Rafed English

AL-Kashif-Juzuu Ya Tatu

AL-Kashif-Juzuu Ya Tatu by : Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya

 

Kitabu hiki kilichoko mikononi mwako hivi sasa ni juhudi ya miaka mingi sana ya watu waliojitolea kuona kazi hii imefanikiwa bila ya kumsahau Marhum Abu Muhammad wa London.

Kama lilivyo jina la Tafsiri yenyewe ndivyo ilivyo Tafsiri yenyewe ambayo mwanachuoni huyu mahiri kabisa aliyeifafanua ni mtu aliyebobea katika fani zote ambazo mfasiri (Mfafanuzi) anatakiwa awe nazo.

Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya ameonesha cheche zake katika vitabu vingi alivyoviandika katika maudhui mbali mbalimbali na hivyo kujipatia wasomaji wengi sana.

Msomi huyu, mwenye fikra huru na anayetetea kile anachokiamini, ni mtu mwenye mawazo mapana na kuyaangalia mambo kwa undani sana, kipaumbele chake ni katika maslahi ya umma huu na amejaribu sana kwenda na wakati.

Sifa kubwa pekee ya mwanachuoni huyu ni kuwa yeye hakujihusisha sana na kung'ang'ania madhehebu fulani tu, labda hii yatokana na wadhifa wake wa ukadhi aliokuwa nao katika nchi ya Lebanon ambayo ina madhehebu mengi, ambapo sula la madhehebu ni nyeti nchini humo, hata hivyo yeye aliweza kuamua matatizo ya watu kwenye ofisi yake kulingana na madhehebu yao pale walipomwendea, hiyo ilimsaidia sana hata kuweza kutoa kitabu kitwacho 'Al-Fiqh a'laa madhaahabil-khamsah' (Fikhi ya madhehebu matano) yaani ya Hanafi, Maaliki, Shafi, Hambali na Shia (ambacho twataraji kitatoka hivi karibuni Inshaallah).

Jambo lililotupa msukumo wa kukifasiri kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili ni zile faida nyingi atakazozipata msomaji na kujua mambo mengi na ya ajabu yaliyo mapya kwake ambayo si rahisi kuyapata kwa wafasiri wengine.

Msomaji atapata faida katika fani za Sayansi, Siasa, Historia, Mashairi, visa vizuri, na Saikolojia miongoni mwa mengine; ndiyo maana msomaji atashangaa kidogo anapoisoma Tafsiri hii atakapoona mwandishi amewataja na kuwanukuu watu kama kina Mfalme Edward, wanasyansi kama kina Enstein, Charlie Champlin (Mchekeshaji maarufu), na wengineo, hali inayoifanya tafsiri hii kuwa ni ya kipekee kabisa.

Mtindo alioutumia mwandishi ni sahali uliokusudiwa watu wa tabaka mbalimbali, wanavyuoni na watu wa kawaida. Nia yetu ni kukigawanya kitabu hiki bure lakini tumelazimika kukiuza kwa bei nafuu ili kurudisha gharama za uchapishaji.

Mwisho: Shukrani kubwa iwaendee bila ya kuwataja watu waliojitolea usiku na mchana, jopo la wafasiri, wahariri, wachapaji, waliotupa moyo na kutoa maoni yao na walioisimamia ili kuhakikisha kwamba kitabu kimemfikia msomaji.
Masahihisho:
Katika Juzuu ya kwanza kuna makosa ya uchapishaji baadhi yamegunduliwa na wasomaji wetu, na wakatujulisha- tunawashukuru sana.

1. Ukurasa wa xiii ibara ya 2- badala ya (5:212) ni (2:212)

2. Ukurasa wa 7 Aya 3 kuna maneno yaliyoongezwa ambayo ni ‘na wanaotoa Zaka’

3. Ukurasa wa 19 Aya 26 maneno: "na huwaongoza wengi" yamekosekana katika Aya hii pale inaposema: huwapoteza kwa mfano huu wengi na huwaongoza wengi.

4. Ukura wa 41 Aya 69 maneno ya mwanzo kabisa ya Kiarabu yamekatika nayo ni:

5. Ukurasa wa 65 Aya ya 109 maneno ya mwisho kabisa kwenye tarjuma ni: " ni Muwezo juu ya kila kituna sio anayeona mnayoyafanya.

6. Ukurasa 87 sio 80:36 ni 80:34.

Tunawaomba wasomaji wetu watuandikie kila wanapoona kosa, na sisi tutafanya masahi- hisho katika kila Juzuu inayofuatia. Mchapishaji
Makosa ya Chapa
Sikumbuki kama nimewahi kusoma kitabu kilichotoka kupigwa chapa, cha zamani au cha sasa, bila ya kukuta makosa ya chapa. Nafikiri sitasoma kitabu kisichokuwa hivyo. Nimejaribu sana kuliepuka hilo katika tungo zangu, lakini sikufanikiwa.

Nilikuwa sifikirii kama ninaweza kuona makosa haya katika maandishi ya msahafu mtukufu, kama yale yaliyo katika baadhi ya chapa; kwa mfano neno yabswatu kwa swad, badala ya yabsutu kwa sin, na katika chapa ya Tafsir Arrazi ya Misr ya mwaka 1935, Sura ya (2:146). Imeandikwa La Ya'alamuun, (hawajui) badala ya Ya'alamuun (wanajua). Mfano wa makosa haya hausameheki.

Katika Tafsir Al-Manar, chapa ya Pili, sura (5:212), imeandikwa "Fawqahum ila yawmil qiyama badala ya Fawqahum yawamal qiyama". Hatuwezi kusema kosa hili ni kubwa zaidi kuliko lile.

Lakini mkosaji atatuletea udhuru kwa msemo mashuhuri huko kwetu jabal amail 'Makosa ya chapa.'

Katika Tafsiri Majmau chapa ya Urfan, Sura (46:15), imeandikwa: "Hatta idaha balagha arbai' na sanah badala ya: Hattaidaha balagha ashuddahu arbai ' na sanah"

Kusema hivi sio kama ninajitetea kutokana na makosa ya chapa atakayoyakuta msomaji katika kitabu hiki, ijapokuwa naomba msamaha kama litatokea hili, lakini makusudio yangu hasa ni kumwambia yule atakayefungua macho yake kwenye makosa ya matamko ya kuufungia macho uzuri wa maana. Vilevile ninamwambia yule ambaye siku moja aliniambia: "Vitabu vyako vimejaa makosa ya chapa, kama kwamba hakuna kitu chochote katika vitabu hivyo isipokuwa makosa ya chapa tu. Wote hao ninawaambia: Mungu awasamehe na aniongoze mimi na nyinyi.

Vyovyote iwavyo, mimi ninaomba msamaha kutokana na makosa ya kifikra na ya chapa. Anasema Amirul Muminiin (a.s): "Watu wote ni wapungufu wenye kuchanganyikiwa, isipokuwa yule aliyehifadhiwa na Mwenyezi Mungu." Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye mwenye jukumu la kunikubalia yale niliyoyapatia na kunisamehe niliyakosea, kwa jaha ya Mtume na kizazi chake, ziwashukie rehema na amani (Amin).
MUHAMMADJAWADMUGHNIYYAH
تِلْكَ الرُّسُلُ فَضَّلْنَا بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ ۘ مِنْهُمْ مَنْ كَلَّمَ اللَّهُ ۖ وَرَفَعَ بَعْضَهُمْ دَرَجَاتٍ ۚ وَآتَيْنَا عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ الْبَيِّنَاتِ وَأَيَّدْنَاهُ بِرُوحِ الْقُدُسِ ۗ وَلَوْ شَاءَ اللَّهُ مَا اقْتَتَلَ الَّذِينَ مِنْ بَعْدِهِمْ مِنْ بَعْدِ مَا جَاءَتْهُمُ الْبَيِّنَاتُ وَلَٰكِنِ اخْتَلَفُوا فَمِنْهُمْ مَنْ آمَنَ وَمِنْهُمْ مَنْ كَفَرَ ۚ وَلَوْ شَاءَ اللَّهُ مَا اقْتَتَلُوا وَلَٰكِنَّ اللَّهَ يَفْعَلُ مَا يُرِيدُ {253}
Mitume haotumewafadhilisha baadhi yao zaidi kuliko wengine. Miongoni mwao yuko ambaye Mwenyezi Mungu alisema naye; na wengine akawapandisha vyeo, na tukampa Isa mwana wa Maryam dalili zilizo wazi na tukamtia nguvu kwa roho takatifu. Na kama Mwenyezi Mungu angelitaka wasingelipigana wale waliokuwa baada yao, baada ya kuwafikia dalili zilizo wazi; lakini walihitilafiana kuna katika wao walioamini na wengine katika wao waliokufuru, lakini Mwenyezi Mungu hufanya anayoyataka.
Maana
Mitume hao tumewafadhilisha baadhi yao zaidi kuliko wengine.

Mwenyezi Mungu alimwambia Mtume Wake Muhammad (s.a.w.) katika mwisho wa Aya iliyotangulia; "Na hakika wewe ni miongoni mwa Mitume," Halafu akafuatisha moja kwa moja na kauli Yake hii: "Mitume hao ..." Kwa hivyo basi, makusudio yanakuwa ni mitume wote ambao miongoni mwao ni Muhammad, sio kundi maalum, kama walivyosema wafasiri wengi.

Mitume wote ni sawa katika asili ya utume kuchaguliwa kwao na katika kufikisha ujumbe, wa Mwenyezi Mungu na kuongoza viumbe Vyake, lakini wanatofautiana katika mambo fulani. Yaani baadhi ya mitume wamekuwa mashuhuri kwa baadhi ya mambo fulani waliyohusika nayo, ambayo wengine hawakuwa nayo, ambayo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewasifu nayo katika Kitabu chake.

Kwa mfano Ibrahim alikuwa mashuhuri kwa kuitwa rafiki wa Mwenyezi Mungu (Khalilullah) kutokana na kauli Yake Mwenyezi Mungu: "….Na Mwenyezi Mungu amemfanya Ibrahim kuwa ni rafiki," (4:125).

Musa naye akawa mashuhuri kwa jina la aliyesema na Mwenyezi Mungu (Kalimullah) kutokana na kauli Yake Mwenyezi Mungu: "... Na Mwenyezi Mungu akasema na Musa maneno." (4:164)

Isa naye akawa mashuhuri kwa, roho wa Mwenyezi Mungu (Ruhullah); kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Hakika Masihi Isa bin Maryam ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na neno lake alilompelekea Maryam. Na ni roho iliyotoka kwake ... " (4:171)

Muhammad naye akawa mashuhuri kwa, mwisho wa Mitume (khatamun nabiyyina) kwa kauli Yake Mwenyezi Mungu: "Na Mtume wa Mwenyezi Mungu na mwisho wa Mitume ..." (33: 40)

Mwenyezi Mungu ametaja baadhi ya Mitume waliofadhilishwa au baadhi ya yanayohusika nao, kwa kauli Yake:

Miongoni mwao yuko ambaye Mwenyezi Mungu alisema naye.

Huyu ni Musa bin Imran kama walivyoafikiana wafasiri

Na wengine akawapandisha vyeo .

Mwenye Tafsiri ya Al Manar amesema: "Wafasiri wamesema huyo ni Mtume wetu ..." Na amesema Razi: "Umekubaliana umma wote kwamba Muhammad ni bora ya Mitume," Ametoa dalili 19 juu ya hilo kwa dalili, Miongoni mwa dalili hizo ni kwamba Ali bin Abu Twalib siku moja alitokeza kwa mbali, Mtume akasema: "Huyu ni bwana wa Waarabu."Aisha akasema: "Siye wewe bwana wa Waarabu? "Mtume akasema: "Mimi ni bwana wa walimwengu na yeye ni bwana wa Waarabu."

Dalili bora zaidi juu ya ubora wa Mtume kwa Mitume wote na watu wema wote ni sharia yake ilivyo na ukunjufu katika utukufu wake na utu wake. 1

Na tukampa Isa mwana wa Maryam dalili zilizo wazi na tukamtia nguvu kwa roho takatifu.

Dalili zilizowazi hapa ni dalili ambazo zinadhihirisha haki; kama kufufua wafu, kuponyesha wagonjwa, kuumba ndege, n.k. Makusudio ya roho takatifu ni roho njema yenye kutakaswa. Imekwishapita tafsiri ya roho katika Aya ya 87 ya Sura hii.

Na kama Mwenyezi Mungu angelitaka wasingelipigana wale waliokuwa baada yao.

Yaani baada ya Mitume kuwajia na hoja zilizowazi na kuzifafanua haki kwa dalili, basi watu wao walihitalifiana baada yao.

Kuna katika wao walioamini na wengine katika wao waliokufuru.

Unaweza kuuliza: Kauli Yake Mwenyezi Mungu: "Na kama Mwenyezi Mungu angelitaka wasingelipigana. Si inafahamisha kwamba binadamu ni mwenye kuendeshwa hana hiyari na kwamba kukaririka jumla hii ni kutilia mkazo kunasibika kupigana na matakwa ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.)?

Jibu: Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amempa uwezo mja na akambainishia heri na shari na kumkataza hili na kumwamrisha lile. Mwenyezi Mungu anasema: "Na shikamaneni na kamba ya Mwenyezi Mungu nyote wala msiachane..." (3:103)

Mtu akifuata njia ya mshika- mano na kupendana, atakuwa yeye mwenyewe ndiye anayenasibika na huko kufuata, kwa sababu kumetokana na yeye na kwa hiyari yake iliyomfanya aone bora njia hiyo kuliko njia ya kutoelewana; wakati huo huo huko kufuata njia hiyo ya mshikamano kunafaa kunasibishwe kwa Mwenyezi Mungu, kwa sababu Mwenyezi Mungu ndiye aliyemwezesha kuifuata na ndiye aliyemwamrisha kuifuata.

Ama akifuata njia ya chuki na uhasama, basi njia hiyo itanasibika na mtu pekee wala haina- sibiki na Mwenyezi Mungu, kwa sababu mtu ameifuata kwa radhi yake na akaiona ni bora kuliko njia ya maafikiano; wala haifai kuinasibisha kwa Mwenyezi Mungu, kwa sababu Mwenyezi Mungu amemkataza.

Unaweza kuuliza tena: Kwa nini Mwenyezi Mungu amemwezesha mtu kuifanya shari ambapo ilikuwa inatakikana ampe hima ya kuaacha na kufanya heri tu?

Jibu: Lau Mwenyezi Mungu angelifanya hivi, binadamu asingebakiwa na fadhila yoyote wala vitendo visingekuwa na sifa ya heri na shari au vizuri na vibaya. Kwa sababu sifa hizi zinafungamana na matakwa ya mtu na hiyari yake.

Bali lau Mwenyezi Mungu angelimfanya mtu kufanya kitu fulani tu, kusingelikuwako na tofauti ya mtu na mawe au tofauti na unyoya ulio katika mavumo ya pepo. Kwa ajili hii na kwa ajili ya kudumu mtu na utu wake, hakutaka Mwenyezi Mungu kuwalazimisha watu kwenye kitu fulani

"Na kama angelitaka wasingelipigana."

Kwa ufupi kupigana ambako kumepatikana kati ya watu sio kama kumekhalifu matakwa ya Mwenyezi Mungu yanayoitwa Kun fa yakun. Isipokuwa kumekhalifu matakwa ya Mwenyezi Mungu ya sharia yake, ambayo ni ubainifu na uongozi; na hekima yake imetaka kumpa mtu uwezo wa kutosha wa kufanya heri na shari, ili ajichagulie yeye mwenyewe uongozi na heri na awe ni mtu anayetofautiana na mawe na wanyama.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَنْفِقُوا مِمَّا رَزَقْنَاكُمْ مِنْ قَبْلِ أَنْ يَأْتِيَ يَوْمٌ لَا بَيْعٌ فِيهِ وَلَا خُلَّةٌ وَلَا شَفَاعَةٌ ۗ وَالْكَافِرُونَ هُمُ الظَّالِمُونَ {254}
Enyi mlioamini! Toeni katika vile tulivyowapa. Kabla haijafika siku ambayo hapatakuwa na biashara wala urafiki wala uombezi. Na makafiri ndio madhalimu
 
________________________
1. Wamesema sana kuhusu sababu za kuzorota kwa Waislamu na udhaifu wao katika nafsi zao; wametunga vitabu vingi kuhusu hilo na wakatoa sababu nyingi sana. Sisi tunaona sababu ya kwanza na ya mwisho ni kupuuzwa sharia ya Kiislamu kwa kinadharia na kimatendo. Na ukoloni ulitambua hakika hii, kwa hivyo kazi walioifanya tangu walipokanyaga miji ya Waislamu ni kuiondoa sharia ya Kiislamu kwenye mashule na mahakama, na badala yake wakaweka sharia za kutungwa. Kwa hiyo wakawaweka mbali Waislamu na dini yao. Qur'an yao na Sunna ya Mtume wao, tutalifafanua hilo kila itakapohitajika.
Maana
Mwenyezi Mungu amehimiza kutoa mali kwa mifumo mbali mbali. Yameshatangulia maelezo katika tafsiri ya Aya 245; na unakuja tena mfano wake katika Aya hii:

Enyi mlioamini! Toeni katika vile tulivyowapa.

Mwenyezi Mungu anahimiza kutoa pamoja na kuashiria kwamba mali iliyo na watu ni mali Yake aliyoitoa Yeye Mwenyezi Mungu (s.w.t.); na kwamba kesho fursa itakosekana, kwa hivyo ni juu ya mumin mwenye akili kuchukua fursa kabla ya kupitwa na wakati.

Kabla haijafika siku ambayo hapatakuwa na biashara wala urafiki wala uombezi.

Makusudio ya biashara hapa ni kulipa fidia ili kujikomboa na moto kwa mali; urafiki ni urafiki wa kusameheana na uombezi na kuombewa na mtu mwingine kuepukana na moto.

Maana yake ni kwamba kesho mtu atakuja peke yake hana chochote isipokuwa amali njema. Aya hii ina maana sawa na Aya ya 48 ya Sura hii. Tumeuzungumzia uombezi katika Aya hiyo.

Na makafiri ndio madhalimu.

Wamejidhulumu wenyewe kwa kuacha amali njema ambayo inawaokoa na adhabu. Kwa ujumla ni kuwa neno dhulma na ukafiri yanakuja katika matumizi ya maana mamoja. Mara nyingine hutumiwa ukafiri katika dhulma, kama alivyosema Mwenyezi Mungu (s.w.t.): "... Hakika ushirikina ni dhulma kubwa." (31:13)Na mara nyingine hutumiwa dhulma katika ukafiri, kama alivyosema Mwenyezi Mungu (s.w.t.): "...Lakini madhalimu wanakanusha ishara za Mwenyezi Mungu..." (6:33)
اللَّهُ لَا إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ ۚ لَا تَأْخُذُهُ سِنَةٌ وَلَا نَوْمٌ ۚ لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۗ مَنْ ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِنْدَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ ۚ يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ ۖ وَلَا يُحِيطُونَ بِشَيْءٍ مِنْ عِلْمِهِ إِلَّا بِمَا شَاءَ ۚ وَسِعَ كُرْسِيُّهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ ۖ وَلَا يَئُودُهُ حِفْظُهُمَا ۚ وَهُوَ الْعَلِيُّ الْعَظِيمُ {255}
Mwenyezi Mungu hakuna mola ila Yeye Aliyehaimsimamiziwakila kitu. Hakumshiki kusinzia wala kulala. Ni Vyake vilivyomo ardhini na vilivyomo mbinguni. Na ni nani huyo awezaye kuombea mbele YakebilayaidhiniYake. Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao; wala wao hawalijui lolote lililo katikaelimu Yakeilakwaalitakalo. Elimu Yakeimeeneambinguna ardhi.Walahakumshindikuzilinda.
 
NaYeyendiyeMtukufualiyeMkuu.
 
Maana
Mwenyezi Mungu hakuna mola ila yeye aliye hai, Msimamizi wa kila kitu. Mwanafalsafa mashuhuri wa elimu inayohusika na mambo ya Mungu, aitwaye Mulla Sadra anasema: Neno Allah (Mwenyezi Mungu) linafahamisha kupwekeka dhati Yake Mwenyezi Mungu na sifa Zake. Kufahamisha juu ya kupwekeka katika dhati, ni kwamba jina hili tukufu haliitiwi mtu mwingine kiuhakika wala majazi. Mwenyezi Mungu anasema: "... Basi mwabudu Yeye tu na udumu katika ibada Yake. Je, unamjua (mwingine) mwenye jina lake?" (19:65)

Ama kufahamisha kupwekeka Kwake katika sifa, ni kwamba jina hili linafahamisha juu ya dhati yenye kukusanya kila sifa za ukamilifu na utukufu, kinyume cha majina mengine kama; Mjuzi, Mweza na Muumbaji, ambayo umoja wake haufahamishi isipokuwa umoja wa maana katika elimu, au uweza au utendaji.

Unaweza kuuliza: Hakika sifa za ukamilifu na utukufu ni nyingi na zenye kubadilika kulingana na kueleweka kwake; vipi ifae kusema zimepwekeka na tunaziona zinahisabika na kubadilika?

Jibu: Ukisema huyu ni mtu mjuzi yataeleweka mambo mawili - Sifa na Mwenye kusifiwa; na vyote ni vitu tofauti. Mtu sio ujuzi na ujuzi sio mtu. Hayo ni kwa upande wa kiumbe. Ama kwa upande wa Muumbaji hakuna jingine isipokuwa kuweko kiutukufu; na huko kuweko ndiko ujuzi ndiko uwezo, na ndiko hekima, n.k. Hakuna sifa na mwenye kusifiwa vyote ni vimoja tu; na huku hakukufanana na kitu kingine.

Hakuna mola ila Yeye

Inasemekana maana yake ni hakuna anayepasa kuabudiwa kwa haki isipokuwa Yeye. Lakini kueleweka kwake ni hakuna yoyote mwenye kukusanya sifa za uungu isipokuwa Yeye. Vyovyote iwavyo, maana zote mbili ni zenye kulazimiana.

Aliye hai Msimamizi wa kila jambo

Ukiunasibisha uhai kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, maana yake yanakuwa ni kukua, kuhisi na utambuzi. Lakini ukiunasibisha kwa Mwenyezi Mungu unakuwa ni elimu na uweza.

Makusudio ya kusimamia kila kitu ni kukisimamia katika mambo yake na kukipangilia vizuri. Mwenyezi Mungu anasema: "Akasema: Mola wetu ni Yule aliyekipa kila kitu umbo lake kisha akaongoza." (20:50) Na amesema tena: "....Na ameumba kila kitu akakikadiria kipimo (chake)." (25:2)

Mulla Sadra anasema: Kauli ya Aliye Hai inafahamisha kwamba Yeye ni Mjuzi na Muweza. Na kauli ya Msimamizi wa kila kitu inafahamisha kuwa Yeye ni Mwenye kujisimamia Mwenyewe na kumsimamia mwingine. Kwa hiyo sifa mbili hizi ni zenye kuafikiana katika maana na ni zenye kuingiliana."

Anakusudia kuwa usimamizi hauepukani na uhai; kama vile ambavyo uhai kwa maana ya uwezo na elimu hauepukani na usimamizi.
Mwenyezi Mungu Na Desturi Ya Maumbile
Unaweza kuuliza: Je maana ya kusimamia Mungu juu ya mipango ya vitu vyote, ni kwamba mambo yote ya dhahiri ya kimaumbile mpaka mafungu yake yanasimamiwa na Mwenyezi Mungu moja kwa moja Yeye Mwenyewe bila ya kuweko kati sababu yoyote ya kimaada; kama inavyodhihiri katika Aya isemayo: "Kisha tukamfanya tone la manii, katika makao madhubuti . Kisha tukaliumba tone hilo kuwa pande la damu, na tukaliumba pande la damu kuwa pande la nyama, kisha tukaliumba pande la nyama kuwa mifupa na mifupa tukaivika nyama, kisha tukalifanya umbo jengine. Basi ametukuka Mwenyezi Mungu mbora wa waumbaji." (23:13-14)

Kwa sababu yenye kuja haraka fahamuni katika Aya hii, ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameingilia Yeye Mwenyewe moja kwa moja kwenye makuzi mbali mbali ya tone la manii; na tunajua kuwa nadharia ya kielimu inasema kuwa tone la manii linakuwa na kuzidi kulingana na kanuni maalum? Katika kujibu hayo, hapana budi kupambanua kati ya jambo lisilokuwa la kawaida, kama vile kufufua wafu na kupatisha kitu bila ya kitu kingine, na matukio yanayo kuwa kulingana na kanuni za kimaumbile, kama kupatwa jua mwezi, n.k. Hili la aina ya kwanza linategemezwa kwake Mwenyezi Mungu moja kwa moja.

Na hili la aina ya pili linategemea desturi ya maumbile na linategemezwa kwa Mwenyezi Mungu, kwa sababu Yeye ndiye aliyeweka desturi ya maumbile pamoja na vilivyomo ndani yake vikiwa ni pamoja na nguvu na viasili. Viasili hivi kwa kupitia njia zake vinafanya dhahiri za maumbile zikiwa ni pamoja na tone la manii. "...Na ameumba kila kitu akakikadiria kipimo (chake)."(25:2)

Yaani anakipitisha katika desturi na kanuni za kitabia. Lau angelikuwa Yeye Mwenyezi Mungu ndiye anayesimamia umbile moja kwa moja bila ya kuweko kati kitu kingine, kusingelikuweko na sababu na msababishaji.

Kwa hivyo basi, inatubainikia kuwa kila mwenye kuamini kwamba kila tukio la kimaumbile linategemea Mwenyezi Mungu moja kwa moja bila ya kuweko kati sababu yoyote yenye kuhisiwa ambayo imegunduliwa na utaalamu au inaweza kugunduliwa, mtu huyo atakuwa mjinga mwenye kukosea katika imani yake.

Na lau ingelikuwa sahihi imani yake hii, kusin- gelikuweko na wajibu wa kitendo chochote na elimu isingelikuwa na faida yoyote; wala uvumbuzi na maendeleo ya mtu yasingekuwa na athari yoyote.

Vile vile amekosa yule mwenye kuitakidi kwamba maumbile ndio kila kitu, kuwa ndiyo sababu ya kwanza na ya mwisho, wala hakuna kitu nyuma yake. Hayo ni makosa. Kwani kama ni hivyo kusingelikuwa na nidhamu wala athari yake na kungelikuwa na migongano na natija ingelikuwa kutokuwepo elimu wala uhai.

Haya tumeyafafanua zaidi katika Aya ya 21 ya Sura hii, kifungu cha Tawhid.

Hakumshiki kusinzia wala kulala.

Mwenyezi Mungu alipobainisha kwamba Yeye ni Hai Msimamizi wa kila jambo, ameendelea kulitilia mkazo hilo kwamba Yeye ni Mwenye kutukuka, haumzuwii usingizi wala kusahau au kitu chochote, katika kupanga kuumba Kwake kwa njia ya ukamilifu. Kwa sababu hilo linapingana na ukubwa Wake na kujitosha Kwake na kila kitu. Imam Ali amesema akimwambia Mola wake: "Sisi hatujui kiasi cha ukubwa wako, isipokuwa tunajua kuwa Wewe ni Aliye Hai wa Milele, Msimamizi wa kila jambo, hakukushiki kusinzia wala kulala; hutazamwi; wala halikuoni jicho, lakini Wewe unaliona; umezithibiti amali na ukazishika barabara."

Ni vyake vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini Makusudio ya vilivyomo ni ulimwengu wote na kila kilichomo ndani yake hakitoki nje ya ufalme Wake na mipangilio Yake. Imam Ali (a.s.) aliulizwa kuhusu: "Hapana hila wala nguvu isipokuwa kwa msaada wa Mwenyezi Mungu."

Akajibu: "Sisi hatumiliki chochote mbele ya Mwenyezi Mungu, wala hatumiliki isipokuwa kile tulichomilikishwa; na anapomilikisha kile ambacho amekimiliki zaidi kuliko sisi, basi ametukalifisha nacho; na anapokiondoa, huwa ametuondolea taklifa."

Na ni nani huyo awezaye kuombea mbele Yake bila ya idhini Yake.

Umekuja mfumo wa swali kwa maana ya kukanusha; yaani hataombea yeyeote mbele Yake isipokuwa kwa amri Yake na hayo ni jibu na kubatilisha kauli ya washirikina kwamba masanamu ndiyo yanayowakurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anawasimulia hao kwa kusema: "... Na wanasema: hao ndio waombezi wetu mbele ya Mwenyezi Mungu! Sema: 'Je, mnamwambia Mwenyezi Mungu asiyoyajua katika mbingu wala katika ardhi? ..." (10: 18)

Tumekwisha zungumzia uombezi katika Aya ya 48. Baadhi ya ulama wamesema kwamba siku ya Kiyama kutakuwa na aina mbalimbali za watu. Kama ifuatavyo:- Waliotangulia ambao ni wenye kukurubishwa; watakaokuwa upande wa kuume ambao ni watu wema watakaookoka, watakaokuwa upande wa kushoto ambao ni waovu watakao adhibiwa, na watakaokuwa na msamaha ambao amali zao njema zimechanganyika na maovu.

Na hawa watakubaliwa kuombewa; kama alivyosema Mwenyezi Mungu: " Na wengine walikiri dhambi zao, wakachanganya vitendo vyema na vingine viovu, huenda Mwenyezi Mungu akapokea toba yao. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kusamehe Mwenye kurehemu." (9:102)

Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao.

Maana yake ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.), anajua yaliyokuwa na yatakayokuwa katika waja wake, iwe heri au shari; na anamjua mwombezi na anayeombewa na anayestahiki msamaha na thawabu au adhabu na mateso. Ikiwa mambo yako hivyo, basi uombezi (shafaa) hauna nafasi yoyote isipokuwa kwa amri Yake Mwenyezi Mungu kwenye mipaka Yake anayoridhia.

Wala hawalijui lolote lililo katika elimu Yake ila kwa alitakalo.

Dhamiri katika hawalijui inawarudia waja wote wakiwemo Malaika na Mitume. Makusudio ya elimu ni linalojulikana. Maana yako wazi. Ukipenda kujua zaidi unaweza kuangalia Aya hizi:" Yeye ni mjuzi wa siri; wala hamdhihirishii yoyote siri Yake isipokuwa Mtume aliyem- ridhia ..." (72: 26-27) "... Utakatifu niwako! Hatuna elimu isipokuwa ile uliyotufundisha ..." ( 2: 32)

Elimu Yake imeenea mbingu na ardhi.

Kauli zimekuwa nyingi na zimegongana kuhusu maana ya neno Kursiy. Baadhi ya kauli hizo ni za kumzungumzia Mwenyezi Mungu bila ya elimu, lakini bora ya kauli ni mbili: Ya kwanza, ni fumbo la utukufu Wake Mwenyezi Mungu na cheo chake yaani enzi. Ya pili, ni elimu; yaani elimu Yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.) imezunguka kila kitu. Mpangilio wa maneno unarudia maana haya.

Wala hakumshindi kuzilinda na Yeye Ndiye Mtukufu aliye Mkuu

Yaani hakumtii mashaka wala uzito wowote kuilinda mbingu na ardhi na kupangilia vizuri yaliyomo ndani yake. Vipi isiwe hivyo! Na hali kuumba nzi na kuumba ulimwengu Kwake ni sawa tu; maadamu Yeye Mwenyezi Mungu (s.w.t.) "... Akitaka chochote ni kukiambia kuwa, kikawa." (36:82)
 
Kitu Bila Ya Kitu
Kutengeneza vitu kuko aina mbili: kutegeneza kitu kutokana na maada na kutengeneza bila ya maada. Na kunatofautiana kwa njia nyingi.

1. Anayetengeneza kwa maada anahitaji harakati na zana, lakini asiyetengeneza kwa maada hahitaji.

2. Wa maada anachoka, lakini asiyetumia maada hachoki.

3. Mwenye kutumia maada hawezi kupata kitu bila ya kitu kingine, lakini kwa asiyetumia, hilo sio jambo zito.

Kwa hivyo inabainika kwamba kumlinganisha Muumbaji na Mwenye kuumbwa ni kulinganisha na kisicholingana. Itawezekana vipi kumfananisha mwenye kujitosha na mwenye kuhitajia; atakuwaje sawa na mwenye kushindwa?
لَا إِكْرَاهَ فِي الدِّينِ ۖ قَدْ تَبَيَّنَ الرُّشْدُ مِنَ الْغَيِّ ۚ فَمَنْ يَكْفُرْ بِالطَّاغُوتِ وَيُؤْمِنْ بِاللَّهِ فَقَدِ اسْتَمْسَكَ بِالْعُرْوَةِ الْوُثْقَىٰ لَا انْفِصَامَ لَهَا ۗ وَاللَّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ {256}
Hakuna kulazimisha katika dini; uongofu umekwisha pambanuka na upotofu. Basi anayemkataa taghuti na akamwamini Mwenyezi Mungu, hakika yeye ameshika kishiko madhubuti kisichovunjika. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikiaMjuzi.
اللَّهُ وَلِيُّ الَّذِينَ آمَنُوا يُخْرِجُهُمْ مِنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ ۖ وَالَّذِينَ كَفَرُوا أَوْلِيَاؤُهُمُ الطَّاغُوتُ يُخْرِجُونَهُمْ مِنَ النُّورِ إِلَى الظُّلُمَاتِ ۗ أُولَٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ ۖ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ {257}
Mwenyezi Mungu ni mtawala wa wale walioamini; huwatoa gizani na kuwaingiza katika mwangaza, lakiniwaliokufuruwatawalawao ni mataghuti. Huwatoa kwenye mwangaza, na kuwaingiza katika giza, hao ndio watu wa motoni, watadumuhumo.
 
Maana
Hakuna kulazimishwa katika dini

Lau tungeiangalia jumla hii peke yake, tungelifahamu kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakuweka hukumu yenye aina yoyote ya kulazimisha na kwamba anayolazimishwa mtu katika kauli au vitendo hayaambatani na kitu chochote katika mtazamo wa sharia, si katika dunia wala akhera.

Lakini kauli Yake Mwenyezi Mungu "Uongofu umekwisha pambanuka na upotofu", ambayo ndiyo sababu ya kuacha kulazimisha, inaonyesha kuwa neno katika, hapa lina maana ya juu ya; Yaani uislamu haumlazimishi yeyote kukubali isipokuwa unamlazimisha mpinzani kwa hoja na dalili tu; kama inavyosema Qur'an: "Na sema: (Huu) ni ukweli uliotoka kwa Mola wenu, basi anayetaka na aamini na anayetaka na akufuru ..." (18:29) "... Je, wewe utawashurutisha watu kwa nguvu wawe waumini? (10:99)

Unaweza kuuliza: Hakika dini haiwezekani kufungamana na kulazimishwa, kwa sababu dini ni katika mambo ya moyo yaliyo nje ya uwezo. Sawa na kuleta picha ya kitu akilini. Vinavyoweza kufungamana na kulazimishwa ni kauli na vitendo ambavyo inawezekana kutendeka bila ya matakwa ya msemaji na mtendaji. Kwa hivyo umepita njia gani mpaka ukasema habari ya kukataza kulazimishwa juu ya dini?

Jibu: Hakika kauli Yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.): "Hakuna kulazimishwa katika dini" Imekuja kwa tamko la kuelezea habari. Kama hivyo ndivyo, basi swali litakuwa halina msingi, kwa sababu maana yatakuwa dini ni itikadi na hilo ni jambo linalorudia kwenye kukubali ambako mtu halazimishwi kukubali.

Ikiwa tamko limekuja kwa kukusudiwa kukataza, basi maana yatakuwa ni: Enyi Waislamu msimlazimishe yeyote kusema "Lailaha illa Llahu Muhamadurasuli Llahi." baada ya kuwako hoja na dalili juu ya Tawhid na Utume.

Lakini jibu hili linaweza kuzalisha swali jipya kwamba hayo hayataafikiana na kauli ya Mtume (s.a.w.): "Nimeamrishwa nipigane na watu mpaka waseme: 'Laillahailla Ilah'; wakisema hivyo, basi damu zao na mali zao zimehifadhika na mimi."

Jibu: uislamu unaruhusu kupigana kwa sababu mbali mbali. Miongoni mwa sababu hizo ni: Kujikinga - Mwenyezi Mungu anasema: "Na piganeni katika njia ya Mwenyezi Mungu na wale wanaowapiga, wala msipituke mipaka." (2: 190). Kudhulumiwa - Mwenyezi Mungu anasema : "... Lipigeni (kundi) lile linaloonea (wenzao) mpaka lirudi katika amri ya Mwenyezi Mungu ..." (49:9)

Kupigana ili kuudhihirisha uislamu, ijapokuwa ni kwa ulimi. Hilo ni kwa ajili ya maslahi yanayowarudia wote, sio waislamu peke yao. Na maslahi haya anayakadiria aliye Masum au naibu wake; wala haifai kwa mwislamu yeyote, vyovyote alivyo, kupigana kwa ajili ya kutamkwa tamko la uislamu au kuueneza, isipokuwa kwa amri ya Masum au naibu wake, ambaye ni mujtahid1 mwadilifu.

Ni kwa njia hii peke yake ndio inachukuliwa Hadith "Nimeamrishwa nipigane na watu ..."; Yaani mimi nitapigana nao nitakapoona mimi au kaimu wangu kwamba maslahi ya kiutu yanalazimisha kupigana kwa ajili ya 'Lailaha illa llah'.

Hapo inaonyesha kuwa kupigana kwa kujikinga au kuikinga dini na haki, hakungojei idhini ya yeyote. Tumekwisha yaeleza hayo katika tafsiri ya Aya ya 193 kifungu cha 'Uislamu unapiga vita dhulma na ufisadi.'

Uongofu umekwisha pambanuka na upotofu.

Makusudio ya uongofu hapa ni imani na upotofu ni ukafiri.

Mwenyezi Mungu amekwisha ibainisha haki kwa uwazi zaidi, na ubainifu na dalili zenye nguvu, mpaka kafiri akaishiwa na hoja au udhuru wowote. Mwenye kuijua njia ya haki na ya uongofu atakuwa amekwisha ijua njia ya upotofu na ya batili. Kwani hakuna kitu kingine baada ya haki isipokuwa upotofu.

Mulla Sadra anasema: Maana ya uongofu umekwisha pambanuka na upotofu ni kuitambua haki kutokana na batili na imani kutokana na ukafiri kwa dalili na hoja pamoja na kuzifahamu na kuziangalia vizuri. Yeyote mwenye kuikubali haki kwa kufuata tu, hana tofauti na mnyama. Hata hivyo mwenye kuwafuata watu wema kwa nia njema na kwa dhamiri nzuri atayapata yale watakayoyapata wao kesho.

Basi anayemkataa taghuti na akamwamini Mwenyezi Mungu, hakika yeye ameshika kishiko madhubuti kisichovunjika.

Kauli zimekuwa nyingi kuhusu tafsiri ya taghuti, baadhi ya wafasiri wamefikisha kauli tisa. Miongoni mwa hizo ni kuwa makusudio yake ni shetani. Nyingine ni dunia iliyo twevu. Iiliyo karibu na ufahamu na yenye kufahamisha kutokana na tamko lenyewe, ni kauli ya Sheikh Muhammad Abduh kwamba taghut ni yule ambaye kwa kumwabudu na kumwamini yeye, ndiyo sababu ya kupetuka mpaka na kutoka katika haki.

Makusudio ya kishiko madhubuti, ni kwenda kwenye njia iliyonyooka ambayo hapotei mwenye kuifuata. Maana kwa ujumla ni kwamba kumwamini Mwenyezi Mungu ni kishiko cha kutegemewa hakikatiki milele na kwamba mwenye kushikamana nacho hapotei.

Katika Sahih Muslim anasema: "Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: Hakika mimi ninaacha kwenu vitu ambavyo kama mkishikamana navyo hamtapotea baada yangu, kimojawapo ni kikubwa kuliko kingine, nacho ni kitabu cha Mwenyezi Mungu kamba yenye kuvutwa kutoka mbinguni hadi ardhini na kizazi changu Ahlul Bait wangu, vitu viwili hivyo havitaachana mpaka vije kwangu kwenye birika." Hadith hiyo pia imepokewa na Tirmidhyi. Lakini hivi sasa vitu vyote hivyo viwili vimeachwa. Ndio Imam Ali (a.s.) akasema: "Utakuja wakati Qur'an haitabaki isipokuwa maandishi yake na Uislamu utabaki jina lake tu."

Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mjuzi.

Anasikia tamko la Tawhid kutoka kwa waumini, na la kufuru kutoka kwa makafiri; na anajua yaliyo katika nyoyo za watu wawili na atamlipa kila mmoja kwa amali zake.

Mwenyezi Mungu ni mtawala wa wale walioamini; huwatoa gizani na kuwaingiza katika mwangaza.

Wafasiri wametofautiana sana katika Aya hii. Baadhi yao wakazalisha mushkeli wa kiitika- di; mpaka Mulla Sadra akasema: "Kuna mushkeli mkubwa ambao ni vigumu kuutatua kwa wenye fahamu." Sheikh Muhammad Abduh amesema: "Hakika baadhi ya tafsiri ni tafsiri za wafasiri wasiokuwa wataalamu ambao hawafahamu mifumo ya lugha ya hali ya juu, au ni tafsiri za wasiokuwa Waarabu ambao zaidi huwa hawafahamu." Ama sababu ya kutofautiana wafasiri na kuzalisha matatizo ya kiitikadi ni kwamba wao wamefahamu Aya kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni mtawala na mwangalizi wa mambo ya waumini tu; na wala sio kwamba waumini wanamfanya Yeye tu kuwa ni mtawala na mwangalizi wa mambo yao. Hapo kuna tofauti kubwa kati ya maana hizi mbili.

Kuanzia hapa ndipo umekuja mushkeli katika wanavyofahamu wafasiri, kwamba utawala wa Mwenyezi Mungu na msaada Wake unakuwa kwa viumbe vyote katika nidhamu moja; na wala sio kwa waumini tu.

Vyovyote itakavyokuwa, kauli za wafasiri au wengi wao hazioani na mfumo, na kwamba maana yaliyo salama, ambayo hayana matatizo yoyote na yanayoafikiana na kauli Yake Mwenyezi Mungu, Basi anayemkataa taghuti na akamwamini Mwenyezi Mungu, hakika yeye ameshika kishiko madhubuti kisichovunjika ni kuwa waumini hawamfanyi mtawala asiyekuwa Mwenyezi Mungu wala hawamfanyi yeyote kuwa mlinzi wao isipokuwa Mungu pekee Yake; Kwake wanakimbilia, na kwa Kitabu Chake na sunna ya Mtume Wake wanaongoka katika itikadi zao, kauli zao na vitendo vyao.

Wala hawategemei watu wapotevu na mataghuti, hata wawe vipi. Kinyume chake ni makafiri ambao wanawafanya mataghuti ndio watawala wao.

Hapana mwenye shaka kwamba mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu na akaendelea kumtii na kuongoka kwa Aya Zake na ubainifu Wake kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu na msaada Wake atasalimika kutokana na giza la bid'a na upotevu, vilevile matamanio na ujinga. Na atapata mwanga kwa nuru ya maarifa ya kweli na imani sahihi. Hayo ndiyo maana ya Huwatoa gizani na kuwaingiza katika mwangaza.

Lakini waliokufuru, watawala wao ni mataghuti. Huwatoa kwenye mwangaza na kuwiangiza katika giza.

Maana kwa ujumla ni kuwa makafiri wanawafanya watu wapotevu na mataghuti kuwa watawala wao badala ya Mwenyezi Mungu; wanachukua amri zao na kuacha makatazo yao. Hawa wanakwenda katika njia ya kuhiliki na wanawatoa kwenye mwangaza wa akili na maumbile na kuwatia katika giza ukafiri na uzushi.
Kudumu Motoni
Watadumu humo.

Mara nyingi sana Qur'an imetaja kuwa kuna aina ya waasi watakaodumu motoni; na imebainisha kuwa miongoni mwa aina hii ni: Mwenye kumkufuru na akakadhibisha Aya zake. Mwenyezi Mungu anasema: "Na wale ambao wamekufuru na kukadhibisha ishara zetu, hao ndio watakoakuwa watu wa motoni, humo watadumu." (2:39)

Mwenye kumua mumini kwa makusudi, Mwenyezi Mungu anasema: "Na mwenye kumuua Muumin kwa kukusudia, basi malipo yake ni Jahannam, humo atadumu ..." (4:93)

Mwenye kumwasi Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na kuruka mipaka. Mwenyezi Mungu anasema: "Na anayemuasi Mwenyezi Mungu na Mtume, na kuiruka mipaka ya Mwenyezi Mungu, atamwingiza motoni, humo atadumu." (4:14)

Mwenye kuzungukwa na makosa yake; Mwenyezi Mungu anasema: "Ndio wanaochuma ubaya na makosa yao yakawazunguka, hao ndio watu wa motoni, humo watadumu." (2:81)

Hapana mwenye shaka kwamba kwa mujibu wa uadilifu Wake Mwenyezi Mungu, hamwadhibu isipokuwa mwenye kustahili adhabu na adhabu yake inatofautiana kwa ukali na udhaifu kulingana na makosa na maasi. Kosa la mwenye kuhangaika akieneza ufisadi duniani, akaangamiza mimea na viumbe, si sawa na kosa la mwenye kuiba shillingi moja au aliyem- sengenya anayeshindana naye katika kazi.

Pamoja na haya tunaweza kujiuliza kudumu katika moto kusikokuwa na mwisho, kugongwa kichwa kwa macheche yaliyo kama majumba, kuvurumishiwa marungu ya chuma mgongoni na kujazwa tumbo kwa maji ya usaha; kisha mtu asife akapumzika wala asipunguziwe angalau akapumua; mtu huyu ambaye anaumizwa na chawa na kufa kwa kusongwa koo na jasho humfanya anuke; kama alivosema Amirul Muminin Ali (a.s.).

Tujiulize je machungu yote haya makubwa kwa mnyonge huyu mwenye kushindwa na chawa, yanaafikiana na dhati ya Mwenyezi Mungu ambaye ni heri tupu na rehema, ukarimu, neema, upole na hisani?" Je inaingilika akilini mtu huyu kuadhibiwa milele au kunyimwa kabisa neema ... Au huko kuwa milele na kila ngozi inapoiva kubadilishwa ngozi nyingine bila ya kupumzika, yote hayo ni ya kujiuliza.

Akisema msemaji: Hakuna adhabu ambayo itazidi ya mwenye kumuua Hussein bin Ali (a.s.) au aliyetupa bomu la Atomic au Haidrojeni kwa watu na akawamaliza wote, au mwenye kuanzisha mambo mabaya, yakadumu na uovu wake ukazidi?

Jibu: Ni kweli kuwa hazidi yeyote katika uliowataja, lakini sio kila asi ni Yazidi wala sio kila bomu ni Atomic na Hadrojeni; wala sio kila desturi inawatawanya watu. Lakini swali halikuwa juu ya hawa, bali swali ni juu ya kudumu walio na daraja nyingine.

Unaweza kusema: Maelezo ya Qur'an na Hadith za Mtume juu ya kudumu milele utazifanyaje?

Jibu: Hakuna katika hizo inayokataa Taawil.

Ukisema tena kuwa, kila kilicho elezwa ikiwa kukielewa kunawezekana kwa dhahiri, basi ni wajibu kudumu juu ya dhahiri yake, kwa hiyo kudumu wakosaji katika moto si muhali.

Jibu: Ndio, lakini lichukuliwe la kudumu muda mrefu badala ya milele, kwa kukusanya kati ya Qur'an na dalili za rehema ambako, hakukataliki wala hakupingwi na sharia na akili.

Utasema mara ya tatu: Hakika mafaqihi hawawezi kuridhika na jawabu hili, kwa sababu wao hawaruhusu kuchukulia kinyume cha dhahiri ya tamko isipokuwa kwa sababu tatu: Kuunganisha na kitu kingine kwa kidesturi, kama vile kuchukulia mahsus kutoka katika jumla; au kisheria, kama kauli wazi yenye kuthibiti kutoka kwa Masum; au kiakili kusikokubali uwezekano wa kinyume, Na sisi hatuna chochote katika hivyo vitatu.

Jibu: Kwanza: Ninadhani kuwa mafaqihi waliozitambua dalili za rehema ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) wataafikiana nami, kwamba inawezekana kuziacha dhahiri za dalili za kudumu milele katika moto kwa baadhi ya wakosaji. Miongoni mwa dalili hizo ni Hadith Qudsi: "Rehema yangu imeshinda ghadhabu yangu." Vilevile Hadith tukufu inayosema: Hakika waombezi siku ya Kiyama ni wengi na mwisho wa waombezi ni mwenye kurehemu wenye kurehemu. Na kwamba rehema yake Mwenyezi Mungu itaenea siku ya Kiyama mpaka ibilisi atakuwa na tamaa na kunyoosha shingo yake.

Katika baadhi ya riwaya ni kwamba Hassan al Basri alisema: "Si ajabu kwa aliyeangamia, kuwa vipi ameangamia. Lakini ajabu ni ya mwenye kuokoka vipi ameokoka." Imam Zainul Abidin (a.s.) akasema: "Ama mimi ninasema; sio ajabu kwa aliyeokoka kuwa ameokoka vipi; isipokuwa ajabu ni kwa aliyeangamia kuwa ameangamia vipi pamoja na ukubwa wa rehema ya Mwenyezi Mungu!"

Tukiiunganisha riwaya hii na Aya inayosema: "Sema! Enyi waja wangu waliojidhulumu! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu; hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote ..." (39:53). Tunapata ulinganisho mkataa wa kuacha dhahiri ya dalili za kudumu milele motoni.

Pili: Sisi tunazungumza mambo ya kiitikadi mkataa, sio masuala ya matawi ya kudhania; na mafaqihi pamoja na kujichunga kwao na nguvu ya imani zao, wanakuwa ni wataalamu wa hukumu za Mwenyezi Mungu za kisharia sio mambo ya itikadi. Bali wengi katika wao wako katika daraja ya kufuata yale yanayorudia sifa za Mwenyezi Mungu na vitendo Vyake.

Ama yale yanayorudia kwenye dalili za kuweko Muumbaji (s.w.t.) ni dalili za mzunguuko na kuendelea. Hata hivyo ni lazima ieleweke kuwa sisi tunaamini kuswihi kufuata katika misingi ya itikadi ikiafikana na mambo yalivyo.

Tatu: Akili huona vibaya kukhalifu ahadi, lakini sio kiaga. Ukimwambia mtu mwingine nitakufanyia wema; kisha uvunje ahadi, basi utakuwa mwenye kulaumiwa mbele za wenye akili. Ama ukamwambia unayemdai haki: Nitachukua haki yangu tu kutoka kwako kisha umsamehe, basi wewe utakuwa mwenye kusifiwa mbele ya Mwenyezi Mungu na watu; hasa akiwa yule unayemdai ni fukara na wewe ni tajiri. Na Mwenyezi Mungu ni tajiri kwa viumbe na adhabu zao. Na wao wana haja sana ya rehema Yake na msamaha Wake.

Swali la nne na la mwisho: Kwa nini unaleta taawil ya Aya za kudumu motoni na ni maana gani unayoyachukulia?

Jibu: Inawezekana kuchukulia maana ya kudumu muda mrefu, lakini sio milele; au kudumu motoni bila ya adhabu; kama hema la Hatimtai2 au kuwepo Ibrahim katika moto.

Haya yanatiliwa nguvu na yaliyopokewa katika baadhi ya Hadith kwamba baadhi ya watu wa motoni watakuwa wanacheza na makaa ya moto kama mpira wakirushiana. Hapana mwenye shaka kwamba mchezo huu hauwezi kuwa pamoja na adhabu hata hafifu sikwambii kali yake.

Na Mungu si Mwenye kushindwa kuufanya moto baridi na salama kwa asiyekuwa Ibrahim kama alivyoufanya kwa Ibrahim (a.s.).

Muhhiddin Ibn al Arabi anasema katika al Futuhul Makkiyya J2 uk. 127: "Hatobaki motoni mwenye kumwamini Mungu mmoja katika waliopelekewa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.), kwa sababu moto utarudi kuwa baridi na salama kwa wanaompwekesha Mwenyezi Mungu kwa baraka za Ahlul Bait katika akhera. Ni utukufu ulioje wa baraka za Ahlul Bait!
أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِي حَاجَّ إِبْرَاهِيمَ فِي رَبِّهِ أَنْ آتَاهُ اللَّهُ الْمُلْكَ إِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ رَبِّيَ الَّذِي يُحْيِي وَيُمِيتُ قَالَ أَنَا أُحْيِي وَأُمِيتُ ۖ قَالَ إِبْرَاهِيمُ فَإِنَّ اللَّهَ يَأْتِي بِالشَّمْسِ مِنَ الْمَشْرِقِ فَأْتِ بِهَا مِنَ الْمَغْرِبِ فَبُهِتَ الَّذِي كَفَرَ ۗ وَاللَّهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ {258}
Je, hukumjua aliyehojiana na Ibrahim juu ya Mola wake kwa sababu Mwenyezi Mungu alimpa ufalme ? Ibrahim aliposema: Mola wanguniyuleambayehuhuishana kufisha. Yeye akasema: Mimi pia nahuhuishanakufisha. Ibrahim akasema:HakikaMwenyeziMungu hulichomoza jua mashariki, basi wewe lichomoze magharibi. Akafedheheka yule aliyekufuru, na MwenyeziMunguhawaongoziwatu madhalimu.
________________________
1. Mujtahid aliye marjaa: yaani kiongozi anayefuatwa katika madhehebu ya Shi'a katika zama za kughibu kwa Imam Mahdi (a.s)

2. Katika baadhi ya riwaya ni kwamba Hatimtai ataingia motoni kwa sababu ya kufuru yake, lakini atakuwa na hema la kumkinga joto kwa sababu ya ukarimu wake. Huyu alikuwa ni mtu aliyepigiwa mfano kwa ukarimu wake wa kupindukia.
Maana
Mwenyezi Mungu, katika Aya iliyotangulia, amebainisha kuwa mtawala wa waumini ni Mwenyezi Mungu, na kwamba wao wanatoka katika giza la shaka kuingia kwenye mwangaza wa uongofu na imani. Na makafiri watawala wao ni mataghuti wanaowatoa kwenye mwangaza wa kimaumbile na kuwaingiza katika giza la ukafiri na upotevu.

Baada ya hapo anatoa kisa, kwa Mtume wake mtukufu juu, ya Mumin aliyetoka kwenye giza la shaka na kuingia katika nuru ya imani, katika Aya ijayo. Na kisa cha kafiri aliyehojiana na Ibrahim juu ya Mola wake baada ya kutoka kwenye nuru ya kimaumbile kwenda kwenye giza la ukafiri, katika Aya hii.

Je, hukumjua yule aliyehojiana na Ibrahim juu ya Mola wake, kwa sababu Mwenyezi Mungu alimpa ufalme? Ibrahim aliposema: Mola wangu ni yule ambaye huhuyisha na kufisha. Yeye akasema: 'Mimi pia na huhuyisha na kufisha'

Hii ni hoja anayoitaja Mwenyezi Mungu kwa Mtume na kwa watu wote katika mfumo wa kus- taajabu pamoja na kukanusha.

Ibrahim (a.s.) alitoa mwito wa kutupiliwa mbali masanamu na mataghuti na kuwa kwenye dini ya uadilifu na usawa, lakini akapingwa na watawala., sio kwa kuona mwito wake sio sawa, bali ni kwa kuhofia manufaa na chumo lao na kupupia wasishuke vyeo vyao.

Kama kawaida walianza kujadiliana na Ibrahim kwa maneno; waliposhindwa wakawa hawana la kusema, ispokuwa walitangaza vita na wakajaribu kummaliza kwa kumchoma katika moto; sawa na wanavyofanya wakoloni hivi sasa - wanaeneza propaganda za upotevu kwa njia ya magazeti, radio na mashirika ya habari yaliyonunuliwa; wakishindwa wanaanza kampeni za mapinduzi, wakishindwa hutupa mabomu ya Napalm kwa watu wanyonge wasiokuwa na hatia yoyote.

Basi yule ambaye amepetuka mpaka kwa mali na jaha alimuuliza Ibrahim: "Ni nani Mola wako?" Ibrahim akajibu: "Mola wangu ni yule anayempa uhai anayemtaka kisha huuondoa na wala hana anayeshirikiana naye katika hilo."

Yule Taghuti akasema: "Mimi pia ninaweza hivyo." Akawaleta watu wawili; akamwua mmoja wao na kumwacha mwingine. Ibrahim alipoona kujigamba kwa Taghuti kwa kutegemea, maneno na kujitia kutofahamu hoja na maana halisi yaliyokusudiwa, alileta mfano mwingine ambao hauwezi kuingizwa makosa wala madai yoyote, akasema:

Hakika Mwenyezi Mungu hulichomoza jua Mashariki, basi wewe lichomoze Magharibi. Akafedheheka yule aliyekufuru.

Kwa sababu alishindwa kubabaisha na kupotosha. Hivi ndivyo anavyojaribu kufanya kila mbatilifu - kujisifu na kufanya hila; hila zinaposhindwa hudangana akawa hana la kufanya.

Kundi la wafasiri wamesema kuwa ni jawabu la pili la Ibrahim; la kwanza ni 'Ambaye huhuisha na kufisha' na la pili ni 'Basi wewe lichomoze magharibi' ili akate mjadala upesi bila ya kurefusha.

Razi na Sheikh Muhmmad Abduh, wanasema kuwa hilo ni kuleta mfano mwingine ili kufafanua zaidi dalili; kwa maana yakuwa yule ambaye anatoa uhai ndiye ambaye analichomoza jua kutoka mashariki; na kama ukiweza kuwafunika watu wako kwa mfano wa kwanza basi utashindwa kuwafunika katika mfano huu.

Vyovyote itakavyokuwa, iwe ni majibu mawili au mifano miwili, lakini ni kwamba kafiri alishindwa na kuzibwa mdomo; na alishindwa kwa vile hana haki, naye hana haki, kwa vile ni kafiri.

Na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu madhalimu.

Ambao wamejidhulumu kwa kuinusuru batili na kuipinga haki.

Aya haikutaja jina la Taghuti kwa sababu, muhimu ni kupata mazingatio ya kisa sio jina la mhusika. Imetangaa kwamba alikuwa ni Namrud bin Kan'an bin Sam bin Nuh. Inasemekana kwamba yeye ndiye wa mwanzo kuvaa taji kichwani; akatakabari na kudai uungu. Tutarudia kuelezea kisa cha Ibrahim na watu wake katika Sura ya Anbiya (Mitume) na sehemu nyinginezo.
أَوْ كَالَّذِي مَرَّ عَلَىٰ قَرْيَةٍ وَهِيَ خَاوِيَةٌ عَلَىٰ عُرُوشِهَا قَالَ أَنَّىٰ يُحْيِي هَٰذِهِ اللَّهُ بَعْدَ مَوْتِهَا ۖ فَأَمَاتَهُ اللَّهُ مِائَةَ عَامٍ ثُمَّ بَعَثَهُ ۖ قَالَ كَمْ لَبِثْتَ ۖ قَالَ لَبِثْتُ يَوْمًا أَوْ بَعْضَ يَوْمٍ ۖ قَالَ بَلْ لَبِثْتَ مِائَةَ عَامٍ فَانْظُرْ إِلَىٰ طَعَامِكَ وَشَرَابِكَ لَمْ يَتَسَنَّهْ ۖ وَانْظُرْ إِلَىٰ حِمَارِكَ وَلِنَجْعَلَكَ آيَةً لِلنَّاسِ ۖ وَانْظُرْ إِلَى الْعِظَامِ كَيْفَ نُنْشِزُهَا ثُمَّ نَكْسُوهَا لَحْمًا ۚ فَلَمَّا تَبَيَّنَ لَهُ قَالَ أَعْلَمُ أَنَّ اللَّهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ {259}
Aukamayulealiyepitakaribuna mji nao umeangukiana sakafu zake,akasema: MwenyeziMungu atauhuisha vipi (mji) huu baada ya kufa kwake? Mwenyezi Mungu akamfisha kwa miaka mia, kisha akamfufua, akamuuliza: Umekaa mudagani? Akasema:Nimekaa muda wa siku moja au sehemu ya siku. Akasema: Bali umekaa miaka mia, tazama chakula chako na kinywaji chako hakikuharibika. Na mtazame punda wako na ili tukufanye uwe ni ishara kwa watu. Na itazame mifupa jinsi tunavyoinyanyua, kisha tunaivisha nyama. Basi yalipombainikia alisema: Najua kwamba Mwenyezi Munguni Mwenye uwezojuu ya kila kitu.
 
Maana
Aya iliyotangulia ilikuwa ni mfano kwa kafiri ambaye amemfanya Taghuti kuwa ni mlinzi na mtawala wake, na kutoka katika mwangaza na kuingia katika giza; na Aya hii ni mfano wa Mumin aliyemfanya Mwenyezi Mungu kuwa mtawala wake; akatoka gizani na kuingia katika mwangaza.

Au kama yule aliyepita karibu na mji nao umeangukiana sakafu zake akasema: Mwenyezi Mungu ataufufua vipi (mji) huu baada ya kufa kwake?

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakufafanua jina la mji wala jina la aliyepitia. Hapo ndipo wakahitalifiana wafasiri - kwamba je, mtu huyo alikuwa kafiri, je alikuwa Uzairi (Ezra), Armila (Nehemia) au Khidhr? Vile vile wametofautiana kuhusu mji, je ulikuwa Baitil Maqdis au mji mwingine?Hakuna dalili yoyote juu ya hayo isipokuwa Hadith za Kiisrail tu.

Maana ya mji ulioangukiana sakafu zake ni kuwa hauna watu na majumba yamevunjika umebaki magofu; na swali lilikuwa la kuuliza kufufuliwa watu wa mji sio mji wenyewe.

Yule anayedai kuwa aliyepita katika mji alikuwa kafiri kwa vile alitia shaka katika kudura ya Mwenyezi Mungu, tunamwambia kuwa, sio kila anayepitiwa na shaka akilini mwake na akataka ufafanuzi, ni kafiri; bali ni kinyume cha hivyo. Ibrahim alimtaka Mola wake amuonyeshe anavyohuisha waliokufa na hali yeye alikuwa akilingania imani na yakini.

Zaidi ya hayo ni kwamba kutaka kujua zaidi kudura ya Mwenyezi Mungu ndio imani yenyewe. Kwa hivyo basi linabainika kosa la anayedai kuwa aliyepita mjini alikuwa kafiri sio kwa jengine ispokuwa tu, ati amesema: Mwenyezi Mungu ataufufua vipi (mji) huu baada ya kufa kwake?

Hapana! Huko sio kukanusha, isipokuwa kubomoka huko alikokuona kulimfanya apigwe na butwaa na kushindwa kujua njia ambayo itawarudishia uhai watu wa mji huo.

Mwenyezi Mungu akamfisha kwa miaka mia.

Hayo yalikuwa ni mauti ya hakika sio majazi. Hapo hapahitaji taawil.

Kisha akamfufua.

Alimfufua kama alivyokuwa. Wala si zito hilo kwa ambaye anauambia ulimwengu na kilicho katika ulimwengu 'kuwa', kikawa. Hakuna kitu cha ajabu kabisa kama kumlinganisha Muumbaji na viumbe katika uwezo Wake.
Hisabu Ya Kaburini
Akamuuliza: Umekaa muda gani?

Hili ni swali la kuthibitisha, sio la kutaka kufahamu.

Akasema: Nimekaa muda wa siku moja au sehemu ya siku.

Lau si Ijmai (kongamano la wanavyuoni) na hadithi ingeliwezekana kusema kuwa hakuna hisabu kaburini wala kuulizwa, isipokuwa siku ya ufufuo kwa kutegemea Aya hii na Aya nyingine inayosema: "Na siku kitakaposimama kiyama wataapa wenye makosa kuwa hawakudumu isipokuwa saa moja tu ..." (30:55)

Wala hakuna sababu ya wakosaji kuapa na kughafilika na muda uliopita toka kufa kwao isipokuwa kwa kukosa uhai, kwa sababu kuhisi muda hakuwi isipokuwa mtu huyo awe na uhai.

Sheikh Mufid katika kitabu Awailul Maqalat anasema kwamba, watu baada ya kufa wako tabaka nne: Tabaka ya kwanza ni yule aliyeijua haki na akaitumia. Huyu atapewa uhai mzuri baada ya mauti kabla ya kufufuliwa. Tabaka ya pili ni yule aliyeijua haki na asiitumie kwa inadi.

Huyu vile vile atakuwa hai lakini ataadhibiwa. Tabaka ya tatu ni yule aliyefanya madhambi na maasi kwa kupuuza, sio kwa inadi. Huyu uhai wake ni wenye kutiliwa shaka baada ya kufa na kabla ya kufufuliwa. Tabaka ya nne ni wenye kuzembea kufanya twaa bila ya inadi na walio wanyonge. Hawa hawatafufuliwa, bali watabaki katika ulimwengu wa mauti mpaka siku ya kufufuliwa.

Sheikh Mufid amechukua ugavi huu kutokana na riwaya za Ahlul bait (a.s.); miongoni mwa hizo ni: "Hataadhibiwa kila maiti, isipokuwa ataadhibiwa kwa ukafiri hasa na atapata neema kwa imani hasa; na wasiokuwa hawa wawili watapuuzwa na wala hawataulizwa mpaka siku ya ufufuo. "Haya tumeyazungumza kwa ufafanuzi katika kitabu Falsafatul Mabdai Wal Ma'ad mlango wa "Baina ya dunia na akhera" na mlango "Hisabu ya kaburi."

Akasema: Bali umekaa miaka mia, tazama chakula chako na kinywaji chako hakikuharibika.

Amesema hakikuharibika na hakusema havikuharibika, kwa maana ya kuwa chakula na kinywaji ni aina moja tu katika kuharibika haraka. Maana ya hakikuharibika ni kwamba havikubadilika, pamoja na kupita miaka, bali vimebakia katika hali yake. Huu ni muujiza wa Mungu, kwa sababu chakula na kinywaji huharibika haraka. Hapa nahofia yule anayejaribu kuiambatanisha Qur'an na sayansi asije akasema kuwa vilikuwa katika jokofu (friji).

Na mtazame punda wako

Jinsi alivyogeuka na kuoza, lakini chakula na kinywaji vimebakia katika hali yake. Huu ndio muujiza zaidi na kudhihirisha kudura inavyogeuza kawaida. Kwa sababu anga ndiyo inayoathiri, kinywaji kingeharibika kabla ya punda, kwa sababu ndiye mwenye nguvu kuliko chakula na kinywaji. Kwa hivyo kufa punda na kudumu chakula, ni dalili ya kuwa Mwenyezi Mungu hashindwi na kitu chochote.

Inasemekana kuwa punda alibakia hai miaka mia bila ya kinywaji wala chakula. Kwa hali zote mbili, ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliyafanya hayo ili aondoe kustaajabu kwa Uzayr na kuona kwake ajabu ya kufufuliwa kwa mji huo; na pia ili amfanye kuwa ni hoja ya kupatikana ufufuo kwa yule atakayejua hali yake katika watu wa wakati huo. Hayo ndiyo makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.): "Na ili tukufanye uwe ni ishara kwa watu."

Na itazame mifupa jinsi tunavyoinyanyua, kisha tunaivisha nyama.

Wamehitalifiana kuhusu mifupa hii: Je ilikuwa ya Uzair au mifupa ya punda wake? Msemaji mmoja alisema kwamba hiyo ni mifupa ya mwenye punda, na kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alifufua jicho lake kwanza ili aone sehemu iliyobakia ya mwili jinsi inavyokusanyika na kupata uhai lakini huku ni kujisemea tu juu ya Mwenyezi Mungu bila ya elimu.

Lenye nguvu zaidi ni kwamba hiyo ni mifupa ya punda kwa sababu mwenye punda alisema: "Nimekaa muda wa siku moja au sehemu ya siku." Kwani lau angeliiona mifupa yake ilivyoharibika, angelitambua urefu wa muda aliokaa Mwenyezi Mungu aliivika nyama; sawa na alivyoanza kumuumba. Imam Ali (a.s.) anasema: "Kuisha dunia baada ya kuweko sio ajabu kuliko kuianzisha."

Basi yalipombainikia alisema: Najua kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu. Aliyasema haya baada ya kupitiwa na majaribio binafsi yasiyo na shaka. Vipi atie shaka na yeye ameshuhudia kwa macho miujiza mitatu: Kurudishwa hai baada ya kufa, kufufuliwa punda wake na kudumu chakula chake miaka mia bila kuharibika.

Funzo tunalolipata kutokana na kisa hiki ni kwamba mwenye akili hatakikani kukanusha lile lisilotambuliwa na akili yake, au lisiloafikiana na aliyoyasoma katika kitabu au kusikia kuto- ka kwa mwalimu wake, bali inatakikana ajizuie hata lile analoona linatofautiana na kanuni za kimaumbile. Elimu imethibitisha kuwa hakuna kanuni ya maumbile kabisa.
وَإِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ رَبِّ أَرِنِي كَيْفَ تُحْيِي الْمَوْتَىٰ ۖ قَالَ أَوَلَمْ تُؤْمِنْ ۖ قَالَ بَلَىٰ وَلَٰكِنْ لِيَطْمَئِنَّ قَلْبِي ۖ قَالَ فَخُذْ أَرْبَعَةً مِنَ الطَّيْرِ فَصُرْهُنَّ إِلَيْكَ ثُمَّ اجْعَلْ عَلَىٰ كُلِّ جَبَلٍ مِنْهُنَّ جُزْءًا ثُمَّ ادْعُهُنَّ يَأْتِينَكَ سَعْيًا ۚ وَاعْلَمْ أَنَّ اللَّهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ {260}
Na Ibrahim aliposema: Mola wangu! Nionyeshe jinsi unavyofufua wafu. (Mwenyezi Mungu) akasema: Huamini? Akasema: Kwanini!(naamini) Lakiniupate kutulia moyowangu. Akasema: Basi chukua ndege wanne na uwakusanye kisha (uwachinje) uweke juu yakilajabalisehemu katika wao. Kisha waite, watakujia mbio. NajuakwambaMwenyezi Mungu ni Mwenye n

Share this article

Comments 0

Your comment

Comment description

Latest Post

Most Reviews

MOST READ