Rafed English
site.site_name : Rafed English

Utumwa by : Allamah Sayyid Saeed Akhtar Rizvi

 

Kitabu hiki kimerudiwa kimechapishwa tena kwa ruhusa ya waandishi, ili kuafikiana na Kongamano la Kilimwengu la Umoja wa Mataifa dhidi ya Ubagazi wa Rangi, (United Nations World Conference against Racism) ambalo lilitegemewa kufanyika katika jiji la Durban, Afrika ya Kusini, mwezi Augosti, 2001. Mada mbili zilizo pendekezwa kuwepo kwenye agenda zilisababisha migongano ya kimataifa. Agenda hizi zilikuwa: Malipo ya fidia kwa utumwa na biashara yake ambayo ilifanywa na mataifa ya Ulaya na Marekani (U.S.A) hapa Afrika na nyingine ilikuwa kulinganisha Uzayuni (Zionism) na ubaguzi wa rangi.

Suala la malipo ya fidia kwa Afrika kutoka kwa mataifa yaliyojihusisha na utumwa limeachwa kushugulikiwa kwa muda kwa makubaliano baina ya mataifa yanayodaiwa na Afrika, kuweka nguvu na msukumo mkubwa katika kuisaidia Afrika kuendeleza mpango wake wa kurejesha hali nzuri ya uchu mi. Mpango mmoja wapo unaojulikana sana ni ule wa: Millenium Africa Recovery Plan, ambao unasimamiwa na Rais Thabo Mbeki wa Afrika ya Kusini. Msaada unaozungumziwa hapa bila shaka unaeleweka kwamba ni aina ya ukandamizaji wa kiuchumi kwa kuendeleza utumwa wa kiuchumi hapa Afrika daima milele.

Wayahudi wapatao milioni tatu (3) waliuawa wakati wa vita kuu ya Pili ya Dunia ambapo zaidi ya Waafrika milioni kumi (10) walichukuliwa kuwa watumwa. Malipo ya fidia kwa ajili ya mauaji ya Halaiki ya Wayahudi yanaendelea hadi leo. Msaada wa ruzuku kwa serikali ya Uyahudi (Israeli) kutoka Marekani ambao ulianza kutolewa tanga 1948 sasa umefika kiwango cha dola za Kimarekani billion 18. Utafutaji wa watu watuhumiwa wa “makosa ya kivita” ambao yasemekana ndio walio husika kuwaua Wayahudi tangu 1939 hadi 1943 unaendelea hadi leo. Kwa mara ya kwanza Wayahudi walidai fidia mnamo mwaka wa 1951 kiasi cha dola za Kimarekani bilioni (1.5) moja na nusu. Madai haya yalifanyika miaka sita baada ya kukoma Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Ni takribani miaka 140 tangu kupigwa marufuku utumwa katika nchi za Magharibi. Makubaliano yalisainiwa na Chansela akiwakilisha Ujerumani mnamo tarehe 10 Septemba, 1952.

Je uhai wa Mwafrika hauna thamani ya kutosha ili ulipiwe fidia? Majumba ya makumbusho na makaburi makubwa yanajengwa kwa madhumuni ya kuhuisha kumbukumbu ya wale wanaodaiwa “kuuawa kikatili na Manazi wa Kijerumani.” Dunia inalazimishwa kutubu dhambi zake dhidi ya Wayahudi, na pamoja na kisingizio hiki bandia, hakuna uhalali wa hata kidogo unoifanya Israeli kulundika silaha nyingi kiasi hicho kisicho linganishwa. Yeshayahou Lebowtz (Israel and Judaism, Jerusalem, 1987) ameandika kwa ufupi: “Israeli si dola yenye kumiliki jeshi, bali ni jeshi lenye kumiliki dola.”
Utumwa Mambo Leo
Uendelezaji wa wazi wa aina za utumwa unaweza kufanikiwa kwa njia ya kusaidia Mipango kama vile “Millenium African Recovery Plan.” Utandawazi kupitia umiliki wa nguvu za uzalishaji unaofanywa na “Muungano wa Kimataifa wa Wakiritimba” (Multi Ntional Cartels) tayari upo. Mfumo huu hupenya kwenye kila tabaka la uchumi wa dunia, iwe ni bidhaa zinazo zalishwa, kama sukari, silaha za kivita, madawa ya tiba au biashara ya dhahabu na madini ya platinamu. Utumwa wa kiuchumi kupitia udhibiti mkali wa mtiririko wa mitaji ulimwenguni uko imara mikononi mwa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF). Uharibifu kwa Afrika ulitokea kwa njia ya utawala wa mabavu wa kikoloni wa moja kwa moja, uliofanywa na Uingereza, Udachi, Ufaransa, Ureno na Ubeligiji. Hii ilifu atiwa na udhibiti wa nje ya Afrika, kwa kuanzisha serikali kidhalimu ili kuendelea kudhibiti kwa njia za hila zaidi. Kwa kufichuliwa vibaraka hawa kwa ajili ya ulimwengu kuwaona, ikawa vigumu zaidi kuendelea kwa uwazi kusaidia vitendo vyao viovu dhidi ya jamaa zao. Vurugu zilidhibitiwa ili kuhakikisha kuendelea uingiaji kwenye hakiba kubwa za madini.

Njia changamano ilikuwepo kazini kwa zaidi ya miaka 30, ambayo ni kulitumbukiza bara hili (la Afrika) kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe visivyo na maana yoyote. Ahadi za “kusamehe madeni” zinatolewa kwa lengo la kuendeleza utumwa kwa Waafrika. Huu “Utumwa Mpya” unaweza kuonekana tofauti kwa nje na ule wa “West African Slave Trade” (Biashara ya utumwa ya Afrika ya Magharibi), lakini misingi yake inafanana. Kwa kuanzishwa kwa mfumo wa makao makuu ya fedha (Benki ya Dunia na shirika la Fedha la Kimaraifa), Polisi wa Dunia (North Atlantic Treaty Organization), imewarahisishia wakoloni kazi ya kuwa na mamlaka ya kuitawala Afrika. Mfano wa wazi unaoonyeshwa na nguvu hizi za wakoloni na washirika wake, ni kuunda taifa la Israeli katikati ya Rasi ya Arabia. Kwa hiyo ni muhimu sisi kuchambua na kuonye sha ulinganifu huu baina ya Uzayuni (Zionism) na washiri ka wake na ukubwa na vipimo vya utumwa unaoendelezwa na nguvu za wanyonyaji.

Kwa hiyo, tumeona ni muhimu kukichapisha kitabu hiki, kiitwacho: “Utumwa, kwa Mtazamo wa Kiislamu na Usio wa Kiisilamu”, kilichoandikwa na Allamah Sayyid Saeed Akhtar Rizvi (ambacho kilichapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1972).

Kwa madhumuni ya: Kuwataarifu kwa mara nyingine washiriki kwenye Kongamano hili kuujua uovu halisi wa utumwa ambao umekuwa unaendelea kwa karne tano zilizopita.

Kupanua akili za wasomaji na hivyo kutambua jinsi utumwa ulivyogeuzwa na kuwa kama ulivyo sasa katika hali yake ya udanganyifu zaidi, na njama za nchi ya Israeli na Marekani zenye sera za kuuendeleza ili ziweze kutimiza malengo yao ya siri.

“Ahlul Bait (A.S) Foundation of South Africa” inaona fahari kuitambulisha kazi hii rasmi yenye thamani na wanayo matumaini kwamba usiri unaogubika akili zetu utaondolewa na kuamsha akili za watu wote wenye msimamo unaostahili.

Kwa kweli sisi ni wadeni kwa Muadhama Allamah Sayyid Saeed Akhtar Rizvi (Dar es salaam, Tanzania) na kwa unyenyekevu tunashukuru juhudi zake za miongo michache katika kueneza mafundisho ya Uislamu hapa Afrika. Tabia yake ya kisomi imeonekana kwenye mfululizo wa mada nyingi zilizo chapishwa zikijumuisha maelekezo ya jumla kama vile “Haja ya Dini”, hadi kufikia kazi za kisomi kama hii. Bilal Muslim Mission of Tanzania, imefanya kazi kubwa ya kueneza kazi hii na zingine nyingi za maandishi na akawatia moyo Waislamu na wasio Waislamu duniani kote pamoja na Afrika ya Kusini katika kipindi cha zaidi ya miaka 50 iliyopita.

Mwenyezi Mungu amzidishie neema hapa duniani na akhera, na tunamwomba Muweza wa yote amjaalie nafasi kubwa zaidi ya kutunufaisha kwa kutumia kalamu yake, Insha-Allah.

Syed Aftab Haider
Ahlul Bait Foundation of South Africa
August 2001
Kitabu kilichoko mikononi mwako, ni tarjuma ya kitabu cha Kiingereza, kwa jina la “Slavery – Islamic & Western Perspectives kilichoandikwa na Mwanachuoni mkubwa Marhum Allamah Sayyid Sa’eed Akhtar Rizvi.

Kitabu hiki kwa ufupi kinaelezea juu ya biashara ya utumwa ilivyokuwa ikiendeshwa na wazungu hapa Afrika, wakisaidiwa na Kanisa Katoloki na Makinisa mengine yaliyofu-atia. Mwandishi kwa kutumia elimu, akili, mantiki na utafiti wa kina, amefichua ukweli wote uliokuwa umejificha nyuma ya biashara hii ya udhalilishaji wa binadamu. Hapa Afrika na duniani kote, watu wangali wanaamini kwamba biashara ya utumwa hapa Afrika (hususan Afrika ya Mashariki) ilianzishwa na kuendeshwa na Waraabu wakiungwa mkono na Uislamu. Kwa hiyo mbele za watu Uislamu ulionekana kama dini isiyojali ubinadamu, iliyowaswaga mababu zetu kama wanyama na kuwafanya watumwa kwenye nchi zao. Mwandishi anayakanusha yote haya, na kuonyesha jinsi gani Uislamu ulivyokuwa dhidi ya biashara hii ya tumwa, na ulivyofanya ili kukomesha biashara hii. Na kuonyesha jinsi gani Wazungu walivyoing’ang’ania biashara hii, na jinsi Mapadre na Maaskofu walivyozibariki meli zilizokuwa zimebeba watumwa.

Tumeona tukitoe kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili ili kizidishe mwanga wa elimu kwa Waislamu (na wasio kuwa Waislamu) wazungumzaji wa Kiswahili, na hili likiwa ndilo lengo kubwa la Taasisi yetu ya ‘Al`Itrah Foundation’ katika kuwahudumia Waislamu hususan wazungumzaji wa Kiswahili.

Tunamshukuru Ndugu yetu al-Akh Salman Shou kwa kukubali jukumu hili la kukifanyia tarjuma kitabu hiki. Vile vile tunawashukuru wale wote walioshiriki kwa njia moja au nyingine hadi kufanikisha kuchapishwa kwa kitabu hiki.

Ni matumaini yetu kwamba kitabu hiki kitakuwa ni mwanga kwa wasomaji wetu na kuzidisha upeo wao wa elimu, na kuondokana na dhana hii potofu juu ya biashara ya utumwa.

Mchapishaji:
Al-Itrah Foundation
S. L. P. 1017
Dar-es-Salaam
Tanzania.
Utumwa ni moja wapo ya maovu ambayo yamekuwepo katika jamii tangu kuwepo kwa mwanadamu hapa duniani na jitihada za wanamageuzi kujaribu kuuzuia zimeshindwa kwa karne nyingi sana. Ustaarabu wa kale haukuweza kuondoa utumwa, kwa hiyo jamii za wakati huo ziliafiki kuwa nao. Baadhi ya jamii hizo za kistaarabu ziliulea utumwa. Makanisa ya Kikristo yalishiriki katika biashara ya utumwa. Mapadri wao walizibariki meli zilizokuwa zinabeba shehena za binadamu na waliwaonya watumwa kuwa watiifu, lakini hawakuwasihi mabwana wenye kumiliki watumwa kuwa wapole kwa shehena hizo za watu. Hivi karibuni mnamo mwaka 1970 Kanisa Katoliki lilinunua wasichana 1500 kutoka India, eti kwa sababu wasichana wa kizungu huko Ulaya hawakutaka kuishi maisha ya kitawa (usista). Miongoni mwa dini zote ni Uislamu tu ndio ulioharibu misingi yote ya uovu huu. Lakini, ni kejeli ya histo ria kwamba watu walio rutubisha utumwa wakasaidia uendeleaji wake na walifaidika nao, baadaye ndio wakawa mabingwa wa kuukomesha.

Allamah Sayyid Saeed Akhtar Rizvi, Mhubiri Mkuu wa Bilal Muslim Missioni of Tanzania, amekiandika kitabu hiki kwa uwezo mkubwa na jitihada. Kama ilivyo kwa msomi mtafi- ti kama yeye, ameshuhgulikia mada ya kitabu hiki bila upendeleo, Ameupanga ukweli baada ya ukweli kutoka kwenye historia; amenukuu kutoka kwenye Qur’ani, hadithi na waandishi wa zama za leo kuhusu somo hili, na ameonyesha sheria za Kiislamu na zile zilizotumika kabla ya Uislamu.

Ameonyesha waziwazi kwamba ustaarabu wa Kimagharibi sio bingwa mkubwa kiasi hicho wa kuwaokoa watumwa kama unavyojionyesha. Kwa kweli kitabu hiki kitathibitisha kuwa kifungua macho kwa wale ambao hukubali bila kuchunguza kuhusu propaganda ya ubinadamu wa Kimagharibi.

Peermahomed Ebrahim Trust kwa fahari kubwa wanakileta kitabu hiki kwa wasomaji na wana matumaini kitakubaliwa na jamii.

Wadhamini,
Peermahomed Ebrahim Trust Karachi, Pakistan
15 Jamadi, 1392
27 June, 1972.
Kitabu hiki kiliandikwa kwa ombi la marehemu Haji Hasanali P. Ebrahim, ambaye ndiye aliye kichapisha kutoka kwa Peermahomed Ebrahim Trust, Karachi, mnamo mwaka 1972. Mara baada ya kuchapishwa, nakala zote zilinunuliwa, lakini mahitaji yakawa bado yanaendelea.

Kwa kukidhi mahitaji hayo, mwanangu, Hujjatul Islam Sayyid Muhammad Rizvi sasa ametayarisha toleo la pili.

Baadhi ya mabadiliko madogo madogo yamefanywa katika mpangilio wa Sura; ibara zimeongezwa hapa na pale; na mwanangu ametayarisha maelezo ya ufafanuzi chini ya kurasa, ambayo yameongeza ubora wa kitaaluma wa kitabu hiki. Mwenyezi Mungu na amrefushie maisha na amwongeze nguvu za kuendelea kuutumikia Uislamu wa kweli kwa uaminifu. Pia ninawashukuru marafiki ambao wamenisaidia kwa namna yoyote ile katika kufanikisha kuchapishwa toleo hili:

S.S. A. Rizvi
Gopalpur (India)
28 Novemba 1987.
"Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na wanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni aliye mchamungu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari." (Qur'an 49:13).

Utumwa sio taasisi iliyoanzishwa na Ukristo au Uislamu. Ni Utumwa ulikuwepo kwa muda mrefu hata kabla ya kuanzishwa hizi dini mbili. Kwa mtazamo wa haraka kuhusu utumwa wa kale, ninamnukuu Jaji Ameer Ali:

“Shughuli ya Utumwa ina rika moja sawa na kuwepo kwa binadamu. Kihistoria dalili zake zinaonekana katika kila zama na kila taifa…Wayahudi, Wayunani, Warumi na Wajerumani wa kale, watu ambao taasisi zao za kisheria na za kijamii zilizoathiriwa mno na tabia na desturi za kisasa, walizitambua na kuzifanya aina zote za utumwa, utumwa wa kazi za kiuchumi na wa kazi za nyumbani. Baada ya kuanzishwa kwa makundi ya washenzi wa Magharibi na Kaskazini katika mabaki ya dola ya Warumi, zaidi ya utumwa wa mtu binafsi, utumwa wa taifa moja kulifanya taifa lingine kuwa mtumwa, ambao haukujulikana sana kwa Warumi, ukashamiri kwenye nchi zote mpya zilizo kaliwa… kanuni za kishenzi, kama zile za Warumi, ziliona utumwa kama hali ya kawaida ya binadamu; na kama mtumwa alipewa ulinzi, ilikuwa kwa sababu mtumwa alikuwa mali inayo milikiwa na bwana wake, ambaye ni yeye peke yake baada ya nchi, alikuwa na mamlaka juu ya uhai na kifo kwa mtumwa.1 Katika nchi ya Uajemi (Persia) ikulu ya Mfalme ilikuwa na watumwa wanawake elfu kumi na mbili. Wakati Mfalme wa Byzantine anaketi kwenye kiti chake cha enzi, maelfu ya watumwa walikuwa tayari kutoa huduma kamili na mamia ya watumwa waliinama kuonyesha heshima wakati mfalme anainama kuvaa viatu. Huko Ugiriki au Uyunani, idadi ya watumwa ilikuwa kubwa zaidi ya watu walio kuwa huru, licha ya kwamba Ugiriki ilitoa watetezi wakubwa wa ubinadamu na haki.

Kila jeshi la Kiyunani ambalo lilirudi nyumbani na salamu za ushindi, lilifuatwa na kuindi la watumwa. Aristotle, mwanasalsafa maarufu wa zamani, alipokuwa anazungumzia suala la iwapo kila mtu alikusudiwa na maumbile kuwa mtumwa au la, anasema: “Hakuna ugumu katika kujibu swali hili, katika misingi yote miwili, ya akili na kweli.

Ya kwamba watu baadhi fulani watawale na wengine watawaliwe si tu kwamba ni jambo muhimu bali ni kitu chenye manufaa kuanzia saa ya kuzaliwa kwao, watu wengine wameumbwa ili wawe watumwa, wako kwa ajili ya kutii tu, na wengine wameumbwa kwa ajili ya kutawala.” Halafu anahitimisha; “…watu wengine kwa asili wako huru, na wengine ni watumwa, na kwa utumwa huu (uliotajwa) wa mwisho, wote ni wenye manufaa na haki.”2 Katika utawala wa Rumi, utumwa wa kale ulifika kilele chake, lakini Dola ya Kirumi ilipoanza kuanguka, watumwa wengi wakaanza kuwa na hali nzuri kwa kiwango kidogo.

Lakini uovu wa utumwa ulionekana wazi kabisa. Uovu huu ulishinda ujuzi wa uhalali wa Kiyunani kama ambavyo imeshinda falasfa stadi ya Kigriki.

Kuonyesha mapenzi kwa watumwa lilionekana si tendo la hisia za kawaida lakini ilikuwa tabia pekee ya mtu mwenyewe binafsi. Mtumwa hakuonekana kama binadamu, hakuwa na haki, hakuwa na roho.3 Wakati huo wa ujio wa Uislamu (mnamo karne ya 7 CE) utumwa ulikwisha enea kote kote huko India, Ajemi, Rumi, Rasi ya Arabia, Romania na Ugiriki. Watu waliokuwa na hali nzuri na nafasi nzuri na wasomi wa nchi hizi hawakuwatilia maanani watumwa kustahiki kupatiwa hata angalao pia haki za msingi za kibinadamu.

Mtumwa alikuwa anaonekana kama bidhaa isiyo na thamani zaidi kuliko hata ya ng’ombe.4 Mara nyingi mtumwa aliuzwa kwa bei rahisi kuliko kondoo na mbuzi. Kwenye hafla maalum za kijamii wageni waheshimiwa wa nchi walikuwa na tabia ya kukusanyika pamoja na Kiongozi wa Nchi kutazama michezo ya kupigana watu na katika michezo hii watumwa walifanywa wapigane kwa kutumia mapanga na mikuki kama vile maonyesho ya mapigano ya jongoo wawili na kware katika kipindi cha zamani cha jamii ya kikabaila. Watu walishangilia kwa kupiga makofi hadi mtu mmoja miongoni mwa wapiganaji aliuawa. Watazamaji walimshangilia sana mshindi.5

Kwa upande mwingine, Rasi ya Arabia ilizunguukwa na nchi ambazo bado zilikuwa na dalili za ufahari wa ustaaraabu wa Kirumi na Kiyunani uliokuwa unaporomoka, na kwa upande mwingine, ilizunguukwa na nchi zilizogubikwa na imani za dini za “Zoroastria” na “Uhindi.” Kama ilivyo tajwa hapo juu, kwenye nchi zote hizi utumwa ni taasisi iliyo tambuliwa.

Vibao kumi na mbili vya maandiko (ya sheria zao) vilitoa mhuri wake rasmi kuithibitisha taasisi hii. Ukali usiopunguka wa matatizo na ukatili ambao watumwa walifanyiwa, haukupungua, lakini, kwa namna yoyote ile, watumwa sasa walikubaliwa kama wanyama (hayawani) ambao hatima yao ilikuwa ni kufanya kazi na kufa tu kwa manufaa ya hao walio wamiliki.

Sina nia ya kukifanya kitabu hiki kuwa historia ya unyama waliofanyiwa watumwa lakini itoshe tu kusema kwamba mtu lazima siku zote abebe hatia katika dhamira yake kwamba wakati fulani alijiingiza kwenye uovu wa utumwa.
________________________
1. Ameer Ali, Spirit of Islam (London: University paper back, 1965), PP. 259-261; pia angalia Will Duratnt, The Story ofa Civilisation, juzuu ya III (New York, 1944), P.397.

2. Aristotle, Politics, Book one, Sura ya 5 (New York: Modern Library, 1943), uk. 58-60.

3. Durant, W., op.cit., Juzuu ya III uk. 397, Juzuu IV (New York), uk. 29).

4. Ibid

5. Ibid.
Ingawaje utumwa ulikuwa taasisi ya kale ambayo ilianza kabla ya historia ya binadamu haijaanza kuandikwa, ni salama kusema kwamba ukubwa wa biashara hii ulifika kilele chake kwa kuendelezwa na mataifa ya Kikristo ya Ulaya na Amerika ambao kama ilivyo kawaida yao, waliigeuza kuwa biashara yenye utaratibu uliopangwa kwa uangalifu sana na wakaanza kuwakamata watumwa kwa maelfu. Kabla hatujaanza kutoa maelezo ya biashara hii mbaya sana ya utumwa ambayo ilianzishwa na Wareno, Wahispania na mamlaka zingine za kiubaharia za Kikristo kutoka Magharibi kwa ajili ya makoloni yao mapya, hebu tuangalie kwanza tuone kama Ukristo, kama mfumo na imani, ulifanya lolote wakati wa siku za mwanzo sana kupunguza ukali wa mateso kwa wengi wa watumwa. Jaji Ameer Ali anaandika kuhusu Ukristo:

Ukristo uliona utumwa kuwa ni taasisi iliyo tambuliwa na himaya (dola); na wenyewe ukakubali mfumo huu bila ya hata kujaribu kupunguza uovu wake, au kuahidi kukomesha polepole, au kuboresha hadhi ya watumwa.

Chini ya sheria ya nchi, watumwa walikuwa kama mali inayo hamishika. Waliendelea kuwa hivyo chini ya utawala wa Kikristo.

Utumwa ulishamiri miongoni mwa Warumi tangu zama za kale. Watumwa hao ama wamezaliwa wazalendo au wamezaliwa kutoka nje, ama walipatikana kutokana na ushindi wa vita au kununuliwa, walijulikana kama mali tu ya kuhamishika. Mabwana zao walikuwa na mamlaka na uwezo wa kuamua juu ya uhai au kifo kwao. Ukristo ulishindwa kabisa kukomesha utumwa au kupunguza uovu wake.1

Will Durant anatoa maelezo kuhusu nafasi ya Kanisa kama ifuatavyo. Kanisa halikulaani utumwa. Kanisa la Orthodox na waasi, Kanisa la Rumi na washenzi wote walidhani taasisi hii ilikuwa ya kawaida na haingeharibiwa. Sheria za kipagani zilimwingiza utumwani mwanamke yeyote aliye huru ambaye aliolewa na mtumwa; sheria za Mfalme Constantine (Mfalme Mkristo) ziliamuru mwanamke wa aina hiyo kuuawa kwa kukatwa kichwa, na mtumwa mwanamume kuchomwa moto akiwa bado yu hai.

Mfalme Gratian alitoa amri kwamba mtumwa yeyote aliye mshitaki bwana wake kuhusu kosa lolote isipokuwa uhaini dhidi ya serikali, lazima achomwe moto akiwa bado yu hai mara moja bila hata kufanya uchunguzi ili kupata uhalali wa shitaka.2

Rekebisho moja tu lililoagizwa na Ukristo linaonekana katika barua ya Mtakatifu Paulo kwa mtu fulani aitwaye Filemoni alipomrudisha mtumwa wake, aliyeitwa Onesimo, na kupendekeza amfanyie wema. Hakuna zaidi ya hapo. Inavutia kuona kwamba neno “slave” (“mtumwa”) la asili ya lugha ya Kiebrania limebadilishwa na kuwa “mtumishi wa nyumbani” kwenye toleo la Biblia liitwalo “Authorised Version of the Bible,” na likabadilishwa kuwa “mtumwa mtumishi” katika toleo liitwalo “Revised Standard Version,” kwa sababu, katika maneno ya “The Concise Bible Commentary,” neno hili (yaani mtumwa) limeachwa kutumiwa kwa sababu ya maana yake.3 Mtu hushanga iwapo mtarjumi anayo haki ya kubadilisha asili ya neno kwa sababu tu ya maana zake au ukumbusho wake?”

Itavutia kuona hapa kwamba neno “slave” (“mtumwa”) ni la asili ya Wazungu. Lilianza kuwapo na kutumika wakati Wajerumani (Franks) walipokuwa wanajishughulisha na kulipatia “Washenzi” soko la watumwa la Wahispania, na mateka hao walio wengi walikuwa Waturuki kutoka jimbo la Slovakia (sasa ni sehemu ya Czecoslovakia).

Watu hawa huitwa “Slav” na kwa hiyo mateka wote wakaitwa “slaves.”

Nukuu ifuatayo inaonyesha dhahiri mtazamo wa Uislamu na Ukristo kuhusu suala la utumwa na rangi ya ngozi: “Mwondoshe mtu mweusi! Siwezi kuzungumza naye,” alisema Archbishop Mkristo aliyeitwa Cyrus wakati Waarabu walioshinda walipowatuma wawakilishi wao wenye uwezo mkubwa ili wazungumze kuhusu makubaliano ya kusalimu amri mji mkuu wa Misri, ujumbe huu wa wawakilishi hawa uliongozwa na mtu mweusi aliyeitwa Ubaydah kama mtu mwenye uwezo mkubwa sana kuliko wote. Archbishop, alishangaa alipoambiwa kwamba mtu huyo mweusi alipewa ukubwa na maelekezo na Generali Amr, na kwamba Waislamu huwapa watu weusi na weupe heshima na daraja sawa na huwahukumia watu kwa tabia na si kwa rangi.4

Tukio hili linakupa tu maelezo kwa ufupi kile ninachotaka kueleza kwa urefu zaidi katika kitabu hiki.
________________________
1. Ameer Ali, op. cit., uk. 260-261

2. leeky, W.E. History of European Morals, Juzuu ya II ( New Yolk, 1926), kama ilivyonukuliwa na Will Durant, op. cit., juzuu ya IV, uik. 77.

3. Clarke, Rev. W. K. L, The Concise Commentary (London: S.P.C.K, 1952) uk. 976.

4. Leeder, S.S., Veild Mysteries, of Egypt (London, 1912), Uk. 332.
Uislamu mara nyingi umeelezwa na waandishi wa Kristo kwamba ni dini ambayo si tu kwamba ilifumbia macho utumwa bali pia iliuhimiza. Hii ni shutuma nzito sana iliyoelekezwa dhidi ya Uislamu, na kwenye kitabu hiki nakusudia kuonyesha uwongo wake. Kama ingewezekana, ningechukua mtizamo wenye huruma kwamba shutuma dhidi ya Uislamu zinatokana na kutokujua ukweli, lakini nahuzunika kuona kwamba wakosoaji wengi wanaonyesha kuwa na mwelekeo wa chuki na uovu. Tumeeleza kwa ufupi msimamo wa Ukristo kuhusu utumwa, na maelezo mengi zaidi yatatolewa baadaye. Hapa, kwa kuanzia ngoja tuuan- galie Uislamu na mfumo wa kanuni zake.

Kwa kadiri utumwa ulivyohusika, Waarabu katika siku za kabla ya Uislamu walikuwa wakosaji wabaya kama majirani zao. Watumwa walikuwa bidhaa ya biashara na utumwa ulikuwa ni asasi iliyokwisha anzishwa. Utumwa ulikuwa chanzo cha kupatia maisha kwa maelfu ya watu na chanzo cha kazi kwa maelfu ya wengi. Kwa watu wenye nafasi nzuri ya maisha idadi ya watumwa ndani ya kaya moja ilikuwa ni alama ya hadhi ya kaya hiyo.

Hii ndio hali iliyo kuwa wakati wa ujio wa Uislamu. Utumwa ulipinga msimamo wa Uisilamu kwa kiasi kikubwa kama ambavyo ibada ya masanamu inavyofanya. Lakini ambapo ibada ya masanamu ina mizizi yake katika mambo ya kiroho na kwa hiyo kuweza kukabiliwa na akili, utumwa mizizi yake ilikuwa katika biashara, katika muundo wa kijamii, katika miradi ya kilimo, na akili peke yake ilikuwa silaha dhaifu ya adui mwenye madhara mno na aliye jikita mizizi yake kwa ndani sana. Ni vipi basi utumwa ungeweza kukomeshwa?

Watu waliofahamishwa vibaya wanaweza kushauri kwamba Mtume wa Uislamu angeliweza kutumia nguvu. Lakini udhaifu wa nguvu kwa madhumuni haya unatambulika vizuri sana kwa wanafunzi wote wa elimu ya jamii wasio na upendeleo. Nguvu inaweza kufanikisha kusalimu amri, lakini bila kuepuka hufanikisha uadui. na mara nyingi uadui ni mkali sana kiasi kwamba mambo mengi mazuri yamepotea wakati nguvu ilipotumika kwa ajili ya maendeleo yake. Hali mbaya ya kusikitisha inayowapata watu weusi wa Marekani, ni mfano mmoja unaoonyesha jinsi gani matumizi ya nguvu yanavyoweza kuwa dhaifu wakati ikiwa lengo ni kupata mageuzi ya kijamii. Ukombozi wa watumwa haukubadilisha msimamo wa watu weupe kwa watumwa wao waliokombolewa, na uchungu ulioje wa urithi wa uhasama wa ubaguzi wa rangi ulioachwa katika jamii! Toynbee ameandika, “Watu weusi ambao walikomolewa kisheria kutoka kwenye utumwa huko Marekani (U.S.A) mnamo mwaka 1862, pamoja na sababu nzuri sasa wanayojisikia kwamba bado, zaidi ya karne moja baadaye, wananyimwa haki kamili za kibinadamu na raia wenzao walio wengi ambao ni Waamerika weupe. 1

Vita vya Uislamu dhidi vya utumwa vililenga kubadili, msimamo na fikira kwa jamii yote, ili kwamba baada ya kukombolewa, watumwa wangekuwa wafuasi wake waliofunzwa na wenye uzoefu wa muda mrefu, bila ya kuwepo na haja yoyote ile ya kufanya maandamano, migomo, maasi ya kijamii na ghasia au fujo za ubaguzi wa rangi. Na Uislamu ulilipata lengo hili lilioonekana haliwezekani (kupatikana) bila vita yoyote ile kupiganwa. Kusema kwamba Uislamu haukupigana vita kwa sababu ya kukomesha utumwa itakuwa si maelezo sahihi.

Uislamu ulipigana vita kwa sababu ya kuondoa utumwa, lakini, ni vita ambayo ilipiganwa si kwa kutumia upanga, wala hakuna damu iliyomwagika. Uislamu ulilenga vita yake kwenye chimbuko la adui yake (yaani utumwa) na kuunda washirika wake kwa kuamsha hisia zilizo bora zaidi za wafuasi wake. Mashambulizi dhidi ya utumwa yaliendeshwa kwa kulenga pande tatu.

Kwanza, Uislamu ulikataza kununua watumwa na kuwamiliki. Kabla ya kuja kwa Uislamu, utumwa uliendeshwa kiholela. Watu waliokuwa wanadaiwa walifanywa watumwa, mateka wa kivita, ama waliuawa. Kwenye mataifa yaliyo kuwa dhaifu, watu waliwindwa kama wanyama, wakauawa au kutekwa na kufanywa watumwa. Uislamu katika hali isiyo ya utatanishi, uliwakataza wafuasi wake kuwafanya binadamu wenzao watumwa kwa kisingizio chochote kile. Isipokuwa tu kwa yule adui mwabudu sanamu ambaye ametekwa kwenye vita ambayo ilipiganwa ikawa ama ya kujitetea au kwa ruhusa ya Mtume au warithi wake halali. Tofauti hii ilikuwa, kama anavyoieleza Jaji Ameer Ali: “Ili iwe kama dhamana kwa kulinda maisha ya mateka.”2

Kama Allamah Tabatabai alivyokwisha eleza kwa undani na urefu zaidi, kabla ya Uislamu, watu wenye nguvu, na wapendao kutawala wengine kuwa watumwa, walikuwa na desturi ya kuwafanya watumwa binadamu wenzao waliod- haifu bila kusita. Sababu muhimu miongoni mwa sababu nyingi za kuwafanya watu wengine kuwa watumwa ni hizi zifuatazo:

Vita: Mshindi aliweza kufanya chochote anachotaka kwa adui aliye mshinda. Angeweza kuwauwa wapiganaji waliokamatwa mateka, angefanya kuwa watumwa au pengine kuwaweka chini ya mamlaka yake au makucha yake.

Utawala: Mkuu au mtawala angeweza kumtia utumwani, kutegemeana na hiari yake ipendavyo, mtu yeyote aishiye katika himaya yake.

Ulezi: Baba au babu alikuwa na mamlaka yote kwa kizazi chake. Angeweza kumuuza au kumtoa zawadi; angeweza kumwazimisha kwa mtu mwingine, au kubadilishana na mtoto mwingine mvulana au msichana.

Uislamu ulipotokeza, ulibatilisha na kutangulia sababu mbili za mwisho kabisa. Hakuna mtawala au mlezi aliye ruhusiwa kuwafanya raia wake au watoto wake kuwa watumwa wake. kila mtu alipewa haki zake kikamilifu; mtawala na mtawaliwa, mzazi na mtoto walitakiwa kuishi katika mipaka iliyowekwa na dini; hakuna mtu aliye ruhusi- wa kuchupa mipaka hiyo.

Na Uislamu ulikataza kwa ukali sababu ya kwanza, yaani, vita, kwa kuruhusu kuwafanya watumwa wale tu waliotekwa kwenye vita iliyopiganwa dhidi ya adui aliye kafiri. Hapakuwepo na njia nyingine yoyote ambayo mtu angefanywa mtumwa. Wakati huo huo, Uislamu ulinyanyua hadhi ya utumwa na kunfikishia mtumwa hali ya kuwa mtu aliye huru na ukafungua njia nyingi za kuwakomboa watumwa.3

Kabla biashara ya utumwa haijaanza kufanywa katika kiwango kikubwa na watu wa Magharibi (wakati ukoloni ulipoanza), ilikuwa ni katika kupigana vita tu ndipo watu walifanywa mateka. Lakini Uislamu haukuruhusu vita vya uvamizi. Vita vyote vilivyo fanyika wakati wa uhai wa Mtume, vilikuwa vya kujitetea. Si hivyo tu, mbadala ulianzishwa na kuanza kutekelezwa: “Kuwaacha mateka kuwa huru, ama kwa fidia yoyote au bila ya fidia yoyote.” (Qur’ani 47:4) Kwenye vita vilivyolazimishwa kwa Waislamu, Mtume aliamuru mateka walioangukia kwenye mikono ya Waislamu wafanyiwe wema wa kibinadamu.

Wenye uwezo waliruhusiwa kununua uhuru wao kwa kulipa fedha kidogo, na baadhi yao waliachwa huru bila malipo yoyote.

Yote yalitegemea uamuzi wa Mtume au warithi wake halali, kwa kuzingatia usalama wa Waislamu na ukubwa wa hatari kutoka kwa adui. Mateka wa vita ya kwanza ya Kiislamu, yaani vita ya Badr, walipewa uhuru kwa malipo ya fidia (malipo yalikuwa fedha au kazi ya kufundisha watoto kumi wa Kiislamu kusoma na kuandika), ambapo mateka wa kabila la Tay waliachwa huru bila malipo yoyote yale ya fidia. 4

Hata kwenye utumwa wa aina hiyo palikuwepo na sharti lililoambatanishwa kwamba mama asitenganishwe na mwanae, wala ndugu asitenganishwe na ndugu yake wala mume na mkewe wala mtu na ukoo fulani asitenganishwe na watu wa ukoo wake. Mtume na Imamu wa kwanza wa madhehebu ya Shia, Ali bin Abi Talib, walipitisha adhabu zilizokuwa kali sana kwa mtu yeyote yule aliyemfanya mtu huru kuwa mtumwa: adhabu hiyo ilikuwa kukata mkono wa mhalifu. Ameer Ali anaandika katika kitabu chake kiitwacho “Mohammedan Law:

“Kumiliki mtumwa kwa mujibu wa sheria za Qur’ani ilitegemea na sharti la aina ya vita ambayo Waislamu walipigana, iliyo halisi, halali yaani vita ya kujitetea dhidi ya maadui waabudu masanamu; na iliruhusiwa kwa sababu ya kudhamini ulinzi wa maisha ya mateka… Muhammad aliikuta desturi hiyo ipo miongoni mwa Waarabu wapagani; alipunguza ubaya wa uovu huo, na wakati huo huo akaweka sheria kali kwamba isipokuwa kwa ukaidi wa wafuasi wake, utumwa kama anzisho la kijamii ungekoma kuwepo kwa kusitishwa vita ambazo taifa la Kiislamu lilihusika mwanzoni.

Kukata mwili wa mtu vipande vidogo vidogo pia ilikatazwa kwa dhahiri na Muhammad, na taasisi ambayo ilisitawi huko katika falme ya Ajemi na falme ya Byzantine ilipigwa marufuku na iliwekewa masharti makali sana. Biashara ya utumwa haikujulikana wakati wa utawala wa makhalifa wanne wa mwanzo, “makhalifa waongofu,” kama wanavyoitwa na madhehebu ya Sunni. Hakuna ushahidi hata kidogo, wa kuaminika kimaandishi kwamba kuna mtumwa yeyote alimilikiwa kwa kununuliwa wakati wa utawala wa makhalifa hao.

Lakini baada ya ukoo wa Umayya kuchukua utawala wa ukhalifa, mabadiliko yaliingizwa kwenye msimamo wa Uislamu. Muawiyah ndiye aliyekuwa mtawala wa kwanza Mwislamu ambaye aliingiza katika ulimwengu wa Muhammad (wa Kiislamu) mpango wa kuwapata watumwa kwa njia ya kuwanunua. Pia Muawiyah alikuwa khalifa wa kwanza kutumia mila ya Byzantine ya kuwalinda wanawake zake kwa kutumia watu walio hasiwa. Wakati wa utawala wa ukoo wa Abbas, Imamu wa madhehebu ya Shia, Jafar al- Sadiq alihubiri dhidi ya utumwa, na fikira zake zilikubaliwa na Mutazila. Karmath, ambaye alisitawi wakati wa karne ya tisa kwa kalenda ya Kikristo… anaonyesha aliuona utumwa kuwa kinyume cha sheria.5

Hivyo tunaona kwamba bidii ya Uislamu kujaribu kuwazuia wafuasi wake kupatana na kumiliki watumwa ilikwamishwa na Banu Umayyah. Na lazima niweke kwenye kumbukum- bu kuonyesha fedheha inayo endelea na kugusa idadi kubwa ya Waislamu, hawakujali kabisa maagizo ya Mtume na amri za makatazo za Qur’ani, na Waarabu pia walishirikiana na Wakristo wa Ulaya kwenye biashara inayo chukiza mno ya watumwa ya Afrika ya Mashariki. Biashara ya utumwa ya Afrika ya Magharibi, yote ilikuwa katika mikono ya Wakristo wa Ulaya.

Pili, Uislamu ulianzisha kampeni kabambe ya kuwakomboa watumwa. Ukombozi wa watumwa ulitangazwa kuwa fidia ya kulipia dhambi kadhaa. Suala hili linahusiana na sheria za Uislamu lakini, tutaorodhesha chache miongoni mwao ili kuonyesha jinsi gani dhambi ndogo zilisamehewa kwa adhabu ya fidia ya kumwacha mtumwa huru.

Mathalani, kama mtu alishindwa kufunga saumu bila sababu ya maana wakati wa mwezi wa Ramadhani, au kama alishindwa kufunga saumu ya itikafu au kiapo cha nadhiri, na kadhalika, fidia yake ilikuwa kumpa uhuru mtumwa mmoja kila siku aliyokosa kufunga, pamoja na kulipa kwa kufunga saumu baadaye.

Vivyo hivyo, kwa kila kosa la nadhiri, mtumwa mmoja aliachwa huru kama fidia; au kosa la kuchana mtu nguo zake kama kuonyesha huzuni yake mtu kwa kufiwa na mke au mtoto; au kama mwanamke anajipigapiga au kujikata au kuvuta nywele zake kuonyesha huzuni ya kufiwa na yeyote; au kujiua kwa ajali na; wakati mwingine hata kwa sababu ya kumuua Mwislamu kwa kukusudia; au kama mume alimwambia mkewe kwamba alikuwa kwake kama mama yake, na kwa makosa mengine mengi.6

Kutoka kwenye mifano hii, mingine haina uzito lakini ilipenya kwa kina kwenye utamaduni wa Waarabu, mtu anaweza kuona jinsi gani sheria za kidini zilivyofungwa kwa lengo la kuwakomboa watumwa, na hatimaye kukomesha kabisa laana ya utumwa katika jamii.

Inawezekana pia ikahojiwa kwamba kwa kuamrisha ukombozi wa watumwa kama kafara ya dhambi, Uislamu ulikuwa unaruhusu taasisi ya utumwa iendelee kudumu. Hii haikuwa hivyo. Kwa kila namna ya ukombozi wa mtumwa kulikofanywa kama kafara, aina nyingine vile vile ya kafara ilielekezwa badala yake-ikionyeshwa wazi kwamba lengo la Uislamu lilikuwa katika wakati muafaka wa kujenga jamii iliyo huru kutokana na taasisi hii yenye madhara.7

Pia Uisilamu ulitangaza kwamba mwanamke yeyote mtumwa ambaye anazaa mtoto na bwana wake anayemmili- ki, ilikuwa si ruhusa kumuuza, na kama mzazi mwenzake (mmiliki wake) akifa, mwanamke huyo anakuwa huru moja kwa moja.8 Aidha, kinyume na mila zingine zote za huko nyuma, Uislamu uliamuru kwamba mtoto aliyezaliwa na mama mtumwa kutokana na bwana wake anayemmiliki, basi lazima mtoto afuate hadhi ya baba yake.

9Watumwa walipewa haki ya kujikomboa wenyewe ama kwa malipo ya fedha au kufanya kazi kwa mapatano ya kipindi cha makubaliano. Kauli ya makubaliano ya kisheria huitwa mkataba.

Mwenyezi Mungu anasema katika Qur’ani:

الَّذِينَ يَبْتَغُونَ الْكِتَابَ مِمَّا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ فَكَاتِبُوهُمْ إِنْ عَلِمْتُمْ فِيهِمْ خَيْرًا ۖ وَآتُوهُمْ مِنْ مَالِ اللَّهِ الَّذِي آتَاكُمْ ۚ{33}
“Na wanaotaka kuandikiwa wapate uhuru katika wale ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki, basi waandikieni kama mkiona wema kwao. Na wapeni katika mali ya Mwenyezi Mungu aliyo kupeni….” (Quran 24:33)

Neno kitab kwenye maana yake ni makubaliano ya maandishi baina ya mtumwa na mmiliki wake unaojulikana kama “Mukatabah – hati ya mkataba.” Jambo la muhimu kwenye mukatabah ni kwamba pale ambapo mtumwa anataka kufanya makubaliano ya maandishi ya aina hii, bwana wake lazima akubali.10 Kwenye aya iliyonukuliwa hapo juu, Mungu amefanya wajibu kwa Waislamu kuwasaidia watumwa katika kujikomboa.

Mtumwa anapotaka kujikomboa, bwana wa mtumwa si tu kwamba akubali, lakini pia anatakiwa amsaidie mtumwa kiasi fulani kutoka kwenye utajiri wake mwenyewe,11 kiasi tu cha utoaji wa kuridhisha katika hali ambayo mtumwa ataweza kuishi maisha ya kuheshimika baada ya kupewa uhuru wake Hivyo, miaka 1400 iliyopita, Uislamu ulishughulika katika njia ya ufanisi zaidi kuangamiza utumwa. Pia Uisilamu ulielekeza kwamba watumwa waliokuwa wanataka kujikomboa, kuwa uhuru lazima wapewe msaada kutoka hazina ya taifa (baytul mal).12

Hivyo, kama tegemeo la mwisho, Mtume na warithi wake wa haki walitoa fidia ya kuwapa uhuru watumwa kutoka kwenye hazina ya taifa. Qur’ani inatambua ukombozi wa watumwa kama ni njia moja wapo ya ruhusa ya matumizi ya sadaka na misaada. (Angalia (Qur’ani 9: 60, 2:177)

Na inafaa kukumbuka kwamba mtumwa anakuwa uhuru moja kwa moja kama bwana wake akimkata sikio lake au kumpofua jicho lake.13 Pia kama watumwa anayeishi kwenye nchi ya Kiislamu, wakikubali Uislamu mbele ya wamiliki wao, basi, watakuwa huru moja kwa moja.

Kama mtumwa akiwa kipofu au akipata kilema chochote ataachwa huru.14 kwa mujibu wa Imamu Jafar al-Sadiq (amani iwe juu yake.), kama mtumwa ni Mwisilamu na amefanya kazi kwa miaka saba, basi alistahili kupewa uhuru wake.

Kumlazimisha mtumwa huyo kuendelea kufanya kazi hairuhusiwi.15 Ni kwa sababu ya hadithi hii kwamba wanachuoni wa kidini wana maoni kwamba kumpa uhuru mtumwa baada ya kufanya kazi kwa miaka saba ilikuwa ni tendo la wema linalopendekezwa sana.

Kwa nyongeza katika njia hizi za lazima, na za hiyari za kuwakopmboa watumwa, ilitajwa kama muundo safi sana wa sadaka.

Imamu Ali aliwakomboa watumwa elfu moja, aliwanunua kwa fedha yake mwenyewe.16 Imamu wa saba–Musa al-Kazim naye aliwakomboa watumwa elfu moja. Imamu wa nne, Ali bin Al-Husein, alikuwa na tabia ya kumpa uhuru kila mtumwa aliyekuwa chini ya miliki yake kila Sikukuu ya Iddi (adhimisho la kila mwaka la Waislamu.) Ni muhimu kuzingatia kwamba katika matukio yote yaliyotajwa hapo juu, watumwa wote waliopewa uhuru walipatiwa njia za kutosha za kuwawezesha kujipatia riziki katika hali ya kuheshimika.

Uislamu ni ya kwanza na ndio tu dini ambayo iliagiza ukombozi wa watumwa kama jambo jema na likiwa ni sharti la mtu kutambulika kuwa ana imani ya kweli katika kumwamini Mungu. Hakuna dini nyingine zaidi ya Uislamu ambayo ilihubiri na kuamuru kwa njia ipi iliyo bora kabisa kuliko zote ya kuonyesha mapenzi kwa binadamu wenzetu walioko kwenye utumwa. Kwenye sura ya 90 ya Qur’ani, kumwacha mtumwa huru imeagizwa kama msingi mwema na ulio mkuu kabisa wa imani:
لَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنْسَانَ فِي كَبَدٍ {4}
أَيَحْسَبُ أَنْ لَنْ يَقْدِرَ عَلَيْهِ أَحَدٌ {5}
يَقُولُ أَهْلَكْتُ مَالًا لُبَدًا {6}
أَيَحْسَبُ أَنْ لَمْ يَرَهُ أَحَدٌ {7}
أَلَمْ نَجْعَلْ لَهُ عَيْنَيْنِ {8}
وَلِسَانًا وَشَفَتَيْنِ {9}
وَهَدَيْنَاهُ النَّجْدَيْنِ {10}
فَلَا اقْتَحَمَ الْعَقَبَةَ {11}
وَمَا أَدْرَاكَ مَا الْعَقَبَةُ {12}
فَكُّ رَقَبَةٍ {13}
“Hakika tumemuumba mtu katika taabu. ” Je, anahani kwamba hapana yeyote mwenye uwezo juu yake? anasema: Nimeharibu mali nyingi (bure) je, anadhani kwamba hapana yeyote anayemuona? Je, hatukumpa macho mawili? Na ulimi na midomo miwili. Na tuka- muongoza njia mbili Lakini hakupita njia nzito Na nini kitakujulisha njia nzito ni nini! Ni kumwacha huru mtumwa: (Qur’an 90:4-13)

Ni lazima ielezwe kwamba uachaji uhuru mtumwa ni jambo ambalo limependekezwa sana. Uislamu ulidhibiti utumwa kwa njia nzuri, yenye upendo na inayotekelezeka, hivyo kwamba ilifanya kumtunza mtumwa ilikuwa ni wajibu mkubwa sana kwa bwana wake, na wakati huo huo uliamuru kuwajali na kuwatendea wema mkubwa watumwa, hivyo kwamba mara nyingi watumwa walipoachwa huru hawakutaka kuondoka na kutengana na wale walio wamiliki.

Tatu, Uislamu uliwarejeshea watumwa heshima na kunyanyua hadhi zao kijamii. Uislamu haukutofautisha baina ya mtumwa na mtu aliye huru, na wote walitendewa kwa usawa, bila ubaguzi. Ulikuwa ukweli huu kwamba ndiyo siku zote ulivyo wavuta watumwa kwenye Uislamu. Inasikitisha na inaumiza moyo kuona kwamba wale wasioacha makelele yao yasiyo ya haki ya kuukosoa Uisilamu hawataki kuona msimamo huu wa usawa, ambapo hata wakati huu wa kipindi cha kuelimika zipo nchi zenye kutunga sheria zinazobagua umati wa walio wengi, na kuwaweka kwenye hali halisi ya utumwa.

Uislamu hautambui tofauti ya taifa au rangi ya ngozi, nyeusi au nyeupe, raia au wanajeshi, watawala au watawaliwa; wote hawa wapo sawa, si tu kinadharia bali katika hali halisi. Muadhini wa kwanza (mpiga mbiu wa mwito wa Sala) wa Uislamu, mfuasi mtiifu (mpenzi) wa Mtume na sahaba aliyeheshimika sana, alikuwa mtumwa mweusi (Mhabeshi).

Qur’ani inaweka kipimo cha ubora wa mtu kwenye Aya ya 13 Sura ya 49. Maneno haya yameelekezwa kwa binadamu, umati wote wa dunia yote, na yanahubiri undugu asilia wa mwanadamu bila kutofautisha kabila, ukoo, taifa au rangi ya ngozi. Inasema:

يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّا خَلَقْنَاكُمْ مِنْ ذَكَرٍ وَأُنْثَىٰ وَجَعَلْنَاكُمْ شُعُوبًا وَقَبَائِلَ لِتَعَارَفُوا ۚ إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِنْدَ اللَّهِ أَتْقَاكُمْ ۚ إِنَّ اللَّهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ {13}

“Enyi watu! Hakika sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamune na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa mbali mbali na makabila mbali mbali ili mpate kujuana tu. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni yule aliye mchamungu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye habari.” (Qur’an 49:13)

Aya hii inaweka wazi mtazamo wa Uislamu kuhusu maisha ya binadamu hapa duniani. Inaweka kigezo kimoja tu cha ubora au hadhi na hicho ni uchaji Mungu, chenye maana ya utiii na unyenyekevu kamili kwa ayapendayo Mwenyezi Mungu. Aya hii inateketeza na kuangamiza kabisa tofauti zote zilizotengenezwa na binadamu na zilizo za bandia kuhusu taifa na rangi ya ngozi, ambazo tunaziona kila mahali duniani kote hadi sasa. Kuelzea ubora wa uchamungu, ngoja tuangalie Mwenyezi Mungu anavyosema:

لَيْسَ الْبِرَّ أَنْ تُوَلُّوا وُجُوهَكُمْ قِبَلَ الْمَشْرِقِ وَالْمَغْرِبِ وَلَٰكِنَّ الْبِرَّ مَنْ آمَنَ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَالْمَلَائِكَةِ وَالْكِتَابِ وَالنَّبِيِّينَ وَآتَى الْمَالَ عَلَىٰ حُبِّهِ ذَوِي الْقُرْبَىٰ وَالْيَتَامَىٰ وَالْمَسَاكِينَ وَابْنَ السَّبِيلِ وَالسَّائِلِينَ وَفِي الرِّقَابِ وَأَقَامَ الصَّلَاةَ وَآتَى الزَّكَاةَ وَالْمُوفُونَ بِعَهْدِهِمْ إِذَا عَاهَدُوا ۖ وَالصَّابِرِينَ فِي الْبَأْسَاءِ وَالضَّرَّاءِ وَحِينَ الْبَأْسِ ۗ أُولَٰئِكَ الَّذِينَ صَدَقُوا ۖ وَأُولَٰئِكَ هُمُ الْمُتَّقُونَ {177}

“Sio wema kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa Mashariki na magharibi. Bali wema ni wa anayemuami- ni Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii, na anawapa mali kwa kupenda kwake, jamaa na mayatima na masikini na wasafiri, na waombao na katika kuwakomboa watumwa na akawa ana shika Sala, na akatoa Zaka, na wanao timiza ahadi yao wanapo ahidi na wanao vumilia katika shida na dhara na wakati wa vita hawa ndio walio sadikisha, na hao ndio wajilindao.” (Qur’ani 2:177)

Aya hii kwa wazi kabisa inaonyesha kwamba kwa yenyewe, hakuna wema maalum katika kuelekea upande wowote mahususi wakati wa Sala. (Umoja wa Qibla unaonyesha umoja wa imani ambayo hupelekea kwenye umoja wa kiro- ho na kufikia kilele cha ulinganifu wa kimwili.) Imani na ibada iliyoamrishwa katika aya hii ndio wema halisi, na mbali ya kuamriwa na Mungu, zinavutia kwenye fikra za mwanadamu.

Tafadhali zingatia kwamba, “kutoa mali kwa upendo kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ili… wale walioko kwenye utumwa,” ni mojawapo ya wema huo. Katika hadithi ya Imamu Muhammad al-Baqir, inasemekana kwamba mtu anapompiga mtumwa wake (mwanamume au mwanamke), bila ya sababu yoyote ile ya halali, ipo njia moja tu ya fidia ya kosa hilo nayo ni kumpa uhuru hata kama tendo hilo la kupiga lipo katika mipaka iliyowekwa na Mungu.

Katika hadithi nyingine, Zurarah alimuuliza Imamu huyo huyo kuhusu msimamo wa bwana kwa watumwa. Imamu akamjibu kwamba; “kitendo kinachofanywa na watumwa bila kukusudia hakistahili adhabu lakini watumwa wakikataa kumtii bwana wao mfululizo na kwa kukusudia, basi hapo ndipo wanapostahili kuadhibiwa.” Itakuwa ni jambo la kuvutia kwamba, mtumwa alipewa haki ya kumshitaki bwana wake. Hadithi ya tatu kutoka kwa Imamu huyo huyo inasema kwamba mtu mwenye tabia nne zifuatazo atasamehewa dhambi zake na atapandishwa na kuwekwa juu sana katika mazuri ya himaya za Peponi.

(1) Mtu anayempa hifadhi yatima na kumtimizia mahitaji na kumwondolea matatizo yake na anakuwa mwema kwake kama baba yake, anampa mapenzi ya wazazi wake;

(2) mtu aliye mwema na mwenye huruma na anawasaidia wasio na uwezo;

(3) mtu anaye toa matumizi kwa wazazi wake na ni mwenye huruma, mwenye kuwafikiria na kuwaangalia;

(4) na mwisho, mtu ambaye hamkasirikii mtumishi au mtumwa wake na humsaidia kazi ambayo ameamriwa kuifanya na hampi kazi ambazo zipo nje ya uwezo wake kuzifanya.

“Uisilamu umeagiza kwamba bwana amfanyie mtumwa wake kama mmoja wa jamaa ya familia yake, mtumwa lazima apate mahitaji yote ya muhimu katika maisha yake, kama anavyopata mtu mwingine katika familia hiyo. Mtume alikuwa na tabia ya kula pamoja na watumwa na wafanyakazi wake, na kuketi na kuzungumza nao, yeye mwenyewe Mtume hakula chakula kizuri zaidi kuliko wao wala hakuvaa nguo nzuri zaidi kuliko wao, wala hakuwabagua kwa namna yoyote ile.

“Wamiliki wa watumwa walilazimishwa wasiwape shida watumwa wao, ilikuwa si ruhusa kuwatesa, kuwatukana au kutowatendea haki watumwa. Watumwa walipewa fursa ya kuoana wao kwa wao (kwa ruhusa ya wamiliki wao), au na wanamume walio huru au wanawake walio huru. Watumwa waliruhusiwa kutao ushahidi, na kushiriki katika mambo yote pamoja na watu walio huru. Wengi katika wao wali- teuliwa kuwa magavana, makamanda wa jeshi na watawala.

“Mbele ya macho ya Uisilamu, mtumwa mcha Mungu anapewa nafasi ya juu zaidi kuliko mtu aliye huru lakini si mcha Mungu.”17

Imeelezwa kwenye hadithi za kuaminika kutoka kwa Mtume kwamba, bwana ni lazima amlishe mtumwa wake chakula anachokula yeye na amvishe mavazi anayovaa yeye.

Kwenye hotuba yake maarufu aliyo hutubia huko Arafat tarehe 9 Dhul-Hijjah 9 A.H. wakati wa hija yake ya mwisho, Mtume alisema; “…na watumwa wenu, zingatieni kwamba mnawapa chakula mnachokula nyinyi na muwav- ishe nguo ambazo nyinyi mnavaa.

Na kama wakifanya kosa ambalo hungependa kusamehe basi wauzeni, kwani wao ni watumishi wa Mwenyezi Mungu na si vema kuwatesa…” 18

Kusema kwamba Uisilamu uliwatendea watumwa wema kwa mujibu wa msingi wa usawa ni kutokusema ukweli wote.

Kwa sababu, kwa kweli, kwa idadi fulani ya makosa, adhabu inayotolewa kwa mtumwa ilikuwa nusu ya ile iliyotolewa kwa wengine.19 Hii ilikuwa tofauti na jinsi mataifa mengine yalivyo wapa adhabu kali zaidi watumwa kuliko watu wengine.

Profesa Davis anaandika; “Sheria ya makosa ya jinai takriban kila mahali ilikuwa kali zaidi kwa watumwa kuliko watu huru.” 20

Mtume wa Uislamu kila mara aliwasihi wafuasi wake kuwatendea wema watumwa wao kama jamaa wa familia zao. Yeye na familia yake mara kwa mara waliwatendea wema watumishi wao.

Mtumishi mwanamke katika familia ya Fatimah, binti yake Mtume, anasadikisha kwamba, bimkubwa wake (Fatuma) alikuwa na desturi ya kugawana naye kazi zote ngumu za nyumbani na alisisitiza kwamba mtumishi lazima apumzike kila baada ya siku moja ambapo yeye, Fatimah, angefanya kazi zote. Hivyo, palikuwepo na mgawanyo sawa wa kazi baina ya bimkubwa na mfanyakazi wa ndani.

Pia imetaarifiwa kwamba siku moja Ali na mtumishi wake wa kiume Qambar walikwenda dukani ambapo Ali alich- agua nguo mbili, moja ilikuwa nguo ya bei ya chini na hafifu na nyingine nzuri na ghali. Ali alimpa Qambar ile nguo nzuri.

Qambar akashtuka: “Ewe Bwana wangu!” Alisema: “Nguo hii ni nzuri zaidi na wewe ni mtawala wa Waislamu. Chukua wewe nguo hii.”

Ali akajibu, “Hapana, Qambar, wewe ni kijana na vijana sharti wavae nguo nzuri.” Je? kitendo cha namna hii kingemfanya mtumishi ajihisi kuwa yeye ni mtu duni miogoni mwa watumwa? Wamiliki wa watumwa hawakuruhusiwa kuwapa watumwa wao kazi nyingi kuzidi uwezo wao.

Waliagizwa kamwe wasiwaite watumwa wao wanaume na wanawake kwa majina ya kudhalilisha, lakini badala yake walitakiwa wawaite majina yenye huba zaidi kama: “kijana wangu,” au “msichana wangu wa kazi” iliamriwa pia kwamba watumwa wote lazima wavae nguo na wale chakula sawa na wamiliki wao wa kiume na wa kike.

Iliagizwa pia kwamba katika hali yoyote ile mama asitenganishwe na mtoto wake, wala kaka kutenganishwa na kaka yake, wala baba kutenganishwa na mtoto wake, wala mume kutenganishwa na mkewe, wala ndugu kutenganishwa na ndugu yake.

Sasa ngoja turejee kwenye Qur’an:

وَاعْبُدُوا اللَّهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا ۖ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا وَبِذِي الْقُرْبَىٰ وَالْيَتَامَىٰ وَالْمَسَاكِينِ وَالْجَارِ ذِي الْقُرْبَىٰ وَالْجَارِ الْجُنُبِ وَالصَّاحِبِ بِالْجَنْبِ وَابْنِ السَّبِيلِ وَمَا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ ۗ إِنَّ اللَّهَ لَا يُحِبُّ مَنْ كَانَ مُخْتَالًا فَخُورًا {36}

“Na mwabuduni Mwenyezi Mungu wala msimshirikishe na chochote. Na wafanyieni wema wazazi wawili, na jamaa na mayatima na masikini na jirani wa karibu na jirani wa mbali, na rafiki wa ubavuni na mpita njia (msafiri) aliyeharibikiwa, na walio milikiwa na mikono yenu ya kulia. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi mwenye kiburi, ajivunaye.” (Qur’an 4:36)

Mtukufu Mtume alimpa mtumwa Abu Dharr al-Ghifari kama zawadi yake na akamwambia amtunze katika hali iliyo bora kabisa, ampe chakula kile anachokula yeye, amnunulie nguo zozote zile anazozipenda yeye.

Abu Dharr alikuwa na joho ambalo kwa haraka alilikata vipande viwili, na akampa kipande kimoja mtumwa. Mtume akasema: “vizuri sana!” Abu Dharr akamchukua mtumwa huyo hadi nyumbani kwake na akampa uhuru. Mtume akafurahi sana kwa kiten- do cha Abu Dharr na akasema: “Mungu atakulipa kwa hilo.” Jinsi Imamu wa nne, Zaynul Abidin alivyomtendea – msichana wake mtumwa inajulikana sana katika historia ya Kiisilamu. Wakati fulani ilitokea mtumwa huyo msichana alikuwa anamtengea chakula Imamu, kwa bahati mbaya, akaangusha bakuli lenye mchuzi wa moto na ukamwagika juu yake. Mtumwa huyo wa kike alitambua dhara na mau- mivu aliyomsababishia Imamu. Mtumwa huyo alikuwa anajua tabia ya mtukufu Imamu na akaanza kukariri aya ya Qur’an:

“… Na wazuiao ghadhabu.” Imamu akajibu: “Nimejizuia ghadhabu yangu,” Mtumwa akaendelea: “Na wanaosamehe watu;” Imamu akasema: “Nimekusamhe,” Hatimaye, mtumwa huyo msichana akasema: “Na Mwenyezi Mungu anawapenda wafanyao ihsani;” Imamu akajibu: “Nimekuacha huru ili nitafute radhi ya Mungu.”

Mtumwa huyo msichana alinukuu maneno hayo kutoka aya ya 134 Sura ya 3 ya Qur’an. Aya hii inasomeka ifuavyo: “Ambao hutoa katika (hali ya) wasaa na katika (hali ya) dhiki, na wajizuiyao ghadhabu na wanaowasamehe watu (na wawafanyiao ihsani); na Mwenyezi Mungu anawapenda wafanyao ihsani.”

Wakati fulani mtu mmoja alisema kwamba watumwa wa Imamu Zaynul Abidin huambizana wao wakisema kwa wao kwamba walikuwa hawamwogopi bwana wao. Aliposikia habari hii, Imamu alisujudu kwa Mungu kumshukuru na akasema: “Ninamshukuru Mungu kwamba viumbe wake hawaniogopi.” Kutokana na yale ambayo tumeyasema hapo juu lazima ieleweke dhahiri jinsi gani watumwa walivyopendwa na kutendewa wema na Mtukufu Mtume na Maimamu wa Ahlul Bait, na wale waliofuata maamrisho ya Qur’an na mifano iliyowekwa na Mtume na Maimamu.

Kuhusu msimamo wa bwana Mwislamu anaye miliki mtumwa na watumwa wake, Will Durant anasema: “…. Aliwatendea katika hali ya ubinadamu mchangamfu na wa huruma hali iliyowafanya wajione wanafuraha na labda pengine salama zaidi kuliko mfanyakazi wa kiwandani katika kipindi cha karne ya 19 huko Ulaya.” 21

Mwishoni mwa karne ya 18, Mouradgead’ Ohsson (chanzo kikuu cha taarifa cha waandishi wa Magharibi kuhusu ufalme wa Ottoman) alitamka: “Labda pengine hakuna taifa ambalo mateka, watumwa, wavuja jasho katika manchani wana kirimiwa vizuri zaidi au kutendewa wema zaidi ya vile watendewavyo miongoni mwa wafuasi wa Muhammad.” 22

P. L. Rwiere anaandika: “Bwana mwenye kumiliki mtumwa aliamuriwa kumgawia mtumwa wake riziki aliyopewa na Mungu. Lazima itambuliwe kwamba, kwa hili, mafundisho ya Kiisilamu yaliafiki heshima ya namna hiyo kwa utu wa mwanadamu na kuonyesha maana hasa ya usawa ambao ulitafutwa bila kupatikana katika kipindi cha ustaarabu wa kale.”23

Na si katika ustaarabu wa kale tu; hata pia wakati huu wa sasa wa ustaarabu wa Kikristo, imani iliyojengeka ya mam- laka ya juu sana ya kimbari bado ingali inajionyesha kila siku. A.J. Toynbee anasema kwenye kitabu kiitwacho “Civilazation on Trial,” “Kufutika kwa tofauti katika msingi wa kiambari (kitaifa) miongoni mwa Waisilamu ni moja ya mafanikio makubwa kabisa ya Uislamu, na katika dunia ya leo, kama inavyotokea kuna kilio cha haja, kwa ajili kuutangaza na kuueneza wema wa Kiisilamu…”

Halafu anasema kwamba “katika jambo hili la hatari la kuendekeza kujihisi tofauti ya kiambari (kitaifa) hakuwezi hata kidogo kukataliwa kwamba (ushindi wa watu wanaosema Kiingereza) kumekuwa ni balaa.” 24

Napoleon Bonaparte amenukuliwa akisema kuhusu hali ya watumwa kwenye nchi za Kiisilamu: “Mtumwa hurithi mali ya bwana wake na anaweza kumuoa binti yake. Wengi wa watu wa vyeo juu waliwahi kuwa watumwa. Wengi wa Mawaziri Wakuu, wamameluke wote, Ali Ben Mourad Beg, walikuwa watumwa! Walianza maisha yao kwa kufanya kazi za mikono nyumbani kwa wamiliki wao na baadaye walipandishwa katika daraja kwa sifa zao au kwa upendeleo.

Katika nchi za Magharibi, kinyume chake, wakati wote mtumwa wa nyumbani; nafasi yake ni ile ya chini kabisa. Warumi waliwaacha huru watumwa wao, lakini kamwe watumwa walioachwa huru hawakulinganishwa na wazawa. Fikira za watu wa Mashariki na Magharibi zinato fautiana sana hivyo kwamba ilichukuwa kipindi kirefu kuwafanya Wamisri kuelewa kwamba jeshi lote lilijumuisha watumwa walio milikiwa na Sultan al-Kabir.25
________________________
1. Toynbee A.J. Mankind and Mother Earth, (N.Y.: Oxford University Press, 1976), uk. 12.

2. Ameer Ali, Muhammadan Law, j. 2, uk. 31.

3. Al-Tabataba’i Sayyid Muhammad Husein, al-Mizan fi Tafsir'l Qur'an, j. 16, toleo la pili (Beirut, 1390/1971), uk. 338-358.

4. Al-Waqid, Muhammad bin Umar, Kitabul Maghazi, toleo la M. Jones, j. 1. (London: Oxford University Press, 1966), uk. 129; Ibn Sa'd, al-Tabaqatul Kabir, j. 11: 1 (Leiden: E. j. Brill, 1912), uk. 11, 14.

5. Ameer Ali Muhammadan Law, j. 2, uk. 31-2.

6. Al-Khu'i, Sayyid Abu'l Qasim, Minhajus-Salihin, toleo la tatu, j. 11 (Najaf, 1974), uk. 328-331, vile vile tazama Qur'an: 4:92, 5:89 na 58:3.

7. Ibid.

8. al-Amili, Hurr, Wasa'ilu'sh-Shi'ah, j. 16 (Tehran, 1983), uk. 128.

9. Ibid.

10. al-Amili, op. cit., j. 16, uk. 101

11. Ibid.

12. Ibid, uk. 121-2

13. Al-Hilli, Muhaqqiq, Sharaya'ul Islam, (kitabul-'Itqad), vile vile tazama Encyclopaedia of Islam, j. 1. (Leiden: E. J. Brill, 1960), uk. 31.

14. Ibid., uk.31-3

15. Ibid, uk. 43-4.

16. Ibid., uk. 3.

17. at-Tabataba'i, op, cit, j. 338-358.

18. Ibn Sa'd, op, cit, j. 11:1, p. 133; al-Amili, op. cit., j. 16, 21.

19. al-Amili, op. cit., j. 18, uk. 401f. 527-8, 586-7; j. 19, uk. 73, 154f.

20. Davis, D.B., The problem of Slavery in Western Culture (N. Y: 1969), uk. 60.

21. Hurgronje C.,Muhammedanism, (N.Y., 1916), uk. 128, kama ilivy- onukuliwa na W. Durant, the story of Civilization, j. 4. (N.Y., 1960)

22. Kama ilivyonukuliwa katika The Encyclopaedia of Islam, j. 1 uk. 35

23. Riviere P.L., Revue Bleaue (June 1939).

24. Tonbee, A.J., Civilization on Trial (New York, 1948), uk. 205.

25. Cherfils, Banaparte, et l'Islam (Paris, 1914).
Kutoa mfano kuonyesha namna gani Uislamu umenyanyua hali na hadhi ya watumwa na kuwatendea wema kama binadamu badala ya kuwafanya mzigo wa mhayawani (ambavyo ndivyo walivyo fanyiwa kabla ya Uisilamu), hadithi ifuatayo ni yenye mvuto maalum.

Siku moja Mtume aliketi mahali akiwa na Salman, Bilal, Ammar, Shuhayb, Khabbab (wote walikuwa watumwa kabla ya hapo) na kundi la Waisilamu fukara, ambapo watu fulani wasio Waisilamu walipita karibu na hapo.

Walipowaona hawa watu “duni” wapo pamoja na Mtume, walisema, “Umewachagua watu hawa kutoka miongoni mwa watu wako? Unataka sisi tuwafuate wao? Je, Mwenyezi Mungu amewaneemesha wao, hivyo kwamba wao wameamini na sio sisi?

Ni vizuri zaidi utokane nao na usishirikiane nao; ukifanya hivyo, basi labda tunaweza kukufuata wewe.” Mtume hakukubaliana na matakwa yao, na Mwenyezi Mungu akateremsha aya ifuatayo kuhusu suala hili:
وَلَا تَطْرُدِ الَّذِينَ يَدْعُونَ رَبَّهُمْ بِالْغَدَاةِ وَالْعَشِيِّ يُرِيدُونَ وَجْهَهُ ۖ مَا عَلَيْكَ مِنْ حِسَابِهِمْ مِنْ شَيْءٍ وَمَا مِنْ حِسَابِكَ عَلَيْهِمْ مِنْ شَيْءٍ فَتَطْرُدَهُمْ فَتَكُونَ مِنَ الظَّالِمِينَ {52}
وَكَذَٰلِكَ فَتَنَّا بَعْضَهُمْ بِبَعْضٍ لِيَقُولُوا أَهَٰؤُلَاءِ مَنَّ اللَّهُ عَلَيْهِمْ مِنْ بَيْنِنَا ۗ أَلَيْسَ اللَّهُ بِأَعْلَمَ بِالشَّاكِرِينَ {53}
وَإِذَا جَاءَكَ الَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِآيَاتِنَا فَقُلْ سَلَامٌ عَلَيْكُمْ ۖ كَتَبَ رَبُّكُمْ عَلَىٰ نَفْسِهِ الرَّحْمَةَ ۖ أَنَّهُ مَنْ عَمِلَ مِنْكُمْ سُوءًا بِجَهَالَةٍ ثُمَّ تَابَ مِنْ بَعْدِهِ وَأَصْلَحَ فَأَنَّهُ غَفُورٌ رَحِيمٌ {54}
“Wala usiwafukuze wanaomwabudu Mola wao Mlezi asubuhi na jioni kwa kutaka radhi yake. Si juu yako hisabu yao hata kidogo, wala hisabu yako si juu yao hata kidogo, (hata uwafukuze). Ukiwafukuza utakuwa miongoni mwa wenye kudhulumu. Na hivi ndivyo tunavyo wajaribu wao kwa wao, ili waseme: Je, hao ndio Mwenyezi Mungu amewafadhilisha miongoni mwetu? Je, Mwenyezi Mungu hawajui wanao mshukuru? Na wanapokujia wanaoziamini ishara zetu waambie: “Asalamu alaikum! Amani iwe juu yenu! Mola wenu Mlezi amejilazimisha rehema…” (Qur’an 6:52 –54)

Salman, Bilal, Ammar na masahaba wao wanasema:

“Wakati Mwenyezi Mungu alipo teremsha aya hizi, Mtume alituelekea sisi, akatuita twende karibu zaidi naye, na akasema; ‘Mola wenu amejiamrishia rehema juu Yake.’ Halafu tulikuwa na kawaida ya kukaa pamoja naye, na alipotaka kusimama (na kuondoka hapo) alifanya hivyo. Halafu Mwenyezi Mungu akateremsha aya:

وَاصْبِرْ نَفْسَكَ مَعَ الَّذِينَ يَدْعُونَ رَبَّهُمْ بِالْغَدَاةِ وَالْعَشِيِّ يُرِيدُونَ وَجْهَهُ ۖ وَلَا تَعْدُ عَيْنَاكَ{28}

“Na isubirishe nafsi yako pamoja na wanao muomba Mola wao Mlezi asubuhi na jioni hali ya kuwa wanataka radhi Yake. Wala macho yako yasiwaruke…” (Qur’an 18:28)

“Ulipoteremshwa ufunuo kama huu, Mtume alikuwa na mazoea ya kututaka tuketi karibu naye sana hivyo kwamba mapaja yetu yalikaribia sana kuguuza mapaja yake; na hakusimama kabla yetu. Tulipo hisi muda wake wa kusimama umefika, tulimuomba ruhusa yake kuondoka; na hala- fu alisimama baada ya sisi kwisha kuondoka. Na alikuwa na desturi ya kutuambia; Nina mshukuru Mungu ambaye hakuniondoa hapa duniani mpaka Aliponiamuru kuwa na subira na kikundi cha ummah wangu. Nitakuwa na nyinyi katika maisha yangu, na, baada ya kufariki, nitaendelea kuwa na nyinyi.”1

Ninaorodhesha kwa ufupi majina ya baadhi ya watumwa ambao daraja lao la kiroho limenyanyuliwa juu sana katika Uisilamu na katika jamii ya Kiisilamu, tangu hapo Uisilamu ulipoanza kuwepo:
1. Salman, Muajemi:
Wa kwanza na wa mbele kabisa ni Salman al Farsi (Muajemi). Alikuwa mtoto wa mchungaji wa dini ya Zoroasta katika jimbo la Fars. Tokea mwanzo kabisa, alikuwa na shauku ya kuwa mfuasi wa dini isiyokuwa na nyongeza au pungufu zilizofanywa na binadamu.

Hali hii alikuwa nayo siku nyingi hata kabla ya ujio wa Uislamu.

Akabadili dini ya uzoroasta akaingia kwenye Ukristo, na akawa mtumishi wa mchungaji maarufu mmoja baada ya mwingine akiwa katika harakati ya uchunguzi wa elimu ya kidini. Baada ya kupata matatizo na shida kwa muda mrefu alijihusisha na mtawa mmoja huko Antiokia, ambaye wakati wa kufa kwake, alimpa ushauri kwamba muda muafaka ulikwisha fika wa kuja kwa Mtume wa mwisho hapa duniani. Akamwambia afanye safari ya kwenda Hijaz, jimbo la Arabuni ambalo ndani yake mna miji ya Makka na Madina. Alipokuwa njiani anaelekea huko, alikamatwa na kuwa mateka na kikundi cha wapiganaji, na akauzwa kutoka bwana mmoja hadi mwingine, hadi akafikisha wamiliki kumi. Hatimaye, alinunuliwa na mwanamke wa Kiyahudi huko Madina. Si rahisi kutoa maelezo ya kina kuhusu mate- so aliyofanyiwa wakati akiwa mateka kwa kipindi kirefu.

Hata hivyo ilionyesha kwamba hatima yake hiyo ilikuwa inamsogeza karibu na lengo lake, kwa sababu ilikuwa kati- ka mji wa Madina alikutana na Mtukufu Mtume wa Uisilamu. Baada ya majaribu magumu Salman alidhihirikiwa ndani ya nafsi yake na “Mtume” yule ambaye alikuwa anangojewa kwa muda mrefu kama ilivyotabiriwa katika Agano Jipya, (Yohana 1: 19-25) akakubali kuwa Mwisilamu.2 Mtukufu Mtume wa Uisilamu akamnunua kutoka kwa bimkubwa wake wa Kiyahudi na akamwacha huru. Ilikuwa ni baada ya vita ya Badr, vita ya kwanza ya Uisilamu, na kabla ya vita ya Uhud.3

Imani, ujuzi na uchaji Mungu wa Salman na mafanikio yake yasiyo na mfano wa kulinganisha, ilimuweka juu ya masahaba wengine wote wa Mtukufu Mtume. Yeye ni mmo- jawapo wa nguzo nne za Waisilamu wa kw