Rafed English
site.site_name : Rafed English

Ukweli Wa Shia Ithna Ashariyyah by : Dr. ‘Asad Wahid Al-Qaasim

 

Mtungaji ni mtafiti katika misingi ya ukweli, mwenye kujitahidi jitihada kubwa kabisa katika njia ya kuufikia, hadi Allah (s.w.t.) akamwongoa katika njia ya sawa, “Na wale ambao wamejitahidi katika njia yetu. tutawaongoa katika njia zetu.”

Amezaliwa katika kijiji cha Dairul-Ghusun katika ukingo wa Magharibi, katika nchi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Amehitimu masomo yake ya Sekondari, kisha akaenda Jordan Na akapata Diploma ya Uhandisi, kisha akaenda Ufilipino na akapata Shahada ya kwanza ya Uhandisi kisha akapata Shahada ya pili katika Idara ya ujenzi. Na hivi sasa amepata shahada ya Udaktari katika Idara ya utawala wa serikali baada ya kumaliza utafiti wake (wa “Islamic public Administration” “Mfumo wa utawala wa Kiislam”).

Kitabu kilichoko mikononi mwako, ni tarjuma ya kitabu cha Kiarabu, kwa jina la: Haqiqat Shi’a Ithna-Asahariyyah kilichoandikwa na, Dr. ‘Asad Wahid Al-Qaasim.

Kitabu hiki ni utafiti wa kina uliofanywa na mwanachuoni huyu mahiri, kuhusu mitafaruku iliyotokea katika Uislamu na baina ya Waislamu, kuanzia wakati wa Mtukufu Mtume (saww), na mara tu baada ya kufariki kwake hadi sasa. Katika utafiti wake huu, ameiangalia sana historia ya Kiislamu kama ilivyohifadhiwa katika vitabu vya historia vilivyo andikwa na wanachuoni wa Kiislamu wa kuaminika wa madhehebu zote za Kiislamu zijulikanazo. Katika kujadili masuala mbali mbali yenye utata, huwa ametumia dalili, hoja, akili na elimu.

Pia katika jitihada yake hii, amejaribu kuelezea kwa urahisi kabisa njia za kupunguza (kama si kuondoa kabisa) misuguano iliyopo baina ya Waislamu na baina ya madhehebu.

Tumekiona kitabu hiki ni chenye manufaa sana, hususan wakati huu wa maendeleo makubwa ya elimu katika nyanja zote, ambapo watu hawakubali kitu mpaka kwa hoja na dalili za wazi. Kutokana na ukweli huo, Taasisi yetu ya ‘Al-Itrah Foundation’ imeona ikitoe kitabu hiki kwa luhga ya Kiswahili, kwa madhumuni yake yale yale ya kuwahudumia Waislamu, hususan wazungumzaji wa Kiswahili.

Tunamshukuru ndugu yetu, Sheikh Abdul Karim J. Nkusui kwa kukubali jukumu hili la kukifanyia tarjuma kitabu hiki. Vile vile tunawashukuru wale wote walioshiriki kwa njia moja au nyingine hadi kufanikisha kuchapishwa kwa kitabu hiki.

Ni matumaini yetu kwamba kitabu hiki kitakuwa ni mwanga kwa wasomaji wetu na kuzidisha upeo wao wa elimu katika dini.

Mchapishaji:

Al-Itrah Foundation
S. L. P. 1017
Dar-es-Salaam.

Mtunzi wa kitabu hiki Haqiqat Shi’a Ithna-’Ashariyyah amejitahidi sana kutoa ushahidi wa hoja zake katika Kitabu cha Sahih Al-Bukhari na hiyo ni kutokana na uzito na umuhimu wa Kitabu hicho ambacho kinazingatiwa na ndugu zetu Ahl as-Sunnah wal Jama’a kuwa ni Kitabu Sahih zaidi baada ya Kitabu cha Allah (s.w.t.).

Na yaonyesha kuwa Mtunzi amenukuu ushahidi wake kutoka Sahih Al-Bukhari (Arabic- English) cha Dr. Muhammad Muhsin Khan-chapa ya Dar al-Arabia Beirut.

Ama kuhusu Sahih zingine kama vile Sahih Muslim na nyinginezo, Mtunzi ametaja ni mlango na maudhui gani amenukuu ushahidi wake jambo ambalo halitamwia vigumu msomaji kufuatilia pindi atakapopenda kufanya hivyo.

Ni matumaini yetu kuwa - wasomaji wetu watavutiwa na mtiririko wa Kitabu hiki; pili, watakuwa ni wadadisi, waadilifu na wapambanuao haki na batili. Hivyo hawatakanusha au kukubali jambo bila ya ushahidi wowote.

Tunamwomba Allah (s.w.t.) atuonyeshe njia ya haki na atujaalie kuifuata na atuonyeshe njia ya mfarakano na atujaalie kuiepuka.

Wabillaahi Taufiq.
Abdul Karim J. Nkusui
27/11/2001

Natoa Zawadi Ya Kitabu Hiki

Ulimwengu wa Kiislamu siku hizi unashuhudia majaribio mengi ya kuchochea fitina na kuleta mparaganyiko baina ya Madhehebu ya Kiislamu na kuyachongea baadhi yake kwa mengine, na unashuhudia mashambulizi makali yanayo elekezwa kwa Shi’a Al-Imamiah Al-Ithna- ’Ashariyah kwa kuitukana itikadi yao ya Kiislamu na kuishambulia bila ya adabu au huruma.

Na ulimwengu wa Ki-Islamu umegharikishwa kwa mamilioni ya nakala za vitabu ambavyo vinatukana itikadi ya madhehebu hii. Na ambacho hakifichikani kwa yeyote ni kwamba vingi kati ya vitabu hivyo vinatungwa kwa msukumo unaotoka kwa Mawahhabi, na misaada kutoka kwao inaendelea kwa madai ya kutetea Ahl as-Sunnah wal- Jama’a.

Na majarabio yao haya si kingine isipokuwa ni kutaka kutimiza malengo ya wakubwa wao ambao wanaenda mbio kuwagonganisha Waislam wao kwa wao, na wanashutumu dhehebu la Shi’a kwa ukafiri, ushirikina, umajusi, kuritadi na tuhuma za mazushi mengine.

Na haikuwa kuandika kwetu maudhui haya isipokuwa ni kuuzindua ‘Ummah kuhusu ukweli wa dhehebu hili linalo singiziwa, ambalo mizizi ya itikadi yake na fikira zake ni kutoka ndani ya Kitabu Kitukufu na Sunnah Tukufu za Nabii, na utaona katika kurasa za utafiti huu, hoja na dalili zinazounga mkono hayo kutoka katika Qur’an Tukufu na vitabu Sahih vya Hadith kutoka kwa Ahl as-Sunnah, na hasa kitabu cha Al- Bukhari ambacho wanakizingatia kuwa ni kitabu Sahih baada ya Kitabu cha Allah (s.w.t.).

Na Mwandishi wa maudhui haya ni mmoja tu miongoni mwa wengi walioona haki na wakaifuata baada ya kuwa amekumbwa na fitina, lakini akakataa kujiingiza humo isipokuwa baada ya utafiti na uchunguzi kama alivyoamrisha Allah (s.w.t.):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنْ جَاءَكُمْ فَاسِقٌ بِنَبَإٍ فَتَبَيَّنُوا أَنْ تُصِيبُوا قَوْمًا بِجَهَالَةٍ فَتُصْبِحُوا عَلَىٰ مَا فَعَلْتُمْ نَادِمِينَ {6}

Enyi mlioamini kama Fasiq akikujieni na habari: (yeyote ile, msikubali tu) bali pelelezeni (kwanza) msije mkawadhuru watu kwa ujahili na mkawa wenye kujuta juu ya yale mlio yatenda. (49:6)

Mwanzo ulikuwa ni pale nilipopata vitabu vya Ihsan Ilahi Dhahiri, Musa Al-Musawi na wengineo katika Waandishi ambao wanadai kuwa Shi’a ni makafiri na wala hawaamini Sunnah za Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) na kwamba wana Qur’an nyingine na wananasibisha kwenye misingi isiokuwa ya Ki-Islamu kabisa. Mwanzo sikuwa natilia maanani kauli zote hizo, na hiyo ni kwa sababu ya elimu yangu ya mwanzo kwa misingi ya vitabu hivyo vyenye sumu na ambavyo havina malengo isipokuwa kuchochea fitina na mparaganyiko, tukiachilia mbali kutia chumvi mno na kukuza mambo kupita kiasi.

Haikuwa rahisi kuviamini, hasa kwa kuwa sikuwa na shaka kabla ya hapo ya kwamba Shi’a ni Waislamu kama wengine miongoni mwa Ahl as-Sunnah, na hiyo ni pamoja na kuwa na elimu ya kuwepo baadhi ya hitilafu ambazo haziafikiani na fujo hilo la kutia shaka na kukufurishana.

Lakini kutokuwa kwangu na elimu ya uhakika wa itikadi ya Kishia kwa undani, na kutosheka kwangu kwa mwanzo, hakukuwa kunastahimili mbele ya mawimbi makubwa ya kuwa na shaka. Mawimbi ambayo yalikuwa yanaletwa na watu ambao wametumbukia na kuwa mateka wa baadhi ya vitabu vyenye sumu, baada ya kuamini kila kilichopo humo bila ya kudadisi wala kujaribu kujua rai ya Shi’a katika hilo kama kwamba watunzi wa vitabu hivyo ni ma’asum (wasio na madhambi), ambao haijuzu kufikiri juu ya kauli zao au kuzijadili au kuhakikisha upeo wa usahihi wake.

Na kwa masikitiko makubwa miongoni mwa hawa mateka kuna mwenye nia nzuri, na kwa mashambulizi yake dhidi ya Shi’a hataki chochote isipokuwa kutetea itikadi Sahih ya ki-Islamu kama anavyoona yeye.

Lakini Ta’assub ya upofu wenye kuchukiza na ujahili ni udhuru ambao haukubaliki baada ya kutimia njia za utafiti na uchunguzi. Mu’umin ni mwerevu na wala haamini kila kinachosikiwa na kusemwa, kwani kuna wapiga debe wa masultan na maulamaa waovu, jambo ambalo linatulazimu kuchukua kinga na tahadhari katika anga lenye kufunikwa na mawingu ya fitina na kugubikwa na giza lake.

Na mbele ya nyenzo hizi nilikuta nafsi yangu inasukumwa kwenye utafiti na uchunguzi ili kujua ukweli wa hawa Mashi’a, na nimetazama maoni ya pande mbili, na hoja zao kimaudhui na akili timamu. niliepusha nafsi yangu kutokana na Ta’assub ya kimadhehebu ya upofu ambayo haisaidii chochote katika haki, hasa katika utafiti wa masuala ya hitilafu baina ya Shi’a na Sunni unazingatiwa kwamba ni utafiti ambao uko katika duru la Uislamu kwa dalili zitokazo katika Qur’an Tukufu na Hadith tukufu za Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.)

Hapa naleta mukhtasari wa utafiti wangu kwa msomaji mtukufu, ambaye namuomba afikirie katika yale anayoyasoma, kwa hakika katika utafiti huu tumetegemea sana Hadith kutoka katika vitabu Sahih vya Ahl as-Sunnah na hasa Sahih Bukhari ambayo wameizingatia kuwa Hadith zake ni sahih haziguswi na shaka wala haiwezekani kuwatuhumu wapokezi wake 1mpaka ikawa daraja ya Sahih Bukhari kwao inafuatia Kitabu cha Allah (s.w.t.). Na katika uchunguzi huu tutaeleza nukta muhimu za Ikhtilafu baina ya Sunni na Shi’a, mfano; Uimamu, msimamo wa Mashi’a kwa Masahaba, Qur’an na Sunnah tukufu za Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) tukiongezea baadhi ya maudhui ambayo ni mashuhuri kwa Mashi’a kama vile ndoa ya Muta’ (ndoa ya muda maalum) na Taqiyah …. Kwa dalili na hoja kutoka katika Kitabu Kitukufu cha Allah (s.w.t.) na Hadith sahih kutoka kwa Ahl as-Sunnah. Na hapa tunaashiria misingi tulioitegemea katika utafiti wetu na tunaitakidi kuwa ni salama zaidi katika kufikia ukweli.

Nayo ni kwamba, tumezingatia kwamba mwongozo wetu katika kutoa dalili uwe ni katika yale yote yanayoafikiana na mafuhumu ya Kitabu Kitukufu, na ambao utangulizi wake ni salama kwa sababu tunaweza kuitakidi dalili zinazoonekana kuwa ni Sahih lakini bila ya kuangalia utangulizi wake kiakili ambao huenda haukuafikiana na kinachotolewa ushahidi, na hili ni jambo ambalo limewatumbukiza wengi kwenye dimbwi la kuchanganyikiwa katika kujua ukweli na kuwapeleka mbali na ukweli.

Anayeamini tangu mwanzo kwamba Masahaba wote ni katika wale ambao hawaguswi na masharti ya kukosolewa na kurekebishwa, anaweza kukubali baadhi ya uwongo kuwa ni kweli, kwa matokeo ya nyendo za baadhi ya Masahaba ambao hawaendi sambamba na ubainifu wa Kitab na Hadith tukufu. Kisha hakuna budi tueleze baadhi ya nukta za makala ya daktari Muhammad Ar-Ramihi chini ya maudhui yenye anuani:

“Je, tunahitaji kujifunza namna ya kufikiria?” kutokana na faida inayopatikana humo, tumeonelea katika kumfumbua macho msomaji mtukufu kwa misingi ya fikira Sahih ya kielimu, na misingi yake huenda itamsaidia katika kusoma kwake utafiti huu katika upande mmoja bila ya mwingine.

Hii ni pamoja na kuongezea kwamba ushahidi wa Shi’a kwa Hadith zinazotoka katika vitabu Sahih vya Ahl as-Sunnah haimaanishi kwa hali yeyote ile kuamini kwao usahihi wa yote yaliopokelewa humo bali ni kwa kusimamisha hoja na dalili kwa wanao wapinga kwa yale yaliokuja kwa njia yao na kuwalazimisha kwa yale walio jilazimisha nafsi zao na huu ndiyo usawa na uadilifu halisi kwa watu wa mantiki na uadilifu.

Na kuhusu manhaji (njia) sahihi ya kufikiria au utafiti sahihi wa kielimu tumeonelea kwamba tuelezee baadhi ya nukta za makala ya daktari Muhammad Al-Ramihi Mhariri wa Jarida la Kiarabu la Kuwait:

Je, Tunahitaji Kujifunza Namna Ya Kufikiri?

“Moja ya mambo ambayo yamekuwa ni muhimu katika akili ya Mwarabu (binadamu) wa leo ni jambo la fikra sahihi au kufikiria kielimu - tukitaka ukweli halisi - nalo ni jambo ambalo lipo katika mifumo yetu ya malezi na katika jamii zetu kwa upana zaidi, na bila ya kuwepo mapito mema kwa mkabala wa kufahamu jambo hili tutabaki tunasikia, kusoma na kusema mambo ambayo Allah (s.w.t.) hakuyateremshia dalili, yanayoonekana mazuri kwa mandhari yake, lakini yana kila madhara kwa jamii yetu ya Kiarabu (Kiislamu) kwa sasa na kwa wakati ujao, na hatua za awali za fikra sahihi ni kutojisalimisha kwa kila kinachosemwa na kuandikwa na kukichukua kijuujuu, ikiwa hakina tegemeo la dhahiri la kiakili.

Mwanadamu ni kiumbe hai anapatwa na mambo, anapatia na kukosea, na sio lazima kila anachokisema ndiyo mwisho na kikomo kama ile kauli isemayo “kauli ya zamani tu ndio Sahihi kwa sababu waliotangulia wamekwishaisema,” haimanishi kikomo cha usahihi wake.

Rai ya zamani kuhusu jambo miongoni mwa mambo imekwisha semwa na kizazi kilichoishi katika wakati ambao binadamu walikuwa bado hawajapata maarifa waliyo nayo hivi sasa, na kwa kiasi vizazi vinavyokuja vitapata maarifa makubwa na mapana zaidi kuliko tuliyo nayo leo, kwa sababu elimu na maarifa ni kitu kipana na sio mazoea yanayobadilika kila siku kulingana na matamanio ya baadhi yetu au kutokana na ufinyo wa fahamu zao.

Hakika ubaya ambao unaenea baina yetu kwa wingi unatutishia kubaki mateka wa kutokuwa na maendeleo hali ya kuwa tunaghariki katika vita bila ya lengo, tunapigana na kuzozana kwa matamanio na kujisababishia matatizo ya kipuuzi, na tunazozana baina ya hitilafu bila ya kufikiria fikra ya kielimu ambayo ndiyo alama ya leo na ni kigezo cha kubaki hai” 2

Dhana Nzuri Ya Moja Kwa Moja Kwa Maulamaa Walio Tangulia Mara Nyingine Inamwongoza Mtafiti Kwenye Upotovu

Na ushahidi ni kwamba, fikra potofu zimekuwa nyingi baina yetu. Ametoa Fatwa hata yule ambaye usahihi hana hata chembe ya kuweza kutoa Fatwa katika siasa, dini, utamaduni na uchumi, na tukashangilia (kuwa ni wenye kujitahidi). Upeo wa elimu yao ni ton lililodondoka kutoka kwenye maandishi ya waliotangulia, na waliokuja baada yao au kuyasoma katika zama na nyakati zinazo tofautiana sana na zama zetu na hali zetu, wao katika hali zote - ni wenye kujitahidi au kunukuu - hawafikirii kwa yale yalioandikwa au kusemwa katika wanayo yatolea Fatwa katika mambo ya dunia na dini.

Hakika ni kwa ajili ya kupenda kutoa fatwa bila ya elimu katika mambo kumewafanya watu wawe na wasiwasi katika mambo yao ya msingi, mambo ya dini na dunia yao. Ni kweli elimu mpya za kijamii zinatuambia: “Hakuna kisomo kisicho fungamana na dalili, kwani wewe unaposoma dalili unasoma kwa maarifa yako ya kielimu, kisiasa, kiutamaduni … lakini ni kweli vile vile kuna dalili ambazo kuna uwezekano wa kuwepo Ikhtilaf (tofauti) ndogo ndogo na kuna dalili zinazo gongana na akili kwa mara ya kwanza.

Na kabla hatujaingia katika maudhui ya Kitabu hiki ambacho msomaji atapata humo ukweli wenye kuathiri na hoja zenye nguvu, ni vema tuelezee baadhi ya kauli chache za maulamaa wa Ahl as-Sunnah ambazo zinathibitisha na kukiri Uislamu wa Mashi’a na ambazo bila shaka zinaweka wazi uongo wa kauli za wale ambao wanawakufurisha, na wana watuhumu kwa mengi yasiokuwa hayo na ambayo hawanayo.

Imam Shahid Hassan Al-Banna alikuwa ni mmoja wa wajumbe wa kamati ya kuleta uelewano kati ya pande mbili za Sunni na Shi’a. Na ustadh Saalim Al-Bahnasaawi anasema juu yake “Tangu ilipoanzishwa ‘Jamaatut-taqribi’ baina ya Madhehebu ya Kiislamu na ambayo Imam Hassan Al-Banna alitoa mchango wake na Al-Qummi, ushirikiano unaendelea baina ya Ikhwanul-Muslimin na Shi’a”.3

Na huyu Al-’Allamah Al-Sheikh Muhammad Al-Ghazaali anasema: “… hakika pande mbili zinasimamisha uhusiano wao kwa Uislamu kwa kuamini Kitabu cha Allah (s.w.t.) na Sunnah za Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) na wanaafikiana maafikiano ya moja kwa moja juu ya misingi ya jumla katika dini hii,4 vile vile anasema: “Hakika kila kilichobaki katika wakati wetu huu miongoni mwa Ikhtilaf ni fitina iliyozuliwa baina ya Sunni na Shi’a! Nayo ni fitina inayoenezwa na ukoloni na kwa uchache wanataka kuibakisha ili iwe ni utambi daima baina yao kisha watekeleze malengo yao kupitia utambi huo.5

Na ustadhi Anwar Al-Jundi anasema: “Ukweli ni kwamba tofauti kati ya Sunni na Shi’a haizidi tofauti zilizopo tofauti baina ya madhehebu manne”6

Na anasema Sheikh Hassan Ayyub katika maneno yake ya kusifu Shi’a al-Imamiah Al-Ithna-’Ashariyah: “Huenda kundi la Imamia kwa ujumla liko mbali sana na ghuluu (kusifu kupita kiasi) na lililo kubaliana na akili katika dini yake, na ni katika makundi ya Kishi’a yaliyo karibu sana na Ahl as-Sunnah …”, dhehebu lao ni ya Tawhid halisi katika sifa za Allah (s.w.t.) na kumtakasa Muumba kutokana na kufanana na viumbe …7

Sheikh wa Al-Azhar Muhammad Shaltut anatoa Fatwa ya kujuzu kufanya ‘ibada kulingana na madhehebu ya Shi’a Ithna- ‘Ashariyah. Na anayetaka ziada ya kauli za maulamaa wa Ahl as-Sunnah ambazo zinashuhudia Uislamu na itikadi ya Kishi’a basi arejee Kitabu cha As- sunnatu wa Shi’a dhajatu muftailah au Kitabu cha Araul-Ulamaai l- Muslimina Fi Shiati wa Thawrahtil-Islamiyah vya Dr. Izzudin Ibrahim.

Ikiwa Maulamaa watukufu mfano wa Al-Banna, Kishki, Al-Maududi, Anwar Al-Jundi Al-Ghazaali na Hawway, Hassan Ayyub, Fatihi Yakun, Atilimisani, Abu Zahra, Shaltut na wengineo wengi ambao nafasi haitoshi kuwataja - wanaona kuwa Shi’a ni Waislamu wenye kumpwekesha Allah (s.w.t.), je, ni mantiki na akili kuacha kauli zao na kuchukuliwa kauli za Dhahiriy, Al-Khatib Al-Jazairi, Al-Gharib, na wengineo miongoni mwa waandishi wanaowakufurisha Shi’a na ambao hawakumsikia yeyote isipokuwa kupitia katika vile vitabu vyao vyenye sumu?

Wako wapi wao kati ya Maulamaa wajuzi ambao wametoa Fatwa juu ya Uislamu mzuri wa Shi’a?

Na ni nani Musa Al-Musawi ambaye baadhi wanakitolea ushahidi Kitabu chake dhaifu, na kukizingatia kuwa ni msingi wa hukumu yao juu ya Shi’a isipokuwa ni kati ya watu waovu waajiriwa (mamluki) aliye tayarishwa na maadui wa Uislamu baada ya kufaulu mapinduzi ya Kiislamu ili kufanya mambo maovu wakamvalisha kilemba cha Maulamaa wa Kishi’a ili atukane itikadi yao kwa jina la Ushi’a baada ya kujazwa mifuko yake kwa kile kitakacho fikisha paji lake motoni siku ambayo haitofaa mali wala watoto isipokuwa yule atakayemwendea Allah (s.w.t.) kwa moyo safi, na watajua wale ambao wamedhulumu ni mwisho gani wataishilia.
________________________
1. Rejea Jarida la Al Mujtamaul Kuwaitiyyah No:920 la juni 13/1989 ambapo utaona jinsi ulivyokuwa ukali wa kumjibu sheikh Muhammad Al Ghazali naye ni katika maulamaa wakubwa wa Ahl as- Sunnah kwa sababu ya kutia shaka baadhi ya ushahidi wa Hadith zilizopo katika Sahih Bukhari, pia rejea ukurasa wa kitabu hiki utaona riwAyah za kisa cha Malaika wa mauti pamoja na Mtume Musa (a.s.) ambazo sheikh huyu alizitilia shaka.

2. Jarida la Kiarabu No 372 la Novemba 1989.

3. Kitabu cha As-Sunnatul- muftaraa alayha uk. 57.

4. Kitabu cha Kaifa nafhamul Islam uk. 144 -145.

5. Kitabu cha Difaun ‘anil- ‘aqidati wa-sh-Shariah.

6. Kitabu cha Al-Islamu waharakatu-t-taarikh Uk. 421.

7. Kitabu cha Tabsitul-aqaidi-l-Islamiyyah uk. 429 na uk. 430 kilichochapishwa 1980.

Tunaeleza katika mwanzo wa utafiti huu nini makusudio ya neno Shi’ah, vipi limeanza, na kuenea kwa Ushi’a . Tunakuta katika kamusi za lugha kuwa neno Shi’a lina maana ya “Kufuata na wafuasi, na aghlabu limetumika jina hili kwa wafuasi wa Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) na watoto wake mpaka likawa ni maalum kwao”.

Na wa mwanzo aliepanda mbegu ya Ushi’a katika Uislamu ni Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) naye ni wa kwanza kutamka jina la Shi’a kwa wafuasi wa Ahlul Bayt (a.s.) kama alivyopokea hayo As-Suyuti katika tafsiri yake Durrul-Manthur katika Ayah tukufu (Hao ni viumbe bora). Amesema: Amepokea Ibn Asakir katika Sanad yake kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillah amesema: Tulikuwa kwa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) na akaingia Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) basi akasema Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.): “Naapa kwa ambaye nafsi yangu iko mkononi mwake, hakika huyu na wafuasi wake wao ni wenye kufaulu siku ya Qiyamah na kwake imeteremka! “Hakika walioamini na kufanya vitendo vyema hao ndiyo viumbe bora.”1

Hivyo Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) alilingania Manhaj (njia) hii na akawafanyia Ahlul-Bayt (a.s.) wapenzi na wafuasi. Na utapata juu ya hayo katika sehemu ya kwanza ya utafiti huu, dalili zinazothibitisha wosia wa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.)kwa Ahlul-Bayt (a.s.) wake kwa Uimamu katika ‘Ummah huu baada yake, kuanzia kwa Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) na kuishia kwa Al Imam Muhammad Mahdi Sahibu-z- Zamaan (a.s.) ambaye atadhihiri mwisho wa zama ili kujaza dunia kwa haki na uadilifu kama ilivyojaa dhuluma na ujeuri.

Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) alipoaga dunia, kundi katika Masahaba, walionelea ukhalifa usiende kwa Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.), na Imam (a.s.) alikwishasema kwa kupinga kwake juu ya hilo kwa kukataa kwake kumbai Abubakr kwa kipindi cha miezi sita kama alivyopokea hayo Bukhari katika Sahih yake ambayo maelezo yake yatakuja katika sehemu ya kwanza kwa idhini ya Allah (s.w.t.). Na walikataa kumbai pamoja naye kundi la Masahaba wakubwa, mfano wa Zuber, ‘Ammar, Salman, Abudhar na wengineo.

Kisha Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) alipoona kukataa kwake kunasababisha mbomoko usiotengenezeka katika Uislamu, na sote tunajua kuwa Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) hakuwa akitaka Ukhalifa wala hakutaka kutawala wala kupupia Ufalme na kushinda - alikubali na akayafumbia macho yale anayo yaona kuwa ni haki yake kwa kuunusuru Uislamu kutokana na kubomoka na kuparaganyika. Wafuasi wake walibaki chini ya uongozi wake, na Ushi’a haukuwa na nafasi ya kudhihiri katika zama za Makhalifa wa kwanza, kwa sababu Uislamu ulikuwa unapita katika manhaj yake iliyo sawa sawa. Na alipopewa Bai’a Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.), Mu’awiyah bin Abi Sufian alikataa kumbai na akampiga vita katika sehemu ya Siffin, na alimtangulia kwa hilo ‘Aisha bint Abubakr as- Siddiq.

Alitoka akiongoza jeshi linalompiga vita Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) katika vita vinavyojulikana kama vita vya Jamal. Masahaba wengi walijiunga pamoja na Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) katika vita vya Siffin hadi wengi wao wakauliwa chini ya uongozi wake, kama vile ‘Ammar bin Yaasir, Khuzaimatu Dhi Shahadatain, Abu Ayyubil-Ansari na wengineo.

Na baada ya mambo kumnyookea Mu’awiyah bin Abi Sufian na kumalizika kwa duru ya Makhalifa, Mu’awiyah bin Abi Sufian alifuata sera ya madikteta, akawakandamiza Waislam na kuchukua Bai’a ya mwanae Yazid bin Mu’awiyah bin Abi Sufian kwa, ‘Ummah kwa mabavu, na akazikhalifu Ayah za Allah (s.w.t.) zilizo wazi, kama vile kumnasibisha Ubaydullah bin Ziyad kwa baba yake na kupanua meza za vyakula, kujenga mahekalu makubwa na mengineyo katika israf na upuuzi, yote hayo kwa mali za ‘‘Ummah na pato la Waislamu.

Haya yote na watu bado wako karibu na zama za Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) na makhalifa, na namna walivyokuwa wakiyapanyongo mambo ya dunia na matamanio yake.

Kisha akamtilia sumu Al Imam Hasan ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) na akamuua baada ya kutengua ahadi na masharti yote aliyomuahidi, kisha akachukua bayi’a kwa mwanae Yazid bin Mu’awiyah bin Abi Sufian kwa mabavu na hali yake inajulikana kwa ‘Ummah bila ya kuwa na ikhtilafu - Waislamu walishamjua kuwa ni mtu wa dunia hana uhusiano na dini… mpaka yakatokea mapinduzi ya Al Imam Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) Karbala, na kuuawa kwake Shahid pamoja na wafuasi wake wasiopungua sabini na mbili miongoni mwa Aali zake na wafuasi wake, baada ya kukataa kumbai Yazid bin Mu’awiyah bin Abi Sufian.

Vivyo hivyo ulikuwa ni mwendo wa watawala wa Bani Ummayyah na Bani Abbas, katika kuwakandamiza Ahlul-Bayt (a.s.). Ukandamizaji kwa Ahlul Bayt (a.s.), ulikuwa kwa muda wote huo, na waliyapata (matatizo) mengi, miongoni mwayo ni kuuliwa, kufungwa jela na kuadhibiwa.

Ukiuchunguza mwendo wa watoto wa Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) na Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) kwa ujumla, na ukaulinganisha na mwendo wa wafalme wa Bani Umayyah na Bani ‘Abbas, utagundua kuwa ndio umesababisha kuenea kwa Ushi’a ambao ndio Uislamu wa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) na si vinginevyo, na wala si kama walivyosema wapumbavu ambao walikuwa wakikariri wanayo yaeneza watawala wa Bani Umayyah na Bani ‘Abbas kuwa Ushi’a ni upuuzi wa ‘Abdillah bin Saba’ au mengineyo yasiyokuwa hayo miongoni mwa uongo ambao unasambaratika mbele ya macho ya anayesoma Itikadi hata kwa uchache tu.

Katika kipindi cha kwanza cha Bani Abbas, Al Imam Ja’afar as-Sadiq (a.s.) ambaye ni Imam wa Sita wa Mashi’a - kutokana na siasa yake ya hekima, aliweza kushirikiana na watawala na watu.

Na kwa sababu ya watawala kushughulika na kuimarisha utawala wao - alianza kueneza hukumu na kusambaza Hadith ambazo alizichukua kwa baba yake Al Imam Muhammad Al-Baqir (a.s.) kutoka kwa baba yake Al Imam Zaynul ‘Abidiin (a.s.) kutoka kwa Al Imam Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.), Bwana wa Mashahid (na Imamu Hasan as), kutoka kwa Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) kutoka kwa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.).

Ushi’a ukadhihirika bila ya kuwa na mfano katika zama hizo, kupanuka Madrasah ya Al Imam Ja’afar as-Sadiq (a.s.) katika zama hizo na umashuhuri wake ndiyo sababu ya kuitwa madhehebu ya Ja’afariyyah katika manhaji (njia) ambayo Shi’a Imamiyyah Ithna-’Ashariyyah wanaiamini tangu wakati huo hadi leo hii, na ambayo si kingine isipokuwa ni madhehebu ya Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) na ambayo ndiyo dhehebu la ki-Islamu la asili.

Miongoni mwa waliokuwa wanafunzi wake wakubwa ni kama vile Hassan Al-Basriy na Abu Hanifa An-Nu’uman ambaye amesema katika kauli yake mashuhuri. “Kama sio miaka miwili angeangamia Nu’uman” alikuwa na maana ya miaka miwili ambayo alikuwa mwanafunzi katika darasa la Imam Jaafar bin Muhammad bin Ali bin Hussein bin Ali bin Abu Talib (a.s.), na ambaye amepewa laqab ya As-Sadiq. Abu Hanifa aliuawa kwa sumu katika jela ya Abu Ja’afar Al-Mansur kwa sababu ya mapenzi na ufuasi wake kwa Ahlul Bayt (a.s.), na kumpinga kwake Mansur, na kwa sababu alikataa cheo cha Qadhi katika utawala wake. (rejea chochote ukitakacho katika vitabu vya historia juu ya hilo) Mansur alimkataza kutoa Fatwa hali yuko ndani ya jela.

Ama aliye eneza yanayojulikana kama madhehebu ya Hanafi ni Qadhi Abu Yusuf ambaye alikuwa mwanafunzi wa Abu Hanifa, Haruna Rashid alimpa uqadhi, jambo ambalo lilimsaidia katika kueneza madhehebu hayo.

Ni maarufu katika tarikh kuwa madhehebu manne yamechipukia kwa Al Imam Ja’afar as-Sadiq (a.s.), Imam Malik amechukua elimu yake kutoka kwenye vitabu vya Abu Hanifa ambaye amesoma miaka miwili kwa Al Imam Ja’afar as-Sadiq (a.s.) kama tulivyo bainisha juu, kisha Shaf’i akachukua kutoka kwa Malik, kisha Imam Ahmad akasoma kwa Shaf’i. Hivyo kinacho patikana katika vitabu vya madhehebu manne na kikaafikiana na madhebu ya Al Imam Ja’afar as-Sadiq (a.s.), basi kimetoka kwa Al Imam Ja’afar as-Sadiq (a.s.); na kinacho tofautiana ni Ijtihad yao.

Hakika Shi’a al-Imamiyyah Ithna-’Ashariyyah ni dhehebu ambalo limeepukana na Shub-ha na shaka, kwa sababu chini ya jina la Ushi’a yamechipuka makundi mengi sio katika Shi’a wala Shi’a sio miongoni mwa hayo na wala sio katika Uislamu hata chembe, Shi’a wako mbali nayo kama vile mbwa mwitu na damu ya Yusuf. Mfano wa baadhi ya madhehebu ambayo yamesema juu ya uungu wa Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.), wakidai kuwa sehemu ya uungu ipo kwa Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) na imeungana na mwili wake, na baadhi yake yanasema kuwa Maimam ni Manabii wakidai kuwa wao ni waungu. Al Imam Ja’afar as-Sadiq (a.s.) alipojua Itikadi yao akawa mbali nao akawalaani na akawaambia wafuasi wake wawe mbali nao, na akatoa kauli kali juu ya hilo.

Na sijui ni kwa nini tunaona baadhi wanAyahesabu makundi haya na mfano wake katika Ushi’a pamoja na kujulikana kwake kuwa yako nje ya Uislamu na Mashi’a wako mbali nayo.
________________________
1. Durrul - Manthuur ya Suyuti na Sawaiqul - Muhriqah ya Ibnu Hajar.

Kauli ya Uimamu sio bida’a iliyozuliwa na Shi’a kwani makundi yote ya Kiislamu yanasema kuwa Uimamu ni wajib, bali ni dharura ya kimaumbile kwa watu wote. Pamoja na kwamba Shi’a wana maoni maalumu, yaliyo muhimu zaidi ni kwamba, Uimamu ni maalumu kwa Maimamu kumi na mbili kutoka katika Ahlul-Bayt (a.s.) wa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.), na utaona hoja zenye nguvu juu ya hili kutoka katika vitabu Sahih vya Hadith vya Ahl as-Sunnah.

Na kama Uimamu usingekuwa faradhi kwa Waislamu wote basi wasingekuwa chini ya uongozi wa Makhalifa na kuwafuata wafalme ambao walichukua utawala kwa jina la Ukhalifa kama vile Banu Umayyah, Banu Abbas na wengineo, na kukataza kuwakhalifu na kutoka katika utawala wao, kwa sababu wao ni Makhalifa na Ulul-’Amr. kwa hiyo Uimamu ni dharura ya kimaumbile, akili ina hukumu hivyo kwa ajili ya kulinda Shariah kutopuuzwa na kuchezewa. Hivyo ilikuwa ni dhuluma kuwatukana Shi’a kwa kauli yao juu ya Uimamu. Amma kuhusu itikadi yao ya kuwa Uimamu ni maalumu kwa Maimamu wa Ahlul Bayt (a.s.) kumi na mbili, kuna dhambi gani kwa hilo? Je siyo vyema kwetu kuwauliza Shi’a ni dalili gani waliyo nayo juu ya hilo? Tutafupisha hoja na dalili zetu katika majibu yetu juu ya swali hili kwa utaratibu ufuatao:-

Kwanza - Hoja Za Kuthibitisha Uimamu Wa Ahlul- Bayt (A.S.)

Dalili zilizopokelewa kutoka kwa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) juu ya Uimamu wa Ahlul-Bayt (a.s.) katika ‘Ummah baada yake ni nyingi. Tunaorodhesha zilizo mashuhuri kati ya hizo:

*Katika Sahih Muslim kwa Isnad yake kutoka kwa Zaid bin Arqam amesema: “Hakika Mtume alisimama akahutubia katika Ghadir Khum (baina ya Makkah na Madina), akasema: “Enyi watu hakika mimi ni binadamu, anaweza kunijia Mjumbe wa Mola wangu (Malaika wa Mauti) basi nikamwitikia, hakika mimi nawaachieni vizito viwili cha kwanza ni Kitabu cha Allah (s.w.t.) humo kuna uongofu na Nuru, basi chukueni (uongofu) katika Kitabu cha Allah (s.w.t.) na shikamaneni nacho, na Ahlul Bayt wangu”.1

*Na katika Sahih At-Tirmidhi kwa isnad yake kutoka kwa Ja’bir bin ‘Abdullah amesema: “Nilimwona Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) katika Joho lake siku ya ‘Arafa naye yuko juu ya ngamia wake anahutubia, basi nilimsikia anasema: “Enyi watu hakika mimi nimekwisha kuachieni ambayo kama mtashikamana nayo hamtapotea kamwe, Kitabu cha Allah (s.w.t.) na kizazi changu, Ahlul Bayt wangu2

Tanbihi

Pia imepokewa kwamba Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) amesema: “Hakika mimi ninawaachieni ambacho kama mtashikamana nacho hamtapotea kamwe, Kitabu cha Allah (s.w.t.) na Sunnah zangu”.

Tukikadiria usahihi wa Hadith hii basi haipingani na Hadith mbili zilizo Sahih hapo juu, kwa sababu Ahlul-Bayt (a.s.) wao ndiyo njia zinazoaminika zaidi katika kupokea Sunnah za Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.). Isipokuwa neno wa sunnatiy peke yake kama ilivyo katika Hadith ya mwisho halitoshelezi kujua (hiyo sunnah), kwa sababu madhehebu zote za Kiislamu zinadai kuwa zinafuata Sunnah za Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) pamoja na kuwepo hitilafu nyingi baina ya madhehebu. Kwa kutazama hitilafu zao katika Hadith iliyopokelewa kutoka kwa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.), basi ni Sunnah ipi tutafuata?

Bila shaka Sunnah ya Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) ni moja lakini njia za kuipokea ni nyingi. Hivyo Sunnah imetofautiana kwa kutofautiana mapokezi ya wanaopokea, hivyo Sunnah ya Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) ikawa ni nyingi, na matokeo ya hayo Waislamu wamekuwa madhehebu mengi. Imepokewa kwamba idadi yake ni makundi sabini na tatu, kila kundi linasema kuwa linafuata Sunnah Sahih ya Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.), na kushikamana na kundi lolote kati ya haya hakuleti uongofu unaotakiwa kupatikana kama ilivyokuja katika Hadith.

Hivyo ikawa kuamini Hadith inayosema kushikamana na Kitabu cha Allah (s.w.t.) na Ahlul-Bayt (a.s.) inakubalika zaidi katika akili na mantiki, kwa sababu kuna yanayotufanya tujue na yanaondosha shaka na Ikhtilaf kwa kujulikana kutakaswa kwa Ahlul Bayt (a.s.) kutokana na uchafu kama utakavyoona katika yanayofuata. Katika Sahih Muslim hakika Mtume amebainisha kuwa Ahlul-Bayt (a.s.) wake ni Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.), Bi.Fatimah az- Zahra (a.s.) na watoto wao Al Imam Hasan ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) na Al-Imam Hussain ibn Ali ibn Abi Talib na kwamba wao ndiyo ambao imeteremka kwao Ayah ya Tat-hiir (kutakaswa) kama anavyopokea Muslim kwa isnad yake.

“Kutoka kwa Swafiyyah bint Shaibah amesema: ‘Aisha amesema: “Alitoka Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) ana Kisa’(amejifunika shuka), basi alikuja Al Imam Hasan ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) akamuingiza pamoja naye (chini ya shuka), kisha alikuja Al Imam Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) akamuingiza pamoja naye, kisha akaja Bi.Fatimah az-Zahra (a.s.) akamuingiza pamoja naye, kisha akaja Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) akamwingiza, kisha akasema: “Hakika Allah (s.w.t.) anataka kukuondoleeni uchafu nyinyi Ahlul Bayt na kukutakaseni kabisa kabisa”3

Na katika Sahih At-Tirmidhi inabainika kwa hoja zilizo wazi kuwa wake wa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) sio waliokusudiwa katika Ayah ya Tat-hiir kama baadhi ya watu wanavyodai ambapo At-Tirmidhi amepokea kwa isnad yake. Kutoka kwa ‘Amr bin Abi Salamah, mtoto wa kulelewa wa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) kwamba amesema: “Imeteremka Ayah hii ‘Hakika Allah (s.w.t.) anataka kukuondoleeni uchafu Ahlul Bayt na kukutakaseni kabisa kabisa” Katika nyumba ya ‘Umm Salamah, basi akamwita Bi.Fatimah az-Zahra (a.s.),Al Imam Hasan ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) na Al Imam Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) na akawafunika kwa Kisa’ (shuka), na Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) yuko nyuma ya mgongo wake akawafunika kwa Kisa’ kisha akasema: ‘Ee Allah (s.w.t.) hawa ni Ahlul Bayt wangu basi waondolee uchafu na watakase kabisa kabisa.’

‘Umm Salamah akasema: ‘Na mimi niko pamoja nao ewe Mtume wa Allah (s.a.w.w.)?’ Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) akasema: ‘Wewe uko mahala pako na uko katika kheri.’ “4

Na katika Musnad ya Ahmad amepokea kwa Isnad yake kutoka kwa ‘Umm Salamah: “Hakika Mtume wa Allah (s.a.w.w.) alimwambia Bi Fatimah az-Zahra (a.s.): ‘Niitie mume wako na watoto wako’, basi akaja nao, hivyo akawafunika kwa Kisa’, kisha akaweka mkono wake juu yao akasema: ‘Ewe Allah; hakika hawa ni Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) basi jaalia rehema zako na baraka zako kwa Muhammad na Aali wa Muhammad, hakika wewe ni Mwenye kuhimidiwa mtukufu’. ‘Umm Salamah akasema basi nikanyanyua Kisa’ ili niingie pamoja nao akakivuta kutoka kwenye mkono wangu na akasema: ‘Hakika wewe uko katika kheri.’ “5

Hadith Ya ‘Umm Salamah Katika Mapokezi Ya Bukhari

Katika Mustadrak As-Sahihain amepokea Al-Hakim kwa isnad yake kutoka kwa Hanashi Al-Kinaani, amesema: “Nilisikia Abu Dhar anasema akiwa ameshika mlango wa Ka’aba: Enyi watu anaenijua basi mimi ni yule mnaemjua na asienijua basi mimi ni Abu-Dhar, nimemsikia Mtume wa Allah (s.a.w.w.) akiwa amesema; ‘mfano wa Ahlul Bayt wangu kwenu ni kama mfano wa Jahazi la Nabii Nuh (a.s.), atakayelipanda amenusurika na atakayeacha kulipanda ameghariki na kuteketea”6

Vilevile katika Mustadrak As-Sahihain kwa isnad yake kutoka kwa Ibn ‘Abbas: Amesema Mtume wa Allah (s.a.w.w.) “Nyota ni tumaini kwa watu wa ardhini kutokana na kughariki, na Ahlul Bayt wangu ni tumaini kwa ‘Ummah wangu kutokana na ikhtilaf, kama kabila katika Waarabu litawakhalifu basi watakhitilafiana na kuwa kundi la Iblis “7

Na kwa kufafanua zaidi na kuongezea katika yaliyopita miongoni mwa dalili katika kuthibitisha kuwa Ahlul Bayt (a.s.) ndio wenye vyeo hivyo vitukufu kwa kutakaswa, wamefanywa kuwa ni maalumu kwa kupewa sifa ya tamshi la Alayhi Salaam (katika vitabu, kunatumika vifupisho vya hivyo kama (a.s.) bila ya Masahaba wengine wote na wake wa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.), na hiyo ni kutokana na vyeo vyao vitukufu na kwa yale aliyo yafanya Allah (s.w.t.) kuwa ni maalumu kwao kwa kuwatakasa kutokana na uchafu na makosa madogo kwa makubwa kama yanavyo dhihirika katika sehemu nyingi katika Sahih Bukhari: “‘Ali alayhi-s-salaam amesema:’Nilikuwa na ngamia katika hisa yangu ya ngawira na Mtume (s.a.w.w.) alikuwa amenipa sehemu katika (mali ya) Khums, basi nilipotaka kumwoa Fatimah alayha-s-salaam binti wa Mtume wa Allah (s.a.w.w.)…“.8

Katika mlango wa kuhimiza Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) Sala ya usiku na Sunnah bila ya kuifanya kuwa ni wajib, akasema “Mtume (s.a.w.w.) aliwagongea mlango Fatimah na ‘Ali alayhima-s-salaam usiku kwa ajili ya Sala “9

Na katika riwaya nyingine: amesema: “Nilimwona Mtume (s.a.w.w.) na Hasan ibn ‘Ali alayhima-s-salaam alikuwa anafanana naye…”10 Na vilevile: kutoka kwa Ali ibn Hussein alayhima-s-salaam alimwambia11 “Hakika Al Imam Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) amemwambia kwamba Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) amemwambia kuwa Mtume wa Allah (s.a.w.w.) alimgongea mlango usiku yeye na Bi.Fatimah az-Zahra (a.s.) binti wa Mtume wa Allah (s.a.w.w.), akawaambia je, hamsali?”

Na ni mashuhuri kwamba sifa hii ya (Alayhi Salaam) hakupewa asiye kuwa Ahlul Bayt isipokuwa Manabii tu.

Na ameamrisha Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) ya kwamba kuwasalia Ahli bayt wake kuambatane na kumsalia yeye, katika hadith ya Bukhari kupitia kwa Abdul-Rahman bin Abi Layla, amesema: “Alinikuta Kaab bin ‘Ujrah akasema: Je, nikupe zawadi? Hakika Mtume (s.a.w.w.) alitujia (siku moja) basi tukasema: “Ewe Mtume wa Allah (s.a.w.w.), tumeshafahamu namna ya kukusalimia, basi ni namna gani tutakusalia?” akasema: “Semeni: Allahumma Salli ‘alaa Muhammadin wa Aali Muhammadin kamaa Sallayta ‘alaa Ibrahima wa aali Ibrahima Innaka Hamidum Majid”.12

Hiyo ni kwa sababu Ibrahim alikuwa ni mtume na ahlul-bayt wake walikuwa ni manabii na wenye kulinda Shariah baada yake, vivyo hivyo walikuwa Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) lakini tofauti ni kwamba wao wamekuja ili wawe Maimamu na wala sio Manabii kama alivyobainisha hayo Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) alipomwambia Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) “Nafasi yako kwangu ni kama nafasi ya Harun kwa Mtume Musa (a.s.) isipokuwa hakuna Nabii baada yangu”13 kama yatakavyokuja hayo baadaye. inafahamika katika yote yaliotangulia miongoni mwa Hadith kwamba Allah (s.w.t.) Mtukufu kama alivyomfanya Mtume Wake kuwa ni maalumu anayeteremshiwa wahyi - Kwa Uma’asum na kutakaswa kwa kuwa sifa yake ni kufikisha ujumbe na dhamana ya usalama wa tablighi yake vinginevyo watu wasingeamini maneno yake na wala wasingekuwa na uhakika wa ujumbe wake. vile vile amewafanya Maimamu wa Ahlul Bayt (a.s.) kuwa ni maalumu kwa Uma’asum na kutakaswa kwa dalili ya Ayah:

إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّهُ لِيُذْهِبَ عَنْكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ وَيُطَهِّرَكُمْ تَطْهِيرًا {33}

“Hakika Allah anataka kukuondoleeni uchafu Ahlul Bayt na kukutakaseni kabisa kabisa (Al-Azhab 33:33)

Na kwa sifa yao ya kujaza nafasi ambayo ameiacha Mtume. Na hiyo ni kwa kubeba Shariah ya Allah (s.w.t.) kwa vizazi vijavyo kwa ajili ya kuihifadhi dini kutokana na upotovu wa wapotoshaji, uongo wa wadanganyifu na shaka za wenye shaka. Kwani kitu kibaya mno kilichokumba Shariah zilizotangulia ni kwamba wafuasi wake walikuwa wanachukua hukumu za Manabii wao baada ya kuondoka kwao kwa kila mtu. Basi upotovu ukawa kama ilivyosema Qur’an Tukufu basi wakapotoka na kupotea:

أَفَتَطْمَعُونَ أَنْ يُؤْمِنُوا لَكُمْ وَقَدْ كَانَ فَرِيقٌ مِنْهُمْ يَسْمَعُونَ كَلَامَ اللَّهِ ثُمَّ يُحَرِّفُونَهُ مِنْ بَعْدِ مَا عَقَلُوهُ وَهُمْ يَعْلَمُونَ {75}

“Mnatumaini ya kwamba watakuaminini (hao WAyahudi) na hali baadhi yao walikuwa wanasikia maneno ya Allah kisha wanayabadilisha baada ya kuwa wameyafahamu, na hali wanajua” (Surah Al-Baqarah 2:75)

Na kwa hiyo Uimamu unazingatiwa kuwa ni mlolongo wa Unabii katika jumla ya kazi zake isipokuwa kinachohusiana na Wahyi kwani huo ni maalumu kwa Manabii, na makusudio ya kuwa Uimamu ni mlolongo wa Unabii ni kule kuhifadhi Shariah kinadharia na kivitendo. Hivyo ikawa ni wajib Maimamu wawe Ma’asum kutokana na uwajib wa kunukuu Shariah ya Allah (s.w.t.) - ambayo alikuja nayo Mtume wa Allah (s.a.w.w.) - Kwa vizazi vijavyo kupitia katika njia safi, na ya asili ambayo imepitia kwa Maimamu kumi na wawili wa Ahlul Bayt (a.s.).Na kuna dalili za Qur’an zinazoashiria kuwa Uimamu ni cheo kitukufu hakipati mtu, dhalimu au fasiki, amesema Allah (s.w.t.):

قَالَ إِنِّي جَاعِلُكَ لِلنَّاسِ إِمَامًا ۖ قَالَ وَمِنْ ذُرِّيَّتِي ۖ قَالَ لَا يَنَالُ عَهْدِي الظَّالِمِينَ {124}

“Hakika mimi nitakufanya kuwa Imam kwa watu”; akasema (Ibrahim): “Je na katika kizazi changu?”; (Allah) akasema: “(ndiyo, lakini) ahadi yangu haitawafikia madhalimu”. (Al Baqarah 2:124)

Hivyo makosa madogo na makubwa yanamfanya anayeyatenda kuwa ni dhalimu, hivyo ikawa hakuna budi ya Imam kuwa ni Ma’asum kutokana na makosa yeyote au dhambi kama ilivyoonyesha Ayah iliyotangulia.

Uchunguzi Juu Ya Ayah Ya “Tat-Hiir”

Hakuna shaka kwamba Ayah ya “Hakika Allah anataka kukuondoleeni Uchafu Ahlul-Bayt na kukutakaseni kabisa kabisa” inaonyesha Uma’asum wa wale iliyo teremshwa kwa ajili yao, kwa sababu rijsi katika lugha ina maana ya uchafu (na uchafu ni kinyume cha usafi), na tohara katika lugha ina maana ya utakaso na usafi.

Rijsi ni dalili ya dhambi na tohara ni dalili ya uchamungu, hivyo mradi wa Allah (s.w.t.) Mtukufu kuwaondolea rijisi (uchafu) ni kuwaepusha na kuwaweka mbali na mambo yanayo sababisha upungufu kwao, hii haina maana nyingine isipokuwa ni Uma’asum na utakaso ambao Ayah imeteremka kwa ajili yao nao ni Ahlul Bayt (a.s.) “Muhammad, Ali, Fatwimah, Hassan na Hussein” kama zilivyo onyesha hayo kwa uwazi Hadith zilizotangulia.

Pamoja na hayo, kuna baadhi ya wanaosema kwamba Ayah hii siyo maalumu kwa Ahlul Bayt wa Nabii (s.a.w.w.), (Ali, Fatwimah, Hassan na Hussein) tu, bali inawahusu wake zake pia kwa hoja ya kuja Ayah ya Tat- hiir katikati ya Ayah nyingi (Katika sura ya Al-Ahzab) zinazohusu wake wa Nabii.

Lakini Ushahidi huu haukubaliwi, kwa kuongezea tuliyoyaeleza kuhusu Hadith ya ‘Umm Salamah kuwa Ayah hii ni maalumu kwa waliobainishwa majina yao miongoni mwa Ahlul Bayt (a.s.).

Hakika Ayah inaonyesha kwa dalili ya wazi juu ya Uma’asum wa ambao imeteremka kwa ajili yao kama tulivyotangulia kubainisha na wanawake wa Nabii sio Maasumu na hakusema yeyote juu ya hilo, na kutishiwa kwao talaka kama ilivyokuja katika Ayah zilizo tangulia Ayah ya Tat-hiir inatosha kuthibitisha ukweli huu, tukiachilia mbali kutoka kwa ‘Aisha bint Abubakr ibn Abu Quhafa na kuongoza jeshi lenye kumpiga vita Khalifa wa Waislamu na Imam wao ambaye ni wajib kumtii, na mengineyo mengi utakayoyaona kwa ufafanuzi zaidi huko mbele. Na yanayotilia nguvu pia, kutoingia wake wa Nabii katika makusudio ya Ayah ya Tat-hiir ni dhamira ya wenye kusemeshwa katika Ayah zilizotangulia Ayah hizo, ni dhamiri ya wingi wa wanawake zitazame Ayah:
 

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُلْ لِأَزْوَاجِكَ إِنْ كُنْتُنَّ تُرِدْنَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا وَزِينَتَهَا فَتَعَالَيْنَ أُمَتِّعْكُنَّ وَأُسَرِّحْكُنَّ سَرَاحًا جَمِيلًا {28}

 

وَإِنْ كُنْتُنَّ تُرِدْنَ اللَّهَ وَرَسُولَهُ وَالدَّارَ الْآخِرَةَ فَإِنَّ اللَّهَ أَعَدَّ لِلْمُحْسِنَاتِ مِنْكُنَّ أَجْرًا عَظِيمًا {29}

 

يَا نِسَاءَ النَّبِيِّ مَنْ يَأْتِ مِنْكُنَّ بِفَاحِشَةٍ مُبَيِّنَةٍ يُضَاعَفْ لَهَا الْعَذَابُ ضِعْفَيْنِ ۚ وَكَانَ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّهِ يَسِيرًا {30}

 

وَمَنْ يَقْنُتْ مِنْكُنَّ لِلَّهِ وَرَسُولِهِ وَتَعْمَلْ صَالِحًا نُؤْتِهَا أَجْرَهَا مَرَّتَيْنِ وَأَعْتَدْنَا لَهَا رِزْقًا كَرِيمًا {31}

 

يَا نِسَاءَ النَّبِيِّ لَسْتُنَّ كَأَحَدٍ مِنَ النِّسَاءِ ۚ إِنِ اتَّقَيْتُنَّ فَلَا تَخْضَعْنَ بِالْقَوْلِ فَيَطْمَعَ الَّذِي فِي قَلْبِهِ مَرَضٌ وَقُلْنَ قَوْلًا مَعْرُوفًا {32}

 

وَقَرْنَ فِي بُيُوتِكُنَّ وَلَا تَبَرَّجْنَ تَبَرُّجَ الْجَاهِلِيَّةِ الْأُولَىٰ ۖ وَأَقِمْنَ الصَّلَاةَ وَآتِينَ الزَّكَاةَ وَأَطِعْنَ اللَّهَ وَرَسُولَهُ ۚ إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّهُ لِيُذْهِبَ عَنْكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ وَيُطَهِّرَكُمْ تَطْهِيرًا {33}

“Yaa ayyuha Nnabiyyu qul-liaz’waajika in kuntunna turidnal-hayata- d-dun’yaa waziynatahaa fataalayna....umatti’ikunna wa usarrihkunna saraahan jamilan wain kuntunna… minkunna … ya nisaa Nnabiyi man yya’ti minkunna bifaahishatin… lastunna… falaa takhdha’na... waqarna fiy buyuutikunna walaa tabarrajna...” (Al Azhab 33:28-33)

Na maneno yalipoanza kuhusu jambo la Tat-hiir, dhamiri ya mwenye kusemeshwa ikabadilika kwenda katika dhamiri ya wingi wa wanaume “Innamaa yuriydullahu liyudh’hiba ankumu-r-rijsa ahlal-bayti wa yutwahhirakum tat’hiyra”, na hakika kuteremka Ayah za Qur’an kwa kuwahofisha wanawake wa Nabii kwa talaka, na Allah (s.w.t.) kutaka kuwataka Ahlul Bayt (a.s) kuja kwa kufutana, haina maana ya ulazima wa makusudio ya minasaba miwili kuwa ni wanawake wa Nabii, hiyo ni kwa sababu kuna Ayah nyingi za aina hii katika Qur’an zinazo zungumzia kuhusu mambo mawili tofauti, na huenda sababu ya kuja pamoja katika Ayah hiyo hiyo ni kuafikiana kwa kutokea minasaba miwili kama amabavyo Qur’an Tukufu haikupangwa kulingana na mfuatano wa Ayah kama zilivyoteremka, na hii inajulikana.

Hivyo basi hakuna ushahidi wowote kuwa sehemu ya Ayah ya Tat-hirr ni katika kipande ambacho kipo katika Qur’an iliyokusanywa.

Mwisho, katika yanayothibitisha kutoteremka Ayah ya Tat-hiir kwa wake wa Nabii ni Hadith ya Thaqalain (vizito viwili) ambayo inaamrisha kushikamana na Kitabu na Ahlul Bayt (a.s.). Kama makusudio ya Ahlul- Bayt (a.s.) ni wake zake, je kunapatikana Hadith tukufu kwa Waislamu inayosema tufuate wanawake na kushikamana nao baada ya kufa kwa Nabii sambamba na kushikamana na Kitabu cha Allah (s.w.t.)? Bila shaka hakuna. Namna gani itakuwa hivyo hali wamekwisha amrishwa kujilazimisha kubaki katika nyumba zao tukiachilia mbali kuwa wote walikuwa katika wakati mmoja, na kama itasemwa kwamba kushikamana nao ni kufuata walioyapokea, miongoni mwao katika Hadith za Nabii tunasema; kuna miongoni mwao ambaye hakupokea hata Hadith moja.

Pili -Dalili Za Kuthibitisha Idadi Ya Maimamu Wa Ahlul Bayt (A.S.)

Ni Kumi Na Mbili

Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) ameeleza kwamba Idadi ya Maimamu wa Ahlul Bayt (a.s.) ambao wanafuata baada yake ni kumi na mbili. Imekuja katika Kitabul-Ahkam katika Sahih Bukhari: “Amesema: nimemsikia Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) anasema: ‘Watakuwa Maimamu kumi na mbili’, akasema neno sikulisikia, baba yangu akasema amesema kwamba wote ni kutoka katika Maquraish.”14

Na katika Sahih Muslim: “Dini haitaacha kuwa imesimama hadi siku ya Qiyamah na watakuwepo kwenu Makhalifa kumi na mbili wote ni katika Maquraish”.15

Na “mambo ya watu hayataacha kutengemaa maadam wataongozwa na Maimamu kumi na mbili.”16

Na katika Musnad ya Ahmad kwa isnad yake kutoka kwa Abdallah bin Mas’ud kwamba amesema “Aliulizwa Mtume wa Allah (s.a.w.w.) kuhusu jambo la Makhalifa, akasema ni kumi na mbili kama vile idadi ya viongozi wa Bani Israil.”17

Na katika Taurati ya Ahlul-Kitab (kuna aya) ambayo madhumuni yake ni: “Hakika Allah (s.w.t.) Mtukufu alimbashiria Mtume Ibrahim kuhusu Ismail kwamba atamkuza, atampa kizazi na atamjaalia katika kizazi chake viongozi kumi na wawili na ‘‘Ummah mkubwa. Na tamko la neno kwa neno kama ilivyokuja katika (Taurati) kutoka katika Kitabu kitakatifu: “Na kwa habari za Ishmaeli nimekusikia, nimembariki, nitamzidisha, nami nitamwongeza sana sana. Atazaa maseyidi kumi na wawili, nami nitamfanya awe taifa kuu”.18

Hakika Hadith za hapo juu baadhi yake zinabainisha kwamba utukufu wa Uislamu umejaaliwa katika Makhalifa kumi na mbili, na baadhi yake zinaonyesha kuwa uhai wa dini na kubaki kwake hadi siku ya Qiyamah umeegemezwa kwao na kwamba wao wote ni katika Maquraish. Na katika mapokezi mengine wote ni katika Bani Hashim, mapokezi haya hayaafikiani na madhehebu yeyote isipokuwa madhehebu ya Ahlul Bayt (a.s.) - Madhehebu ya Shi’a Al-Imamiah Al-Ithna ‘Ashariyyah - na hiyo ni kwa kuafikiana idadi hii pamoja na idadi ya Maimamu wa Ahlul Bayt (a.s.) kumi na mbili, wakati ambapo Maulamaa wa Ahl as-Sunnah katika kufasiri Hadith hii wamefikia katika njia yenye kikomo. Je makusudio yake ni Makhalifa wanne kwa kuongezea na makhalifa wa Bani Umayyah na Bani ‘Abbas?

Sisi tunajua kwamba Makhalifa wa mwanzo hawakuwa kumi na mbili, na wala kuwajumuisha kwao Bani Umayyah na Bani Abbas idadi hii haipatikani kwao na wala maulamaa wa Kisunni hawatatofautiana katika jambo kama walivyo tofautiana katika kufasiri kwao Hadith hii. Tunatoa mfano mmoja ili uone mgongano wao katika tafsiri ya Hadith hii, nayo ni rai ya As-Suyuti, anataja katika Kitabu chake cha tarekhe: “Na walishapatikana Makhalifa kumi na mbili, Makhalifa wanne, Al Imam Hasan ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.), Mu’awiyah bin Abi Sufian, Zuber na ‘Umar bin ‘Abdul-Azizi, hawa ni nane, na inakisiwa anaweza kuunganishwa nao Al-Mahdi Al-Abbas kwa sababu yeye katika Bani ‘Abbas ni kama vile Abdul-azizi katika Bani Umayyah, na Tahir Al-’Abbas vile vile, kwa kile alichopewa miongoni mwa uadilifu, wanabaki wawili wanaosubiriwa mmoja wao ni Al-Mahdi kwa sababu yeye ni katika Ahlul Bayt (a.s.).”19

Na idadi ya kumi na mbili haitopatikana katika kundi lolote isipokuwa katika Maimamu wa Shi’a Ithna-’Ashariyyah. Na Hadith zilizo pokelewa maalumu kwa jambo hili katika njia za Kishi’a ni nyingi zinapita mpaka wa Tawatur ambapo humo kumetajwa majina ya Maimamu kumi na mbili kwa ufafanuzi zaidi kiasi ambacho haikubaliki shaka wala Ikhtilaf.

Basi ni kipi kinachotufanya tuache tafsiri ya Hadith iliyo wazi inayoafikiana na mfuatano wa Maimamu kumi na mbili wa Kishi’a na tunatupia nafsi zetu wenyewe katika matatizo ambayo hakuna pa kutokea.

Ni mashuhuri kwamba bwana wetu Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) na Ahlul- Bayt (a.s.) na kizazi chao kimetokana na Mtume Ismail (a.s.) na viongozi kumi na mbili ni maimamu wa Ahlul Bayt (a.s.) na ‘Ummah mkubwa ni ‘Ummah wa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) na hii inafaa kuwa hoja kwa Ahlul-Kitab kuhusu ukweli wa bwana wetu Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.).

Tatu-Hoja Za Kuthibitisha Kupewa Ukhalifa Al Imam ‘Ali Ibn Abi Talib (A.S.)

Tumekwisha tanguliza hoja za Uimamu wa Ahlul Bayt (a.s.) na kwamba Maimamu wao kumi na mbili ndiyo Makhalifa wa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.). Na katika yafuatayo tunabainisha Hadith zinazoonyesha Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) kumfanya Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) kuwa Khalifa katika ‘Ummah baada yake, na Imam wa kwanza (katika Maimamu kumi na mbili). Hadith hizi ni Mutawattir katika pande mbili isipokuwa Ikhtilaf baina yao imepatikana katika ushahidi wake, Hadith zilizo muhimu zaidi kuhusu hili ni ile inayojulikana kama hotuba ya Ghadiir, tunaitaja kwa muhtasari.

Katika Sahih Tirmidhi katika sanad yake kutoka kwa Zaidi bin Arqam kwamba Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) amesema:” (yeyote) ambaye Mimi ni kiongozi wake, basi ‘Ali (pia) ni Kiongozi wake.”20

Na katika Sunan Ibn-Maajah kwa isnad yake kutoka kwa Al-baraa’ bin ‘Aazib amesema: “Tulirejea pamoja na Mtume wa Allah (s.a.w.w.) kutoka kwenye Hijja ambayo alihiji akateremka katika baadhi ya njia akaamuru Sala ya Jama’a, basi akashika mkono wa Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) akasema: “Je, mimi si bora zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao?” Wakasema: “Ndiyo!! Wewe ni bora”, Akasema: “Je, mimi si bora zaidi kuliko kila mumini kwa nafsi yake?” Wakasema: “Ndiyo”, Akasema: “Basi huyu ni kiongozi wa (yule) ambaye mimi ni kiongozi wake; Ewe Allah, mpende atakayemfanya kuwa kiongozi, Ewe Allah mfanye adui atakaye mfanyia uadui.”21

Na katika Musnad Ahmad bin Hambal kwa isnad yake kutoka kwa Al-Barra’ bin Aazib amesema “ Tulikuwa pamoja na Mtume kutoka kwa Al-Barra’ bin Aazib amesema “Tulikuwa pamoja na Mtume wa Allah (s.a.w.w.) katika safari tukateremka Ghadir Khum, tukalinganiwa Sala ya Jama’a, pakasafishwa kwa ajili ya Mtume wa Allah (s.a.w.w.) chini ya miti miwili basi akasali Adhuhuri na akamshika Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) mkono akasema: “Je, si mnajua kuwa mimi ni bora zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao?” Wakasema: “Ndiyo.” Akasema: “Je, si mnajua kuwa mimi ni bora zaidi kwa kila Muumin kuliko nafsi yake?” Wakasema: “Ndiyo.” Basi akashika mkono wa Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) na akasema: “Ambaye nilikuwa kiongozi wake basi ‘Ali ni kiongozi wake! Ee Allah, mpende atakayempenda na mfanyie uadui atakayemfanyia uadui.” Baada ya hapo ‘Umar bin Al-Khattab akasema: “Pongezi ewe mtoto wa Abu Talib, umekuwa kiongozi wa kila Muumin mwanamume na mwanamke.”22

Hadith hii imekuwa ni Mashuhuri kwa jina la Al-Ghadir kwa kutokea katika sehemu ya Ghadir al-Khum, nayo ni miongoni mwa dalili za Shariah zenye nguvu na iliyo wazi zaidi juu ya Ukhalifa wa Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) na Uimamu wake baada ya Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.). Na Hadith hii inazingatiwa ni katika daraja la juu la usahihi na yenye nguvu kwa sababu ni Mutawatir kwa Waislamu wote Sunni na Shi’a.

Baadhi katika wale ambao hawakuweza kuutilia shaka usahihi wa sanad ya Hadith hii wamejaribu kutilia shaka ushahidi wake juu ya Uimamu na Ukhalifa kwa kuchukulia kuwa neno mawla: lina maana ya Urafiki au Mpenzi na sio kiongozi, lakini neno Maula kama lilivyo katika Hadith ifuatayo kwa mfano limekuja kwa maana ya kiongozi au M-bora zaidi kwa uongozi au uwakala.

Kutoka kwa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) amesema: “Hakuna Muumini (yeyote) isipokuwa mimi ni bora kwake zaidi kuliko watu (wote) katika dunia na akhera”.

Mkipenda someni: “Annabiy awla bil-mu’minina min anfusihim, Fa ayyumaa Muumin taraka maalan falyarithuhu as-habuhu man kanuu, fa in taraka dainan au dhiyaa’n falyaatini wa anaa mawlaahu.”23

Tukiangalia mazingira ya Hadith ya Ghadir, wakati wake na sehemu ambayo imeizunguka na vielelezo vingine, vyote hivyo vinaonyesha kweli kwamba makusudio hayakuwa isipokuwa Uimamu na utawala ambao una maana ya uongozi kwa maana zake zote na kati ya vielelezo hivyo ni: -

1. Hakika Ayatu-t-Tablighi “(Ewe Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) fikisha uliyo teremshiwa kutoka kwa Mola wako na kama hutofikisha basi utakuwa hujafikisha Ujumbe wake, na Allah (s.w.t.) atakulinda na watu),”24 ambayo ilishuka kabla ya tukio la Ghadiri kwa tamko lake kali na vielelezo vilivyopo, inaonyesha kuwa mazungumzo hayakuwa ni juu ya urafiki wa kawaida, kwa sababu haya hayawajibishi umuhimu wote huo na mkazo, kwani Allah (s.w.t.) amefanya jambo la kufikisha kuwa ni lenye kutegemea kuthibiti kwa Ukhalifa baada yake kwa sababu ni kwa Ukhalifa tu na wala sio jambo lingine Allah (s.w.t.) na Mtume wake watausalimisha ‘Ummah huu na dini yao kwa wale waliorithi elimu ya Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) baada kufariki kwake.

Kama ilivyo Ayah maalumu kwa kukamilisha dini: (“Leo nimekukamilishieni dini yenu na nimekutimizieni neema zangu na nimekuridhieni Uislamu kuwa ni dini yenu”)25 ambayo iliteremka baada tu ya kumalizika hotuba ya Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.), ambapo alimtawaza Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) kuwa Khalifa na Imam kwa ‘Ummah. Inaonyesha kwa dalili ya wazi kwamba maudhui yalikuwa ni muhimu mno kama vile maudhui ya uongozi na Ukhalifa baada ya Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.), na kwamba alikuwa katika mnasaba wa kumteua Imam baada yake. Huyu atakayekuwa Imam baada yake si mwingine ila ni Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.), na makusudio ya Hadith sio (“Ambaye nilikuwa kipenzi chake na msaidizi wake basi Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) ni kipenzi chake na msaidizi wake).

2. Njia ambayo Hadith imeelezwa kwa hali zake zote, jangwa lenye joto kali, ambapo hotuba ilitolewa hapo na kuchukua muafaka wa watu katika hali hiyo na sehemu hiyo yote, haya yanaonyesha usahihi wa mwelekeo tulio uchukua wa kumtawalisha Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) katika nafasi ya Uimamu na wala sio jambo lingine, kwa sababu ni jambo muhimu na ni wajibu lijulikane kabla ya kufika mauti ya Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.), ambayo yeye mwenyewe hakuwa anajua itakuwa ni lini kwani yanaweza yakamfika kabla ya kufika kwake Madina. Hivyo ni wajibu wake kutangaza jina la kiongozi baada yake wakati huu, kwani kutangaza jina la kiongozi kuna athari za kivitendo kwa Waislamu baada yake na kwa dunia yao.

Ama kujua kwao kwamba Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) ni kipenzi cha waumini - kwa mfano - ni jambo ambalo halina athari katika maisha ya watu na kutojua kwao hakubadilishi kitu katika maisha yao na taratibu zao.

3. Na katika Sahih Tirmidhi kwa isnad yake kutoka kwa Imran bin Huswayn amesema: “Mtume wa Allah (s.a.w.w.) alituma jeshi na akampa uongozi wake Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) wakaenda katika sariya (kikosi) akampata msichana akamchukua, wakamkataza, na wanne katika Masahaba wa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) wakakubaliana wakasema tutakapokutana na Mtume wa Allah (s.a.w.w.) tutamweleza aliyo yafanya Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.), basi Mtume wa Allah (s.a.w.w.) alikuja na ghadhabu inaonekana katika uso wake na akasema: “Mnataka nini kwa ‘Ali? Hakika ‘Ali ametokana na mimi na mimi nimetokana na yeye, naye ni kiongozi wa kila muumini baada yangu.”26

Na kauli ya Allah (s.w.t.):

إِنَّمَا وَلِيُّكُمُ اللَّهُ وَرَسُولُهُ وَالَّذِينَ آمَنُوا الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَهُمْ رَاكِعُونَ {55}

Hakika kiongozi wenu ni Allah, Mtume wake na walioamini ambao wanasimamisha sala na wanatoa zaka hali wakirukuu”. (Al Maidah 5:55)

Imeshuka kwa ajili ya Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.), kama inavyofafanuliwa katika tafsiri za wafasiri wengi27 alipotoa sadaka pete yake kwa maskini aliyemjia akiwa katika sala hali akirukuu.

Na katika Hadith zingine ambazo zinaashiria Ukhalifa wa Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) ni Hadith ya Manzilah (Cheo), kutoka kwa Mus’ab bin Sa’ad kutoka kwa baba yake: ‘Hakika Mtume wa Allah (s.a.w.w.) alitoka kwenda Tabuk, na akamwacha ‘Ali (a.s.).

Ambaye alisema: “Unaniacha pamoja na watoto na wanawake?” Mtume akasema: “Je, huridhii kuwa cheo chako kwangu ni kama cheo cha Harun kwa Musa, isipokuwa hakuna Nabii baada yangu?”28

Hadith hii inaonyesha kuwa vyeo vyote alivyokuwa navyo Harun kwa Bani Israil katika upande wa Mtume Musa (a.s.) kwa kuondoa Unabii. - Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) alikuwa navyo, kwa sababu Hadith haina kizuizi chochote au sharti, na kwa hivyo yanafahamika kutoka ndani ya hadith hiyo yafuatayo:-

1. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) alikuwa ni waziri wa Mtume na msaidizi wake maalumu na mshirika wake katika uongozi wa ‘Ummah kwa sababu vielelezo vimethibitsha vyeo hivyo kwa Haruna. Qur’an Tukufu inasema:

وَاجْعَلْ لِي وَزِيرًا مِنْ أَهْلِي {29}

 

هَارُونَ أَخِي {30}

 

اشْدُدْ بِهِ أَزْرِي {31}

 

وَأَشْرِكْهُ فِي أَمْرِي {32}

 

كَيْ نُسَبِّحَكَ كَثِيرًا {33}

 

وَنَذْكُرَكَ كَثِيرًا {34}

 

إِنَّكَ كُنْتَ بِنَا بَصِيرًا {35}

 

قَالَ قَدْ أُوتِيتَ سُؤْلَكَ يَا مُوسَىٰ {36}

“Na nijaalie waziri katika jamaa zangu, Ndugu yangu Haruna (mfanye awe ndiye waziri wangu), nitie nguvu kwa (ndugu yangu) huyu, na umshirikishe katika kazi yangu (hii)…” (Allah) Akasema: “Hakika umepewa maombi yako (yote haya uliyoyataka)., ewe Musa! (Twaha 20:29-36)

2. Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.), alikuwa ni bora zaidi katika ‘Ummah baada ya Mtume kama alivyokuwa Harun katika Bani Israil.

Na yanayotilia nguvu kustahiki Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) katika cheo hiki kitukufu na kuwa kwake Khalifa wa ‘Ummah baada ya Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) ni kwamba yeye alikuwa ni mjuzi kati ya Masahaba wote. Katika kutambua hili walio mashuhuri kati yao ni hawa wafuatao:-

Kutoka kwa Said Bin Jubeir kutoka kwa Ibn ‘Abbas: “Amesema ‘Umar:’ Msomaji wetu mzuri ni Ubay na hakimu wetu ni Ali’.”29 Hiyo ni kwa sababu mwenye kuhukumu zaidi ndiyo mjuzi zaidi wa hukumu na kanuni, na hilo liko wazi,na inatosha kuthibitisha ujuzi wake mkubwa kule kuwa kwake mlango wa mji wa elimu ya Mtume wa Allah (s.a.w.w.), na hekima yake, kama ilivyo katika Sahih Tirmidhi kwa isnad yake kutoka kwa Ibn ‘Abbas amesema: ‘Amesema Mtume (s.a.w.w.): “Mimi ni mji wa hekima na ‘Ali ni mlango wake.”30

Na katika Mustadrak As-Sahihain kwa sanadi yake kutoka kwa Ibn ‘Abbas (r.a.) amesema: “Mimi ni mji wa elimu na ‘Ali ni mlango wake, basi anayetaka elimu apitie mlangoni.”31 Al-Hakim amesema isnad ya Hadith hii ni S