Rafed English

Ashura Shahada ya Imam Husayn Mtazamo wa Kihistoria

Ashura Shahada ya Imam Husayn Mtazamo wa Kihistoria by : al-islam.org

 

Kisa Cha Siku Ya Ashura Na Kuuliwa Kwa Imam Husayn

Hii ni kumbukumbu ya kujitolea mhanga na kuu­liwa kwa Imam Husayn na takriban jamii yote ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) katika kuinusuru dini na kuitetea haki dhidi ya hao walowezi na wapi­nzani wa dini, na kuregesha mwito ule ule wa “ha­kuna Mungu apasae kuabudiwa ila Allah”.

Imam Husayn ambaye ni mjukuu wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) aliuwawa kwa ajili ya kuutetea Uislamu.

Sababu kuu ya kuuwawa Imam Husayn ni kwamba yeye alikataa dhulma na uwongo. Alikataa kula kiapo cha utii (baiyat) kwa Yazid. Imam Husayn (a.s) alitaka kuisimamisha haki na ukweli kama aliokuwa nao babu yake Mtume Muhammad (s.a.w.w).

Utangulizi

Sifa njema zote ni zake Mwenyezi Mungu, Bwana wa viumbe vyote aliyeniwezesha kufasiri mfulu­lizo wa ‘tukio la Siku ya Ashura na kuuwawa (Shahidi) kwa Imam Husayn’ (a.s) kama ulivyochapishwa kwa lugha ya kiingereza katika gazeti la ‘Daily Nation’ tarehe 19th hadi 28th Mei 1996 kwa hisani ya ‘Tawhid Distribu­tion Service’.

Inapata zaidi ya miaka 1360 tangu kuuwawa (shahidi) kwa Imam Husayn (a.s) na wafuasi wake katika uwanja wa Karbala na majeshi katili ya Yazid ibni Muawiya ibni Abu Sufyan. Tukio hili halikuwa la kawaida kwani alishalibashiri Mtume Muhammad (s.a.w.w.) aliposema:
 

إن لقتل الحسين حرارة في قلوب المؤمنين لا تبرد أبدًا

‘‘Kwa hakika kifo (shahada) cha (Imam) Husayn kitaamsha mori katika nyoyo za waumini ambao hautapoa milele’ (mustadrak juz. II uk. 217).

Hakuna shahidi aliyeheshimika na kukumbukwa kila mara, na kwa wakati mrefu zaidi kama Imam Husayn, kujitoa kwake muhanga, kupigania haki na kumuamini Mwenyezi Mungu hata katika majaribio mengi ni hakikisho wazi la ukweli wa Uislamu.

Mfululizo huu una azma ya kutilia nguvu Aya inayosema:

وَ لا تَحْسَبَنَّ الَّذِيْنَ قُتِلُوْا فِيْ سَبِيْلِ اللهِ اَمْوَاتًا ط بَلْ اَحْيَآءٌ عِنْدَ رَبِّهِمْ يُرْزَقُوْنَ. (3:169)

‘‘Usiwadhanie wamekufa wale waliokufa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu bali wahai na Mwenyezi Mungu anawaruzuku’’. (Qur'ani 3:169)

na kukumbusha hekima na mafundisho ya Imam Husayn (a.s). Ni tumaini letu kwamba mawazo ya Imam Husayn (a.s) yatakuwezesha kuwa na mtazamo usio wa anasa za dunia, bali wa kutafuta malengo makuu zaidi una­porudi kwa Muumba wako.

Wasomaji wanaulizwa kutuandikia maoni yao na maswali kuhusu tukio hili au jambo lolote kuhusu Uislamu.

Tunawatunukia kitabu hiki mashujaa shahidi wa Karbala akiwemo kiongozi thabiti Sayyidu Shuhada Aba Abdillah Husayn bin Ali bin Abi Talib na mashujaa wote waliojitolea mhanga kuitetea dini tukufu ya Uislamu.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu s.w.t. atukubalie juhudi zetu za kuchapisha kitabu hiki.

Bilal Muslim Mission of Kenya

P. O. Box 82508, Mombasa – Kenya.
Dhul Qa'ad 1421
February 2001

Yazid Ni Nani?

"Sisi tu watumwa wa Yazid na ni kwake yeye kutu­weka huru au kutuuza kwenye soko."

Watu wa Madina walilazimishwa kuyasema maneno haya kama ishara ya kumkubali Yazid bin Muawiya ambaye alitawala dola ya Kiislamu toka mwaka wa 680 mpaka 683 miladi. Fikra hii ya kuwatawala raia kama watumwa wa mtawala ilikuwa kinyume kabisa na mafundisho ya Kiislamu. Maneno tuliyo­yataja hapo juu ambayo yalikuwa ni kiapo kilicho­lazimishwa watu wa Madina katika mwaka wa 683 ni thibitisho tosha la kuonyesha fikra za Yazid pamoja na viongozi wengine wa utawala wake.

Uislamu ulileta mizani ya kubainisha haki za mtawala na raia. Qur'ani tukufu yaeleza haya:

"Hakika Mwenyezi Mungu anawaamrishieni kuru­disha amana kwa mwenyewe. Na mtakapo hukumu baina ya watu, hukumuni kwa uadilifu”. (Qur'ani 4:58)

Ikiwa mtawala hatekelezi majukumu yake kama inavyotakikana (Utawala wa Uadilifu) basi hupoteza hadhi ya kuwa kiongozi. Imam Ali bin Abi Talib anasema:

"Kwa kuniwekea majukumu yenu, Mungu ameifanya haki yangu kwenu nyinyi na vile vile nyinyi mnayo haki juu yangu".

Kwa ufahamu huu, ni kitu cha kusikitisha kuona historia baada ya miaka 50 tu, tangu kufariki kwa Mtume (s.a.w.w), mtu kama Yazid bin Muawiya kuwa kiongozi wa Waislamu! Kwake Yazid, raia walikuwa ni kama vitu alivyo virithi kutoka kwa babake.

Kwa ujumla, karibu Waislamu wote wa wakati huo walikuwa wamelazimishwa aidha kwa vitisho au kwa kuhongwa, kumkubali Yazid kuwa mtawala baada ya Muawiya, babake. Mipango hii ilifanywa mwishoni mwa utawala wa babake.

Wakati Yazid aliingia kwenye utawala, mtu wa pekee aliyekuwa na sifa na tabia nzuri na ambaye pia alikuwa tisho kwake ni Imam Husayn bin Ali, mjukuu wa Mtume Muhammad (s.a.w.w).

Husayn bin Ali ndiye tumaini la mwisho kwa Umma wa Kiislamu kupambana na Yazid. Na kweli Husayn hakuuvunja moyo Umma wa babu yake.

Roho Ya Karbala Matengenezo Ya Ummah Leo

Ili tuweze kuielewa roho ya Karbala, hatuna budi kuielewa Karbala yenyewe ni nini, na duri yake katika historia.

Karbala ni jina la mahali katika Iraq. Mahali hapo palitokea mapambano makali sana baina ya ma­kundi mawili ya Waislamu. Kundi moja liliongozwa na Husayn bin Ali, na la pili liliongozwa na wafuasi wa Yazid bin Muawiya.

Katika mapambano hayo, wale wa jeshi la Husayn - waliopata watu 75 hivi, waume na wake - waliu­wawa kikatili karibu waume wote, pamoja na Husayn "wao", isipokuwa wachache tu wakiwemo wanawake. Hivyo kidhahiri "ushindi" ukawa ni wa jeshi la Yazid lililo­kuwa na watu wasiopungua 60,000.

Kisa na sababu ya vita hivyo ni nini? Alivyosema Husayn, ambaye ndiye aliyetoka kwenda kupigana, ni kwamba hakutoka kwa sababu yoyote nyengine isipokuwa ni kwa kutaka "kuutengeneza" umma wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), na "kutaka kuamrisha mema na kukataza maovu", na "kufuata sera" ya Mtume Muhammad (s.a.w.w).

Lakini ni nani Husayn, na ni nani Yazid? Husayn ni mtoto wa Ali bin Abi Twalib kuzaa na Mwana Fatimah binti ya Mtume Muhammad (s.a.w.w). Na Yazid ni mtoto wa Muawiya bin Abi Sufyan. Na kila mmoja katika hao ameelezwa kwa sifa zake katika vitabu vya Kiislamu vya historia.

Kukielewa vizuri chanzo cha vita hivyo, bila ya kwenda nyuma sana katika historia, ni sharti tuelewe khalfia ya mkataba uliofanywa baina ya Muawiya bin Abi Sufyan, babake Yazid, na Hasan bin Ali bin Abi Twalib, ndugu yake Husayn, na jinsi ulivyovunjwa. Pia ni muhimu kuelewa tabia na khulka za wahusika wawili hao. Yazid na Husayn, na jinsi jamii ya Kiislamu wakati huo ilivyokuwa imezorota katika nyanja mbali mbali za maisha yao.

Katika hali kama hiyo, ile roho ya kiislamu ya kupam­bana na maovu ilipotea. Kitu kilikuwa na thamani zaidi kuliko utu! Dini haikuwa na uzito tena. Nyoyo zilijaa khofu; tamaa ikawa mbele. Waislamu waliga­wanyika kikabila na kitabaka. Rushwa ikawa ndiyo sera rasmi. Vitisho vikawa ni jambo la kawaida. Ukatili waliofanyiana Waislamu, wenyewe kwa wen­yewe, hausemeki; na mengi mengineyo.

Ugonjwa ueneapo namna hiyo, na wale wa kuuganga wawapo hawana moyo wa kuuganga kwa khofu au ghafla zilizowashika, pafanyweje? Ni lazima papigwe mshindo mkubwa sana ili "walio­kufa wafufuke." Na mshindo huo, zama hizo, uli­kuwa ni shahada ya Imam Husayn (a.s.) huko Karbala. Asingejitolea yeye muhanga, na watu wake, Uislamu usingekuwako hadi hii leo.

Hiyo ndiyo roho ya Karbala’, Ilihitajika siku hizo Inahitajika leo, na itaendelea kuhitajika popote penye dhulma. Kama isemwavyo: "Kila siku ni Ashura, na kila ardhi ni Karbala”.

Hiyo ni khotuba iliyotolewa na Sheikh Abdillahi Nassir
kwenye semina ya Imam Husayn. (Tarehe 28/5/2000)

Utume Wa Muhammad (s.a.w.w)

Kama ilivyoahidiwa katika Torah, (Taurat) kitabu kita­katifu cha Musa na Injili (Biblia) ya Isa, Muhammad, muokozi wa Binaadamu, alizaliwa katika Al-Hijaz ambayo kwa sasa inajulikana kama Saudi Arabia miaka 53 kabla ya hijra (570 A.D). Na kulingana na ahadi hii ya vitabu vya kale, Qur’ani tukufu yasema:

وَ اِذْ قَالَ عِيْسَى ابْنُ مَرْيَمَ يبَنِيْ اِسْرَآءِيْلَ اِنِّيْ رَسُوْلُ اللهِ اِلَيْكُمْ مُّصَدِّقًا لِّمَا بَيْنَ يَدَيَّ مِنَ التَّوْرةِ وَ مُبَشِّرًام بِرَسُوْلٍ يَّأْتِيْ مِنْم بَعْدِي اسْمُه اَحْمَدُ ط فَلَمَّا جَآءَهُمْ بِالْبَيِّنتِ قَالُوْا هذَا سِحْرٌ مُّبِيْنٌ. (61:6)

“Na (wakumbushe) aliposema (Nabii) Isa bin Mariam (kuwaambia Mayahudi): “Enyi wana wa Israil, mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, nisadikishaye yaliyokuwa kabla yangu katika Taurati, na kutoa habari njema ya Mtume atakayejia nyuma yangu ambaye jina lake litakuwa Ahmad. (Muhammad).” (Qur'ani 61:6)

Na kutokana na Ibrahim na mtoto wake Ismail, Muhammad pia hutajwa kama Ahmad. Mtume alizaliwa akiwa yatima, maana babake Abdullah ibni Abdulmuttalib, alifariki kabla ya Mtume kuzaliwa.

Alilelewa na Babu yake Abdulmuttalib, hata alipo­fikisha umri wa miaka 6, mamake mzazi Amina binti Wahab, alifariki pia, vile vile baada ya kifo cha babu yake Abdulmuttalib, alilelewa na Ammi yake Abu Talib, ambae alimtunza kwa mapenzi kama mzazi wake na juu ya hayo alijitolea kumridhisha na kum­tekelezea kila alilohitaji.

Muhammad alitambuliwa kitambo kwa tabia zake njema, utukufu na uaminifu aliokuwa nao hata kabla ya kutangazwa kwake Utume. Alidhihirika wazi kama huyo ndiye Mtume wa mwisho kama ilivyo­teremshwa aya:
 

مَا كَانَ مُحَمَّدٌ اَبَآ اَحَدٍ مِّنْ رِّجَالِكُمْ وَلكِنْ رَّسُوْلَ اللهِ وَ خَاتَمَ النَّبِيّنَ ط وَ كَانَ اللهُ بِكُلِّ شَيْئٍ عَلِيْمًا. (33:40)

“Muhammad, si baba wa yeyote katika wanaume wenu, bali yeye ni Mtume wa Mungu na wa mwisho wa mitume na Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa kila kitu.” (Qur'ani 33:40)

Mjumbe wa mwisho wa Allah alizaliwa katika enzi ambapo wanawake hawakuwa wakinyanyaswa tu, bali wakidhulumiwa na kuchukiwa. Watoto wa kike walizikwa wakiwa hai. Hii ilikuwa ni desturi ya watu hao katika enzi hiyo. Na kuipinga na kuio­ndosha desturi hii isiyokuwa ya haki katika jamii, kukawa ndio mwanzo wa jukumu la utukufu wa kazi yake.

Mnamo mwaka 23 K.H. (599 A.D), alizaliwa mtoto aliyeitwa Ali kwa Abu Talib, ndani ya Al-Ka’ba, nyumba takatifu ya Allah katika mji wa Makkah. Ali alikusudiwa kuwa mtetezi imara, na mfuasi mtiifu wa Mtume Muhammad.

Katika umri wa miaka 25, Mtume alimuoa mjane aliyeitwa Bibi Khadijah ambae alikuwa mwanamke mfanyibiashara mashuhuri katika nyakati zake. Khadijah alivutiwa na kupendezwa na tabia za utukufu wa adabu na uaminifu wa Mtume, hata akaamua kufunga nae ndoa ambayo Mtume hakuikataa. Aliku­bali ingawa bibi Khadijah alimpita kwa umri wake.

Kutokana na ndoa hiyo, Mtume alijaliwa mtoto mmoja tu wa kike, ambae ni Fatimah aliyezaliwa katika Makkah mwaka wa 6 K.H (616 A.D) nae hakuwa ni kipenzi cha moyo wake tu bali alitokea kuwa mfano mwema na wakuigizwa katika mwendo wa wanawake ndani ya Uislamu.

Mtume aliwatoa watu Gizani na kuwafunza utu kamili, aliwafunza jinsi mwanamke na cheo chake ipasavyo, kama ilivyotakiwa na Mwenyezi Mungu.

يـاَيُّهَا الَّذِيْنَ اامَنُوْا لا يَحِلُّ لَكُمْ اَنْ تَرِثُوا النِّسَآءَ كَرْهًا ط وَ لا تَعْضُلُوْهُنَّ لِتَذْهَبُوْا بِبَعْضِ مَآااتَيْتُمُوْهُنَّ اِلاّ اَنْ يَاْتِيْنَ بِفَاحِشَةٍ مُّبَيِّنَةٍ ج وَعَاشِرُوْهُنَّ بِالْمَعْرُوْفِ ج فَاِنْ كَرِهْتُمُوْهُنَّ فَعَسى اَنْ تَكْرَهُوْا شَيْئًا وَّ يَجْعَلَ اللهُ فِيْهِ خَيْرًا كثيرا (4:19)

“Enyi, Mulioamini! si halali kwenu kurithi wanawake kwa jeuri. Wala msiwazuie (kuolewa na waume wengine kwa kuwa hamuwataki wala hamtaki kuwaacha ila kwa pesa) ili mpate kuwanyang’anya baadhi ya vile mlivyowapa. (Hapana ruhusa haya) isipokuwa wawe wamefanya uovu ulio wazi. Na kaeni nao kwa wema, na kama mkiwachukia basi (msiwaache) kwani huenda mkakichukia kitu, na Mwenyezi Mungu ametia kheri nyingi ndani yake.”
(Qur'ani 4:19)

Mtume alimuheshimu mno binti yake kama itaki­wavyo katika utukufu wa sharia na kadhalika ali­sema, Fatimah ni pande la nyama yangu na yeyote anayemfurahisha yeye, atanifurahisha mimi na yeyote yule anayembughudhi huwa amenibughudhi mimi, na anayenibughudhi mimi anambughudhi Mwenyezi Mungu.

Mtume alipofikisha umri wa miaka 40 mwaka 13 K.H. (610 A.D), malaika mtakatifu Jibril alim­wasilishia ujumbe wa kwanza kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kuutangaza utume wake ambapo Muhammad aliwaita watu wote wa jamii katika dhifa na kutaka maoni na rai zao kuhusu ukweli na uaminifu wake nao waliku­bali kwa kauli moja.

Ndipo alipowatangazia ujumbe wake:

"Semeni hakuna mungu apasaye kuabudiwa ila Allah, nanyi mtapata kufanikiwa” ‘kisha aliwajulisha habari za utume wake, ambapo baadhi ya jamaa zake waliokuwepo ma-ami zake na wengineo isipokuwa Sayyidna Ali walimpuuza na kumfanyia stizahi kwa kutoamini ndipo Mtume alipomtangaza hadharani Sayyidna Ali aliyekuwa na umri wa miaka 11 kama msaidizi na khalifa wake pasikuwajali waliokuwepo.’

Hijra Na Ahlul Bayt

Mwito wa kwamba ‘hakuna mungu apasae kuabudiwa ila Allah’ ulizuwa chuki dhidi ya Mtume kutoka kwa maadui zake, ingawa ni mwito wa kuu­ngana na kuji­komboa kutoka katika udhilifu na utumwa ulioathiri utu wa mwanaadamu. Watu wake waliokuwa wakim­heshimu na kumtambua kwa cheo kama ‘mkweli na mwaminifu’ sasa walim­geukia na kumtusi kwa majina ya kila aina.

Walimwendea kinyume, kumtupia mawe na kum­fanyia fujo katika kila njia na kushindwa kumuan­gusha ili kumzuia Mtume.

Makafiri wa Makkah hawakuweza kumdhuru kwa kutokana na nguvu na ulinzi aliowekewa na ammi yake Abu Talib, ambae alikuwa tayari kupambana na yeyote yule aliyetaka kumdhuru Mtume.

Wathama Bibi Khadijah, mkewe Mtume alitumia pesa zake zote alizokuwa nazo katika mchango wake wa kuikuza dini ya kiislamu. Huyu ndiye mwanamke wa kwanza aliyeingia na aliyetetea na kuutukuza Uislamu. Ama utiifu wake haukuwa na mfano.

Alipoishiwa na mali yake huyo bibi tajiri mkuu wa waarabu, alijitolea na kujimudu kuishi kula majani makavu, alitengana na starehe zote za jamii na marafiki, aliridhika siku zote na sadaka alizotoa na kutakabaliwa na Mwenyezi Mungu , alifurahia ba­hati yake yakuwa sehemu na fungu katika kuima­risha ujumbe mtukufu wa Mtume.

Muda wa miaka kumi na mitatu tangu tangazo la Mtume wa Islam, watu wa Makkah walifanya chuki sana juu ya Mtume na ujumbe wake hasa alipoon­dokewa na wasaidizi wake wote wawili; Abu Talib, ammi yake na Khadijah mke wake aliyekuwa msaidizi wake katika kila lililohitajika.

Mwaka wa 1 B.H. (621 A.D) Mtume alihamia Madina ambako watu wa huko walikuwa wazuri, marafiki wema na wakarimu kwake.

Maadui wa Mtume hao wakazi wa Makkah, hawa­kutosheka pia na kuhama kwake kutoka Makkah, baadhi ya ma-ammi zake na a’li zao, walimfanyia matata na fujo za kila aina. Mtume alilazimika kupi­gana vita visivyo pungua 59, vilivyoanzilishwa na wenyeji wa Makkah dhidi ya waislamu katika muda mfupi wa miaka isiyopungua kumi na katika mfulu­lizo wa vita hivi vilivyofuatia moja baada ya nyen­gine ni Sayyidna Ali, ndiye aliyekuwa kiongozi mwenye ushindi.

Vita vya Badr, Uhud, Khandaq na Khaibar ni baadhi ya vita vyenye ushindi wa Mtume na Makkah ilita­waliwa kwa amani mnamo mwaka 10 B.H (630 A.D), juu ya ushindi huo Mtume aliyavunja masanamu 360, yaliyokuwa yamewekwa kama miungu katika Al-Ka'ba.

Katika mwaka wa pili 2 B.H. (624 A.D) Mtume alimuoza Ali ibni Abu Talib binti yake Fatimah kwa sherehe ya harusi iliyofanywa kwa ufupi kabisa ambayo yafaa kuigizwa mfano. Na kutokana na ndoa hii Ali na Fatimah walijaaliwa watoto wanne kama ifuatavyo;

Hasan, katika mwaka 3 B.H. (625 A.D)

Husayn mwaka wa 4 B.H. (626 A.D)

Zainab mwaka wa 6 B.H (628 A.D)

Umm-kulthum mwaka wa 8 B.H. (630 A.D)

Baada ya kuhamia kwao Madina, palikuwa na tukio jengine la muhimu na la kukumbukwa mbali na vita vilivyopiganwa. Ni katika mwaka 8 B.H. (630 A.D) ambapo Mtume alimtembelea binti yake akiwa mgeni wake nyumbani, ambapo alikaa na kujifunika ‘utaji’ wa nguo, akifuatiwa na binti yake Fatimah na mumewe Ali na watoto wao Hasan na Husayn pia. Wote waliingia ndani ya utaji aliojifunika Mtume. Na katika kikao hiki cha watu watakatifu watano, Mtume aliinua mikono yake na kuomba dua:

“Ya Allah, hawa ni watu wa nyumba yangu Ahlul Bayt. Ni watu wanaonihusu na wasaidizi wangu, wao ni nyama yangu na damu yangu. Kwa yeyote yule atakaewasumbua hawa, atanisumbuwa mimi, yeyote atakae waudhi hawa ataniudhi, na mimi nitapigana na yeyote yule atakae pigana nao, na nitakuwa na amani na yule atakae kuwa na amani nao, mimi ni adui wa maadui zao na rafiki wa wale marafiki zao."

Hapo aliteremka malaika Jibril na ujumbe huu:
 

...اِنَّمَا يُرِيْدُ اللهُ لِيُذْهِبَ عَنْكُمُ الرِّجْسَ اَهْلَ الْبَيْتِ وَ يُطَهِّرَكُمْ تَطْهِيْرًا. (33:33)

“...Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu enyi watu wa nyumba (ya Mtume), na (anataka) kukuta­kaseni kabisa kabisa.” (Qur'ani 33:33)
Vile vile alivyosema Mwenyezi Mungu:

...قُلْ لآ اَسْئَلُكُمْ عَلَيْهِ اَجْرًا اِلا الْمَوَدَّةَ فِيْ الْقُرْبى (42:23)

“…sema, sitaraji kupata chochote kwako ila mapenzi kwa ‘akraba’ zangu.” (Qur'ani 42:23)

Kadhalika wakati mwingine ilipoteremshwa aya isemayo:

فَمَنْ حَآجَّكَ فِيْهِ مِنْم بَعْدِ مَا جَآءَكَ مِنَ الْعِلْمِ فَقُلْ تَعَالَوْا نَدْعُ اَبْنَآءَنَا وَ اَبْنَآءَكُمْ وَنِسَآءَنَا وَنِسَآءَكُمْ وَ اَنْفُسَنَا وَاَنْفُسَكُمْقف ثُمَّ نَبْتَهِلْ فَنَجْعَلْ لَّعْنَتَ اللهِ عَلَى الْكذِبِيْنَ. (3:61)

“Watakaokuhoji (sasa) katika haya baada ya kukufikilia ilimu (hii na kuwafikilia wao), waambie, ‘Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu; na wanawake wa kwetu na wanawake wa kwenu, na sisi na nyinyi, kisha tuombe kwa unyenyekevu tutake laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie waongo.” (Qur'ani 3:61)

Mtume aliongoza ujumbe wake akiwa na Ali kama Akraba wake, Fatimah kama mwanamke wake na watoto wao Hasan na Husayn kama watoto wake katika pambano lililojulikana kama “Mubahala" (Yamini) dhidi ya watu wa Najran (Yemen). (Neno Mubahala limetokana na Bahala ina maana ya ‘kuapiza’ au ‘kulaani ‘laana’. Hivyo lina maana ya kuapizana kati yao).

Ama watu watakatifu hawa “Ahlul Bayt” hawakuwa ni wapenzi wa Mtume (s.a.w.w) kwa kuwa ni ma­pande ya nyama yake na damu yake tu, bali ni watu walio­kuwa na msimamo imara mbele yake, watu walio­kuwa watiifu na waadilifu waliojitolea kumtii kama ilivyoshuhudiwa katika mienendo ya tarikhi zao.

“Mfano wa watu wa nyumba yangu ni kama vile safina ya Nuhu, yoyote aingiaye humo atapata kuokoka na yule atakaye kupinga na kusita kuingia atatwaliwa na kutoswa na maji.”
Mtume Muhammad (s.a.w.w)

Khalifa Wa Mtume

Mtume katika rejeo lake Madina baada ya kwenda kuhiji Makkah, katika mwaka wa 10 B.H. (632 A.D) iliteremshwa aya aliyopokea kama ifuatavyo:

يـااَيُّهَا الرَّسُوْلُ بَلِّغْ مَآ اُنْزِلَ اِلَيْكَ مِنْ رَّبِّك َط وَاِنْ لَّمْ تَفْعَلْ فَمَا بَلَّغْتَ رِسلَتَه ط وَاللهُ يَعْصِمُكَ مِنَ النَّاسِ ط اِنَّ اللهَ لا يَهْدِى الْقَوْمَ الكفِرِيْنَ. (5:67)

"Ewe Mtume! peleka ujumbe uliopokea kutoka kwa Bwana wako na iwapo hukutekeleza (ni kwamba) hukupeleka ujumbe wake na Allah atakulinda na watu, hakika Allah hatowasaidia watu wasioamini." (Qur'ani 5:67)

Hapo Mtume aliwakusanya watu wote walio­kuwa pamoja nae katika jangwa lilijulikana kama 'Ghadeer' na kuwatolea hotuba moja mu­himu kabisa katika ujumbe wake na juu ya hayo, alithibitisha rasmi ukhalifa wa Imam Ali, na suala la uongozi baada ya kuondoka kwake Mtume.

''Mimi ninawaachia nyinyi vitu viwili vizito 'Kitabu kitakatifu’ cha Mwenyezi Mungu na ‘watu wa nyumba yangu Ahlul Bayt’ na kwa yeyote yule ambaye mimi ni kiongozi wake, na Ali ni kiongozi wake vile vile. Ewe Allah, na uwe rafiki wa atakaekuwa rafiki yake na adui wa yule atakaekuwa mpinzani wake."

Alitangaza, akiwajulisha umati kwamba hii ni safari ya mwisho ya Hijja yake na karibuni ataaga dunia.

Ama sifa za Ali zilitangaa katika nyanja zote na kutambuliwa na kila mmoja:- kwa ujuzi wake wote, kazi yake Nahjul Balagha, inafuatia Qur’ani tukufu isiyokuwa na badili.

Katika Sahih Muslim imeandikwa kwamba Zayd b. Arqam amesema kuwa Mtume (s.a.w.w) alisema: ‘Enyi watu! Hakika mimi ni binadamu; nami nataraji (hivi karibuni) kujiwa na mjumbe (malaika wa mauti) wa Mola wangu na kuitika (mwito Wake). Kwa hivyo ninawaachia nyinyi vizito viwili; cha kwanza ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu chenye uongozi na mwangaza. Basi shikamaneni na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na watu wa Nyumba yangu (Ahlul Bayt). Ninawakumbusha nyinyi watu wa Nyumba yangu. Ninawakumbusha nyinyi watu wa Nyumba yangu. Ninawakumbusha nyinyi watu wa Nyumba yangu.’

Kitabu ‘Al Fadhail’ Mlango wa ‘Fadhail Ali’. Kwa Kiingereza ni Vol. 4, Uk. 1286, Hadith 5920.

Utiifu Wake

Kulala kwa Imam Ali juu ya kitanda cha Mtume usiku wa Hijra alipohamia Madina, wathibitisha jinsi alivyo­jitolea katika dini, nguvu zake na ushujaa aliokuwa nao katika vita alivyopigana, ukweli na uaminifu, unyenyekevu na uchaji wake kwa Mungu haufana­nishwi na yeyote.

Mara baada ya tangazo la Mtume, iliteremshwa aya ifuatayo:

...اَلْيَوْمَ اَكْمَلْتُ لَكُمْ دِيْنَكُمْ وَ اَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِيْ وَ رَضِيْتُ لَكُمُ الإِسْلامَ دِيْنًا... (5:3)

"…Leo nimekukamilishieni dini yenu na kukutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe dini yenu…" (Qur'ani 5:3)

Wanafiki na watesi ingawa hawakufurahishwa na tangazo la Mtume kuhusu Ali, wakati huo walificha chuki zao juu ya 'Ahlul Bayt' na kuwapongeza kinyume na kusikia maoni matakatifu na mithali ya hekima waliyopewa na Mtume kuhusu Ali ibn Abi Talib, kama:

‘Mimi ni jiji kuu la elimu na Ali ndie lango la kuingilia’;
‘Ali ametokana na mimi na mimi natokana na Ali’;
‘Ali kwangu ni kama Harun alivyokuwa kwa Musa’;
‘Ali yumo ndani ya ukweli na ukweli umo ndani ya Ali’.

Miongoni mwa wafuasi wake na watu ambao hawakukubaliana na maoni matakatifu ya Mtume, walijaribu na kufanya kila waliloweza ili kuvuruga na kutarakanya maneno na kumpinga khalifa wake baada ya Mtume kuondoka.

Mtume alifariki Madina baada ya siku sabini tokea alipotoa tangazo lake, aliugua kidogo na kuaga dunia.

Walipopokea habari za kifo cha Mtume, wale watu waliokuwa wavunjifu waliondoka mara moja na kukusanyika ili kulazimisha khalifa wa chaguo lao juu ya umma; huku wakiyaondoa mawazo ya waumini katika jambo muhimu kama mazishi ya Mtume.

Imepokewa katika historia kwamba akali ya watu wapatao kumi tu, hivi ndio waliohudhuria katika mazishi ya huyu Mtume mtakatifu wa Mwenyezi Mungu. Hata baadhi ya jamaa zake na wake zake wengine hawakuwa na habari za matayarisho ya mazishi yake hadi waliposikia sauti ya mashepe (wakichimba kaburi).

Baada ya kuchagua kiongozi wamtakae hao watu walifululiza moja kwa moja kuelekea nyumba ya Fatimah, wakitaka bay'ah yaani kutambuliwa na Ali japo ikibidi kumlazimisha. Namna walivyokwenda kwa vishindo na fujo, waliharibu viamba vya nyumba yake iliyokandikwa na kuitia moto, mlango wake ulimuangukia Fatimah aliyekuwa amesimama nyuma yake, na kusababisha kifo cha kitoto chake Mohsin aliyekuwa tumboni bado na kusababisha majeraha makali katika mwili wa binti yake Mtume ambaye alisema:

"Fatimah ni kipande cha mwili wangu na atakayemdhuru, amenidhuru mimi na atakaye mfurahisha, amenifurahisha mimi."

Ali pamoja na jamii yake walipatwa na fadhaa na huzuni juu ya madhila yaliyowapata hadi Fatimah, alipoomboleza, ‘laiti madhila hayo yangeangukia jabali, lingalipasuka na kuvunjika vunjika. Laiti yangeliangukia mwangaza wa mchana, ungeligeuka usiku na kutanda kiza cheusi.’

Bi Fatimah alifariki baada ya siku sabini tokea alipojeruhiwa na nyumba yake kuvamiwa katika mwaka wa 11 B.H. (632 A.D) akiwa na umri wa miaka 18 tu, nae alizikwa na vijana wake wawili, Hasan na Husayn ambao Mtume alisema:

"Hasan na Husayn ni viongozi wa vijana wa peponi na Husayn ametokana na mimi, na mimi natokana na Husayn," na watoto wawili wa kike; Zainab na Umm-kulthum.

Ali alikaa kando pasi kudai haki yake ya ukhalifa kwa muda wa miaka 25, hadi alipoandamwa na 'kuchaguliwa' kama khalifa wa nne. Na katika wakati wake huo wa ukhalifa alishughulishwa mno na wapinzani wake kutetea Uislamu katika vita visivyopungua 40, vilivyozushwa mfululizo kwa miaka 4 ya utawala wake.

Udhalili Na Ugandamizi

Pindi Ali alipochaguliwa kwa wingi wa kura za watu, Muawiya bin Abi Sufyan, alizuka na kujitangazia yeye kuwa ni ‘khalifa’ wa Islamu katika mwaka wa 36 B.H. (659 A.D) baada ya kuuliwa Uthman aliyekuwa khalifa wa tatu.

“Yoyote apendae kumfurahisha mtawala wake, japo kwa kitu kidogo, kitakacho kuwa ni sababu ya kumuudhi Mola wake, huwa ameshaitoka dini ya Allah.” Mtume Muhammad (s.a.w.w)

Utawala wake wa dhuluma na ubinafsi uligeuza kila sehemu ya dola ya waislamu wa Hijaz katika upotofu na kuitawala nchi kutoka karibu na mbali na kuendelea kupanua utawala wake pamoja na ‘Damascus’ (Sham) kama jiji lake kuu. Katika kupuuza kwake si misingi tu ya kiislamu, bali kuendelea kwake na upotofu aliye­sambaza machafu na mambo yote maovu yaliyo­katazwa katika Uislamu kama kuruhusu unywaji pombe, kuendeleza ukahaba na pia kusambaza fitina baina ya waumini na wafuasi wa Mtume pamoja na kuwatesa na kuwadharau ‘Ahlul Bayt’ yaani watu wa nyumba ya Mtume.

Mwenendo wa upotofu wa kwenda kinyume cha sharia ya kiislamu kadhalika na kuwatesa watu wa nyumba ya Mtume na kutotambuliwa haki zao tu­kufu, hata kubatilisha sala tukufu ya siku ya Ijumaa kusaliwa siku ya Jumatano na kadhalika, haukuku­baliwa katu na wafuasi waadilifu wa Mtume, jambo ambalo lilimkasirisha sana Muawiya na kuwaadhibu wale waliojaribu kumpinga.

Enyi watu, Mtume amesema, kwamba “yeyote anaekuta mtawala dhalimu, anaekwenda kinyume na kukiya mipaka mitakatifu na kuvunja sharia ya Allah, kukataa mwendo wa Mtume na kutawala watu kwa ubaya, basi asipompinga mtawala huyo kwa maneno na matendo Allah hatompokea na kumweka mahali pema siku ya kiyama.” Imam Husayn ibn Ali (a.s)

Jambo lingine la upotofu wa Muawiya, mtoto wa Abu Sufyan lilikuwa kutarakanya maneno ya kinyume cha Ali akiamrisha kutusiwa kwake katika mimbari na kubeza kwamba Mtume ati alimchagua yeye (Ali) kama nafsi yake na kuongeza kwamba Muhammad hakupokea wahyi kamwe.

Hatimaye Muawiya alipanga njama ya kumuua Imam Ali wakati alipokuwa akisali ndani ya msikiti wa Kufa katika mwaka wa 40 B.H. (661 A.D).

Hasan ibni Ali, mtoto mkubwa wa Ali, pia Imam wa pili vilevile alisumbuliwa, ingawa katika tukio moja la vita Hasan ibni Ali alipigana kishujaa dhidi ya wanafiki walioongozwa na Muawiya na kuandikiana mkataba wa amani.

Mkataba huu wa amani baina ya Hasan na Muawiya ulihusu hifadhi ya ulimwengu wa Uislamu kutokana na masharti kadha yaliyotolewa na Hasan, ambayo yalikubaliwa hadharani na Muawiya na kisha kupuuzwa, inamaanisha kwenda kinyume na Uislamu.

Baadhi ya masharti hayo, ni kuendeleza na kudumisha sharia za kiislamu kulingana na Qur’an tukufu na mwenendo wa sunna ya Mtume Muhammad (s.a.w.w), kukomesha mara moja matusi aliyokuwa akitukanwa Ali ibni Abi Talib katika mimbari na Muawiya hata­chagua khalifa mwengine baada yake yeye.

Hata hivyo hakuna sharti lolote lililotekelezwa na Muawiya kulingana na mkataba wa amani uliotiwa saini, na mali ya wananchi yaliyoporwa na haki zao hazikushughulikiwa wala; mwenendo wa Muawiya kinyume cha Uislamu haukubadilika bali maonevu na upotovu ulizidi kuendelezwa katika uongozi wake hata kufikilia kiwango cha kutotambulika tofauti kati ya haki na batil, hitilafu baina ya ukweli na urongo au uzuri na ubaya.

Ama kwa kuwapo uhadhiri wa Hasan, muungano wa watu wengi ulikuwa pamoja naye kwa sababu ya ukweli kutawala uongo, ambapo Muawiya na watu wake hawakuridhishwa na msimamo wake Hasan. Walikereka daima na umaarufu wake. Hatimae Muawiya alimshawishi mke wake wa Hasan, Jo’ada binti As’ash ambaye alishawishika katika njama ya kumtilia sumu mumewe na matokeo yake yakawa ni kifo cha Imam Hasan, jamaa mwingine wa nyumba ya Mtume “Ahlul Bayt” katika mwaka 51 B.H. (671 A.D).

Jo’ada aliyehadaiwa na kuahidiwa kuolewa na Yazid mtoto wa Muawiya ambaye alifanywa kuwa mrithi katika utawala, alidanganyika na kuvutiwa na tamaa na ahadi ya urongo ya Muawiya kwamba atakuwa malkia wa pili wa Hijaz, nchi tukufu ya kiarabu, hakuweza kujizuia na matamanio yake ya kutajirika, na kumuua mumewe Hasan ibni Ali, mjukuu wa Mtume.

Mara tu baada ya kukamilisha njama yake alivyo pangiwa na Muawiya, Jo’ada alichukuliwa kama kafiri na alikataliwa kwa kuwa mwanamke asiyekuwa mwaminifu na ahadi aliyopewa ya kufanywa malkia wa Hijaz ikaishilia hapo, na kuharibikiwa na matokeo ya Akhera yake pia.

Husayn ibni Ali ndiye aliyekuwa khalifa wa tatu wa Mtume na wa mwisho katika jamii ya watu wa nyumba ‘Ahlul Bayt’, baada ya Ali ibni Abi Talib na Hasan ibni Ali. Husayn alimzika nduguye Hasan katika maziara ya Madina kuepukana na vita vilivyozushwa na baadhi ya watu waliokuwa na ujamaa kabisa na Mtume lakini hawakuwa katika fungu la watu wa nyumba ya Mtume ambao pia waliamua kumimina mfululizo wa mishale juu ya maiti ya mjukuu wa Mtume ili kuzuia mazishi yake karibu na Mtume.

Ndipo nduguye Husayn aliyatenga mazishi ya nduguye kuepukana na umwagikaji wa damu bilashi.

“Kufa katika utukufu ni bora kuliko kuwa na maisha ya udhilifu”. Imam Husayn ibni Ali (a.s)

Husayn Kuhama Kutoka Madina

Mwaka wa 60 B.H. (680 A.D) Muawiya alifariki na kuvunja tena mkataba walioandikiana na Imam Hasan kwa kumchagua mtoto wake Yazid kama Khalifa baada yake. Yazid, ambaye alikuwa ni mbembefu wa wanawake dhahiri hakuwa na maarifa yoyote, wala uhusiano na mwenendo wa waislamu. Hata Uislamu wenyewe hakuutambua, akawa yeye ndiye Khalifa. Nae hakuwa mwenye kusali, alitumia nguvu na kuendeleza ufalme wake kwa kuwatisha watu. Alipendelea sana watu walio­kuwa upande wake, aliruhusu vitendo vyote vichafu kama unywaji pombe, uzinifu na kutumia ovyo mali ya mchango wa umma wa Kiislamu kwa njia isiyo­kuwa haki na maamrisho ya Mwenyezi Mungu yalipuuzwa dhahiri.

“Yeyote anaekwenda kwa tajiri na kujifanya mnyonge mbele yake kwa sababu ya mali aliyo nayo huwa ameshapoteza thuluthi mbili ya dini yake”. Mtume Muhammad (s.a.w.w)

Mpotofu huyo Yazid, aliyetokana na ukoo wa Banu Umayya alitafuta bay’ah ya watu wote walio chini yake na kuwaapisha juu ya utawala wake. Kadha­lika hakuwaacha watu wa Makkah na Madina. Alimtaka na Husayn pia kumpa bay’ah kupitia kwa Gavana wake katika Madina, Walid bin Utbah ambae alikuwa ni mjombake Yazid. Walid akiwa na naibu wake, Marwan bin Hakam walitaka kukutana na Husayn katika kasri ya Madina mwezi wa Rajab, ambao ni mwezi wa saba wa kalenda ya kiislamu mwaka wa 60 B.H. (680 A.D)

Watu wa Madina kwa jumla walijawa na hofu hasa kwa sababu ya Husayn kuitwa katika kasri ya ufalme. Kinyume cha kutembelewa yeye. Wasiwasi ulisambaa kote na hali yao ilikuwa ya kutishia na kiwewe. Katika mkutano huu, Walid alimjulisha Husayn juu ya kifo cha Muawiya na kutawazwa kwa Yazid kama kiongozi na kwamba sasa Yazid ataka bay’ah kutoka kwa watu wa sehemu zote khususan kwake yeye Husayn.

Wasomaji: Hebu tufikirini iwapo tabaka zote za kila sehemu isipokuwa (Husayn na wafuasi wake wachache) wamempa bay’ah na kumtambua Yazid, ina maana gani kumsisi­tiza Husayn na iwapo Husayn amekataa na kutupilia mbali ombi lake, basi angeharibikiwa na nini Yazid aliyekuwa na nguvu zote katika utawala? Ama Yazid, alielewa vyema bay’ah ya Husayn haimaanishi kwamba amemkubali kuwa khalifa bali kwa hakika yeye (Yazid) alijiamini nafsi yake kama ndio khalifa wa haki, na kwamba watu wa nyumba ya Mtume ‘Ahlul Bayt’ wamekubali na kukubaliana na hilo, kungelimaanisha watu wa nyumba ya Mtume na mmoja katika wao wamekubali mwenendo wake wa upotofu kinyume cha Uislamu na kuhalalisha unya­ng'anyi wa haki na mali ya watu. Mtu yeyote mwenye fikira njema asingekubali hilo kwa sababu ingemaanisha ujumbe wa Mtume na dini ya Mwenyezi Mungu haitokuwa na maana yoyote.

Husayn alidhukuru na kulipima suala hilo kwa makini sana katika mizani ya akili yake licha ya kiti­sho juu ya usalama wa maisha yake na kulitupilia mbali ombi la Yazid. Walid na Marwan, tangu hapo walikwisha panga njama ya kummaliza iwapo Husayn angekataa kumtambua Yazid, kama walivyotarajia, hata kama utakatifu wa nchi ya Madina utaharibiwa na hasa ndivyo ilivyotokea. Baada ya mkutano huo Husayn aliamua kuihama Madina ili kuepukana na uharibifu katika nchi tu­kufu na uovu wa Yazid. Husayn alitoka na jamii yake isipokuwa Ummi Salma (mke wa Mtume), Fatimah binti Kalebiya (Mke wa pili wa Ali ibni Abi Talib na mama wa Abbas ibni Ali) na binti yake Fatimah, hawakusafiri pamoja nae.

Msafara huo wa masikitiko na huzuni ulisimamiwa na kutayarishwa na nduguye wa kambo Abbas ibni Ali. Wenyeji wa Madina walipopata habari za kusikitisha za kuhama kwa Husayn, watu wa se­hemu zote waliwasili na kumpa pole na hata wen­gine walimuonya asiende Iraq, kama walivyopokea kutoka kwa Mtume kwamba watu wa nyumba ya Mtume wangeuliwa na kumalizwa Iraq.

Abbas, alikuwa ni mtoto wa Ali ibni Abi Talib na Fatimah binti Kalebiya mke wa mwisho wa Ali, ali­yetamani kuwa na mtoto atakae kumwakilisha katika vita vitakatifu vya Karbala. Na vita hivi vili­ bashiriwa kitambo na Mtume mwenyewe baada ya mapokeo ya wahyi. Maadamu Mtume atawakili­shwa na Husayn, Ali vile vile alipenda awakilishwe na Abbas.

Msemo wa Mtume:

“Makhalifa wangu watakuwa ni kumi na wawili na wote watatokana na kizazi changu. Mfano wa kwanza ni kama Muhammad, na wa mwisho ni kama Muhammad kila mmoja wa-wao ni kama Muhammad na kwa jumla wote ni kama Muhammad”.

Msemo huu, ulidhihirisha ukweli wake katika kila neno. Wakati wakipanda ngamia wao wakusafiria, Husayn alionyesha ulimwengu jinsi wanawake wanavyo­heshimiwa katika Uislamu kuliko mila ama desturi yoyote nyingine. Yeye mwenyewe alisimamia msa­fara wakati wakipanda ngamia wao akishuhudiwa na maelfu ya watu ambapo kila mwanamke alion­gozwa na maharimu yake akiwa katika vazi lake rasmi la hijab, na vijana wa ukoo wa Hashimia wali­hakikisha adabu na heshima yao.

“Taifa linalonunua starehe za maisha kwa kubadilishana na hasira ya muumba halipati kuongoka.” Imam Husayn ibni Ali (a.s)

Husayn Kuwasili Karbala

Husayn aliondoka Madina siku ya 28, mwezi wa Rajab 60 B.H. (7th May 680 A.D) na kuwasili Makkah, nchi tukufu yenye usalama kwa watu wote. Hapo mwezi wa Dhulhajj ambao ni mwezi wa ibada ya Hajj katika nchi hiyo tukufu, Husayn aligundua njama ya Yazid aliyetuma majasusi wake wachache na silaha, wakijifanya mahujaji kumbe kusudio lao ni kumuua Husayn akiwa katika ibada hiyo tukufu ya Hijja. Kinyume cha makatazo kwamba hakuruhu­siwi kuwinda wala kuua japo kijidudu katika nchi hiyo tukufu wakati wa Hijja.

Yazid alipanga njama za kumuua mjukuu wa Mtume huku akijidai kuwa ni khalifa wa Mtume. Siku ya 9, Dhulhajj, 60 B.H. (13th September 680 A.D) mahujaji wote wa nyumba tukufu ya Allah wanapo­elekea mlima wa Arafat wakiwa na mavazi ya Ihram, Husayn alikatiza hijja yake ambayo ni ibada kuu na kwenda kwenye Umrah na siku hiyo hiyo aliondoka Makkah kwa kusudi la kuhifadhi nyumba tukufu ya Allah, na hiyo ni faradhi yake. Yeye na jamii yake walielekea Kufa, katika mji wa Iraq.

Watu wa Iraq, walikwishamuandikia nyaraka nyingi za kumsairi Husayn na kumuita ili aende huko na kuwapa muongozo wake mtakatifu. Na ili kujua undani wa ombi lao, Husayn alimtanguliza balozi wake, Muslim ibni Aqeel, ambaye ni binamu yake na mhifadhi wa mafundisho ya sharia za Mtume. Alipokuwa njiani kuelekea Kufa, Husayn alibaini udanganyifu wa watu wa Kufa, ambao walitoroka na kumuacha balozi huyu peke yake kwa kumuo­gopa Yazid na ubaya wake.

Muslim ibni Aqeel, aliyesafiri na watoto wake wawili hawakujulikana mahala walipo. Kuendelea mbele na safari yake Husayn vile vile alipokea habari ya kukatwa vichwa vya watoto hawa, ambao mmoja alikuwa na umri wa miaka minane na mwingine miaka tisa hivi. Msafara wake ulisimamishwa njiani na mlolongo wa majeshi yapatayo elfu moja wa­panda farasi walioongozwa na Hurr bin Riyahi ambae aliupindua msafara huo na kuuelekeza upande wa Karbala katika jangwa lililoko kusini mwa Iraq na ambalo limepakana na mto wa El-Furat kwa upande wa kaskazini mwake.

“Amrisheni mema na kukataza maovu, la sivyo waovu watawatawala na mwito wenu kuwa yule aliye bora (anapasa kutawala) hautatiwa maanani.” Mtume Muhammad (s.a.w.w)

Kufika Karbala Husayn alikita hema lake karibu na ukingo wa mto El-Furat. Kuanzia siku ya pili ya Muharram 61 B.H. (5th October 680 A.D) majeshi ya Yazid yaliendelea kuongezeka na mara waliwa­zunguka Husayn na watu wake.

Walimlazimisha yeye Husayn pamoja na wenzie waondoshe hema zao kutoka ukingo wa mto na kuzikita mbali kidogo wakiacha nafasi ya uwanja karibu na mto ili kuuzidisha masongamano wa kuteka maji. Hii vile vile ikiwa ni hila moja ya Yazid, kutaka kuwasumbua.

Yazid alimtuma kiongozi shupavu wa watu wake, Umar ibn Sa’ad aliyekuwa mjuzi kamili kuhaki­kisha kwamba viumbe vyote tangu ndege, wanyama na watu wengine wote wapata nafasi ya kuteka maji, isipokuwa watu wa nyumba ya Mtume wasipatiwe maji zaidi.

Siku ya tisa ya Muharram majeshi ya Yazid yalion­gezeka na kufikia 'elfu sabini' ambapo Husayn am­bae hakujiandaa kivita alikuwa na akali ya watu sabini tu, nao ni pamoja na watoto wadogo. Mara hii tena Yazid alimtuma Umar ibn Sa’ad, akimtaka Husayn amtambue Yazid lakini ombi lake lilikataliwa pia. Na kufikia hali hii, Husayn akijua yatakayompata, aliwaita na kuwakusanya watu wake wote akawafahamisha huzuni yake juu ya hali ilivyo na kuwaonya kuhusu yatakayotokea: kukutuliwa ki­shahidi na wala hakutakuwa na mali itakayo­tekwa na kuongeza, majeshi ya Yazid yanataka damu yake (Husayn) kwa hivyo yeye yu radhi iwapo wenziwe wangetaka kuondoka na kumuacha yeye peke yake.

Usiku alizima taa zote za kambini ili wapendao kuondoka watoke waende zao wasionekane, lakini hakuna yeyote aliyekubali kuondoka na kumuacha peke yake.

Hatimaye watu watatu kutoka kwa jeshi la Yazid walivuka na kumjia Husayn katika hema lake na kuomba msamaha walipojua vita hivi si vya kupi­gania ufalme bali ni vita vilivyoanzishwa na Yazid, kutaka kutambuliwa kwake kama Khalifa pasipo haki.

Watu hao waliotoka kwa majeshi ya Yazid, ni Hurr bin Riyahi na ndugu yake na mtoto wake. Hurr ndie yule yule aliyezuia na kuuzunguka msafara wa Husayn. Kuambatana na utukufu wa tabia yake ya ukarimu, Husayn hakuukubali msamaha wa Hurr tu, bali alimuombea Dua njema. Vile vile alimruhusu kupigana na majeshi dhalimu ya Yazid.

“Utajiri bora ni kukinai; Na ufakiri ni unyonge mbele ya mtu tajiri.” Imam Hasan bin Ali (a.s)

Mauaji Ya Kikatili Ya Watu Wa Nyumba Ya Mtume

Ilikuwa Jumatano, siku ya kumi, (Ashura) ya mwezi wa kwanza wa Muharram kwa kalenda ya kiislamu katika mwaka wa 61 B.H. (13th October 680 A.D) Husayn alipomwambia mwanawe wa pili Ali Akbar, kuadhini minajili ya sala ya Alfajri ili kuwakum­busha na kuwazindua wale waliomuona na kum­sikia Mtume juu ya utakatifu wake Husayn, kwa vile Ali Akber alifanana na Mtume kwa sauti yake na umbo lake pia.

Hili lilikuwa ni lengo la kuwazindua wale walio­potea, ili kuzuia umwagikaji wa damu. Kabla ya kuamkia usiku wa tukio la Ashura (Siku ya tisa maghribi), Abbas ibni Ali ambae ndie aliyekuwa muangalizi mkubwa wa usalama katika kambi ya Husayn, ali­tokwa na machozi akiona kila mwanamke akiungana na mumewe na watoto wao wakiwahimiza kujitolea kufa kwa kumsaidia Husayn. Huu ndiyo ulikuwa uthabiti wa imani yao kwa Imam. Husayn alipanga vikosi vya usalama, chini ya uongozi wa nduguye Abbas ibni Ali kuji­tetea mbele ya majeshi dhalimu ya Yazid.

Kama ilivyo, Husayn hakutarajia kupata sifa na ushindi akijitetea na akali ya watu aliyokuwa nao bali alikuwa na lengo la kuwakilisha na kudumisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu kutoka kwa Mtume wake aliyem­chagua. Alipochoka kuwasairi maadui wake,

Husayn aliangua kilio na kuita:

“Iwapo dini ya Muhammad, haiwezi kunusurika bila ya ushahidi wangu (kukutuliwa), basi enyi mapanga, njooni mpate kunimaliza”.

Kufikia wakati wa adhuhuri nusu ya watu wa Husayn walikwisha kukutuliwa (kuwa mashahidi) na baada ya kumalizika mashujaa wao ikaja zamu ya watu wa ukoo wa Hashimiya ingawa wafuasi hao walipigana na maadui mpaka dakika yao ya mwisho wa pumzi yao, hawakukubali vijana wa Hashimiya waingie vitani. Husayn juu ya fahari ya watu wake alitangaza akisema: “Hakuwa babu yangu wala baba yangu wala ndugu yangu aliyekuwa na watu waaminifu kama hawa wangu.”

Mmoja baada ya mmoja watu wa Husayn na marafiki zake walima­lizwa, akiwamo Habib ibni Mazahir mwenye umri wa miaka thamanini na sita aliyekuwa rafiki yake mpendwa tangu siku zao za utotoni, Muslim ibni Ausajah, Hurr ibni Riyahi, John na Wahab na baadhi ya wengine.

Wafuasi hawa hawakutokana na asili moja, kabila, wala nchi. Miongoni mwao mulikuwa na waafrika kumi na watatu waliojitolea kupigania upande wa Husayn wakawa mashahidi minajili ya dini ya Kiis­lamu na Mwenyezi Mungu. Ilipofika zamu ya vijana wa Hashimiya, waliokuwa baina ya umri wa miaka sita hadi thelathini na nne, hapo Husayn alimtoa kijana wake wa pili Ali Akbar aingie katika uwanja wa vita. Husayn alisema iwapo Mtume angekuwa pamoja nao katika vita hivi, basi yeye Husayn angechukua nafasi badala ya Ali Akbar kuunusurisha Uislamu.

Ali Akbar alifanana na Mtume katika kila njia na fani ya maisha yake hata kwa usemi wake na mwenendo wake wa tabia na umbile na alikuwa mzuri mno katika vijana wa Hashimiya na yeye alishahidiwa katika uwanja wa vita.

Habari za kifo cha kijana huyu, zikamfanya Husayn kuomboleza na kujiuliza: "Ni kitu gani kilichobaki ulimwengu huu baada ya kuondokewa na wewe?"

Qassim mtoto wa Hasan ibni Ali, ambae ombi lake lilikubaliwa baada ya kunyenyekea sana, alijitolea na kwenda vitani, alikuwa na umri wa miaka kumi na mitatu tu, kisha alikuwa ni yeye pekee ukumbusho wa Hasan kaka yake. Qassim alikanyagwa kanyagwa na kuthinyangwa na mafarasi wa maadui akiwa hai hata akafa.

Bibi Zainab, aliyeandamana na watoto wake wawili, Aun na Muhamad, wenye umri wa miaka sita na saba hivi walijitolea vitani na mara walikutuliwa pia, na Zainab akawachwa pekee. Mmoja baada ya mmoja vijana wote wa Hashimiya waliingia uwanja wa vita na kushahidiwa. Hatimaye kabla ya zamu ya Husayn mwenyewe kufika kwenda kupigania Uis­lamu, ndugu yake Abbas ibni Ali aliyekuwa shujaa mno mwenye nguvu na ujuzi mwingi wa kijeshi, alinyenyekea sana akitaka ruhusa ya kwenda yeye vitani ingawa alikatazwa mara nyingi. Badili yake, Abbas akaagizwa akateke maji kwa ajili ya watu wa nyumba kutoka mto wa El-Furat.

Ilikuwa ni siku tatu tangu jamii ya Mtume kuishiwa na maji ya kunywa toka watu wazima hadi mtoto mchanga wa miezi sita hawakuwa na tone la maji. Abbas ibni Ali aliji­tahidi, akafanikiwa kuteka na kujaza kiriba wa maji kutoka mtoni na alipokuwa akirejea huku amebeba kiriba chake, maadui walimshambulia kutoka nyuma waki­hakikisha kwamba maji hayakufikia watoto wa kambi ya Husayn bali na kumuua nduguye Husayn aliye­kuwa mpiganaji hodari, kion­gozi mtukufu wa majeshi yote, akabakia Husayn peke yake.

“Kwa hakika kifo (shahada) cha Husayn kitaamsha mori katika nyoyo za waumini ambao hautapoa milele.” Mtume Muhammad (s.a.w.w)

Mwisho Wa “Watu Wa Nyumba” (Utaji)

Akijikuta peke yake pasi kuwa na mtu aliyeko ndani wala nje ya kambi yake, Husayn aliita kwa sauti: “Je... yuko yeyote wa kutusaidia?, yuko yeyote wa kutuitikia na kututimizia haja yetu?” Mwito huu haukuitikiwa na yeyote ila mtoto mchanga Ali Asghar ibni Husayn aliyekuwa wa mwisho katika watoto wake, ambae alikuwa na umri wa miezi sita tu, aliangua kilio kana kwamba kuitikia mwito wa babaake.

Husayn alimbeba mtoto huyu mchanga akipapatika mikononi mwake kwa kiu ya maji, mtoto huyo hakuweza kustahimili dhiki, Husayn alitoka nae nje lakini ah... maadui walimjibu kwa kumfuma mtoto huyo kwa mshale wa vyembe vitatu na mtoto akafa mikononi mwa babaake. Husayn alirudi katika hema lake na mwili wa mtoto mikononi mwake. Mamaake alipomuona aliliya na kuomboleza akisema: “Je watoto wa umri wenu pia huuliwa namna hii?”

Husayn hatimae alimchimbia kaburi ndogo kwa upanga wake na kumzika mtoto huyo. Baada ya mazishi ya mtoto Ali Asghar yasiyo kuwa na sherehe yoyote, Husayn aliingia tena kambini, akamwita kila mwanamke mmoja mmoja aliyekuwako na watoto, akawaaga kwaheri ya mwisho, akamuaga dadake Zainab pamoja na binti yake Sakina aliyekuwa kipenzi cha moyo wake, ambae alikuwa na umri wa miaka minne tu. Alimnasihi kuvumilia na kuwa na subira juu ya dhuluma yote yatakayo kuja, kwa sababu ya matakwa ya Mwenyezi Mungu, kupitia kwa Mtume wake mtukufu, ni muhimu kuliko kumhusu yeye mwenyewe. Katika dini ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake mtukufu, hayana budi khususan kumu­husu yeye mwenyewe.

Hatimaye akiandamana na Zainab, Husayn aka­mwendea mtoto wake mkubwa, aliyekuwa akiugua siku nyingi, Ali Zainul Abideen, ambae ni mtoto mkubwa katika watoto wake na khalifa wakuelekea.

Ali ibni Husayn, alivyokuwa katika hali ya maradhi kwa muda wa siku nyingi, hakuwa na khabari yoyote juu ya matukio ya siku na vifo vya watu wote wa babaake, alishtushwa na majeraha yaliyo­mpamba babaake Husayn. Husayn alimtuliza na kumuaga kwaheri. Alipanda farasi wake mara ya mwisho akisaidiwa na dadake Zainab. Sasa Zainab ndiye mwangalizi mkuu wa usalama na jeshi katika kikundi chake kilichokuwa hakina yeyote, ila Zainul Abideen, Ali ibni Husayn na wanawake waliopo­telewa na waume zao, watoto na ndugu zao kwa ku­shahidiwa vitani na baadhi ya watoto wachache.

Husayn alisimama kati kati ya maadui na kuwaita akiwaambia wamuachilie na kusalimisha maisha yake ili apate kwenda zake baada ya kumuulia watu wake wote, marafiki zake, ndugu zake na wajomba zake na watoto wake ndani ya siku moja.

Jawabu lake alijibiwa kwa umoja wa maadui, kwamba hawatamuachilia hadi atakapomtambua Yazid licha ya alivyodokezewa na Mtume. Husayn hapo alisema na kujitambulisha nafsi yake mbele ya majeshi ya Yazid kwamba yeye ni mjukuu wa Mtume, mtoto wa Ali na Fatimah binti ya Mtume na ndugu yake Hasan na kuimwaga damu yake ha­kutawafalia chochote katika ulimwengu wao sasa na wa baadaye pia. Alijaribu pia kuamsha fikira zao akiwambia: “iwapo hamuamini katika dini yoyote basi fikirini kama watu walio huru” (kwamba yatendwayo si haki).

Husayn mwenye umri wa miaka 57, bado alikuwa mkakamavu na mvumilivu juu ya kupoteza watu wake 72, katika kambi yake ambamo walikuwako miongoni mwao watu 18 wa jamii yake, ukoo wa Abu Talib. Naam, Husayn sasa alipigana kishujaa na maadui zake hata kufikia wakati wa sala ya Al-asiri, Umar bin Sa’ad aliamuru vikosi vyote vya majeshi yake wamzingire kwa umoja na kupigana naye.

Katika kipindi hicho ardhi yote ilitingishika, na jua lilipatwa na kutanda kiza cheusi kwa kutangazwa, “Husayn ameuawa katika Karbala, Husayn ameku­tuliwa katika Karbala” miongoni mwa sauti za maadui ilisikika na kuleta takbira ya “Allahu Akbar”, Mungu ni mkubwa, kwamba jamaa wa mwisho, mtakatifu wa nyumba ya Mtume (utaji) amean­gushwa na kukatwa kichwa akiwa na njaa na kiu na Shimer ibni Joshan kwa tamaa ya kidunia aliyoa­hidiwa na Yazid.

Dhuluma yao haikukomelea hapo kwa kumkutuli Imam Husayn, bali mwili wake pamoja na miili ya wenzie wote ilikanyagwa kanyagwa na kuvurugwa na kwato za farasi wa maadui kiasi cha kuanga­mizwa kabisa. Historiya inajidhihirisha yenyewe.

Baadaye majeshi ya Yazid, yaliwavamia watu wa nyumba ya Mtume na kuzitia moto hema zao, waliwapokonya wanawake mavazi yao ya mitandio na hijab za vichwani, wakawapokonya kila kitu chao kichache walichokuwa nacho, waliwapokonya hata na bembeya ya mtoto Ali Asghar; jamii ya Mtume ilitendewa kinyama ikidhalilishwa na kuchukuliwa mateka.

Zainab binti Ali, “Fatimah” wa pili na mshirika wa Husayn alijitolea kishujaa nakusimama imara, akijipa nguvu na kupiga moyo konde, alivuta subira, baada ya kupotelewa na waume wote, alishika jukumu la kuwa­kinga na kuwasaidia wanawake wote na watoto pamoja na Zainul Abideen aliyekuwa mgonjwa akiugua ndani ya hema lililoshika moto na kuziponya nafsi zao. Alikuwa ndiye mwangalizi wao, mkuu wa usalama, alisamehe usingizi na kujitolea kukesha usiku kucha akitekeleza jukumu lake kuihudumia jamii yake iliyo athiriwa.

“Iwapo hamuamini katika dini yoyote basi tafakurini japo kama watu walio huru.” Imam Husayn bin Ali (a.s)

Watu Wa Nyumba Ya Mtume Wakiwa Kizuizini

Ilikuwa siku ya kumi na moja ya mwezi wa Muharram mwaka mpya wa kiislamu, Ali ibni Husayn, ambae daraja yake na heshima yake tukufu imeambatana na ‘fakhari ya swalihina’ Zainul Abideen na ‘kiongozi wa wenye kusujudu’ Sayyidu Sajideen, alichukuliwa akafungwa kwa mnyororo mzito pasi kuhurumiwa juu ya hali yake ya ugonjwa. Wanawake na watoto wa nyumba wote walichukuliwa na kufungwa kwa kamba pamoja, walipandishwa juu ya migongo ya ngamia pasi kuwa na matandiko ya kukalia, na maiti za wale waliokutuliwa (mashahidi) ziliachwa vile vile pasi kuzikwa.

Wafungwa hawa walichukuliwa kutoka Karbala na kupelekwa Sham (Damascus), Jiji kuu la utawala wa Yazid, kupitia Kufa, ambako ni umbali wa mwendo upatao maili elfu moja, kukiwa na jua na joto kali lenye kuchoma katika jangwa. Njiani walimopitia, katika kila kijiji, “watu wa nyumba” walitembezwa na kutambulishwa kwa wana kijiji wa pale katika hali ya kufedheheshwa mno. Wanawake ilibidi wafunike nyuso zao kwa nywele zao za kichwani, kwa sababu ya kupokonywa hijabu zao au vitambaa vya kufunga vichwani, majeshi hayo ya Yazid aliyejiona khalifa hayakuwa na heshima wala majuto japo tembe juu ya watu hawa watakatifu wa nyumba ya Mtume, licha ya adabu mbele za wanawake hata kuwatendea haki mayatima kama yalivyo mafunzo ya Mtume na pia kuelezwa katika kitabu kitakatifu cha Qur’an.

Wafungwa hawa, kisha walipelekwa katika baraza ya ibni Ziad, huko Kufa. Ibni Ziad alikuwa mtoto wa haramu wa Abu Sufyan, hivyo ni ndugu wa Muawiya. Tabia zake za hila na ubaya na ukatili usiokuwa na huruma zilijulikana kote katika ulimwengu wa waarabu.

Aliwapokea wafungwa hawa watakatifu wa nyumba ya Mtume kwa shangwe kuu. Aliamrisha kila pembe ya mji wa Kufa barabara zake zipambwe kwa ma­pambo mazuri mazuri na kushangilia ushindi wa Banu Umayya juu ya ‘Ufalme’ wa Hashim na watu wa nyumba ya Mtume Muhammad, watembezwe mbele za umati walio kusanyika. Katika msafara mmoja kama huo, Ibni Ziad alipomchochea bibi mta­katifu Zainab aliyeheshimiwa sana akashangazwa mno kumwona bibi huyu (simba mke) alivyomjibu kishujaa katika barabara ya mji kwa sauti ya juu pasi kumjali hata watu wakadhania kwamba ni sauti ya Ali ibni Abu Talib alipohutubu pasi na uoga: “Kama wewe ni mtoto mmoja wa watumwa aliye­nunuliwa na kukom­bolewa...” Hapo akamweleza mababu na babu zao wa ukoo wa Umayya walio­kombolewa na kuachiliwa huru na Mtume Muhammad wakati wa ushindi wa kutekwa Makkah.

Ama hotuba ya Zainab katika Kufa ilishitua na kuzi­ndua watu wa Kufa hata Ibni Ziad akawa hawezi tena kuwazuilia, kwa hivyo aliamua kuwahamisha mara moja. Labda alisahau kwamba wanawake hawa si kitambo kirefu, (miaka ishirini tu) iliyopita walikuwa ni mabanati watakatifu katika utawala wa Kufa wakati wa ukhalifa wa Imam Ali aliyekuwa na jiji lake kuu hapa hapa.

Wale watu wa nyumba ya Mtume, walipelekwa Sham (Damascus) pamoja na vichwa vilivyo anguliwa vya hao mashahidi kama alama ya kuonyesha ushindi wa Banu Umayya katika kasri kuu ya makao ya Yazid. Mateka hao waliwekwa kizuizini kwa muda wa mwaka mzima.

Katika tukio moja la baraza la Yazid, alimdhihiki Ali ibni Husayn, akimuuliza: “Je, N’nani mshindi mkuu na shujaa aliyetambulika katika vita hivi?”

Ali ibni Husayn, Zainul Abedeen, alimjibu: “Ushindi mkubwa na ushujaa uko upande ule ule wenye lengo lililobakia la dini, madamu mwito wa Muhammad Rasulullah (Muhammad ni Mtume wa Allah) kutajwa baada ya Allahu Akbar (Allah ni mkubwa) kuta­endelea kudumu, basi Husayn ni mshindi mkuu.”

Yazid, alitumia njia zote za hila na udhalimu na unyama wake juu ya kuwatesa na kuwaadhibu watu wa nyumba ya Mtume wakiwa kizuizini katika gereza la Damascus mpaka siku moja Sakina binti Husayn alikufa akiwa kizuizini. Ama tukio la kifo cha mtoto huyu Sakina, lilishutua watu, walianza kukusanyikana na kuungana dhidi ya majeshi na kumkera Yazid wakitaka watu wa nyumba ya Mtume waachiliwe mara moja. Yazid alitambua sasa tisho lao juu ya utawala wake ambao wazee wake walipanga kwa hila na kumrithisha, alilazimika kukubali ombi lao na kuwaachilia watu wa nyumba ya Mtume katika mwaka wa 62 B.H. (862 A.D) Hakuwaachilia na kuwapa heshima zao tu, bali aliwakubalia matakwa yao ya kuadhimisha siku za maombolezo wakiwa Sham (Damascus) kabla ya marejeo yao Madina.

Ali ibni Husayn, aliwasili Madina na baada ya kupi­tia ziara ya babake aliyeshahidiwa pamoja na wenziwe wote katika Karbala, lakini alikuwa ni yeye mmoja tu, mwanamume kutoka jamii yake aliyerejea.

Bashir ibni Jazlam ndie aliyeongoza msafara huu uliovunjikwa na moyo.

Walipokurubia kuta za Madina, Binti mdogo wa Ali ibni Abi Talib aliangua kilio na kuomboleza: “O jiji la babu yetu (Mtume mtukufu) usitukubalie sisi... kwa heshima tuliondoka hapa, tumeteseka na kutendewa kinyama, tumerejea pasi na mashujaa wetu na watoto wetu.” Msafara ulisimama kando nje ya jiji la Madina, Bashir aliteremka na kuingia mjini akito­ngoa khabari zenye kuliza na kumiminikwa na machozi.

“Enyi watu wa Madina, mjukuu wa Mtume alisha­hidiwa katika Karbala na jamaa zake wamerejea.” Kwa kusikia tangazo hili lenye kushutua na kuhu­zunisha mno, watu wote wa Madina walikusanyika katika msikiti mtukufu wa Mtume, ambapo kila mmoja mke kwa mume aliomboleza.

“Tahadhari na uepukane na Ushirika wa mtu dhalimu maana yeye hukuuza kwa kupata tonge moja (ya chakula) ama kiasi kidogo zaidi ya hicho.” Imam Ali ibni Husayn (a.s)

Bayana Wazi

Yazid baada ya yote hayo, alihisi na kujiona kashindwa, kwa hivyo alikusanya majeshi ya watu wapatao elfu kumi na kuwapeleka Madina ili kwenda kuharibu haribu na kuhasiri watu wa huko, katika mwaka wa 62 B.H. (681 A.D) mara baada ya rejeo la Ali ibni Husayn.

Majeshi hayo dhalimu hayakutosheka na kuhasiri watu wa Madina na kubomoa nyumba zao bali walihakikisha walimkosea adabu hata Mtume mtu­kufu kwa kuwafungia farasi zao na ngamia juu ya kaburi lake. Ziyada ya uharibifu na unyama wao, waliwashika na kuwanajisi wanawake wa kiislamu na kuwaulia waume zao. Hatimaye mwaka wa 63 B.H. (682 A.D) Yazid alitoweka ghafla pasi kujuli­kana alikotokomea.

“Uhusiano wa ushirika na tangamano la jamii na watu watendao dhuluma na ukatili, husababisha lawama na kutoaminiwa.” Imam Husayn ibni Ali (a.s)

Mtoto wake, Muawiya wa pili, alikamata ufalme na kutawala baada ya kutoweka Yazid. Mara tu Muawiya wa pili aliposhika ufalme aliwashambulia na kuwa­laumu wazee wake wote waliotangulia kwa sababu ya kuifuja haki ya watu wa nyumba ya Mtume, na kuwa­endea kinyume cha sharia. Naye hakuendelea kutawala mara alijiuzulu kutoka kiti cha ufalme.

Utawala dhalimu wa Banu Umayya, haukuishilia hapo, kwa sababu ya vikundi vyao vya njama walihakikisha kuendeleza utawala wao hadi mwishoni mwa mwaka wa 132 B.H. (749 A.D) ndipo walipofikilia ukomo wao. Ali ibni Husayn, fakhari ya wenye kuabudu katika muda wa miaka arubaini (40) baada ya tukio la kuhu­zunisha Karbala, aliendelea kuwafundisha na kuwa­elimisha wananchi juu ya dhuluma zilizo fanywa na Banu Umayya, naye mwishowe alitiliwa sumu na Hisham ibni Abdul Malik, akafa katika mwaka wa 98 B.H. (716 A.D).

Mwaka wa 102 B.H. (720 A.D) kundi la ukoo wa Banu Abbasiya walianza kupigana na Banu Umayya ambao mwisho wao walishindwa na nguvu za Banu Abbasiya. Katika muda wote huu wa vita baina ya Banu Umayya na Banu Abbasiya, wakishughulika na kupigana, kung’ang’ania ufalme wa Hijaz, Muhammad ibni Ali (Al-Baqir) na Ja’fer ibni Muhammad (As-Sadiq) wote wakiwa ni dhuriya wa Mtume mtukufu waliotokana na nasaba ya Husayn bin Ali walijitolea kueneza na kufunza watu mafunzo tofauti kwa umma.

Mafunzo haya yalifikia kilele wakati wa Ja’fer ibni Muhammad (As-Sadiq) ambapo takribani wanafunzi wapatao elfu nne walielimishwa taaluma tofauti chini ya uangalizi wake. Wataalamu wakubwa kama Abu Hanifa na Avicenna (Ibne Sina) ambaye alikuwa mashuhuri katika mafunzo ya hesabu na elimu ya utambuzi ni katika baadhi ya wanafunzi waliosifika wa Ja’fer ibni Muhammad (As-Sadiq).

Ama tukidhukuru na kuichunguza hali ya historia na tukio lake, itaeleweka wazi kwamba mauwaji ya kikatili yaliyotokea Karbala katu hayakuwa ni ajali, bali nitukio lililopangwa na hakikisho dhidi ya Mtume na watu wa nyumba yake kabla ya mauaji ya Ashura. Vilevile imedhihiri pasi na shaka yoyote kwamba ni mashambulizi dhidi ya Islamu dini tukufu ya Mwenyezi Mungu na watu walioabudu masanamu, wasiokuwa waumini, waliojibandikiza majina ya kiislamu, lakini hawakupendezewa na dini tukufu ya Mwenyezi Mungu.

Shukrani kuu, kwa jitihada ya mashujaa wa Karbala, waliojitolea na kukabiliana na mapambano na ku­shahidiwa katika njia za haki wakipigania Uislamu. Leo jina la mtukufu Mtume Muhammad likifuatana na jina la Mwenyezi Mungu linasikilika mara tano kwa siku katika wito wake wa ibada kutoka kila pembe ya dunia. Mafunzo ya Mtume ya kuwa na tabia njema na mavazi rasmi ya sitaha kwa wanawake, (Hijab, mitandio na vitambaa vya ki­chwani) vinaendelea kutumiwa kote. Na Uislamu ungali hai. Kwa hivyo ushindi ni wa Husayn.

Imam Shafi amesema: “Sala zetu hazikamiliki iwapo hatuwasalii enyi watu wa nyumba ya Mtume.”

Watawala kama Banu Umayya na Banu Abbasiya walikuja na wakaondoka, nguvu za utawala walizi­pata na kuzipoteza, walitenda ukatili wao na udikiteta wao na kuwasumbua watu wa “nyumba ya Mtume” na kuzidisha sheria zao za kutawala kinguvu lakini Husayn anatawala nyoyo za walimwengu hata leo.

Siku zimebadilika katika majuma, miezi na miaka hadi karne, katika vizazi na vizazi hakuna akumbu­kwae kwa usawa ila Husayn, roho huliliwa na kuomboleza juu ya kifo chake, wengine japo kwa masaa machache na wengine kwa miezi lakini wa­kati husahaulisha yaliyopita ila Husayn, jinsi alivyotendewa kinyama na kukutuliwa pamoja na wenziwe wote katika uwanja wa Karbala, hakutasa­haulika na ni kama moto unao waka ndani ya nyoyo za waumini, ambapo kila mwaka mashiko yao huka­zanishwa na kurejelea upya wake.

“Na musiwadhanie wale waliouliwa katika njia za Allah kuwa maiti la-Hasha, wao wangali hai na wanaruzukiwa na Mola wao.” (Qur’ani 3:169)

Msimamo wa Husayn ungali hai na mhanga aliyo­jitolea haupuuzwi, yeye ni mfalme mkuu katika mashahidi na daima yumo ndani ya nyoyo za mmoja na wote. Waumini kote ulimwenguni, siyo kumta­mbua na kumuheshimu tu, bali kila mwaka ifikapo siku kama hii (Ashura) kumbukumbu za tukio la ku­shahidiwa kwake huadhimishwa. Ana heshimiwa baada ya Mtume Muhammad, babake Ali ibni Abu Talib, mamake Fatimah binti Muhammad na ndugu yake Hasan ibni Ali.

Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yao pamoja na kizazi chao.

Hapa tuna furaha kuwaletea utenzi huu tulioupokea kutoka kwa malenga mashuhuri Al-ustadh Bahri D.P. wa Mombasa.

Mauwa Ya Peponi

Mauwa matakatifu, Ya bustani nadhifu,

Yaliyopamba sharafu Ya jamii Hashimiya.

Mauwa yalo abadi Yapembeo “Mashahidi”,

Toka jadi na jududi Ya jamii Hashimiya.

Mauwa yaliyoshani, Yalotukuka peponi,

Ni Hasani na Huseni, Ya jamii Hashimiya.

Mtume ndo shina lao, La jivuli na uzao,

Na Ali pamwe nao, Ya jamii Hashimiya.

Fatimah mlezi wao, Binti asifiwao,

Peponi yao makao, Ya jamii Hashimiya.

Ashura ili yaumu, Iloogesha kaumu,

Kwa mito yao ya damu, Ya jamii Hashimiya.

Twarikhi iloandikwa, Milele itakumbukwa,

Hadi sikuye kufikwa, Ya jamii Hashimiya.

Pamwe na wote ambao, Waliyotoka makwao,

Kufuata sabili yao, Ya jamii Hashimiya.

Watakumbukwa dahari, Kwa laili wa nahari,

Mashahidi, wafakhari, Ya jamii Hashimiya.

Ya rabbi uwaliwaze, Mahali pema walaze,

Mashahidi watulize, Ya jamii Hashimiya.

Ya Rabbi Mola wa haki, Twakuomba tubariki,

Tusikose itifaki, Ya jamii Hashimiya.

Tamma nasi waumini, Utuuongoze manani,

T

Share this article

Comments 0

Your comment

Comment description

Latest Post

Most Reviews

MOST READ