Rafed English
site.site_name : Rafed English

Chemchem Ya Uhuru - Imamu Husain Sayyid-us-Shuhada (a) by : al-islam.org

 

Shukrani
Kitabu hiki kimeandikwa kwa lugha ya Urdu na Mtukufu Sayyadul Ulama Maulana Sayyid Ali Naqi Saheb, Mujtahid wa huo Kikuu cha Lucknow, Uhindi.

Kimetafsiriwa kwa Lugha ya Kiingereza na Sayyid Hashim Raza Rizvi, B.A., B.T., Yadgar-e-Husayni H.S. School, Allahabad, Uhindi na kutolewa na Imamia Mission, Lucknow U.P., Uhindi.

Kimetafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili kutoka hiyo tafsiri ya kiingereza na Marehemu Bwana L.W. Hamisi Kitumboy aIiyekuwa Mubalighi Mkaguzi wetu) na kikachekiwa na kusahihishwa na Mwalimu Dhikiri (Zakir Ali) U.M. Kiondo. Edita wa "Sauti ya Bilal".
Utangulizi
Maisha ya mwanadamu ni mnyororo wa mapambano. Ni lazima apambane katika kuyashinda mapenzi yake na misukumo ambayo ni lazima imkabili kwa vile yu mwanadamu, naye ni lazima kuwa macho katika unyonge wake na kuyatii maamrisho yote ya akili zake kuhusu mambo yote anayoamini kuwa ni bora zaidi kuliko aina zote za starehe.

Na kwa upande mwingine ni lazima ajiambatanishe na njia yake ya ukweli katika meno ya nguvu zote zinazompinga ambazo humkingia njia yake. Hana budi kupigana na dhoruba ya fikara, mapokeo, faida za daima na zile nguvu zote za dhuluma na uovu ambazo humfikiria mtu huyu kuwa yu mwovu, na hivyo kumfanyia chanzo cha kuyarudisha nyuma maendeleo yake.

Vitabu vya akhlaki (elimu ya tabia nzuri au mema na mabaya vimejaa mafundisho ya kale, lakini tunahitaji kuona mifano ya siku hizi ya kutushawishi, kuifuata mifano hiyo. Imamu Husayn [a] alikuwa mfano wa aina hiyo.
Nasaba
Sayyidina Abu Abdallah Husayn [a] alikuwa lmamu wa Tatu wa nyumba ya Mtukufu Mtume [s]. Alikuwa mwanawa binti wa Mtukufu Mtume [s], Bibi Fatimah [a], binti ambaye Mtume [s] alikuwa akisimama kuonyesha heshima yake kila alipoingia mahali alipokuwepo Mtume [s]. Baba yake alikuwa Sayyidina Ali [a] binamu yake Mtume [s] na alikuwa mjukuu wa Mtume [s].
Kuzaliwa Kwake
Imamu Husayn [a] alizaliwa mnamo siku ya Alhamisi tarehe tatu ya mwezi wa Shaaban mnamo mwaka wa nne wa Hijiriya. Alipozaliwa Mtume [s] alikuja, akamchukua mikononi mwake na akatia ulimi wake kinywani mwa mtoto huyu mchanga ambaye aliunyonya.

Mnamo siku ya saba ilifanyika sherehe ya Aqiqa (kunyolewa kwa nywele alizozaliwa nazo mtoto). Kuzaliwa kwa mtoto huyu kulikuwa chanzo cha furaha kwa familia yote lakini Mtukufu Mtume [s] alijua yatakayomtokea mtoto huyu baadaye na hivyo alilia sana. Tokea wakati huo jamii nzima ya Mtume [s] ilianza kuyazungumzia masaibu ya maishani mwake yatakayomsibu na ambayo yatahusiana kabisa na maisha yake.
Kulelewa Kwake
Mtukufu Mtume [s] alikuwa akiwalea wajukuu zake Hasan [a] na Husayn [a] na vile vile alikuwa akiulea Uislamu; na Hadhrat Ali [a] na Bibi Fatimah [a] walikuwa nao vile vile wakiwalea watoto hawa ambao Mtukufu Mtume [s] aliwaita wanawe. Alikuwa akiwachukua popote pale aendapo. Mara nyingi Imamu Hasan [a] alikaa katika bega lake Ia kuume na Imamu Husayn [a] alikaa katika bega lake Ia kushoto. Kila mara Mtume [s] aliwataka Waislamu wawapende hao watoto wake Mtume [s], na mapenzi yake kwa Imamu Husayn [a] yalikuwa na kiwango kikubwa.

Mtume [s] alipokuwa akisali, Imamu Husayn [a] alikuwa akija na kukaa mgongoni pake. Mtume [s] alikuwa akiendeleza Sajdah yake mpaka Imamu Husayn atelemke kwa hiari yake. Wakati fulani Imamu Husayn [a] alikuja kwenye Msikiti wa Mtume [s], msikiti wa mjini Madina, wakati Mtume [s] alipokuwa akihutubia. Imamu Husayn [a] alijikwaa na kuanguka chini. Mtume [s] mara moja aliacha kuhutubia, akateremka chini na kumnyanyua mwanawe kwanza. Kisha aliwahutubia watu waliokuwepo hapo akisema, "Huyu ni Husayn; mfahamuni vizuri".

Vile vile Mtume [s] alisema, "HUSAYN ANATOKANA NA MIMI, NA MIMI NINATOKANA NA HUSAYN", akiwa na maana ya kuwa lmamu Husayn [a] alikuwa ndio maisha ya Mtukufu Mtume [s] na jina Ia Mtume [s] litadumu kupitia kwake.
Alipofariki Mtume [s] Imamu Husayn [a] alikuwa na umri wa miaka sita tu. Kipindi cha miaka ishirini na mitano kilichofuatia ambacho Imamu Ali [a] aliishi maisha ya kujitenga, Imamu Husayn [a] alipata muda wa kutosha kujifunza tabia za babiye. Mafunzo haya yalichukua muda wa ujana wake na alipokuwa na umri wa miaka thelathini na moja baba yake alipewa Ukhalifa. Imamu Hasan [a] alifuatana na babiye katika vita za Jamal, Siffin na Nahrawan. Katika mwaka wa 40 Hijiriya Hadhrat Ali [a] alikufa kishahidi katika msikiti wa Kufa (Iraq) na Imamu Hasan [a] alilazimika kuzishika kazi za Ukhalifa. Imamu [a] Husayn akiwa ndugu mtiifu, alimsaidia Imamu Hasan [a] na Imamu Hasan [a] alipofanya mapatano na Muawiyyah ili kuziokoa haki za Uislamu, Imamu Husayn [a] nae aliishi maisha ya kujitenga kama alivyofanya Imamu Hasan [a].

Imamu Husayn [a] alitumikia Uislamu kimya kimya kwa muda wa miaka ishirinl. Miaka kumi chini ya kaka yake Imamu Hasan [a] na miaka kumi baada ya kifo cha Imamu Hasan [a]. Lakini katu Muawiyyah hakuyatimiza masharti ya mapatano aliyoyafanya na Imamu Hasan [a]. Alimtilia sumu Imamu Hasan [a] na akawasumbua sana wafuasl wa Imamu Ali [a] na akawafunga, akawakata vichwa na hata kuwasulubisha. Mwishoni kabisa alivunja masharti ya mapatano kwa kumchagua mwanawe Yazid kuwa mrithi wake na alitumia kila aina ya nguvu na propaganda ili kuungwa mkono wa Waislamu.
Tabia Yake
Imamu Husayn alikuwa lmamu wa tatu na alikuwa mcha Mungu na mnyofu sana. Hata maadui wake waliukubali ukarimu wake na sifa zake nzuri. Alikuwa akienda Sajdah elfu moja katika muda wa masaa ishirini na manne (siku moja). Alikwenda Hija mara ishirInI na tano kwa miguu. Mtukufu Mtume [s] yeye mwenyewe alisema, "Husayn ana ushupavu na ukarimu wangu".

Mlangoni pake kila wakati palikuwa na maskani na kila mara nyumba yake ilijaa wageni na hakuna mtu yeyote yule aliyerudi kutoka nyumbani kwa Imamu Husayn [a] bila ya kuridhika. Kwa sababu hiyo alikuwa akijulikana kwa jina la "Baba wa maskini". Alikuwa na kawaida ya kuchukua mikungu ya tende na mikate wakati wa usiku kwenda kuwapa watu fukara na maskani. Na kazi hizi za usiku ziliweka alama katika mgongo wake. Kila mara alikuwa akisema, "Kama akikujia maskini yeyote yule kutaka msaada, ina maana kuwa maskini huyo kakuuzia heshima yake na sasa ni wajibu wako kutomrudishia akiwa na wazo baya kuhusu heshima yako."

Jinsi alivyokuwa akiwatendea watumwa na watumishi wake ilikuwa na kama vile atendavyo baba mwenye huruma. Kila mara alikuwa akitafuta nafasi ya kuwapatia uhuru.

Watu wote wa wakati wake waliitambua vizuri elimu yake bora. Katika kila tatizo Ia kidini aliendewa na kutakiwa alitatue tatizo hilo. Mkusanyo wa Sala zake unaoitwa "Sahifah Husayniah" (kitabu cha Husayn) upo hadi sasa.

Ailkuwa na huruma sana kiasi ambacho aliwaonea huruma hata maadui zake. Kila mara aliwashughulikia sana maskini wa watu wengine kabla ya wale maskini wake. Imamu Husayn [a] akiwa na sifa zote hizi nzuri. Alikuwa mpole na mnyenyekevu sana kiasi ambacho siku moja alipokuwa akipita mahali Fulani maskini fulani walimkaribisha kula chakula pamoja nao. Imamu [a] alikwenda kukaa pamoja nao ingawa hakuweza kula nao kwa kuwa sio halali kwa watu wa nyumba ya Mtukufu Mtume [s] kutumia chochote kile kilichotolewa sadaka.

Matokeo yake yalikuwa kila awapo, watu hawakuweza kumtazama. Aliheshimiwa sana kiasi ambacho hakuna mtu ye yote yule aliyezikataa sifa zake nzuri, hata wale wa kabila lililokuwa adui kwa ukoo wake. Siku moja alimwandikia barua kali sana Muawiyyah akimlaumu kwa matendo yake yasiyo sahihi. Muawiyyah alipoisoma barua hiyo alichomwa sana moyoni. Wafuasi wake walimshauri amwandikie Imamu [a] barua kama hiyo. Muawiyyah alijibu, "Kama nikiandika mambo yasiyo ya kweli katika barua hiyo basi barua hiyo haitatimiza lengo lake, na kama nikijaribu kutafuta upungufu wowote ule katika tabia zake (lmamu Husayn [a]), Wallah, nashindwa kupata wowote ule".

Masaibu ya Karbala wanaonyesha sura ya ushujaa wake, ukweli, nia, uvumiIivu, ustahimilivu na amani. Hakuzilegeza juhudi zake katika kufanya mapatano hadi mwisho, lakini hakukubali kugeuka japo inchi moja kutoka kwenye njia yake ya wajibu wake na aliridhika kufa kuliko kufanya hivyo.

Aliishi akiwa mwana chini ya baba yake Imamu Ali [a] na akiwa ndugu mdogo wa Imamu Hasan [a] na aliwatii kwa kuwa ilikuwa haki kwake kufanya hivyo. Huko Karbala aliwaongoza watu wake vizuri sana kama alivyowatii wakubwa wake. Imamu Husayn [a] yu mnara wa taa ya Uongozi kwa wanadamu wote.
Moja ya masharti muhimu sana ya mapatano yaliyofanywa baina ya Imamu Hasan [a] na Muawiyyah ni kuwa Muawiyyah hana haki ya kumchagua mrithi wa Ufalme wake. Lakini kama alivyovunja masharti mengine ya mapatano hayo, vile vile alilivunja sharti hili nalo bila ya aibu yoyote ile.

Sio kuwa tu alimchagua mwanawe Yazid kuwa mrithi wa Ufalme wake, bali vile vile alifanya msafara wa kuwatembeiea Waislamu na kuwataka wafanye "Baiat" (kiapo cha utii) kwa ajili ya mwanawe. Imamu Husayn [a] alikataa jambo hilo. Sio kuwa tu Yazid hakuwa na haki ya kuwa Khalifa, lakini kama kila mmoja wetu ajuavyo sana siku hizi, alikuwa na tabia mbaya sana kiasi ambacho hata kuzitaja tu tabia zake ni uchafu mkubwa. Na vivyo katika hali hiyo Muawiyyah alitaka kibali cha kuidhinishwa kwa tabia hizo mbaya za mwanawe kwa kibali cha lmamu Husayn [a] cha kuteu1iwa kwake kuwa Khalilfa.

Hivyo baada ya kifo cha Muawiyyah, jambo Ia kwanza alilolifanya Yazid lilikuwa ni kujaribu kupata kibali cha Ukhalifa wake kutoka kwa Imamu [a]. Hivyo, alipomwandikia gavana wa Madina kumjulisha kifo cha baba yake, Muawiyyah, vile vile alimwandikia kuhusu jambo hilo. Gavana huyo aliyeitwa Walid alimwita Imamu Husayn [a] na kumweleza ujumbe wa Yazid. Kukubali au kupatana na Imamu [a] kuhusu jambo hili hakukuwa kitu cha kutegemea. Imamu [a] alijua vizuri sana kuwa haiwezekani kwake kuukubali utawala wa Yazid; na vile vile pia alijua matokeo yatakayotokana na kukataa kwake. Lakini njia ya wajibu wake ilikuwa wazi kabisa kwake. Hivyo baada ya kumpa Walid jibu Iifaalo, Imamu [a] alirudi nyumbani.

Baada ya Imamu [a] kuona kuwa haingefaa kwa yeye kuendelea kukaa Madina, aliamua kuondoka mjini humo. Siku hiyo alipoondoka Madina ilikuwa ni tarehe 28 ya mwezi wa Rajab mwaka wa 60 Hijiriya. Kwa vile mji wa Makka ulikuwa mahali pa kukimbilia kwa watu wote kufuatana na desturi za watu wa Uarabuni na sheria za Uislamu kwa ujumla, Imamu [a] pia alikwenda huku. Aiifuatana na jamii yake wakiwemo wanawake wa ukoo wa Mtukufu Mtume [s] na hata watoto.

Wakati huo, wakati wa Hija ulikuwa karibuni sana na Imamu [a] alitaka kuhiji. Lakini Imamu huyu aliyekwenda kuhiji huko Makka mara ishirini na tano kwa miguu, safari hii alilazimika kuondoka mjini humo bila ya kuhiji. Serikali shari ya Shamu ilituma watu kadhaa kwa jina Ia mahujaju ili kumuulia mbali lmamu [a], hata kama wakiifanya dhambi hii ndani ya Kaaba yenyewe, si kitu.

Imamu [a] hakupenda kuona utakatifu wa Kaaba ukivunjwa kwa sababu yake. Siku mbili zilipobakia kwa Hija, lmamu [a] aliondoka Makka pamoja na jamii yake yote na wafuasi wake. Kwa kuwa alikuwa akipokea barua kutoka Kufa, zikimtaka aende huko na zikisisitiza kuhusu kumkubali kuwa yu Imamu wa haki, Husayn [a] katika hali hii ya kutoweza kuamua, alianza safari yake kwenda Iraq. Alimtuma binamu yake Bwana Muslim bin Aqil kwenda Kufa kutazama hali ilivyo na kumjulisha Imamu [a].

Bwana Muslim alipofika Kufa alipokewa vizuri sana lakini upesi sana Yazid alimteua Ubaidullah Ibn Ziyad kuwa gavana wa Kufa na mtu huyu aliyekuwa katili sana miongoni mwa watu wa kabila ya Bani Umayyah, mara moja alitoa amri kali sana kuhusu Bwana Muslim bin Aqil. Akaufunga mji wote na mara moja wale wote waliokuja kuonana na Bwana Muslim waliondoka mjini humo.

Mnamo tarehe 9 ya mwezi wa Dhul Hajj (Mfunguo Tatu) mwaka wa 60 wa Hijiriya Bwana Muslim bin Aqil alikamatwa na akauwawa kikatili sana. Habari za kuuwawa kwake zilimfikia lmamu Husayn [a] alipokuwa njiani kuja Iraq mahali paitwapo Zubalah. Jambo hili liliziumiza sana fikara za Imamu [a] lakini dhamira yake isiyobadilika haikutambua njia yoyote ile nyingine; na zaidi ya hapo halikuwepo tena suala la kurudi nyuma.

AIiendelea kusafiri hadi alipofika mahali paitwapo Zu-Hasm ambapo alikingiwa njia na kikosi cha jeshi la Ibn Ziyad chini ya uongozi wa mtu mmoja aliyeitwa Hurr bin Yazid Riyah.

Hawa watu wa Hurr walihitaji sana maji na walikuwa wakifa kiu. Ingawa lmamu [a] alikuwa na watoto wadogo na wanawake wengi pamoja naye, aliwapa maji ya kunywa wote na akawaacha watosheke. Lakini askari hao waliyakumbuka maagizo waliyoyapewa na wakasimama kusimamisha maendeleo ya safari ya Imamu [a].

Wala hawakumruhusu arudi alikotoka. Imamu [a] alilazimishwa kupiga kambi katika wanda wa mchanga mtupu wa Karbala mnamo tarehe 2 ya mwezi wa Muharram (Mfunguo Nne) wa mwaka wa 61 Hijiriya. Siku iliyofuatia majeshi ya Yazid yalianza kumiminika katika uwanja wa vita. Sehemu hizo watu wake zililindwa vikali mno. Imamu [a] alikuwa na marafiki waaminifu sabini na wawiIi tu na upande wa Yazid ulikuwa na maelfu ya askari.

Majaribio ya kudumisha amani yalifanyika kwa muda wa siku saba. lmamu [a] alikubali hata kuhama Uarabuni ili kuzuia kutokea kwa vita yoyote ile ambayo ingeliweza kutokea. Lakini katika alasiri ya tarehe 9 ya mwezi huo, mategemeo yote ya mapatano fulani yalikufa. Omar bin Saad ambaye alichukua Uamiri jeshi wa jeshi hilo kutoka kwa Hurr (baada ya Hurr kujiunga na jeshi la Imamu [a] alipata barua kutoka kwa Yazid kwa mkono wa mtu mmoja aliyeitwa Shimr ikimwamrisha kuanza vita mara moja kama Imamu Husayn [a] hakusalimu amri bila ya masharti yoyote yale.

Ingawa njia zote za kufikia kwenye maji zilifungwa na watoto wa lmamu [a] walikuwa wakililia maji na hakukuweko tazamio lo lote Ia amani, lilikuwa jambo lisilowezekana kwa vyo vyote vile, kwa lmamu Husayn [a] kuyakubalia masharti ya watu waYazid. Hivyo, baada ya yote hayo aliwaomba wampe nafasi ya usiku mmoja ili aweze kumwomba Mwenyezi Mungu na vile vile pande zote mbiIi zipate nafasi ya kufikiria zaidi jambo hilo kabla ya kutoa uamuzi wa mwisho.

Wakati wa usiku Imamu [a] aliwakusanya watu wake pamoja na aliwahutubia akisema. "Kesho ni siku ya kujitoa mhanga. Watu hawa wana kiu ya damu yangu tu. Basi kwa nini muyahatarishe maisha yenu? Nakuruhusuni mniache na kwenda popote pale mpapendapo kwa kiza hiki cha usiku". Lakini watu hao waaminifu walisema kwa pamoja, "Hatuwezi kufanya japo kuwa tulazimike kufa mara sabini".

Usiku ulikucha. Katika siku ya 10 ya Muharram, hawa marafiki wachache waaminifu wa Imamu [a] walifanya kama walivyosema na waliuthibitisha ustahiki wao. Walikuwepo watu wazee kama vile Mabwana Habib bin Muzahir, Muslim bin Ausajah, Suwaid bin Amr, Anas bin Harith, na Abdur-Rahman bin Abd-i-Rab ambao walikuwa na umri wa miaka sitini, sabini na hata themanini.

Vile vile walikuwepo masahaba wachache wa Mtukufu Mtume [s] "mahafidhi" (watu waliokariri Qur'ani yote) kama vile mabwana Burair Hamdani, Kinanah bin Atiq Taghlibi, Nafi bin Hilal, Hanzalah bin Asad na watu wengine walio na elimu ya kutosha ya Qur'ani na Hadithi za Mtukufu Mtume [s] na wale ambao sala zao zisizokoma ambazo hata kiza cha mausika pia kinazishuhudia. Vile vile walikuwepo maaskari wasioogofya na kitu cho chote kile ambao majina yao yalikuwa yakitolewa mifano.

Marafiki zake walipomalizika kufa, zamu iliwaangukia watu wa jamii yake. Wa kwanza wa wale walio wajibikiwa kufa alikuwa Bwana Ali Akber, mwana wa Imamu [a] aliyefanana sana na Mtukufu Mtume [s] kwa umbo lake, sauti yake na mwendo wake. Kifo cha mwana huyu kilikuwa pigo kali sana kwa Imamu [a], lakini alimpeleka wana wa Bwana Abdullah bin Jaafar kwenye uwanja wa vita na watu wengine wa jamii ya Bwana Aqil, ami yake Imamu [a].

Kisha alifuatia Bwana Qasim mwana wa nduguye Imamu Hasan [a]. Mwisho kabisa wana wa Hadhrat Ali [a] waliyatoa mhanga maisha yao. Sasa ikawa amebakia mshika bendera "Mwenzi wa Ukoo wa Bani Hasham", Bwana Abul Fadhl AI-Abbas. Imamu [a] hakumruhusu bwana huyu kwenda kupigana lakini mwishoni alimruhusu kwenda kuchota maji kwa ajili ya watoto wadogo waliokuwa wakilia kwa ajili ya kiu.

Bwana Abbas alitoka kwenda mtoni na kiriba cha maji na huku ameshika bendera. Ingawa alikuwa na mizigo hiyo yote alipigana vizuri sana hata akafaulu kufika mtoni na akakijaza kiriba na akarudi. Mikono yake ilikatwa mmoja baada ya mwingine lakini alijaribu kila aliloliweza, kuwafikishia maji wale watoto wenye kiu. Akiwa bado hajafika kule waliko; mshale mmoja ulikitoboa kiriba na maji yakamwagika. Moyo wa Bwana Abbas ukavunjika na akaanguka chini kwa pigo la rungu lililompiga kichwani.

Sasa Imamu Husayn [a] alikuwa peke yake, lakini bado orodha ya mashahidi haijakamilika.

Aliingia hemani mwake na kuomba apewe mwanawe mdogo wa miezi sita, Bwana Ali Asghar, ambaye alikuwa akifa kwa kiu. Alimchukua mtoto huyo na kutoka naye nje kuwaendea maadui. Lakini badala ya mtoto huyu kupewa maji, koo la mtoto huyu lilipatiwa mishale mitatu na mtoto akafa.

Sasa lmamu Husayn [a] yeye mwenyewe alikwenda kupambana nao, na ingawa alipata mishtuko mingi kwa kufiwa na watu wake alipouchomoa upanga wake aliwakumbusha watu siku za mabwana Hamza, Jaafar, na Hadhrat Ali [a] kwa jinsi alivyopigana kishujaa. Lakini kupoteza damu, majeraha mengi, na kuzongwazongwa na maadui mwishoni kulimuangusha. Hapa kila aina ya silaha ilitumika kumjeruhia na mwishoni upanga wa kafiri mmoja aliyeitwa Shimr ulikata kichwa cha mjukuu huyu wa Mtukufu Mtume [s] tangu nyuma ya shingo yake ili kumwongezea maumivu zaidi na kwa ajili ya laana ya Mwenyezi Mungu juu ya Shimr.

Mahema ya lmamu [a] yalichomwa moto. Maiti yake iliyokuwa bila ya nguo ilikanyagwa kanyagwa na farasi za maadui.

Baada ya kufariki Imamu Husayn [a], alibakia mwanawe aliyekuwa mgonjwa, aitwaye Ali Zainul Abidiin peke yake na ambaye alichukua Uimamu sasa.

Imamu Ali Zainul Abidiin alitekwa pamoja na wanawake wote na watoto. Hawa Waislamu wa kujifanya tu waliziacha maiti za mashahidi hao hivi hivi bila ya kuzizika. Watu wa kabila Asad ndio waliozizika mnamo tarehe 12 Muharram mwaka huo wa 61 Hijiriyah.

Kaburi tukufu la lmamu Husayn [a] huko Karbala (Iraq) bado mpaka leo lingali Kuba la Haki lizipelekeazo mionzi ya Nuru ya Mwenyezi Mungu roho zote zimchanzo Mungu. Njia mbali mbali ya kuzidhihirisia fikara zetu, 'Taziah', sadaka na vitu vingine bado vinatukumbusha mhanga wa Imamu Husayn [a] usio na kifani.

Kama ulimwengu ukiyaangalia kwa makini yale aliyoyatenda Imamu Husayn [a] tuna uhakika kuwa udugu wa kweli na kujitoa kwetu kwa ajili ya kudumisha ukweli, vitakuwa tena katika iIe sura ya miaka mingi iliyopita.

Watabarikiwa wale wanaomkumbuka huyo Shahidi wa Ubinadamu na kujaribu kuzifuata nyayo zake - Ameen.
1. Baadhi ya watu humwabudu Mwenyezi Mungu kwa matumaini (ya kupata Pepo); hiyo ni ibada iliyo kama ile ya wafanyi biashara; baadhi ya watu humwabudu Mwenyezi Mungu kwa sababu wanamwogopa; hiyo ni ibada ya watumwa; na wengine humwabudu kwa shukrani; hiyo ndio ibada ya mtu kamili.

2. Kama kusingalikuwa na vitu vitatu mwana Adamu asingelitii kitu cho chote - umasikini, maradhi na kifo.

3. Bahili (mbaya) sana ni yule anayefanya ubahili katika salamu.

4. Usiwe mbaya kwa mtu asie (saidiwa) na mtu yeyote yule dhidi yako ila Mwenyezi Mungu.

5. Jihadhari na vitendo vinavyotaka uombe msamaha; kwa kuwa mtu mwaminifu hafanyi maovu na mnafiki hufanya.

6. Katika mafungu sabini ya neema, mafungu sitini na tisa ni ya yule aanzae kitu kizuri na (fungu) moja ni kwa wale wanaofuatia.

7. Wakati maskini anapoitoa mhanga heshima yake katika kukuomba, ilinde heshima yako kwa kujizuia usimuudhi.

8. Kosa kubwa Ia wafalme ni woga mbele ya adui, ukatili kwa wanyonge na kutokuwa na ukarimu.

9. Kama utajiri wako hauwezi kukuhudumia utauhudumia wewe, hivyo usiuweke wote, kwa sababu hautakuweka mzima; utumie kabla haujakutumia.

10. Yoyote yule aupokeaye ukarimu wako hukusaidia katika kuwa mtu bora.

11. Ukweli ni heshima, uwongo ni kukata tamaa, siri ni dhamana, ujirani ni udugu; msaada ni urafiki, vitendo ni ujuzi, wema ni Ibada (kwa Mwenyezi Mungu), kunyamaza (kukaa kimya) ni pambo, ubahili ni umasikini, na huruma ni hekima, ukarimu ni ustawi.

12. Kufa kwa heshima, ni bora kuliko kuishi kwa aibu.

13. Wakati Imamu [a] alipoulizwa, kwa nini Mwenyezi Mungu aliamrisha watu kufunga, alijibu: "Ili kwamba tajiri ajue jinsi njaa ilivyo na aweze kuwa na huruma kwa maskini."

14. Yavumilie mabaya kwa kuufuata Ukweli na vumilia kutengana na vitu uvipendavyo kwa kuitika mwito wa Akili.

15. Mojawapo ya mambo yaliyo bora kwa mtu ni kuliacha lile jambo Iisilomhusu.

16. Nyingi ya dhambi (azifanyazo mwanadamu) ni bora kuliko toba zao.

17. Kutafuta elimu ni njia ya kuutambua Ukweli; upana wa maarifa ni ukamilishaji wa hekima; ubora huambatana na uchamungu; kutosheka ni usalama wa miili; ye yote yule akupendae atakuzuia (usifanye maovu) na adui yako atakushawishi kufanya maovu.

18. Wanadamu ni watumwa wa Ulimwengu. Dini ni kama chakula kupendeza kwa ndimi zao na binadamu huishikilia (hiyo dini) kwa muda mrefu wa kadri itakavyowapa uwezo wa kujipatia riziki zao. Na kila wanapopatwa na tatizo lo lote lile, ni wachache sana wanaobakia katika dini.

19. Kama mtu ye yote akimwabudu Mwenyezi Mungu kama ipasikavyo, Mwenyezi Mungu humpa zaidi ya mategemeo yake na mahitaji yake.