Rafed English
site.site_name : Rafed English

Kukusanya Sala Mbili by : Sheikh Jafar Sub’hani

 

Kitabu kilichoko mikononi mwako, ni tarjuma ya kitabu cha Kiarabu kwa jina la: "Al-Jam’u Bayna Salaatayn" Sisi tumekiita: "Kukusanya Sala mbili." Kitabu hiki, "Kusanya Sala mbili" ni matokea ya utafiti wa kielimu uliofanywa na Mwanachuoni wa Kiislamu, Sheikh Jafar Subhani. Sheria ya Kiislamu ni ya kipekee kwa kuwa inahusika na kila jambo huku ikiweka utatuzi wa matatizo yote yanayompata mwanadamu katika sekta zote za maisha yake.

Wanachouni wa Kiislamu kama kawaida ya wanadamu wamehitilafiana katika hukumu ndogo ndogo katika matendo ya ibada, lakini kama ilivyo, tofauti ndogo kati ya wanachuo kwa wafuasi inakuwa ni mlima wa tofauti na kusababisha zongo lisilo na maana. Mambo ambayo wanachuo wetu wamehitilafiana si katika asili au misingi ya dini, na isitoshe ni mambo machache sana ukilinganisha na yale tunayokubaliana nayo.

Kukusanya Sala mbili ni suala ambalo wanachuo wetu wamehitalifiana; ndani ya madhehebu moja na kati ya madhehebu. Kwa hiyo hii sio hitilafu ya madhehebu, bali ni hitilafi ya wanachuo wa madhehebu zote wamehitilafi- ana juu ya suala hili. Lakini bahati mbaya Waislamu wengi hawaitambui hitilafu hii kwa usahihi na hivyo kuongelea katika dhana na kusababisha mizozo isiyokuwa na maana. Kutokana na hali hii Sheikh wetu, Jafar Subhani amelifanyia utafiti wa kina suala hili na kuweka wazi asaili ya hitilafu hii, kisha akamuachia mso- maji mwenyewe kutoa uamuzi.

Kitabu hiki ni chenye manufaa sana, hususan wakati huu wa maendeleo makubwa ya elimu katika nyanja zote. Kutokana na ukweli huu, Taasisi yetu ya 'Al-Itrah Foundation' imeona ikitoe kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili, kwa madhumuni yake yale yale ya kuwahudu- mia Waislamu, hususan wazungumzaji wa Kiswahili, ili kuongeza ujuzi wao katika masuala ya dini na ya kijamii.

Tunamshukuru ndugu yetu, Hemedi Lubumba Selemani kwa kukubali jukumu hili la kukifanyia tarjuma kitabu hiki. Vilevile tunawashukuru wale wote walioshiriki kwa njia moja au nyingine hadi kufanikisha kuchapishwa kwa kitabu hiki.

Mchapishaji:

Al-Itrah Foundation
S. L. P. 19701
Dar-es-Salaam, Tanzania.
Kwa Mtazamo Wa Qur’ani Na Sunna
Kila sifa njema ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa ulimwengu. Rehma na Amani zimfikie mbora wa viumbe na hitimisho la mitume Wake, pia kizazi chake kitakatifu ambacho ndio kasha la elimu yake na hazina ya mafunzo yake.

Hakika Uislamu ni imani na sheria. Imani ni kuamini Mwenyezi Mungu, mitume Wake na Siku ya Mwisho.

Na sheria ni hukumu za Mwenyezi Mungu ambazo zina jukumu la kumpa mwanadamu maIsha bora na kumhakikishia wema wa dunia na akhera.

Sheria ya Kiislamu ni ya kipekee kwa kuwa inahusika na kila jambo huku ikiweka utatuzi wa matatizo yote yanayompata mwanadamu katika sekta zote za maIsha yake, hivyo Mwenyezi Mungu akasema:
الْيَوْمَ يَئِسَ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْ دِينِكُمْ فَلَا تَخْشَوْهُمْ وَاخْشَوْنِ ۚ الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا ۚ{3}
“Leo nimewakamilishieni dini yenu na kuwatimizieni neema YangunanimewapendeleeniUislamuuwedini yenu.”(5:3).
Isipokuwa kuna masuala madogo madogo ambayo wanazuoni wa sheria wametofautiana kwa sababu ya kuhitilafiana kwao kuhusu riwaya zitokanazo kwa Mtume (s.a.w.w.).
Jambo ambalo limepelekea kutofautiana kuhusu masuala madogo madogo ya sheria.
Kwa kuwa ukweli hutokana na utafiti, basi hakika katika mtiririko wa masomo haya tumejaribu kuliweka suala hili juu ya meza ya utafiti, kwani huenda ikawa ndio njia ya kuunganIsha mtazamo na kusogeza hatua katika uwanja huu, kwani tofauti iliyopo si katika asili na misingi ya dini hata ipelekee kuwa na uadui na chuki, bali tofauti iliyopo ni kuhusu riwaya zilizonasibishwa na Mtume, nalo ni jambo dogo ukilinganIsha na mambo mengi ambayo tunaafikiana kati ya madhehebu za Kiislamu.
Na muongozo wetu katika njia hii ni kauli ya Mwenyezi Mungu (s.w.t):
وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا ۚ وَاذْكُرُوا نِعْمَتَ اللَّهِ عَلَيْكُمْ إِذْ كُنْتُمْ أَعْدَاءً فَأَلَّفَ بَيْنَ قُلُوبِكُمْ فَأَصْبَحْتُمْ بِنِعْمَتِهِ إِخْوَانًا{103}
“Na shikamaneni na kamba ya Mwenyezi Mungu nyote wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu, mlipokuwa maadui naakaziunganIshanyoyozenu,hivyokwaneemazake mkawandugu."(3:103).
JafarSubhany
TaasisiyaImamSadiq(a.s.)
Qum
Kukusanya kati ya Sala mbili kuna sura tofauti:

• Kukusanya Sala mbili Muzdalifa na Arafa.

• Kukusanya Sala mbili safarini.

• Kukusanya Sala mbili pasipokuwa safarini kwa udhuru kama vile mvua na tope.

• Kukusanya Sala mbili pasipokuwa safarini bila ya kuwepo udhuru wowote.

Hivyo sura mbili za kwanza ndizo zinazoingia katika hukumu ya safari na si sura mbili za mwisho. Wanazuoni wa sheria ya Kiislamu wamekubaliana kuhusu kukusanya Sala hapo Muzdalifa na Arafa lakini wametofautiana kuhusu kukusanya Sala eneo lingine lisilokuwa kaati ya hayo mawili. Hivyo sisi hapa tutazungumzia kwa ufupi sura moja baada ya nyingine huku tukitaja kauli zinazohusu suala hili na vyanzo vya kauli hizo.
1. Kukusanya Sala Mbili Muzdalifa Na Arafa
Wanazuoni wa sheria ya Kiislamu wamekubaliana kuhusu kupendelea kukusanya Sala Muzdalifa na Arafa na wala hakuna tofauti katika hilo.

Al-Qurtuby amesema: “Wamekubaliana kuwa ni sunna kukusanya kati ya Adhuhuri na Al-Asr wakati wa Adhuhuri uwapo Arafa, na kati ya Magharibi na Isha wakati wa Isha uwapo Muzdalifa, huku wakitofautiana kuhusu kukusanya sehemu nyingine zisizo hizo mbili.1

Ibnu Quddama amesema: “Al-Hasan na Ibnu Sirin na watu wa rai wote wamesema: “Hairuhusiwi kukusanya isipokuwa siku ya Arafa uwapo Arafa, na usiku wa Muzdalifa uwapo Muzdalifa."2

Amepokea Muslim toka kwa Jabir bin Abdillah kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu alikaa miaka tisa bila kuhiji, kisha akawatangazia watu mwaka wa kumi kuwa Mtume (s.a.w.w.) atahiji, hivyo watu wengi wakaenda Madina huku wote wakitaka waongozwe na Mtume na wafanye kama atakavyofanya.

Akaendelea mpaka akasema - mpaka alipofika Arafa akakuta quba limepambwa kwa madoa, akashuka hapo mpaka jua lilipopinduka, akaamrIsha aletewe ngamia, akaondoka mpaka alipofika ndani ya bonde akatoa hotuba - akaendelea mpaka akasema - kisha akaadhini na akakimu, akaswali Sala ya Adhuhuri, kisha akakimu akaswali Sala ya Al-Asr wala hakuswali chochote baina ya hizo mbili, - akaendelea mpaka akasema - akaenda mpaka akafika Muzdalifa, hapo akaswali Sala ya Magharibi na Isha kwa adhana moja na iqama mbili wala hakufanya tasbihi yoyote baina ya Sala hizo mbili.3

Kwa kuwa suala hili ni jambo linalokubalika kwa Waislamu wote basi tutafupIsha kwa kiasi hiki.
________________________
1. Bidayatul-Mujtahid Juz. 1 / Uk. 170 chini ya anuani: sehemu ya pili kuhusu kukusanya Sala.

2. Al-Mughny: Juz. 2, Uk. 112.

3. Sahih Muslim: Juz. 4, uk. 39 - 42 mlango: Hija ya Mtume.
Wanazuoni wengi wa Kiislamu wamekubaliana kuhusu kukusanya Sala mbili safarini isipokuwa Al-Hasan, An- Nakhai, Abu Hanifa na jamaa zake wawili. Hivyo inaruhusiwa kukusanya kati ya Adhuhuri na Al-Asr kwa kutanguliza kwa kuziswali wakati wa Sala ya mwanzo, na kwa kuchelewesha kwa kuziswali wakati wa Sala ya pili, hii ni kwa wote isipokuwa kwa hao tu.

Na Magharibi na Isha wakati mmoja kwa kuzitanguliza na kuzichelewesha.

Sala zinazokusanywa ni: Adhuhuri na Al-Asr, Magharibi na Isha katika wakati wa mojawapo ya hizo, huitwa kuku- sanywa hizo Sala za mwanzo Jam’u taqdiim, (kwa kutanguliza), na katika nyakati za Sala za pili huitwa Jam’u taakhiri (kukusanya kwa kuchelewesha).

As-Shaukani ametaja kauli mbali mbali kuhusiana na suala hili kwa namna ifuatayo: Wanazuoni wengi wa sheria wameruhusu kukusanya safarini kwa hali yoyote kwa kutanguliza na kuchelewesha, na kauli hii ndio ya maswahaba wengi na wanafunzi wa maswahaba na wanazuoni wa sheria huku miongoni mwao ni: At-Thaury, As-Shafy, Ahmad, Is’haqa na As- Shahaby.

Wengine wakasema: “Hairuhusiwi kukusanya kwa hali yoyote ile isipokuwa Arafa na Muzdalifa. Na hii ndiyo kauli ya Al-Hasan, An-Nakhai, Abu Hanifa na wenzake wawili.

Al-Laythu amesema: “Na kauli hii ni mashuhuri toka kwa Malik kuwa kukusanya kunamuhusu yule tu mwenye haraka na safari."

Ibnu Habibu amesema: “Kunamhusu mwenye kutembea." Al-Awzay amesema: “Hakika kukusanya safarini kunamhusu mwenye udhuru.”

Ahmad amesema: Inaruhusiwa kukusanya kwa kuchelewesha (taakhiri) na wala si kwa kutanguliza (taqdiim). Kauli hii ndio chaguo la Ibnu Hazm nayo imepokewa toka kwa Malik.

Hizi ndizo kauli sita: Hivyo ikiwa suala kwa ufupi wamekubaliana wote isipokuwa wachache kama ulivyowaona, basi ni lazima tujadili suala hili sehemu mbili:

Je? Kukusanya kunamhusu tu yule mwenye haraka na safari.

Je? Inaruhusiwa kukusanya kwa kuchelewesha tu wala hakujumuishi kukusanya kwa kutanguliza?

Ama sehemu ya kwanza tunasema, habari zinazoonyesha kitendo cha Mtume (s.a.w.w) ziko katika makundi maw- ili: Kundi moja linaweka wazi kuwa alikuwa akikusanya awapo na haraka na safari, au aharakishwapo na safari:

Ameandika Muslim toka kwa Nafiu toka kwa Ibnu Umar kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa akikusanya kati ya Magharibi na Isha awapo na haraka na safari.1

Ametoa Muslim toka kwa Salim, toka kwa baba yake: “Nilimuona Mtume wa Mwenyezi Mungu akikusanya kati ya Magharibi na Isha awapo na haraka na safari."

Ametoa Muslim toka kwa Salim bin Abdallah kuwa baba yake alisema: “Nilimuona Mtume wa Mwenyezi Mungu anapokuwa na haraka ya safari, akichelewesha Sala ya Magharibi mpaka anapokuja kuikusanya na Sala ya Isha.”2

Ametoa Muslim toka kwa Anas toka kwa Mtume kuwa aharakishwapo na safari huchelewesha Adhuhuri mpaka mwanzo mwa wakati wa Al-Asr hivyo huzikusanya pamoja, na huchelewesha Magharibi mpaka anapokuja kuikusanya na Isha pindi mawingu mekundu yanapozama.3

Kundi la pili linaonyesha kitendo cha Mtume wa Mwenyezi Mungu bila sharti lolote (iwapo ana haraka na safari).

Ametoa Muslim toka kwa Anas bin Malik amesema: “Iwapo Mtume akianza safari kabla ya kupinduka jua alikuwa akichelewesha Adhuhuri mpaka wakati wa Al-Asr, kisha hushuka na kuzikusanya pamoja. Na iwapo jua litapinduka kabla ya safari, basi huswali Adhuhuri kisha hupanda kipando.4

Ametoa Muslim toka kwa Anas amesema: “Ilikuwa Mtume akitaka kukusanya kati ya Sala mbili safarini basi huchelewesha Adhuhuri mpaka mwanzoni mwa wakati wa Al-Asr kisha huzikusanya pamoja.5

Abu Daud na Tirmidhy wamepokea toka kwa Maadh bin Jabal kuwa: “Mtume alikuwa katika vita vya Tabuk anapotaka kusafiri kabla ya kupinduka kwa jua akachelewesha Adhuhuri mpaka akaja kuikusanya na Al-Asr pamoja, na anapotaka kusafiri baada ya kupinduka jua, huswali Adhuhuri na Al-Asr pamoja kisha huondoka, na ilikuwa akitaka kuondoka kabla ya Magharibi, huichelewesha Magharibi mpaka aiswali na Isha pamoja, na ilikuwa akitaka kuondoka baada ya Magharibi huitanguliza Isha na kuiswali na Magharibi pamoja.6

Ahmad amepokea ndani ya Musnad yake toka kwa Abbas` (r.a.) toka kwa Mtume kuwa Mtume akiwa na safari alikuwa kabla ya kupanda kipando hukusanya Sala za Adhuhuri na Al-Asr iwapo jua limepinduka akiwa nyumbani kwake.

Na iwapo halijapinduka akiwa nyumbani kwake, basi huondoka mpaka unapofika wakati wa Al-Asr ndipo hushuka kisha hukusanya Adhuhuri na Al-Asr.

Na iwapo Magharibi itaingia akiwa nyumbani kwake basi hukusanya Magharibi na Isha pamoja, na iwapo Magharibi haijaingia akiwa nyumbani kwake huondoka mpaka Isha inapoingia ndipo hushuka na kuzikusanya pamoja.7

Baada ya As-Shaukany kunukuu riwaya hii akasema: Shafy amepokea riwaya hii katika Musnad yake kwa namna yake akasema: “Na akiondoka kabla jua halijapinduka huchelewesha Adhuhuri mpaka aje aikusanye na Al- Asr wakati wa Al-Asr 8

Nasema: Kanuni ni kuchukuwa chenye sharti maalumu na kukitanguliza kabla ya kisicho na sharti maalumu, hivyo kuziwekea riwaya zisizo na sharti maalum lile sharti maalum lililomo kwenye riwaya zenye sharti maalumu, ndio maana hata Anas kanukuu kitendo cha Mtume bila ya kuwa na sharti maalumu na mara nyingine kikiwa na sharti maalumu. 9

Naongeza kuwa riwaya zinazoonyesha kitendo cha Mtume ni dalili ya ufahamu si tamko la Mtume, na suala linapokuwa hivi linakuwa halina sifa ya kuwa au kutokuwa sharti, kwa sababu hali hii ya kuwa au kutokuwa sharti ni hali ya tamko si ya kitendo, na wala katika suala hili hakuna tamko lolote lililopokewa toka kwa Mtume bali ni kitendo alichokinukuu mpokezi, na huenda kitendo chake hiki kilikuwa kimekutana na hali ya kuwa na haraka na safari, na ikawa mpokezi hakutaja hali hii kwa kutegemea kuwa haihusiki na hukumu.

Kutokana na haya maelezo hakusanyi isipokuwa anapokuwa na haraka na safari. Na inawezekana ndilo aliloliashiria Ibnu Rushdi aliposema: “Kukusanya kumenukuliwa kwa kitendo tu.” 10

Na kinachoweza kuipa nguvu kauli ya pili (bila sharti maalum) ni kuwa sharti lililopo katika riwaya hizi (iwapo ana haraka na safari) ni miongoni mwa masharti yatokanayo na hali ya mara kwa mara, masharti ambayo huwa hayafahamiki kama sharti, hiyo ni mfano wa kauli ya Mwenyezi Mungu: “Na binti zenu wa kambo walio katika ulinzi wenu, waliozaliwa na wake zenu mliowaingilia”11

Hakika binti wa kambo ameharamishwa, sawa awe katika ulinzi wa mwanaume au hapana, lakini mara nyingi mwanamke anapoolewa huenda na binti yake kwa mume wa pili.

Kwa ajili hiyo binti yeyote wa kambo ni haramu bila sharti lolote sawa awe katika ulinzi wa mwanaume au hapana.
________________________
1. Sahih Muslim, Juz. 2, uk. 150 Kitabu cha Sala. Mlango: Ruhusa ya kukusanya Sala mbili safarini. Mlango wa Sala.

2. Sahih Muslim, Juz. 2, uk. 150 Kitabu cha Sala. Mlango: Ruhusa ya kukusanya Sala mbili safarini. Mlango wa Sala.

3. Sahih Muslim Juz. 2 Uk. 151 Kitabu cha Sala. Mlango: Ruhusa ya kukusanya Sala mbili safarini. Mlango wa Sala

4. Sahih Muslim, Juz. 2, Uk. 151 Kitabu cha Sala. Mlango: Ruhusa ya kukusanya Sala mbili safarini. Mlango wa Sala

5. Sahih Muslim, Juz. 2 Uk. 151 Kitabu cha Sala. Mlango: Ruhusa ya kukusanya Sala mbili safarini. Mlango wa Sala

6. Sunan Abi Daud: Juz. 2, uk. 8 Kitabu cha Sala mlango: Kukusanya Sala mbili. Hadithi ya 1220

7. Musnad Ahmad bin Hambal: Juz 5 Uk. 241, Sunan Abi Daud: Juz. 2, uk. 2 kitabu cha Sala mlango: Kukusanya kati ya Hadithi mbili 1220

8. Naylul-Awtwar: Juz. 3, Uk. 213

9. Bidayatul-Mujtahid: Juz. 1, Uk. 173 Chapa nyingine iliyohakiki- wa: Juz. 2, Uk. 374.

10. Bidayatul-Mujtahid: Juz. 1, Uk. 173 Chapa nyingine iliyohakiki- wa: Juz.2 Uk. 374

11. Nisaa; 4: 23
Jambo lililo mashuhuri ni kuwa inaruhusiwa kukusanya kati ya Magharibi na Isha kwa ajili ya udhuru kinyume na Hanafiyya ambao hawajaruhusu kukusanya kwa hali yoyote ile isipokuwa msimu wa Hijja uwapo Arafa au Muzdalifa.

Ama wanaoruhusu kukusanya nao wametofautiana kwa namna zifuatazo:

Je ruhusa inahusu mvua tu au inajumuisha udhuru mwingine?

Je ruhusa inahusu Magharibi na Isha au inajumuisha Adhuhuri na Al-Asr?

Je ruhusa inahusu kukusanya kwa kutanguliza tu au inajumuisha kukusanya kwa kuchelewesha?1

Yafuatayo ni maneno yao kuhusu sura hizo tatu: Ya kwanza: Dhahiri toka kwa Shafy ni kuwa ruhusa inahusu mvua tu.

As-Shiraziy amesema: “Inaruhusiwa kukusanya Sala mbili katika hali ya mvua. Hairuhusiwi kukusanya kwa ajili ya hali ya upepo mkali, tope, ugonjwa na giza."2

(1). Ibnu Rushdi amesema: “Shafi ameruhusu kukusanya usipokuwa safarini kwa ajili ya mvua, mpaka aliposema ama kukusanya kwa ajili ya ugonjwa usipokuwa safarini ni kuwa Malik ameruhusu iwapo atahofia kuzimia au ana ugonjwa wa tumbo, lakini Shafy kakataza hilo.3 (2). Akasema ndani ya kitabu As-Sharhul-Kabiru kuwa: Na je ni ruhusa hilo - kinyume na mvua - kwa ajili ya tope na upepo mkali wenye baridi, au kwa mwenye kuswalia nyumbani au msikitini huku njiani kuna mvua nyingi.4

Ya pili: Yaani je ruhusa inahusu Magharibi na Isha tu au inajumuisha Adhuhuri na Al-Asr? Ibnu Rushdi amesema: “Shafy ameruhusu kukusanya usipokuwa safarini kwa udhuru wa mvua usiku au mchana, ama Malik yeye ameruhusu usiku akakataza mchana.5

An-Nawawy amesema: “Shafy na jamaa wamesema inaruhusiwa kukusanya Adhuhuri na Al-Asr, Magharibi na Isha katika hali ya mvua. Imam wa haramaini akaeleza kuwa inaruhusiwa kukusanya Magharibi na Isha wakati wa Magharibi, wala hairuhusiwi kati ya Adhuhuri na Al- Asr, na haya ndio madhehebu ya Malik.

Al-Mazny amesema: “Hairuhusiwi kwa hali yoyote. Madhehebu ya kwanza ndiyo yanayotokana na maelezo ya Shafy, ya zamani hadi mapya.”6

Ya tatu: Yaani ruhusa inahusu kukusanya kwa kutanguliza bila kujumuisha kukusanya kwa kuchelewesha.

A-Shirazy amesema: “Ni ruhusa kukusanya Sala mbili katika hali ya mvua katika wakati wa Sala za kwanza, na je inaruhusiwa kuzikusanya katika wakati wa Sala za pili?" Hapa kuna kauli mbili: Shafy amesema ndani ya Al-Imlau: “Inaruhusiwa kwa sababu ni udhuru unaoruhusu kukusanya katika wakati wa Sala ya mwanzo hivyo ikaruhusiwa kukusanya katika wakati wa Sala ya pili kama kukusanya kwa safarini.

Akasema katika Al-ummu: “Hairuhusiwi kwa sababu iwapo akichelewesha huenda mvua ikakatika hivyo akawa kakusanya bila udhuru."7

Huu ni ufupi wa kauli katika nukta hizi tatu. Pia wao wana tofauti katika sehemu nyingine ambazo hakuna haja ya kuzitaja.

Baada ya kutambua hilo la muhimu ni kuwepo dalili juu ya ruhusa ya kukusanya kwa udhuru usipokuwa safarini.

Wamethibitisha hilo kwa Hadithi mbili:Inayoonyesha kuwa inaruhusiwa kukusanya usipokuwa safarini katika hali yoyote ile, hivyo wakaichukulia katika hali ya mvua au udhuru wowote ule.

Bukhari ametoa toka kwa Ibnu Abbas` (r.a.) kuwa Mtume aliswali Madina rakaa saba na rakaa nane, yaana Adhuhuri na Al-Asr, Magharibi na Isha.8

Ibnu Rushdi amesema: “Ama kuhusu kukusanya usipokuwa safarini bila udhuru wowote ni kuwa Malik na wanazuoni wengi hawaruhusu, lakini hilo limeruhusiwa na wengi kati ya kundi la dhahiri na Ash’habu ambaye ni kati ya wafuasi wa Malik.

Sababu kubwa ya kutofautiana kwao ni tofauti yao kuhusu ufa- hamu wa Hadithi ya Ibnu Abbas`, hivyo wapo waliy- oitafsiri kuwa ilikuwa ni katika hali ya mvua kama alivyosema Malik, na wapo walioichukulia kuwa ni hali yoyote. Aliyoipokea Ibnu Abbas` kuwa Mtume alikusanya Adhuhuri na Al-Asr na kati ya Magharibi na Isha Madina bila ya hofu, safari wala mvua. Akaulizwa Ibnu Abbas: Alitaka nini katika hilo? Akasema: “Alitaka asiutaabishe umma wake.”9

Dhahiri inaonyesha kuwa kukusanya wakati wa hali ya mvua ni jambo lililokuwa linajulikana kabla, ndio maana Ibnu Abbas` alijaribu kubainisha kuwa kukusanya huku hakukuwa ni kwa lengo la mvua au nyudhuru nyingine bali ilikuwa ni msamaha kwa lengo la kutokuutaabisha umma wake.

Hivyo ikiruhusiwa kukusanya katika hali isiyo ya safari kwa udhuru wowote, basi kukusanya safarini bila udhuru wowote itakuwa ni hiyari kati ya hukumu za safari. Kwa sababu msafiri atakusanya Sala mbili safarini bila udhuru.

Ama yule asiye safarini yeye atakusanya kwa ajili ya udhuru au kwa lengo lingine. Ama tukisema kuwa inaruhusiwa kukusanya bila udhuru wowote usipokuwa safarini, basi haitakuwa kukusanya kati ya Sala mbili ni kati ya hukumu za safari.

Mpaka hapa maneno yametimia kuhusu sura ya tatu, hivyo imebakia sura ya nne.
________________________
1. Tuliyoyataja ni vichwa vya tofauti zao, lakini matawi yake ni mengi hatuna haja ya kuyaingilia

2. Al-Majmuu: Juz. 4, Uk. 258, Kifungu cha matni

3. Bidayatul-Mujtahid: Juz. 1, Uk. 173-174 mahali pawili

4. Al-Mughni, Juz. 2, Uk. 118

5. Bidayatul-Mujtahid, Juz. 1, Uk. 173

6. Al-Majmuu: Juz. 4, Uk. 260

7. Al-Majmuu: Juz, 4. Uk. 258

8. Katika sura ya nne utaona vyanzo vya riwaya hizi.

9. Katika sura ya nne utaona vyanzo vya riwaya hizi.
Imamiyya wameafikiana kuwa inaruhusiwa kukusanya Sala mbili bila ya udhuru wowote pasipo safarini, japokuwa kutenganisha ni bora.

Sheikh Tusi amesema: “Inaruhusiwa kukusanya Sala mbili kati ya Adhuhuri na Al-Asr na kati ya Magharibi na Isha, uwapo safarini au usipokuwa safarini na katika hali yoyote ile. Wala hakuna tofauti kati ya kukusanya wakati wa Sala ya mwanzo au wakati wa Sala ya pili.

Kwa sababu wakati wa baada ya kupinduka jua ni wakati wa kushirikiana, na wakati wa baada ya Magharibi ni wakati wa kushirikiana pia kama tulivyobainisha.1

Hakika upande wa madhehebu ya Imamiyya haina maana kuwa kukusanya Sala mbili ni kuiswali Sala nje ya wakati wake wa kisheria, bali muradi wake ni kuiswali katika muda usiyo wa ubora. Hivyo ufuatao ni ufafanuzi wa madhehebu yenyewe:

Kutokana na maelezo toka kwa Maimamu wa Ahlul-Bayt Imamiyya wamesema kuwa jua likipinduka basi umeingia wakati wa Sala mbili, yaani wakati wa Adhuhuri na Al-Asr, isipokuwa Sala ya Adhuhuri huswaliwa kabla ya Al-Asr, hivyo wakati uliyopo kati ya kupinduka jua na kuzama kwake ni wakati wa kushirikiana kati ya Sala mbili hizo.

Isipokuwa muda wa kutosha rakaa nne kabla ya kuzama kwa jua ni muda mahususi kwa ajili ya Sala ya Adhuhuri, na muda wa kutosha rakaa nne mwishoni mwa wakati ni wakati mahususi kwa ajili ya Sala ya Al-Asr, na muda uliyopo kati ya nyakati hizo mbili ni wakati wa kushirikiana kati ya Sala mbili.

Hivyo akiswali Sala ya Adhuhuri na Al-Asr katika muda wowote kati ya kupinduka jua na kuzama kwake atakuwa kaswali Sala hizi ndani ya wakati wake, kwa sababu ni wakati wa kushirikiana kati ya Sala mbili hizo. Isipokuwa muda wa kutosha kuswali rakaa nne toka mwanzo wa wakati ni mahususi kwa ajili ya Adhuhuri hivyo haisihi kuswali Al-Asr humo.

Na muda wa kutosha kuswali rakaa nne mwishoni mwa wakati ni mahususi kwa ajili ya Al-Asr hivyo haisihi kuswali Adhuhuri humo.

Hii ndio hali halisi ya madhehebu, kwa ajili hiyo mwenye kukusanya Sala mbili nje ya wakati mahususi ametekeleza faradhi ndani ya wakati wake, hivyo Sala yake inakuwa ni kutekeleza (ndani ya wakati) na wala si kulipa.

Hivyo ni kuwa kila Sala ukiachilia mbali wakati wake wa kusihi bado ina wakati wake wa ubora. Hivyo wakati wa ubora wa Sala ya Adhuhuri ni kuanzia kupinduka kwa jua mpaka kivuli cha kitu kilichosimama kufikia urefu wa kipimo cha kitu chenyewe, baada ya kile kivuli cha mwanzo cha kabla ya kupinduka jua kuwa kimeondoka au kimetoweka.

Na mashuhuri ni kuwa wakati wa ubora wa Al-Asr ni kuanzia pale kivuli kinapolingana na kipimo mpaka pale kinapokuwa mara mbili ya kipimo husika.

Kwa wakati wa Magharibi na Isha hujulikana kuwa likizama jua zimeingia nyakati mbili mpaka nusu ya usiku.

Wakati wa mwanzo ni mahususi kwa ajili ya Magharibi kwa muda wa kutimiza Sala nzima, na wakati wa mwisho ni mahususi kwa Isha kwa muda wa kutimiza Sala nzima, na wakati uliyopo kati ya muda huo ni wakati wa kushirikiana.

Hivyo kila Sala kati ya Sala mbili hizi ina wakati wa ubora. Wakati wa ubora wa Magharibi ni kuanzia kuzama kwa jua mpaka kuondoka kwa wekundu wa Magharibi, na wakati wa ubora wa Isha ni kuanzia kuondoka kwa wekundu wa Magharibi mpaka theluthi ya usiku.2

Mara nyingi anayewashangaa Imamiyya kukusanya kati ya Sala mbili hudhani kuwa mwenye kukusanya huswali moja ya Sala mbili nje ya wakati wake, lakini amesahau kuwa mwenye kuswali huwa ameiswali nje ya wakati wa ubora lakini huwa ameiswali ndani ya wakati wa kusihi, na wala si ajabu Sala kuwa na nyakati tatu.

Ya kwanza: Wakati mahususi ni ule wa kutosha rakaa nne mwanzoni mwa kuingia wakati, na wakati wa mwisho ni pale unapokaribia kwisha wakati. Au rakaa tatu baada tu ya kuzama jua na rakaa nne kabla kidogo ya nusu ya usiku.

Ya pili: Wakati wa ubora ambao tayari maelezo yake yameshatangulia kuhusu Adhuhuri na Al-Asr, Magharibi na Isha.

Ya tatu: Wakati wa kusihi ambao ni wakati wote uliyopo kati ya vipimo viwili isipokuwa ule tu uliyo mahususi kwa moja ya Sala mbili, hivyo wakati wa kusihi unaju- muisha wakati wa ubora na ule wa baada ya ubora.

As-Swaduq amepokea kwa isnadi yake toka kwa Zararatu toka kwa Abu Jafar (a.s.) alisema: “Jua likipinduka umeingia wakati wa Sala mbili: Adhuhuri na Al-Asr.

Na jua likizama umeingia wakati wa Sala mbili: Magharibi na Isha ya mwisho.”3

Shekhe Tusi amepokea toka kwa Ubaydu bin Zararatu alisema: “Nilimuuliza Aba Abdillah kuhusu wakati wa Adhuhuri na Al-Asr. Akajibu: “Jua likipinduka umeingia wakati wa Adhuhuri na Al-Asr isipokuwa hii inakuwa kabla ya hii, kisha wewe unakuwa katika wakati ambao ni wa sala zote mbili mpaka jua lizame.”4

Riwaya zenye maana hii ni nyingi lakini sisi tunaishia hapa.

Hivyo ikiwa Sala zina nyakati tatu kama tulivyobainisha basi inatubainikia kuwa kukusanya si jambo baya isipokuwa kinachokupita ni wakati wa ubora wala si wakati asili wa Sala, kwa ajili hiyo imepokewa toka kwa Maimamu wa Ahlul-Bayt kuwa kutenganisha ni bora kuliko kukusanya, hivyo hapa tutataja baadhi ya riwaya zinazoruhusu kukusanya ili tupate baraka tu kwani suala hili kwenye fiqhi ya shia Imamiyya ni suala la wazi sana.

Amepokea As-Saduqu toka kwa Abdallah bin Sanani toka kwa Swadiq (a.s.) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu alikusanya Adhuhuri na Al-Asr kwa adhana moja na iqama mbili, na akakusanya Magharibi na Isha kwa adhana moja na ikama mbili, bila ya kuwa safarini na bila ya udhuru wowote.5

Pia amepokea toka kwa Is'haqa bin Ammar toka kwa Aba Abdillah alisema: “Hakika Mtume aliswali Adhuhuri na Al-Asr sehemu moja bila ya udhuru wala sababu yoyote. Umar akauliza: “Je kuna kitu kimezuka ndani ya Sala?” Akajibu: “Hapana isipokuwa nimetaka kuupa nafuu umma wangu.”6

Kulayny ametoa toka kwa Zararatu toka kwa Aba Abdillah amesema: “Mtume aliwaswalisha watu jamaa Adhuhuri na Al-Asr baada ya kupinduka jua bila ya udhuru wowote, na aliwaswalisha jamaa Magharibi na Isha kabla ya kuondoka wekundu wa Magharibi bila ya udhu- ru wowote, hakika alifanya hivyo ili aupe umma wake nafuu ya wakati.7

Na kuna riwaya nyingi ambazo amezikusanya shekhe Al- Hurru AlAamily ndani ya kitabu chake Wasailul-Shia. 8

Mpaka hapa umebainika mtazamo wa Shia Imamiyya kuhusu kukusanya Sala mbili.
________________________
1. Al-Khilafu: Juz. 1 Uk. 588 mas'ala ya 351 Huko mbele utaona jinsi wakati ulivyobainishwa

2. Angalia Al-Ur'watul-Wuthqa: Uk. 171. Kipengele cha nyakati za Sala

3. Al-Faqihi: Juz. 1 Uk. 140. Pia inapatikana kwenye Hadithi ya 1 mlango wa 17

4. At-Tahadhibu: Juz. 2, uk. 26

5. Al-Faqihi: Juz. 1, Uk. 186 namba 886

6. Ilalul-Sharaiu: 321 mlango wa 11

7. Al-Kafiy: Juz. 3 Uk. 286 Hadithi ya 1

8. Al-Wasailu: Juz.4 Uk. 220-223 mlango wa 32 kati ya milango ya nyakati.
Huenda mtu asiyejua akadhani kuwa mgawanyo huu wa nyakati unahusu fiqhi ya Imamiyya tu, bali ni kuwa mgawanyo huu wa nyakati katika aina tatu unahusu fiqhi zote mbili japokuwa kunatofauti kuhusu muda wa wakati.

Ndani ya Sharhul-Muhadhabu An-Nawawiy amesema: “Tawi: Adhuhuri ina nyakati tatu: Wakati wa ubora, wakati wa hiyari na wakati wa udhuru, hivyo wakati wa ubora ni mwanzoni mwa wakati, na wakati wa hiyari ni baada ya wakati wa ubora mpaka mwisho wa wakati, na wakati wa udhuru ni wakati wa Al-Asr kwa mwenye haki ya kukusanya kwa ajili ya safari au mvua.”

Kisha akasema: Al-kadhi Huseini amesema: “Adhuhuri ina nyakati nne: Wakati wa ubora, wakati wa hiyari, wakati wa ruhusa, na wakati wa udhuru. Hivyo wakati wa ubora ni pale kivuli cha kitu kilichosimama kitakapofikia robo ya kipimo cha kitu hicho, na wakati wa hiyari ni kitakapofikia nusu yake, na wakati wa ruhusa ni kitakapolingana kivuli na hicho kitu na hapo ndio mwisho wa wakati.

Na udhuru ni wakati wa Al-Asr kwa mwenye kukusanya kwa ajili ya safari au mvua.1
________________________
1. Al-Majmuu Juz.3 Uk. 27
Pia wapo wanaoafikiana na Imamiyya katika baadhi ya nukta za suala hili.

An-Nawawy amenukuu kwa kusema: Atwau na Tausi wamesema: “Kivuli cha kitu kikilingana na kitu chenyewe hapo umeingia wakati wa Al-Asr na ufuatao ni wakati wa Adhuhuri na Al-Asr kwa kushirikiana mpaka jua litakapozama.

Kauli hii inahusu Adhuhuri kwa kivuli cha kitu kulingana na kitu husika, kisha inafanya wakati uliobaki ni wa kushirikiana Adhuhuri na Al-Asr mpaka jua litakapozama. Kauli hii inakaribiana na ile ya Imamiyya.

Malik amesema: “Kivuli kikilingana na kipimo cha kitu kilichosimama ndio mwisho wa wakati wa Adhuhuri na mwanzo wa wakati wa Al-Asr kwa kushirikiana. Hivyo kivuli kikizidi kipimo ziada ya wazi basi wakati wa Adhuhuri umekwisha.1

Kauli hii inafanya sehemu ya wakati kuwa wakati wa kushirikiana kati ya Adhuhuri na Al-Asr nao ni - baada ya kivuli kulingana na kipimo cha kitu kilichosimama - mpaka kivuli kinapokizidi kipimo hicho kwa ziada ya wazi, ni wakati wa kushirikiana kati ya Adhuhuri na Al- Asr.

Pia imenukuliwa toka kwake kuwa, wakati wa Adhuhuri unaendelea mpaka kuzama kwa jua.2

Na kuna kauli nyingine ambazo zina namna fulani ya muafaka na fiqhi ya Imamiyya.
________________________
1. Al-Majmuu, Juz. 3, Uk. 24

2. Al-Majmuu, Juz. 3, Uk. 27
Japokuwa kukusanya Sala bila udhuru ni kati ya mambo ya wazi katika fiqhi ya Imamiyya lakini suala hili si mahususi kwa Imamiyya peke yao bali kuna baadhi ya wanazuoni wa sheria wa kisunni wameafikiana nao katika suala hili.

Ibnu Rushdi amesema: “Ama kukusanya bila udhuru usipokuwa safarini hakika Malik na wanazuoni wengi wa sheria hawaruhusu, lakini wameruhusu hilo baadhi ya jamaa katika watu wa Dhahir na Ash'habu katika wafuasi wa Malik. Na sababu ya kutofautiana kwao ni tofauti yao kuhusu kuifahamu hadith ya Ibnu Abbas, hivyo wapo walioifafanua kuwa ilikuwa kwa sababu ya safari, na wapo walioichukulia katika hali yoyote ile.

Muslim katika Hadithi yake ameondoa kauli: ‘Bila ya hofu wala safari wala mvua.’ Hili ndilo waliloshikilia watu wa Dhahir.1

An-Nawawy amesema: Tawi: “Kuhusu madhehebu yao kuna kukusanya bila hofu, safari, mvua, wala ugonjwa. Madhehebu yetu (ya Shafy) na madhehebu ya Abu Hanifa, Malik, Ahmad, na jamuhuri ni kuwa hairuhusiwi.

Ibnu Al-Mundhir ameelezea kuhusu kundi linaloruhusu bila udhuru wowote. Akasema: Ibnu Sirin ameruhusu kwa ajili ya haja maalum au asipochukulia kama mazoea.2

Kwa namna yoyote ile la muhimu ni dalili si kauli, hivyo iwapo kauli zitaafikiana na dalili basi ni vizuri, na kama si hivyo basi marejeo ya mwisho ni dalili.
________________________
1. Bidayatul-Mujtahid, Juz. 2, Uk. 374 chapa iliyohakikiwa

2. Al-Majumuu, Juz. 4, Uk. 264
Mwenyezi Mungu amesema: “Simamisha Sala jua linapopinduka, mpaka giza la usiku na Qur'ani ya alfajiri. Hakika Qur'ani ya alfajiri inashuhudiwa” 1

Aya imebeba jukumu la kubainisha nyakati za Sala tano, hivyo iwapo tukisema makusudio ya giza la usiku ni nusu ya usiku basi wakati uliyopo kati ya kupinduka kwa jua na giza la usiku utakuwa wa Sala nne, isipokuwa dalili imeonyesha kuwa wakati wa Adhuhuri na Al-Asr unakomea kwa kuzama jua, hivyo wakati uliopo kati ya kupinduka jua na kuzama jua ni wakati wa kushirikiana kati ya Adhuhuri na Al-Asr.

Kama inavyokuwa wakati uliyopo kati ya kuzama kwa jua mpaka kuingia giza la usiku ni wakati wa kushirikiana kati ya Magharibi na Isha.

Na huenda mtu akafasiri giza la usiku kwa maana ya kuzama jua, hivyo Aya itakuwa imebeba jukumu la kubainisha wakati wa Adhuhuri, Al-Asr na Sala ya alfajiri bila kubainisha Magharibi na Isha. Na maarufu ni tafsiri ya mwanzo.

At-Tabarasiy amesema: “Katika Aya hii kuna dalili ionyeshayo kuwa wakati wa Sala ya Adhuhuri umerefushwa mpaka mwisho wa mchana, kwa sababu Mwenyezi Mungu alifanya wakati wa kuanzia kupinduka kwa jua ambako ndio kugeuka mpaka giza la usiku ni wakati wa Sala nne, isipokuwa Adhuhuri na Al-Asr zinashirikiana katika wakati mmoja nao ni kuanzia kugeuka kwa jua mpaka kuzama kwake.

Na Magharibi na Isha zinashirikiana katika wakati mmoja nao ni kuanzia kuzama kwa jua mpaka giza la usiku. Na Sala ya alfajiri ameitenganisha kwa kusema: ‘Na Qur'ani ya alfajiri’, hivyo Aya inabainisha wajibu wa Sala tano huku ikibainisha nyakati zake.2

Tuliyoyataja ndio maelezo aliyoyatoa Imam Al-Baqir (a.s.) aliposema: “Mwenyezi Mungu alimwambia Mtume wake: ‘Simamisha Sala jua linapopinduka mpaka giza la usiku.’

Hizi ni Sala nne alizozipa majina Mwenyezi Mungu, akazibainisha na kuziwekea nyakati. Na giza la usiku ni nusu ya usiku. Kisha Mwenyezi Mungu akasema:

‘Na Qur'ani ya alfajiri, hakika Qur'ani ya alfajiri inashuhudiwa,’ hii ni Sala ya tano.”3

As-Sadiq (a.s.) amesema: “Ndani ya Aya hiyo kuna Sala mbili mwanzo wa wakati wake ni kupinduka kwa jua isipokuwa hii ni kabla ya hii. Na kuna Sala mbili mwanzo wa wakati wake ni kuzama kwa jua mpaka nusu ya usiku isipokuwa hii ni kabla ya hii.”

Al-Qurtuby amesema: “Kuna watu wameona kuwa wakati wa Sala ya Adhuhuri unaanzia kupinduka kwa jua mpaka kuzama kwake, kwa sababu Mwenyezi Mungu ameuweka wajibu wake kutegemeana na kupinduka kwa jua na wakati wote huu ni kupinduka kwa jua. Kauli hii kaisema kwa upana Al-Awzay na Abu Hanifa. Ama Malik na Shafy wenyewe wameashiria kauli hii wakati wa dharura.4

Ar-Raziy amesema: “Laiti tukitafsiri giza la usiku kwa maana ya kuingia kwa giza la mwanzo, basi ibara giza la usiku itamaanisha mwanzo wa Magharibi, kwa maana hii nyakati zilizotajwa na Aya zitakuwa tatu: Wakati wa kupinduka kwa jua, wakati wa kuanza Magharibi na wakati wa alfajiri.”

Akasema: “Hili linapelekea kupinduka kwa jua kuwe ni wakati wa Adhuhuri na Al-Asr hivyo wakati huu unakuwa ni wa kushirikiana kati ya hizi Sala mbili.

Na mwanzo wa Magharibi uwe ni wakati wa Magharibi na Isha, hivyo uwe ni wakati wa kushirikiana kati ya hizi Sala mbili. Hii inapelekea kuruhusiwa kukusanya katika hali yoyote ile kati ya Adhuhuri na Al-Asr Magharibi na Isha, isipokuwa dalili inaonyesha kuwa kukusanya bila udhuru pasipo na safari hairuhusiwi, hivyo ikalazimika iruhusiwe kukusanya kwa ajili ya udhuru wa safari, mvua na udhuru mwingine.”5

Aliyoyahakiki Ar-Razi katika mada hii ni ukweli mtupu, lakini kuiacha kwake haki kwa hoja ya: ‘Hakika kukusanya bila udhuru wowote pasopo na safari hairuhusiwi kwa kuwa kuna dalili juu ya hilo,’ni dhana tu.

Ni dalili ipi iliyopo inayokataza kukusanya bila udhuru wowote, je, dalili ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu? Huku Kitabu kwa mujibu wa uhakiki wake kinaruhusu kukusanya. Au ni Sunna? Baada ya muda utaona jinsi maelezo ya Sunna yanavyoruhusu.

Lakini pia umeshajua jinsi Masunni walivyosema kuwa inaruhusiwa, zaidi ya hapo ni kuwa Maimamu wa Ahlul- Bayt nao wameruhusu. Hivyo baada ya Kitabu, Sunna na ijmai hakuna hoja nyingine kama ilivyo ‘baada ya Abadan hakuna kijiji kingine.’6
________________________
1. Israa; 17:78

2. Maj'maul-Bayan, Juz. 3, Uk. 434

3. Nuru-Thaqalain, Juz. 3, Uk. 202 Hadith ya 377

4. Al-Jamiu-liah'kamil-Qur'ani, Juz. 1, Uk. 304

5. Tafsirul-Kabir, Juz. 12, Uk. 27

6. Mara ngapi Imam Ar-Razi amehakiki na kuongea lile lililo haki ambalo yeye mwenyewe anastahiki kulifuata lakini huliacha kwa hoja ya kipuuzi. Angalia aliyoyahakiki kuhusu kupaka miguu miwili katika tafsiri ya: “Na mpake vichwa vyenu na miguu yenu mpaka vifundoni.” Na yale aliyozungumza kuhusu makusudio ya “Wenye mamlaka katika ninyi” katika tafsiri ya Aya: “Mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume na wenye mamlaka katika nyinyi". Na sehemu nyingine kama hizi.
Kuna riwaya nyingi zinazodhihirisha haki kuhusu ruhusa ya kukusanya Sala mbili bila udhuru pasipokuwa safarini, riwaya hizo zimepokewa na waandishi wa Sahih sita, Sunan na Masanidi. Hivyo tuanze aliyopokea Muslim kwa sanadi na tamko kisha twende kwenye yale waliyonukuu wengine.

1. Ametuhadithia Yahya mwana wa Yahya amesema: Nilisoma kwa Malik toka kwa Zuberi toka kwa Said bin Jubair toka kwa Ibnu Abbas alisema: ‘Mtume aliswali Adhuhuri na Al-Asr pamoja, Magharibi na Isha pamoja bila ya hofu wala safari.”

2. Ametusimulia Ahmad bin Yunus na Aun bin Salam wote toka kwa Zuhayri, Ibnu Yunus alisema: “Ametusimulia Zuhayri, ametusimulia baba Zuberi toka kwa Saidi bin Jubair toka kwa Ibnu Abbas` alisema: ‘Mtume aliswali Adhuhuri na Al-Asr pamoja Madina pasi na hofu wala safari.’ Baba Zuberi akasema: ‘Nikamuuliza Said, kwa nini alifanya hivyo? Akajibu: Nilimuuliza Ibnu Abbas kama ulivyoniuliza akasema: ‘Alitaka asimpe taabu yeyote katika umma wake.'”

3. Ametusimulia Abu Bakr bin Abi Shaybat na Abu Kuraybi wamesema: Ametusimulia Abu Muawiya na ametusimulia Abu Kuraybi na Abu Said Al-Ashaju (tamko ni la Abu Kuraybi) walisema: ‘Alitusimulia Wakiu wote kutoka kwa Al-A’amash toka kwa Habibu bin Abi Thabit, toka kwa Said bin Jubairi toka kwa Ibnu Abbas alisema: ‘Mtume wa Mwenyezi Mungu alikusanya Adhuhuri na Al-Asr, Magharibi na Isha Madina pasi na hofu wala mvua.’

Katika hadith ya Wakiu amesema: Nikamwambia Ibnu Abbas: Kwanini alifanya hivyo? Akasema: Ili asiupe taabu umma wake. Katika Hadithi ya Abu Muawiya ni kuwa Ibnu Abbas` aliambiwa: Alitaka nini katika hilo?

Akasema: Ili asiupe taabu umma wake.

Ametusimulia Abu Bakr bin Shaybat, ametusimulia Sufiani bin Uyayna toka kwa Amru toka kwa Jabiri bin Zaidi toka kwa Ibnu Abbas alisema: “Niliswali na Mtume wa Mwenyezi Mungu rakaa nane pamoja na saba pamoja.

Nikasema: Ewe baba As-sha’shau, nadhani alichelewesha Adhuhuri na akaharakisha Al-Asr, akachelewesha Magharibi akaharakisha Isha. Akasema: “Na mimi nadhani hivyo.”1

Kama atakusudia kukusanya kwa kimuonekano basi dhana yake si kitu haisaidii haki chochote. Muda si mrefu utakufikia ufafanuzi kuhusu kukusanya kimuonekano.

Ametusimulia Abu Rabiu Az-Zaharany, ametusimulia Hamadi bin Zaid toka kwa Amru bin Dinari toka kwa Jabiri bin Zaid toka kwa Ibnu Abbas kuwa, Mtume aliswali Madina rakaa saba na nane,2 Adhuhuri na Al- Asr, Magharibi na Isha.

Amenisimulia Abu Rabiu Az-Zaharany. Ametusimulia Hamadi toka kwa Zuberi bin Al-Khariti toka kwa Abdallah bin Shaqiqi alisema: “Siku moja Ibnu Abbas alitutolea muhadhara baada ya Al-Asr mpaka lilipokuchwa jua na nyota zikaanza kuonekana.

Watu wakawa wanasema: Sala! Sala! Mara akaja mtu mmoja wa koo ya Bani Tamim huku akisisitiza: Sala! Sala! Ndipo aliposema Ibnu Abbas: “Je unanifundIsha Sunna? Usiye na mama wee! Kisha akasema: ‘Nilimuona Mtume amekusanya Sala ya Adhuhuri na Al-Asr, na Magharibi na Isha.’ Abdallah bin Shaqiqi anasema: ‘Hilo likanitia shaka moyoni mwangu, mara moja nikaenda kwa Abu Huraira nikamuuliza, naye akathibitisha habari ya Ibnu Abbas kuwa ni kweli.”

Ametusimulia Ibnu Abi Omar. Ametusimulia Wakiu. Ametusimulia Amrani bin Hudayri toka kwa Abdallah bin Shaqiq Al-Uqayliy amesema: Mtu mmoja alimwambia Ibnu Abbas: “Sala!” Akanyamaza. Kisha akasema: “Sala!” Akanyamaza. Kisha akasema: “Sala!” Akanyamaza.

Kisha akasema: “Ee usiye na mama we!” Unatufunza Sala ilhali tulikuwa tukikusanya kati ya Sala mbili zama za Mtume wa Mwenyezi Mungu.3

Haya ndiyo aliyoyanukuu Muslim ndani ya Sahih yake. Yafuatayo ni waliyonukuu wengine.

Ametoa Bukhari toka kwa Ibnu Abbas kuwa: “Mtume aliswali Madina saba na nane pamoja, Adhuhuri na Al- Asr, Magharibi na Isha. Ayubu akasema: ‘Huenda alikuwa ndani ya usiku wa mvua.’ Akasema, huenda.”4

Ametoa Bukhari toka kwa Jabiri bin Zaidi toka kwa Ibnu Abbas amesema: “Mtume aliswali saba pamoja na nane pamoja.”5

Ametoa Bukhari kwa kuivusha toka kwa Ibnu Omar na Abi Ayyub na Ibnu Abbas kuwa: Mtume aliswali Magharibi na Isha.6

Ametoa Tirmidhiy toka kwa Saidi bin Jubairy toka kwa Ibnu Abbas alisema: Mtume alikusanya kati ya Adhuhuri na Al-Asr na kati ya Magharibi na Isha Madina pasi na hofu yoyote wala mvua. Akasema: Akaambiwa Ibnu Abbas: ‘Alitaka nini katika hilo?’ Akasema: ‘Alitaka asi- upe taabu umma wake.' Baada ya kunukuu Hadithi hii Tirmidhy akasema: Hadithi ya Ibnu Abbas imepokewa toka kwake na watu zaidi ya mmoja, kaipokea Jabir bin Zaidi, Saidi bin Jubayri, na Abdallah bin Shaqiqi Al- Uqayliy. 7

Imam Ahmad ameitoa toka kwa Qatada amesema: “Nilimsikia Jabir bin Zaidi toka kwa Ibnu Abbas akisema: Mtume wa Mwenyezi Mungu alikusanya kati ya Adhuhuri na Al-Asr, Magharibi na Isha Madina pasipo na hofu wala mvua.’ Ibnu Abbas akaulizwa: ‘Alitaka nini kinyume na hayo?’ Akasema: ‘Alitaka asiupe taabu umma wake.’8

Imam Ahmad ametoa toka kwa Sufiyani amesema Umar: Amenipa habari Jabir bin Zaidi kuwa alimsikia Ibnu Abbas akisema: Niliswali na Mtume wa Mwenyezi Mungu nane pamoja na saba pamoja. Nikamwambia:

‘Ewe Abu Shauthau, nadhani alichelewesha Adhuhuri na akaharakisha Al-Asr, Akachelewesha Magharibi akaharakisha Isha. Akasema: Nami nadhania hivyo.”9

Imamu Ahmad ametoa toka kwa Abdallah bin Shaqiqi alisema: “Siku moja Ibnu Abbas alitutolea muhadhara baada ya Al-Asr mpaka lilipokuchwa jua na nyota zikaanza kuonekana. Watu wakawa wanasema: “Sala! Sala! Alikuwepo mtu mmoja wa ukoo wa Bani Tamimu akaan- za kusema: Sala Sala! Ibn Abbas akaghadhibika akasema: Je unanifundisha Sunna?

Nilimuona Mtume amekusanya baina ya Adhuhuri na Al-Asr, na Magharibi na Isha. Abdallah anasema: Hilo likanitia shaka moyoni mwangu, mara moja nikaenda kwa Abu Huraira nikamuuliza, akalikubali.10

Ametoa Malik toka kwa Saidi bin Jubairy toka kwa Abdallah bin Abbas kuwa alisema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu aliswali Adhuhuri na Al-Asr zote pamoja, Magharibi na Isha zote pamoja pasipo na hofu wala safari.”11

Ametoa Abu Daudi toka kwa Saidi bin Jubairy toka kwa Abdallah bin Abbas` amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu aliswali Adhuhuri na Al-Asr zote pamoja, Magharibi na Isha zote pamoja pasipo na hofu wala safari.

Malik akasema: Mimi naona alifanya hivyo wakati wa mvua.

Abu Daudi ameitoa toka kwa Jabiri bin Zaidi toka kwa Ibnu Abbas alisema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu alituswalisha Madina nane na saba, Adhuhuri na Al-Asr, Magharibi na Isha. Abu Daudi akasema: Ameipokea pia Swaleh bwana wa At-Tauamah toka kwa Ibnu Abbas akasema: ‘Pasipo na mvua.”12

Ametoa An-Nasai toka kwa Saidi bin Jubair toka kwa Ibnu Abbas kuwa: “Mtume wa Mwenyezi Mungu aliswali Adhuhuri na Al-Asr zote pamoja, Magharibi na Isha zote pamoja pasipo na hofu wala safari.”13

Ametoa An-Nasai toka kwa Saidi bin Jubair toka kwa Ibnu Abbas kuwa: Mtume alikuwa akiswali Madina akikusanya kati ya Sala mbili kati ya Adhuhuri na Al-Asr, Magharibi na Isha bila ya hofu wala safari.

Akaambiwa: Kwa nini? Akasema: Ili asiupe taabu umma wake.” (3) Ametoa An-Nasai toka kwa Abi Shauthau toka kwa Ibnu Abbas amesema: “Niliswali nyumma ya Mtume wa Mwenyezi Mungu nane zote pamoja na saba zote pamoja."14

Ametoa An-Nasai toka kwa Jabir bin Zaidi toka kwa Ibnu Abbas kuwa aliswali huko Basra Sala ya mwanzo na Al- Asr bila ya kitu kati yake, na Magharibi na Isha bila ya kitu kati yake. Alifanya hivyo kutokana na shughuli. Na Ibnu Abbas akadai kuwa Aliswali na Mtume wa Mwenyezi Mungu Madina Sala ya mwanzo na Al-Asr sijida nane bila ya kitu kati yake.15

Hafidh Abdu Razaqi toka kwa Daudi bin Qaysi toka kwa Swaleh bwana wa At-Tauamah kuwa alimsikia Ibnu Abbas akisema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu alikusanya kati ya Adhuhuri na Al-Asr, Magharibi na Isha Madina pasipo na safari wala mvua.”

Akasema: ‘Nikamwambia Ibnu Abbas: Unadhani kwa nini alifanya hivyo?’ Akasema: ‘Ninaona ili aupe nafuu umma wake.”16

Ametoa Abdu Razaqi toka kwa Ibnu Abbas amesema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu alikusanya kati ya Adhuhuri na Al-Asr Madina pasipo na safari wala hofu. Akasema: ‘Nikamwambia Ibnu Abbas, unaona ni kwa nini alifanya hivyo?

Akasema: ‘Alitaka asimpe yeyote taabu katika umma wake.”17

Ametoa Abdu Razaqi toka kwa Amru bin Dinari kuwa Aba As-Shauthau alimpa habari kuwa Ibnu Abbas` alimueleza akasema: ‘Niliswali nyuma ya Mtume nane zote pamoja na saba zote pamoja Madina. Ibnu Jarihu akasema: ‘Nikamwambia Abu Shauthau mimi nadhani Mtume alichelewesha Adhuhuri kidogo akatanguliza Al- Asr kidogo. Abu Shaathau akasema: “Na mimi nadhania hivyo.”18

Nasema: Dhana ya Ibnu Jarihu si chochote japo Abu Shauthau ameiafiki, dhana haisaidii haki chochote.

Matokeo yake ni kuwa kukusanya kulikuwa ni kimfano si kihalisi, hivyo tutakubainishia udhaifu wa maana hii ya kukusanya kimuonekano, na kuwa kukusanya kimuonekano kunawajibisha taabu zaidi kuliko kutengan- isha, kwani kujua mwisho wa wakati wa Sala ya mwanzo na mwanzo wa Sala ya pili ni taabu zaidi kuliko kukusanya.

Abdu Razaqi ametoa toka kwa Amru bin Shuaybu toka kwa Abdallah bin Omar amesema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu alitukusanyia bila ya kuwa safarini akakusanya Adhuhuri na Al-Asr.” Mtu mmoja akamwambia Ibnu Omar: “Unaona ni kwa nini Mtume alifanya hivyo.” Akajibu: “Ili umma wake usipate taabu iwapo mtu akikusanya.”19

At-Twahawiy ndani ya kitabu Maanil-athari amesema toka kwa Jabir bin Abdallah: “Mtume wa Mwenyezi Mungu alikusanya kati ya Adhuhuri na Al-Asr, Magharibi na Isha Madina kwa hiyari bila ya hofu wala ila.” 20

Al-Hafidh Abu Naiimu Ahmad bin Abdallah Al-Isfihaniy (aliyefariki mwaka 430 A.H.) ametoa toka kwa Jabir bin Zaidi kuwa Ibnu Abbas alikusanya kati ya Adhuhuri na Al-Asr, na akadai kuwa yeye aliswali na Mtume Madina Adhuhuri na Isha.21

Abu Naiimiy ametoa toka kwa Amru bin Dinari amesema: “Nilimsikia Abu Shauthau akisema: “Ibnu Abbas` amesema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu aliswali rakaa nane zote pamoja, na rakaa saba zote pamoja bila ya ugonjwa wala udhuru."22

Ametoa Al-Bazari ndani ya Musnadi yake toka kwa Abu Hurayra kuwa alisema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu alikusanya kati ya Sala mbili Madina bila ya hofu.”23

At-Tabaraniy ametoa ndani ya kitabu Al-Awsatu na Al- Kabiri toka kwa Abdallah bin Zaid kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu alikusanya Adhuhuri na Al-Asr, Magharibi na Isha. Akaulizwa kuhusu hilo akajibu: “Nimefanya hivyo ili nisiupe taabu umma wangu.” 24

Hizi ni Hadithi thelathini tumezikusanya toka kwenye Sahih Sita, Masnadi na Sunnani.Tumefupisha maneno kwa kutoa riwaya hizi tu ili msomaji ajue kuwa ni Hadithi ambazo wanazuoni wa Hadithi na wakubwa wao wamezitilia umuhimu hivyo wakazihifadhi, na wala mtu hawezi kuzikataa na kuzikanusha. Na kuna riwaya nyingize zaidi ya hizi hatujazitaja kwa ajili ya kufupisha.25

Mtiririko huu wa wapokezi unakomea kwa watu wafuatao:

• Abdallah bin Abbas

• Abdallah bin Omar

• Abu Ayubu Al-Annswariy mwenyeji wa Mtume Madina

• Abu Hurayra Ad-Duusiy

• Jabiri bin Abdillah Al-Answariy

• Abdallah bin Mas'udi.

Riwaya zinaeleza wazi kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu alikusanya Madina kati ya Sala mbili pasipo na hofu, mvua wala sababu yoyote. Alikusanya ili kubainisha ruhusa ya kukusanya na kuwa kufanya hivyo ni sheria. Pia ili mtu asije akadhani kuwa kutenganisha ni lazima kutokana na yeye Mtume kuendelea kuswali ndani ya wakati wa ubora. Hivyo kwa kitendo chake cha kukusanya kimethibitisha kuwa kukusanya ni ruhusa japokuwa kutenganisha ni bora.

Kwa kuwa madhumuni ya riwaya yanapingana na madhehebu za kifiqhi zilizozoweleka hivyo baadhi ya watu wa Hadithi na wanazuoni wa fiqhi wamejaribu kuzilazimisha riwaya zifuate fat'wa za maimamu zao na kufanya fat'wa hizo ndio kipimo cha haki na batili.

Hivyo wengi wao wakaacha kuzitumia riwaya hizi isipokuwa wachache tu ndio waliozitumia wakatoa fat'wa kulingana na madhumuni ya riwaya, hao wametajwa majina yao na Ibnu Rushdi ndani ya kitabu chake Bidayatul-Mujtahidu. Na Wametajwa na An-Nawawiy ndani ya Al-Maj'muu kama ilivyotangulia.

Na kifuatacho ni sababu na nyudhuru walizozitoa waliokhalifu riwaya, nazo ni sababu na nyudhuru dhaifu kuliko nyumba ya buibui.
________________________
1. Kwa alama ya hadith ya tano ni kuwa Mtume alifanya hivyo alipokuwa Madina.

2. Kutaja bila kufuata mpangilio kwani mpangilio ni nane na saba

3. Sherhe ya Sahih Muslim ya An-Nawawiy Juz. 5 Uk. 213-218. Mlango wa kukusanya Sala usipokuwa safarini. Japokuwa huu ni mlango mahususi kwa ajili ya riwaya za kukusanya usipokuwa safarini lakini kanukuu riwaya tatu zinazoonyesha kukusanya Sala mbili safarini hivyo hatujazinukuu. Inawezekana aliziweka riwaya hizi katika mlango huu ili kuonyesha kuwa kukusanya katika hali isiyo ya safari ni vilevile kama unavyokusanya safarini

4. Sahih Bukhari, Juz. 1, Uk. 110 Kitabu cha Sala mlango wa kuchelewesha Sahih Bukhari: Juz.1 Uk. 113, Kitabu cha Sala mlan- go wa wakati wa Magharibi.

5. Sahih Bukhari: Juz.1 Uk. 113 Kitabu cha Sala mlango wa wakati wa Magharibi.

6. Sahih Bukhari: Juz.1 Uk. 113 mlango wa Isha

7. Sunanut-Tirmidhy: Juz.1, Uk. 354 Hadithi namba 187 mlango wa yanayozungumzia kukusanya usipokuwa safarini. Kisha angalia kuwa muhakiki kwenye ufafanuzi kataja njia za upokezi zilizopokea Hadithi hii toka kwa Ibnu Abbas. Pia At-Tirmidhy ana tafsiri isiyokubalika kuhusu Hadithi hii. Utaiona muda wake ukifika.

8. Musnad Ahmad, Juz. 1, Uk. 223

9. Musanad Ahmad Juz.1, Uk. 221 alidhania kuwa alikusudia kukusanya kimuonekano. Dhana hii si hoja hata kwa yeye mwenyewe mdhaniaji. Dhana haisaidii haki chochote

10. Musnad ya Ahmad Juz. 1, Uk. 151

11. Muwatta ya Malik Juz.1, Uk. 144 Hadithi ya 4 mlango wa kuku- sanya Sala safarini na pasipo safari.

12. Rejea iliyopita, Hadith Na, 1214

13. Sunanun-Nasai, Juz. 1 Uk. 290 mlango wa kukusanya Sala mbili usipokuwa safarini.

14. Sunanun-Nasai, Juz.1 Uk. 290 mlango wa kukusanya Sala mbili usipokuwa safarini.

15. Sunanun-Nasai, Juz.1 Uk. 286 mlango: Wakati ambao asiye safarini hukusanya Sala, na makusudio ya sijida

16. -2- Muswanafu Abdu-Razaqi, Juz. 2 Uk. 555-556 Hadithi ya 4434, 4435.

17. 1-2- Muswanafu Abdu-Razaqi, Juz. 2 Uk. 555-556 Hadithi ya 4434, 4435.

18. Muswanafu Abdu-Razaqi: Juz. 2, Uk. 556 Hadithi ya 4436

19. Muswanafu Abdu-Razaqi, Juz. 2 Uk. 556 Hadithi ya 4437

20. Maanil-Athari, Juz.1, Uk. 161

21. Hil-yatul-Awliyai, Juz. 3, Uk. 90 mlango wa Jabir bin Zaid

22. Hulyatul-Awliya, Juz. 3, Uk. 90 mlango wa Jabir bin Zaid

23. Musnadul-Bazari, Juz. 1, Uk. 283 Hadithi namba 412

24. Al-Muujamul-Kabiri Juz.10, Uk. 269 Hadithi ya 10525

25. Angalia Al-Maujamul-Awsatu, Juz. 2, Uk. 94. Kanzul-Ummal, Juz.8 Uk.246-251 namba 22764, 22767, 22771, 22774, 22777, 22778.
Hakika kati ya mambo yanayozisibu riwaya hizi ni wanazuoni wengi wa kisunni kuacha kuzitumia, jambo ambalo linawajibIsha zisiwe na hoja.

Baada ya kutaja Hadithi za kukusanya, Tirmidhiy anasema: Kuzifanyia kazi hizi riwaya kwa masunni ni kutokukusanya kati ya Sala mbili isipokuwa safarini au Arafa.1

Watafiti wengi wa dini wameijibu kauli hii:

a). An-Nawawiy anasema: “Riwaya hizi zimethibiti ndani ya Muslim kama unavyoziona. Na wanazuoni wana tafsiri na madhehebu mbalimbali kuhusu riwaya hizi, na Tirmidhiy mwisho wa kitabu chake amesema: Ndani ya kitabu changu hakuna Hadithi ambayo umma umeafikiana juu ya kuiacha na kutokuifanyia kazi isipokuwa Hadithi ya Ibnu Abbas inayohusu kukusanya Madina bila ya hofu wala mvua, na Hadithi ya kumuua mnywaji wa pombe mara ya nne.”2

Hili alilolisema Tirmidhiy kuhusu Hadithi ya mnywaji wa pombe ndivyo lilivyo, yenyewe ni Hadithi iliyofutwa kwani ijmai imethibitisha hilo. Ama kuhusu Hadithi ya Ibnu Abbas hakuna ijmai inayothibitIsha kuacha kuifanyia kazi, isipokuwa kuna baadhi ya tafsiri ambazo tutaziashiria.3

b). As-Shaukaniy amemjibu At-Tirmidhiy kwa kusema: “Haijifichi kuwa Hadithi ni Sahih, na wala kitendo cha masunni wengi kuacha kuifanyia kazi hakitii dosari usahih wake, na wala hakiwajibishi kuporomoka hoja yake. Baadhi ya wanazuoni wameifanyia kazi kama ilivyotangulia. Japokuwa dhahiri ya maneno ya Tirmidhiy ni kuwa yeye haifanyii kazi lakini wengine wamethibitisha kuifanyia kazi, na kilichothibitishwa hutangulizwa.4

c). Al-Alusiy amesema: “Madhehebu ya kundi la maimamu linaruhusu kukusanya usipokuwa safarini kwa mwenye haja asiyefanya kuwa ni mazowea. Kauli hii ndiyo ya Ibnu Sirini, na Ash'habu mfuasi wa Malik.

Al-Khatabiy Ameinukuu toka kwa Al-Qufali As-Shashiy Al-Kabiru mfuasi wa Imam Shafy, na kutoka kwa Abi Is'haqa Al-Marwaziy na toka kwa jamaa kati ya watu wa Hadithi.

Ibnu Al-Mundhiru amechagua kauli hii, na inaungwa mkono na dhahiri iliyosihi toka kwa Ibnu Abbas` na iliy- opokewa na Muslim kuwa alisema: Mtume wa Mwenyezi Mungu alikusanya kati ya Adhuhuri na Al-Asr, Magharibi na Isha Madina pasipo na hofu wala mvua. Akaambiwa: Kwa nini amefanya hivyo? Akasema: “Hakutaka yeyote apate taabu katika umma wake.”

Inatokana na taabu kwa maana ya uzito hivyo hajatoa sababu ya ugonjwa wala ya kitu kingine. Kutokana na tuliyoyataja inafahamika kuwa kauli ya At- Tirmidhiy mwishoni mwa kitabu chake: Ndani ya kitabu changu hakuna Hadithi ambayo umma umeafikiana juu ya kuiacha na kutokuifanyia kazi isipokuwa Hadithi ya Ibnu Abbas inayohusu kukusanya Madina bila ya hofu wala mvua, na Hadithi ya kumuua mnywaji wa pombe mara ya nne. Inatokana na kutokufanya utafiti .

Ndio! Aliyoyasema kuhusu Hadithi ya pili ni sahih kwani wameeleza wazi kuwa Hadithi hiyo imefutwa na ijmai imethibitisha kufutwa kwake.5

d). Kwa ukosoaji huu imedhihirika kuwa hakuna hali ya kususa kuifanyia kazi Hadithi hii, na huenda masunni wengi hawajatoa fat'wa kulingana na makusudio ya Hadithi hizi kwa sababu ya ubora wa kutenganisha na kuzigawa kwa nyakati.

Lakini ubora huu unapingana na ubora mwingine, nao ni kuwa katika zama zetu hizi kitendo cha kutenganisha kinapelekea watu wengi wenye shughuli kuacha kuswali (kama tunavyoshuhudia kwa macho). Kinyume na kukusanya kwenyewe ambako kunarahisisha kuhifadhi Sala kwa kuziswali, kwa ajili hiyo ubora umegeukia upande wa pili, hivyo ni bora wanazuoni wa sheria wakatoa fat'wa ya kukusanya, na watie wepesi badala ya kutia uzito.

Allah (s.w.t.) anasema: “Mwenyezi Mungu huwatakieni yaliyo mepesi wala hawatakieni yaliyo mazito.”6 “Wala hakuweka juu yenu uzito katika dini.”7 Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwani zipo dalili zina- zoruhusu kukusanya katika hali yoyote, tena ni dalili sahih na za wazi kama ulivyoona, bali ni Kitabu chenye hekima ndio kimebainisha hivyo.8
Hadithi Haielezi Kukusanya Kwa Kutanguliza Au Kwa Kuchalewesha.
Al-Qadhiy Sharafudini Al-Husein bin Muhammad Al- Maghribiy amesema ndani ya kitabu chake Al-Badru At- Tamamu fi sharhu Bulughul-Marami kuwa: “Hakika Hadithi ya Ibnu Abbas haisihi kuwa hoja kwa sababu haiainishi ni kukusanya kwa kutanguliza au ni kwa kuchelewesha, hiyo ni kama ilivyo dhahiri katika riwaya ya Muslim na kuainisha moja kati ya hizo ni kulazimisha.

Hivyo inawajibika kuhama kwenda kwenye lile la wajibu kwa kubakia katika Hadithi za nyakati zinazomjumuisha mwenye udhuru na asiye na udhuru kisha kumuainisha msafiri tu kwa kuthibiti kiainishi.9

Anajibiwa kuwa: Ibnu Abbas hakunukuu namna ya kuku- sanya kwa kuwa jambo lenyewe liko wazi, kwani kukusanya katika hali isiyo ya safari ni sawa na kukusanya katika hali ya safari, hivyo kama inavyoruhusiwa kuku- sanya kwa namna zote mbili uwapo safarini yaani kuku- sanya kwa kutanguliza na kwa kuchelewesha kama maelezo yalivyotangulia ndivyo hivyo hivyo hata usipokuwa safarini.

Kunyamaza kwa Ibnu Abbas na kitendo cha wapokezi kutokumuuliza kuhusu namna ya kukusanya ni dalili kuwa kutokana na maneno yake walifahamu kukusanya si mahususi kwa namna moja tu kati ya namna mbili, kwani laiti isingekuwa hivyo ingewalazimu kuuliza tena: Je, Mtume alikusanya kwa namna ya kutanguliza au kuchelewesha?

Linalounga mkono hilo ni umoja wa sababu iliyopo kwenye maneno ya Ibnu Abbas kwani inapatikana katika namna zote mbili.

Ametoa Muslim toka kwa Ibnu Abbas kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu alikusanya Sala mbili katika safari aliyosafiri katika vita vya Tabuk, hivyo akakusanya kati ya Adhuhuri na Al-Asr, Magharibi na Isha. Said akasema: ‘Nikamwambia Ibnu Abbas kitu gani kilimpelekea kufanya hivyo, akasema: “Alitaka asiupe taabu umma wake.”10

Hivyo kinachoupa nguvu uhusikaji wa namna zote mbili bila tofauti kati ya namna hizo ni kule kuenea kwa sababu nayo ni kuuondolea taabu umma wake, kwani kwa hakika taabu inayopatikana kwa kutenganisha Sala mbili inaondoka kwa kukusanya kwa namna yoyote ile kati ya namna mbili. Sawa iwe kwa kutanguliza au kuchelewesha.

Zaidi ya hapo ni kuwa Ibnu Abbas aliifanyia kazi Hadithi kwa sura ya kukusanya kwa kuchelewesha. Imeshatangulia kuwa Ibnu Abbas siku moja alihutubia baada ya Al-Asr mpaka jua likazama na nyota zika- chomoza; watu wakaanza kusema: ‘Sala! Sala!’ Akaja mtu toka ukoo wa Bani Tamimu akaanza kusisitiza kwa kusema: ‘Sala! Sala!’ Ibnu Abbas akasema: “Je unanifundIsha sunna? Ee usiye na mama we!" Mpaka mwisho wa Hadithi kama ilivyotangulia.

Kwa hakika ndugu msomaji ni kuwa mpinzani alipofika mbele ya riwaya hizi nyingi zinazoruhusu kukusanya dhidi ya kutenganiha, kisha akaona wanazuoni wengi wako kinyume basi kwa makusudi akaanza kushakia, na kwa ajili hiyo akaleta utata huu ambao unafanana na swali la Bani Israeli kwa Nabii Musa bin Imran kuhusu miaka na rangi ya ng'ombe jike.11
________________________
1. Sunanut-Tirmidhiy, Juz.1, Uk. 354

2. Taz. Al-Ilali, Juz. 2, Uk. 331 na Juz. 4, Uk. 384

3. Sharh ya Sahih Muslim ya An-Nawawiy Juz. 5 Uk. 224

4. Naylul-Awtwari ya As-Shawkaniy Juz. 3, Uk. 218 mlango wa kukusanya kwa asiye msafiri kwenye mvua au kingine.

5. Ruhul-Maaniy, Juz. 15 Uk. 133-134 katka tafsiri ya Aya: “Simamisha Sala jua linapopinduka”

6. Al-Baqara: 185

7. Al-Hajji: 78

8. Masailul-Fiqihiya ya Imam Sharaful-dini: 9

9. Ameelezea As-Sayyid Muhammad bin Ismail As-Swanaaniy aju- likanae kwa jina la Al-Amiru ndani ya kitabu chake Subulus-Salami: Juz. 2, Uk. 43

10. Sharhu ya Sahih Muslim ya An-Nawawiy, Juz. 5, Uk. 224 mlango wa kukusanya Sala mbili Hadithi ya 51

11. Al-Baqarat; 2: 67-71
Wengi wanaojaribu kutatua suala hili hukimbilia kudai kuwa haikuwa ni kukusanya kwa halisi kama kukusanya kwa safarini, bali ilikuwa ni kukusanya kwa kimuonekano, yaani Mtume alichelewesha Adhuhuri mpaka ulipobakia muda wa rakaa nne ndipo akaswali Adhuhuri na baada ya kumaliza tu ukawa umeingia wakati wa Al-Asr akaswali Al-Asr, hivyo akawa kakusanya Sala mbili huku akiwa kaswali kila moja ndani ya wakati wake.

Hili ndilo linalodhihirika toka kwa wengi wanaofafanua Hadithi; na yafuatayo ni maelezo yao: An-Nawawiy amesema: “Wapo waliofasiri kuwa ni kuchelewesha ya mwanzo mpaka mwisho wa wakati wake kisha aiswali ndani ya wakati wake, hivyo baada ya kumaliza ukawa umeingia wakati wa Sala ya pili akaiswali, hivyo Sala yake ikawa katika muonekano wa kukusanya.”

Kisha akapinga akasema: “Kauli hii nayo ni dhaifu au batili kwa sababu inapingana na dhahiri kwa namna isiy- otegemewa. Kwa sababu kitendo cha Ibnu Abbas tulichokitaja katika hotuba kisha kutoa kwake Hadithi kama hoja ya usahihi wa kitendo chake, kisha kuthibitisha kwake Abu Huraira bila kukanusha ni hoja tosha katika kupinga tafsiri hii.1

An-Nawawiy alipasa amjibu kwa hoja tuliyoitaja nayo ni kuwa: Mtume alikusanya Sala mbili kwa lengo la kuuondolea umma wake taabu, na kukusanya kwa namna hiyo iliyotajwa kunataabisha zaidi kuliko kutenganisha.

Ibnu Quddama amesema: “Kukusanya ni hiyari, hivyo ingekuwa kukusanya ni kwa namna waliyoielezea basi ingekuwa ni taabu zaidi kuliko kuiswali kila Sala wakati wake. Kwa sababu kuiswali kila Sala wakati wake ni wepesi zaidi kuliko kulinda mwisho wa