Rafed English

Amani na Jihadi Katika Uislam

Amani na Jihadi Katika Uislam by : Sayyid Muhammad Rizvi

 

“Nasi Hatukutuma Ila Uwe Rehema Kwa Walimwengu (21:107)

“Nimeumchunguza yeye (Mohammad). Ni umtu anayevutia ajabu; na kwa maoni yangu, mbali na kuwa mpinga Kristo, ni lazima aitwe mwokozi wa wanadamu.”

“Nina amini kwamba endapo umtu kama huyo angeshika udikteta wa ulimwengu wa kisasa, ange fanikiwa katika kutatua matatizo yake katika namna ambayo ingeuletea ile amani na furaha inayohitajika hasa”

“Kama dini yoyote ingekuwa na fursa ya kutawala uingireza, hasha, bali Ulaya nzima katika kipindi cha miaka 100 ijayo, itakuwa ni Uislamu.”

“Siku zote nimeichukulia dini ya Mohammad katika hadhi ya hali ya juu kwa sababu ya changamoto zake za ajabu. Ndiyo dini pekee ambayo kwangu mimi ninaiona kuwa na uwezo wakuwiana mabadiliko ya kila zama za maisha ambayo inaweza kuvutia katika kila zama.”
George Barnard Shaw
katika “The Genuine Islam” Juz. 11 na. 8 (1936)
Kijitabu kilichoko mikononi mwako ni tarjuma ya Kiswahihi kutoka Kiingereza.

Ni tafsiri pana ya khutba iliyotolewa na mmoja wa wanachuoni wetu mashuhuri wa Kiislamu Sayyid Muhammad Rizvi, katika Bunge la Canada, Ottowa tarehe 20 Septemba, 2006 katika lugha ya Kiingereza.

Tarjuma yake inatolewa hapa kwa faida ya ndugu zetu wazungamzaji wa Kiswhili wa Afrika ya Mashariki na pengine popote.

Amani na Jihadi. ni mada ambayo imetumiwa nje ya muktadha wa Kiislamu dhidi ya Uislamu na vyombo vya habari visivyo amini (Uislamu) vya mlengo wa kulia, wanasiasa na pia wanahistoria.

Sayyid Muhammad Rizvi kwa ufupi anaelezea hapa kuhusu amani na Jihadi kama ilivyo katika Uislamu.

Kwa hakika wasomaji wasio na upendeleo watafaidika kutokana na toleo hili.

Tunawashukuru wale wote ambao kwa njia moja au nyingine wamechangia katika utoaji wa tarjuma hii ya Kiswahili ambayo inawasilishwa hapa.
Mchapishaji:
Al-Itrah Foundation
S. L. P. 19701
Dar-es- Salaam , Tanzania
Mnamo tarehe 11, Septemba, 2001, watu wachache waliteka nyara ndege ne za kiraia na kuzitumia kama silaa kuzua hofu ndani ya Marekani, hususan kwenye yale majengo mawili ya kituo cha Biashara cha Ulimwengu. Wafanyakazi wote na abiria katika ndege hizo, na vile vile takriban raia wapatao elfu tatu walipoteza maisha yao katika mashambulizi yake.

Sera za mambo ya nje za Marekani kuhusiana na nchi za Kiislam hazithibitishi uhalali wa kwamba raia wa Marekani waliokuwa ndani ya ndege zile na yale majengo ya Kituo cha Biashara cha Dunia wauawe. Hivi sivyo Uislam unavyofundisha. Hebu yaangalie yale maelekezo ya Mtukufu Mtume (s.a.w.) katika wakati wa vita: Yeye kwa uwazi kabisa alikataza mauaji ya wazee, watoto na wanawake.1 Wale ambao walipoteza maisha yao katika yale majumba marefu ya kituo cha Biashara cha Dunia na ndani y a ndege zile wote walikuwa ni raia, na wachache wao walikuwa ni Waislam.

Viongozi wote wa Kiislam ndani ya Marekani, Canada, na Duniani kote kwa uwazi kabisa walishutumu utekaji nyara ule ambao ulitendwa huko Marekani kama ni kitendo cha kigaidi ambacho hakikubaliki katika Uislam.

Shutuma hizo ziliegemea kwenye thamani ya kidunia ya utukufu wa maisha ya mwanadamu. Qur’an Tukufu inasimulia kisa cha mauaji ya kwanza katika historia, kile cha watoto wawili wa Adam (a.s.) ambamo Qabil (Cain) alimuua ndugu yake, Habil (Abel). Hili liko katika Sura ya 5 ya Qur’an Tukufu, aya ya 27 hadi 31.

Mwishoni mwa kisa hiki, Mwenyezi Mungu anasema:

“………………yeyote atakayemuua mtu ambaye hakuua, au kufanya uchafuzi katika nchi, basi ni kama amewaua watu wote, na mwenye kumwacha mtu hai ni kama amewaacha watu wote hai……….” (5:32)

Ni dhahiri kutokana na aya hii kwamba (1) isipokuwa kama mtu ameshitakiwa na kuthibitika kuwa amemuua mtu, yeye hawezi kuuawa – na (2) kwamba kumuua mtu asiye na hatia ni sawa na kuua watu wote.
Hivyo ni Vipi Kuhusu Jihadi?
Moja ya mambo yaliyo kinyume ya zama hizi ni kwamba ingawa njia za mawasiliano zimeendelea kwa kiasi kikubwa mno, watu bado wana matatizo katika mawasiliano yenye maana ya makusudi kabisa na mazungumzo na tamaduni nyingine na dini mbali mbali. Kuna upotovu wa taarifa mwingi na kutoeleweka kwa imani ya Kiislam.

Watu wengi binafsi, wale wa kawaida na wataalam pia wamejaribu kuiunganisha tarehe 9/11 na dhana ya Jihadi katika Uislam. Katika moja ya mazungumzo ya maonyesho ya redio ya Toronto, mara baada ya Septembea kumi na moja, nilimsikia mpiga simu mmoja akasema kwamba kile kilichotokea siku ile kilikuwa kwa 10% ni ugaidi na 90% ni Uislam. Kiongozi mmoja wa kikristo mwenye siasa kali huko Marekani alisema katika onyesho lake la kwamba “Yumkini (inawezekana) Muhammad alikuwa gaidi.”

Hivyo ni muhimu kuzungumza Kuhusu Jihadi katika Uislam.
a) Uislam ni Dini ya Amani
Uislam kimsingi ni dini ya amani. Jina lake “Islam” linatokana na neno la kiarabu “Silm” ambalo lina maana mili: moja ni “kujisalimisha kwa Mwenyezi Mungu” na ya pili ni “amani”. Maana zote zinaingiliana.

Wakati wowote Waislam wanapokutana, wanatumia maamkizi ya amani “as-salaam alaykum – amani iwe juu yako,” na huyo mtu mwingine anajibu kwa kusema “alaykums-salaam – juu yako iwe amani.”

ISLAM
SILM
1. Kujisalimisha kwa Allah
2. amani (kwa wanadamu wenzio)

Sala za kila siku zinaanza na kumsifu Allah kama “Rehema na Mwenye fadhila” na zinaishia na salam za amani kwa wote.
b) Dhana ya Jihad
Dhana ya Jihadi inahitaji kueleweka vizuri. Watu wengi katika vyombo vya habari wanayachukulia maneno ya Qur’ani nje ya muktadha wake. Na kwa hiyo hebu tuone ni nini maana ya Jihadi?

Hili neno “Jihad” halina maana ya “vita takatifu.” Huu ni utoaji wa ki- magharibi wa dhana pana katika mafundisho ya Kiislam. Muulize mtaalam yoyote yule wa lugha ya kiarabu na atakwambia kwamba “Jihad” haina maana ya “vita takatifu.” Maneno, au usemi huu wa “vita takatifu” umekuja kutokana na dhana ya Kikristo ya “vita ya haki,” na umetumika hovyo hovyo kama lahaja ya Kiislam tangu zile siku za Krusedi.

Hivyo basi, Jihadi ina maana gani?

Katika lugha ya kiarabu, neno Jihadi kwa maana halisi ni kujitahidi na kufanya kazi kwa bidii sana kwenye jambo fulani. Katika Istilahi za Kiislam, linabakia na maana halisi hizo katika vipimo viwili tofauti, ambavyo vinaelezewa kwa “Jihadi kubwa” na “Jihadi ndogo.”

Jihadi kubwa – inajulikana kama mashindano ya kiroho, mashindano kati ya nguvu mbili ndani yetu: nafsi na mwili. Moyo unapambana na matamanio ya kimwili. Mapambano haya ya kiroho ni Jihadi inyoendelea ndani ya kila mmoja wetu. Uislam unawatarajia wafuasi wake kutoa kipaumbele kwenye nafsi na dhamira juu ya mwili na tamaa zake.

Kule kufunga katika mwezi wa Ramadhani ni mfano wa mafunzo ya kila mwaka kwa ajili ya Jihadi hii.

Jihadi ndogo ni yale mapambano ya silaha. Hata hivyo, hii haina maana ya moja kwa moja kwamba ni matumizi ya kufanya vurugu za kidhalimu zisizo na haki. Hii Jihadi ndogo inaweza kugawanywa kwa namna mbili: Uchokozi na ulinzi. Uchokozi na uvamizi dhidi ya watu wowote wale hauruhusiwi katika Uislam; kwa hali yoyote ile, ulinzi ni haki kamili ya kila mtu na kila Taifa.

JIHAD
(Mapambano)
KUBWA NDOGO
(ya kiroho) (Mapambano ya silaha)
Ulinzi Uchokozo

Uislam umeruhusu hii Jihad ndogo kwa ajili tu ya kuwalinda Waislam na ardhi zao, na kudumisha amani katika jumuiya za Kiislam.
Jihadi Ndani ya Qur’ani Tukufu

a) Aya za mwanzo
Hebu sasa tuende kwenye baadhi ya aya kutoka kwenye Qur’ani Tukufu.

Vita vya kwanza alivyopigana Mtume na wafuasi wake vilikuwa ni vita vya kujihami kiulinzi. Vinajulikana kama vita vya Badr, sehemu ambayo iko karibu na mji wa Madina (ule mji wa Mtume huko Arabuni). Hivi vilikuwa ni vita ambavyo Mtume alitoka na wafuasi wake kukabiliana na majeshi ya adui ambayo yamekuja kutokea Makkah ambako kulikuwa bado kunadhibitiwa na makafiri.

Aya ya kwanza ya Jihadi ndogo, mapambano ya silaha, ambayo ilishuka kwa wakati huo, imo kwenye Sura ya 22 ya Qur’an Tukufu, aya ya 39-40. inaelezea wazi kabisa lengo la hii Jihadi ndogo:
“Imeruhusiwa (kupigana) kwa wale ambao wanapigwa, kwa sababu wamedhulumiwa, na kwa hakika Mwenyezi Mungu anao uwezo wa kuwasaidia, wale ambao wametolewa majumbani mwao bila sabau ya haki………”
Halafutena ikizungumzia kuhusu wale makafiri wa Makkah ambao walipigana vita baada ya vita dhidi ya Mtume na wafuasi wake huko Madina, Qur’ani Tukufu katika sura ya 2, aya ya 190 inasema:
“Na wapigeni vita katika njia ya Mwenyezi Mungu wale ambao wanakupigeni vita, wala msiruke mipaka, hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wanaoruka mipaka.”
Katika aya hii, mazungumzo ni kuhusu kutoa majibu kwenye vita kwa kujilinda na kujihami wenyewe, hakuna kauli ya kuanzisha uchokozi hata kidogo. Hata katika mtindo wa mapambano ya kujihami, Mwenyezi Mungu Mtukufu bado anawaonya Waislam kwamba wasije “wakavuka” mipaka inayostahiki.
Uislam unawafundisha Waislam wawe wenye nguvu ili kuweza kujilinda wenyewe, lakini hivyo haina maana kwamba wao wawe wachokozi au madhalimu. Katika Sura ya 8, aya ya 60-61 ya
Qur’an Tukufu, Mwenyezi Mungu ametoa mwongozo huu wa jumla kwa uwazi kabisa pale ambapo anazungumza na Waislam kwa namna ifuatayo:
“Na waandalieni nguvu kiasi mnavyoweza, na kwa farasi ambao wamefunzwa (kwa maandalizi hayo) ili muogopeshe maadui wa Mwenyezi Mungu, na maadui zenu, na wengine wasiokuwa wao, msiowajua, bali Mwenyezi Mungu anawajua.”
Baada ya kutoa maelekezo hayo ya Jumla na mwongozo wa kuwa wenye nguvu na waliojiandaa tayari kwa kujilinda wao wenyewe, aya inaendelea kusema:
“Na kama wakiaelekea (hao maadui) kwenye amani, nawe pia ielekee na umtegemee Mwenyezi Mungu……..”
Kwa ufupi, Uislam unawataka Waislam kuwa na nguvu ili kwamba watu wengine wasije wakawaonea; lakini pia wanapaswa kunyoosha mkono wa amani hata kuelekea kwa maadu zao kama kuna kuwepo na mwelekeo wa amani kwa upande wa adui.
b) Tatizo la Maandiko na Muktadha wake
Baadhi ya waandishi na wazungumzaji wanazinukuu aya za Qur’an Tukufu nje ya muktadha wake na kujaribu kuulaumu Uislamu kwa kueneza vurugu na ugaidi. Wanachukua maandishi na wanayatumia nje ya “muktadha” wake.

Ni sawasawa kabisa na mtu anayetafuta ndani ya Biblia na kuchukua maneno au sentensi zifuatazo ili kuthibitisha kwamba Biblia inaendeleza vurugu:
“Chukua viongozi wote wa watu hawa na uwauwe.” (Hesabu 25:7)
“Sasa wauwe watoto wa kiume wote. Na muue kila mwanamke ambaye amelala na mwanaume, lakini muacheni kila msichana ambaye hajalala na mwanaume kamwe.” (Numbers 31:17-18)
“Muue kila mwanaume na kila mwanamke ambaye sio bikira.” (Waamuzi – 21:11)
Hakuna mtu mwenye akili timamu atakayekubali uwasilisho wa “nje ya muktadha” kama huo wa mistari ya Biblia. Hata hivyo, bado tunawaona wainjilisti na wahubiri wengi wa Kikristo wakifanya hivyo hivyo hasa kwenye Qur’an bila hata kusita kokote kule.

Hivyo hebu tuangalie baadhi ya mifano ya kuchukua “maneno” ya Qur’an Tukufu nje ya “muktadha” wake.
Mfano wa kwanza
Sura ya 2 aya ya 191 inanukuliwa kama ifuatavyo:
“Waueni popote mtakapowakuta.”
Ili kuuelewa muktadha kamili wa aya hii, soma kuanzia aya ya 190 hadi 193 kwa pamoja zote:
“Na wapigeni vita katika njia ya Mwenyezi Mungu wale ambao wanakupigeni vita, wala msiruke mipaka, hakika Mwenyezi Mungu hawapendi warukao mipaka. Na wauweni popote muwakutapo, na muwatoe popote pale walipowatoeni, na fitna ni mbaya zaidi kuliko kuua. Wala msipigane nao katika Msikiti Mtukufu mpaka wao wawapigeni ndani yake. Na ikiwa watakupigeni basi nanyi pia wapigeni, kama hiyo ndio malipo kwa makafiri. Lakini watakapokoma, basi (waacheni) hakika Mwenyezi Munguni mwingi wa kusamehe, mwenye kurehemu. Na wapigeni mpaka pasiwepo na mateso, na dini iwe ni ya Mwenyezi Mungu peke yake, watakapokoma basi pasiwepo na uadui ila dhidi ya madhalimu.”
Muktadha huu unafafanua kwamba ile aya ya 191 inawaruhusu Waislamu wa Madina kujihami wenyewe kiulinzi dhidi ya uchokozi na uvamizi wa makafiri wa Makkah. Kwa hakika haisemi kwamba waende wakipita duniani kote ili kumuua kila kafiri watakayemkuta!
Mfano wa pili
Sura ya 4, aya ya 74 ambayo inadhaniwa kwamba inahimiza umwagaji damu:
“Basi wapigane katika njia ya MwenyeziMungu wale wanaouza maisha (yao) ya dunia kwa akhera.Na anayepigana katika njia ya Mwenyezi Mungu akauawa auakashinda, basi hivi karibuni tutampa malipo makubwa.”
Wale wanaoinukuu aya hii, kwa manufaa yao, kwa urahisi tu wanaiacha ile aya inayofuatia ya 75 ambayo inaelezea lengo na uhalali wa hii Jihadi ndogo.
“Na mna nini, hampigani katika njia ya Mwenyezi Mungu, na wale wanaoonewa katika wanaume na wanawake na watoto ambao husema: Mola wetu! Tutoe katika mji huu ambao watu wake ni madhalimu, na utujaalie mlinzi kutoka kwako, na utujaalie msaidizi kutoka kwako…………”
Aya hii dhahiri kabisa inawahimiza Waislam kusimama kwa ajili wanaume, wanawake na watoto wanaonewa.

Hivi dini za kimungu zisiwatetee wanaume, wanawake na watoto wanaoonewa?
Mfano wa tatu
Sura ya 9, aya ya 12: “Basi wauweni viongozi wa ukafiri.”

Hii ni sehemu tu ya fungu zima la maneno ambamo Mwenyezi Mungu anazungumzia kuhusu Waislam huko Madina na mkataba wao wa makubaliano ya kusimamisha mapigano na makafiri wa Makkah. Tazama aya ya 12 -14:
“Na kama wakivunja viapo vyao baada ya kuahidi kwao na wakatukana dini yenu, basi wauweni viongozi wa ukafiri kwani viapo vyao havina maana ili wapate kujizuia. Je, hamtapigana na watu waliovunja viapo vyao na wakafunga nia ya kumfukuza Mtume, nao ndio waliokuanzeni mara ya kwanza? Je mnawaogopa? Basi Mwenyezi Mungu anastahiki zaidi mumuogope, ikiwa nyinyi mmeamini. Peganeni nao, Mwenyezi Mungu atawaadhibu kwa mikono yenu, na awahuzunishe na akunusuruni juu yao na avipoze vifua vya waumini aondoe ghadhabu ya nyoyo zao, na Mwenyezi Mungu humkubalia toba ampendaye, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.”
Muktadha huu kwa uwazi kabisa unatoa haki ya kujihami kwa Waislam, bali kwa hali yoyote ile, hautangazi uchokozi.
Mfano wa Nne
Sura ya 9, aya ya 36: “Na nyote piganeni na washirikina.” Kwa kweli, msitari huu ni sehemu ya aya nzima ambamo Mwenyezi Mungu anazungumzia kuhusu utakatifu wa miezi minne kati ya miezi yote kumi na mbili, ambamo kupigana kumekatazwa. Kisha inasema:

“Na piganeni na washirikina kwa pamoja kama wao wote wanavyopigana nanyi, na jueni kwamba Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wanao muogopa.”
Wale wanaopenda kuzichukua aya za Qur’an Tukufu nje ya muktadha wake kwa faida yao wanaiacha ile sehemu “kama wao wote wanavyopigana nanyi.” Kama unavyoona, aya hii pia inatoa majibu kwa ule uchokozi ulioanzishwa na washirikina dhidi ya Waslamu; haizungumzii juu ya kuanza vita.
c) Hitimisho
Kutokana na mifano hii, ni dhahiri kabisa kwamba Uislam hauzungumzii juu ya Jihadi ndogo kwa ajili ya uchokozi; bali inawaruhusu Waislam kujilinda kivitendo maisha yao, mali zao na ardhi zao dhidi ya uchokozi wowote ule, na pia kupigana kwa ajili ya kukomesha udhalimu dhidi ya wanaume, wanawake na watoto wanaoonewa.

Zile aya kuhusu waabudu masanamu wa Makkah zenyewe ni makhsusi sana na zilizohusika kwa kipindi kile tu. Hebu tuangalie tena ile sura ya 22, aya ya 39 hadi 40:
“Imeruhusiwa kupigana kwa wale wanaopigwa kwa sababu wamedhulumiwa, na kwa hakika Mwenyezi Mungu anao uwezo wa kuwasaidia. Ambao wametolewa majumbani mwamo pasipo haki ila kwa sababu wanasema Mola wetu ni Mwenyezi Mungu. Na kama Mwenyezi Mungu asingeliwakinga watu baadhi yao kwa wengine, bila shaka yangelivunjwa mahekalu na makanisa, masinagogi na misikiti ambamo jina la Mwenyezi Mungu hutajwa kwa wingi. Na bila shaka Mwenyezi Mungu humsaidia yule anayemsaidia Yeye. Hakika MwenyeziMungu ni Mwenye nguvu Mtukufu.”
Uislamu unashughulika na jamii ya mwanadamu yenye uhalisia na sio ya kidhanifu. Katika maneno ya Dr. Sayyed Hussain Nasr, “Waislam wanayaona maadili ya Kikristo ni adhimu sana kwa wanadamu wa kawaida kuweza kuyafuata; inaelekea kwamba ile amri ya sheria ya kugeuza shavu la pili ilikuwa ikilengwa kwa watakatifu tu. Wakristo kwa karne nyingi hawakuonyesha kujizuia katika vita kuliko watu wasiokuwa Wakristo. Wazo lililohubiriwa na utaratibu uliofuatwa vimekuwa wakati mwingi havihusiani.” 2
Tumalizie na Sura ya 109 ya Qur’an Tukufu:
“Sema: Enyi makafiri! mimi siabudu mnachokiabudu, wala ninyi hamuabudu ninayemuabudu. Wala sitaabudu mnachoabudu. Wala ninyi hamtaabudu ninayemuabudu. Ninyi mna dini yenu nami nina dini yangu.”
 
Matumizi mabaya ya “Jihãdi”
Kwa sababu tu kwamba neno “Jihad” linatumiwa vibaya na baadhi ya Waislamu kwa ajili ya ajenda zao za kisiasa, Waislamu hawapasi kuitelekeza dhana hii tukufu ya Imani ya dini yao. Wakati wa kuzungumzia kuhusu Jihadi, mimi nimewasikia Waislam wengi wakielezea ile Jihadi kubwa (ya kiroho) tu na kukwepa kuzungumzia hii Jihadi ndogo kwa maana ya mapambano ya silaha (kijeshi) juu ya kujihami. Sisi kama Waislam, tunasimama imara mafundisho yetu na hatuhitaji kuomba samahani kwa ajili ya hilo hata kama nyoyo au nafsi zilipotoka zitateka nyara Istilahi za Imani yetu kwa ajili ya manufaa yao ya kisiasa.

Sio watu kama Bin Laden tu ambao wanateka na kutumia vibaya Istilahi tukufu za Kiislam; tumeona vile vile hata serikali ya Marekani ikitetea hii dhana ya Jihadi ndogo pale ilipokubaliana na maslahi yake binafsi ya siasa za kidunia.

Wakati wa ukaliaji kivamizi wa Urusi huko Afghanistan katika miaka ya themanini (1980’s), Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa lilitumia mamilioni ya dola kwa ajili ya kuwagawia wanafunzi wa Afghanistani vitabu vya kiada vilivyojazwa mapicha ya vurugu na mafundisho ya “Upenda Mapambano wa Kiislamu.” Vikiwa vimechapishwa katika lugha zinazotawala za ki Afghan za Dari na Pashtu. Vitabu hivi vya kiada viliendelezwa katika miaka ya mwanzoni ya 1980 chini ya msaada juu ya ukimwi (Aids) kwa Chuo Kikuu cha Nebraska – Omaha na Kituo chake cha Mafunzo yaAfghanistan. Shirika hilo lilitumia Dola 51 milioni katika program ya elimu ya Chuo hicho ndani ya Afghanistan kuanzia 1984-1994.

Vitabu vya kwanza, ambavyo vilijazwa habari za Jihadi na kuonyesha michoro ya mabunduki, risasi, askari jeshi na mitego ya mabomu, vimetumika tangu wakati huo kama kiini cha mtaala wa mfumo wa shule wa Afghanistan. Tofauti na watoto wote duniani kote kulikobakia, ambao vitabu vyao vya kiada vya hisabati vina mapicha ya matunda ya tufaha na machungwa, watoto wa Afghanistan walifundishwa kuhesabu kwa michoro inayoonyesha vifaru, makombora na mabomu ya kutegwa ardhini.

Na kwa hiyo pale ilipofaa maslahi yake ya kimkakati, wa hila, Marekani iliendeleza utamaduni wa Jihadi miongoni mwa watoto wa Afghanistan kwenye miaka ya themanini na Raisi Reagan aliwahi hata kuwakaribisha “Mujahidina” wa Afghanistani huko White House. (Hata Taleban walitumia hivyo vitabu vilivyotolewa na Marekani, ingawa chama hicho chenye siasa kali kulikwaruza na kufuta nyuso za binadamu katika kuendana na mfumo wao msingi halisi.) Kwa sasa kwamba ule utamaduni wa vurugu umekuja kuisumbua Marekani, utawala wa Marekani uko kinyume kabisana wazo la Jihadi na unawategemea Waislam kuiacha dhana hiyo kabisa kabisa.

Waislam hawawezi kutegemea kubadili mawazo yao juu ya dhana hii tukufu ya Jihadi, kwa sababu tu kwamba baadhi ya Waislam wapotovu au mamlaka kadhaa za kidunia wanaitumia vibaya Jihadi kama neno. Waislam wanapaswa kushutumu vikali.

Matumizi mabaya ya Jihadi na kwa kujiamini kabisa waithibitishe na kuitamka kwa dhati dhana hii ya Jihadi kama inavyoelezwa na Qur’an Tukufu na mifano mitukufu ya Mtume Muhammad (s.a.w.).
Vyombo vya habari na kuwapiga chapa Waislam
Kwa kuzingatia haya tuliyoyasema hapo juu, hakuna uhalali wa kuhusisha tukio la Septemba 11 na ile dhana ya Jihadi ndogo katika Uislam.

Hata hivyo, tumesikitishwa sana kuona kwamba vitengo Fulani vya vyombo vya habari, hususan vipindi vya mazungumzo ya maonyesho vya radio bado vinazidi kuchochea chuki dhidi ya Waislamu, Waarabu na ile imani Tukufu ya kuamini Mungu mmoja ya Uislam. Hii ni licha ya ukweli kwamba Waislamu kiulimwengu walikishutumu kile kitendo cha kigaidi cha Septemba kumi na moja ambamo yalipotea maisha ya watu wasio na hatia.

Kuwalenga Waislam au Waarabu kulikoegemea kwenye hatia kwa ushiriki ni makosa kabisa. Huu undumilakuwili katika vyombo vya habari kwa kweli unatisha. Hebu fikiria japo kwa muda:

Wakati bomu lilipolipuka mnamo siku za mwanzoni za mwezi wa Septemba 2001 huko Ireland ya Kaskazini karibu na shule ya katoliki katika eneo jirani la Protestante, hakuna hata mtu mmoja aliyeilaumu jamii nzima ya Waprotestanti kama “magaidi na wauaji”. Wakati wanaharakati wa IRA walipofanya vitendo vya ugaidi huko Ireland ya Kaskazini au Uingereza, hakuna hata mtu mmoja katika vyombo vya habari va Magharibi ambaye aliipachika Imani ya Katoliki jina kama “Dini ya Ugaidi.”

Pale Dr. Goldstein Mloweziwa Kiyahudi huko Israeli, alipoingia kwenye msikiti wa huko Habron miaka michache iliyopita na akawapiga risasi wafanya ibada wa Kipalestina, hakuna mtu aliyesema kwamba Wayahudi wote ni “magaidi.” Wakati Wa-Serbia walipowaua Waislam kikatili huko Bosnia, vyombo vya habari kamwe havikulilaumu Kanisa la Orthodox kwa jambo hilo ingawa baadhi ya Wahubiri wa Kanisa hilo walikuwa wakiwabariki wanamgambo wa Serbia kabla wao hawajaingia katika kuwaua wafungwa wa Kiislam.

Hata hivyo bado tunaona kwamba wakati Waarabu au Waislamu wachache wanapofanya vitendo vya kuogofya, Waislam wote na Waarabu wote wanapewa jina la “magaidi na wauaji” moja kwa moja. Kama Waislam, tunaviomba vyombo vya habari kutenda haki na sio jingine lolote.

Vyombo vya habari vinapaswa kutambua kwamba wale wateka nyara ambao walitumia ndege zile kama silaha hawakuteka nyara tu zile ndege na kuua maelfu ya watu wasio na hatia huko Marekani; vile vile wamewaonea na kuwaathiri Waislam bilioni moja na ambao sasa wamepewa au kupachikwa jina kama “wauaji na magaidi.”

Share this article

Comments 0

Your comment

Comment description

Latest Post

Most Reviews

MOST READ