Rafed English

Safari Wa Kuifuatianuru

Safari Wa Kuifuatianuru by : Sayyid Abbas Noor Eddine

 

Kitabu kilichoko mikononi mwako ni tarjuma ya kitabu cha Kiingereza kiitwacho, The Journey to the Light kilichoandikwa na Sayyid Abbas Noor Eddine. Sisi tumekiita, Safari ya Kuifuatia Nuru.

Kitabu hiki kinazungumzia maisha ya Imam Mahdi (a.s.) na Ughaibu wake, jinsi ulivyotokea na anavyoishi sasa katika maisha hayo ya kutoonekana. Waislamu wamehitalifiana juu ya Ughaibu wake na jinsi anavyoendelea kuishi akiwa katika Ughaibu.

Mwandishi wa kitabu hiki amejaribu kuelezea kwa lugha nyepesi juu ya hitalafu hizo, na hatimaye kwa kuonesha jinsi alivyozaliwa mpaka kuingia kwenye Ughaibu, jinsi anavyoishi Ughaibuni huko na jinsi wafuasi wake (ambao ni Waislamu) wanavyonufaika naye pamoja na kwamba yuko Ughaibuni.

Tumekiona kitabu hiki ni chenye manufaa sana, hususan wakati huu wa maendeleo makubwa ya elimu katika nyanja zote, ambapo uwongo, ngano za kale na upotoshaji wa historia ni mambo ambayo hayana nafasi tena katika akili za watu.

Kutokana na ukweli huo, Taasisi yetu ya Al-Itrah Foundation imeamua kukichapisha kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili kwa madhumuni yake yaleyale ya kuwahudumia Waislamu, hususan wazungumzaji wa Kiswahili.

Tunamshukuru ndugu yetu, Selemani Salum Matumula kwa kukubali kukitarjumi kitabu hiki. Vilevile tunawashukuru wale wote walioshiriki kwa njia moja au nyingine hadi kufanikisha kuchapishwa kwake.

Mchapishaji:

Al-Itrah Foundation
S. L. P. 19701
Dar-es-Salaam, Tanzania.

Imepokewa kutoka katika hadithi kwamba kabla ya kurejea kwa Imam Al-Mahdi (a.s), jina lake na kutajwa kwake kutazidi katika ndimi za watu. Kama ambavyo tunaamini kwamba sasa tunaishi katika zama zenye baraka za kabla ya kurejea kwake, na kwamba ni wajibu wetu kushiriki huko ‘kuendelea kumtaja’ kama sehemu ya kuendelea kutimiza ahadi zetu tulizojiwekea katika kutoa maarifa bora ya Uislamu katika jumuia yetu hususan kwa vijana, tunakitambulisha kitabu hiki kwako, “Safari ya kuifuata nuru.” Ni kitabu cha tatu kutolewa baada ya vitabu vilivyotangulia; “Tukio la Karbala” (An Emergence over Karbala) na, “Njia ya kuufikia ukamilifu” (Your Way to Perfection).

Kitabu hiki si kipya kwa maudhui yake, kwani fikra zilizotolewa humu zimo katika vitabu vingine. Hata hivyo, namna yake ya uandishi imeelekezwa kwa uangalifu kwa mtu yeyote yule anayetaka kupata habari za kweli juu ya Imam Mahdi (a.s), ni utaratibu mpya na utamfanya muda wote awe anafuatilia kuisoma kwa mazingatio.

Sayyid Abbas Noor Eddine ameweza kumuelezea Imam Mahdi (a.s) katika kurasa hizi chache katika namna ambayo ameweza kulifikia lengo lililokusudiwa na pia inaweza hata kuanzisha mwenendo mpya wa jinsi ya kuyafumbua masuala yaliyo tete kama haya.

Ni vyema ifahamike kwamba kitabu hiki kimewalenga zaidi vijana ambao wanajitahidi kuujenga utamaduni wao wa Kiislamu katika njia nyepesi kwa kadri iwezekanavyo. Hata hivyo, hii haina maana kwamba kitabu hiki kitakosa manufaa kwa wengine, na hasa hata kwa wale ambao wana maarifa makubwa juu ya mada hii muhimu.

Mwisho tungependa kumshukuru mwandishi, Sayyid Abbas Noor Eddine, mtarjumi Zaid Al-Salaami, na mtangazaji, dada Nada Haidar, kutokana na Juhudi zao kubwa mno

Pia tunawashukuru wote ambao wametusaidia katika kipindi chote ambacho kitabu hiki kilikuwa kinatayarishwa.

Kitabu hiki ni utambulisho mfupi juu ya mtu mkubwa sana na mwenye shakhsiya isiyofanana na mwingine aliye na siri nyingi zilizofichika na kubwa mno. Wale waliopata kumfahamu na wanaomuamini maisha yao yamebadilika kabisa, na kuna uhusiano maalum kati yao na mtukufu huyu.

Hatuwezi kujua kiwango cha mabadiliko haya kwa sifa zake na ukubwa wake, kwa sababu yanatofautiana kati ya mtu na mtu. Hata hivyo, kadiri tunavyofahamu, ni mageuzi makubwa, na mfano wake asilan usingeweza kutokea kwa mahusiano yeyote mengineyo.

Mtukufu huyu anangojewa na ulimwengu wote, na anatajwa na wafuasi wote wa dini zinazoamini kwamba Mwenyezi Mungu ni Mmoja kwa majina mbalimbali. Waislamu humuita Mtukufu huyu kama “Al–Mahdi” (a.s), na baadhi yao wanalijua jina lake kamili na mambo mengi kuhusiana na yeye.

Waislamu Mashi’a wanafahamu kwamba ni “Imam Muhammad bin Al- Hasan” (a.s). Walikuwa wakiieneza siri hii (ya jina lake sahihi) miongoni mwao wenyewe, wakikataza kuitangaza siri kwa hofu ya kuhatarisha maisha ya mwenye jina hili. Na wakati walipokuwa na uhakika kwamba hakuna hatari yoyote ambayo ingeweza kumpata waliruhusu na kuanza kulieneza bila woga au hofu ya kukamatwa kwake.

Mtukufu huyu ndiye yupi basi, ambaye idadi kubwa sana ya watu, wanaozidi milioni mia moja, wanaunganishwa na yeye, kiasi kwamba wamenasibishwa na jina lake na wanatambulika kwa jina hilo? Mashi’a hususan hujulikana kama “Shi’a Imamia,” jina linalotokana na huyu Imam.

Ni vipi mataifa mengine yalipata kuwa na uhusiano na Mtukufu huyu, na vipi wamekuwa wakimzungumzia? Kwa nini jina lake limefichuliwa na kwa nini siri nyingi zinazohusiana na yeye zimefichuliwa, hususan kwa Mashi’a peke yao tu? Na kwa nini Mashi’a wamekuwa wakijiamini sana na hata kuwa na ari ya kuutangaza ujumbe huu kwa mataifa yote ya Ulimwengu?

Maswali haya ya kuvutia yatajibiwa ndani ya kurasa za kitabu hiki pamoja na maswali mengine ambayo yatatokeza kadri tutakapokuwa tukiendelea.

Na ni kwa vile Mashi’a ndio ambao wanamtaja mtu huyu wa ajabu mara kwa mara, na wakiwa na mambo mengi zaidi kwa undani kuhusiana naye, tutaanza na wao ili tuweze kuyatolea ufumbuzi maswali haya.

Kama maswali haya yataachwa bila ya majibu ya kutosheleza, wale ambao wanafanya utafiti ili waupate ukweli watakuwa wamewekwa katika hali ambayo watakuwa hawajui wafanye nini, kwa kutopewa fursa muhimu ya kubadili maisha yao kuwa bora zaidi, maisha yaliyo na mengi yanayopendeza na mengi yanayovutia.

Nimeshawahi kupata kuwaona baadhi ya hawa Mashi’a ambao wanamfa- hamu vyema mtukufu huyu, na wamekuwa na uhusiano wa karibu zaidi na yeye.

Nimeshayaona maisha yao yakiwa yamejaa mno matumaini huku wakiwa ni wenye kusubiria hiyo siku itakapofika, wakiwa hawajakata tamaa, wala hawana hofu wala kufadhaishwa na maisha ya kipuuzi, zaidi ya matumaini hayo makubwa. Nimewaona watu hawa wana ari na ushujaa.

Nimepata kuwajua watu ambao mfano wake haupatikani popote pale ulimwenguni. Ingawa watu wengi kutoka mataifa mbalimbali humtaja Mtukufu huyu na humuamini, maisha yao hayajabadilika na sijaona chochote kwao kama ambavyo nimeona kwa Mashi’a. Siri ya jambo hili, na siri yote hii hasa ni habari zenye maelezo kwa undani zaidi.

Ni vipi Mashi’a walikuja kumfahamu Imam Mahdi (a.s)? Je, wengine walikuja kumfahamu?

Katika namna ambayo walivyomfahamu Imam Mahdi (a.s), Mashi’a wamegawanyika katika sehemu mbili:

Kundi la Kwanza: Waliomfahamu Imam baada ya kupita njia ndefu katika kupata elimu. Walimjua mwanzoni ambapo palikuwa na masuala mengi yaliyowaongoza wakamfahamu. Kwa sababu waliishi katika mazingira na mahali ambapo palikuwa na habari nyingi za kweli, na moja kwa moja wakatokea kumwamini Imam.

Wakazifahamu sifa zake njema, lengo na makusudio ya kazi yake anayoitekeleza na atakayoitekeleza, wadhifa wake na wajibu katika maisha yetu kwake.

Kundi la Pili: Ni wale ambao waliuona ukweli wa mambo yanayotokea hapa ulimwenguni. Walishuhudia dhuluma za kutisha, maafa ya kutisha, ubadhilifu, uongo na kutawaliwa kwa mabavu kwa wanyonge na wenye nguvu, kwa sababu walikuwa ni watu wenye hisia na waliweza kuhisi hali ya madhila na shida wazipatazo watu, hivyo walikuwa wakifanya utafiti wapate wokovu kuokoka na jinsi ya kuzuia haya madhila ambayo yalikuwa yakiwapeleka binadamu kuelekea mwisho mbaya.

Kutokana na hisia zao kubwa na jitihada zao njema walizokuwa nazo, ziliwaongoza kutambua kwamba upo mpango maalum unaotoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuuokoa ulimwengu dhidi ya dhulma na ukandamizaji na baadae kuleta haki na amani. Jambo hili halikukawia sana kulitambua, kwani imani yao kwa Allah (s.w.t) iliwaongoza kuufahamu mpango huu.

Kama Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehma, katika kipindi chote cha maelfu ya miaka katika historia ya mwanadamu Aliwatuma watu waje kuwaokoa wanadamu, vipi asifanye hivyo tena? Je, huruma Yake imeisha? Au neema zake zimetoweka? Au je, hawezi kufanya chochote?

Maadam Mwingi wa Rehema, Mkarimu, Mwenye Nguvu Allah (s.w.t) ambaye Huruma Zake zisizo na kikomo na Ukarimu wake usiokwisha, na ambaye Ayafanyayo hayazuiliki, Yu Hai, Yu Mjuzi wa yatendekayo, Yu Aona na Yu Asikia, na Uumbaji Wake wanadamu kila siku ni uthibitisho juu ya hili, na ni alama ya wazi ya ukarimu Wake, na ni kutokakana na imani hii juu ya uumbaji Wake kwamba upo Mpango, ambao utekelezaji wake unangojewa.

Mtu Mtukufu, yaani mwanadamu aliye karibu zaidi na Mola wake, yaani Imam ambaye ndiye mwenye Mpango huu wa Mwenyezi Mungu Mwenye Huruma, hakika naye vilevile yu hai. Ama sivyo, Mwenyezi Mungu ana uwezo kwa wepesi mno kuumalizia mbali msiba huu kwa kuyasitisha maisha ya hapa duniani.

Hapa kundi la kwanza walijaribu kujibu swali hili na kutueleza juu ya namna ya kumjua na kumtambua, kwa jina lake, kwa sifa zake na umbile lake! Yeyote anayekulia na kulelewa katika mazingira ya wafuasi halisi wa madhehebu ya Shi’a, kwani kuna watu wengi wanajiita Mashi’a lakini hawajui chochote juu ya Ushi’a, na kukaa karibu na wanazuoni huweza kumfahamu Bwana Mlezi wa Ulimwengu (swt) ambaye wote humuabudu kwa namna ya kushangaza siku zote.

Zipo hadithi nyingi za Kishi’a zinazomhusu ambazo ni nzuri mno, zina- zoelezea namna Mwenyezi Mungu (s.w.t), anavyowatendea viumbe wake, na jinsi anavyohusiana nao, katika namna ambayo maarifa yanayopatikana kutokana na hadithi hizo, pamoja na hazina kubwa ya kisayansi ya Kiislamu humfanya mtu aweze kumaizi mambo yaliyofichika katika uhai na siri zake, kimahusiano na mfuatano, bila ukinzani wala kasoro.

Binadamu anapendwa na kuthaminiwa na Allah (s.w.t). Mapenzi ambayo yapo kati ya Allah (s.w.t) na viumbe wake ni jambo lisiloweza kuelezeka kwa maneno matupu. Mwenyezi Mungu (s.w.t), ameumba kila kitu kwa ajili ya binadamu, na Yeye atafanya lolote lile ili amuongoze, amuokoe, na kumfanya afikie kikomo cha furaha kubwa kabisa na ukamilifu.

Chochote kile kilichopo hapa ulimwenguni ni kutokana na kazi ya Allah (s.w.t) isipokuwa uovu ambao umefanywa na watu waovu na madhalimuna yote ayafanyayo Allah (s.w.t) ni kwa ajili ya maslahi ya huyu huyu mwanadamu.

Ingawa hatufahamu ni vitu vingapi vinavyoishi, na ni vitu vingapi vinavyotokea hapa Ulimwenguni, dunia hii imeumbwa katika namna ambayo kila chembe ina hisia za mapenzi kwa kiumbe huyu, na hutaka kumtumikia, na kumfanya awe mwenye furaha.

Hatujui ukweli wowote juu ya ndege anayelia kwenye tawi la mti bustanini kwetu kwamba humwomba Mola atusamehe dhambi zetu na kutupa Rehema na Baraka juu yetu. Allah (s.w.t) amemuumba kwa ajili ya kutuombea sisi Kwake.

Je, na vipi kuhusu miti na majani yake, majani ya ardhini na mimea yake na kila jabali na jiwe, na kila mlima na sayari? Akili hutulia unaposikia ukweli huu na moyo hujawa furaha unaposimuliwa hadithi hizo.

Mola wa Ulimwengu ni Mwingi wa Rehema na Mwenye Haki, Huongoza viumbe wake na humshika mkono yeyote yule atakaye uongozi na ambaye amechagua njia ya wokovu.

Huwatuma wajumbe wake wakiwa kama Mitume wake ambao hutoa mafunzo ya dini na kuonya, wakiwa na amri zitokazo Mbinguni na kutangaza mwongozo wa Allah na kueneza sheria za Mwenyezi Mungu ambaye ni Mmoja.

Hata kama Mitume watauawa, Rehema Yake haiishi asilan. Utoaji toka Kwake huendelea, na ule mstari wa Rehema ambao hukizunguka kila kitu baina ya mbingu na ardhi utaendelea kuwepo.

Ingawa Utume ulishafungwa na Bwana wa viumbe na Mbora Kabisa wa Mitume Muhammad ibn Abdillah (amani iwe juu yake na Aali zake), hii haina maana kwamba Rehema za Allah zitakwisha.

Mpango wa wokovu wa Ulimwengu, Utawala wa Mwenyezi Mungu na urithi na kuchukuliwa kwa dunia hii na wachamungu, ushindi wa wanyonge kushindwa kabisa kwa madhalimu, yote haya ni ahadi za Mola Mwenye Nguvu ambaye havunji ahadi yake asilan.

Hivyo, Mpango huu bado upo. Mwenyezi Mungu Allah (s.w.t) anasema katika Qur’ani:

قُلْ فَانْتَظِرُوا إِنِّي مَعَكُمْ مِنَ الْمُنْتَظِرِينَ {102}

“Sema (ewe Mtume wetu Muhammad): Subirini, hakika Mimi nipo pamoja na wenye kusubiri” (Qur’ani: 10:102).

Wanazuoni wa Kishi’a wametaja katika vitabu vyao kazi kubwa ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w) kwamba ilikuwa ni kuongoza watu, kuhifadhi Qur’ani na kuzuia kuifanyia mabadiliko na kuipoteza (ikiwa ndio Mwongozo wa maisha na Mpango wa kuleta mabadiliko), na majukumu haya yalihamishiwa kwa Maimamu Ma’asumu (amani iwe juu yao) baada ya kifo chake.

Na ili watu wasipotoke kwa kutowafuata wao, kama kweli walikuwa wanautafuta mwongozo, Mtume (s.a.w.w) aliwatajia majina yao na kuzitaja sifa zao. Maimamu kwa upande wao waliubainisha mpango huu kwa ufasaha, na walionyesha njia ya wokovu, huku wakiyataja mambo ya lazima ya kuzingatia.

Moja kati ya mambo ya muhimu ya Mpango huu ilikuwa ni kumtambulisha kiongozi wake, Msimamizi wa utekelezaji wake na mwenye kuhakikisha kwamba unaendelea kuwepo kama inavyotakiwa, ili uweze kukabidhiwa kwa kizazi ambacho kitakuja kutokea na kuutumia kwa ukamilifu kabisa ulimwenguni pote wakiwa pamoja na Imam.

Hili litatokea katika siku na muda aujuao Mwenyezi Mungu - Allah (s.w.t) tu peke yake.

Basi Kwa Nini Mashi’a Wa Kweli Wana Matumaini, Uhai Na Nguvu?

Ni kwa sababu tu hawakuridhishwa kwa kuona tu misiba ya hapa Ulimwenguni, na kulia kwa kutoa machozi na kuonyesha huzuni na simanzi. Katika hali hii hii ya vurugu, na kutokana na wingi na undani wa matukio haya maovu, waliweza kutambua kuwepo kwa Allah (s.w.t).

Allah (s.w.t) ambaye Yu-Kila Mahali ndiye Yeye ambaye anadhibiti kila kitu na hakuna chochote kinachotokea bali huwa ni kutokana na Mapenzi Yake na Hekima zake katika kuyaendesha mambo ya Ulimwengu na kuon- goza na kuwaokoa waumini.

Hivyo ni namna gani ambavyo sisi tunadhani hali ya mtu itakavyokuwa, ambaye amejifunza yote haya, na vile vile jinsi ambavyo rehema itakayoletwa na kuwafikia wote, na jinsi Allah (s.w.t) atakavyouondoa uovu kutoka hapa ulimwenguni.

Zaidi ya hapo, yule ambaye amejifunza, ikiwa ni pamoja na Mpango wa wokovu, sababu za kutokea kwa udhalimu na ufisadi, na sababu za kuendelea kwa huzuni na majonzi; baada ya kuyaona yote haya pamoja na habari sahihi, kwa uwazi kabisa na kwa undani, huwezesha kuipa mwanga na kuifungua njia yake na kumuita aweze kushiriki katika kuunusuru ulimwengu, kuuokoa na kuzitokomeza huzuni na machungu yake.

Lakini si wito tu; bali ni uteuzi katika nafasi hii na ni jukumu la kuwaita pamoja wale wote ambao wameuitikia wito huu.

Hivyo, Mashi’a huzihusisha imani zao juu ya Allah (s.w.t) na vile wanavyoyaelewa yale yanayotokea Ulimwenguni, yaani, hivyo ni kusema kwam- ba ni baina ya mambo yanayoonekana na yasiyoonekana (al-ghaib wa al-shahada), kati ya roho na vinavyoonekana (al-ruh wa al-dhahir) na kati ya moyo na matendo (al-qalb wa al-amal).

Kwao, imani kwa Allah (s.w.t) sio tu hisia za moyoni bali ni kuendelea kutafiti kuwepo kwa Allah (s.w.t) katika kila uwanja wa maisha yao na kuweza kupata kuifahamu Hekima Yake, Ayatendayo na namna anavy- ouendesha Ulimwengu.

Hawatenganishi hali ya kila siku na imani yao juu ya Allah; hivyo ndio kusema, wanaishi katika maisha yao wakiwa wanafahamu fika kuwa hivyo ndivyo Allah (s.w.t) anawataka wao waishi.

Hawadanganyani wala hawawadanganyi wengine kwa kujiamulia wao wenyewe kwamba yupi ni mwadilifu na yupi si mwadilifu.

Mizani wanayotumia ni Allah (s.w.t) ambaye kwao hayupo mbinguni tu basi. Kwa sababu hii wameamua mara moja kufuata tabia ambayo inalingana na mani yao na uhusiano wao na Allah (s.w.t).

Hivyo yeyote yule ambaye ni adui wa Allah (s.w.t) kwao pia ni adui yao, na yeyote yule amtakaye Allah (s.w.t) yu pamoja nao. Hivi ndivyo namna walivyopata kumjua Imam (a.s) na kumfuata na kuungana na Mpango wake.

Imam haonekani hivyo huwezi kupata hisia za kuwepo kwake; mtu hawezi kumuamini mpaka awe na imani juu ya yale yasiyoonekana.

Imam ni Uadilifu wa daraja ya juu kabisa; mtu hawezi kumuamini mpaka awe hana imani juu ya watawala madhalimu na kuacha dhuluma.

Imam ni Rehma ya upeo wa juu kabisa, mtu hawezi kumuamini mpaka ndani ya nyoyo zao ziwe hai kwa mapenzi juu ya wanaodhulumiwa na wenye shida.

Hii ndiyo habari ya Mashi’a na Imam Al-Mahdi (a.s) ambayo ni sehemu ya siri ya uhusiano wao uliopo na kushiriki kwao katika Mpango wake.

Hata hivyo ……

Endapo mtu anajifanya anamuamini Allah (s.w.t) lakini hafanyi utafiti wa kumjua alipo katika maisha yake ….

Endapo mtu anajifaharisha kwa kumpenda Allah na bado akawa haonyeshi huruma juu ya wanaodhulumiwa na wenye shida………..

Wakati mtu anajua ghadhabu za Allah juu ya madhalimu na bado akawa kimya kwa vitendo vyao wanavyovifanya……………….

Ndipo hapo bila ya kujali kwa kiasi gani anajifanya na anadai anapenda kumpenda Mwokozi na kutangaza na kumlilia, hataweza kumfikia wala kumjua wala kuwemo katika Mpango wake.

Mwokozi huyu si masimulizi ya habari ya mtu ya kihistoria au utabiri wa mambo yajayo; yeye ni mkubwa zaidi ya hapo na mtukufu wa daraja la juu zaidi kuliko hivyo, pamoja na kwamba ametajwa katika historia na amekuwa ni utabiri wa hapo baadaye.

Yeye ndiye aliye na Mpango, Majukumu na Lengo…………..

Yeye ndiye Mwadilifu wa upeo wa juu kabisa ambaye hatafanya mkataba wa amani na madhalimu.

Tutasoma juu ya maisha ya Imam Mahdi (a.s) kwanza kabisa juu ya jinsi alivyozaliwa ambapo itatukumbusha alivyozaliwa Nabii Musa (a.s) ambapo Allah (s.w.t) alimficha ili Firauni na askari wake wasimuone.

Ni hadithi inayofanana… kwani kila baada ya dhuluma ya madhalimu kukikithiri, na watu kukata tamaa ya kutafuta ufumbuzi wao wenyewe, huwa na tamaa ambayo huwarudisha katika dini ili watafute njia ya wokovu. Hali hii ina athari kubwa katika kuhuisha suala la Imam Mahdi (a.s) kwa uwanja mpana zaidi baada ya kuwepo kwa watu wachache tu hapo kabla.

Watawala wa wakati huo kabla ya kuzaliwa Imam Mahdi (a.s) walielewa kuwa jambo hili ni la kweli na kwamba limeshaanza kuonesha tishio kali kwao kwa sababu tu ya hamu ya watu kwa ajili ya muundo mbadala wa utawala, vyovyote utakavyokuwa, utahatarisha ufalme wao. Kwani ni nini kama watu walichokuwa na hamu nacho ni Matumaini, Mwokozi, Uadilifu na Uislamu wa kweli!

Ndipo hapo kazi kubwa ya kutafuta kumtambua yule ambaye angeweza kuwa ndiye Imam, hata kama hawakumuamini. Hali ya watu kumsubiri mtu yeyote awaye yule ili awaongoze, kwa mtazamo wa watawala ulichukuliwa kuwa ni tishio kubwa kwa maslahi ya wafalme ambao wao aliupora utawala uliokuwa unapaswa kuwa ni wa Waislamu.

Baada ya kufanya upelelezi mbalimbali na uchunguzi iliwathibitikia kwamba tishio lingetokea kutoka kwa mtu atakayezaliwa kutoka katika nyumba ya Mtume (s.a.w.w.), aidha, waligundua kwamba kulikuwa na harakati za dhati hasa za watu katika kumfuata.

Kutokana na upelelezi wao huo unaoendelea, waliweza kuthibitisha lengo halisi. Hivyo walimfunga Imam Ali al Hadi (a.s) babu yake Imam al-Mahdi (a.s) na Imam Hasan al-Askari (as) baba yake Imam Al-Mahid. Hata hivyo, Allah (s.w.t) aliwaficha kuzaliwa kwa Imam mwenye kusubiriwa, kama vile ambavyo aliwaficha kwa Nabii Musa (a.s).

Katika kipindi hiki cha kuendelea kufuatia, ilikuwa ni kwa wale Mashi’a ambao waliifahamu siri hii wakalificha kabisa jina la Imam, ama sivyo maisha yake yangekuwa hatarini zaidi. Watawala wa wakati huo walijua kwamba Imam atatokea kutokana na watu wa nyumba hii, lakini hawakuweza kwa usahihi kuamua kwamba atakuwa ni nani.

Kwa maneno mengine, walijua kwamba kuna mtu ambaye anatarajiwa na watu kwamba atazaliwa, na iliwezekana kwamba wangeweza kumtangaza kwamba ndiye mwokozi na kiongozi wa Waislamu kutokana na amri ya Mtume (s.a.w.w).

Kufichwa kwa siri hii ilikuwa hakuna budi kwa vitisho hivi halisi. Uwekaji wa usiri huu na kufichwa huku kuliendelea kutoka kwenye ghaibu ya kimaajabu ya Imam mpaka kutokeza kwa waumini kumekuwa na uhakika kwamba hakuna madhara yatakayompata, kiasi kwamba suala la ulinzi wake linakuwa kitu kilichofichika sana.

Akatoweka machoni pa watu katika namna ambayo hakuna yeyote ambaye angeweza kumfikia.

Imefahamika kwa Mashi’a kuanzia sasa na kuendelea kutafuta sababu za kutoweka kwake, ambako kumekuwa kwa muda mrefu… katika wakati huu, suala la mwokozi kidogo kidogo likaanza kufifia, na likawa ni matumaini tu yaliyomo mioyoni mwa watu. Ashi’a wakagundua kwamba ghaiba ya Imam Mahdi (a.s) ya namna hii ni kutokana na ukosefu wa watu wanaomfuata.

Kama Imam alitaka kuutekeleza Mpango wake mkubwa ambao anao, basi angehitaji wafuasi. Wafuasi wake lazima wawe na tabia na sifa maalumu ambazo zingewawezesha kuutekeleza Mpango kwa uaminifu wa kiwango cha juu kabisa. Ni Mpango wa muda mrefu na ni mgumu kabisa, na suala hilo lahitaji watu imara kabisa, waadilifu kweli kweli.

Inasemekana kuwa, moja ya sababu za kutoonekana kwake ni watu kutofikia hali ya kuwa tayari katika kiwango kinachohitajika ili kuhimili na kuivumilia Serikali yake, ambayo ni ya haki tupu.

Hivyo, ni muhimu kuandaa mazingira yanayofaa kwa ajili ya kuja kwake, na kuyaweka mataifa katika hali ya kuwa kweli wanaihitaji Serikali hiyo.

Vipengele vyote hivi vikafanya utaratibu wa kutangaza kuhusu Imam na kuwajulisha watu haiba na ukweli wake kuwa ni suala lenye kuhitajika sana na muhimu kabisa, kwa sababu kurejesha matumaini mioyoni mwa watu kunahitaji uthibitisho wa kweli ambao hauwezi kupatikana kwa maelezo ya juu juu na visa vya kufikirika tu.

Kwa hiyo, wanachuoni walianza kutafuta hadithi zinazomhusu Mahdi (a.s) anayengojewa na mpango wake. Walizikusanya na wakaanza kuzisambaza kwa watu, na hivyo likawa suala lililotangazika na kuaminiwa na wale ambao wanazifahamu hadithi nyingi ambazo zimesimuliwa na Mtume na Ahlul Bayt (a. s).

Kama ambavyo ulivyo Mpango wa Imam Mahdi (a.t.f.s) ni Uislamu, Malengo yake vilevile ni malengo ya Uislam, na hapa ingefaa kuyaweka wazi malengo haya:

Hapana shaka kwamba Uislamu ni Mpango na sheria ya Allah (s.w.t). Allah (s.w.t) amewaumba wanadamu ili wawe na furaha, na kuufikia kamilifu wa furaha kubwa kabisa katika maisha yao yote.

Hivyo vipi furaha hii inaweza kufikiwa na ni utaratibu upi katika Uislamu ufuatwe ili kuweza kuipata furaha hii?

Furaha ya mwanadamu ipo katika kuufikia ukamilifu wa daraja la juu kabisa. Ukamilifu huu umekusudiwa na kutaraijwa katika maisha yao yote, na chochote kile zaidi ya hilo hakina maana yoyote. Binadamu atahusiana na chochote ambacho kinamwakilisha yeye katika ukamilifu huu, au iwe ni njia ya kupitia ili kuupata ukamilifu huo.

Kwa upande mwingine mwanadamu huyu hukikataa chochote kile ambacho huwa ni kikwazo kwake katika njia ya kuweza kuufikia ukamilifu huu. Hivyo chochote kile ambacho kinakuwa ni kikwazo, bila kujali kitakuwa karibu kiasi gani, kitachukiwa na kukataliwa.

Lengo kubwa la Uislamu ni kuuelezea ukamilifu huu na kuufichua uwongo na upotofu uliofikia kiwango cha juu kabisa. Binadamu wanaweza kuwa na uhusiano kama vile ambavyo watu wengi walivyo, na vitu ambavyo wanadhani ni vya ukamilifu. Hivyo fikra za mtu huyu lazima zielekezwe na kuongozwa ili kuufikia ukamilifu halisi.

Sehemu muhimu sana ya mafunzo ya Uislamu yanazunguka katika uwanja huu, na hicho ndicho sisi tunakiita ilmu ya kiroho (ma’rifa) na kutam- bua (wa’i). Uislamu haujaridhika na kuelezea ukweli tu, bali huweka wazi sababu za upotofu huu na jinsi watu wanavyoifikia hali hii mbaya kabisa.

Uislamu unatoa mpango wa kuwaokoa na kuwalinda kutokana na uongo huu, wakati karibu wanadamu wote kwa muda wote wamepotoshwa na fikra hizi potofu, si hivyo tu bali unautukuza mpango wake kwa kutoa miongozo ya jinsi ya kuufikia ukamilifu halisi na kuulinda.

Ni kweli kwamba mwanadamu kama mtu binafsi yupo katikati ya mpango huu, na kwamba kila mwanadamu anawajibika kwa ajili yake mwenyewe. Hata hivyo, jamii na watu wanaomzunguuka kwa kiasi fulani ni sehemu yake, kama ambavyo kuna msemo usemao kwamba, “Jamii ni kipengele kimoja cha mtu.” Au kipengele muhimu cha shakhsiya yake.

Hivyo kama mtu anawaacha wengine na hawajali basi atashindwa na atapata taabu sana. Anaweza hata asipate ukamilifu unaotakiwa na furaha kubwa ya kweli.

Jamii si idadi ya watu tu, au watu ambao tunahusiana nao tu, bali ni mfumo wa kiutawala, desturi na sheria, mfumo ambao jamii imo ndani yake, na kwa msingi huu, mahusiano yanajengwa na watu na watu wanashirikiana.

Mtawala au kiongozi wa jamii hufanya kazi ya kuweka na kulinda mfumo huu. Kwa sababu mfumo huhakikisha kwamba maslahi yake yanalindwa, yeye atakuwa ndiye mlinzi mkubwa kabisa. Atakuwa yupo tayari kuuwa na kuyatokomeza makundi ya watu endapo atawatilia shaka kwamba wanakwenda kinyume na mfumo wake!

Mtawala huyo, ambaye huitwa dhalimu atawaongoza wale wote ambao huukubali mfumo wake motoni kwenye Adhabu ya Akhera. Dhalimu ni adui wa Allah (s.w.t) na humwakilisha Shetani hapa duniani.

Watu hawawezi kujitenga na athari za mfumo huu wa utawala ambao wanaishi humo, na kuukubali mfumo wa maisha na kuishi kulingana na mfumo huo, maisha yao yatabadilika na kuwa maisha ya kidhalimu, maisha yenye uadui dhidi ya Allah (s.w.t ). Ni juu yao, na ni muhimu sana kuukataa mfumo huu. Kukataa huanzia ndani ya moyo, akilini na katika imani.

Katika hali fulani wakati mwingine haiwezekani kufanya chochote kwa kutokana na kuikataa hali hii; hata hivyo, kukataa kwa moyo kwabakia kuwa sehemu muhimu ili kumfungulia mtu milango iwe wazi mbele yake, na kumwekea njia iliyo wazi ili aweze kuufikia ukweli.

Endapo watu hawataweza kurekebisha hali hii, hata kama ni kwa kiwango cha imani na kwa moyoni, basi hawataweza kufanikiwa katika kurekebisha sehemu nyingine za shakhsia zao, na hivyo vikwazo vitabaki, vya kuwazuia wasiufikie ukamilifu.

Kwa hiyo, wanayo dhima kubwa kwa jamii, kwa maana ya kwamba dhima juu ya mfumo, na dhima juu ya wawakilishi wake wanaotenda kazi zao ili kuulinda mfumo huo.

Mfumo wa kidhalimu ambao upo kwa ajili ya kulinda maslahi ya mtawala – ama mtawala huyu awe mtu mmoja au kikundi cha watawala – ni mfumo wa kikatili, ambao huwadhulumu watu haki zao na kwa namna hii unawatawala watu na kuwafanya watumwa kwa kutumia hila mbalimbali.

Si kama ulivyokuwa utumwa wa hapo siku za nyuma huko Marekani kwa Waafrika; bali umebadilishwa na kuwa wa kisasa zaidi, uliojificha zaidi na wenye uovu zaidi.

Mfumo wa kisasa wa Utumwa upo katika kuhodhi uchumi, ambapo mtumwa anaonekana ana uhuru wa kufanya chochote apendacho, lakini ukweli ni kwamba hali yake ya kiuchumi imedhibitiwa barabara kabisa, na vile vile amedhibitiwa barabara kabisa na mfumo unaotawala uchumi.

Anachokula, asome wapi na asome nini, vipi apate pesa na vipi azitumie, afikirie vipi, ampigie kura kumchagua nani, yote haya yamepangwa kabla kwa makusudi kwa ajili yake, na yote haya ni kwa kisingizio cha uhuru na uhuru wa kuchagua.

Watu wachache sana wanaweza kuimaizi hali hii ya sasa ya utumwa. Dhalimu haishii hapa, kwani atazitafuta kanuni za ukweli na za haki na wale ambao wangeweza kuzitetea kutishia maslahi yake. Kwa hiyo ata- jaribu kuzivunjavunja hizi kanuni, hii ndio kusema kwamba atayaondoa yale katika yaliyobaki katika kulinda utu na furaha ya mwanadamu, na kuwaangamiza wale wanautetea ukweli.

Haiwezekani kumpata mtawala dhalimu anayeukubali ukweli. Ni upuuzi mtupu kudhani kwamba mtawala dhalimu angeweza kuishi kwa kufuata kanuni za maisha ya kibinadamu. Ni ujinga mkubwa kabisa na ni kiwango cha juu kabisa cha kukosa mazingatio!

Ni Wapi Yalipo Maadili Ya Hali Ya Juu Ya Mwanadamu, Na Ni Nani Ambaye Huudhihirisha Ukweli,
Na Kuwafanya Watu Kuielewa Bayana Hali Yao Waliyo Nayo?

Kwa urahisi mno kabisa ni Uislamu ambao unaweza kufanya hivyo; dini ya Allah (s.w.t) na ujumbe Wake ambao umekuja kuwaokoa wanaodhulumiwa na wanaoteswa, wanaofadhaishwa na wanaonyonywa. Maadili yote na ukweli utapatikana kutokana na huduma ya wale ambao wamejitolea wenyewe kutoka kwenye minyororo ya mtawala dhalimu na mfumo wake.

Mtawala Dhalimu Anachofanya Tu Ni Kuufunika Na Kuuficha Ukweli

Mtawala dhalimu anachofanya ni kuharibu tu maadili (hayo) ya hali ya juu na kuwapotosha wafuasi wake. Katika kivuli cha mazingira haya inawezekana kabisa kwa mtu kuungana na chanzo cha Nuru, Uongozi, Maadili na Ukweli. Mtu kwanza na kabisa huhitaji kuuacha huu mfumo hata kama ni kwa moyoni tu. Hata hivyo, uhuru kamili ndiyo njia pekee ya kupata wokovu wa mwanadamu.

Wamekosea wale wanaodhani kwamba unyoofu wa hali ya juu na maadili ya kiroho ya Kiislamu yanapatikana kwa wale ambao hujisalimisha mbele ya madhalimu na kuwakubali.

Wanajidanganya wale ambao hufikiria kwamba Swala na amali nyingine kubwa kubwa za kiibada zitakuwa na manufaa wakiwa chini ya utawala wa wakandamizaji.

Kwa hiyo tunaweza tukayatambua malengo ya Uislamu: Lengo kuu kabisa ni kuipata furaha ya mwanadamu.

Na furaha hii imo katika kupata aina zote za ukamilifu. Ili kulifikia lengo hili vikwazo vyote lazima viondoshwe Kikwazo kikubwa kabisa na cha hatari zaidi ni kuwadhulumu watu.

Mtawala dhalimu ni yule ambaye anaulinda mfumo wa kidhalimu na kuuimarisha, na zaidi ya hapo huwaongoza watu wake katika kuifanya dhulma hiyo.

Tunapoitumia nadharia hii iliyo dhahiri na rahisi katika kuupata ukweli ndiyo tunakuja kuyafahamu kwa wepesi malengo ya Imamu Mahdi (a.s). Pia tunakuja kujua siri ya kutoafikiana kati ya wale wanaoamini juu ya malengo yake.

Baadhi ya wanaomuamini hutilia maanani kipengele cha kiroho na unyofu katika kungojea kurejea kwake, na humchukulia yeye kuwa ni kiongozi wa kiroho ambaye atawachukua na kuwafikisha katika kilele cha ukamilifu wa kiroho.

Wengine huangalia juu ya jukumu lake kubwa katika kuwafundisha watu na kueneza maarifa na hekima ulimwenguni. Wengine humuona kama ni kiongozi mkubwa wa majeshi ambayo yataangamiza viti vya enzi vya tawala dhalimu na mifumo ya kidhalimu na ubadhirifu.

Wote hawa wapo sahihi, hata hivyo mawazo yao lazima yaongozwe ili kuweka wazi picha halisi. Upinzani dhidi ya dhulma ni hatua ya mwanzo kuufikia ukamilifu wa kiroho, uongozi na imani. Ni katika imani na ucha- ji (Mungu), maarifa yatazidi kukua na matawi yake mazuri yataendelea kumea.

Si ujumbe wa mapinduzi tu ambao Imam Al-Mahdi (a.s) ameubeba, bali anataka kuitoharisha ardhi kutokana na madhalimu na kuwazuia wasifanye ubadhirifu na kuuvuruga ulimwengu, kwa lengo la kupata mazingira yanayotakiwa ili kuwakamilisha wanadamu katika mambo yote ili waweze kuipata furaha ambayo wanaitafuta.

Maarifa haya yana umuhimu sana kwa maisha yetu… Kwa nini? Kwa sababu tunaamini kwamba Imam (a.s) tangu kilipoanza kipindi cha ghaiba yake alikuwa akiandaa mazingira yanayofaa kwa ajili ya kipindi atakapokuja kurejea na kufanya maandalizi ya kuumalizia Mpango wake ambao ulikuwa ndiyo ndoto ya Mitume (a.s) tangu hapo mwanzo wa wakati.

Je, Na Hii Itakuwaje?

Ni rahisi sana, maadam tumekwisha yafahamu malengo yake, basi tunaweza kuwajua wale waendao sawa sawa kufuatana na mpango wake huu mtukufu.

Maadam tunataka tuwe miongoni mwa wale ambao wanaandaa mazingira mazuri ya kurejea kwake kuliko na baraka na tuna imani juu ya umuhimu wa kumsaidia, basi hakika tutaungana na msafara wa wale ambao wanamuandalia arejee na hatutaingia katika mtego wa wanafiki na waongo.

Angalia jinsi gani ambavyo hisia zetu juu ya malengo ya Uislamu zinatuleta moja kwa moja kufika mahali ambapo tunapaswa tuwepo.

Kama tunamjua adui mkubwa kabisa na mwenye hatari zaidi ni mtawala dhalimu, hapo ndipo tutaweza kujua maadui zake na wale ambao watakuwa ni wasaidizi wa Imam na wanyoofu.

Hivi ndivyo jinsi tunavyojua hatua ya kwanza ya kumfuata Imam, na kama tutachukua hatua hii tutakuwa ni miongoni mwa wale ambao kwa hakika wanamngojea Imam, wakisubiri wokovu wetu wa kweli.

Wasioamini Kuwepo Kwa Imam Al - Mahdi (A.S)

Tunafahamu kwamba wale ambao hawauamini ukweli, kwa vyovyote uwavyo, wapo katika makundi mawili:

Kundi la kwanza: Ni kinzani na lenye kukanusha, wanaufahamu ukweli, lakini hawataki kuukubali kwa sababu utawaletea hasara kwenye maslahi na manufaa yao.

Kundi hili limekuwepo siku zote na bado lipo. Kukabiliana na watu wa aina hii kwa kutumia hoja na ushawishi hauna faida yoyote; bali ingelikuwa si busara kufikiria kuwa hoja hizo zingeweza kuleta matokeo mazuri.

Kundi la pili: Hukanusha ukweli kwa sababu wana mashaka na wamedan- ganyika, wakidhani uongo ndio ukweli, ambao huwazuia wao kutoufikia kweli. Makundi yote haya mawili hayaamini kuwepo kwa Imam Al–Mahdi (a.s). Baadhi ya watu wanafahamu kutokana na hadithi za Mtume (s.a.w.w.) zilizosimuliwa kwao kwamba atakuja kuishi mjukuu wa Mtume (s.a.w.w) na jina lake ni Imam Al–Mahdi (a.s), na kwamba atatokea katika kipindi cha mwisho wa dunia ili kuujaza ulimwengu usawa na haki baada ya kuwa umeshajazwa dhuluma na uonevu.

Lakini watu hawa hufikiri kwamba kwa kuuonyesha ukweli huu utavuta nadhari ya watu kuwaelekea wasaidizi wa kweli wa Imam, na kusababisha wao kuwaacha. Kwa hiyo, huzificha hadithi hizi na hawazisambazi kwa wafuasi wao.

Kundi jingine la watu hudai kwamba wanaamini kuwepo kwa Imam (a.s) lakini wanakataa kabisa kuzungumzia wazi wazi juu ya jukumu lake na malengo yake, kwa sababu hii itawaongoza watu waweze kuwa wasaidizi wake wa kweli, kitu ambacho kitaharibu maslahi yao, kwani wao hupata fedha na manufaa mengine mengi kutoka kwa wafuasi wao. Hivyo kama wafuasi wale wakijua watu wanyoofu ni akina nani, hawatawapa tena pesa zao na watawapuuza.

Bila shaka baadhi ya wanaopinga hawaamini kuwepo kwa Imam (a.s) kwa sababu hawaamini baadhi ya itikadi, kanuni na mambo ya kweli ambayo kwa kweli ni utangulizi katika kuamini kuwepo kwake, tunamuomba Allah (s.w.t) afanye haraka kurejea kwake.

Watu hawa kamwe hawazungumzi habari zake, kwa vile kutokuwa kwao na imani juu ya mambo ya kweli ya kimsingi huwazuia wao katika njia hii moja kwa moja.

Imani ya ukaidi ina miundo na aina mbalimbali, na ina viwango mbalimbali; baadhi ya hivi vimejificha kuliko vingine. Hata hivyo, kinachovihusisha hivi viwango na aina zake ni mapenzi ya maisha ya dunia hii na kutanguliza mbele maslahi binafsi kuliko kuufuata ukweli.

Ama kwa kundi la pili la wasioamini, kwa sababu ya hadaa na fikra wali- zonazo, huona kwamba kumuamini Imam Al-Mahdi (a.s) ni upotofu.

Uongo mwingi huchangia kuifikia hali hii ya kutoamini na kutokukubali. Kabla hatujautaja uongo huu ni lazima tutambue ukweli kwamba tunaposhughulikia suala la Imam Mahdi (a.s) mbali kabisa na kanuni za Uislam kutaufanya utafiti kuwa mgumu, kama sio kutowezekana kabisa.

Kitu cha kwanza na muhimu kabisa kwenye kanuni hizi ni: Imani juu ya Allah (s.w.t) na kudra Zake kwamba hawezi kushindwa. Yeye, Mtukufu, ni Muweza wa kufanya kitu chochote.

Maadam suala la Imam Mahdi (a.s) linatokana na Mwenyezi Mungu, Allah (s.w.t), hivyo basi maisha yake marefu hapa duniani na yote yale ambayo yanamhusu yapo mikononi mwa Allah.

Kwa hiyo, kutokukubali juu ya kuwepo kwake hai, maisha yake kuwa marefu, ama kuweza kunusurika na kuishi katika kipindi hiki chote kirefu ambacho kinazidi zaidi ya miaka elfu moja, inaashiria kukataa na kutozijua Nguvu za Mwenyezi Mungu.

Kanuni nyingine ya Uislamu ambayo ni muhimu katika kulifahamu suala la Imam Al–Mahdi (a.s) na kulifanyia utafiti kwa usahihi ni: Imani juu ya Mtume wa mwisho, Umaasum wake na kazi yake ambayo inajidhihirisha yenyewe katika maisha yake, tabia yake na hadithi.

Hii inakusudia kumuiga yeye, na kukichukulia kila kitu akisemacho kwamba ni kweli, kwa sababu huyu ni Mtume Mkubwa (Amani iwe juu yake na Aali zake) na anao wajibu ulio muhimu katika kuteuliwa kwa Imam Al–Mahdi (a.s).

Kwa hiyo, tukienda moja kwa moja kwenye suala la anayengojewa Imam Al–Mahdi (a.s) bila ya kuzizingatia kanuni zilizotajwa hapo juu, ama kuzitegemea, yawezekana tusifikie mwisho wowote.

Wale wanaouamini Uislamu na Qur’ani, wanafahamu vyema kwamba hakuna jambo lolote geni kwa yale yanayoelezewa juu ya Imam Al-Mahdi (a.s), kama vile maisha yake marefu.

Kwa nini iwe hivyo? Kwa sababu Qur’ani ina mifano mingi kama hiyo, na wanachuoni wameyasoma mno mambo hayo katika vitabu vingi na wameweka mada hasa juu ya Imam Mahdi (a.s) kama ifuatavyo:

Kuwepo hai kwa Imam Mahdi (a.s), mwana wa Imam Al-Askari [ambaye ndiye mwana wa Imam Al-Hadi, mwana wa Imam Al-Jawad, mwana wa Imam Al-Ridha, mwana wa Imam Al-Kadhim, mwana wa Imam Al-Sadiq, mwana wa Imam Al-Baqir, mwana wa Imam Al–Sajjad, mwana wa Imam Al–Husein, mwana wa Imam ‘Ali ibn Abi Talib (Amani Iwe Juu Yao Wote), ambao ni warithi wa Mtume wa Allah (s.w.t), (kama ambavyo Mtume amesisitiza katika moja ya ujumbe wake) inathibitishwa kwa namna mbili; kupitia mapokezi na hoja za kiakili.

Katika mapokezi, zipo hadithi sahihi nyingi mno ambazo zinatoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w) na vipo vitabu vingi ambavyo humo mna hadithi ambazo zinathibitisha kuwepo kwa Imam.

Kwa hoja za kiakili, tunaweza kuthibitisha umuhimu wa kuwepo kwake, kwa kutumia hoja mbalimbali ambazo zote zimejengwa na msingi wa Imani juu ya Uwezo wa Allah, Huruma Yake, Hekima na Rehema ya Allah (s.w.t). Inasemekana kwamba imani juu ya Muumba na Sifa Zake thabiti bila shaka zitatufikisha kuamini juu ya Imam Mahdi (a.s).

Kinyume cha haya, wapimzani wa hoja hii – kwamba ni hoja ya kuwepo kwa Imam – inakuwa haiwezikani kupambanua kinachotokea Ulimwenguni na katika maisha ya watu, ingawa wanadai kumuamini Allah (s.w.t) na sifa Zake.

Kama tunavyosoma katika dua, Imam Mahdi (a.s) ni Rehema ya Mwenyezi Mungu ambayo kwamba Allah (s.w.t) ameileta Mwenyewe, na Ukarimu Wake ambao hauwezi kutenganishwa na Utukufu Wake na Uangalizi wa Ulimwengu huu. Pia tunawaeleza: Endapo Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa Rehema na Mwingi wa Hekima, na ameahidi kwa waja wake kwamba wachamungu wataurithi Ulimwengu huu, basi iwapi hiyo Rehema, Ukarimu na Hekima ya Allah (s.w.t) kutokana na hali ambayo imekuwa ikitokea!

Vipi Tutaweza Kuwa Na Uhusiano Wa Karibu Zaidi Na Imam?

Kama maarifa ya kumuelewa Imam (a.s) yatakuwa yameimarika kwa dhati ndani ya nafsi; hutokea kumfahamu kwa undani zaidi; na hamu ya kutaka kunufaika kutoka kwake na kutaka kuungana naye inakuwa kubwa zaidi.

Kama mtu huyu ataishuhudia hali halisi ya jamii ilivyo na kuja kuyajua matukio yanayotokea ulimwenguni na ukandamizaji na ubadhirifu ambao unafanyika, basi hamu hii itageuka kuwa kubwa mno na kuona huruma.

Yote haya ni kwa sababu yeyote amjuaye Imam na kumuamini kwa moyo wake na nafsi yake, haiwezekani aone watu wakiteseka na akaona si chochote si lolote!!

Imani huamsha asili ya mwanadamu, na vilevile kuwa na mapenzi kwa wengine na humfanya mtu mchamungu awe anawajali watu wengine na kuwa na moyo wa huruma. Anapoona hali ya kutisha ya ukandamizaji, mateso, majonzi, na huzuni ambazo zinavunja moyo na kuiua roho, basi mara moja ataelekea kwenye mambo mawili:

Kwanza: Ataulizia apate kujua ni nani anayesababisha majonzi yote haya.
Pili: Atautafuta wokovu, au mwokozi.

Hivyo, maadam imani ya mtu huyu ina utambuzi fika wa Imam na dhima yake katika maisha ya watu, moja kwa moja atamfuata mwokozi wa kweli ambaye ndiye aliye na mpango wa mageuzi ya ulimwengu na kuzitokomezea mbali aina zote za ukandamizaji na ubadhirifu. Kwa hiyo, hapa kuna nukta mbili za kuziangalia:

Kwanza: Kumtambua Imam.
Pili: Kiwango cha maarifa juu ya ulimwengu na jamii tuliyomo.
Haya mawili kwa pamoja humfanya mtu ageuke kwa kina kumwelekea Imam Al–Mahdi. Kama mtu mwaminifu anamtambua Imam kwa Utukufu wake, Umuhimu wake, na Hadhi yake aliyonayo mbele ya Allah (s.w.t) bila ya kupata kufahamu majonzi yaliyopo hapa ulimwenguni, basi inawezekana kwamba hamu yake kubwa ya kutaka kumfuata Imam ikawa ina upungufu na yenye kikomo.

Kwa upande mwingine, kama atajiingiza katika madhila ya wanadamu, shida za jamii, na moyo wake ukajawa na uchungu na simanzi kwa yale yanayotendeka, basi, hali yake kwa jinsi alivyo na katika kumtafuta ili kumfuata Imam kutakuwa na nguvu. Jina la Imam Al–Zaman (Imamu wa zama hii yetu) limeambatanishwa na dhima yake kubwa mno.

Ghaiba yake haikutokea katika karne zote hizi hivi hivi tu, bali ilikuwa ni kwa ajili ya kumuokoa mwanadamu. Hivyo kwa yule ambaye atauweka moyo wake uhisi taabu za ulimwengu, atakuwa karibu zaidi na Imam.

Je, Kuna Kitu Ambacho Mtu Anaweza Kukifanya?

Bila shaka, hisia za ndani peke yake hazitoshi kwa maisha haya, kwani zinaweza kutoweka. Kwa hakika, imani yoyote bila ya kujali kwamba namna gani imejijenga moyoni na akilini, kama haikufanyiwa kazi inaweza kusahauliwa kwa urahisi ama kukataliwa. Ni vitendo tu na harakati ambazo zinatokana na imani ndizo hujikita moyoni na kuhifadhika mwongozo wake.

Fikiria juu ya mtu aliyeuamini utukufu wa Imam Al–Mahdi (a.s) na daraja aliyonayo mbele ya Allah (s.w.t), lakini kwa upande mwingine akawa anajihusisha katika shughuli na vitendo vya wakandamizaji, na akawasaidia katika kutekeleza mipango yao, ambayo inaelekezwa katika kuwanyonya wanyonge pamoja na rasilimali zao.

Aidha, maslahi yake yakawa yana uhusiano na maslahi yao, kwani maisha yake na kipato chake kinatoka kwao. Je, tunaweza kumtegemea kwamba yeye awe anampenda, au mwenye kumngojea Imam al–Zaman, mwenye kuisambaza haki?

Kila namna ya mahusiano na wakandamizaji yanapunguza imani moyoni, na hali hii huendelea hadi kufikia kuwa mapenzi na imani kwa Imam hufutika vyote kabisa kwa pamoja. Kwa hiyo, kitu muhimu kabisa baada ya kumjua Imam ni kukiacha chochote kile ambacho kinaweza kuidhoofisha athari ya maarifa haya ya kumtambua Imam kwa mtu binafsi.

Hivyo, inawezekana kufanya baadhi ya mambo ili kuiimarisha na kuuongeza zaidi uhusiano na Imam, baadhi yake ni:

1. Kuwa Imara Katika Kumfuata Yeye:

Hii ina maana ya kujiwajibisha siku zote kuwa katika mwongozo wake na mwongozo wa wale ambao humsaidia, kufuata utaratibu wake, na kuweka mazingira yanayofaa kwa ajili ya kurejea kwake.

Imepokelewa kutoka kwa Imam Muhammad Al-Baqir (a.s), amesema kwamba: “Utakuja fika wakati kwa watu ambapo Imam wao atatoweka machoni mwao, baraka ziwe juu ya wale ambao watakuwa imara katika kutufuata sisi katika wakati huo. Malipo ya kiwango cha chini kabisa ambayo watayapata ni kwamba Allah (s.w.t) atawaita na kusema: “Enyi waja wangu, mmeiamini siri yangu, na mmeamini katika yasiyoonekana, hivyo shuhudieni malipo toka Kwangu.

Enyi waja wangu hakika nayapokea kutoka kwenu, na kwenu ninatoa msamaha, na ninawasamehe. Na kwa ajili yenu ninainyesha mvua kwa ajili ya waja wangu, na ninawaondolea mabalaa. Kama isingelikuwa ni ninyi, ningeliwashushia wao adhabu yangu.”1

Yeyote ambaye yupo imara katika kuifuata njia ya Ahlul Bayt (a.s) ndiye huyo ambaye amefungamana na mpango wao wa kuleta mageuzi ulimwenguni na huuchukulia kuwa huo ndiyo mpango wa maisha yake.

2. Kuepukana Na Maadui Zake:

Kuepukana kwa kweli ni kuachana nao kabisa na kukabiliana nao. Uadui na maadui wa Imam Al–Zaman huimarisha uhusiano naye, na humfanya mtu kuwa tayari katika kuufuata mwongozo wa Imam, kuepukana (bara’ah) na maadui wa mtu ni sawa na kumfuata (wilayah), na bila ya hivyo, kumfuata hakutakuwa kwa kweli au kwa hakika.

Mtume (s.a.w.w) amesema: “Ewe Ali! Naapa kwa yule ambaye amenituma mimi na utume na amenichagua mimi miongoni mwa viumbe vyote. Kama Mchamungu amefanya ibada kwa ajili ya Allah (s.w.t) kwa miaka elfu, hataweza kukubaliwa mpaka amekufuata wewe (wilayah) na maimamu kutokana na kizazi chako, na kukufuata wewe hakutakubaliwa bila ya kuepukana na maadui wa maimamu wa kizazi chako.

Hivi ndivyo Jibrili (Malaika Jibril) alivyonifahamisha Mimi. Ni juu ya mtu ama kuwa mwenye kukataa ama kuwa mwenye kuamini.”2

Kama mtu mwaminifu hawezi kusema waziwazi kuacha na kuepuka kwake hivyo itabidi chuki yake iwe kwa maadui wa Imam ili kuiweka nafsi iwe katika hali ya kuwa tayari.

Kusahau kutokuwa na chuki na kutoihisi kuendelea kuwepo kwake, maana yake mwisho wake ni kutoweka kwa Wilaya kutoka katika nafsi ya mtu. Kwa hiyo, Imam al–Sadiq (a.s) alimuusia mtu aliyemtembelea nyumbani akimtajia kasoro yake kwa kutokufanya chochote dhidi ya maadui, kwa kusema:

“Baba yangu aliniambia kwamba baba yake alimuambia kwamba babu yake alimuambia kwamba Mtume wa Allah (s.w.t) alisema: ‘Yeyote yule ambaye amedhoofu na hawezi kutusaidia sisi, Ahlul Bayt, lakini bado akawalaani maadui zetu katika nyakati zake za ibada kwa siri akiwa peke yake, Allah (s.w.t) ataifanya sauti yake iwafikie Malaika wote, kuanzia duniani hadi kwenye kiti cha enzi.

Wakati wowote ambao mtu huyu anawalaani maadui zetu malaika pia humsaidia katika kuwalaani wakifanya hivyo mara mbili yake, hivyo hivyo!

Kisha watasema: Ewe Allah (s.w.t) mbariki mja wako ambaye amefanya kile kilicho katika upeo wa uwezo wake, na kama angekuwa na uwezo wa kufanya zaidi ya hapo angefanya. Ndipo hapo sauti kutoka kwa Allah (s.w.t) itakuja, ikisema: Nimeipokea dua yako na nimelisikia ombi lako. Nimeibariki roho yake miongoni mwa roho na nimemfanya yeye kuwa kwangu Mimi miongoni mwa watu walioteuliwa na wenye upendeleo.”3

Pia imepokelewa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w), akisema: “Furaha kubwa sana ipo kwa wale watakaomfikia Al-Qaim na kumfuata yeye katika kipindi cha ghaiba yake kabla ya kuonekana kwake tena. Wanaowafuata watu watukufu wanaomwakilisha, na wanaoonesha chuki dhidi ya maadui zake. Wao ni marafiki zangu na watu ambao nitawapenda, na ni watu wenye thamani kubwa sana katika umati wangu katika Siku ya Hukumu”.4

3. Kuwajibika Kwenye Sheria Za Kiislamu (Shari’ah) Katika Mambo Yote Ya Maisha:

Lazima tusisahau kwamba wakati Imam atakapojitokeza, ataifanya sheria ya dini kama ndiyo sheria inayofuatwa katika maisha ya mwanadamu na kwa kuiongoza jamii yote ulimwenguni.

Ni dhahiri kwamba wale wanaofuata Shari’ah, katika kila kipengele cha maisha yao, kabla ya kujitokeza kwake kulikobarikiwa, watakuwa tayari zaidi kukubali hii sheria kuliko wengine.

Watalifanya suala hili (la kufuata sheria za Mungu kama sheria ya kawaida) kuwa kubwa kabisa kama mafanikio ya Imam Al–Mahdi (a.s), kufuatia utekelezaji wa haki ulimwenguni.

Kama tutazingatia hadithi ambazo zinataja sifa na tabia za watu wanaomsaidia Imam Al–Zaman na wale ambao wanatayarisha mazingira mazuri ili ajitokeze, tutaona kwamba sifa muhimu kabisa kati ya hizi ni uchamungu (taqwa), ambao maana yake ni kutekeleza sheria zote za Mwenyezi Mungu katika kila hatua ya maisha.

Mtume wa Allah (s.w.t), amesema: “Mwishoni mwa umma huu wataishi watu ambao watapata malipo sawa kabisa na wale waliokuwapo mwanzoni, wataamrisha mema na kukataza maovu, na kupigana dhidi ya watu wapotovu.”5

Kama ambavyo tunajua kuamrisha mema na kukataza maovu ni mambo mawili ambayo ni ya wajibu katika Uislamu, ambayo ndiyo yaliyokuwa sababu ya umma wa Muhammad (s.a.w.w.) kuwa bora kuliko umma nyingine. Allah (s.w.t), anasema:

كُنْتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنْكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ ۗ{110}

“Ninyinikundiboramliotolewakwaajiliyawatu,mnaamrishamema na mnakataza maovu, na mnamuamini Mwenyezi Mungu (s.w.t).” (Qur’ani,3:110).

Kuutekeleza wajibu huu wa kidini ni uthibitisho kwamba hakika mtu anafuata barabara mambo mengine ya wajibu ya dini na sheria. Imepokewa katika hadithi kwamba Imam al–Baqir (a.s), amesema: “Kuamrisha mema na kukataza maovu ni njia ya Mitume na ni mwenendo wa wachamungu, na ni kazi kubwa. Kwa namna hii, majukumu hutekelezwa, makundi ya watu huwa salama, biashara huwa za halali, dhuluma huondoshwa, na ulimwengu hujengwa, na utulivu huimarika.”6

Kuuacha wajibu huu utamfanya Imam awe mbali na sisi, na muda wake wa kujitokeza kuongezeka, kwa sababu wakati atakapojitokeza atahitaji watakaomsaidia ambao wanaona wanao wajibu wa kuubadili ulimwwengu, kuugeuza na kutokomeza ubadhirifu ndani yake. Amirul Muuminin Imam Ali (a.s), amesema: “Msiache kuamrisha mema na kukataza maovu, ama sivyo Allah (s.w.t) atachagua watu miongoni mwenu kusimamia mambo yenu, mtaomba lakini maombi yenu hayatakubaliwa.”7

Imam Muhammad al–Baqir (a.s) amesema: “Laana ya Allah (s.w.t) kwa viumbe wake imetutoa sisi kuwa mbali nao.”8

4. Kuomba Du’a:

Kuomba Du’a kuna jukumu kubwa katika kuweka mawasiliano ya kiroho, na kuyaimarisha. Maombi huipa nafsi hisia muhimu ili iweze kuwa imara na kuendelea, hasa kama tutakuwa tunatambua kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameahidi kuyasikiliza maombi ya wale ambao wanamuomba kwa dhati. Kusikiliza hapa kuna maana kwamba Allah (s.w.t) atawafahamisha kwamba amewasikia na anajua ni yapi ambayo wamekuwa wakimuomba. Wakati muumin anapojua hili, ndipo hapo imani na kumuamini Allah itaongezeka.

Wakati waumini wakimuomba Mwenyezi Mungu juu ya Imam al–Zaman, na kuomba kuharakishwa kutokeza kwake, hii itaongeza hisia zao na imani kwamba Imam anaishi, yu hai na yupo. Hisia hii huwafanya wawe imara kuhusiana na kukaribia njia ya Imam.

Kumuomba Mwenyezi Mungu juu ya Imam Mahdi (a.s) ni muhimu sana, tunaona kwamba Maimamu wengine wa Ahlul Bayt (a.s) pia walikuwa wakimuomba Mwenyezi Mungu kwa ajili yake. Na hawakuridhika tu kwa kutuongoza sisi ili tumfuate Imam.
Maombi mengi muhimu yamesimuliwa kuwa yanatokana na wao.

Kama hili lingekusudia kitu kingine, basi lingekusudia kwanza kabisa, awali ya yote kwenye kazi kubwa mno ambayo Imam (a.s) atakuja kuimalizia, ambayo ndiyo ilikuwa lengo la Maimam wote Maasum (a. s) vilevile.

Baba yake Imam Mahdi (a.s) amesema: “Naapa kwa Allah (s.w.t) atakuwa ghaibu katika ghaiba ambayo hakuna hata mmoja ambaye atanusurika kutokana na uharibifu isipokuwa wale ambao Allah (s.w.t) amewaimar- ishia katika nyoyo zao imani ya Uimamu wake, na amewapa dua ya kuom- ba kuharakishwa kwa nusura yake (Imam)”9

Katika barua iliyoandikwa kwa hati ya mkono wake Imam Al-Mahdi (a.s) na kuwekwa saini yake imeandikwa: “Na ongezeni kuomba dua kwa ajili ya kuharakishwa kwa nusura (nusura ya Imam), kwani hiyo ni nusura yenu.”10

Zipo dua kwa idadi ya makumi kadhaa ambayo hulifanya suala hili la Imam Mahdi (a.s) kuwepo katika nafsi, na kuzifanya roho kuwa na tamaa kubwa ya kutaka kukutana naye, na kuyafanya mambo kulingana na mpan- go wake mkubwa. Tutazitaja baadhi ya hizi dua mwishoni mwa kitabu hiki. Ama kwa dua nyingine, zimo katika vitabu vya dua vinavyofahamika.

5. Kujiandaa Kwa Ajili Ya Kuja Kwake:

Hii ina maana kwamba tuendelee kutekeleza vitendo na mipango ambayo itakuwa ndiyo sababu ya kujitokeza kwake, na kuharakisha kujitokeza kwake. Yeyote ambaye anajua sababu za kughibu kwake atafahamu kwamba kujitokeza kwake kulikobarikiwa kwahitaji maandalizi na kuwapo katika hali ya utayari.

Watu wengine wataandaa mazingira ya kujitokeza kwake, na wengine watakuwa tayari kwa kujitokeza kwake. Hivyo msingi mkubwa ambao Imam atauhitajia kwa ajili ya kuleta mabadiliko ulimwenguni utakuwa upo tayari.

Imam Sayyid Ali Khamenei, mmoja kati ya watu muhimu sana kwa wakati huu kwa kuweka mazingira bora kwa Imam, anasema yafuatayo kwa wale wote ambao wanaelewa vyema maana ya wilayah:

“Wajibu wenu leo hii ni kuweka mazingira bora ambapo Imam Mahdi (a.s) atakuja na kuanza kazi yake kutokana na msingi uliokuwa tayari ambao umeshaandaliwa. Haiwezekani kuanza bila ya kuwepo na msingi wowote ule.

Jamii ambayo inaweza kukubali serikali ya anayengojewa, Imam Mahdi (a.s) - roho zetu ziwe sadaka kwa ajili yake - ni jamii ambayo ipo tayari na imejiandaa kwa jambo hilo. Vinginevyo, itakuwa na mwisho ule ule ambao umezipata jamii nyingi katika nyakati kama ilivyo katika historia.”

Anaendelea kusema:

“Kwa hiyo, inawezekana kuandaa mazingira. Kama mazingira haya yatazidi kuwa makubwa kwa uwezo wa Allah (s.w.t), ndipo hapo ambapo patakuwa pameandaliwa kwa ajili ya kujitokeza kwake Imam (a.s) (Baqiyatullah) - roho zetu ziwe mhanga kwa ajili yake - na kisha matakwa ambayo yalikuwa mioyoni mwa mwanadamu na Waislamu, yatapatikana.” (15 Shaaban, 1418 A.H.).

Hali hii ya kuwa tayari ndiyo maana halisi ya kungojea Faraja (Al Faraj). Yule ambaye hasa kweli anamngojea Imam Mahdi (a.s) ndiye ambaye ameweka mazingira bora na msingi unaofaa kwa ajili ya kujitokeza kwake.

Huwatafuta wale wengine wote ambao wanashughulika kwa kuipitia njia hii, na ya wale wote ambao wanasaidia kazi hii.
Zaidi ya hapo, muda wote ambao hutafuta njia hii bora ya kuandaa mazingira kwa ajili ya kujitokeza kwake, hajisikii kuwa ameridhika baada ya kuwa ameshafanikiwa katika sehemu ndogo tu ya kazi hii.

Amiir Muuminiin Imam Ali (a.s) amesema: “Matendo bora kabisa ambayo hukubaliwa na Allah (s.w.t) ni kungojea Faraja (faraja ya Imam).”11

Imam Musa al–Kadhim (a.s) amesema: “Ibada bora kabisa, baada ya kumjua na kumpenda Mwenyezi Mungu, ni kusubiri kuja kwa Faraja (Faraja ya Imam).”12

Imam al–Sadiq (a.s) anawasifia wale ambao kweli wanamngoja kwa kusema: “Furaha kamili (ni) kwa ajili ya wafuasi (Shi”a) wa Qaim ambao hungojea kuonekana kwake katika kipindi cha ghaiba yake, na wanamtii baada ya kutokeza kwake. Wao ni mawalii wa Allah (s.w.t) ambao kwao hawatakuwa na hofu wala kuhuzunika.”13

Hapana shaka kwamba maandalizi yanahitaji umoja na ushirikiano ili kusije kukatokea kutokuelewana na kutawanya nguvu.

Siku hizi, kama tutawaangalia watu wengi miongoni mwetu ambao wanadai kwamba wao ni wafuasi wa Imam (a.s) tunaona kwamba hawayajui masharti ambayo ni muhimu sana na sababu za kuja kuonekana kwake, ambako kunakubalika kwa pande zote, na kuachana kabisa na kujitenga. Utengano pia ni sababu kubwa ya kuchelewesha kuja kwa Imam na kurejea kwake kuliko na baraka.

Haimchukui mtu mwenye busara kufikiri sana kutambua kwamba njia bora ya kuudumisha umoja miongoni mwa wanaomsubiri Imam ni kuwa na uongozi imara wa mtazamo mmoja.

Sifa njema ni za Allah (s.w.t) ambaye ameuweka uongozi katika umma huu ambao ulimwengu wote unafahamu, na wote wanashuhudia kwamba unasimama imara dhidi ya maadui wa dini na ubinadamu.

6. Kuiadabisha Nafsi:

Wakati tunafahamu maana ya kuiadabisha nafsi tunatambua athari yake juu ya uhusiano wake na Imam al–Mahdi (a.s). Nafsi safi yenye tabia njema wakati wote ipo tayari kuukubali ukweli na matendo yake yakalingana na ukweli huo, tofauti na nafsi zilizo ovu hata kama zitakuwa na Imani sahihi.

Imepokewa kutoka kwa Imam Jafar al–Sadiq (a.s) amesema: “Yule ambaye amependezwa kuwa mmoja wa wafuasi wa wa al–Qaim, basi anapaswa akae akingojea, na matendo yake yawe ya uchamungu na tabia njema, wakati akingojea.

Basi kama atakufa na al–Qaim akatokeza (baada ya kifo chake) atapata malipo sawa sawa na yule ambaye amemuona al–Qaim, hivyo ajitahidi na asubiri.”14

Imam Khamene’i amesema: “Imani juu ya Imamuz-Zaman itakuwa ni kwa Mashi’a, kama watauelewa ukweli wake na kufanya kama wanavyopaswa, chanzo cha matokea ni nuru.

Imani hii pia itamuongoza kila Mwislamu na muumini na Shi’a kufanya jitihada kimawazo na kivitendo kuyalinda mahusiano yao na Imam kiroho na kiakili, na kusafisha nafsi zao katika namna ambayo itapendezwa na Imam wao Maasum.”

7. Kuhuzunika Na Kulia Kwa Ajili Ya Kughibu Kwake:

Tutaanza kwanza kwa kutaja kisa hiki chenye maana:

Sudair al–Sairafy, mfuasi wa Maimam (a.s) anasema kwamba: Siku moja bila ya kumpa taarifa kabla alifanya ziara ya kumtembelea Imam Jafar al–Sadiq (a.s) akiwa pamoja na al–Mufadhal ibn Umar, Abi Basiir, na Aban ibn Taghab, na walimuona akiwa amekaa chini kwenye mchanga katika namna ambayo si ya kawaida, akilia kama vile mama ambaye amefiwa na watoto wake wote. Uchungu ulionekana machoni usoni mwake na mashavu yake yalilowana kwa machozi, na alikuwa akisema:

“Ewe Maula, kughibu kwako kumeniondolea usingizi, kumekifinyanga kitanda changu, na kumeupokonya utulivu wa moyo wangu.
Ewe Maula, kughibu kwako kumefanya mateso yangu kuwa yenye mau- mivu ya milele.

Nahisi machozi yakinidondoka kutoka machoni mwangu, na udhaifu ukiunyong’onyeza moyo wangu kwa misiba inayoendelea na iliyopita…”

Mioyo ya wafuasi wake ikastushwa walipomsikia, wakapatwa na huzuni. Walidhani kwamba wamesikia jambo kubwa na msiba mkubwa, ndipo wakamuuliza:

“Allah (s.w.t) ajaalie usilie, Ewe mwana wa mbora wa wanadamu, ni kwa kutokana na jambo gani unalia na kutoa machozi, na ni hali gani imekufanya uwe katika hali hii ya huzuni?” Imam al–Sadiq (a.s) akashusha pumzi kwa nguvu, kisha akasema:

“Ole wenu. Nimeangalia katika kitabu cha Ilm Al–Ja’far asubuhi hii, kitabu ambacho kina maarifa yote juu ya vifo na misiba, na maarifa ya kuna nini na itakuwaje Siku ya Hukumu, ambacho Allah (s.w.t) amempa Muhammad na Maimamu baada yake (s.a.w.w) tu peke yao.

Nikatafakari juu ya kuzaliwa kwa al–Qaim wetu na kughibu kwake na kuchelewa kurejea kwake, na umri wake mkubwa na madhila makubwa watakayopata waumini katika muda huo, na chanzo cha shaka katika nyoyo zao kutokana na kughibu kwake kwa muda mrefu, na wengi wao kutoka katika dini na kuuacha Uislamu, kama Allah (s.w.t) alivyosema ndani ya Qur’ani:

وَكُلَّ إِنْسَانٍ أَلْزَمْنَاهُ طَائِرَهُ فِي عُنُقِهِ ۖ وَنُخْرِجُ لَهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ كِتَابًا يَلْقَاهُ مَنْشُورًا {13}

‘Nakilamwanadamutumemfungiamatendoyakeshingonimwake, na tutamtolea Siku ya Kiyama daftari atakayoikuta imekunjuliwa.’ (Qur’ani,17:13).

Maana ya aya hii ni Wilaya. Huruma ikanijia na nikapatwa na uchungu.”15

Habari hii inaonesha ni kwa kiasi gani jinsi Maimamu wetu walivyokuwa na uchungu kwa kughibu kwa Imam Mahdi (a.s) ambako ni kukubwa, na kadiri ambavyo yeye akiwa yu katika ghaiba huu uchungu utaendelea kuwepo. Kama tutapata kufahamu yupi ni Shi’a wa kweli, basi tutajua uhu- siano uliopo baina ya kuhuzunika kwa ajili ya Imam na kuungana naye.

Imepokewa kwamba Amirul Mu’miniin Imam Ali (a.s) amesema: “Allah (s.w.t) alichunguza duniani na akatuchagua sisi, na akachagua wafuasi wa kutusaidia, na watafurahi tukiwa na furaha, na watahuzunika tukiwa na huzuni. Watatoa sadaka pesa zao kwa ajili yetu. Wao wanatokana na sisi na sisi tunatokana na wao.”16

Kinachotakiwa hasa ni huzuni ya kweli na mapenzi, si tu kwa kuijua huzuni ya Imam. Sayyid Ibn Tawuus ana kitu kizuri mno cha kusema kuhusiana na hili, anasema: “Nimemwona yule ambaye anadai kwamba ni wajibu kuwa na furaha kwa ajili ya furaha ya Imam, na kuwa na huzuni kwa ajili ya kuwa kwake na huzuni.

Baraka za Allah (s.w.t) ziwe juu yake. Anasema kwamba anaamini kwamba kila kitu ulimwenguni hapa kimeporwa kutoka katika mikono ya al–Mahdi (a.s), na watawala na watu wamevipora toka mikononi mwake.

Hata hivyo sijamuona mtu huyu akiwa ameathiriwa na kuporwa na kunajisiwa huku, kama ambavyo angeathirika kama angenyang’anywa dinari au dirham au ardhi au mali zake. Utiifu ulioje au maarifa yalioje ya Mitume na Maimamu katika kumjua Allah (s.w.t)?”

Matendo mengi yametajwa ili kuuimarisha huu uhusiano. Mojawapo ya kitabu chenye manufaa katika uwanja huu ni, “Wajibu wa muumini kwa Imam al Zaman”. (The responsibilities of a believer towards Imam al- Zaman), cha Sheikh Mahdi ‘Alaa’ al–Diin.

Yeyote ambaye amepata kusikia juu ya Imam Mahdi (a.s) atajua kwamba maisha yake yamejaa miujiza na ni ya aina ya kipekee. Miaka kadhaa kabla ya kuzaliwa kwake, jitihada za kutaka kumjua na kumtafuta zilianza. Wale ambao walimuamini na waliamini juu ya kazi yake kubwa ya kuyaleta mageuzi ulimwenguni na kuuokoa ubinadamu walimsubiri kwa miaka kadhaa kabla bado hajazaliwa.

Na wale ambao walisikia juu ya yale ambayo angewafanyia, na namna ambavyo angewaangamiza walikuwa wakisubiri ili siku atakayozaliwa wamuuwe wakati akiwa bado mtoto anayenyonya.

Ama kwa waumini walikulia katika mikono ya Viongozi wa dini (a.s) ambao waliwapa habari njema juu ya mwokozi ambaye siku moja angeonekana. Maimam walisema mengi kwa watu juu ya sifa zake, nini kingetokea baada ya kuzaliwa kwake, na nini kingemtokea. Matumaini ya wengi yalikuwa mioyoni mwao, na walianza kusimulia toka kizazi kimoja hadi kingine.

Matumaini haya yaliongezeka kwa ahadi tukufu na mpango wa kisiasa. Ikawa ndiyo sababu ya kuwakusanya hao watu ambao wanamsubiri Imam, chini ya chama cha kisiasa chenye mtazamo wa kuleta mabadiliko ambapo wanaamini juu ya hoja ya kufanyika mabadiliko kutokana na ubadhirifu mkubwa, ambao watawala waovu na wenye sifa mbaya watawajibishwa.

Ama kwa maadui walifuatilia harakati za wanaomsubiri Imam kwa miaka kadhaa. Ndipo wakaja kujua kwamba waumini wanasubiri kuzaliwa kwa kiongozi wanayemwita Al–Mahdi (a.s) na ambaye angewaunganisha.

Walijua pia kwamba wanaomsubiri Imam wangeweza kuungana pamoja na kuleta nguvu kubwa ambayo ingeweza kuviyumbisha viti vyao vya enzi na kuzitishia tawala zao. Kwa hiyo, walizifuatilia habari za Imam Al–Mahdi (a.s) kama ambavyo waumini walivyofanya – lakini kwa nia tofauti!

Mtu anaweza kuuliza kwa mshangao, je, hii ina maana kwamba maadui walimwamini Al–Mahdi (a.s) na kwa ambayo angeyafanya, kama ilivyoahidiwa katika Hadithi na Aya? Kama walikuwa wanamwamini basi wasingelikuwa maadui zake. Je, si ndivyo hivyo? Kama hawakumuamini yeye na bishara zake njema, hivyo kwa nini basi wanajisumbua kiasi hi

Share this article

Comments 0

Your comment

Comment description

Latest Post

Most Reviews

MOST READ