Rafed English
site.site_name : Rafed English

Haja Ya Dini by : Sayyid Saeed Akhtar Rizvi (Kwa Maneno Ya Mfasiri)



Namshukuru Mwenyezi Mungu Tabarakal Lahu wa Taala, kwa kunipa muda wa kuanza hadi kumaliza tafsiri ya kijitabu hiki kilichoandikwa na Mwalimu wangu Maulana Sayyid Sa’eed Akhtar Rizvi, ambaye pia ni Chief Missionary wetu.

Kitabu hiki ni tafsiri ya kitabu chake kiitwacho "Need for Religion" alichokiandika kwa lugha ya Kiingereza, kwa ajili ya vijana wa Kiislamu wanaochukua "Diploma" ya Elimu ya Kiislamu kwa Njia ya Posta.

Nimeona kuwa kitabu hiki kitawasaidia sana ndugu zangu Waislamu wa hapa Afrika ya Mashariki, iwapo nitakitarajumu kwa Lugha ya Kiswahili, lugha ambayo hutumiwa sana hapa kwetu.

Kila mtu hupenda kitu na kukithamini sana baada ya kukiona kuwa ni cha faida kake. Kadiri ya faida ya kitu hicho itakavyozidi ndio jinsi mtu huyo atakavyozidi kukithamini na kukipenda kitu hicho.

Dini nayo ni hivyo hivyo, Mtu ataipenda tu, baada ya kuzielewa faida zake kwake.

Katika kijitabu hiki Allamah Sayyed Saeed Akhtar Rizvi, kwanza anaeleza Dini ni nini, kisha anaelezea faida zake, anakanusha hoja za wale wasemao kuwa dini ni kitu kipingacho sayansi n.k.

Analinganisha dini na "Maendeleo na Mabadiliko a viumbe", halafu anakanusha hoja za wale wasioamini kuwepo kwa siku ya Ufufuo. Mwisho kabisa anamalizia kwa kuzitaja sifa muhimu za dini.

Sifa zote ni zake Mwenyezi Mungu aliyemjaalia ndugu yetu Allamah Sayyid Saeed Akhtar Rizvi kwa elimu na akatunufaisha sisi Waislamu wa hapa Afrika Mashariki na duniani pote kwayo.

Mwenyezi Mungu atujalie Waislamu, tuzidi kupata "Alim" kama huyu ndugu yetu. Tuwe wasikivu wa mahubirio yao, na Atuongoze katika Njia iliyonyooka Amin.

Allahuma Swali alaa Muhammadin wa-aali Muhammad.

Mallam: Dhikiri U. M. Kiondo.
Haja Ya Dini

1) Dini Ni Nini?
Neno hili lenye asili ya Kiarabu, "Diin (dini) linatumika kwa maana nyingi kidogo.

(1) "Uislamu; imani ya Umoja wa Mwenyezi Mungu; Ibada; Utii; Matendo yote ya kiibada na Ucha Mungu." Maana zote hizi zinahusiana zenyewe kwa zenyewe na zahusika na imani ya kuwepo Muumba.

(2) "Hukumu; Thawabu au Adhabu; Hesabu Amri; Sheira." Maana hizi, nazo pia, zahusiana zenyewe kwa zenyewe na zatushabihisha kwenye imani ya Maisha ya Akhera.

(3) Kikundi cha tatu cha maana ya neno hili ni "Desturi; Tabia; Mazoea; Aina zote mbili za Dini iliyoteremshwa na Mwenyezi Mungu au ya kimapokeo kutokana na wahenga."

Maana hasa ya neno hili Diin ni kuwa mwanadamu kwa silika zake za asili, hana budi kuwa na mpango wa maisha wenye msingi wa fikara za kiroho au fikara zile tuziitazo "Imani".

Hivyo basi, inaonekana kuwa, neno "ad-Diin" lina maana kubwa mno kuliko ile ya neno la Kiingereza "Religion", ambayo husisitiza maana ya Mwanadamu kuitambua Nguvu kubwa kuliko yeye, na ambayo inautawala ulimwengu mzima, na hasa Mungu au miungu ya mtu kibinafsi, ipasikayo kutiiwa na kuabudiwa; matokeo ya utambuzi wa aina hiyo; mwongozo wa kiroho wa mtu; au mpango maalum wa Kiimani na kiibada.
2) Faida Za Dini Ni Zipi?
Zipo sababu nyingi zimfanyazo mwanadamu ahitaji Dini.

(1) Sote twajua kuwa mwanadamu ni mnyama ahitajiye kuishi kijamii pamoja na wenzake. Kila mtu anategemea mamilioni ya watu wenzake kwa maisha yake na kwa mahitaji muhimu ya hayo maisha yake. Pia tunajua kuwa kila jamii inahitaji sheria fulani fulani ili kuzuia dhulma na kuhifadhi haki ya kila mtu katika jamii hiyo.

Lakini basi swali lifuatalo ni hili, ni nani aliye na haki ya kutunga Sheria hizo? Mtu mmoja? (mtu huyo na awe mfalme au mtawala wa Kiimla)! Jibu ni "Hapana." Yeye hataweza, maana kwa ajili ya silika za kibinadamu, atatunga sheria kwa kufuatana na tamaa yake ya kibinafsi.

Kikundi cha watu? (Watu hao na wawe wa kikundi cha Utawala wa watu wa koo Bora au wa kikundi cha kidemokrasi)! Jibu ni kuwa, "Hawa pia hawataweza kuifanya kazi hiyo vipasikavyo, maana kila mmoja wao hawezi kujiepusha na uamuzi usio sawa na wingi wa uamuzi usio, sawa, hauwezi kupatana na uamuzi ulio sawa.

(2) Vile vile ni dhahiri kuwa hakuna kikundi cha watu kiwezacho kujiepusha na kujitia katika tamaa za kibinafsi. Kwa mfano katika siku za utawala wa kikoloni, mabunge na halmashauri za Makoloni zilikuwa zikitunga sheria kufuatana na mapendekezo ya watawala wa Kizungu. Siku hizi, mabunge na Halmashauri hizo hizo hutunga sheria kufuatana na mapendekezo ya wananchi. Kujali ubinafsi kulikuwa na bado kungali jambo muhimu la kutunga sheria duniani pote.

(3) Zaidi ya hapo hakuna mtu au kikundi cha watu chenye uwezo wa kutunga sheria za mambo mengi na ambazo zimo katika msingi wa usawa na uadilifu kamili.

Kwa sababu hiyo, ni lazima sheria hizo zitungwe na mtu fulani ambae ni mbora kuliko mwanadamu, ambae hana chochote cha kupoteza au cha kufaidika nacho kutokana na sheria hizo, na ambae kila mwanadamu ana uhusiano wa aina iliyo sawa kwake.

Na "Mtu Huyu" ni Allah. Kwa sababu hiyo tunawajibikiwa kuwa na dini.

(4) Zaidi ya hapo ni kuwa, sheria na desturi zilizotungwa na mwanadamu zina upungufu mmoja mbaya sana: Sheria na desturi hizo haziwezi kuzuia matendo ya jinai. Upungufu huu, hukufanya kuwepo kwa sheria za aina hii kuwa kusiko na faida yo yote.

Kwa mfano, mwizi anaingia nyumba isio na watu, katika kijiji cha ughaibuni, usiku wa manane kwa ajili ya kutaka kuiba vitu vyenye thamani. Yeye aelewa wazi kuwa hakuna mtu aiwakilishaye Serikali, kwa maili nyingi sana kutoka nyumba hiyo. Hivyo ataona kuwa na usalama kutokana na kukamatwa. Je! Katika hali hii, iko sheira ya serikali ambayo itamzuia mwizi huyu kutimiza jinai hii? Jibu ni kuwa "Hakuna".

Kusema kweli hakuna serikali itakayomzuia mtu huyu asiibe lakini Dini inaweza, Dini iliyo ya kweli, kama tulivyoieleza hapo juu, huwafundisha watu kuwa yupo Mwenyezi Mungu, ambae ajua kila kitu na anayeona kila kitu. Yeye Mwenyewe ni Mwadilifu na Mwema na anatutaka nasi tuwe waadilifu na wema; kuwa tunahusikana na matendo yetu mbele yake na tutakuja mpa hesabu ya matendo yetu baada ya kufa kwetu.

Kama mtu anaiamini dini hiyo basi, hivyo (Na kwa hivyo tu) anaweza kujiepusha na kutenda dhambi, majinai na kuwadhulumu watu wengine popote awapo.

Sheria za serikali zaweza kuzuia mtu kutenda matendo mabaya ya wazi wazi na hata hivyo, ni katika muda na mahali ambapo mikono ya serikali hiyo yaweza kupafika. Lakini kumwamini Mwenyezi Mungu na dini, hutawala si matendo ya mwanadamu, ya kiwazi wazi tu bali hata yale yaiiyojificha na yaliyo mawazo ya moyoni pia.

Utawala huu, hauna mipaka kwa kutegemea mahali maalum au muda fulani, kwa sababu Mwenyezi Mungu yupo kila mahali na anaona kila kitu.

(5) Ili kuzielewa vizuri faida zilizo wazi wazi, ambazo jamii yazipata kutokana na imani ya kuwepo Mwenyezi Mungu na dini, hebu jaribu kufikiria machafuko na ghasia ambazo wanaadamu wangeliweza kujitia, kama imani ya kuwepo Mungu ingalitupiliwa mbali. Hakutakuwa na jamii yoyote. Badala yake, kutakuwa na umati wa watu tu. Katika hali hiyo, kila mmoja anao uhuru wa kufanay chochote kile akipendacho.

Mtu atafikia kuwa hakuna Mungu, na hakuna maisha ya Akhera, na kuwa yeye amekuwepo hapa duniani kwa bahati ya hali ya asili iliyojitokeza tu. Na pia anajua kuwa muda wa maisha ni mfupi. Kwa hivyo, kikawaida atashawishika na kuyafaidi maisha kwa kadri iwezekanavyo bila ya kujali kitu chochote kile. Kitu atakacho kiwazia ni kujaribu kuepeka kukamatwa akiwa anatenda jambo lolote baya, au kuonwa na serikali tu. Na wakati wowote atakaojiona kuwa yu salama, hataacha kutenda jinai lolote ili kujikidhia tamaa zake, bila ya kujali dhara la tamaa yake hiyo kwa wenzake.

Swali: Hata MIahidi (mtu asiyeamini kuwa kuna Mungu) anaweza kuishi maisha mema kama yale ya mfuasi wa dini. Kama jambo hili lawezekana bila ya dini, nini basi faida ya dini?

Jawabu: Ni kosa kufikiria kuwa, maisha mema ya mlahidi hayana uhusiano kabisa na dini; kwa sababu fikara hizo njema hazikuhifadhiwa akilini mwa mtu huyo na kitu kingine chochote ila na dini tu. Mafundisho mema ya kidini yameimarishwa akilini mwa mtu kwa maelfu ya miaka. Yamekuwa yakihifadhiwa toka kwa baba hadi kwa mwana kwa njia ya asili ya mwanadamu ya mwana kurithi tabia za baba; na pia toka rafiki hadi rafiki kwa njia ya mazingira. Hizi faida njema zimekuwa zisizotengeka toka akilini mwa mtu huyo.

Lakini, akili ni nini? Akili ni fikara za kidini na kiutu ambazo zimemwingia mtu huyo kutoka kwa Wahenga wake wenye maisha ya kidini; na ambazo yeye hawezi kuziepuka. Akili inategemea na mafunzo mema ya dini.

Je ni kwa muda gani akili yaweza kubakia kichwani mwa mtu wakati mafundisho ya kidini yaondolewapo kabisa toka kichwani mwa mtu huyo?

Jibu ni kuwa: Mtu ye yote yule alifikiriaye jambo hili kwa makini ataamua kuwa, hakuna vime unaweza kubakia mwilini mwa mtu, kama utatengwa na imani ya kuwepo Mungu na dini.
3) Kutoielewa Dini
Mara kwa mara tunasikia maneno mabaya yakisemwa wazi wazi, ili kuipinga "Dini". Maneno haya yanatumiwa sana siku hizi, na Makomyunist. Maneno hayo ni:

(i) Dini inapinga sayansi

(ii) Dini ni dawa iliyogunduliwa na mabeparili kuwatuliza watu wa tabaka linalodhulumiwa, na kuwafanya watosheke na hali yao hiyo ya kimaskini, kwa usemi mwingine dini ilikuwa kasumba ya kuwalazia watu.

(iii) Dini huonelewesha maendeleo ya kimwili na kiakili.

Basi hebu ngoja tuzichunguze hoja hizi. Habari hizi hizi zimesemwa na Wazungu wengi toka Karl Marx hadi Bertrand Russel) ambao walikuwa na ujuzi wa dini moja tu, nayo ni Ukristo, hakika wametenda dhambi kubwa ya kiakili, kwa kuona dini fulani, na kudhania kuwa dini zote (hata Uislamu) ni lazima ziwe na fikara hizo hizo.

Hakika kwa vyo vyote vile maneno yao hayo kama si fikara zilizotolewa kwa shabaha maalum, ni udanganyifu mtupu.

Ili kuueleza kinaga naga usemi huo hapo juu, inatulazimu kuieleza kwa muhtasari tu hali ya fikara za Kimasihia ilivyokuwa kuhusu ujuzi na maendeleo.

Tangu karne ya kumi na sita ya baada ya Nabii Isa [a], ulitokea ugomvi kati ya Kanisa na sayansi. Ugomvi huu mbaya sana haukuanzwa na wanasayansi, ila ulianzwa na viongozi wa Kimasihia; ambao walihofu kuwa dini yao ilikuwa katika hatari kubwa ya kupoteza nguvu zake miongoni mwa Wamasihia.

Ngome ya mafundisho yao ilikuwa katika hatari ya kuanguka. Madhehebu zote mbili (Wakatoliki na Maprotestanti) ingawa zilikuwa zikigombana zenyewe kwa zenyewe, zilikuwa na msimamo mmoja kuhusu mapambano baina ya mafundisho yao na njia za kimapinduzi za kisayansi, za Bwana Cupernicus, na mwenzie bwana Galileo.

Walifanya kile kile ambacho kila mdhalimu anayeogopa unyoge wake wa kiasili angeliweza kukitenda. Mateso makali sana yalitolewa kwa wanasayansi washupavu waliolipinga Kanisa na ambao walisema kuwa kile wakijuacho kilikuwa ukweli mtupu.

(1) "Kwanza hatuna budi tumchukue Bwana Cupernicus (Nicolaus Koppernigh) aliyeishi kati ya mwaka 1473-1545, maana yeye alikuwa ndiye aliyeanzisha jambo hilo, Bwana huyu kwa muda mrefu hakuthubutu hata kuchapisha kitabu chake kijulikanacho kwa jina la "On the Revolution of Heavenly Bodies" (katika mzunguko wa sayari za Angani)."

Kwa ajili ya kuliogopa Kanisa. Mwishoni alifaulu kulituliza Kanisa kwa kukiandika kitabu hicho kwa heshima ya Papa (afisa wa cheo cha juu sana wa Kanisa Katoliki). Mchapishaji wa kitabu hiki aliandika utangulizi kuthibitisha kuwa maelezo juu ya mzunguko wa dunia ni jambo linalokubaliwa tu, wala si jambo Iililothibitishwa kabisa.

Kwa maneno ya Bwana Bertrand Russel, "Kwa muda fulani, mbinu hizi zilitosha, na ni kutokana na wito wa kijasiri wa Bwana Galileo (wa kuwaita wana dini kuja kushindana na Wanasayansi) ambao ulileta shutma za wakati uliopita wa Bwana Cupernicus (rejea katia kitabu kiitwacho "Religion and Science").

(2) Bwana Luther pia, aliupinga 'utaratibu' wa Bwana Cupernicus kwa kutumia njia za Kitheolojia (za kiujuzi wa Sifa na Tabia za Mwenyezi Mungu).

(3) Mwanasayansi mwingine, Bwana Galileo Galilei aliyeishi kati ya mwaka 1564-1642 Masihiy, ingawa alikuwa rafiki wa Papa Urban VllI, alitiwa katika jela ya Mahakama ya kuhukumu kesi za wazushi wa mambo ya kidini, kwa amri ya Papa huyo huyo na kutishiwa atapata mateso makali kama hataacha mafundisho yake hayo.

Makosa ya Galileo yalikuwa kuunga mkono mafundisho ya Copernicus kutokana na uchunguzi alioufanya kwa darubini yake. Kwa upande wa Kanisa, uchunguzi huu ulikuwa mgumu zaidi kupambana nao, kuliko ile elimu ya kimaandishi tu ya Bwana Copernicus.

(4) Mwana Sayansi mwingine Bwana Giardino Bruno aliyeishi kati ya mwaka 1549-1600 Masihiy, alikuwa madhabuha mwingine wa ukatili uliotendewa wanasayansi. Bwana huyu alichomwa hali ya kuwa yu hai, Hababi Bertrand Russel, ameandika katika kitabu chake kiitwacho "Religion and Science" hivi: Wataalamu wa Elimu Lahuuti hawakuchelewa kusema kuwa, mafundisho hayo mapya yatafanya yale mafundisho ya kuchukua umbo la kiutu (incarnation, kwa mfano Yesu kuwa ni Mungu aliyegeuka katika umbo la Binaadamu) kuwa ni vigumu kuaminika. (Rejea katika kitabu kiitwacho "Religion and Science").

"Hivyo mahakama ya hukumu za wazushi wa Kidini, ilitangizia haya yafuatayo kuwa ndiyo ukweli. "Usemi wa kwanza, kuwajua ndio kitovu (centre) cha Ulimwengu na kuwa jua haliizunguki dunia ni wa kijinga, kipuuzi, usio kweli hata kidogo katika Elimu lahuuti na ambao ni uzushi mtupu, maana hauafikiani na maandishi Matakatifu.....

Usemi wa pili usemao kuwa dunia si kitovu cha ulimwengu na kwa hiyo dunia ina lizunguka jua ni upuuzi, ni uwongo katika elimu ya hekima (filosofia) na kwa upande wa elimu Lahuuti, kwa ujumla haitofautiani na imani sahihi." (Rejea katika kitabu kiitwacho "Religion and Science".)

Na kwa kuongezea zaidi, Kasisi wa Kanisa la Jesuit aliyeitwa Melchoir Inchofer ilimbidi aongezee kusema wazo lihusulo mzunguko wa dunia ni uzushi mtupu, lichukizalo zaidi, lenye madhara zaidi na lenye kuaibisha zaidi. Kutulia kwa dunia ni kutakatifu mara tatu; hivyo basi hoja zipingazo maisha ya milele ya roho, kuwepo kwa Mwenyezi Mungu na wa Mungu kuchukua umbo Ia kiutu ni lazima zikubaIiwe upesi kuliko hoja zithibitishazo kuwa dunia inasogea. (Reja kitabu kiitwacho "ReIigion and Science).

Kwa sababu ya kukabiliwa na dhuluma kali, Wanasayansi waliueleza Ukristo, kuwa ni "imani isiyo pendelea mambo ya kiakili na isiyopendelea mambo ya Kisayansi; ni ushirikina na ni kitu kirudishacho nyuma maendeleo ya binaadamu." Jambo la kustaajabisha ni kuwa wameichukulia kila dini kwa ujumla kuwa ni sawa na Ukristo. Kwa hakika Uislamu hauwezi kuwekwa miongoni mwa dini 'zisizoafikiana na sayansi, zisizo za kihoja, au zisizoafikiana na maendeleo ya kibinaadamu.'
4) Dini, Mabadiliko Na Maendeleo
Inasemekana kuwa "Mabadiliko na maendeleo", vimethibitisha kuwa hakuna ulazima wa kuwepo Mwenyezi Mungu katika utaratibu wa Ulimwengu.

Ingawa jambo hili lafaa kuzungumziwa katika sehemu ya pili (Mungu wa Uislamu) ya masomo haya, ningependelea kutoa maoni machache ili mwanafunzi ayafikirie.

Kwanza, ni lazima ieleweke wazi kuwa, sizungumzii kuhusu ukweli au uongo wa maelezo yahusuyo mabadiliko na maendeleo, kwani hapa sio mahali pafaapo kulizungumzia zaidi jambo hili.

Pili, ni lazima ieleweke kuwa mabadiliko tu yatokeayo kwa viumbe asili vyenye uhai si 'Mabadiliko ya maendeleo'.

Kitabu cha maarifa yote kijulikanacho kwa jina la "World Book Encyclopaedia" cha 1966 kimeandikwa yafuatayo: "Ufafanuzi wa 'Mabadiliko na maendeleo ya viumbe vyenye uhai hujumlisha mawazo haya matatu yafuatayo:

1. Viumbe vyenye uhai hubadilika kizazi hadi kizazi vikitoa vizazi vyenye tabia zitofautianazo na zile za wahenga wao.

2. Tendo hili limetendeka kwa muda mrefu sana hata likazalisha vikundi vyote na aina zote za viumbe viishivyo sasa, na vile vilivyoishi zamani, ambavyo vimekwisha kufa au vimekwisha potea.

3. Hivi viumbe tofauti tofauti vyenye uhai vina uhusiano wa kiasili kati yao.

Tatu, ieleweke kuwa, ingawa kuna thibitisho hizo, maelezo kuhusu "Mabadiliko na maendeleo', bado ni makisio (theory) tu, wala sio ukweli (fact).

"Ukweli" kama Kamusi la Lugha ya Kiingereza lijulikanalo kwa jina la "Websters Third New International Dictionary", liufafanuavyo ni "Tukio halisi, katika muda au nafasi", ni "Habari zilizothibitishwa".

Hivi kuna uthibitisho gani juu ya maelezo haya ya 'Mabadiliko na Maendeleo?'

Mtaalamu mmoja wa 'Mabadiliko na Maendeleo' aliyejulikana sana, Bwana W. Le Gros Clark, ameandika katika kitabu chake kiitwacho "The Fossil Evidence for Human Evolution" hivi.

"Uwezekano wa kupata mabaki ya zamani ya miili ya wajenga halisi, au hata mfano tu wa Kikundi cha kijiografia cha mahali maalum, ambavyo ndivyo vilivyotoa wahenga hasa ni wa kubuniwa tu, kiasi ambacho haustahili hata kidogo kuufikiria ukweli wake.

"Ufafanuzi wa ushahidi kuhusu 'Maendeleo na mabadiliko' ya binaadamu wa zamani sana ulitokana na uchimbuzi wa sehemu walizoishi binaadamu wa zamani, ambao wameelezwa katika sura iliyopita ni ufafanuzi wa muda tu, kwa sababu ya kutotimilika kwa ushahidi huo haiwezekani kuwa vinginevyo zaidi ya hivi".

Gazeti liitwalo "Science News Letter" la mwaka 1965 lilisema hivi: "Kuna ugomvi baina ya wanasayansi kuhusu tu, jinsi mwanadamu alivyobadilika na kuendelea: ni lini alifanya hivyo na alivyokuwa kabla."

Bwana Clark tuliyemtaja hapo juu aliandika hivi, "Ni nini chanzo asili cha mwanaadamu?....Kwa bahati mbaya, majibu yo yote yawezayo kutolewa hivi hapa kuhusu maswali kama haya yanategemea ushahidi usio wa dhahiri kabisa, na kwa hivyo mengi ya majibu hayo ni makisio tu."

Rais wa zamani wa "Shirika la Umarikani Ia Maendeleo ya Sayansi aliandika katika gazeti liitwalo "Science Magazine" haya yafuatayo ili 'kuunga mkono' mabadiliko na Maendeleo:

Hebu njoo sasa, kama unaweza, katika safari ya kukisia ya nyakati za zamani sana zisizo na kumbukumbu za kuaminika. Tufikirie wakati ambao jamii ya viumbe vyenye akili vimetokea kutokana na aina ifananayo na.....; fanya hima katika muda wa maelfu ya miaka, muda ambao habari za sasa zautegemea, kwa ajili ya sehemu kubwa ya makisio ya ufafanuzi wa wakati wa kwanza wa kumbukumbu zilizoandikwa, ambazo kutokana nazo, uhakika fulani fulani waweza kuokotezwa."

Mwanasayansi mmoja wa Kiingereza, Bwana L. M. Davies wakati fulani alisema hivi: "Imekisiwa kuwa, vifungu vya maneno visivyopungua 800 katika maneno yaonyeshayo wazo Ia kukisia (maneno kama vile "Tuchukulie tu," au Tunaweza kudhania kuwa" n.k) vinaonekana kati ya majalada ya kitabu cha Bwana Darwin kiitwacho "Origin of Species" (Asili ya viumbe vyenye asili moja), peke yake."

Ukivifikiria vifungu vya maneno tulivyoviandika hapo juu, na hasa maneno yale tuliyoyapigia mistari, utaamua kuwa "Mabadiliko na maendeleo si ukweli uliodumishwa ila ni maelezo tu miononi mwa maeIezo mengi yaliyokuwepo tangu mwanzoni mwa binaadamu, ili kuieleleza asili ya ulimwengu, Mengi ya maelezo ya namna hii, sasa yamedharauliwa, lakini hapo mwanzoni yalikuwa na nguvu akilini mwa watu kama yalivyo haya maelezo ya mabadiliko na maendeleo hivi sasa. Na nguvu zake hizi, katika akili ya watu, hazifanyi mawazo haya kuwa ya ukweli zaidi.

Hakika, mwanasayansi mmoja, Dakta T. N. Tahmisian, ambae ni mtaalamu wa mambo ya viumbe vyenye uhai, wa Tume ya Nguvu za Atomiki, alisema, "Wanasayansi waendao huku na huku na kufundisha kuwa maelezo kuhusu mabadiliko na maendeleo ni ukweli uliothibitika wa masiha ni wadanganyifu wakuu na hadithi watoazo kuyaeleza mabadiliko na maendeleo, hazina ukweli hata kidogo. Aliuita uelezaji wa mabadiliko na maendeleo kuwa ni "fumbo la mchezo wa mchanganyiko wa dhana na mazingaumbwe ya matumizi ya nambari."

Mwanasayansi mwingine aliyekuwa mkuu wa idara ya sayansi katika chuo kimoja, Bwana J. W. Klotz, alisema mnamo mwaka 1965 Masihiya kwamba, "kuyakubali maelezo ya mabadiliko na maendeleo bado kunategemea tu, kuwa ni imani zaidijuu yajambo hilo.

Na juu ya hapo maelezo haya mpaka sasa yanawajibikiwa kutafuta ushahidi utoshao kuyaunga mkono. Basi vipi maelezo haya yawezavyo kutumika kupinga maelezo ya kuwepo kwa Mwenyezi Mungu?

Mwisho kabisa, hata wanamabadiliko na maendeIeo wenyewe wanakubali kuwa kunahitajika kuwepo, "Mwenyezi Mungu Mwenye kuishi milele, Mjuzi wa yote, Mwenye nguvu zote." Katika utaratibu wa Ulimwengu kama inavyoelezwa katika maelezo ya "Mabadiliko na maendeleo."

Lakini, hapo mwanzo wanasayansi walikukataa kuwepo Mwenyezi Mungu; na kuzihusisha sifa njema hizi na "Asili", wanasema kuwa "Asili" ilichukua kile, na "Asili" ilifanya kile.

Hata hivyo hebu tutazame hii 'Asili' ni nini? Asili ni wazo la kuwazika tu, lililo katika ubongo wa watu, baada ya kujifunza kwa makini tabia za vitu. Asili yaweza kuonekana katika vitu; lakini si yenye kuishi yenyewe.

Na kwa hali yoyote, hakunia kumbukumbu ya mkutano wo wote uliofanyika kuhusu asili za vitu mbali mbali; ili kuamua kuhusu jinsi ya kupatanisha kazi zao. Maua hayafanyi kazi pamoja na nyuki ili kutafuta ushirika wa nyuki katika uzalishaji wao, na kuwapa nyuki asali kama ujira wao. Bali twajua wazi kuwa nyuki hawawezi kuishi hata kwa siku moja tu, bila ya maua, na kuwa maelfu ya maua yangelipotea kama si sababu ya nyuki.

Hivyo basi, unaona kuwa wana mabadiliko na maendeleo wanatambua umuhimu wa Mtengenezaji na "Msanii". Lakini kimafundisho, wanafundisha kwa kurudia rudia kuwa, huyo Mtengenezaji na Msanii alikuwa ni "Asili" (fundisho ambalo ni oni la kuwazika tu) au "Jauhari" ambayo ni kitu kisicho na "Akili wala Uhai".
5) Hoja Ijulikanayo Kama "Hoja Ya Pascal"
Hadhrat Amiirul Mu'miniin Ali bin Abi Talib alisema:

Wanajimu na waganga husema kuwa wafu hawatafufuliwa kamwe, "Nikasema: Haya shikilieni maoni yenu hayo. Kama oni lenu litakuwa sahihi, sitapata dhara lolote (kutokana na imani yangu, ya kuiammi sika ya Hukumu); lakini iwapo imani yangu itakuwa sahihi basi mtakuwa wakosefu (katika siku hiyo kwa kutoiamini siku ya Hukumu)".

Allama Abu Hamid Al Ghazali (Aliyefariki mnamo mwaka 1111 Masihiya) aliandika katika kitabu chake kiitwacho "Mizanul Aamal" kuwa "Ali (Mwenyezi Mungu amteremshie baraka zake) alimwambia mtu mmoja aliyekuwa akibishana naye sana kuhusu Akhera akisema: Kama ukweli ni huo unaoufikiria (kuwa hakuna maisha ya Akhera); basi ninyi wote mtaokoka; lakini iwapo ukweli ni kama hivi nilivyokwisha kueleza (kuwa kuna maisha ya Baadaye), basi ninyi mtalaaniwa na mimi nitaokolewa." Huo ndio ukweli uliopo. Thibitisho tuzipatazo sisi wenyewe tuvionapo viumbe vilivyomo humu duniani, zaunga mkono imani ya kuwepo Mwenyezi Mungu Muumba, na kuwepo kwa siku ya Hukumu.

Kisha Mwanachuoni huyo, Bwana Al-Ghazali alieleza kuwa, Hadhrat Ali [a] hakuitoa hoja hii ili kuficha mdhihiriko wa kuwepo kwa maisha ya Akhera, ila aliitoa kwa kutaka kuwahakikishia watu jambo hili kwa maelelezo ya kihoja.

Miaka elfu moja, baada ya Hadhrat Ali bin Abi Talib [a] alitokea mtaalamu wa hesabu maarufu sana Bwana Pascal ambaye alifariki mnamo mwaka 1662 Masihiya; pamoja na "Parido Pascal" (Hoja ya Pascal) yake maarufu, ambayo allitumia ili kulihakikishia kundi la watu wa aina hiyo hiyo, jambo hilo hilo.

Hoja yake hiyo, yaweza kuelezwa kwa kifupi zaidi kwa maneno yafuatayo: "Kama unaamini kuwepo maisha ya Akhera, utapata kila kitu kama kweli maisha hayo yapo kweli, na hutapata hasara yoyote kama maisha hayo hayapo. Hivyo basi ni afadhali kuyakinisha kuwa, hakika siku hiyo ipo." (Habari hizi zinatoka katika UK. 439 wa kitabu kiitwacho "Pascal", kilichoandikwa na Bensees na kutayarishwa Bwana Y. Brunchirey huko Paris - Ufaransa mnamo mwaka 1912 Masihiya).

Je huu ni ulinganifu tu? Au Pascal alipata wazo la (Pari) imani yake kutokana na Uislamu?

Bwana Asin Palalcios anaamini kuwa Bwana Pascal alisoma hoja hizi katika kitabu kiitwacho "Ihya-ul-Uluum" cha Mwanachuoni Al-Ghazali.

Lakini, Bwana Al-Ghazali mwenyewe anaeleza katika kitabu hicho Mizanul-Aamal tulicho kitaja hapo juu kuwa, Hadhrat Ali bin Abi Talib [a] ndiye asili ya hoja hii.

Hivyo basi, inatubidi tuziweke sifa hizi pale zipasikapo kuwapo na kukubali kuwa Bwana Pascal (ingawa yeye binafsi hakutueleza kazipata habari hizi kutoka kwa Hadhrat Ali bin Abi Talib [a].
6) Sifa Za Dini
Mpaka sasa nimeeleza umuhimu wa dini kwa ujumla.

Sasa hebu ngoja nizitaje sifa za lazima kwa dini kuwa nazo, ili itimize mahitaji ya dini niliyoyataja hapo juu.
1) Kwanza kabisa dini ni lazima ipatane na akili na udadisi wa mtu.
Hakika zipo dini zenye kuwataka wafuasi wake waamini kwanza kisha ndipo waelewe. Kusema kweli dini kama hizi huzirudisha nyuma fikara za mwanaadamu na ni haki ziitwe (na kwa hakika zinaitwa) dini zisizopatana na fikara za Mwanaadamu.

Uislamu kama unavyofafanuliwa na imani ya madhehebu ya Shia Ithna-sheria, hutoa nafasi ya mbele zaidi kwa akili za binadamu na hoja zake. "Akili" ni moja wa misingi minne ya Sheria ya Shia Ithna-Asheria. Sio hivyo tu, bali vile vile imani hii inahimiza kuwa mafundisho ya dini ni lazima yaeleweke kwa mwenye kuiamini dini hiyo.
2) Ni lazima dini ifundishe na ifanye kwa vitendo, hekima ya mwanaadamu.
Ziko dini ambazo huwataka wafuasi wake wasujudie picha au sanamu za watu fulani fulani au wanyama fulani fulani au vitu vingine ambavyo havina uhai.

Dini kama hizi hushusha sana heshima za wafuasi wao, na ni haki zilaumiwe kwa jambo hilo. Baadi ya dini hufundisha ubora wa watu wa taifa fulani au kudharau watu wa ukoo mwingine.

Uislamu tu ndio uliokuwa na bado ni kiongozi wa usawa wa binaadamu na ambavyo, kwa mara ya kwanza katika historia ya dini, umefundisha na ukafanya kwa vitendo, udugu, usawa na haki kwa binadamu na ukaonyesha heshima ya Mwanadamu kiasi cha kuweza hata kuyashangaza macho ya watu wote.
3) Dini ni lazima iwe mwongozo ulio kamili wa kumwendeleza mwanadamu kimwili, kiakili na kiroho kwa ujumla.
Zipo baadhi ya dini ambazo hutilia mkazo zaidi katika mambo ya kiroho na kuachilia mbali mwili na akili; na zipo nyingine ambazo huzungumzia tu kuhusu maendeleo ya kimwili, au ya kiakili lakini haziyafanyi kimatendo mambo hayo.

Dini za aina hii haziwezi kuwachukua wafuasi wake mbali sana kwa sababu maendeleo yafundishwayo na dini hizo yamekwenda kombo.

Ni Uislamu tu, kama unavyofundisha na Madhehebu ya Shia Ithnaasheria, ambao humwendeleza mtu kimwili, kifikara na kiroho kwa ujumla.
4) Ni lazima dini iwe na mkusanyiko wa sheria zihusuzo maisha ya binaadamu.
Dini ambazo hufundisha tu kuwa "wapende jirani yako" bila ya kuonyesha jinsi ya kufanya hivyo, ni dini zisizo na faida yo yote wakati zikaribiwapo na suala la kulifanya jambo kimatendo.

Uislamu unao mkusanyiko timamu wa sheria za maisha ya mwanaadamu ambazo humwongoza mtu sawa sawa katika maisha yake ya kifamilia, kijamii, kiuchumi, kitabia za kiutu na kiadilifu.
5) Ni lazima dini iafikiane na asili ya mwanaadamu.
Zipo dini zinazojaribu kuiepuka asili ya mwanaadamu. Kwa mfano, baadhi ya dini zinafundisha utawa. Wanaamua kwa matendo yao (kama si kwa maneno mengi) kuwa Mwenyezi Mungu alikosea alipoumba hamu ya tendo la mke na mume katika mwili wa mwanaadamu. Vile vile wanasahau (au wanajifanya kusahau) kuwa silika za kiasili haziwezi kuharibiwa na kuwa silika hizi zisizo za kiasili zinamwongoza mtu kwenye undanganyifu wa kisiri.

Na sijui, ni nini kingelitokea kuhusu kuwepo kwa mwanaadamu hapa duniani, iwapo watu wote wangelikuwa wafuasi wa kimatendo wa dini hiyo. Hakika watu wote wangelimalizika katika muda wa miaka kati ya arobaini na hamsini hivi.

Bila ya kusema kuwa dini kama hii haiwezi kuwaongoza watu kwenye ustawi, kwa sababu kufuatana na asili yake, dini hii ni kinyume na mdumisho wa kuwepo kwa wanadamu hapa duniani.
6) Ni lazima dini isitumike kama zana mikononi mwa wadhalimu, ili kuudhulumu umma.
Dini nyingi zinalaaniwa na makafiri kwa kuwa silaha ya makabaila kwa ajili ya kuudhulumu umma unaoonewa na kuzifunika sauti za walalamikaji.

Dini kama hizi, kwa mfano zile zilizofundisha mawazo ya "Kudra". Hivyo basi, umma ulilazimishwa kuamini kuwa matendo yote mabaya, udhalimu, na uovu wa watawala ulikuwa ni Penzi la Mwenyezi Mungu; hivyo basi vitu kama hivi ni lazima vivumiliwe bila ya malalamiko yo yote.

Dini kama hizo hazina nafasi katika karne iliyoendelea kama hii yetu. Ni Uislamu peke yake, kama ulivyoelezwa na madhehebu ya Shia Ithna-asheria ambao ulisema kuwa imani kama hiyo ilikuwa upuuzi mtupu; kuwa kila mtu ana madaraka kamili ya matendo yake na kuwa madaraka yake yasihusishwe na Mwenyezi Mungu.

Itadhihirika wazi, kutokana na kanuni ya hapo juu kuwa, miongoni mwa dini nyingi sana za duniani, ni Uislamu tu (Imani ya Shia Ithna-asheria) ambao Unatimiza mashaiti haya ya lazima ya dini ya kweli, na yenye maarifa mengi.