoishi katika hali ya asili kuliko kuirudisha tena kwenye mwenendo mzuri ule utaratibu wa jamii wenye maradhi.

Ilibidi afundishe uvumilivu, unyenyekevu na msamaha kwa wale ambao kwao sifa hizi zilionekana kuwa dalili za unyonge. Ilibidi afundishe usawa wa binadamu na udugu kwa wale ambao walijivunia nasaba zao. Uislamu pia, umeharamisha matumizi ya pombe (ulevi) matendo ya uchezaji kamari na michezo ya bahati nasibu na kutoa au kupokea riba - yote haya yakiwa maarufu sana miongoni mwa waarabu. Pia ulichukia sana matendo mengine yote maovu.

Uislamu ulileta ujumbe wa uhuru kwa kila mtu kutoka kwenye pingu za ukasisi, kutoka kwenye udhalimu wa wenye ukwasi (utajiri) ambao waliyatumia vibaya matunda yaliyotokana na kazi ngumu za wengine, na kutokana na ukatili wa mabwana kwa wafungwa wao. Pia Uislamu ulitoa faraja kwa wanawake ambao walikuwa wamenyimwa hata zile haki za kibinadamu za kimsingi. Uislamu ulifundisha uhuru, undugu na usawa na kwa mara ya kwanza katika historia ya mwanadamu ulitoa kwa watu wote haki kamili za kiraia na kibinaadamu, ukiamsha matumaini mapya katika nyoyo za waliodhulumiwa na mafukara.

Uislamu ulibashiri kutokuwezekana kupata usawa wa nje wakati watu wakiwa wamejigawa katika makabila mbalimbali na mataifa.

Lengo la Uislamu, kwa hiyo, lingeweza kupatikana kwa mapinduzi ya kisomi, na ulijaribu kuvuta uzingativu wa watu kwenye mamlaka mamoja pekee, kuutengeneza mwishilizio wake bila ya kuingiliwa na vitu vya kimaada.

Njia pekee ya kupata kukubalika kwa jumla kwa ajili ya usawa wa watu wote na undugu ni kuanzisha uhusiano wa moja kwa moja kati ya wingi wa vikundi na umoja mkuu. Kwani ina maana kwamba sehemu za huo wingi zingekuwa baadae zinalingana.

Lakini umoja mkuu ambao wanaadamu wote lazima wauelekee inabidi kwa lazima uwe si wa kimaada kwani vile vyote ambavyo ni vya kimaada vitakuwa ni vyenye kutegemea mipaka mbalimbali kama ile ya umbali, nafasi na idadi. Kwa hiyo, ilikuwa jambo lenye umuhimu sana kwamba mawazo ya mwanadamu yangelenga kwenye ule uwezo usiokuwa wa kimaada, uliozidi ule wa mwanadamu, ambao, kwa kutofungwa na ile mipaka ya nafasi, vipimo na viwango, ungebeba uhusiano kwa kila mtu, na ambao kila mtu alihusika nao. Uwezo huu ni yule Mungu mmoja aliyedhihirishwa na Uislamu kwa kufanyiwa ibada na watu wote, Muumba wa vitu vyote.

Kutambua kwamba wanadamu wote ni viumbe vya Mwenyezi Mungu kumefanya ujenzi wa hali ya usawa na undugu miongoni mwa watu kuwa mwepesi vya kutosha. Baadhi ya dini zimemfanya Mungu kuwa ni wao pekee, na wafuasi wao wanadai kuwa ni watoto Wake. Uislamu umekanusha madai kama haya na kuwafundisha Waislamu kutamka kwamba: “Yeye (Allah) ni mlinzi wetu na mlinzi wenu.” Wakati uki- wafanya wanadamu wote kuwa ni sawa, ulifanya uwezo na ubora kuwa ni sifa ambazo zinaamriwa pekee na tabia za mtu mwenyewe.

Utekelezaji tu wa wajibu wa mtu kama mwanadamu ndio ulivutia ubora wa hali ya juu kabisa. Hivyo tabia za asili zilikataliwa katika kuyachukua mamlaka kwa nguvu za idadi ya watu uongozi na mambo mengine kama hayo. Ubora wa tabia na usafi wa maadili vilisisitizwa sana. Mtume aliutangaza ujumbe wake kwenye kuwaendeleza wanaadamu na ukamilifu wa tabia njema.

Mwislam ameelezewa kuwa ni yule mtu ambaye amejisalimisha kabisa kwa Mwenyezi Mungu. Usawa kwa wote, kimaumbile na kiasili ulitangazwa katika Aya ya Qur’ani, “Amekuumbeni kutokana na nafsi moja.”1 Waarabu waliambiwa kwamba nafasi ya kipaumbele haitokani na utaifa; Mquraishi kwa asili hakuwa mbora juu ya asiyekuwa Mquraishi. Matendo yalifuata maagizo mwongozo na maadili ya Mtume. Alimteua Bilal, mtumwa wa Kihabeshi, kuwa mwadhini wake, na wakati mtu mmoja alipolizungumzia jambo hili kwa dharau, Aya ya Qur’ani iliteremshwa ikisema, “Enyi watu kwa hakika sisi tumekuumbeni (nyote) kutokana na mwanamume na mwanamke,”2 hivyo kwamba wanadamu wote ni sawa.

Uislamu kwa kweli kabisa unataka kusimamisha serikali ya Mungu. Serikali ya Mungu inasimama moja kwa moja katika uadilifu na usawa. Qur’ani inawaelekeza Waislam, “...Na mnapohukumu baina ya watu, hukumuni kwa uadilifu,”3 na tena inasema “Wala kuchukiana na watu kusikufanyeni kutotenda uadilifu. Fanyeni uadilifu. Hivyo ndio kuwa karibu mno na uchamungu. Na mcheni Mwenyezi Mungu.”4. Kwa sababu hiyo Mtume alitangaza, “Hakuna mtu aliye mbora juu ya mwingine isipokuwa tu kwa sababu ya imani yake na ucha-Mungu.” Hata hivyo ingawa alikuwa hodari kuendesha mamlaka yasiyofungwa juu ya wafuasi wake, Mtume kamwe hakujiita yeye mwenye, au kufikiria kwamba yeye alikuwa mfalme.
________________________
1. Qur’an; 4:1

2. Qur’an; 49:13

3. Qur’an; 4:58

4. Qur’an; 5:9
Sheria, matendo na desturi za Uislamu, kwa ufupi, mfumo wake wa kijamii, ulianzisha wakati wa uhai wa Mtume. Kwa kusababisha mabadiliko haya makubwa, ilimbidi avumilie machungu mazito sana mateso na matatizo makubwa kwake yeye mwenyewe na akakabiliana na upinzani mkali kabisa kutoka kwa wale ambao nafasi yao ya utawala ilitishiwa na Uislamu.

Miongoni mwa mambo mengine, kwa mfano, ulipiga marufuku utozaji na ulipaji wa riba, ukaondoa chanzo chenye manufaa cha mapato kwa wale ambao waliutumia mpango huu. Uislamu pia ulifundisha kwamba utukufu miongoni mwa watu, sana ulitegemea juu ya ubora wa tabia (mwenendo) wa utekelezaji kamilifu kabisa wa wajibu wake mtu.

Hili lilikuwa tishio la hatari sana kwa wale ambao hadhi zao katika jamii zilitegemea kabisa juu ya mali, utajiri na rasilimali za kimaada zilizo sawa na hizo. Kinyume cha hayo, Uislamu uliendeleza kuwepo matumaini kwa mtu masikini sana kupata heshima na utukufu kama atakuwa ametimiza yale yaliyotakiwa kwake katika utekelezaji wa wajibu wake na uchamungu.

Bani Umayyah chini ya uongozi wa Abu Sufyan, wakichochewa na wingi wa uadui na wivu wa zamani na wa karibuni, waliuongoza upinzani kwa Mtume. Alirushiwa mawe. Malundo ya uchafu yalitupwa juu yake na usumbufu mwingi usio na mwisho, mateso na udhalilishaji vilitumiwa dhidi yake. Maisha yake yalitishwa na ami yake, Abu Talib, alimwondoa na kumpeleka kwenye sehemu ya usalama ya ngome yake ya mlimani ambako huko waliipitisha (walikaa) miaka mitatu kwa kujitenga kabisa. Maquraishi walikataa kabisa maingiliano (ushirikiano) ya kijamii na Bani Hashim.

Ndani ya mwaka mmoja wa ufungaji wa sura hii ya msuso wa kijamii, ami yake Mtume, Abu Talib, na mkewe kipenzi, khadija, walifariki dunia na upinzani kwa Mtume ulibuni njama ya kumuua (Mtume). Alitorokea Madina, akimwacha Ali, binamu yake, akiwa amelala fofofo kitandani mwake.

Hata huko Madina Mtume na wafuasi wake hawakupata nafuu yoyote ile kutokana na vitendo vibaya visivyo vya huruma vya maadui zake ambao waliishambulia Madina zaidi ya mara moja, hata kumlazimisha Mtume kupingana nao.

Vita vya kwanza vya Uislamu, vilipiganwa Badr ambamo Waislam 314 tu,1 waliokuwa na farasi watatu tu,2 kwa mafanikio makubwa waliyashinda majeshi yaliyokuwa bora na imara ya Bani Ummayah. Hamza bin Abdul Muttalib, Ubaydah bin Harith na Ali bin Abi Talib walikuwa miongoni mwa mashujaa maarufu wa Bani Hashim.

Ali alifanya mambo makubwa ya ajabu ya ushujaa kiasi kwamba maadui walivunjika moyo. Hasara ya kuhuzunisha kwa Bani Hashim ilikuwa kwamba Ubayda aliuawa. Upande wa Bani Umayyah ulipata hasara nyingi: mtoto wa Abu Sufyan, Hanzal, aliuawa na Ali, ambaye alimchukua mateka mwingine katika watoto wake, (aliyeitwa) Amr. 3 Hind, mke wa Abu Sufyan aliomboleza vifo vya baba yake, Utba; ami yake, Shayba; na nduguye, al-Walid 4. Misiba hii ilimzidi nguvu Abu Sufyan kiasi kwamba aliweka nadhiri ya kutokuoga mpaka awe ameon- goza mashambulizi dhidi ya Mtume.

Vita nyingine muhimu kati ya Mtume na makafiri vilipiganwa katika mwaka wa 3 A.H. kule Uhud.5 Abu Sufyan alikuwa amekusanya jeshi la askari 3,000 wakati Mtume alikuwa na wanajeshi wapatao 700 tu,6 na farasi wawili. Idadi kubwa ya wanawake ilifuatana na Abu Sufyan kulitia ari na moyo jeshi lake kwa muziki wao wa kijeshi na nyimbo. Hapa pia, Waislam walishinda kupitia ushika upanga mahiri na bora wa Ali bin Abi Talib.

Hamza, ami yake Mtume aliuawa katika vita hivi, na Hind mke wa Abu Sufyan katika kudharau mwenendo wote mwema wa kibinadamu alilichomoa ini lake na akajaribu kulila. 7 Alijipamba kwa kuvaa masikio na viungo vingine vya miili ya wale waliouawa katika vita. Matendo hayo ya kinyama huonyesha kusisitiza kuwepo kwa chuki ya muda mrefu ambayo Bani Umayyah walikuwa nayo dhidi ya Hashim kwa ujumla na hususan kwa Mtume mwenyewe.

Maquraishi walifanya jaribio la mwisho katika mwaka wa 5 A.H. kuupiga Uislamu na kuumaliza. Walifanikiwa kuwapata Mayahudi kwenye kusudio lao na wakaibuka na jeshi lenye askari 10,000 kwa ajili ya “vita ya Makundi” dhidi ya waislam ambao idadi yao ilikuwa ya watu 3,000.

Maadui hawa wa Uislamu kwa mara nyingine tena walishindwa na shujaa wao Amr bin Abd-Wudd alianguka chini kwa upanga wa Ali (aliuawa).

Na hapo Abu Sufyan aliondoka kwenda Makka akiwa amevunjika moyo na tamaa ya kupigana tena na Mtume ikawa imevunjwa kabisa moyoni (mwake).

Alipoona kwamba Maquraishi hawakudhihirisha ishara za uvamizi kwa kipindi kirefu kidogo, Mtume aliongoza baadhi ya Waislam kwenda Makka kufanya Umra au Hijja ndogo, pamoja na ngamia wa kuchinja kuwatoa kafara. Alipogundua kwamba Khalid bin al-Walid alikuwa anajiandaa kumzuia, Mtume aliiacha njia aliyokuwa anaifuata.

Tendo hili la Mtume la kipatanishi lilipelekea kutiwa sahihi kwa mkataba wa amani kati yake na Maquraishi. Mkataba huo ulipiga marufuku vita kati ya makundi hayo kwa kipindi cha miaka kumi, na ukaacha wazi kwa wengine kujiunga na upande wowote waupendao. Iliamuliwa kwamba Waislam wangerudi bila ya kutekeleza ibada hiyo ya Hijja na warudi tena Makka katika mwaka ufuatao na kuikamilisha hija hiyo ndogo ya Umra ndani ya muda wa siku tatu tu na kisha wautoke mji.

Pia (mkataba) huo uliandaa kwamba mtu yeyote yule atakayetorokea kwenye kundi la Muhammad bila ya ruhusa ya mlezi wake lazima arudishwe kwa mlezi wake, lakini kama Quraishi akitoka kwenye ufuasi wa Muhammad huyo asirudishwe. Baadhi ya masharti haya yalikuwa kwa wazi kabisa yasiyo na manufaa kwa Waislamu na baadhi yao walifikiria kuwa ni dalili ya unyonge kutia saini mkataba kama huo. Kwa kweli misingi ya imani ya baadhi ya Waislam ilitingishwa na mkataba wa Hudaibiyyah, kama unavyoitwa.

Mtume aliyakubali masharti yasiyolingana ya mkataba huu ili kukwepa kushutumiwa kwa uchokozi. Aliyachunga masharti ya mkataba kwa maandishi na mazingatio. Mtume alirudi Makka mwaka uliofuata na akatekeleza hijja ndogo ya Umra kama ilivyoelezwa katika mkataba.

Makabila ya Khuzaa na Bakr yalikuwa na hisia za uadui yenyewe kwa yenyewe zilizojengeka kwa muda mrefu, kabila la Khuzaa lilikuwa lenyewe limejishirikisha kwa Mtume, na kabila la Bakr lilijiunga na makafiri.

Mkataba wa amani, kama tulivyokwishaona ulitoa haki ya kukomesha uhasama kati ya makundi haya kwa kipindi ya miaka kumi, na kwa maana hii, hili pia lilitumika kwa makundi yaliyoungana na watiaji sahihi wakuu wa mikataba huo. Kwa hiyo watu wa kabila la Khuzaa waliweka chini silaha zao na wakashtukizwa kwa ghafla na kabila la Bakr ambao kwa siri wakisaidiwa na Maquraishi, waliwaua watu wengi wao wakati wakiwa katika sala zao.

Maelezo ya mauaji haya makubwa yalisimuliwa kwa huzuni kubwa kwa Mtume na msaada wake ulitafutwa kwa kusihiwa sana kiasi kwamba mara moja alikwenda Makka kuwasaidia watu wa kabila la Khuzaa, akiwa amekasirishwa sana na uvunjwaji wa masharti ya mkataba na kwa tabia ya kikatili na ya kufehedhesha ya Maquraishi.

Makafiri walikuwa katika mtawanyiko kabisa na alipogundua hakuna njia nyingine zozote zile za kusalimisha maisha yake, Abu Sufyan aliingia katika Uislam.8 Mtume wa Uislamu alitoa msamaha siyo kwake tu (Abu Sufyan) bali aliufikisha kwa wale ambao walipata hifadhi ndani ya nyumba yake.

Kisha akawaacha huru watu wote wa Makka. Baada ya haya, hata Hind mke wa Abu Sufyan aliukubali na kuingia katika Uislam kama kwa hakika walivyofanya watu wote maarufu wa kabila la Maquraishi.

Kukubali Uislamu kwa Bani Umayyah na wapinzani wengine wa Uislamu hakukulazimu kuleta badiliko katika hisia zao halisi kuhusu Mtume.
________________________
1. Ibn Ish’haq, uk 336

2. Ibn Ish’haq, 741/Ibn Hisham: Sirat, Juz. 1.uk. 407

3. Ibn Ish’haq, uk. 313

4. Ibn Ish’haq, uk. 358

5. Ibn Ish’haq, uk. 370 - 391

6. Ibn Ish’haq, uk. 373

7. Ibn Ish’haq, uk. 385

8. Ibn Ish’haq, uk. 546
Mtoto wa pili wa Ali bin Talib na Fatima, binti ya Mtume alizaliwa mwezi wa 5 Shabaan mwaka wa 3 A.H., na aliitwa kwa jina la Husein na Mtume.

Baba yake alijibainisha mwenyewe kama askari asiyeshindika wa Kiislam, aliyekuwa tayari kuzichukua zile kazi zenye hatari sana katika kuulinda Uislamu. Mama yake alionyesha mfano wa tabia mzuri sana kwa wanawake na akaongezea nguvu mafundisho ya baba yake kwao kwa kuwapa maonyesho ya vitendo.

Husein na kaka yake mkubwa walikabidhiwa wote kwenye malezi ya mapenzi na upendo mkubwa wa mwalimu mtukufu kama huyu mjumbe mkuu wa Mwenyezi Mungu, ambaye lengo lake pekee lilikuwa ni kuzitakasa roho.1 Watoto waliokuzwa katika hali na mazingira ya kimungu mara walipata ubora wa kupigiwa mfano wa tabia na ukamilifu wa maadili.

Tabia nzuri za wajukuu wake ziliwafanya kuwa vipenzi wakuzidi mno kwa Mtume. Aliwataka watu wengine kushiriki katika upendo wake huu na akatangaza, akasema: “Mtu yeyote yule awapendaye hawa, huyo amenipenda mimi na yeyote ambaye atawafanyia uadui huyo ni adui yangu.2

Alimwomba Mwenyezi Mungu kuwa shahidi kwamba yeye aliwapenda sana sana wote wawili.3 Husein alijua, hata hivyo, kwamba Mtume alijizatiti na kujitoa kwa ajili ya mafanikio na utukufu wa Uislamu, na kwamba asingesita kumtoa mhanga kwa ajili ya hilo, kama uhifadhi wa Uislamu ungetaka hivyo.

Mtume alitoa changamoto kwa Wakristo wa Najran nchini Yemen kwa ajili ya shindano la kiroho (mubahila) ambalo ndani yake washindani walikuwa waombe laana ya Mwenyezi Mungu ianguke juu ya kundi amba- lo madai yao yalikuwa ya uwongo. Mtume aliwataka waje na watoto wao, wanawake wao na nafsi zao wenyewe. Yeye (mtume) alimchukua pamoja naye Hasan, Husein, Fatima na Ali. Wakristo walifadhaishwa sana kwa kutokea kwa kundi la Mtume kiasi kwamba walikataa kushindana na wakalipa jizya (kodi) kwake.4

Tukio hili limepata kutajwa katika Qur’ani,5 na miongoni mwa malengo lililoyatumikia ilikuwa kuwafunza watu wa Nyumba ya Mtume kubeba majukumu mazito, na kuwaonyesha watu kwamba ni wao tu pekee wangeweza kutegemewa katika kuulinda Uislamu, na kwamba Uislamu ulimtegemea kila mtu – mwanamume, mwanamke na mtoto – kutoa mchango wake kwa ajili ya usalama wake (Uislamu).

Mtume alieleza wafuasi wake mara nyingi sana kuwafuata Ahlul Bayt wake. Wakati fulani aliwaambia (watu) kwamba anaacha nyuma yake (anawaachia) vitu viwili vizito mno: Kitabu cha Mungu (Qur’ani) na watu wa nyumbani kwake na kivifuata viwili hivyo kungewazuia watu kupotea. Alisisitiza kwamba Hasan na Husein walikuwa ndio viongozi wa vijana wa peponi.

Alibainisha umuhimu wa maana sana wa Husein wakati aliposema “Kama vile maisha ya Husein yanavyotokana na mimi ndivyo uhai wangu unavyotokana na Husein,”6 akiwa na maana yake kwamba ujumbe wake ungehuishwa na Hussein.

Husein alikuwa hajafikia umri wa miaka 7 wakati Mtume alipofariki dunia katika mwezi wa Rabiul- Awwal, mwaka wa 11 A.H.
________________________
1. Qur’an; 2; 129 na 151

2. Ibn Maja, Sunan, Juz. 1 uk. 33

3. Sahih Muslim, Juz. 2 uk. 282

4. Irshad, Kur. 116-119

5. Qur’an; 3:131

6. Ibn Maja, Sunan, Juz. 1 uk. 33
Tangu Kifo Cha Mtume Mpaka Kuuawa Kwa Ali. ( 11 A.H. Mpaka 40 A.H.)
Kifo cha Mtume kiliwaingiza watu wa familia yake kwenye maombolezo makubwa. Miongoni mwa wale ambao walihuzunika sana hasa walikuwa ni binti yake Fatima na wajukuu zake, Hasan na Husein. Huzuni ya Fatima ilikuwa hailiwaziki kabisa kiasi kwamba alilia kilio cha kumwombeleza baba yake mchana na usiku bila kupumzika kiasi kwamba watu waliona haiwezikani kula chakula chao au kuweza kupumzika katika mji wa Madina.

Baada ya malalamiko mengi ya kukaririwa yaliyofanywa kwake kuhusu namna gani maombolezo yake yalivyovuruga maisha ya kawaida mjini Madina, alikubali kwenda kwenye uwanja wa makaburi ya Al-Baqi ili aweze hapo kujishughulisha na uombolezaji wake bila kuzuiliwa juu ya pengo lake lisilozibika.

Ama kuhusu wajukuu zake, Hasan na Husein kifo cha Mtume kilileta mateso yasiyoelezeka. Alitoa upendo mwingi sana juu yao na akawalea kwa uangalifu mkubwa na mapenzi katika njia za Uislamu.

Alichukua hatua za kuwaonyesha wafuasi wake kulikuwa na umuhimu kiasi gani kwao katika kuwapenda wajuu zake, na kuwa kuzembea kidogo kabisa katika jambo hili kulimuudhi sana Mtume kutokana na kuwa katika kitovu cha mambo ya Uislamu. (Vijana waliona kwamba watu wa nyumba ya Mtume, ahlul bayt wake walikuwa wamenyimwa madaraka yote, na kwa nje walikuwa wakionekena hawana mamlaka).

Husein lazima atakuwa ameona kwamba baba yake Ali bin Abi Talib alikuwa amejitoa kutoka mambo ya kidunia ili kujizamisha zaidi tu katika kuikusanya Qur’ani katika utaratibu wa uteremsho (wahyi) wake. Somo la kwamba hata katika hali na mazingira yaliyokuwa magumu kiasi gani watu wa nyumba ya Mtume hawakuweza kuacha kuutumikia Uislam, na kwamba kama Qur’ani ilivyokuwa iwe pamoja nao wakati wote, ni lazima wai- hifadhi na kuilinda, lisingeweza kumpotea Husein.

Katika saa hii ya mtihani, Husein aliona kwamba baadhi ya marafiki kama vile ami yake Mtume, Abbas bin Abdul-Mutallib na washirika wasio waaminifu kama Abu Sufyan bin Harb, mkuu (chifu) wa ukoo wa Bani Umayyah, walimshauri Ali kujaribu kuchukua udhibiti wa dola ya Kiislamu yeye mwenyewe.

Abu Sufyan alimchochea Ali, akisema kwamba ilikuwa siyo sawa kwamba moja ya familia zilizo za chini mno ichukue udhibiti juu yake, na kwamba angempatia askari wa farasi kumsaidia. Ali alimpa jibu la mkato akimwambia, “Naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu, wewe bado ni adui wa Uislamu.”1

Hii ilidhihirisha jinsi Ali alivyokuwa imara katika kuyaweka maslahi ya jumla ya jamii mbele zaidi kuliko maslahi yake mwenyewe, na pia kutokuaminika kwa uingiaji wa Abu Sufyan katika Uislamu, na ikawa kama onyo dhidi ya unafiki ambao kwa sura ya marafiki wa uwongo na maadui wenye kudhuru, ni wenye kuleta madhara makubwa zaidi kuliko wawezavyo kufanya maadui wenye kujitangaza kwa dhahiri.

Miezi michache baada ya kifo cha Mtume, Husein alimpoteza mama yake pia. Kutoka kwenye umri mdogo wa miaka saba mpaka kufikia umri wa ujanadume wa miaka thelathini na nane, Husein aliishi chini ya uongozi wa baba yake aliyejaaliwa kipaji, mwenye elimu, mwenye busara na mwadilifu, na lazima atakuwa amepata picha ya ushirikiano huu mpaka mwisho wa siku zake.

Lazima atakuwa amefahamu kwamba, wakati alipohitajika, baba yake bila ya kinyongo aliyatatua matatizo yaliyowakabili Waislamu, na alitoa ushauri wake kuhusu mipango muhimu na safari zenye nia maalum bila kusita, na ingawaje alisikitishwa sana na uzimwaji wa madai yake juu ya ukhalifa.

Fursa ilijitokeza yenyewe kwa Ali kupata kusimikwa kuwa khalifa wakati wajumbe wote wa baraza la ushauri walioteuliwa na Umar wakati wa kifo chake kuchagua mrithi wake walipokubali kumteua Ali kwa nafasi hiyo iwapo kwa nyongeza ya kufuata sheria za Qur’ani, hadithi na mwendo (sunna) wa Mtume, atakubali pia kufuata hadithi na mienendo ya watawala wawili waliomtangulia yeye. Ali alikataa kukubaliana na ahadi hizi mbili za mwisho na akatupilia mbali ahadi hiyo ya ukhalifa.

Kutokana na mwenendo wa baba yake, Husein alijifunza utumiaji wa kivitendo wa somo muhimu ambalo juu ya hilo, hapo baadaye tabia na mwenendo wake mwenyewe ulitegemea. Aliona kwamba mfumo wa sheria za Kiislam na matendo ya watawala wa Kiislam kwa dhahiri kabisa yalikuwa mambo mawili tofauti na kwamba njia za watawala hazikuweza kutafsiriwa kuwa, au kulinganishwa na mwenendo chini ya mfumo wa sheria ya Uislamu.

Kwa kweli ulikuwa mfumo huu ambao ulikuwa uwafunge watawala wa Kiislam kwa daraja lile lile la ulazimishaji kama ulivyowafunga Waislam wote kwa ujumla. Na wakati mtawala yeyote anapofuata njia zilizo tofauti na kanuni za Uislamu, ilikuwa ni jukumu la Waislam kuilinda dini (imani) na kutoona muhanga wowote kwa ajili ya lengo hilo kuwa na thamani sana.

Katika mwaka wa 31A.H. mabinti wa Yazdigard Mfalme wa Uajemi (Iran), waliletwa Madina kama wafungwa baada ya kuuawa kwake. Ali na Husein waliwaokoa kutokana na makundi ya wadhalilishaji, na Husein akamuoa mmoja wao, aliyeitwa Shahrbanawayh.

Katika kukaribia mwisho wa miaka ya utawala wa Uthman, khalifa wa tatu, watu walianza kujihisi kutoridhika kabisa na utawala wake, na hata wakaishia kwenye kufanya matendo ya vurugu. Ali aliingilia kati mara nyingi sana ili kuleta amani na akafanya baadhi ya malalamiko kuweza kurekebishwa. Aliwashauri wafanyaghasia kutawanyika na warudi walikotoka.2 Lakini Marwan, mkwe na katibu wa khalifa alionyesha ukatili sana kiasi kwamba jitihada za Ali katika kuleta amani zilishindwa, na waasi wakayazingira makazi ya khalifa ambaye maombi yake ya mdomo ya kupatiwa maji yalisikiwa na Ali.

Ali aliwaagiza wanawe, Hasan na Husein, kupeleka maji kwa Uthman katika hali ya hatari kubwa sana kwa maisha yao binafsi. Khalifa huyo hata hivyo, aliuawa na kundi lililokuwa na vurugu nyingi.

Inastaajabisha kwamba ingawaje khalifa alibakia kushambuliwa hapo Madina kwa siku 49,3 hakuna hata mkazi mmoja wa mji huo alijitokeza kuja kumwokoa, na kwamba alibakia bila kuzikwa kwa muda wa siku tatu na kwamba hatimaye mabaki ya mwili wake hayakupata nafasi katika eneo la makaburi ya Waislam.4

Baada ya ghasia kutulia Waislam waliamua kumweka Ali kama khalifa wao. Katika matukio yote ya nyuma ya uchaguzi wa khalifa, Ali alikuwa amehoji kwa nguvu sana kuhusu ubora wa madai yake juu kazi hiyo, lakini sasa hakuwa tayari kabisa kuukubali (ukhalifa), kwani aliona kwamba katika miaka iliyoingilia kati, serikali ya Kiislam ilichukua sura na ari ya falme za kikoo, ambayo ilikuwa na urahisi usio rasmi usiyopatana na moyo wa kupenda usawa wa Uislamu.

Ali asingeweza kuvumilia uozo uliokuwepo katika utawala uendelee, na alijua kwamba katika kujaribu kuusimamisha angezusha wimbi la upinzani usiodhibitika ambao ungechukua muda mrefu kuudhibiti, na kwamba kwa wakati huohuo angejiweka kwenye hali ya kuitwa mtawala asiyefaa. Hata hivyo Waislamu walisisitiza kwamba aukubali tu ukhalifa, na Ali kwa shingo upande sana alikubali kufanya hivyo. Katika mwezi wa Dhil-Hijja mwaka wa 35 A.H. Waislam walitoa kiapo cha utii kwa Ali kama khalifa wao.

Baada ya Ali kuchukua madaraka, wasiwasi wake uligeuka kuwa kweli. Watu hawakuwa na mwelekeo wa kutekeleza maelekezo (maagizo) yake. Baadhi ya Waislam mashuhuri kama vile Usamah bin Zayd, Hasan bin Thabit, Abdallah bin Umar na Sa‘d bin Abi Waqqas walijizuia kutoka kiapo cha utii kwake. Ali, hata hivyo hakuchukua hatua yoyote dhidi yao kwa vile katika Uislamu “hakuna kulazimishana katika dini.”

Kushikilia Syria kwa Mu’awiyah kulitiwa nguvu na kile kipindi kirefu cha ugavana wake wa nchi hiyo, na Ali alishauriwa ambakishe yeye pamoja na maofisa wote walioteuliwa na Uthman katika nafasi zao za kazi, kama hatua ya uangalifu mpaka watakapokuwa wamejinyenyekesha wenyewe kwenye udhibiti wake.

Ali alikataa kukikubali kipande hiki cha ushauri ambacho kingekuwa na maana ya kuunga mkono udhalimu na uharibifu wa watendaji hawa, na kwa kweli ni kama kushiriki kwenye maovu haya. Ali alimwandikia Mu’awiyah barua akimwambia alivyoikubali kwa shingo upande kazi ya ukhalifa na akamtaka apate viapo vya utii kutoka kwa watu wa nchi yake kwa ajili ya khalifa mpya.

Pia alimtaka Mu’awiyah aje yeye mwenyewe pamoja na ujumbe wa watu wa Syria.5 Mu’awiyah hakutekeleza lolote katika maelekezo haya, na uadui wa toka zamani ulimshawishi kuzua shitaka la uwongo la mauaji ya Uthman dhidi ya Ali dhidi ya yule ambaye hata yeye pia alimwasi. Mwanazuoni mkubwa wa Kisunni, Ibn Hajr amemnukuu Marwan bin al-Hakam akiwa amekiri kwamba hakuna aliyekuwa na msaada mkubwa zaidi kwa Uthman kuliko Ali, na kama alivyokuwa amesema kwamba matumizi ya lugha chafu dhidi ya Ali yalifanywa kwa sababu, kwani bila kufanya hivyo Bani Umayyah wasingeweza kusimamisha mamlaka yao.6

Mu’awiyah alichukua hatua za aina mbalimbali kuwachochea watu wa Syria dhidi ya Ali. Mikutano iliyohudhuriwa na watu wengi ilifanyiwa mara kwa mara katika msikiti wa swala za jamaa wa Damascus kuomboleza mauaji ya Uthman ambamo shati lake lililolowa damu na vidole vilivyokatwa vya mke wa khalifa (Uthman) vilionyeshwa kwa makundi makubwa ya watu ambao walipandisha sauti za maombolezo, na katika mfadhaiko huu wa huzuni walishawishiwa kulipizia kisasi mauaji yake.7

Wakati maendeleo haya kiuchochezi yalipokuwa yanafanyika nchini Syria, Talha na al-Zubeir waliweka upinzani mkubwa kwa Ali, wakiungwa mkono na Aisha, mjane wa Mtume na binti ya Abu Bakr, khalifa wa kwanza.

Ali alikwishakuwa mtu mzima na kwa kipindi kirefu aliishi maisha ya faragha. Hata hivyo, alijiandaa kwenda vitani na kupigana dhidi ya Aisha kuzilinda sheria na kanuni za Uislamu na za haki kwa nguvu zake za kawaida kwani jukumu la ulinzi wao ulikuwa hasa juu yake yeye. Kampeni hii ilikomea katika kutokea vita ya Ngamia, kwani Aisha aliliongoza jeshi lake kutoka kwenye kiti chake juu ya ngamia, na kushindwa kwake kabisa mnamo mwezi 10 Rabiul Thaaniya mwaka wa 36 A.H.

Katika wakati wa ushindi wake Ali alimtendea Aisha kwa uungwana na ukarimu usio na kifani na alimpeleka Madina kwa heshima kubwa akisindikizwa na askari ambao wote walikuwa wanawake waliojifanya kama wanaume.

Huko Syria vurugu na uchochezi wa ghasia viliendelea bila kupungua nguvu. Maombolezo kwa ajili ya Uthman yaliendelea kufanywa kwa mwaka mzima kamili na watu wengi wa Syria walichukua nadhiri ya kujiepusha na raha za kidunia mpaka wawe wamewaua wale wote ambao walimuua Uthman, hivyo Mu’awiyah akafanikiwa kuiamsha nchi yake dhidi ya Ali mpaka mwishowe vita vya Siffin vilikuja kupiganwa kati yake na Ali.

Ni lazima itajwe kwamba mpaka wakati wa mwisho kabisa kabla ya kuanza kwa vita Ali alijitahidi kwa kusisitiza kuwashauri wapinzani wake kutenda kwa busara na uadilifui na kutafuta kuungana na wanaodhaniwa kuwa ni maadui zao. Hata hivyo ushauri wake wa usuluhishi ulikataliwa na damu ya Waislam ikamwagika kwa wingi sana.

Kama kawaida, Ali aliliagiza jeshi lake lisianze mashambulizi, wakiliachia jeshi la maadui kuanza vita. Pia alikataza ufukuziaji wa adui aliyeshindwa, kumuua adui aliyejeruhiwa, kuukatakata mwili wa mtu aliyekwishakufa, alikataza kulazimisha kuingia katika hema bila ya kuruhusiwa, kupora mali ya adui na kusababisha madhara kwa wanawake hata katika hali ya kuchokozwa.

Wakati wa vita, majeshi ya Mu’awiyah yalitwaa udhibiti wa mto Furati (Euphrates) na yakasimamisha hudumu ya ugavi maji kwa jeshi la Ali ambalo liligeukia katika kutumia nguvu na hatimaye wakapata tena udhibiti juu ya mto huo. Ali alikataa kulipiza kisasi kwa kusimamisha huduma za kulipatia maji jeshi la Mu’awiyah, na akajishusha mwenyewe kufikia kiwango cha maadui zake.

Ali alipata uchungu sana kuona damu nyingi ya waislamu inamwagika katika vita vya Siffin, na akamwambia Mu’awiyah kwamba kwa vile vita halisi ilikuwa kati yao wawili, ingekuwa ni unyofu juu yao (Ali na Mu’awiyah) kuliamulia jambo hili kwa kukutana wao wawili katika pambano la watu wawili tu. Mu’awiyah hakutoa jibu, akiogopa kwamba asingeweza kunusurika katika pambano kama hilo. Kwa hiyo, yeye alishikilia tu kuwatoa muhanga wengine kwa malengo yake binafsi.

Mu’awiyah, alitembelea uwanja wa vita kwa nadra, wakati Ali alikuwa akionekana kila mahali ndani yake akiliongoza jeshi lake, wakati mwingine akilielekeza na zaidi sana yeye mwenyewe akiwa katikati ya vita vyenyewe. Alitamani kupata shahada na akaapa kwamba mapigo elfu moja ya upanga kwenye kichwa cha mtu yalikuwa yanastahimilika zaidi kuliko kifo cha kuteseka muda mrefu kitandani mwake mtu.8

Mwenendo wake sasa ulifuata mkondo uleule wa kutokusita kujihatarishia kifo kwa ajili ya Uislamu kama ulivyofuatilia hapo mapema katika maisha yake wakati alipolala katika kitanda cha Mtume usiku, Mtume alipotorokea Madina.

Husein na ndugu zake walihusika kikamilifu katika vita hivyo na wakamtumikia baba yao kwa uimara mkubwa katika nyakati za hatari kubwa kabisa.

Wasingeweza kutenda kinyume kabisa kwani walikuwa watoto wa Ali ambaye alikuwa amemwambia Husein wakati wa vita hivi kwamba ilikukwa haina tofauti muhimu kama ni kifo kimwangukie au ni yeye akiangukie kifo.9

Siku moja wakati vita ambapo vilipokuwa vimepamba moto, Ali alionekana akiliangalia jua ili kuhakikisha kama wakati wa swala ya mchana umekwishaingia. Alipoulizwa kama huo ulikuwa ni wakati wa kuswali katikati kabisa ya vita, Ali alijibu, “Ni kitu gani tunachokipigania basi?” Alifundisha kwamba swala ni lazima zisimamishwe katika wakati wake makhsusi iwe inamiminika mishale au moto.

Ili kuifupisha vita, siku moja Ali alifanya shambulio kubwa kabisa juu ya maadui, akiendeleza mashambulizi hadi usiku mzima uliofuatia. Wakati kulipopambazuka, watu wa Syria walikuwa wameshindwa vibaya sana na idadi yao kubwa walikuwa wameuawa na wengine kujeruhiwa.

Ilionekana kwamba wasingeweza kukwepa kushindwa kwa muda mrefu. Amr bin Aas, mshauri wa Mu’awiyah, alikimbilia kwenye hila ya kunyanyua nakala za Qur’ani Tukufu juu zikiwa zimechomekwa kwenye ncha za mikuki na kupandisha sauti zao juu wakidai kwamba tofauti kati ya pande husika zirejeshwe kwenye Kitabu cha Mwenyezi Mungu (Qur’ani) kwa ajili ya uamuzi.

Ali alikwisha ng’amua mtego wa hila hii na akawashauri wafuasi wake dhidi ya kuangukia katika mtego huu uliowekwa na watu wale ambao kamwe hawakuamini Uislamu wala hawakuwa na heshima yoyote juu ya Qur’ani. Aliwakumbusha pia kwamba ombi kama hilo alilokuwa amelitoa yeye kabla ya kuanza kwa vita lilikuwa limekataliwa.

Lakini watu wengi wa jeshi la Ali walikuwa wamepotoka katika kukataa maagizo yake na wakageuka dhidi yake, na hata kumtishia maisha yake. Wakati utovu wa nidhamu kamili ulipozidi ndani ya jeshi lake, Ali alisitisha mapigano. Masuala kati ya pande mbili hizi zenye kushindana yalipelekwa kwa wasuluhishi wawili, Amr bin al-Aas na Abu Musa al-Ash’ari.

Amr bin al-Aas alimwakilisha Mu’awiyah na watu wa Syria na Abu Musa al-Ash’ari alilazimishwa juu ya Ali kuwa kama mwakilishi wake, kinyume kabisa na alivyotaka mwenyewe, na akawa kama mwakilishi wa wakazi wa Kufa. Tabia ya Abu Musa huko nyuma ilikuwa imeonyesha mwelekeo wake usiopendeza kumhusu Ali ambaye alikubali kuchaguliwa kwake kwa ajili tu ya kukwepesha umwagaji wa damu ndani ya kundi lake.

Makundi hayo mawili yalikubaliana kutii uamuzi wa Mwenyezi Mungu na Kitabu Chake na sio kitu kingine kile. Wasuluhishi walikuwa chini ya masharti ya kuiweka Qur’ani wakati wote katika mazingatio na kuifanyia kazi, na kama hawakupata mwongozo kutoka humo, ilikuwa watende kwa mujibu wa matendo na kanuni za Mtume zisizotiliwa shaka. Ali alichukua tahadhari kuwasisitizia kwamba hawakupewa mamlaka yoyote yale ya kuamua kwa kulingana na fikra zao binafsi. Mkataba huu ulifanyika mwezi 13 Safar, 37 A.H.

Makubaliano haya yalikuwa hata bado hayajaanza kutekelezwa wakati fitna mpya ilipoinua kichwa chake kibaya katika sura ya makhariji ambao walinyanyua ndani ya jeshi la Ali ule wito wa makelele kwamba hakuna hukumu isipokuwa ya Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo, wao waliuchukulia ule uteuzi wa hivi karibuni wa wasuluhishi kuwa ni wenye makosa na wakamshinikiza Ali kupigana na Mu’awiyah na wakaahidi kumsaidia. Ali alikataa kuwakubalia akisema kwamba Qur’ani inaagiza kwamba neno lililowekewa ahadi lazima liheshimiwe. Ma-Khariji wakageuka kuwa wasaliti kutoka kwenye Uislamu na wakaunda kundi lao tofauti.

Wasuluhishi wakapuuza kabisa masharti yote ya chombo cha usuhulishi na wakadharau sheria za Qur’ani. Amr bin al-Aas alikuwa bingwa mkubwa katika hila na akamfanya Abu Musa al-Ash’ar kuwa mjinga kabisa. Alimmvutia Abu Musa al-Ash’ari kwa tabia yake ya kiheshima kwamba kwa kweli yeye alimheshimu sana Abu Musa kuwa ni mkubwa na mbora kwake, na kwa hiari kabisa akamkubalia kutangulia. Kati yao wenyewe, walitokea kuamua kuwatangaza wote wawili Mu’awiyah na Ali kuwa hawafia kushika wadhifa wa ukhalifa na (wakaamua) kuwapa Waislam haki ya kuchagua khalifa mwingine.

Wakati muda ulioteuliwa wa kutoa tangazo la uamuzi wa wasuluhishi ulipofika, Abu Musa al al-Ash’ari aliombwa na Amr bin al-Aas kutangaza uamuzi huo, ambao akautangaza kama walivyokubaliana kati yake na Amr bin al-Aas.

Kisha Amr bin al- Aas alisimama kusema kwamba kwa vile Abu Musa anamwakilisha Ali, alikubaliana na uamuzi wake wa kumuuzulu Ali kutoka kwenye ukhalifa. Akaongoza kwamba akiwa kama mwakilishi wa Mu’awiyah, yeye anausimika ukhalifa juu yake.

Uamuzi huu usio wa udanganyifu ulisababisha vurugu na miongoni mwa wale waliokuwepo, na wasuluhishi wakafanyiwa fujo. Uamuzi ukakataliwa na pande zote. Ushindani kati ya pande zote ukabakia bila kufumbuliwa. Tukio hili liliimarisha ile rabsha ya mgawanyiko katika safu za kundi la Ali na liliwapa Makhariji muda wa kujiweka sawa ili kuweza kumpinga Ali kwa upinzani mkali katika vita vya Nahrawan ambayo vilifuata.

Hata baada ya vita vya Nahrawan ambamo Makhawarij walipata kipigo na kushindwa kabisa, bado utovu wa nidhamu, vurugu na uchochezi wa maasi ulikuwa bado haujang’olewa kabisa ndani ya jeshi la Ali. Alikuwa kwa kweli katika masaibu yasiyopendeka. Alikuwa na mzigo wa wafuasi wasio waaminifu waliogawanywa na kutoelewana na mfarakano. Makhawarij ambao walikuwa hawakupigana au walitoroka kule Nahrawan walichochea hisia za kufanya uasi dhidi yake miongoni kwa watu. Mu’awiyah aliitumia nafasi hiyo ya kukosekana umoja uliokuwepo Kufa.

Aliyatumia majeshi yake kuchochea ghasia katika nchi za Kiislam na alikimbilia matendo kama hayo kama ya kuwaondolea wapinzani, kama vile Malik al- Ashtar,10 kwa kuwafanya watiliwe sumu au kwa njia nyingine za kudanganyifu, kama katika suala la Muhammad bin Abu Bakr, ambaye alikuwa amelelewa na Ali na alikuwa mmoja wa wafuasi wake watiifu mno.

Alipelekwa na Ali kuwa gavana wa Misri na kwa ombi la Mu’awiyah, Amr bin al-Aas aliongoza jeshi dhidi yake kwa ushirikiano kabambe na kikosi cha wahaini wa Kimisri11. Hili liliishia katika kushindwa kwa Muhammad bin Abu Bakr na kuuawa kwake. Mabaki ya mwili wake kisha yalichomwa moto.12

Alipoona kwamba ilikuwa vigumu kumshinda Ali katika vita vya viwanja vya wazi, Mu’awiyah alitumia mbinu vita vya msituni kama njia ifaayo ya kuiweka dola ya Kiislam katika hali ya hofu, fujo na ghasia wakati wote.

Idadi ya mashambulizi kama hayo ya ghafla na kukimbia yalifanywa na wafuasi wa Mu’awiyah, na baadhi walizuiliwa kwa nguvu na kurudishwa nyuma. Shambulizi la kikatili sana la namna hiyo liliongozwa na Busr bin Abi Artat dhidi ya Hijaz, tukio ambamo alilazimisha viapo vyao vya utii kwa Mu’awiyah kutoka kwa wakazi wa Makkah na Madina, na akawachinja watoto wawili wa kiume wa Ubaydullah bin Abbas nchini Yemen.

Ali alikuwa anajishughulisha katika kujiandaa kupambana na tishio hili, lakini katika wakati ule ule Ibn Muljam al-Muradi alimpiga dhoruba kichwani kwa upanga uliotiwa sumu wakati akiwa yuko katika kusujudu mbele ya Mwenyezi Mungu ndani ya msikiti wakati wa swala ya asubuhi (alfajiri) ya siku ya mwezi 19 Ramadhani mwaka wa 40 A.H. Siku tatu baadaye, Ali akawa hayupo tena katika ulimwengu huu (akafariki dunia).
________________________
1. Irshad, uk. 136, Tabari, Juz.1, uk. 1827-8

2. Tabari, Juz. 1 uk. 2969 na 2971

3. Tabari, Juz.1 uk. 3009

4. Tabari, Juz.1 uk. 3008

5. Nahjul-Balaghah, Juz. 2, uk. 140

6. Ibn Hajr, al-Sawaaiq, uk. 33

7. Tabari, Juz. 1, uk. 3091

8. Irshad, uk. 177

9. Tabari, Juz. 1, uk. 3294

10. Tabari, Juz. 1, uk. 3401

11. Tabari, Juz. 1, uk. 3404

12. Tabari, Juz. 1, uk.3406
Bani Umayyah walilazimika kuukubali Uislamu ili kuyaokoa maisha yao, na siyo kwa imani yoyote ile kuhusu ubora wa ujumbe wake. Matokeo yake waliendelea kuendekeza, katika nyoyo zao hisia za chuki na uadui juu ya dini (imani) yao mpya waliyoipata, na walisubiri kwa shauku kubwa kuipata fursa ya kuuangamiza mwenendo wake, kwani waliona kwamba ilikuwa nje ya uwezo wao kufanya jaribio la wazi la maangamizi yake ya mara moja.

Walifikiria mpango unaofaa sana wa kiutendaji kuziharibu na kuzichafua tabia na sifa pambanuzi za Uislamu ambazo zilivunjilia mbali uwezo wao. Ilikuwa ni kutumia kivuli cha Uislamu wenyewe kuidhuru imani yake, na kuufagilia njia ufufuaji upya wa maadili na fursa zilizokuwepo kabla ya kudhihiri Uislamu.

Kwa ufupi, walikuwa wanafiki. Madhara kidogo sana yaliyopatikana au kutegemewa kuwapata Waislam yalileta furaha ya kiuovu iliyofichika kwa Bani Umayyah.

Hivyo katika vita vya Uhud, pale watu wote walipokimbia isipokuwa Waislamu wachache waaminifu, Abu Sufyan alionyesha furaha yake kwa lile alilolifikiria kuwa ni ushindi wa sanamu la kipagani liitwalo al-Uzza.1

Hadithi kuhusu namna gani Ali alivyozuia jaribio la kwanza la Abu Sufyan la kutaka kuvuruga Uislamu kwa kukataa kuukubali msaada wa kijeshi alioupewa na yeye Abu Sufyan wakati Abu Bakr alipowekwa kuwa Khalifa kuliko madai yake Ali ambayo yamekwishasimuliwa.

Ali mara moja alikwishauona mchezo huu wa Abu Sufyan na akamwambia kwamba yeye (Abu Sufyan) alikuwa ni adui wa Uislamu na Waislamu.

Abu Sufyan bila kusita alibadilika, na kwa mafanikio makubwa akajadiliana masharti ya ushirikiano na wapinzani wa Ali. Khalifa wa kwanza alipeleka jeshi kubwa kuivamia nchi ya Syria katika mwaka wa 13 A.H., na miongoni mwa wale ambao waliongoza jesi hili walikuwamo watoto wawili wa Abu Sufyan, Yazid (bin Abu Sufyan) na Mu’awiyah.

Abu Sufyan mwenyewe alishughulika kama msimuliaji wa hekaya kwa ajili ya burudani ya viongozi wa vita,2 na binti yake na mkwewe pia walishiriki katika vita hii. Baada ya ushindi wa Syria, Yazid bin Abu Sufyan aliteuliwa kuwa gavana wa nchi hiyo. Alipokufa alirithiwa na ndugu, yake, Mu’awiyah.3

Wakati wa kipindi cha ugavana wa watoto wao, Abu Sufyan na Hind, ambaye alikuwa ameachika, walipata manufaa mengi za kiuchumi. Hind alitanguliziwa fedha kiasi cha dirham 4,000 kutoka kwenye Hazina ya taifa ambazo aliziwekeza katika biashara yenye faida kubwa sana.

Abu Sufyan alilipwa dinari mia moja kama gharama za kujikimu wakati alipotembelea Damascus,4 ingawaje bado alikuwa na nia mbaya dhidi ya Uislamu kwani yeye hakuweza kuzishinda hisia za huruma alizozichukua kwa ajili ya wa-Byzantine, waliokuwa kwa wakati huo wakipigana huko Yarmuk dhidi ya Waislamu.

Uthman alikuwa Khalifa mnamo mwaka wa 23 A.H. na Abu Sufyan akamshauri kuimarisha mamlaka yake kwa msaada wa ndugu zake, Bani Umayyah. Aliongeza kwamba ni maml

Share this article

Comments 0

Your comment

Comment description

Latest Post

Most Reviews

MOST READ